Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

1 TIMOTHEO

MASWALI YA KUJADILI: 1TIMOTHEO 1:1-20

  1. Kwa nini sheria haimhusu mtu wa haki? Kwa nini katika kuifafanua sheria kumekuwepo na upotoshaji mwingi? (fng7) Namna isiyo halali ya kutumia sheria ni ipi? Je kila atendaye dhambi au makosa hufanya hivyo kwa sababu ya ujinga na kwa kutokuwa na imani? (fng13) Je, unapoomba msamaha waweza kuzitaja sababu hizo kama hoja za kumshawishi Mungu akusamehe? Mtu anaweza kumtumikia Mungu katika nafasi yoyote kanisani hata kama hajaoa au hajaolewa?
  2. Je Paulo alikuwa sahihi kusema Himenayo na Iskanda amempatia Shetani ili awafundishe wasimtukane Mungu (fng20)? Je kuna wakati watumishi wa Mungu wanaruhusiwa kutamka maneno kama haya kwa waumini wao? Paulo alikuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu. Unadhani mitume wanaoibuka kila uchao leo hii wapo kwa mapenzi ya Mungu?
  3. Paulo alikuwa akimwabudu Mungu kwa dhamira safi. Nitatambuaje kama namwabudu Mungu kwa moyo safi? Paulo anamsiffia Timotheo kuwa alikuwa na imani isiyo na unafiki. Imani isiyo na unafiki unaitambuaje? Paulo anadai imani ya Timotheo ilikuwapo kwanza kwa mama yake na bibi yake. Je imani inarithishwa? Karama ya Mungu inachochewaje? Je unaweza uwe na karama na usiitambue?
  4. Yesu alituokoa kisha akatuita kwa wito wake mkuu? Kati ya kuitwa na kuokolewa ni kipi huwa kinatangulia? Je matendo yetu yana nafasi gani katika kuokolewa kwetu? Yesu alibatilisha mauti na kuufunua uzima wakati gani na kwa kitendo gani? Je mtu aweza kwa wakati mmoja kuwa mhubiri, mtume, na mwalimu? Paulo anasema anamjua yeye aliyemwamini. Je ni muhimu kumjua uliyemwamini?

MASWALI YA KUJADILI: 1TIMOTHEO 2:1-15

  1. Kwa nini dua na sala zinahimizwa kufanyika kwa ajili ya watu wote na hasa kwa ajili ya wafalme na wenye mamlaka? Je, dua hizo ni za kuwatakia mema au za kuwatakia mabaya? Je, Yesu ni Mwokozi? Kwa nini Mwokozi anaitwa Mungu, je ni kusema Yesu naye ni Mungu? Kwa nini Mungu hutaka watu wote waokolewe? Kuna Ushahidi gani kama Mungu anataka watu wote waokolewe?
  2. Kwa nini ili watu waokolewe wanatakiwa kujua yaliyo kweli pia? Kama Mungu ni mmoja kwa nini kuwe na utatu? Kama Yesu ni Mungu kwa nini anaitwa mwanadamu Kristo Yesu? Kwa nini mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu si Mariamu bali ni Kristo? Huo ukombozi kwa ajili ya wote utakaoshuhudiwa kwa majira yake ni upi?
  3. Kwa nini Paulo anataka wanaume wasalishe kila mahalihuku wakiinua mikono iliyotakata? Je, kwa agizo hilo wanawake wao wamekatazwa kusalisha? Mavazi ya kujisetiri na yenye adabu wanayotakiwa wanawake kujipamba kwayo ni yapi? Je mavazi yanayoonyesha maungo ya ndani au yenye kitambaa kisichosetiri ni ya adabu? Kuna tatizo gani linaweza kutokea Ikiwa wanawake watavaa mavazi yasiyosetiri na yasiyo na adabu?
  4. Kusuka nywele na kuvalia mavazi ya thamani kuna shida gani? Je kufanya hivyo ni dhambi? Mavazi ya thamani huanzia na kiasi gani? Matendo mema yaweza kutumika kama mapambo ya kuwavutia watu badala ya mapambo ya nje wanayohangaikia wanawake? Kwa nini mwanamke anashauriwa kujifunza kwa utulivu huku akitii kwa kila namna?
  5. Je, kwa Adamu kuumbwa kwanza na Hawa baadaye kunampa hadhi yoyote ya ziada Adamu? Kwa nini Maandiko yanasema mwanamke yaani Hawa alidanganywa ila Adamu hakudanganywa? Kati ya Adamu na Hawa ni nani aliyesababisha dhambi kuingia ulimwenguni?
  6. Kwa nini mwanamke haruhusiwi kumtawala mumewe? Kwa nini mwanamke alinyimwa ruhusa ya kufundisha? Je ni kwa sababu hana karama ya kufundisha? Kwa nini utulivu umesisitizwa sana kwa mwanamke? Je kuna namna ambayo aliwahi kukosa utulivu huko nyuma?

MASWALI YA KUJADILI: 1TIMOTHEO 3:1-16

  1. Je ni sahihi kwa mtu kutamani kufanya kazi fulani ya kanisani? Utatofautishaje mtu anayetamani kazi kwa manufaa yake na anayetamani kazi kwa manufaa ya kanisa? Katika mazingira ya sasa mtu anaweza kuleta ombi la kuchaguliwa kwenye nafasi fulani anayoimudu au anayoipenda?
  2. Je askofu anaruhusiwa kuoa? Kwa nini mzee wa kanisa anatambulika pia kama askofu? Kwa nini mojawapo ya sifa za mzee wa kanisa ni kuwa na uwezo wa kufundisha? Kwa nini Biblia inasema mzee wa kanisa asiwe mtu wa kuzoelea ulevi badala ya kusema asiwe anakunywa pombe?
  3. Mtu aliyeongoka karibuni anapimwa kwa umri wake wa uongofu au kwa kasi ya ukuaji wake kiroho? Mtu aliyeongoka karibuni ana uwezekano wa kufanya kosa gani katika uongozi? Uwezo wa kuisimamia nyumba yake unatusaidiaje kumjua mtu mwenye sifa za kuongoza kanisa?
  4. Kwa nini mashemasi wametakiwa kuwa watu wasiotumia mvinyo sana badala ya kusema wasiokunywa pombe kabisa? Kabla ya mashemasi kupewa kazi ya ushemasi wanajaribiwa kwa kupewa kazi gani? Daraja analojipatia mtu aifanyaye kazi ya ushemasi vema ni lipi? Fedha ya aibu ambayo mashemasi wametakiwa kujiepusha nayo ni ipi?
  5. Je mashemasi huwafundisha waumini jinsi iwapasavyo kuenenda katika nyumba ya Mungu? Huyo Mungu aliyedhihirishwa katika mwili na akachukuliwa juu katika utukufu ni yupi?

MASWALI YA KUJADILI: 1TIMOTHEO 4:1-16

  1. Je, Roho ana uwezo wa kunena? Nyakati za mwisho huanzia wakati gani? Je, unaiona hiyo hali sasa ya watu kujitenga na Imani wakisikiliza roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani? Je huyo anayesikiliza roho zidanganyazo huwa anajua kwamba anadanganywa? Je na wale wasemao uongo huwa wanajua kuwa wanasema uongo? Kama dhamira huwa zinawasuta kwa nini wasiache kusema huo uongo?
  2. Je, kuwazuia watu wasioe ni kinyume cha Biblia? Je, watumishi wa kiroho wanatakiwa kuoa? Je kuwaamuru watu wajiepushe na vyakula ni kinyume cha Biblia? Je kuna kikundi chochote cha kiroho kilichowahi kufanya hivyo kwa waumini wake? Je, kwa kuwa kila kiumbe cha Mungu ni kizuri kinafaa kuliwa?
  3. Je ujana unadharaulika kutokana na maoni ya watu au kutokana na yale vijana wanayoyafanya? Je ni kawaida kwa vijana kuwa kielelezo kwa usemi, na mwenendo, na Imani? Kusoma, kuonya na kufundisha kuna nafasi gani katika kufanikisha utumishi wa kiroho? Je karama yaweza kutolewa kwa njia ya kuwekewa mikono ya wazee? Njia ya kutunza nafsi yako na ya wale wanaokusikia ni nini?

MASWALI YA KUJADILI: 1TIMOTHEO 5:1-25

  1. Utaratibu wa kukemea kwa kuangalia rika shida aliyonayo mtu unafaa kuzingatiwa na wahubiri wa leo? Kwa nini kuna malalamiko mengi hasa kutoka kwa wainjilisti kuwa Wazee wa kanisa na wachungaji hawakemei dhambi? Kuna ukweli wowote juu ya madai hayo?
  2. Wajane walioachwa peke yao wanatakiwa kuweka tumaini lao kwa nani na kwa nini? Mpango wa maombi kwa wajane kama hao ukoje? Kwa nini kwa kawaida wajane huachwa peke yao? Kwa nini asiyejizuia nafsi yake huhesabiwa kama aliyekufa ingawa yu hai?
  3. Kwa nini kasi ya wajane wasio wazee kuolewa ni ndogo? Je mjane akiolewa ni lazima ayaache makazi aliyojenga na marehemu mumewe? Huenda hiki kikawa ni kikwazo kinachozuia wasiolewe? Kwa nini asiyewatunza wa nyumbani mwake ni mbaya kuliko asiyeamini?
  4. Kwa nini wazee watawalao vyema na hasa wale wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha wanastahili kupewa heshima maradufu? Kwa nini wale wadumuo kutenda dhambi wanatakiwa kukemewa tena mbele ya watu wote? Je huku si kudhalilisha watu?
  5. Kwa nini Timotheo aliambiwa atumie mvinyo kidogo badala ya kutumia maji peke yake? Je mvinyo una faida gani katika mwili wa mwanadamu? Je fungu hilo linahalalisha watu kunywa pombe?

MASWALI YA KUJADILI: 1TIMOTHEO 6:1-21

  1. Ilikuwa sahihi kwa Paulo kuwasihi watumwa Wakristo kuendelea kuwaheshimu mabwana zao waliowafanya watumwa? Je kwa mtumwa kutomheshimu bwana wake kunatukanishaje jina la Mungu na mafundisho ya Kikristo?
  2. Majadiliano ya watu walioharibika akili zao huwazia maswali na maneno ya mashindano ambayo huishia kwenye matusi na ugomvi na matusi. Je umeshawahi kukutana nao watu wa aina hiyo kanisani kwako. Njia ipi sahihi zaidi ya kukabiliana na watu hao?
  3. Kwa nini kupenda fedha kunaitwa shina la mabaya ya kila namna? Je fedha na mafanikio ya kiuchumi vyaweza kumfanya mtu kufarakana na imani? Je fungu hilo (6) linatuagiza tusitafute fedha au mali?