Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

UCHUMBA NDOA NA HARUSI

Utangulizi

Ujana ni umri wa kufanya maamuzi magumu yenye matokeo ya kudumu. Makosa katika kufanya maamuzi kwenye umri huu huwa na athari katika maisha yajayo. Katika ujana mtu huchagua masomo atakayosoma kwenye ngazi za juu, huchagua aina ya kazi atakayofanya ili kumuingizia kipato, na mwisho huchagua mwenzi wa maisha atakayeshirikiana naye kufikia ndoto za maisha na kumaliza naye safari ya maisha kwa mafanikio. Kuchagua mwenzi wa maisha huenda ukawa ndiyo uchaguzi unaotaka umakini mkubwa zaidi kuliko mwingine wowote maishani. Uchaguzi wa mwenzi wa maisha huhitaji kuzingatia mambo mengi kabla ya kuutekeleza lakini kubwa kuliko yote ni kumuomba Mungu akuonyeshe mwenzi aliyekuandalia.

Mwalike Mungu akusaidie:

Kuchagua mchumba anayefaa ni mtihani unaowakabili wanadamu wote. Kutokana na ugumu na unyeti wa jambo hili Mungu ametoa ahadi kwa wote wanaotafuta wachumba kuwa atawasaidia. (Mithali 19:14) “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Mke mwema au mume mwema hapatikani kwa uchaguzi wa kibinadamu peke yake. Wala hapatikani kwa kuchaguliwa na wazazi au viongozi wa dini. Mume ama mke mwema hutoka kwa Mungu. (Yakobo 1:17). “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Safari kuelekea ndoa:

Safari kuelekea kwenye ndoa huanzishwa na urafiki, kisha uchumba na mwisho ndoa yenyewe. Urafiki na uchumba unaweza kuvunjika lakini ndoa haivunjiki. Uchumba ni hatua ya mpito ambapo watu wawili wa jinsia tofauti hukubaliana kuishi pamoja kama mume na mke hadi mauti itakapowatenga. Kwa kuwa mchumba ni mwenza wa Maisha mtarajiwa umakini unahitajika katika kumtafuta na kumchagua. Kijana asiingie katika hatua hii ya uchumba kwa kukurupuka. Wakati wa kuanza mchakato wa uchumba unatakiwa uwe umeonyeshwa kwenye mpango kazi wa mhusika na kuukabidhi mpango kazi huo kwa Mungu ili upate baraka zake. (Mithali 16:3) “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.” (Mithali 3:5) “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.”

Waseja hawana haja ya kuoa

Kuoa na kuolewa kunawahusu wote waliofikia umri unaostahili na wale wenye vigezo vingine muhimu vinavyohitajika katika kuoa na kuolewa. Vigezo hivyo vingine muhimu ni pamoja na kuwa na via vya uzazi vya jinsia husika vilivyokamilika na vyenye uwezo wa kukidhi majukumu ya kutoshelezana katika ndoa. (1 Wakorintho 7:3) “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.” Kwa kuwa moja ya haki za ndoa ni tendo la ndoa wasio na uwezo wa kutimiza hitaji hilo wasijisumbue kuoa au kuolewa. Dhambi imesababisha baadhi ya wanadamu kupoteza uwezo wa kutoshelezana katika ndoa. Hawa pamoja na kufikia umri unaostahili wasijisumbue kuingia kwenye mchakato wa uchumba. Jitihada ingefanyika mapema katika hatua za makuzi yao (hasa katika umri wa utoto) kurekebisha hali hii ili kuwaondolea kadhia hiyo.

Kutooa na kutoolewa si dhambi

Paulo ni mfano wa waseja ambaye hakuhitaji kuoa. (1Kor. 7:8-9) “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” Paulo anaiangalia hali hiyo kwa mtazamo chanya akiifananisha na karama itokayo kwa Mungu. Hata Yesu anathibitisha kuwa kuna watu waliojaliwa waliotengwa na Mungu kuwa waseja. (Mathayo 19:10-12) “Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” Mungu ana haj ana wale aliowatenga ili wasioe au wasiolewe. Wanaweza kumfanyia makubwa katika hali hiyo kuliko kama wangekuwa wameoa na kuolewa. (1 Wakorintho 7:33 32) “Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana; bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.”

Ukomavu wa akili:

Kuchumbia si jambo la kitoto. Ni jambo linalohitaji waliokomaa akili. Wakati fulani kuchumbia kunahitaji kufikia kiwango fulani cha kujitegemea kwa ama kuwa na kazi ya kuajiriwa ama ya kujiajiri ili kuweza kumya mchakato wa ndoa hapo baadaye. Hata hivyo kutokuwa na ajira hakuzuii mchakato wa uchumba kuanza ikiwa wahusika wamejibainisha kuwa wamekomaa akili na viungo na wanao mpango kazi wa maisha. Kukomaa kiakili kinahusisha uwezo wa kujitambua wewe ni nani, unataka kufikia malengo gani maishani, na mpango kazi unaotembea nao sasa ni upi ili kufikia malengo hayo. Katika mpango kazi kutaonekana lini unataka kuoa ama kuolewa, lini utaanza mchakato wa uchumba, unataka ndoa yenye watoto wangapi, lini unafikiria kufikia ukomo wa kuzaa, na mipango yako mingine ya kujiendeleza kielimu na kiuchumi.

Dalili za ukomavu wa akili

Kushindwa kuonesha mpango kazi wa kufikia ndoto zake za maisha kutaashiria kuwa mhusika hajakomaa kiakili na hivyo hajawa tayari kwa mchakato wa uchumba. Kutokomaa kwa akili kutadhihirika pia kwa njia ya mhusika kutoweka bayana ni yupi hasa anampenda na vigezo anavyotumia. Wapo wanaouchumbia kila msichana anayevutiwa naye na wako wanaochumbiwa na kila mvulana aliye maarufu. Na wengine hufikia hatua ya kuwa na wachumba zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Akili iliyokomaa na iliyotulia haiwezi kufanya kazi ya kubahatisha kama hiyo. Akili iliyokomaa na iliyo makini ina malengo sahihi, yenye mikakati sahihi na vigezo sahihi. Akili iliyokomaa na iliyotulia haikurupuki kufanya uteuzi wa mchumba bila kufikiria. Na akili iliyokomaa na iliyotulia haitoi taarifa zote za uchumba wake kwa kila aliye rafiki yake. Akili iliyokomaa inajua kutunza siri.

Wasiokomaa akili huigiza maisha

Mwenye akili iliyokomaa haigizi Maisha. Hutumia fedha kwa uangalifu na kupanua wigo wa vyanzo vya mapato. Mwenye akili iliyokomaa hatapanyi fedha ili kuhadaa watu kuwa fedha siyo tatizo kwake wakati ukweli wa mambo ni kuwa fedha ni bidhaa adimu. Mwenye akili iliyokomaa hana sababu ya kuazima mavazi ili kuwahadaa watu kuwa yeye ana uwezo wa kubadili mavazi wakati hali yake ya uchumi ni duni. Mwenye akili iliyokomaa akikataliwa na anayemtaka haendi moja kwa moja bali hurudi tena na tena kujiridhisha kama jibu alilopewa lilikuwa la mwisho au bado kuna nafasi. Hata vikwazo vikitokea, mwenye akili iliyokomaa atasimama na mchumba aliyemchagua na kuwa tayari akamilishe jukumu linalokawisha kufungwa kwa ndoa. Hatakatishwa tamaa na maneno ya watu au vikwazo kutoka kwa wazazi.  

Ziishi ndoto zako:

Mwenye akili iliyokomaa haogopi kufanya jambo lenye manufaa hata kama machoni pa vijana wenzake litaonekana linamshusha. Kwake jambo la muhimu ni lile linalomwongezea uwezo wa kiuchumi ama kielimu. Kijana aliyekomaa kiakili anajua kudunduliza kila anachopata. Anauangalia wakati ujao na anatafuta mbinu za kuukabili. Kijana mwenye akili zilizokomaa anaziishi ndoto zake. Haishi kwa ajili ya leo tu. Anatembea katika mpangokazi wake. (Mhubiri 11:9) “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.”

Ukomavu wa kimwili

Kukomaa kwa akili si lazima kuendane na umri wa mtu. Wapo ambao akili zao hukomaa mapema kuliko umri wao. Na wapo ambao akili hukawia kukomaa tofauti na umri wao.  Kwa hiyo kigezo cha ni umri upi unafaa kunza mchakato wa uchumba itategemea sana akili ya mchumbiaji na mchumbiwa. Hata hivyo kwa kawaida umri unaotarajiwa mtu azungumzie uchumba ni kuanzia miaka 24. Inaweza kuwa mapema kidogo kuliko hapo au miaka michache mbele. Umri huo unashabihi mtu aliyesoma bila kukwama kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu. Katika umri huo akili ya kawaida huwa imefikia hatua za kuanza kukomaa. Moja ya majukumu makubwa ya ndoa ni mwanamke kuzaa watoto na mwanaume kuhangaika kutafuta riziki kwa ajili ya familia. (Mwanzo 3:16) “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” (Mwanzo 3:17-19). “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.”

Mchumba mwenye mahusiano na Mungu:

Jiulize, Je, mtu ninayetaka kuoana naye ana mahusiano gani na Mungu wake. Anamtambua Mungu kama ndiye chanzo cha mafanikio yake na anajua kile Mungu alichowekeza kwake na mpango anaotarajia autimize maishani? Na je, yeye anaishi katika huo mpango wa Mungu na anashirikiana naye ili kuufanikisha? Na je, anajua kuwa Mungu atamuwajibisha kwa kutoishi kulingana na mpango na uwekezaji alioufanya kwake? Ikiwa hana uelewa juu ya jambo hili muhimu huyo hajakidhi kigezo cha uchumba. Anahitaji kuendelea kusubiri ili hali yake ya kiroho ikomae. (Mhubiri 11:9) “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.” Mhubiri anaposema “ukaziendee njia za moyo wako” anamaanisha ukaishi kulingana na mpango wa maisha ulio nao. Ni lazima ujihoji ulikuja duniani kwa kusudi gani. Swali hilo litakuelekeza katika kutambua mambo ambayo Mungu amewekeza kwako na ambayo alitaka uyatumie kwa kuokoa na kubariki wengine na kumpa yeye utukufu. 

Chagua mchumba anayempenda Mungu

Wasiofanana hawawezi kutembea pamoja. (Amosi 3:3) “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?” Hali kadhalika mpagani hawezi kwenda njia moja na Mkristo. Mungu anawaagiza vijana na watu wazima kutooana na wasio wa imani moja nao. (2 Wakorintho 6:14) “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza.” Mfalme Sulemani pamoja na hekima yote aliyojaliwa na Mungu wanawake wa kipagani aliowaoa walimgeuza naye akaanza kuabudu miungu migeni. (1 Wafalme 11:4) “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”

Hata Samsoni alipokataa ushauri wa wazazi wake waliomkataza kuoa mpagani aliishia kung’olewa macho baada ya mkewe kumsaliti na kutoa siri ya nguvu zake kwa adui. (Waamuzi 16:20) “Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.” Laiti angesikiliza ushauri wa wazazi wacha Mungu huenda hayo yote yasingemfika.

Faida ya kutofungiwa nira na wasioamini

Faida ya wanandoa kuwa kwenye imani moja ni kuwa matukio ya kiroho yanayowahusu ninyi wenyewe na watoto wenu mtakuwa mkishiriki pamoja. (Luka 2:27-28) “Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema.” Walio kwenye imani moja husaidiana kiroho walio imani tofauti hupingana. (Mhubiri 4:9-10) “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!”

Aliyeoana na asiye wa imani moja naye ni kama aliye peke yake. Atakuwa na wakati mgumu kuilinda imani yake na Imani ya Watoto wake. Vijana wa Kiadventista mnahimizwa kuoa na kuolewa na wenzenu waliopo kanisani. Msijaribiwe kuoa huko nje, waliojaribu kufanya hivyo wamefikwa na matatizo mazito ya kuhuzunisha na sasa wanajutia maamuzi waliyoyafanya. Usikubali kumchumbia asiye na hofu ya Mungu au asiye wa imani moja na wewe. Anayempenda Mungu wako atakupenda na wewe pia.

Usioe na kuolewa mapema:

Mwanamke anayeolewa na kuzaa mapema anahatarisha afya yake kwa kuwa viungo vyake vinakuwa havijakamilika kuweza kuhimili mikiki mikiki ya kujifungua. Wengi ama hufa ama kupata maradhi au kusababisha matatizo kwa watoto wanaozaliwa wakati wa kujifungua. Wazazi wenye tabia ya kuwaoza watoto wao wangali wadogo waache mila na utaratibu huo maana unawanyima watoto wao haki ya kufurahia ndoa. Ukomavu wa viungo huenda sambamba na usalama wa viungo vyenyewe – na hasa viungo vya uzazi. Viungo vya uzazi vikitunzwa vyema huwa salama wakati wa uchumba lakini visipotunzwa huathirika kwa njia ya maambukizo na hatima yake ni kupata ulemavu wa kudumu au maradhi yasioyoponyeka. Maradhi kama ya saratani ya shingo imegundulika kuwa huweza kusababishwa na kujamiiana katika umri wa utotoni. Kanuni ya msingi kwa wavulana na wasichana ni kutoyachokoza mapenzi mpaka wakati muafaka utakapofika. (Wimbo Ulio Bora 2:7) “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”

Wazazi washauriane na watoto wao:

Wazazi wawajibike katika kuwasaidia Watoto wao kukabili Maisha ya kujitegemea kwa kushauriana nao na kuwawekea akiba kwa ajili ya gharama za ndoa na Maisha mapya.  Wazazi wengine wamelaumiwa kwa kutumia fursa ya mabinti zao kuolewa kwa kuwachagulia wachumba wa kuwaoa kinyume cha matakwa yao. Mara nyingi vigezo vinavyoangaliwa ni uwezo wa kiuchumi (mahari) au kabila la muoaji kuliko sifa zingine za msingi. Huo ni ubinafsi unaoangalia faida ya wazazi pekee bila kuzingatia matakwa ya waoanaji. (Mwanzo 31:14) “Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je! Imetubakia sehemu au urithi katika nyumba ya baba yetu? Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa?” Hilo halipo sahihi na linapaswa kurekebishwa. Vijana wanaooana kwa shinikizo la wazazi huanza vibaya ndoa yao na uwezekano wa ndoa hiyo kudumu au kuwa yenye furaha ni mdogo.

Wazazi wasilazimishe mawazo yao:

Wapo na wazazi wengine wanaowaozesha vijana wao wa kiume kwa haraka ya kupata mjukuu. Kijana muoaji anaendelea kuishi kwa wazazi na mkewe na kupangiwa shughuli za kufanya na wazazi wake. Hilo nalo haliko sawa. Ndoa ni taasisi inayojitegemea ikiwa na serikali yake na haipaswi kuingiliwa katika maamuzi yake ya kila siku. (Mwanzo 2:24) “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Ndoa za utotoni na zenye kulenga kujinufaisha kwa upande wa wazazi bila kuzingatia maoni ya waoanaji zinakiuka haki ya msingi ya wanandoa na ni chanzo cha migogoro mingi ya ndoa. Wazazi tujielekeza katika wajibu wetu wa kuwa washauri tu kwa watoto na si kulazimisha mawazo yetu. Pia tuendelee na jukumu la kuwaombea watoto wetu ili Mungu awape hekima katika maamuzi ya jambo hili nyeti. Wale ambao wameweka juhudi ya kutosha katika kuwaombea watoto wao wamevuna mafanikio.

Tatizo la ndoa zilizochelewa:

Tatizo la ndoa za utotoni linaonekana kuanza kutoweka na tatizo jingine linaloonekana kuja kwa nguvu kwa sasa ni la wavulana na wasichana wanaokawia kuoa na kuolewa. Limeanza kuwa jambo la kawaida kuona wavulana na wasichana wenye miaka 35 hadi 45 ambao hawajaoa na kuolewa. Baadhi yao hata hawajui wataoa na kuolewa lini. Kwa sehemu haya ni matokeo ya vijana kuwa katika masomo kwa muda mrefu ama kutafuta kujiimarisha kwanza kiuchumi kabla hawajachukua hatua hii nyeti.

Kukosa uaminifu:

Lakini nyuma ya madai hayo kuna uwezekano mwingine wa mambo yasiyofaa yanayoendelea kwa baadhi ya vijana hawa. Yapo madai kuwa wapo vijana wanaoendelea kujamiiana wakati wanaendelea na masomo na hata baada ya kumaliza masomo na hivyo hawaoni haja ya kuoa na kuolewa kwa sasa. Madai haya yakiwa ya kweli basi kuna janga linalozijia familia za vijana hawa pindi watakapoamua kuoa na kuolewa. Itakuwa vigumu sana kwao kuvunja mazoea hayo wakiingia kwenye ndoa zao. Tunawashauri vijana kujiepusha na mazoea hayo ya kujamiiana kabla ya ndoa. Mahusiano ya mvulana na msichana yazingatie ushauri Mungu anaoutoa kwao. (1 Wakorintho 7:1). “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.”

Usikate tamaa:

Vijana wanaosumbuliwa na majaribu na walioangushwa katika majaribu hayo, Yesu anawaalika waje kwake. (Mathayo 11:28) “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Anaahidi kuwasamehe kabisa na kuwapa nguvu mpya. (Isaya 43:25) “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.” Jambo muhimu ukisamehewa ni kuamini kuwa upo huru. Mungu akikusamehe hakumbuki. Na ukisamehewa unaanza ukurasa mpya wa matengenezo. Hurudii matapishi. Unasonga mbele. Mtu aliyekomaa kiroho anatambua kuwa uwezo wa kutenda mema hautokani na uwezo wake. Ni neema ya Mungu. (Yeremia 10:230) “Ee Bwana, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.”

Mungu ni rafiki yako:

Mungu ametuchagua wanadamu tuwe marafiki zake pamoja na kutambua udhaifu wetu. (Yeremia 31:3) “Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.” Na pamoja na kushindwa kwetu mara nyingi Mungu anaahidi kuwa hatatuacha. Mungu akiahidi kitu kwako habadilishi. Aliwaahidi uzao wa Ibrahimu ahadi na ametimiza. (Mwanzo 28:15)  “Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” Moja ya mambo ambayo Mungu amewaahidi wanaotaka kuoa na kuolewa ni kuwapatia wenzi wa maisha. (Mithali 19:14) “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” (Mwanzo 2:22-23) “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”

Ujue mpango wa maisha yako:

Kila binadamu aliyekuja duniani ana mpango maalumu ambao Mungu amekusudia autekeleze kwa manufaa yake mwenyewe, kwa manufaa ya wanadamu wenzake, na kwa utukufu wa Mungu. Jukumu la binadamu ni kutambua mpango ambao Mungu ameukusudia kwake na uwekezaji ambao Mungu amefanya kwake ili kufanikisha mpango wenyewe. Tunapotambua mpango wa maisha yetu na kutambua na yale Mungu aliyotupatia kufanikisha mpango wa maisha yetu, na kuwa tayari kushirikiana naye katika kufikia malengo hayo ndipo tunapoweza kufikia mafanikio makubwa sana maishani. (Mwanzo 24:13-14) “Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.” Tafuta muda maalum wa kufunga na kuomba ukimuuliza Mungu amepanga nini juu ya Maisha yako.

Mungu anamfahamu atakayekufaa:

Moja ya maeneo ambayo Mungu anataka ufanikiwe ni katika mpango wa ndoa. Ndoa na familia ni msingi wa kujenga jamii iliyo bora na yenye mafanikio. Mungu alitoa ndoa kama zawadi kwa mwanadamu kwa sababu alijua anahitaji ndoa – anahitaji kuwa na mwenzi wa maisha mwenye kumtosheleza pale alipopungua. Ndoa ni kama timu ya mpira ambapo mafanikio huja kwa wachezaji wa nafasi mbalimbali wanaposhirikiana. Na kama ilivyo katika timu ya mpira wachezaji wa nafasi mbambali huchaguliwa na kocha wa timu. Hivyo Mungu anakuchagulia mwenzi wa maisha utakayeshirikiana naye kuleta ushindi wa timu yenu ya ndoa. Mungu amekuchagulia msaidizi wa kukufaa atakayekidhi yaliyopungua kwako. (Mwanzo 2:18) “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.”

Eneo pana la wadau wa uchumba:

Kuna watu wamefiwa na wenzi wao wa maisha na sasa ni wajane. Wanajiuliza waoe na kuolewa tena ama la. Kuna wale walioachika na waume zao au wake wao. Nao wanajiuliza tuone na kuolewa tena au la. Kuna wale wale ambao walizalishwa na kisha kutelekezwa nao wanajiuliza waolewe au wabaki wazazi wanaolea watoto peke yao (single parents) au la. Kuna wale ambao umri umeenda sana kiasi wanshindwa kujitambulisha upande wa vijana au upande wa wanandoa. Hizi ni changamoto ambazo lazima zitafutiwe majibu. Tunawahimiza hata wale ambao si vijana lakini wanahitaji wachumba kutumia fursa iliyopo kupata wachumba kwa kadri Mungu atakavyowaelekeza.

Mungu atakusaidia:

Mungu anajua hali mbalimbali wanazopitia wanadamu na ana mpango wa kuwasaidia. Ikiwa Mungu ana mpango wa kukusaidia naomba usikate tamaa. (Isaya 41:10) “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” Wajane ambao wanajisikia kutaka kuoa na kuolewa tena wanashauriwa kufanya hivyo bila kusita. (1 Timotheo 5:14). “Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.” Na wale walioachika na ama kutelekezwa baada ya kuzalishwa nao waolewe. (1Wakorintho 7:8-9). “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.”

Kuchumbia ni haki ya kila mwenye vigezo:

Tunapozungumzia uchumba tunazungumzia makundi yote. Wale vijana ambao hawajazaa wala kuoa na kuolewa, wale ambao waliwahi kuzaa bila kuolewa na kuoa, wale ambao wamefiwa na kuachika, na wale ambao wanadhani wanaweza kuishi bila ndoa kutokana na kuendelea kulea machungu waliyoyapitia huko nyuma – hawa wote wanayo fursa ya kuchumbia wakitaka. Tatizo linalowakuta wengi kudhani kitendo cha kujitambulisha kuwa unahitaji mchumba ni aibu. Kuchumbia hakuna aibu yoyote. Ni haki ya kila mtu.  Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kuwepo watu wanaoratibu mipango hii ya uchumba. Viongozi wa kiroho na wazazi wa watoto wasilikimbie jukumu hili maana ni lao

Wazazi wanaolea watoto peke yao wanaweza kudhani hawahitaji tena kuolewa kutokana na machungu waliyoyapitia huko nyuma lakini huo siyo utatuzi. (Waefeso 4:26) “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” Wanachotakiwa ni kuchukua hatua za kusamehe na kujisamehe wenyewe na kuendelea na maisha. Kusamehe ni njia sahihi ya kuondosha uchungu moyoni. (Waefeso 4:31) “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” Maisha ili yakae vizuri yanahitaji timu ya mwanaume na mwanamke wanaoishi kama wanandoa. Matatizo yaliyotokea katika ndoa ya zamani si lazima kuwa yatatokea katika ndoa utakayofunga tena. Ukidumisha roho ya msamaha utaishi maisha ya amani. (Waebrania 12:15) “Mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”  

Kutojamiiana kabla ya ndoa:

Ni jambo bora kuoa na kuolewa na aliye bikira. Lakini dunia hii iliyojaa changamoto watu wenye sifa hiyo si wengi kama ambavyo ingetarajiwa. Hii na kwa sababu ya wengine kupitia changamoto fulani fulani za maisha. Jambo la muhimu ni kujua kisa kilicho nyuma ya kila mwenye tabia hiyo na kuona kama alijutia kosa hilo kuliko kutoa hukumu ya jumla. Wapo walioingizwa katika kuzalishwa katika mazingira yaliyokuwa magumu na wanajutia hali hiyo. Hawa wanaweza kuwa wachumba wazuri kama wale walio bikira na hata wakati mwingine kuwazidi. (2 Wakorintho 11:2) “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.”

Usitelekeze uliowaharibia maisha:

Ni wachache sana kati ya wale wanaopenda kuoa mabikira ambao wao wenyewe ni mabikira – yaani wamejitunza katika ujana wao. Na kwa hiyo sababu za kupenda kuoa mabikira zisiwe za ubinafsi. Iwe na wewe pia kweli ulikuwa mwaminifu. Ubinafsi mwingine ambao usingefaa uwepo ni ule wa kuwaharibia mabinti kadhaa usichana wao kwa kuwazalisha na halafu wakati wa kuoa unawaacha na kutafuta aliye bikira. Huo ni ubinafsi mbaya. Ikiwa kwa bahati mbaya ulimzalisha binti au ulimwingilia kwa kumuahidi kumuoa ni lazima utimize ahadi hiyo kwa kumuoa huyo huyo na si mwingine. Idadi ya watoto wa mitaani inayozidi kuongezeka inachochewa na idadi inayoongezeka ya wanaume wanaozalisha bila kutunza watoto wao au kuwaoa wazazi wa hao watoto. Ni jambo lenye uchungu mkubwa kukuta aliyeahidi kukuoa akikutelekeza na kuoa mwingine na huku pengine akikuachia ujauzito. Wengine wamejaribiwa kunywa sumu ili wafe au kutoa mimba na kuishia kuharibu kizazi chao au kupoteza Maisha yao.

Yesu akuwezeshe kushinda tamaa za ujanani:

Kuna uwezekano wa mvulana kutojiingiza kwenye vitendo vya ngono kabla ya kuoa na kuna uwezekano wa msichana kuwa bikira katika jamii yenye maadili mabovu. (Mwanzo 39:12) “Huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.” Hilo linawezekana kwa vijana wanaojitambua na kujiheshimu ambao wameweka nadhiri ya kutomwangalia msichana au mwanamke kwa kumtamani. (Ayubu 31:1) “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?”

Msichana anayeishi kwenye ndoto zake huvuta Subira huku akimtegemea Yesu kushinda tamaa za ujanani. (2 Timotheo 2:22) “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.” Mungu ana kusudi la kukuleta hapa duniani na wala hujaletwa ili utumike kama chombo cha kuburudisha wengine ambao baada ya kukutumia wanakutupa kama kitu kisichofaa. Je ungependa uwe mama wa aina gani kwa watoto wako? Kumbuka kile unachokifanya sasa kina uwezekano wa kuigwa na watoto wako. Je, ungependa wanao warithi tabia gani kutoka kwako? (Mwanzo 24:15-16) Ukitafakari hayo na kisha ukaomba msaada kwa Yesu hakika Mungu atatimiza ndoto yako. Biblia imejaa mifano mingi ya wasichana mashujaa wa jinsi hiyo. “Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.”

Chunguza tabia yake kwa umakini mkubwa

Tabia ndiyo kigezo muhimu katika kuchagua mchumba anayefaa. Tabia hueleza yote kuhusu hali ya mhusika. Tabia hueleza kama mtu anajitambua au bado yupo usingizini. Tabia hueleza kama mtu anamjua Mungu na kumuogopa ama hana dira ya maisha. Tabia hufunua hali ya mtu kama ni mtu anayetegemea neema ya Mungu katika kufikia ukamailifu ama ni mtu anayejihesabia haki na asiyekubali makosa. Tabia hufunua hali ya mtu kama anaweza kuchukuliana na hali zote za maisha zinazoletwa na kupanda na kushuka kiuchumi, kiafya, kimahusiano, na kadhalika au ni mwepesi wa kukata tamaa na kutosimama kwenye maagano mambo yanapogeuka kuwa magumu. Tabia inadhihirisha kama mtu anajua kupenda na yupo tayari kukabili gharama za kupenda au anasukumwa na misisimko na hamu ya kukidhi matamanio ya mwili tu. Tabia ndiyo kitu muhimu katika mchakato wa kutafuta mchumba. Kama utamchunguza msichana au mvulana uliyemtamkia nia ya kumchumbia basi tambua kuwa hutakaa ufahamu tabia yake.

Umri ufaao kuchagua mwenzi

Kuchagua mwenzi hufanyika mtu anapofikia umri wa kujitambua na pale anapoona hitaji la kuwa na mwenzi. (Mwanzo 2:20) “Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye.” Ili mtu awe amekidhi vigezo vya kuoa au kuolewa ni lazima awe amefikia umri wa miaka 18 unaotambuliwa kwa mujibu wa sheria. Katika umri huu mvulana aliyepangilia vyema mambo yake na ambaye hana kiu ya kuendelea na masomo, anaweza kuwa amefikia uwezo wa kujitegemea. Na kwa msichana umri huu unaweza kuwa umemfikisha katika hatua ya viungo vilivyokamilika na mwili wenye utimamu unaoweza kuhimili majukumu ya uzazi.  

Umri wa kawaida wa kuoa na kuolewa

Lakini ili kuwa katika nafasi nzuri ya kuepuka madhara yatokanayo na ndoa za utotoni inashauriwa vijana waanze kufikiria kuoa na kuolewa baada ya miaka 22 muda ambao kwa wale waliokuwa masomoni wamehitimu na wengine wameshajiajiri au wameajiriwa. Kuanza michakato ya uchumba kabla ya umri huo ni kuyachokoza mapenzi kabla ya wakati wake jambo ambalo linapingwa viakali na Maandiko Matakatifu. (Wimbo Ulio Bora 2:7) “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.”

Kuoa na kuolewa mapema au kwa kuchelewa

Msichana anayeolewa mapema sana anahatarisha afya ya uzazi kutokana na changamoto nyingi za uzazi zitokeazo siku hizi. Na msichana anayekawia kuolewa anakaribisha changamoto zinazoweza kuharibu furaha ya Maisha yake yajayo. Kuwahi kuoa kwa mvulana pia kuna changamoto zake kwani kuna uwezekano wa kuwapo maandalizi ambayo hayajakamilika. Majukumu hayo ni pamoja na kujua wapi mtaanzishia familia yenu (makazi) na njia za kujikimu na maisha kutokana na ukweli kuwa walio kwenye ndoa hawapaswi kutegemea tena wazazi kwa mahitaji yao ya msingi kama chakula, malazi, mavazi, matibabu na kadhalika.

Ukiwa na vigezo usichelewe kuoa

Mvulana aliyetimiza vigezo vya umri na mwenye shughuli inayomuingizia kipato au mwenye mipango mizuri ya maendeleo hana sababu ya kuendelea kupoteza muda wa kuanza mchakato wa uchumba. Waswahili wanasema ukitaka Kwenda haraka nenda peke yako lakini ukitaka kufika mbali nenda na mwenzio. Mambo mengine hayawezi kukamilika mpaka uwe na mwenzi wa maisha. Ikiwa mtoto hana mwelekeo wa kutambua kuwa wakati wa kuoa au kuolewa umewadia wazazi washirikiane naye kufanikisha jambo hilo. (Mwanzo 24:4) “Bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.”

Sababu za kuchelewa kuoa

Sababu nyingine za kuchelewa kuoa ni kuogopa gharama za mahari na harusi, na gharama za Maisha kwa ujumla. Mtu hujiuliza kipi kitangulie kati ya kuoa na kupata kazi ya kujikimu na Maisha. Wengine umri wa kuoa umewakuta wakiwa hawana kazi na wanaishi na wazazi wao. Wengine sababu za kuchelewa kuoa ni Maisha yasiyo na usafi ya uzinzi yanayomfanya asione umuhimu wa kuwa na mwenzi wa Maisha. Hawa wenye kawaida hii huwarubuni wasichana kwa ahadi ya kuwaoa na wakishatembea nao au wakiwazalisha huwatelekeza. Kwa kawaida wote waanzao mazoea ya ngono nje ya ndoa hushindwa kuwa waaminifu katika ndoa zao na huendelea na tabia hiyo hata baada ya kupata wenzi wa maisha.

Sababu za kuchelewa kuolewa

Zipo sababu nyingi zinazofanya wasichana wachelewe kuchumbiwa. Hapa nitazungumzia baadhi ya sababu za kujitakia zilizopelekea baadhi ya wasichana kuchelewa kuchumbiwa na kuolewa. Wasichana wengine huchelewa kuolewa kutokana na kukamilisha njozi zao za Maisha za masomo au kazi ambazo huwanyima nafasi ya kuanzisha michakato ya uchumba. Wengine huchelewa kuolewa kutokana na kukataa wachumba wanaowataka kwa matarajio ya kumpata atakayekidhi kikamilifu vigezo vyake vyote. Wengine hupoteza wachumba waliofikiria kuwachumbia kutokana na kutumia kejeli na lugha za kashfa katika kuwakataa wachumba wanaowajia. Taarifa hizi husambaa na kuwakatisha tamaa waliokusudia kuwachumbia. Wengine huchelewa kuchumbiwa kutokana na kutojiweka wazi kuwa wanahitaji mchumba na kutokuwa karibu na yule wamdhaniaye angefaa kuwa mchumba wao. Wengine huchelewa kuolewa kwa kuwa kila wanayemkubalia uchumba hukataliwa na wazazi au walezi kwa madai kuwa hajakidhi vigezo vyao.

Mwenendo unaoweza kuchelewesha kuolewa

Sababu nyingine ya kuchelewa kuchumbiwa ni tuhuma zilizozagaa zingine zikiwa za kweli na zingine zisizothibitishwa kwamba binti au mvulana fulani ana tabia mbaya. Mabinti wengine wamezushiwa kuwa ni malaya eti tu kwa sababu ana mazoea na wavulana bila kujua kuwa wapo wasichana wanaofanya hivyo si kwa sababu ya umalaya. Wapo waliotuhumiwa kuwa ni walevi, wezi, wavutaji kwa sababu tu ya makundi wanayoshirikiana nayo. Kama watu wamekutuhumu kwa lolote baya na unajua hiyo itakuharibia sifa yako jitulize. Kama tabia hiyo unayo tubu na kwa msaada wa Mungu iache tabia hiyo. Na kama ni kwa sababu ulizalia nyumbani endelea kumlilia Mungu wako ili wanaokulaumu watambue ulifanya kwa ujinga na ya kuwa unajutia kitendo hicho na kwamba Mungu amekusamehe. Usigombane na watu. Wewe endelea kumtumaini Mungu naye atakupa haja za moyo wako.

Msichana anaweza kuchagua mchumba?

Swala la kuchagua mchumba kwa mujibu wa tamaduni nyingi huamuliwa na wanaume zaidi kuliko wanawake. Mwanamke anapompenda mwanaume ni vigumu kwake kumtamkia mwanaume. Anachoweza kufanya msichana aliyempenda mvulana ni kuongea kwa lugha ya vitendo. (Mwanzo 24:19, 20, 22) “Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu.”

Uchumba uliokidhi vigezo

Kuoa au kuolewa ni jambo nyeti sana linalohitaji umakini kulipangilia. Ukihisi umefikia wakati unaohitaji kupata mchumba utakayefunga naye ndoa, ongeza umakini. Hakikisha umemshirikisha Mungu kwa kila hatua. Usikurupuke ukamvamia ambaye Mungu hakuwa amekupangia. Mungu wako anakujali na amekuandalia mtu mtakayechukuliana naye. Unachotakiwa ni kumwomba kwa dhati akuoneshe mwenzi aliyekuchagulia. Kumbuka mke mwema mtu hupewa na Bwana. (Mithali 31:10) “Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.” Adamu alipohitaji mwenzi wa Maisha Mungu alimpa usingizi. Mke mwema hupatikana usingizini. Tulia acha kuhangaika huku na huku ukitafuta mtu wa kuoa. Mchumba wako utaletewa hapo ulipo katika mazingira usiyotarajia. Mungu anakuomba umshirikishe ili akusaidie kupata mwenzi mwema.

Mungu atakuongoza kupata mwenzi wa Maisha

Eneo muhimu na linalohitaji umakini wakati wa kufanya uchumba ni aina ya mtu unayemchumbia. Lazima ujiridhishe kuwa unayechumbiana naye ndiye hasa chaguo la moyo wako na anakidhi vigezo vya maisha unayokusudia kuishi huko mbeleni. Wakati wa kufunga ndoa swali moja linaloulizwa kwa kurudiarudia na kwa kubadilisha maneno ni lile linalotaka kufahamu kama mchumba uliyemchagua ulimchagua mwenyewe kwa hiari na utakuwa tayari kuishi naye siku zote na katika hali zote.

Mungu anajua mwenzi wako wa Maisha ni nani, yupo wapi kwa sasa, na atamleta lini karibu nawe ili muanzishe na kukamilisha mchakato wa uchumba.  (Kutoka 2:16-21) “Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.” Musa hakuwa na mahari wala fedha za kutoa. Inawezekana kama unamwamini Mungu. (Zaburi 37:4) “Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.”

Utajuaje kuwa anakupenda

Lakini muhimu zaidi ni kujua upendo ulio nao kwa mchumba wako ni wa kweli ama wa bandia. Upendo wa kweli unadumu. Upendo wa kweli hauvutiwi na mali na mwonekano wa nje peke yake. Ni dhahiri kuwa wavulana wengi huvutiwa na mwonekano kabla ya kitu kingine, wakati wasichana wengi huvutiwa na mafanikio ya mvulana na wakati fulani sura yake. Hivi si vitu vibaya lakini havipaswi kuwa vipaumbele. Jiulize unampenda mchumba wako kwa dhati au kwa msisimko tu? Mtu anayekupenda yupo tayari kuingia gharama na kujitoa mhanga kwa ajili ya mafanikio yako. Upendo wake kwako si wa kulazimisha bali ni ule wa kiutumishi. Hufurahia kuwa karibu nawe na kufurahia kila unachofanya na unapokosea hujitolea kukutetea na kukuombea msamaha.

(Mwanzo 29:4-11) “Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, watu wa wapi ninyi? Wakasema, Tu wa Harani sisi. Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua. Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo. Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha. Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo. Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye. Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia.”

Chumbia anayekuvutia

Kigezo cha pili muhimu cha mchumba anayefaa ni yule anayekuvutia. Kwa kawaida kila binadamu ana kitu fulani katika tabia yake au maumbile yake kinachomvutia mtu fulani aliyekusudiwa na Mungu. Usijaribiwe kumchumbia usiyempenda kwa sababu unamhurumia kwa hali aliyonayo. Usijilazimishe kuoana na usiyempenda ama kwa sababu ya kumhurumia, kwa sababu ya kuwaridhisha watu fulani au kwa sababu ya kutafuta faida fulani ya kitambo tu. Viapo vya siku ya ndoa vimewekwa ili kuthibitisha kama mnaoana kwa hiari mkisukumwa na upendo peke yake. Zimekuwepo siku hizi ndoa zinazodumu kwa muda mfupi kama hiyo moja niliyowahi kufunga iliyodumu kwa chini ya mwezi mmoja. Inakuwa kama watu wanafanya mzaha na ndoa. Vijana acheni kutafuta sifa ya kuwa mmefunga ndoa na kumbe mna mpango wa kuachana baada ya muda mfupi. (Waebrania 13:4) “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.”

Usioe na kuolewa kwa kusukumwa na mihemko

Usioe kwa kuwa umeshindwa kujizuia na tamaa ya ngono. Huyo unayechanganyikiwa kwa ajili ya uzuri wake wa usichana hatabaki katika hali hiyo hiyo siku zote. Utakuja wakati atakapokuwa wa kawaida sana je bado utakuwa unampenda? Usimpende kwa misisimko au mihemko inayosukumwa na tamaa za mwili bali usukumwe na upendo halisi utokao moyoni unaomkubali mtu jinsi alivyo. Yule ambaye Mungu amekuchagulia utamtambua kwa kuona upendo ndani yake; upendo unaokuelekea wewe ukiwa na makusudi ya dhati, ya kudumu, na yasiyofichika. Upendo huo siyo mpofu usioruhusu akili kuchambua na kujiridhisha. Ni upendo usio na haraka, usiolazimisha na usiotafuta faida zake wenyewe. (Waefeso 3:17) “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo.”

Vigezo vingine muhimu vya mchumba afaaye

Mchumba akiwa anampenda Mungu na wewe mwenyewe uwe pia unampenda huyo mchumba hiyo inatosha kukuhakikishia kuwa yeye ni mchumba mwema mradi Mungu awe amekuonesha kuwa huyo ni wako. Kutegemea ndoto au ishara katika kumtambua mchumba ambaye Mungu amekuchagulia si salama katika kizazi hiki cha udanganyifu. Mahusiano yako ya karibu na Mungu, yanatosha kukufanya umfahamu yule aliye wako hasa. Vigezo vingine vya kimo, kabila, utaifa, rangi, elimu, umri, hali ya kiuchumi na kadhalika si muhimu sana katika kuamua mchumba afaaye ingawaje wakati fulani huweza kusaidia. Hata hivyo inashauriwa tofauti ya mambo hayo isiwe kubwa kiasi cha kuathiri maelewano na ukaribu katika ndoa. (Amosi 3:3) “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?”

Moyo mdanganyifu

Kwa nini Mungu amejichukulia jukumu hili la kuwachagulia wanadamu wachumba? Je, ana kusudi la kuwanyima uhuru wao wa kuchagua wampendaye? La, hasha. Mungu anajua kuwa maamuzi yetu ya kibinadamu yanaharibiwa na uwezo hafifu wa mioyo yetu katika kupima mambo. Mioyo yetu ni midanganyifu. “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” (Yeremia 17:9) Ni rahisi mwanadamu kudanganyika kuwa unapenda au unapendwa wakati kiuhalisia sivyo ilivyo. Kuna wengi wamelizwa na wachumba wao. Wavulana wamelizwa na wasichana nao wamelizwa. Baada ya kupotezeana muda kwa ahadi tamu tamu wamekuja kuachana ghafla jambo lililoleta maumivu ya kutisha. Wengi katika hatua hiyo wamekiri hawakuwajua vizuri wachumba wao. Na wengine waliachwa hata na wachungaji! Mchumba mzuri hatokani na kazi anayofanya bali na jinsi alivyo.

Usitegemee ushauri wa wanadamu:

Usitegemee wanadamu katika kufanya maamuzi hasa yanayohusu uchumba. “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.” (Yeremia 17:5). Mtu anayekufaa wewe alishaandaliwa na Mungu kitambo wakati ukiwa huna taarifa yoyote. Kabla wewe hujazaliwa na yeye hajazaliwa. Hata mke wa Adamu aliandaliwa, yeye Adamu akiwa usingizini. “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.” (Mwanzo 2:21-22)

Washirikishe watu makini unapohitaji mwenzi

Swala zito kama uchumba linahitaji kushirikisha watu makini wenye kukutakia mema. Wajulishe wazazi na kuwauliza ushauri wao. Pima ushauri wao na kama unalingana na mashauri ya Mungu uuchukue. Viongozi wa kanisa, marafiki na jamaa wengine utakaowahusisha hakikisha wana sifa ya kuwa watu makini wenye kukutakia mema na wamchao Mungu. Itakapotokea ushauri wa watu hao unapingana na maagizo ya Mungu chukua tahadhari. Mshirikishe zaidi Mungu kwa kuwa na maombi ya dhati ya mara kwa mara huku ukichukua hatua ya kufunga katika siku kadhaa. Mungu atakuelekeza cha kufanya katika kila hatua na hasa pale inapojitokeza changamoto.  (Mithali 3:5) “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” Ibrahimu alipotambua Isaka amefikisha umri wa kuhitaji mwenzi alimshirikisha kijana aliyemwamini miongoni mwa watumwa wake. (Mwanzo 24:2-4) “Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.”

Washirikishe wazazi:

Wazazi wana nafasi katika kutoa ushauri juu ya yule utakayemuoa au utakayeolewa naye. Lakini hawapaswi kulazimisha mawazo yao. Mwisho wa yote atakayeoa ndiye anayefanya uchaguzi wa mwisho. Ingawa Isaka hakushiriki katika mchakato wa kuchagua lakini aliridhia chaguo alilofanyiwa na mtumishi wa baba yake. Na Rebeka naye ingawa alimkubali Isaka wakati hajamuona, bado alipokutana naye aliridhika kutoka moyoni mwake. (Mwanzo 24:64-67) “Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”

Washirikishe viongozi wa kiroho:

Viongozi wa kiroho wana nafasi muhimu katika kuwahimiza vijana kuoana na katika kufanya chaguzi sahihi za wenzi wa Maisha. Si vijana wote wenye uelewa wa kile wanachopaswa kufanya umri wa kuoa au kuolewa unapokuwa umefika. Wengine wana changamoto ya kushindwa kujieleza au kuwasilisha hitaji lake kwa mhusika. Wengine wamekiri kushindwa kujua vigezo sahihi vya mchumba afaaye, na wengine wameshindwa kufahamu dalili za mvulana ama msichana anayempenda na kwa kukosa kuzijua stadi hizo wamepoteza wachumba na kuchelewa kuoa ama kuolewa. Wazazi na viongozi wa kiroho wasilikwepe jukumu hili. Wakutane na vijana wao na wawape ushauri wa namna ya kufanikisha mchakato wa uchumba. Pamoja na ushauri wapate muda wa kuomba nao ili kuwasilisha changamoto zao kwa Yeye asiyeshindwa.   

Usisite kuvunja uchumba

Usisite kuvunja uchumba, utakapogundua kuwa kuna jambo litakalowaletea shida huko mbeleni kwa kuendelea na uchumba. Mambo hayo yaweza kuwa kukosa uaminifu, udanganyifu, maradhi ya kuambukiza na yasiyotibika nk. Ili kuepuka hatua hii ya kuvunja uchumba ambayo huleta maumivu kwa wahusika, kanisa limeweka utaratibu wa kwenda kupima afya kabla ya kuendelea na uchumba ili ikiwa mmoja wa wachumba ameathirika uchumba uweze kuvunjwa. (Mithali 22:3) “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.”

Jiepushe na zawadi

Hatua hii ni vema ichukuliwe mapema kabla ya kuwaona wazazi, ili kuepuka usumbufu wa kurudisha mahari na mambo mengine kama hayo. Usijilazimishe kuendelea na uchumba kwa kuwa ulipewa zawadi ambazo sasa zinakulazimu kukubali kuchumbiwa na usiyempenda tena. Ni afadhali kutafuta uwezekano wa kurudisha zawadi hizo (ikiwa mwenye kuzitoa amesisitiza zirudishwe) kuliko kujilazimisha kuolewa naye. Ili kutojiweka kwenye mtego wasichana na wavulana kujiepusha na zawadi. (Mithali 15:27) “Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.”

Ndoa isiwe yenye gharama kubwa

Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwazuia vijana wengi kuoa mapema ni gharama kubwa inayoandamana na mchakato wa kuoa. Gharama hiyo inasemekana huanzia kwenye mahari kubwa wanayotozwa wavulana na wazazi wa binti, gharama zinazoandamana na tukio la kufunga ndoa, na gharama za sherehe yenyewe ya ndoa. Malalamiko haya kwa sehemu yana ukweli. Kanisa limeendelea kuelimisha wazazi wa mabinti kutotoza mahari kubwa asiyoimudu mvulana anayechumbia. Pale inapowezekana mahari isingetozwa kabisa kwani ni kawaida ya kipagani. Viongozi wa makanisa mahalia wana wajibu wa kuingilia kati pale mchumba anapolalamikia mahari kubwa aliyotozwa ili isiwe kigezo cha wawili hao kushindwa kuoana.

Ndoa iwe rahisi kadri inavyowezekana

Tunawahimiza vijana kufunga ndoa rahisi isiyo na gharama na isiyo na sherehe za anasa. Ndoa yaweza kufungwa siku ya Sabato baada au kabla ya ibada na wanandoa wakarudi nyumbani baada ya ibada wakiwa ni mume na mke. Pale inapokuwa ni lazima kuweka sherehe, viongozi wa makanisa mahalia wahakikishe sherehe zinaisha mapema na zinafanyika kwenye maeneo yanayoleta utukufu kwa Mungu. (Isaya 3:16-23) “Bwana akasema tena, Kwa sababu binti za Sayuni wana kiburi, na kuenenda na shingo zilizonyoshwa, na macho ya kutamani, wakienenda kwa hatua za madaha, na kuliza njuga kwa miguu yao. Basi, kwa hiyo, Bwana atawapiga binti za Sayuni kwa pele za utosini, na Bwana ataifunua aibu yao. Siku hiyo Bwana atawaondolea uzuri wa njuga zao, na kaya zao; na pete za masikio, na vikuku, na taji zao; na dusumali, na mafurungu, na vitambi, na vibweta vya marashi, na matalasimu; na pete, na azama, na mavazi ya sikukuu, na debwani; na shali, na vifuko; na vioo vidogo, na kitani nzuri, na vilemba, na utaji.”

Kanisa lijihusishe katika uandaaji wa harusi

Maeneo ya kanisani yakiwekewa mandhari nzuri yanaweza kufaa kwa sherehe hizo kuliko kufanyia ukumbini ambako mara nyingi ni aghali na ambako uthibiti wake ni mgumu. Kamati za harusi zisiachiwe kuendesha sherehe za vijana wetu kwa kukiuka maadili ya kanisa na kwa kuweka bajeti kubwa isiyo ya lazima inayowafanya vijana wasio na uwezo kuhofia kufunga ndoa zao mapema au kuogopa kufungia kanisani. Wengine kwa kuogopa hali hiyo wameenda kufungia ndoa zao serikalini au wamechukuana bila ndoa. Matokeo yake idadi ya ndoa zinazobarikiwa kwenye makanisa mengine inazidi ile ya wanaofunga ndoa mpya.

Ndoa iwe na baraka za wazazi na kanisa

Ndoa ili itambulike kuwa imefungwa kihalali ikiwa na Baraka zote za Mungu, za kanisa, na za wazazi inahitaji wawili wanaooana na mashahidi wao, wakiwa katika mavazi yoyote ya heshima watakayoyachagua. Kuvaa shela au kutovaa, kuvalishana pete ama kutovalishana, kuwa na wasindikizaji au kutokuwa nao havileti tofauti yoyote. Adamu na Eva hawakuwa na vitu hivyo na bado ndoa yao ilidumu kwa muda mrefu sana. (Mwanzo 24: 57-61) “Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda. Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake. Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao. Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake.”

Tusiige wamataifa waendeshavyo michakato ya ndoa.

Kanisa siyo kisiwa na kwa hiyo haliwezi kujitenga kabisa na yote yatokeayo katika jamii. Hata hivyo tahadhari imetolewa kujiepusha na mitindo inayoibuka isiyo na sura njema katika jamii. Swala la ndoa namna inavyofanywa leo ina kila dalili kuwa imeingiliwa. Hatukuwa na Send off zamani lakini sasa zipo. Hatukuwa na shela, hatukuwa na pete, hatukuwa na kwaito, hatukuwa na shampaign, hatukuwa na kuweka make up, hatukuwa na mambo mengi ambayo leo hii yamo hasa katika ndoa zinazofungwa mjini.

Kumuaga binti

Ushauri hapa ni kuwa ikiwa ni lazima kumwaga binti basi sherehe isiwe kubwa mno ikiwahusisha ndugu wachache wa karibu na ikiwezekana ifanyikie nyumbani. Lengo hapa liwe kumpatia binti wosia ambao pengine usingefaa kutolewa siku ya harusi juu ya namna ya kudumisha maadili mema aliyojifunza akiwa hapo nyumbani. Jambo hilo likifanyika kiroho si tu kwamba litawaongoa waliohudhuria bali litawafanya kutamani kuiga na hivyo kuwa jambo lenye mbaraka kwa wengine. Hata hivyo mara nyingi imeonekana sherehe hii ya kumwaga binti inafaa sana ikifanyika mara baada ya kufunga ndoa na si kabla. Kuifanya mapema kabla ya ndoa hakuleti maana nzuri. Makanisa yaendelee kulitolea elimu jambo hili. (Mwanzo 24:53-54) “Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia. Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.”

Ndoa iwe na utukufu wa Mungu

Ufungaji wa ndoa na sherehe za harusi vithibitiwe na makanisa mahalia yakishirikiana na wazazi wa maharusi ili kuzuia kuwepo kwa mambo yatakayoondoa utukufu wa Mungu. Mavazi ya maharusi na wasindikizaji wao, ni lazima yawe ya adabu na yanayosetiri mwili. (1 Timotheo 2:9) “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani.” Mazoea ya kuruhusu vigelegele vipigwe na kuwa na mshereheshaji anayetoa maelezo ya nani anaingia na amepndeza kiasi gani, vinashusha utukufu wa ibada ya ndoa. Ifahamike kuwa ile inayofanyika pale kanisani ni ibada kamili ya ndoa yenye kicho kama ibada zingine zote. Hapatakiwi vigelegele, na mambo mengine yanayofukuza uwepo wa Mungu. (1 Wakorintho 14:40) “Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu.”