Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WAFILIPI

MASWALI YA KUJADILI: WAFILIPI 1:1-30

  1. Kwa nini Paulo anajitambulisha kama mtumwa wa Kristo Yesu? Kwa nini kwenye utambulisho wake anawataja maaskofu na mashemasi? Yeye anayetajwa kuwa ameianza kazi njema mioyoni na ataimaliza siku ya Kristo Yesu ni nani? Hiyo lazi njema ni ipi? Hiyo siku ya Kristo Yesu ni ipi?
  2. Kwa nini kueneza Injili kulimsababishia Paulo vifungo? Matunda ya haki ambayo Paulo aliwaombea Wafilipi wawe nayo ni yapi? Kwa nini watu waliendelea kuhubiri neno la Mungu pasipo hofu licha ya kufungwa kwa Paulo? Dalili za kuwatambua wanaomhubiri Kristo kwa husuda na fitina ni zipi?
  3. Kwa nini kwa Paulo kuishi ni Kristo na kufa ni faida? Kuna faida gani katika kufa? Mwenendo unaoipasa Injili ya Kristo ni upi? Siri ya kutowaogopa adui ni nini? Je ni lazima kila anayemwamini Kristo ateswe kwa ajili yake?

MASWALI YA KUJADILI: WAFILIPI   2:1-30

  1. Kwa nini kuwa na nia moja, mapenzi mamoja, na roho moja miongoni mwa waumini ni kitu chenye changamoto kubwa? Je ushirika wa Roho ndiyo muarobaini wa changamoto hiyo? Kushindana miongoni mwa waumini kunatokana na nini? (Yakobo 4:1). Kumhesabu mwenzio kuwa bora kuliko nafsi yako kunatokana na nini? Kwa nini kwa kawaida kila mmoja hujiona bora kuliko mwenzie? Kutoangalia mambo yako mwenyewe bali ya wengine kwawezaje kupunguza migogoro katika jamii?
  2. Nia iliyokuwamo ndani ya Kristo ilikuwa nia gani? Je mwanadamu aweza kuwa na nia hiyo? Je nia hiyo ndiyo iliyomuongoza kujitoa kwa ajili ya wanadamu? Kwa nini Yesu hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho. Kama Yesu angeshikamana na hali yake ya Uungu na kuacha kuwa mfano wa mwanadamu wanadamu wangepata hasara gani? Je Yesu angekuwa amefanya dhambi?
  3. Je Yesu aliacha utukufu gani alipokubali kufanyika mwanadamu? (Mathayo 24:30; Mathayo 25:30; Yohana 17:5). Kwa nini Yesu aliyekuwa sawa na Mungu alijinyenyekeza na kuwa mtii hata mauti?Je kumkomboa mwanadamu kulihitaji hali hiyo? Kama Yesu alikuwa Mungu kabla hajawa mwanadam kwa nini Mungu alimzawadia hadhi ya kuwa Mkuu mno baada ya kushinda kifo? Hadhi hiyo anayopewa Yesu yaweza kuwa ni yao hata wale watakaokombolewa?
  4. Je huko chini ya nchi kuna viunbe viishivyo huko vitakavyopiga goti? Kuutimiza wokovu kwa kuogopa na kutetemeka kunafanyikaje? Huyo Mungu atendaye kazi ndani yetu akituhimiza ili tutende kile chema tunachotamani kukitenda ni nani? Hiyo kazi anaifanya kwa njia gani? Kwa nini kizazi cha wasiomwamini Yesu kinaitwa kizazi chenye ukaidi? Kwa nini wale walio ndani ya Kristo huonekana kama mianga katika ulimwengu? Je jamii ya Wakristo mahali unapoishi inatambuika kama wana wa Mungu wasio na lawama? Unadhani ni kwa nini iko hivyo?

MASWALI YA KUJADILI: WAFILIPI 3:1-21

  1. Mambo yale yale ambayo hayamuudhi Paulo kuwaandikia Wafilipi na yapi? Kwa nini mambo hayo hayamuudhi kuyaandika? Mbwa na wajikatao ambao Paulo anawatahadharisha watu kujihadhari nao ni nani? Kwa nini wanaitwa mbwa na wajikatao? Kumwabudu Mungu kwa Roho kunamfanyaje mtu kuwa tohara na kuona fahari juu ya Kristo Yesu? Kuutumainia mwili maana yake nini?
  2. Mambo gani ambayo yangeweza kumfanya Paulo autumainie mwili? Kwa nini mambo hayo hayakumfanya Paulo kuutumainia mwili? Kwa nini Paulo alijiita Mwebrania wa Waebrania? Je, kuwa na juhudi katika kutafuta kujihesabia haki na kuokolewa kama Paulo alivyofanya ni dhambi? Kwa nini kwenye haki ipatikanayo kwa sheria Paulo hakujihisi kuwa na hatia?
  3. Mambo yaliyokuwa faida kwa Paulo ambayo aliyahesabu hasara kwa ajili ya kumpata Kristo ni yapi? Kuna uzuri gani usio na kiasi wa kumjua Kristo? Je, ni lazima mambo yote uyahesabu kama mavi ili umpate Kristo? Kwa nini haki ipatikanayo kwa sheria Paulo anaiita haki yangu mwenyewe? Kwa nini haki ipatikanyo kwa imani inaitwa haki ni haki iliyo katika Kristo?
  4. Ni kwa namna gani tunashiriki mateso yake Kristo na kufananishwa na kufa kwake? Kiyama ya wafu ni tukio la namna gani? Je katika hatua za ukuaji wa kiroho kuna hatua ya kufikia kukamilika? Kwa nini Paulo anasema si kwamba nimekwisha kushika au nimekwisha kuwa mkailifu? Na kwa nini kwenye Wafilipi 3:15 anasema na sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo?
  5. Adui za msalaba wa Kristo ni nani na kwa nini wanaitwa hivyo? Kwa nini utukufu wao upo katika fedheha yao? Mwito mkuu wa Mungu tulioitiwa katika Kristo Yesu ni upi? Kwa nini wenyeji wetu uko mbinguni na si hapa duniani? Kama wenyeji wetu uko mbinguni imekuwaje tumekosa kuwa na tabia za mbinguni?
  6. Yesu atabadili mwili wetu wa unyonge upate kufanana na mwili wake wa utukufu. Kwa nini mwili wetu unaitwa wa unyonge? Mwili wa utukufu wa Kristo utakuwa unafananaje hata uitwe wa utukufu? Je, mwili huo wa utukufu tutakaopewa waweza kutupatia uweza wa kuvitiisha vitu vyote viwe chini yetu?

MASWALI YA KUJADILI: WAFILIPI 4:1-23

  1. Paulo alikuwa na hakika gani kama majina ya walioshindania Injili na waliotenda kazi pamoja naye majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima? Watu hao waliotajwa waliishindaniaje Injili? Ni kwa nini Injili inahitaji kushindaniwa? Je, kufurahi ni jambo linaloweza kufanyika kila siku? Je, Biblia haijasema kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka? (Mhubiri 3:4).
  2. Upole wetu una mahusiano gani na ukaribu wa kuja kwa Yesu? Kwa nini njia zingine za kutatua matatizo kwa Mkristo kando na kusali zinaonekana kama ni kujisumbua? Je changamoto zote zinatatuliwa kwa kusali? Je ni muhimu unaposali au kuomba haja zako zijulikane na Mungu? Je wale wanaoomba kwa lugha haja zao zinajulikana kwa Mungu ikiwa wao wenyewe hawawezi kujua walijuwa wanaongea nini?
  3. Je unadhani hizi lugha zisizotafsirika zinalenga kuwafanya waonbaji wasifikishe haja zao kwa Mungu? Je, mazoea ya kuomba huku ukiwasilisha haja zako kwa Mungu humwacha muombaji akiwa na amani na utulivu wa moyo na akili? Je, kuruhusu mawazo mabaya kunaathiri vipi amani ya moyoni? Kwa nini kuzuia mawazo mabaya ya kukatisha tamaa na kuongeza hofu huwa ni jambo gumu kwa wengine? Je mtu aliyevurugwa anaweza kuwa na amani?
  4. Je, kukosa mahitaji kunaweza kumkosesha mtu amani? Je ukiwa na roho ya kuridhika kama hiyo anayoshauri Paulo unaweza kuwa na maendeleo? Je, Yesu ana uwezo wa kukidhi mahitaji tuliyopungukiwa? Kwa nini makanisa mengine hayaoni umuhimu wa kumhudumia mtumishi wa Injili hata kama wanayaona mahitaji aliyonayo? Udhani wale wasiosaidia wana chuki na kiongozi wao au wana chuki na Injili?
  5. Mungu anaahidi kuwajaza kila wanachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake wale wote wanaoitegemeza kazi ya injili. Unadhani Mungu ameshindwa kufanya hivyo kwa watu wake kwa kuwa hawaitegemezi kazi yake inavyostahili?Watu huitwa watakatifu baada ya kuwa na mwenendo unaoridhisha au baada ya kuipokea injili ya Yesu Kristo? Kwenye dunia ya leo iliyoharibika ni sahihi kumwita mtu mtakatifu?