UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI:
SURA YA NNE
Sura ya nne ya kitabu cha Warumi inazungumzia uhalali wa dhana ya kuhesabiwa haki kwa imani hasa kwa Wayahudi ambao huuona mfumo wao wa kutafuta kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria kuwa wenye chimbuko kutoka kwa mababa wa imani wanaoheshimika kama Ibrahimu. Paulo anathibitisha kuwa hata Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani na wala si kwa matendo ya sheria. (Warumi 4:3) “Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
Haki si ujira apewao mtu baada ya kufanya matendo fulani. Haki ni zawadi apewayo mtu kutokana na kazi iliyofanywa na mtu mwingine. Katika Kristo watu huhesabiwa haki kwa neema yaani wakiwa hawajafanya chochote cha kuwafanya wastahili. Katika mfumo wa kuhesabiwa haki kwa matendo haki hununuliwa na matendo wakati katika mfumo wa kuhesabiwa haki kwa imani haki hununuliwa kwa matendo yaliyofanywa na Mungu mwenyewe na binadamu huipokea kwa neema tu.
Wanaohesabiwa haki kwa imani hawana kazi yoyote wanayofanya kustahili haki hiyo. Wanachotakiwa kufanya ni kuamini kuwa kwa kumwamini Yesu wanahesabiwa haki. (Yohana 5:24) “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Katika hali ya kushangaza hata hiyo imani inayomfanya ahesabiwe haki haitoki kwake. (Waebrania 12:2) “Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”
Ibrahimu hakuhesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake. Ibrahimu alimuamini Mungu kabla hajatimiza agizo alilopewa la kutahiri. (Warumi 4:9-10) “Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa.” Kutahiriwa kulikuwa kunathibitisha imani yake kwa Mungu aliyemhesabia haki.
Ibrahimu aliahidiwa kuwa mrithi wa ulimwengu kutokana na imani yake na si kwa sababu ya kutii sheria. (Warumi 4:13) “Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.” Haki ya Mungu huwajia wanadamu kama urithi utolewao na mzazi kwa mtoto wake. Urithi hauwezi kufananishwa na ujira kwa sababu ujira ni malipo ya kazi iliyofanyika wakati urithi ni stahiki anayopewa mtoto kwa ridhaa ya mzazi na wala haitokani na kazi aliyofanya.
Wanaotaka kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria wanabatilisha agano la ahadi lililotolewa kwa Ibrahimu. (Warumi 4:14) “Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.” Urithi hauwezi kuja kwa masharti ya kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria. Na kama urithi ungepatikana kwa matendo ya sheria hapakuwa na haja ya kumhesabia haki Ibrahimu kwa njia ya imani.
Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani na si kwa matendo ili awe baba wa imani wa wanadamu wote watakaohesabiwa haki kwa imani. Ibrahimu anakubalika na Wayahudi, Wakristo, na Waislamu na kuwa kielelezo cha haki ipatikanayo kwa imani. Paulo haishii kwa Ibrahimu bali anamtaja pia Daudi kama mtu muhimu kwa taifa la Israeli ambaye aliyeamini kuwa wanadamu wanahesabiwa haki kwa imani na si kwa matendo mema.
Hakuna malipo kwa ajili ya dhambi na wale wenye dhana kuwa matendo fulani mema yana uwezo wa kumuondolea au kumpunguzia mtu zigo la dhambi wanafanya jambo lisilowezekana. Dhambi inalipwa kwa kifo cha mwanadamu asiye na hatia. (Warumi 4:6-8) “Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.” Kusitiriwa ni kukingwa na matokeo ya dhambi kunakotokana na kuhurumiwa na wala hakutokani na malipo ya huyo mdhambi kupitia matendo yake mema.
Sheria ilikuja ili kosa lionekane wazi wazi. Tena sheria hailiweki kosa wazi peke yake bali inalifanya kosa lionekane katika ukubwa wake halisi. (Warumi 5:20) “Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi.” Katika Amri Kumi Mungu anasema usiue. (Hesabu 35:17-18) “Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.”
Lakini katika kuua huko huko Mungu alitoa neema kwa mtu atakayekimbilia mji wa makimbilio baada ya kutekeleza hayo mauaji. (Hesabu 35:11-12) “Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe.” Kwa hiyo neema ina nguvu kubwa kuliko ukali wa sheria. Yesu kupitia neema anamtetea mdhambi baada ya kukidhi matakwa yote ya sheria. Yesu ndiye mji wa makimbilio.
Kama Ibrahimu alihesabiwa haki kabla hajatahiriwa vivyo hivyo wanadamu huhesabiwa haki kabla hawajapokea agizo lolote kutoka kwa Mungu. Kama Waisraeli walivyookolewa kutoka utumwani Misri kabla ya kupokea maagizo ya amri kumi na torati, ndivyo wanadamu wanavyookolewa kabla Yesu hajawaagiza kushika amri zake. (Yohana 14:15) “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”
Kutokana na ukweli huo Paulo anawaona watu wa mataifa mengine kuwa wanahusika na agano alilofanya Mungu na Ibrahimu. Agano hilo halikujikita katika sheria bali lilijikita juu ya imani. Hii inamfanya Ibrahimu kuwa baba wa mataifa mengi na si wa Wayahudi pekee. Mungu alitoa ahadi ya kuwakomboa wanadamu kupitia ahadi aliyoitoa kwa Adamu. (Mwanzo 3:15) “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”
Ahadi hii Mungu aliirudia kwa Ibrahimu. (Mwanzo 17:7) “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako.” Hapa Mungu alikuwa anatabiri uzao wa Ibrahimu utakaowahusisha watu wa mataifa yote wakiwamo Wayunani na siyo wazao wa torati tu. (Warumi 4:16-18) “Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote.”
Ibrahimu anakuwa baba wa mataifa mengi kwa sababu mataifa yote yanaokolewa kwa njia ya imani bila kujali kama waliwahi kuwa wazao wa torati hapo awali. (Warumi 4:17) “(Kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.” Ingawa Wayahudi walimtambua kuwa ni baba wa taifa la oleo Ibrahimu ni baba wa Wakristo na Waislamu pia.
Imani ni kuamini kile Mungu alichoahidi hata kama katika hali ya kawaida kinaonekana kama kisichowezekana. (Waebrania 11:1) “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” Ibrahimu alikuwa na imani ya namna hii naye akaitwa rafiki wa Mungu. (Yakobo 2:23) “Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.” Imani inahitajika katika kudumisha mahusiano na Mungu kwa sababu yale Mungu anayoahidi hutimia kutegemeana na kiwango cha kuamini kwa mtu.
Kumwamini Mungu ni kuwa na uzoefu naye. Ni kumwelewa alivyo wa kuaminika. (Waebrania 11:11) “Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.” Hata Ibrahimu alimwamini Mungu kwa kigezo hicho hicho. (Warumi 4:18-19) “Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara.”
Kuhesabiwa haki kulikojengwa juu ya ahadi za Mungu ni kwa kuaminika zaidi kuliko kuhesabiwa haki kulikojengwa juu ya matendo ya sheria yanayotokana na jitihada za kibinadamu. Kuhesabiwa haki kwetu kuliahidiwa kwa kiapo kuthibitisha kuwa ni kwa kuaminika. (Waebrania 6:16-17) “Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu.”
Kuhesabiwa haki kulikoahidiwa hakumhusu Ibrahimu au Wayahudi pekee bali kuliwahusu wanadamu wote. Mzao ambaye Mungu aliahidi kumtuma ili awe suluhisho la dhambi na mrithi wa ufalme ni Yesu na si Isaka. (Wagalatia 3:16) “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.”
Sisi wote tunahesabiwa haki kwa ajili ya Yesu Kristo. Wokovu wake haubagui watu maana upo kwa ajili ya wanadamu wote. (Warumi 4:23-25) “Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.”