Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

YESU ANATOSHA

YESU ANATOSHA

Anguko la dhambi lilimuweka mwanadamu mahali asipoweza kujipigania kwa kuwa alipoteza uwezo. Dhambi iliwafanya wanadamu kuendelea kupungukiwa na utukufu wa Mungu yaani uwezo wa kiroho na kimwili (Warumi 3:23). Kuundwa kwa taifa la Israeli kulibainisha kwa ukamilifu dhana hii ya kupungukiwa na uwezo. Taifa hilo la Mungu kila mara lilishindwa vitani na maadui zake pale lilipotegemea uwezo wa kibinadamu na kuacha kutegemea uwezo wa Mungu. Na kila uwezo wa Mungu ulipotumika taifa hilo lilipata ushindi (Kutoka 17:11).

Hata pale Mungu alipowainua waamuzi na wafalme mahodari, uhodari wao ulidumu kwa muda mfupi nao wakashindwa vibaya mbele za adui zao kwa kuwa walikuwa dhaifu (1 Samweli 4:2, 10; 2 Samweli 18:7). Waliweza tu kushinda pale walipotambua kuwa hawana uwezo wa kupigana na kuchagua kumtegemea Mungu pekee (2 Nyakati 20:10-12). Mara kwa mara Mungu aliwakumbusha kuwa vita hiyo tangu siku alipowatangazia kuingilia kati anguko lao haikuwa yao isipokuwa ni ya Bwana (2 Nyakati 20:15; 1 Samweli 17:47). kwa kutegemea uwezo wa Mungu na si kwa kutegemea uwezo wao.

Mmojawapo wa waamuzi aliyeonekana kurejesha matumaini ya ushindi wa taifa kubwa la Israeli alikuwa Samsoni. Samsoni alikuwa na uwezo wa mwili usio wa kawaida (Waamuzi 16:3). Lakini naye alishindwa vibaya na kutobolewa macho na Wafilisti mahasimu wao wa muda wote (Waamuzi 16:20-21). Baadaye Mungu alimuinua mfalme Suleimani aliyejaliwa uwezo wa hekima awaongoze Israeli (1 Wafalme 4:29). Hata naye alishindwa vibaya pale wake zake walipomgeuza moyo (1 Wafalme 11:3-4).

Yesu alipokuja aliwadhihirishia wasikilizaji wake na wanadamu wote kuwa yeye ndiye aliye mkuu zaidi ya Samsoni na zaidi ya Sulemani (Luka 11:30-31). Kwa maana ya kuwa Yeye anao uwezo wa kiroho ulio wa muhimu sana katika kushinda pambano kuu la nyakati zote kati ya giza na nuru, kati ya wema na uovu na kati ya kweli na uongo. Yeye ndiye mwanadamu mwenye uwezo aliyekuwa akisubiriwa. Yeye mwenyewe alisema pasipo mimi ninyi hamwezi neno lolote (Yohana 15:5).

Katika ahadi ya ukombozi iliyotolewa kwa Adamu alipotolewa bustanini, Mungu aliahidi kumtuma mwanadamu mwenye uwezo ulio bora Zaidi atakayeweza kumponda kichwa Shetani (Mwanzo 3:15). Kumponda kichwa Shetani ni kumshinda katika hila zake za kuwashawishi wanadamu kutenda dhambi. Yesu alishinda majaribu yote ya Shetani ambayo Adamu na mkewe Hawa walishindwa (Mwanzo 3:6). Walijaribiwa katika chakula. Walijaribiwa katika kutamani nafasi ya Mungu kama Shetani naye alivyotamani kukalia nafasi ya Mungu (Mwanzo 3:5; Isaya 14:13). Walijaribiwa na tamaa ya macho pia.

Yesu alipopandishwa na Roho ili ajaribiwe alishinda majaribu yote yaliyowaangusha Adamu na mkewe (Mathayo 4:1-11). Mwenyewe aliwauliza waliokuwa wakishindana naye waseme kama ana dhambi yoyote nao walikaa kimya (Yohana 8:46). Yesu hakuwa na dhambi. Alikuwa na uwezo wa kushinda dhambi kwa kuwa alijikabidhi kwa Mungu (1 Petro 2:23). Ikumbukwe kuwa Yesu alipofanyika mwili iliazimiwa asitumie uwezo wake wa kiungu kupunguza makali ya majaribu. Ilimpasa afananishwe na ndugu zake wanadamu vinginevyo asingetosha kukidhi vigezo vya kuleta upatanisho kati ya Mungu na wanadamu (Waebrania 2:17).

Ndiyo sababu Shetani hakupinga Yesu alipochukua nafasi ya Adamu kushinda majaribu yaliyoleta anguko kwa mwanadamu. Hakuna mwanadamu aliyemtoa jasho Shetani kama Yesu. Yeye ndiye pekee ambaye Shetani anamuhofu maana anajua uwezo wake. Na Yesu akijua kuwa Shetani amejitangaza kuwa ndiye mkuu wa ulimwengu huu kwa kuwa amewashinda wanadamu wote anatamba akisema kwake hafui dafu (Yohana 14:30). Alimshinda kwenye mechi ya nyumbani – mbinguni (Ufunuo 12:7-9) na amemshinda kwenye mechi ya ugenini – duniani (Yohana 19:30). Ile kauli kwamba hakuna mwanadamu hapa duniani ambaye afanya mema asifanye dhambi Yesu ameigeuza

Ushindi wa Yesu ni ushindi wetu. Anaposema nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani isidhaniwe anasema kama nafsi ya Uungu (Mathayo Anayasema hayo kwa niaba yetu. Aliyachukua masikitiko yetu na kujitwika huzuni zetu ambavyo havikumstahili ili kupitia kupigwa kwake sisi tupone (Isaya 53:4-5). Yesu anapowasilisha maombi yoyote kwa Baba anayawasilisha kwa niaba yetu kwa kuwa yeye yupo katika nafasi inayomhalalisha kuomba chochote maana ameshinda dhambi ambayo ni kikwazo kikuu cha wanadamu wote. Kile alichoahidiwa kama ujira kwa ushindi alioupata hajaahidiwa kama nafsi ya Uungu bali ameahidiwa kama Mwana wa Adamu anayewawakilisha wanadamu wote.

Neno alipotambulishwa kama Mwana wa Mungu wakati alipokuwa akichukua majukumu ya Adamu kama Mwana wa Adamu alitambulishwa pia kama Mzaliwa wa kwanza (Wakolosai 1:15-18). Anakuwa mzaliwa wa kwanza kwa kuwa amechukua nafasi ya uzaliwa wa kwanza kutoka kwa Adamu ambaye hakuitendea haki kama ilivyotarajiwa. Amekuwa mzaliwa wa kwanza kwa mfano wa Yakobo aliyeutwaa kwa Esau aliyedharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa dengu (Mwanzo 25:34). Adamu angeweza kuepusha dhambi isiingie ulimwenguni na kusababisha madhara tunayoyashuhudia kama angeitumia vizuri nafasi yake ya mzaliwa wa kwanza (1 Timotheo 2:13). Lakini akakubali kudanganywa na hivyo kupitia kwake dhambi ikaingia ulimwenguni (1 Timotheo 2:14). Na badala ya kumuombea msamaha mkewe Hawa yeye mwenyewe akashiriki dhambi na kumtupia lawama Hawa na Mungu aliyemleta kwake (Mwanzo 3:6,12).

Yesu aliye Adamu wa pili au Mwana wa Adamu alifanya kile ambacho Adamu hakuweza kufanya cha kumtetea mwanadamu, kuchukua nafasi ya kumpatanisha na Mungu na kwa kuchukua adhabu ya kifo iliyomstahili, na kushinda majaribu yote ya Shetani aliyoshindwa kwa niaba yake. Hali hiyo ilimfanya awe mwanadamu wa kwanza wa aina yake kutegua kitendawili kilichokuwa kikiwaelemea wanadamu cha kukosa mtu wa aina yao wa kuwapigania. Kwa sababu hiyo anaitwa mzaliwa wa kwanza wa wanadamu. Wanadamu wote wenye hulka na tabia za Adamu wa kwanza wanatakiwa wapokee hulka na tabia za Adamu wa pili ambaye amekuwa mzaliwa wa kwanza akichukua nafasi ya Adamu.

Wote wanaokubali na kukipokea kwa imani kile Yesu alichofanya kwa niaba yao wanapokea hali ya kuwa wazaliwa wa kwanza. Uzaliwa wa kwanza unapatikana kwa kuzaliwa mara ya pili baada ya kuukana ule uzaliwa wa kwanza wa damu (Yohana 3:6-7; Tito 3:5). Uzaliwa wa kwanza hupatikana baada ya kuufia utu wa kale na kujivika utu mpya (Wakolosai 3:9-10). Na kama ilivyo ada ya mzaliwa wa kwanza ana jukumu la kutangaza fadhila zake aliyemkomboa kama Israeli walivyokuwa na jukumu la kutangaza injili kwa mataifa yanayowazunguka nao wakaitwa mzaliwa wa kwanza wangu (1 Petro 2:9; Kutoka 4:22)

Haki ya mzaliwa wa kwanza ni kupewa ukuu na mamlaka ya juu (Zaburi 89:27). Yesu ameahidiwa ukuu si kwa sababu hakuwa nao kabla ya kuchukua nafasi ya mzaliwa wa kwanza. Ameahidiwa ukuu kwa nafasi ya uzaliwa wa kwanza aliyoshiriki alipokuwa akiwapigania wanadamu wenzake wasio na uwezo wa kujipigania. Yeye pamoja na wazaliwa wa kwanza watakaokusanyika mbinguni kama kanisa watapewa ukuu wa ufalme wa kutawala malimwengu yote yasiyoanguka dhambini (Waebrania 12:22-23; Danieli 7:27). Mungu akusaidie uwe kwenye kundi hilo.