Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WARUMI 2

UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI
SURA YA PILI

Katika sura ya pili Paulo anaendeleza mjadala aliouanza sura ya kwanza kuwa wanadamu wote wametenda dhambi. Anafanya hivi akitambua mazoea ya wanadamu ya kujihesabia haki inayokwamisha wokovu. Moyo wa mwanadamu mwenye asili ya dhambi una tabia ya kujiona hauna hatia hata pale kosa linapowekwa wazi. Aliyetenda dhambi ana kawaida ya kukimbia na kujificha. (Mwanzo 3:9-12) “Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.”

Mtu mwenye hatia hufanya jitihada ya kuhamishia hatia kwa wengine akiamini kuwa kufanya hivyo kunamfanya yeye kutokuwa na hatia au kunampunguzia maumivu ya hatia. (Warumi 2;1) “Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale.” Yesu alipokuja duaniani aliikuta hali hiyo na kuikemea. (Mathayo 7:4-5) “Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

Kwa kuwa hilo ni tatizo la wanadamu wote kutonyoka moyo wake unapomdhihirishia hatia, Mungu anatoa msaada ili kumrahisishia mwanadamu kukiri makosa yake. Paulo anaelekeza kuwa hatua ya kwanza katika mchakato wa kuokolewa ni kujitambua ulivyo mwenye dhambi. Hali hii ya kujitambua ulivyo mwenye dhambi hupelekea hatua nyingine ya kusikia vibaya kutokana na dhambi hiyo na kukusudia kuiacha. Hatua hii ya kukusudia kuondokana na dhambi inayojulikana kama kutubu inachagizwa na upendo wa Mungu unaofurika kwa wingi kwa mwenye dhambi pale anapohisi hatia. (Warumi 2:4) “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?”

Mtu hatubu kwa sababu ya kuhofia adhabu au matokeo ya dhambi. Toba ya namna hiyo ni ya kibinadamu na wala haitoki kwa Mungu. Lakini toba itokayo kwa Mungu humvuta mdhambi hata kupata wokovu. (2 Wakorintho 7:10) “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.” Toba ya kweli husukumwa na Roho Mtakatifu anapousukasuka moyo uliopondeka. (Zaburi 34:18) “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.” Msukosuko huo huulainisha moyo na mwishowe mtu hujisalimisha. (Matendo 2:37) “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.”

Mchakato huu wa wokovu ni lazima uishie katika kuleta mabadiliko ya tabia yaletwayo na Roho Mtakatifu. Matendo haya mema yanayozalishwa na Roho Mtakatifu ni ya muhimu ili yamuandae mwongofu kwa maisha makamilifu ya kule mbinguni na kuwa kichocheo cha wale ambao hawajayatoa maisha yao kwa Yesu watamani nao kuyatoa maisha yao. (1 Petro 2:12) “Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.” (1 Petro 1:18) “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu.” (Ufunuo 21:27) “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.”

Matendo mema hayaokoi lakini yanatofautisha kati ya mwenye imani ya kweli na mwenye imani bandia. (Yakobo 2:14, 17) “Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.” Wokovu ni mabadiliko ya tabia yanayotokana na nguvu ya Mungu ifanyayo kazi ndani ya muumini wa Kristo. (Waefeso 3:20) “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.”

Kuna kutenda mema ukitatafuta kujiinua au kutukuza mwili wa dhambi na kuna kutenda mema kwenye mwelekeo wa kuuendea mwili wa utukufu na heshima na kutokuharibika. Matendo mema yanayozalishwa na Roho Mtakatifu yamejengwa juu kile kitakachoamuliwa na Mungu. Hayafanywi ili kununua upendeleo kwa Mungu kwa kuwa hakuna upendeleo kwa Mungu. Hayajitengenezei matarajio yake. Yamejikita katika kusubiri wakati ulioamriwa na Mungu tangu kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu.

Hofu ya wakati ujao inawahusu wasiotii kweli maana hawana hakika na hatima yao. (1 Wakorintho 3:11-15) “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

Wasiotii kweli ni wale wanaojifariji kuwa mwili wa dhambi usiowezeshwa na Roho Mtakatifu waweza kuzalisha matendo mema yanayokubaliwa na Mungu. Wenye matarajio hayo watapata hasira na ghadhabu, watakapokuja kutambua kuwa Mungu hayatambui matendo yao. (Mathayo 7:21-23) “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

Kwenye mfumo wa kujihesabia haki Wayahudi walikuwa na nafasi kubwa ya kutambulika kama wasio na uovu kwa vile wanayo mausia ya Mungu kuliko Wayunani waliohesabiwa kuwa najisi kwa kuwa hawakuwa kwenye maagano yoyote na Mungu. Lakini Paulo anabainisha kuwa mbele ya Mungu Wayahudi na Wayunani ni waovu mpaka pale watakapotambua na kukubali juu ya udhaifu ulio kwenye miili yao ya dhambi na kuwa tayari kutambua kafara ya Kristo kwa ajili ya wenye dhambi.

Kuwa na sheria hakumfanyi mtu kuwa na kinga ya dhambi mbele ya hukumu. Wenye sheria wasiotenda matakwa ya sheria watahukumiwa kama waliovunja sheria na wasio na sheria watahukumiwa kupitia dhamiri zao kuwa hawakutenda kulingana na dhamiri zao. Hukumu ya Mungu kwa sehemu kubwa haiegemei katika kutafuta ulikuwa makini kiasi gani kutii sheria Iliyofunuliwa kwako au ulikuwa makini kiasi gani kuishi kulingana na dhamiri yako kwa sababu inatambua hakuna mwenye mwili wa dhambi aliyekidhi matakwa ya kisheria kikamilifu. Hukumu itajikita katika kuangalia ni kwa jinsi gani ulitii injili na kumwamini Yesu.