Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

KANUNI ZA KUTOA USHAURI

KANUNI ZA KUTOA USHAURI

Hakuna binadamu asiyepitia zahama katika kipindi fulani cha maisha yake. Tunaposema zahama tunamaanisha mabadiliko fulani yenye kumletea mtu msongo. Mabadiliko hayo kwa kawaida husababishwa na matukio fulani ambayo humpotezea binadamu uwezo wa kawaida wa kukabiliana na hali husika. Katika mazingira hayo mtu huhitaji msaada wa haraka wa kisaikolojia kutoka kwa wengine unaoitwa uingiliaji wa zahama ambao kwa kawaida huwa katika sura ya ushauri.

Uingiliaji kati huu huhusisha matumizi ya mawasiliano ya maneno na yale yasiyotumia maneno yenye lengo la kumtia moyo, kumjenga, na kumuongezea mhusika hali ya kujiamini, ili apambane kwa ufanisi zaidi na hali inayomsonga. Kwa kawaida mwili una mfumo wake wa kukabili changamoto zinazotokea maishani. Lakini wakati wa zahama mwili hupungukiwa kwa kiasi kikubwa na uwezo huo na hivyo mtu kujikuta akishindwa kuikabili zahama iliyomtokea. Mtoa ushauri anachofanya katika mazingira haya ni kumpatia muathirika vitu vinavyoimarisha uwezo wake wa kuikabili zahama. Vitu hivyo ni kama

Mtu anaposhindwa kukabili zahama yake mambo kadhaa hujitokeza. Mtu hupata msongo, hali inayofanya viungo vyake na akili vishindwe kushirikiana katika kupata jawabu la tatizo. Hali hiyo huweza kuleta msongo wa akili, kuumwa kichwa, wasiwasi, vidonda vya tumbo, mapigo ya moyo kwenda mbio nk. Hali hii ikiendelea huweza kumletea mwathirika hali ya kujihisi kushindwa na kupoteza matumaini kunakoweza kumfanya afikirie kunywa pombe sana kujaribu kupunguza mawazo, kuendesha gari kwa kasi au hata kufukiria kujiua.

Kila zahama huwa na kawaida ya kuzalisha hasara kwa muathirika. Ukubwa au udogo wa zahama si jambo linaloamuliwa na asiyefikwa na zahama bali na yule aliyefikwa na zahama yenyewe. Hivyo ni makosa kupuuza kile kinachoonekana zahama kwa mwingine kwa kuwa kile kilicho zahama kwake kinaweza kisionekane kuwa  zahama kwako. Mfano mtu mzima kuogopa kulala chumba cha giza kiasi cha kukaribia kuhatarisha maisha yake. Hili kwa wengine halichukuliwi kuwa zahama kutokana na kuchukulia kuwa watu wazima wote huwa hawaogopi giza. Au binti kutaka kujinyonga kwa sababu mchumba wake amekatiza uchumba. Kila zahama ni lazima ipimwe kwa uzito wake bila kupuuzia kwa kuwa jambo la msingi ni kuondosha kile kinachotia uhai wa mtu hata kama kwa wengine kinaonekana si tishio.

Zahama zinazosumbua sana watu katika maisha ya kila siku ni kifo cha mpendwa, mahusiano yaliyovurugika au yaliyovunjika, kufukuzwa kazi, kuhamishwa eneo la kazi au kubadilishwa kazi, kupata ugonjwa usio na tiba, madeni na hali mbaya kiuchumi, maafa ya kimbunga na mafuriko, kuunguliwa na nyumba, vita na ugaidi, kuachika, kustaafu, mimba isiyotarajiwa, ugumba nk. Ukubwa wa zahama kwa kiasi kikubwa unaamuliwa na jinsi mhusika anavyoruhusu uchungu ulioletwa na zahama udumu kwa muda gani.

Zahama haiashirii ubaya tu bali pia ni fursa ya matumaini ikiwa itatumiwa vizuri. Wale walio kwenye zahama hujikuta wakikabiliana na hasara ya namna fulani na hasara hiyo ndiyo inayowaletea huzuni ambayo isipotawaliwa ndiyo huja na matokeo mbaya. Ikiwa mtu atafahamu mbinu za kitaalamu zinazohitajika kuikabili hasara hiyo hicho kinachoonekana kuwa cha kukatisha tamaa chaweza kuwa fursa mpya maishani. Ni ukweli ulio dhahiri kuwa baadhi yetu tumehusika katika kukuza zahama aliyokuwa nayo mtu, hata kufikia hatua ya kuleta matokeo mabaya kwa mhusika kwa kuwa tulishauri isivyo. Ndiyo maana Biblia inatoa ushauri kuwa kazi ya kushauri ni lazima ifanywe na watu makini wanaojua wanachotakiwa kufanya. Wagalatia 6:1 “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.”

Zahama inaweza kuzuiwa ikiwa mtu atazingatia mambo kadhaa maishani. Hii ndiyo sababu zahama moja yaweza kuzalisha matokeo tofauti kutegemeana na namna kila muathirika alivyoipokea zahama hiyo. Mtu akiwa na mtazamo sahihi kuhusu mambo yanayotokea huweza kusaidia kupunguza athari za zahama inayomkabili. Kwa mfano kama matukio ya kufiwa yakitokea kwa mfululizo katika kipindi kifupi kwenye familia yaweza kumfanya mwingine adhanie ni matukio ya kupangwa na kuingiwa na hofu kuwa kifo kinachofuata kitamhusu yeye wakati ambapo vifo hivyo havikuwa vya kupangwa. Mtu huyu anahitaji maarifa ya kutosha ya kile kinachoendelea katika mfululizo huo wa vifo. Kama chanzo cha vifo ni mazingira yasiyo safi, hatua inayohitajika ili kuzuia vifo visiendelee ni kusafisha mazingira.

Sababu nyingine ya kuathirika na zahama ni kukosa mtandao wa kutosha wa watu kukutia moyo. Binadamu wa kawaida anahitaji kufarijiwa. Faraja ya maneno au hata ya uwepo wao tu hupunguza maumivu na kupunguza ukubwa wa hasara aipatayo mtu anayepitia zahama. 1 Wathesalonike 5:11 “Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.” Wale walio katika jumuiya za kidini, au zingine zenye nafasi ya watu kufarijiana wanajiongezea uwezo wa kuzikabili zahama maana wanakuwa na mtandao wa kutosha wa kuwapatia matumaini wakati wa zahama kuliko wale wasio katika jumuiya hizo. Wakristo wanayo mafungu ya Biblia yenye ahadi za thamani na faraja tele. Wanayo pia fursa ya kufanya maombi juu ya changamoto zao za maisha. Lakini wanayo fursa ya kuwaona watu wenye shida na kushiriki kuwatia moyo jambo linalopunguza uzito wa yale mazito yanayowaelemea. Yakobo 5:14-15 “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.”