Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

BERNARD MAMBWE


WASIFU WA MAREHEMU MCHUNGAJI BERNARD SHAMBA KAZINGO MAMBWE

Mchungaji Bernard Shamba Kazingo Mambwe alizaliwa wilayani Kibondo Mkoani Kigoma, mnamo tarehe 08 Septemba 1957, akiwa mtoto wa tatu kwa tumbo la Mama yake Marehemu Mama Ntibanyendeza Mambwe na Baba marehemu Mzee Mambwe Katoga.

ELIMU:

Bernard S.K. Mambwe alihitimu masomo ya Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kigoma mnamo mwaka 1980. Na kisha mwaka 1985 alihitimu stashahada ya Uchungaji katika chuo cha Tanzania Adventist Seminary and College (TASC). Baadaye mwaka 1995 alihitimu Shahada ya kwanza ya Theologia katika Chuo Kikuu cha Bugema (Bugema University) kilichoko Kampala Uganda. Mnamo mwaka 2009, Mchungaji Bernard S.K. Mambwe alihitimu masomo yake ya Umahiri (Masters) katika Uongozi katika Chuo cha Adventist University of Africa (AUA) kilichoko huko Nairobi, Kenya.

MAISHA YA IMANI:

Bernard S.K. Mambwe alizaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo. Baada ya mafundisho na maelekezo ya kutosha kutoka kwa Waadventista Wasabato, alimkiri Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake mnamo mwaka 1977 na kubatizwa mwaka huo huo. Tangu hapo alifanya kazi mbali mbali ndani ya Kanisa mahalia na kuanza kazi ya Uinjilisti wa Vitabu. Alidumu katika imani ya Waadventista Wasabato na hakuwahi kupata marudi yeyote kikanisa akidumu katika Imani hiyo kwa uaminifu hadi kifo chake.

FAMILIA:

Bernard S.K. Mambwe alifunga ndoa na Esther K. Buzubona tarehe 07 Septemba 1983 kwenye Kanisa la Waadventista wa Sabato Cherabulo, huduma iliyoendeshwa na Mchungaji Marehemu Philipo Mwambalangania. Mke wake anamwelezea kuwa alikuwa Mume, Baba, Mchungaji mcha Mungu, mcheshi, na kiongozi mwenye hekima na busara, aliyempenda na kuwapenda watoto wake akiwajali sana katika miaka yake yote takribani 39 ya ndoa yake.

MAISHA YA UTUMISHI:

Bernard S.K. Mambwe aliajiriwa na Tanganyika General Field (TGF) mwaka 1978 kama Mwinjilisti wa Vitabu kazi aliyoitumikia hadi kufikia hadhi ya Cheti cha Tatu. Alifanya uinjilisti huo tangu 1978 hadi Julai 1981. Mwaka 1981 mwezi Agosti aliitwa na Fildi ya East Tanzania (ETF) kuwa Mchungaji Mlei katika Mtaa wa Kilombero/Ifakara.
Mnamo Julai 1985 aliitwa na Field ya East Tanzania kuwa Mchungaji katika Mtaa wa Dodoma akauongoza mpaka mwezi Desemba 1989. Januar i 1990 aliitwa na kuitika kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Vijana na Shule ya Sabato katika Field ya East Tanzania (ETF) kazi aliyoifanya mpaka mwezi wa August 1991. Mwezi Julai 1995 aliitwa na Field ya East Tanzania kuwa Katibu wa Wachungaji (Ministerial Director), Ukurungezi alioufanya mpaka Desemba 1998. Mnamo Januari 1999 aliitwa kuwa Katibu Mkuu wa North East Tanzania Conference - kazi aliyoifanya mpaka Desemba mwaka 1999.

Mwezi Januari, mwaka 2000, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti (ASKOFU) wa North East Tanzania Conference (NETC) kazi aliyoifanya mpaka Desemba, 2000. Mwezi ule wa Januari 2001 aliitwa kuwa Mwenyekiti (ASKOFU) wa East Tanzania Field (ETF) kazi aliyoifanya mpaka mwezi wa Desemba 2002. Ni katika Kikao Kikuu cha Union Misheni ya Tanzania cha Desemba 2002 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Tanzania Union Misheni, na mnamo Januari 2003 alianza kazi hiyo aliyoifanya mpaka mwezi Desemba 2010.
Na katika Session ya Tanzania Union Misheni ya mwaka 2010, Mchungaji Bernard S. K. Mambwe, alipendekezwa na kupitishwa kuwa Mwenyekiti wa Western Tanzania Field (WTF) kazi aliyoifanya mpaka mwaka 2014, Western Tanzania Field ilipopewa hadhi ya kuwa Conference na jina likabadilika na kuwa Western Tanzania Conference (WTC). Session hiyo ilimchagua kuwa Mwenyekiti (ASKOFU) wa Western Tanzania Conference mpaka Agosti 2015 alipochaguliwa tena kuwa Mwenyekiti (Askofu) wa Western wa Western Tanzania Conference (WTC), ambapo aliifanya kazi hiyo mpaka kustaafu kwake Desemba 2020.

Alikamilisha miaka ya utumishi katika Kanisa la Waadventista Wasabato, akiwa amelitumikia kwa miaka 42 ikiwa ni sawa na miezi 504. Katika utumishi wake, watumishi walimfahamu kama mcha Mungu, mchungaji, baba, mlezi, mpole, mnyenyekevu, mstahimilivu, kiongozi, mwanzilishi wa miradi, mwana maendeleo wa kweli, na mwadilifu - kiongozi ambaye alikuwa ni kielelezo (Role Model) kwa watumishi wengi mpaka sasa.

UGONJWA HADI MAUTI:

Mchungaji Mstaafu Marehemu Bernard S.K. Mambwe alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari (diabetes) ambao umekuwa ukimsumbua tangu miaka ya 2002. Ni ugonjwa huu wa kisukari ambao inaelekea ulisababisha uoni hafifu. Ugonjwa huo ulileta udhaifu mwingine wa viungo kadhaa mwilini mwake na kupelekea alfajiri ya Alhamisi ya tarehe 12, Mei 2022 majira ya saa 10 na dakika 35 alfajiri Mchungaji Bernard S.K. Mambwe kulala usingizi wa mauti. Marehemu Mchungaji Benard Shamba Kazingo Mambwe ameacha mke, watoto wanne wa kiume: (1)Ntiyanka, (2) Masengo, (3) Yilafasha na (4) Ntakiyigola na wajukuu wanane.

PANA MAHALI PAZURI MNO:

Wimbo # 180 kutoka kitabu cha Nyimbo za Kikristo unatufariji unaposema;
1. Pana mahali pazuri mno, Twapaona kwa mbali sana. Baba yetu angoja pale, Amepanga makao yetu.

Chorus:
Kitambo tu bado, Tutakutana ng’ambo pale.
Kitambo tu bado, Tutakutana ng’ambo pale.

2. Tutaimba pale kwa moyo, Nyimbo tamu za wenye heri. Na rohoni hatutaona, Tena haja ya kupumzika.

3. Kwa Baba yetu mkarimu, Tutatoa shukrani sana. Kwa kipaji cha pendo lake, Na baraka anazotupa.

KWAHERI MPAMBANAJI HADI ASUBUHI ILE KUTAKAPOPAMBAZUKA!!!