Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

MWANZO

MWANZO SURA YA 1:1-31

 1. Mwanzo unaotajwa hapa ambao Mungu aliziymba mbingu na nchi ndiyo mwanzo wa kuwepo kwake na wa malimwengu mengine yote? Mbingu na nchi zilizoumbwa hapo mwanzo zipo katika uwingi. Je hiyo ni kumanisha kuna mbingu na nchi kahaa kando ya hii mbingu na nchi tuliyonayo? 
 2. Je, Roho iliyotuama juu ya uso wa maji ilihusika na chochote katika uumbaji wa siku sita wa dunia? Kwa nini dunia ilihitaji siku sita za kuumbwa na si pungufu ya hapo au zaidi? Pangetokea changamoto gani kama dunia ingeumbwa kwa siku moja? Je, mambo yangekuwa mengi sana kiasi cha Mungu kushindwa kuyamudu yote?
 3. Je, unaona mpangilio wa matukio ya siku sita au saba za uumbaji kama unaotegemeana? Kwa nini mwanadamu aliumbwa mwisho kabisa mwa matukio hayo? Je kuna tukio lolote la uumbaji lililofanyika siku ya saba? Kwa nini Biblia inasema Mungu alimaliza kazi yake siku ya saba na si siku ya sita? Kwa nini Mungu alimuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake? Je, mwanamke naye aliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu? 
 4. Kwa nini siku za uumbaji zinatajwa kwa namba yaani siku ya kwanza, siku ya pili nk badala ya kusema Jumamosi, Jumapili, na kadhalika? Kwa nini siku inaonyeshwa kuanza jioni? (Mwanzo1:13) Je siku ya Sabato ambayo Mungu alipumzika kufanya kazi zake leo hii ni siku gani? Je Mungu anataka wanadamu pia wapumzike siku hiyo? (Kutoka 20:8-11).


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 2:1-25

 1. Jeshi linalotajwa wakati mbingu na nchi zilipokamilika ni jeshi gani hilo? Kwa nini linaitwa jeshi? Kwa nini Mungu aliibariki siku ya saba? Je hiyo siku imebaki na hiyo mibaraka hata leo? Kinachoonyesha kuwa hiyo siku imebarikiwa ni nini? Mtu anayetajwa kuumbwa kwenye sura ya pili ya Mwanzo 2:7 ana tofauti gani na yule wa Mwanzo 1:26-28? Kama ni yule yule kwa nini habari yake imerudiwa hapa? 
 2. Kunakomfanya mtu kuwa nafsi hai ni kuumbwa na Mungu au kupuliziwa pumzi ya Mungu? Unadhani nini kitatokea pumzi hiyo ikiondolewa? (Zaburi 146:4). Kwa nini Mungu alipanda bustani kisha akamwambia mwanadamu aitunze? Je mwanadamu mwenyewe asingeweza kuipanda hiyo bustani? Kama Mungu aliweza kupanda bustani kwa nini kazi ya kuitunza akawachia wanadamu? Je kazi ni laana au mbaraka? Je kuitunza bustani kulihitaji majembe na mapanga kama tunavyofanya leo? 
 3. Je kulikuwa na umuhimu wowote wa kuwa na mti wa ujuzi wa mema na mabaya kwenye bustani? Kwenye bustani ya Edeni kulisheheni miti na hasa miti ya matunda. Hii inakuambia nini kuhusu umuhimu wa miti ya matunda na miti kwa ujumla kwa binadamu? Je Mungu alijua kuwa mwanadamu angekula tunda alilokatazwa na angekufa kama matokeo ya uasi huo? Wakati Mungu anatoa agizo hilo Hawa mkewe Adamu alikuwepo? Kwa nini kazi ya kuwaita viumbe majina Mungu alimwachia Adamu na si Eva? Kwa nini hakuifanya mwenyewe? Kwa nini Robot yenye uwezo wa kufanya majukumu mengi ya mwanadamu msaidizi bora kama mwanamke? 
 4. Je mke aliyepewa Adamu ni ujira wa kazi kubwa aliyopewa na Mungu ambayo aliifanya kwa ufanisi? Nini kinapaswa kutangulia kati ya kufanya kazi na kuoa? Je Adamu alitoa mahari kwa ajili ya mkewe? Mahari ni lazima iwe fedha tu? Je Adamu alichagua mchumba? Je aliridhia mke aliyepewa? Kwa nini mwanamke alitolewa ubavuni kwa mwanaume? Kwa nini kuacha ni kwa muhimu kabla ya kuambatana na kuwa mwili mmoja? Je wanandoa kuwa uchi na kutoona haya kuna maana zaidi ya hiyo? Je, yaweza pia kumaanisha kuwa wawazi katika mambo yao?


 MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 3:1-24

 1. Kwa nini viumbe wenye akili na waliojaliwa uzuri mara nyingi huwa wakorofi kwa muumba wao na kwa viumbe wenzao? (Mwanzo 3:1; Ezekieli 28:17). Je unadhani wenye hekima na wenye nguvu za mwili wanafaa kuwaongoza wengine? (1 Wafalme 11:4; Waamuzi 16:20-21). Unadhani yule mwanamke angeambatana na mume wake kama walivyoagizwa na Mungu Shetani angeweza kuwadanganya? Je wanawake ni wepesi zaidi kudanganywa kuliko wanaume? Kama ni hivyo kwa nini Yuda Iskariote (mwanaume) alimsaliti Yesu? Je kati ya Hawa na Adamu ni nani alidanganywa? (1 Timotheo 2:4). 
 2. Kulikuwa na kosa gani kwa Mwanamke kujaribu kusahihisha kauli potofu ya nyoka kuwa wamekatazwa kula matunda ya miti yote? Je, kuna wakati ambao si wa kujibu maswali uliyoulizwa hasa pale mwenye kuuliza anapokuwa na nia ovu? Iliwezekanaje mwanadamu aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu azidiwe maarifa na ujanja na kiumbe ambaye hajaumbwa kwa mfano wa Mungu? Kwa nini akili ya Hawa haikutilia shaka kauli ya nyoka kwamba akila tunda ndipo atafanana na Mungu wakati alikuwa anafanana naye tayari? Kama hujawahi kudanganywa unaweje kuutambua uwongo?
 3. Siku ya anguko la wanadamu ilikuwa ya maswali na majibu; mwanamke akihojiwa na nyoka na Adamu akihojiwa na Mungu? Unadhani mahojiano gani yalikuwa magumu zaidi? Nani alitoa majibu yenye mashiko zaidi kati yao? Adamu alipoletewa mkewe alitoa shukrani kwa Mungu kwa kumsifia mkewe. Je lawama yake kuwa mkewe ndiye aliyechangia anguko lake ina ukweli? Je Mungu amehusika katika anguko la Adamu kwa kumletea mwanamke aliyemshawishi kutenda dhambi? Je kujitengenezea nguo za kuvaa (majani) ili kujisetiri lilikuwa wazo sahihi? Adamu na mkewe waliona aibu kwenda mbele za Mungu wakiwa uchi. 
 4. Kwa nini watu leo hawaoni aibu kwenda kwenye nyumba za ibada wakiwa nusu uchi? Kwa nini Mungu aliamua kuwapatia vazi lililo bora zaidi la kuwahifadhi Adamu na mkewe?Kama Shetani ndiye aliyekuwa ndani ya nyoka, Je kumwadhibu nyoka kwa kosa lililofanywa na Shetani (mpangaji) ilikuwa halali? Je nyoka atakayepondwa kichwa ni yule wa bustanini au Joka yule wa zamani? (Ufunuo 12:9). Kulikuwa na ubaya gani kama Adamu na Hawa baada ya kutenda dhambi wangeachwa bustanini wale matunda ya uzima?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 4:1-26

 1. Adamu alimjua Hawa mkewe baada ya kuondolewa kutoka bustanini au hata kabla ya hapo? Kwa nini kumwingilia mke wa ndoa kunaitwa kumjua? Je, watoto huzaliwa wakiwa na mwelekeo wa kazi watakazofanya wakiwa watu wazima? Kulikuwa na ubaya gani kwa Kaini kuleta mazao ya kazi zake kama ambavyo Habili alileta mazao ya kazi yake? Kwa nini Kaini alimchukia ndugu yake? Je, kuna uwezekano wa kuchukiwa kwa kuwa unatenda mema? (1 Yohana 3:12). Je, unauona uwezekano wa ndugu wa imani moja kutofautiana katika maswala ya ibada katika siku za usoni kiasi cha mmoja kufikiria kumwua mwenzake? (Ufunuo 13:15)
 2. Kitendo cha Mungu kumpunguzia adhabu Kaini kinaonyesha asivyopenda kuwaumiza wanadamu hasa wanaofanya makosa. Kwa nini watu wengine wanakuwa wazito kujitetea na kuomba msamaha kwa Mungu ingawa makosa yao si makubwa kama ya Kaini? Je, unadhani dhambi ya kuua ilistahili msamaha? Je, unadhani Adamu alitambua uchungu wa mauti siku mnyama alipouawa bustanini kwa ajili ya ngozi waliyovikwa au siku waliposhudia kifo cha mtoto wao asiye na hatia Habili? Je, Habili alikufa kifo cha kizembe kwa kutochukua tahadhari ya kuwa mbali na kaka yake anayemchukia?
 3. Jibu la Kaini kwa Mungu kwamba yeye si mlinzi wa ndugu yake lilikuwa na ukweli wowote? Je, wanadamu watatoa hesabu kwa Mungu kuhusiana na namna walivyowajali wanadamu wenzao? Je mauaji ya watu wasio na hatia yaweza kuleta majanga katika nchi? Je msamaha wa Mungu una kawaida ya kukupatanisha na uliowakosea? Kawaida ya kuoa wake wengi ilianzia kwa Lameki mzao wa Kaini. Hii inakuambia nini kuhusu uhalali wa jambo hili? Iliwezekanaje Adamu azae watoto waliotofautiana tabia kama Kaini na Abeli? Tofauti hii inatokana na malezi au jinsi walivyotungwa tumboni mwa mama zao?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 5:1-32

 1. Kwa nini mwanaume na mwanamke wa kwanza waliitwa Adamu? Je, Adamu halikuwa jina la mwanaume peke yake? Kama watoto huzaliwa wakiwa na mfano na sura ya wazazi wao ilikuwaje Kaini hakufanana na wazazi wake kwa tabia? Je watoto wa kike aliozaa Adamu ndiyo waliokuja kuolewa na kaka zao ili kuendeleza uzao? Kwa nini leo hii mtu haruhusiwi kuoa dada yake?
 2. Ikiwa Yaredi alizaa mtoto wake wa kwanza Henoko akiwa na miaka 162 hiyo ni kumaanisha wanawake wa nyakati hizo hawakuwa wanakoma kuzaa mapema? Kwa nini inatajwa kuwa Henoko alienda pamoja na Mungu kwani hao wengine hawakwenda na Mungu? Biblia inaposema Mungu alimtwaa Henoko inamaanisha nini? Methusela ndiye mtu anayedhaniwa kuishimiaka mingi (969) kuliko wengine wote. 
 3. Kwa nini watu wa zamani waliishi maisha marefu na leo tunaishi miaka michache? (Zaburi 90:10). Lameki alijuaje kama mtoto wake Nuhu atakuja kuwafariji hapo baadaye? Wazao wa Sethi na wazao wa Kaini walitofautianaje? Ni uzao gani waliompenda Mungu zaidi? Unadhani Kaini aliridhika na kitendo cha Mungu kuwafukuza wazazi wake kutoka Edeni?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 6:1-22

 1. Katika sura ya sita ya Mwanzo tunakutana na ongezeko la wanadamu lisiloendana na makusudi ya Mungu. Je hii ni kuonyesha kuwa uzao wa Kaini uliwazidi kwa idadi uzao wa Sethi waliokuwa wacha Mungu? Tofauti ya wana wa Mungu na binti za wanadamu ni nini? Je uovu uliongezeka kwa njia ya wacha Mungu kuoa binti wasio wacha Mungu? Je kuna ukweli wowote kwamba mabinti wasio wacha Mungu ni wazuri kuliko mabinti wacha Mungu? Kitendo cha Mungu kupunguza siku za kuishi za mwanadamu kilikuwa mbaraka kwao au kilikuwa adhabu? Mungu alihuzunishwa moyo kwa namna binadamu anavyoelekea kwa kasi kwenye uovu. 
 2. Nini kiliwafanya watu wa nyakati hizo kufikiria uovu tu muda wote? Kwa nini Mungu alighairi kuwa amewaumba wanadamu? Je hakujua wangefikia hatua hiyo? Je kwa kauli hiyo anakiri kuwa alikosea kuumba wanadamu? Ule mfano na sura ya Mungu kwa wanadamu bado vilikuwepo au vilikuwa vimetoweka? Mzazi anapofikia hatua ya kujilaumu kwa nini alimzaa mtoto hiyo inatosha kuwa laana kwa mtoto huyo? Je ni ugumu wa maisha uliowafanya wamuache Mungu? Je shida na mafanikio ni kipi huweza kumshawishi mwanadamu amuache Mungu kirahisi?
 3. Kwa nini Mungu asiwaangamize wanadamu walioishi kabla ya gharika ili kuisafisha dunia na uovu? Je agano alilolifanya Mungu na Nuhu lilitokana na makubaliano waliyoyaweka kwa pamoja au ulikuwa mpango uliobuniwa na Mungu ambao Nuhu alitakiwa auafiki kwa imani? Nuhu aliingia safinani kwa kuwa alionekana kuwa mwenye haki je ni vigezo gani viliyumika kuchagua wanyama wawili wawili wa kuingia safinani? Kutokana na yale aliyofanya baada ya kutoka safinani unaona Nuhu alikuwa kweli mwenye haki? Je, mwanadamu anahesabiwaje haki mbele za Mungu? (Warumi 3:24, 28).
 4. Kutafuta na kukitunza chakula cha kuwatosha wanyama wote katika kipindi chote cha gharika haikuwa shughuli nyepesi. Unadhani jambo hilo lilihitaji imani na utii wa kiwango cha juu? Unachukuliaje usemi kuwa tunaokolewa kwa imani na hivyo hatulazimiki kutii sheria za Mungu? Je kuwalisha chakua wanyama najisi kama nyoka na nguruwe hakungeweza kumtia unajisi yule aliyekuwa akiwalisha?
 5. Unadhani msukosuko wa gharika ulipoanza wanyama hao hawakuwa wanapiga kelele za hofu? Kama kanisa linafananishwa na Safina ni dhahiri kuwa ndani yake watakuwapo wasumhufu na wenye tabia kama za wanyama waliokuwamo kwenye Safina ya Nuhu? Una lipi la kuwaambia wale wanaochukulia kuwa kanisa libaki na walio safi peke yake?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 7:1-24

 1. Ni nini kinachothibitisha kuwa Nuhu alikuwa mwenye haki? Je, sharti la kuingia mbinguni ni kuwa mwenye haki? Haki inayomstahilisha mtu kuingia mbinguni ni haki ipi? Ni ile anayoitafuta mwenyewe kwa juhudi zake au ile anayopewa kwa kumwamini Kristo?
 2. Kwa nini Wanyama safi waliingizwa kwenye Safina saba saba na Wanyama najisi waliingizwa wawili wawili? Wanyama wanaoitwa safi ni safi kwa sababu gani na wanaoitwa najisi ni najisi kwa sababu gani? Kwa nini Mungu alitaka kuwahifadhi hai Wanyama hao ili iwe mbegu usoni pa nchi. Kwa nini hakuamua kuangamiza na kuumba tena upya?
 3. Je, mvua ikinyesha siku arobaini usiku na mchana kuna eneo katika dunia litakalokuwa halijafurikishwa? Kwa nini watu wengine wanakaidi kuwa gharika haikuwahi kutokea maana dunia yote haiwezi kugharikishwa kwa wakati mmoja?kwa nini Wanyama safi na najisi hawakuwafuata wenzao waliokuwa wakiingia kwenye Safina?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 8:1-22

 1. Kuwamo ndani ya Safina kulihitaji Imani. Je, chakula cha Wanyama, ndege, na binadamu kilitosha kwa siku 150 walizokuwamo ndani ya Safina? Kutoka kwao ndani ya Safina kulitegemea huruma za Mungu? Nani aliilinda Safina isiharibiwe na magogo yaliyokuwa yameizonga pande zote? Je Mungu alipanga Safina itue juu ya mlima Ararati au ilitokea kama ajali?
 2. Kunguru aliyetumwa na Nuhu kwa nini hakurudi? Unadhani atakuwa alinogewa na mizoga kwa kuwa yeye ni ndege najisi anayekula mizoga? Kwa nini Nuhu alitoa kafara ya Wanyama safi na si ya Wanyama najisi? Ibada aliyofanya baada ya kutoka kwenye Safina ilikuwa ya kushukuru nini?
 3. Unadhani alijisikiaje Nuhu kuona wamebaki watu wanane tu na huku mizoga ya watu isiyohesabika Ikiwa imetapakaa usoni pa nchi? Unadhani hali ilivyokuwa baada ya gharika ilimfurahisha Mungu? Kwa nini aliahidi kutoleta gharika tena? Kati ya moto wa milele na gharika ya maji ipi ni adhabu mbaya zaidi?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 9:1-29

 1. Kwa nini Mungu aliwaongezea wananadamu wanyama kama chakula cha ziada baada ya kutoka Safinani? Kwa nini aliwazuia kunywa damu ya Wanyama? Kwa nini kumwaga damu ya mwanadamu kulipigwa marufuku? Mungu aliweka agano la kutoleta tena adhabu ya gharika. Unadhani ni kwa nini aliweka agano hilo? Upinde wa mvua ni ishara kuwa Mungu hataleta tena gharika. Kwa nini mashoga wanatumia rangi za upinde wa mvua?
 2. Nuhu alitoa wapi elimu ya kutengeneza pombe? Kwa nini Nuhu alianza kunywa pombe baada ya kazi nzuri ya kuwaokoa wanadamu na viumbe wengine? Mtoto aliyemcheka Nuhu kutokana na kukaa uchi baada ya kulewa ana makosa? Tofauti ya mtoto aliyewapa taarifa kuwa Nuhu yu uchi na wale waliokwenda kumfunika ni nini?
 3. Kwa nini laana haikumwendea aliyeona uchi na badala yake ikamuendea mjukuu? Je laana iliyotolewa na Nuhu iliwahusu Waafrika pia? Nuhu alionyesha mfano mbaya kama kiongozi wa kiroho. Unadhani kwa kosa lile Nuhu alistahili adhabu? Hii inatufundisha nini juu ya uwezo wa Mungu wa kuchukuliana na mapungufu yetu?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 10:1-32

 1. Kutoka kwa vizazi vya wana wa Lutu mataifa ya ulimwengu yakaanza kuwepo yakiwa na lugha zao na usemi wao. Ilitokeaje mataifa mengine yakawa na rangi na mwonekano unaowatofautisha na mataifa mengine?
 2. Je mfalme Nimrodi ndiye aliyesimamia wazo la ujenzi wa Babeli? Njia ya kujinasua na matokeo ya dhambi haikuwa ujenzi wa mnara wa Babeli. Unadhani njia sahihi ingekuwa ipi?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 11:1-32

 1. Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Tofauti ya lugha na usemi ni nini? Lugha na usemi uliokuwa unazungunzwa wakati huo ni upi? Je, lugha ina uwezo wa kuwaunganisha watu katika uasi dhidi ya Mungu? Waliochafuliwa lugha waliwezaje kuongea kwa lugha mpya kabla ya kujifunza kwanza? Je kuwachafulia lugha kulifanikiwa kukwamisha mradi wa ujenzi wa Babeli kwa kiasi gani?
 2. Lengo la ujenzi wa mnara wa Babeli ni kujitafutia jina. Walikuwa wanatafuta jina gani? Je, wanadamu walikuwa wanataka kushindana na Mungu kwa lipi? Je, ni kweli kwamba kama ujenzi wa mnara ule usingesitishwa ungeweza kufika mbinguni? Je, ilikuwa ni lazima Mungu ashuke ili kubaini kinachoendelea au alifanya hivyo ili kuwapa nafasi ya mwisho ya kutubu?
 3. Watu walioishi wakati wa ujenzi wa mnara wa Babeli walikuwa uzao wa Nuhu waliookolewa na Safina. Je, gharika ilisaidia chochote katika kuondoa dhambi na uasi? Je, baada ya moto wa milele kuangamiza dhambi na uasi havitaibuka tena kama ilivyotokea kwenye ujenzi wa mnara wa Babeli. Babeli ya leo ya kiroho inajenga mnara gani ili kushinda naMungu na kujitafutia jina?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 12:1-20

 1. Kutoka mahali ulipo kabla hujatajiwa wala kuonyeshwa unakopelekwa kunahitaji Imani kubwa. Unadhani ni nini kilimshawishi Abrahamu kukubali wito huu wa Mungu? Abrahamu alitumia mbinu gani kuwashawishi jamaa yake kwamba alikuwa anafanya maamuzi hayo akiwa na akili timamu na kwa hiyo wasisite kuandamana naye? (Waebrania 11:8). Kama lengo la Mungu ni kuweka agano na Abrahamu isingewezekana agano likafungiwa pale alipo?
 2. Je, kubarikiwa kunahusu nini hasa? Dalili ya kutambua kuwa mtu amebarikiwa ni nini? Unadhani jamaa zote za dunia zimebarikiwa kwa ajili ya Abrahamu na kwa kupitia kwake? Yunafanya ibada ili kumshukuru Mungu na kutangaza Fadhili zake kuu kwetu. Unaelezeaje kawaida ya Abrahamu ya kumjengea Mungu madhabahu kila alikoenda? Je, unaenda ibadani ili kumshukuru Mungu au kumuomba mahitaji?
 3. Je, Mungu hakujua kuwa anakompeleka Abrahamu kungekuwa na njaa? Kwa nini hakuepusha njaa hiyo kwa mtumishi wake Abrahimu hata ikamlazimu Kwenda kuhemea Misri? Je, kuzuka kwa njaa lilikuwa jaribu la kupima Imani kwa Abrahamu? Je, Kwenda kuhemea chakula Misri halikuwa jambo la kumdhalilisha Mungu? Ukweli kwamba Misri ilikuwa kimbilio kwa watu wa Mungu walipokuwawanakabiliwa na njaa na hatari ya kuuawa inakueleza nini juu ya ukarimu na utajiri wa Afrika?
 4. Kwa nini Abrahamu alisita kumtambulisha Sara kama mkewe? Ni sahihi kumfundisha mwenzio uongo ili uepuke mauti? Je, wenye wake wazuri na waume wazuri wapo kwenye hatari ya kunyang’anywa wake na waume zao na wenye mamlaka au pesa? Je kutumia akili za kibinadamu kujiokoa kulimsaidia Abrahamu? Je, Abrahamu alikuwa ameongoka vya kutosha au alikuwa anaukulia wokovu?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 13:1-18

 1. Abrahamu alikuwa Tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Iliwezekanaje mtu wa Mungu Abrahamu ambaye aliacha yote ya dunia na kumfuata Mungu awe Tajiri wa kiasi hicho? Kuna uhusiano gani kati ya kumfuata Mungu na mafanikio ya kiuchumi? (Kumb. 28:13; 2 Wakorintho 9:8; 1 Samweli 2:7; 1 Nyakati 29:12; Wafilipi 4:19). Kama utajiri si mbaya kwa nini utajiri na matajiri hawesemwi vizuri katika Biblia? (Yakobo 5:1; Mathayo 19:23; 1 Timotheo 6:18-19).
 2. Lutu alimfuata baba yake mkubwa Abrahamu akiwa si tajiri. Lakini miaka ya kusafiri na Abrahamu ikamfanya kuwa tajiri. Unajifunza nini juu ya kufuatana na watu wenye dira ya Maisha na uwezo wa kuona mbali? Je, ni kweli kuwa mafanikio mengine hayawezi kuja mpaka mtu ameondoka alipo na kuelekea kule mafanikio yake yalipo? Utajuaje kama unakokwenda na unachofanya ndicho kitakuletea mafanikio maishani mwako?
 3. Je mafanikio ya kiuchumi yaweza kuzua migogoro mikubwa katika jamii? Njia iliyotumika na Abrahamu kutatua mgogoro uliozuka ilikuwa ya haki? Kwa kuwa kwa sehemu kubwa utajiri wa Lutu ulitokana na baraka zake kwa nini Abrahamu hakujipa nafasi ya kwanza na kuchagua eneo lenye bonde linalofaa kwa malisho? Je, Lutu alionyesha heshima kwa Abrahamu kwa kujichagulia bondeni panapofaa kwa mifugo?
 4. Je, kuna ukweli wowote kwamba ndugu wakikaa pamoja hawaishi kugombana? Je wakati fulani kutengana ni dawa ya magomvi yanayotokea mara kwa mara? Haikuwa sahihi kwa Abrahamu na Lutu kugombana maana walikuwa ndugu na Wakaanani na Waperuzi wasiomjua Mungu walikuwa majirani zao. Kungetokea shida gani katika uinjilisti kwa mataifa hayo kama wangegombana?
 5. Panahitaji hekima ya Mungu kuchagua makazi ya kudumu. Unadhani Lutu alimshirikisha Mungu katika kuchagua kwenda Sodoma? Usalama wake, wa Watoto wake, na wa mali zake ulikuwa hatarini kwa kusogeza makazi yake hadi Sodoma? Je, makazi yako ya kudumu yamezingatia usalama huo? Waishio mjini na waishio mashambani ni nani wana hatari kubwa zaidi ya kupoteza Watoto na mali?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 14:1-24

 1. Lutu aliyejichagulia mji wa Sodoma na bonde lake anajikuta katikati ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambapo yeye mwenyewe anatekwa na mali yake inachukuliwa. Unajifunza nini juu ya ubaya wa tamaa na ubaya wa kudhulumu mali za watu katika kisa hiki? Je, nchi ikiingia vitani, mtu wa Mungu ana wajibu wa kuipigania nchi yake kwa kushika silaha? Je Abrahamu alikuwa na ulazima wa Kwenda kuwatetea watu wa Sodoma?
 2. Je, kupigania haki za watu na kujihusisha na siasa? Unaielezeaje hali ya Abramu aliyeunda jeshi na Kwenda kupigana ili kuwarejesha mateka na mali zilizotwaliwa? Ni wakati gani ambao kujihusisha na utetezi wa watu huwa ni siasa chafu inayofaa kuepukwa na watu wa Mungu?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 15:1-21

 1. Je, Mungu aliona nini kwa Abrahamu hata akamtokea ili kumhakikishia kuwa yupo pamoja naye na hivyo asihofu? Mahusiano ya Mungu na wanadamu yamejengwa juu ya msingi wa kuaminiana. Ni nani katika mahusiano hayo anaonekana kutomwamini zaidi mwenzake na kwa nini? Kazi ya ngao ni kukinga mishale vitani. Je, unahisi uko salama kwa kuwa Mungu ni ngao yako?
 2. Abrahamu hakuwa mnafiki kwa Mungu bali alimkumbusha ahadi yake na changamoto anazopitia kutokana na ahadi hiyo kutotimizwa kwa wakati. Je, tuna utaratibu wa kumweleza Mungu changamoto zinazotukosesha amani au tunachukua muda mwingi wa maombi kutoa sifa za unafiki kwa Mungu huku tukiumia moyoni? Je, Mungu anafurahi tunapomweleza shida na mahitaji yetu au anachukia? (1 Petro 5:6-7; Wafilipi 4:6-7; Isaya 41;21; na Isaya 43:26).
 3. Je, kwa wale wasiopata Watoto ni sahihi kumsaili mtoto atakayewarithi kama alivyofanya Abraham? Je mtoto uliyemsaili ili awe mrithi wako waweza kumwachia majukumu ya kuiongoza familia kama alivyofanya Abraham? (Mwanzo 24:2-3). Je, kijana wa kazi anayeishi na mzee aliyestaafu na anayesimamia miradi yote aweza kufanywa mrithi wa mali Ikiwa Watoto wote walishakufa?
 4. Huyo Mungu aliyesema na Abrahamu mwenye kuwapasua Wanyama vipande viwili alikuwa na mwili wa kibinadamu? Abramu alikuwa anaendelea kuelekezwa muundo wa agano walilokubaliana kuingia na Mungu. Hii inatuambia nini juu ya mambo mengi tusiyoyaelewa yaliyo kwenye agano letu na Mungu? Mungu alimjulisha Abrahamu kuwa utimizo wa ahadi nyingine ungechukua miaka mingi kutimia. Kwa nini Mungu alilazimika kumjulisha yote hayo?
 5. Je, sisi ni sehemu ya uzao wa Abrahamu utakaokaa utumwani duniani kwa miaka 6,000 na kisha tutatoka na utajiri wa uzima wa milele tukielekea nchi ya ahadi? Kuzikwa katika uzee mwema kuna tofauti gani ya maana na kuzikwa katika uzee mbaya? Mojawapo ya ishara ya kuwa mtu amekuwa na uzee mwema ni ipi? Kwa nini Mungu anamwambia Abrahamu akifa ataenda kwa baba zake?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 16:1-16

 1. Huyu Hajiri Mmisri alitokeaje kuwa mjakazi wa Abrahamu? Kwa nini Sarai hakuona vibaya kumpa mumewe Abraham mjakazi wa kiarabu ili awe mke wake na kumzalia watoto? Je, Abrahamu na Sarai walitilia shaka kauli ya Mungu juu ya ahadi ya kuwapa mtoto? Je, kuna nyakati ambazo ahadi za Mungu zinaonekana kuwa kama uwongo? Kwa nini nyakati Fulani Mungu haonekani kuwa na haraka ya kutimiza ahadi zake?
 2. Kwa nini baada ya Hajiri kupata mimba Sarai alikuwa duni machoni pa mjakazi wake? Unadhani ni uhusiano gani ulikuwa umepamba moto kati ya Abrahamu na Sarai na Abrahamu na Hajiri na kwa nini? Kwa nini dharau aliyofanyiwa na Hajiri lawama yake inaenda kwa Abrahamu? Je, Abrahamu alimfundisha Hajiri kumdharau Sarai au kitendo cha kushirikiana na huyu binti kimwili kilipunguza mapenzi yake kwa Sarai?
 3. Kwa nini Abrahamu hakumtetea Sarai badala yake alimhimiza Sarai amfanyie chochote anachotaka Ikiwa ni Pamoja na kumtesa? Je panapotokea wanafamilia kudharauliana ufumbuzi ni yule mkubwa amtese mdogo? Kwa nini Abrahamu hakuwapatanisha wakeze? Je, huu ni Ushahidi kuwa kuoa wake wengi haukuwa mpango wa Mungu na kwamba ni vigumu kuugawanya upendo kwa wake wawili kwa viwango vilivyo sawa?
 4. Je, mateso yakizidi katika ndoa ni sahihi kukimbia ili kujiponya kama alivyofanya Hajiri? Je kuzaa na mwanamke nje ya ndoa ndiyo chanzo cha kuwa na wanawake wengi wanaolea Watoto peke yao (single parents) siku hizi? Je Mungu anawajali wanawake wanaolea Watoto peke yao? Je Mungu aliahidi kumtendea nini Hajiri baada ya kukimbia mateso ya nyumbani kwa Abrahamu?
 5. Je vita ya Wayahudi na Wapalestina ni vita kati ya Watoto wa Ibrahimu waliozaliwa kwa mama tofauti? Ni nani kati ya Ishmaili na Isaka aliye mkubwa kwa mwenzake? Kama Hajiri alikimbia mateso nyumbani kwa Ibrahimu ilikuwaje jina kwa mtoto wa Hajiri? Je, ukiachana na mke unaruhusiwa kuendelea kumhudumia na kuhudumia mtoto?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 17:1-27

 1. Abrahamu alipoambiwa na Mungu kuna agano la kubarikiwa Ikiwa atakuwa mwaminifu aliitikia wala hakubisha wala kuhoji. Kwa nini Mungu hakumshirikisha Abrahamu ili wapange Pamoja agano litakavyokuwa? Je, unafikiri Abrahamu alipata nafasi ya kusoma na kulielewa vyema agano alilolipanga Mungu kwa ajili yake? Je, Abrahamu alikuwa na sifa yoyote ya kumstahilisha kufanya agano na Mungu?
 2. Katika agano lile kulikuwa na mambo mengi na makubwa ambayo Mungu aliyaahidi kwa Abrahamu. Kwa nini Abrahamu hakutilia shaka ahadi hizo? (Warumi 4:3). Mungu anapoahidi kumpa Abrahamu nchi inayokaliwa tayari na watu hatengenezi mgogoro? Je, anayo mamlaka ya kufanya hivyo? Kwa nini katika hatua hii Mungu anabadilisha jina la Abrahamu na kuwa Ibrahimu na Sarai kuwa Sara?
 3. Kwa nini kutahiriwa kuliingizwa kwenye agano la Mungu na Ibrahimu? Kwa nini agizo halikuwahusu wanawake lakini liliwahusu wageni wasiokuwa wa uzao wa Ibrahimu? Kwa nini jitihada za Ibrahimu za kumuomba Mungu wafalme wa kabila za watu watoke kwa Ishmaili ziligonga ukuta? Je kuna Ushahidi kuwa Mungu alitimiza ahadi ya kuwafanya wazao wa Ismaili (Waarabu) kuwa taifa kubwa?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 18:1-33

 1. Je, Ibrahimu alipokuwa anawakarimu wageni alitambua kuwa miongoni mwao yupo Bwana au jambo hilo alilitambua wakati wa kuagana? Je, kuna uwezekano wa kutembelewa na wenyeji wa mbinguni na usifahamu? Kwa nini mara nyingi ukarimu wa chakula hutanguliwa na mibaraka? (Mwanzo 27:7). Unajifunza nini juu ya tabia ya Ibrahimu ya kupiga mbio anapowakaribisha wageni na anapowahudumia?
 2. Watumishi wa Mungu wanapotembelea wanachukuliana na hali watakayoikuta. Unadhani Ibrahimu angejua wageni wake wametoka mbinguni angewakaribisha chini ya mti? Ukarimu ni uwezo wa kutoa kilicho bora kwa wakati hata kwa watu usiotarajia kupata faida kwao. Unaona sifa hiyo unatimia kwa ukarimu wa Ibrahimu? Kwa nini aliwachinjia ndama wageni kati ya Wanyama alionao?
 3. Ushiriki wa Ibrahimu katika kukiandaa chakula unakufundisha nini juu ya tabia yake ya kujituma na kushirikiana na wenzake? Kwa nini wakati wageni wanakula hakula nao? Je, ukiwa mkarimu kwa Mungu, anaweza kukutatulia hata shida ambayo hujamwomba? Je kwa kutokuwa na mtoto Sara alikuwa anakosa furaha na mume wake? Swali na kicheko cha Sara baada ya kuambiwa atapata mtoto vilikuwa vinaashiria kupungukiwa Imani, dharau, au furaha iliyopitiliza?
 4. Je kusindikiza wageni kuna faida gani? Kama wale wageni wasingesindikizwa Ibrahimu angepata kujulishwa kile kinachowapeleka wageni Sodoma? Kitendo cha Ibrahimu kusihi adhabu kwa watu wa Sodoma isitekelezwe kwa kuwa kuna wenye haki ndani yake kilikuwa kinalenga familia ya nduguye Lutu? Hii inatufundisha nini juu ya wajibu wa watu wa Mungu kuwaombea waovu ili wasiangamizwe?
 5. Je adhabu ya Mungu kwa watu aliowakusudia inaweza kuahirishwa au kubadilishwa Ikiwa watu hao wataombewa? Je, unaona hiyo roho ya kuwaombea na kuwaonea huruma waliotangazwa kuwa wataangamizwa kutokana na uovu wao? Ungepokeaje taarifa kama ingetangazwa kuwa hakuna tena moto wa milele kwa waovu? Je, ungefurahi au ungesikitika?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 19:1-38

 1. Je, Lutu aliwatambua wale wageni walioingia jioni Sodoma kama ni Malaika? Tabia gani njema Lutu aliyokuwa nayo licha ya kuishi kwenye mji wenye uovu wa Sodoma? Wale wageni kwa nini walikataa mwaliko wa Lutu na kudai kuwa wangekaa uwanjani usiku kucha? Wenyeji wa Sodoma walimaanisha nini waliposema wanawataka wageni wapate kuwajua? Kama kuwajua wageni ilikuwa vibaya kwa nini Lutu hakuona vibaya kuwatoa mabinti zake ili watu wa Sodoma wawajue?
 2. Hawa mabinti waliwezaje kuishi mji wa uovu kama huo nao hawajajua mtu mume? Watu wa Sodoma walijuaje kuwa Lutu aliyekuja kukaa Sodoma kama mgeni anataka kuwaletea hukumu? Kwa nini watu wa Sodoma wakubwa kwa wadogo waliendelea kutafuta mlango waingie ndani licha ya kupigwa upofu na Malaika? Je, kuna wakati watu wazima na Watoto wote huwa sawa hakuna wa kumshauri mwingine?
 3. Je, ukiwa mwaminifu kwa Mungu kuna uwezekano wa kupewa fursa ya kuokoa ndugu zako? Kwa nini wakweze Lutu hawakupokea fursa ya kuokolewa kwao badala yake walimwona kama achezaye? Unadhani ni kwa nini mabinti wa Lutu walioolewa walipotea lakini waliokuwa hawajaolewa waliokoka? Je tabia za baadaye za mabinti hawa za kumnywesha pombe baba yao na kulala naye zinaonyesha walikuwa waadilifu?
 4. Kwa nini kulikuwa na katazo la kutogeuka nyuma kwa wale waliokuwa wanaokolewa? Kwa nini Yesu aliwahimiza wasikilizaji wake kumkumbuka mkewe Lutu? (Luka 17:32). Je, unadhani mkewe Lutu aliridhika kuuacha mji wa Sodoma na anasa zake? Ni kwa namna gani tunaweza kufanana na mkewe Lutu? Kukawiakawia kwa Lutu kuondoka Sodoma kulichangia kufanya Mawazo ya mkewe kuwazia vitu walivyoviacha Sodoma? Unadhani ile tamaa ya vitu iliyomfanya kufarakana na Ibrahimu ilikuwa bado inamtafuna Lutu?
 5. Kwa nini Lutu aliomba wapelekwe Soari na siyo milimani kama Mungu alivyokuwa amepanga mwanzo? Kwa nini Lutu na binti zake wawili walitoka tena Soari na Kwenda milimani walikokukataa mwanzo? Je, kumwomba Mungu akubadilishie alichokupangia mwanzo kwaweza kukuletea majuto? Je wazo la kumhifadhia baba yao uzao kwa kulala naye lilikuwa sahihi? Kwa nini Mungu aliwazuia Waisraeli kupigana na Waamori na Wamoabu waliozaliwa kwa kitendo hicho kwa madai kuwa ni ndugu zao?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 20:1-18

 1. Katika wakati wa zahama, Lutu alitaka kuwatoa mabinti zake wabakwe na watu wa sodoma na Ibrahimu alimtoa mkewe kwa Abimeleki mfalme wa Gerari ili alale naye. Je ni nani alifanya dhambi iliyo kuu kati yao? Je sababu aliyoitoa Ibrahimu ya kufanya hivyo ina mashiko? Je kuna hatari yoyote ya kuoa au kuolewa na mwanaume au mwanamke mzuri anayependwa na wengi? Unamlindaje huyo anayependwa na wengi ili asikuletee matatizo kama ilivyotokea kwa Ibrahimu? 
 2. Je Ibrahimu alimshirikisha Mungu katika mpango wake wa kujiokoa? Kwa nini Sara alikubali kushiriki uongo wa mumewe? Je kuna wakati kusikiliza sauti ya mumeo kwaweza kukuletea majanga? Kipi kilikuwa nafuu kwa Sara; kushuhudia mumewe akiuawa kwa ajili yake au kuokoa maisha ya mumewe kwa kufanya uzinzi?
 3. Je ni kwa nini Mungu aliingilia kati mpango ule wa uzinzi usifanikiwe? Kwa nini alitaka kumuadhibu mfalme Abimaleki na watu wake badala ya kumuadhibu Ibrahimu na mkewe? Kwa nini Mungu alimsifia mfalme Abimaleki kuwa ni mkamilifu wa moyo wakati alikuwa amekusudia kufanya uzinzi? Je kuna tofauti ya kuzini na mke au mume wa mtu? Je kuna chenye unafuu kati ya uzinzi na uasherati?
 4. Je Abimaleki mfalme alikuwa na haki ya kumfokea Ibrahimu kwa kutomjulisha kuwa Sara ni mkewe? Kwa kuwa Ibrahimu alioa dada yake alikuwa na ulazima wa kusema ni mke wake pia? Je unaweza kusema uongo wa Ibrahimu ulimtajirisha kwa kuwa ulimfanya mfalme ampatie zawadi nyingi? Unajifunza nini kwa Ibrahimu alivyomwombea mfalme Abimaleki apate watoto? Unamuombea nini anayemtamani mkeo au mumeo?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 21: 1-34

 1. Isaka alitahiriwa siku ya nane kama Yesu. Kutahiriwa kulikuwa na umuhimu gani? Je madai ya Wakristo wa Kiyahudi walioshuka kutoka Uyahudi walioshinikiza kuwa Wakristo wanapaswa kutahiriwa yalikuwa na ukweli wowote kwa mujibu wa torati? (Matendo 15:1-3). Kulikuwa na umuhimu gani wa kufanya karamu wakati Isaka alipoachishwa kunyonya? Je, ipo haja ya kumfanyia karamu mtoto anapokua kutoka mwaka mmoja kwenda mwingine?
 2. Je, ni sahihi mtoto asiye na maadili kumfukuza kutoka nyumbani hasa anapokuwa ni mtoto asiyetokana na familia husika? Je, madai kuwa mke huwachukia ndugu wa mume bila sababu yoyote yana ukweli gani? Wajibu wa mume anaposhitakiwa tabia mbaya za Watoto ni nini? Kwa nini Mungu anamsihi Ibrahimu amsikilize Sara kwa hoja ya kumfukuza Hajiri na mwanae wakati hapo nyuma alimlaumu kwa kusikiliza sauti ya mkewe alipomshauri amuoe Hajiri?
 3. Kwa nini Ishmaili anatambuliwa kama mzao wa Ibrahimu wakati alizaa na mjakazi? Je uzao wa Ishmaili (Waarabu) wanatambuliwa na Mungu kama taifa kubwa? Je, Hajiri alistahili kupata shida alizozipata alipojikuta akilea mtoto peke yake (single parent)? Je, wenye ndoa wamehusika katika kuzalisha mama wengi wanaolea Watoto peke yao? Je, Mungu ana ujumbe wowote kwa mama wanaolea Watoto peke yao?
 4. Je, ni sahihi kufanya maagano na watu wa mataifa? Kwa nini Ibrahimu alikaa siku nyingi katika nchi ya Wafilisti? Kisima kilikuwa na umuhimu gani katika Uchumi wa wakati huo hadi kizue ugomvi na majirani? Visima vya maji vina umuhimu gani leo kwa shughuli za ufugaji na kilimo?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 22: 1-24

 1. Maandiko yanatuambia Mungu hamjaribu mtu (Yakobo 1:13). Inakuwaje hapa tunaambiwa Mungu alimjaribu Ibrahimu? Je, kujaribu kulikotumika hapa ni kule kwa kumpima kama amekomaa kiimani vyakutosha na si kule kwa kutenda dhambi? Mahali anapoambiwa Ibrahimu akafanye ibada ya kumtoa kafara mwanae palikuwa na umbali wa kusafiri zaidi ya siku tatu. Unazungumziaje waumini wanaolalamikia umbali wa Kwenda kwenye ibada na makambi kama sababu ya wao kutohudhuria?
 2. Ibrahimu alipowaambia watumishi kuwa wawasubiri yeye na kijana waende kuabudu kisha watawarudia huku akiwa anajua anaenda kumchinja alikuwa anamaanisha kauli yake au alikuwa anawadanganya? Isaka anawakilisha vijana wa kiume (teenagers) ambazo mara nyingi hawaaminiki na hawashirikishwi katika maamuzi. Je unauona umuhimu wa kusikiliza ushauri wa vijana? Kwa nini Ibrahimu hakumwambia Isaka ukweli kuwa yeye ndiye mwanakondoo anayekwenda kuchinjwa?
 3. Je, Ibrahimu angemchinja mwanae kama Mungu alivyomwagiza angekuwa ametenda dhambi ya kuua? Je, majirani wasiomjua Mungu wake wangemwelewa? Je, kuna wakati tunaotakiwa kutii maagizo ya Mungu hata kama hatuyaelewi vizuri? (toa mfano). Je, utii kwa Mungu huleta baraka? Je, kama Ibrahimu asingetii angetamkiwa baraka hizo zote? Je, neno “usimnyoshee kijana mkono wako” linahusu pia kuepuka kuwatendea vibaya vijana wetu wanapopotoka?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 23:1-20

 1. Kufiwa na mke au mume ni pigo kubwa katika maisha ya mwanadamu hasa linapotokea ugenini na ukiwa huna uwezo wa kumudu gharama za msiba. Unadhani Ibrahimu alijisikiaje kufiwa na mkewe ugenini? Je, kumlilia aliyekufa na kumwomboleza ni jambo lililo sahihi kwa wanaomwamini Mungu? Kwa nini Biblia inatushauri kwenye misiba tusihuzunike kama watu wasio na matumaini? (1 Wathesalonike 4:13). Je, kuna haja ya kuwashukuru majirani wasio waumini kwa kushiriki msiba wa muumini?
 2. Kwa nini Ibrahimu alisita kupokea eneo la kuzikia alilopewa bila malipo? Hii inatufundisha nini juu ya kutokubali vya bure bila kujiridhisha kama vina athari yoyote upande wetu? Licha ya kuwa Ibrahimu alikuwa rafiki mkubwa wa Mungu alikuwa na kawaida ya kuinama mbele ya watu wa nchi aliyoishi anaposhukuru na anapoomba kitu kwao. Hii inatufundisha nini juu ya umuhimu kwa amani na watu wote?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 24:1-67

 1. Ibrahimu alikuwa na uzee uliobarikiwa kwa kuwa na vitu vyote. Je mibaraka yake ilitokana na kuwa na uhusiano wa karibu na Mungu? Wale wanaosema kujihusisha na mambo ya Mungu au ya dini ni kutafuta kufilisika wanaitoa wapi dhana hiyo? Je dhana hiyo ina ukweli wowote? Je kuishi maisha yenye uhitaji na umaskini wa kipato ni mpango wa Mungu? (2 Wakorintho 9:8) Je mibaraka huja kwa njia ya kutoa na si kwa njia ya kuzuia? (Mithali 11:24) (Luka 6:38) Je, hali hiyo unaiona katika maisha ya Ibrahimu?
 2. Wajibu mmojawapo wa mzazi ni kumsaidia kijana wao kumudu gharama zinazoandamana na kuoa au kuolewa na kumjengea mazingira ya kutooa au kuolewa na asiye wa imani yake. Je, unaiona hali hiyo katika maisha ya Ibrahimu? Je, wazazi wa leo wanazingatia mambo hayo? Kipi bora kulipiwa mahari na mzazi wako au kujilipia mahari mwenyewe? Kipi bora kati ya kuchaguliwa mchumba na mzazi au mshenga au kujichagulia mwenyewe?
 3. Katika kutafuta mwenzi wa maisha kuna wakati wa kuomba, kutafuta, na kubisha mlango kama Yesu anavyoshauri katika Mathayo 7:7 Je, unaziona hatua hizo kwa Eliezeri aliyetumwa kumtafutia Isaka mke? Ushahidi kuwa uliyemuona ndiye ambaye Mungu amekuchagulia awe Mume wako au mke wako unaupataje? Katika kutafuta mwenzi wa maisha swala la maeneo ya kutembelea ni la msingi sana ili kuepuka kutoa malalamiko kuwa huoni wa kuoa kama vijana wengine wanavyolalamika. Unaiona hali hiyo katika kisa hiki?
 4. Je kisimani palikuwa mahali sahihi pa kupatia wachumba wa kike wenye sifa njema? Taja maeneo mengine yenye uwezekano wa kupata wachumba wafaao. Je msichana ana wajibu wowote wa kufanya kwa mwanaume anayehisi kuwa ndiye ambaye Mungu amemchagulia? Je ni sahihi kwa binti kuulizia uchumba kwa mvulana? Kutokana na kisa cha Mwanzo 24 uchumba unapaswa kuwa wa muda mfupi au mrefu? Je kila uchumba ni lazima uanzie na urafiki wa kutembeleana majumbani?
 5. Je mahari inapangwa na wenye binti au ni wale waoaji wanaotakiwa kutoa kama zawadi? Je kabla ya mahari kishika uchumba ni cha muhimu? Kumuaga binti anayeolewa kwa sherehe nyumbani kabla ya ndoa ni jambo linaloendana na Maandiko au ni desturi za watu wa Mashariki ya mbali? Je katika mchakato wa kuoa na kuolewa binti ana uhuru wa kuulizwa maoni yake? Je wazazi wana haki ya kufanya maamuzi cha mapendekezo ya watoto wao wanaooana?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 25: 1-34

 1. Baada ya kufiwa na mke au mume mtu wa Mungu anaruhusiwa kuoa tena? Kitendo hicho hakiwezi kuwa kumsaliti au kutokuwa na upendo na marehemu? Je, kuoa au kuolewe kufanyike muda gani baada ya kufiwa? Je kuna ukweli kuwa wanaume wanawahi sana baada ya kufiwa?
 2. Hali hiyo inatokana na tabia ya umalaya au hali ya upweke ambayo huwasumbua kuliko wanawake? Je ni halali kumpa au kuwapa wanao mali zote ulizonazo au wao wanatakiwa watafute mali zao wenyewe? Je Watoto wa kike wanastahili kurithi mali za wazazi wao?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 26: 1-35

 1. Kwa nini Mungu aliruhusu njaa imtokee mtumishi wake Isaka? Ahadi za Mungu wakati unapopitia changamoto za Maisha kama njaa zina umuhimu wowote? Kwa nini Mungu hakumruhusu Isaka Kwenda Misri kuhemea chakula na badala yake akamruhusu amwendee Abimaleki mfalme wa Wafilisti? Je, ni sahihi kwa mtu wa Mungu kwenda kuhemea chakula kwa watu wasiomjua Mungu?
 2. Kwa nini Isaka aliamua kumdanganya Abimaleki kuwa Rebeka ni dada yake na si mke wake? Je, upendo wa Isaka kwa mkewe na kwa Mungu wake uliyumba? Je, Ibrahimu aliona ni heri mkewe atembee na mfalme Abimaleki kuliko kumlinda kwa gharama yoyote kama alivyoapa wakati wa kumuoa? Ukiwa na mume aliyekutelekeza wakati wa shida kuna uwezekano wa kumuamini tena mtu kama huyo?
 3. Rebeka alipokula njama na Yakobo wamdanganye Isaka alikuwa analipiza kisasi uongo alionenewa? Isaka alikuwa mkuu sana kupitia shughuli za kilimo ambapo mbegu moja ilizaa mia. Hii inakufundisha nini juu ya umuhimu wa kilimo chenye tija katika kipindi hiki watu wanacholalamikia ukosefu wa ajira? Je, kilimo cha kutegemea mvua na kile cha kutegemea umwagiliaji ni kipi cha uhakika?
 4. Unajifunza nini na namna Isaka alivyoishi na Jirani zake watu wa mataifa waliotaka kumdhulumu? Je, kuna haja ya kuandaa chakula kwa ajiri ya majirani kwa lengo la kuimarisha mahusiano? Je, mafanikio ya kiuchumi ni kishawishi kwa wasiomjua Mungu kutamani kuwa ulivyo na kumfahamu Mungu unayemtegemea?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 27:1-46

 1. Isaka na Rebeka walikuwa na changamoto gani katika kuwalea watoto wao waliofarakana tokea wakiwa tumboni? Je watoto wenye tofauti ya tabia wanatakiwa walelewe kwa mtindo unaofanana au unaotofautiana? Kosa la Rebeka katika malezi ya Yakobo ni lipi na kosa la Isaka katika malezi ya Esau ni lipi? Je wazazi hawa walikuwa wamegawana watoto?
 2. Kama Mungu alisema wakati wa kuzaliwa kwa Esau na Yakobo kuwa mkubwa (Esau) angemtumikia mdogo (Yakobo, Je ilikuwa muhimu kwa Rebeka kukwepesha baraka ambazo mume wake aliziandaa ziende kwa mkubwa kinyume na Mungu alivyosema? Kwa nini baraka zilizopatikana kwa hila zilimwezesha Yakobo kutimiza kilichosemwa na Mungu. Je kuna wakati uongo husaidia kufanikisha mpango wa Mungu?
 3. Je nini husababisha ndugu waliozaliwa kwa baba mmoja na mama mmoja kuchukiana? Wazazi wanahusikaje katika kuharibu tabia za watoto wao? Je unadhani Esau angestahili kuwa mrithi sahihi wa mambo ya kiroho baada ya baba yake kufariki?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 28:1-22

 1. Kati ya Esau na Yakobo ni yupi alikuwa mtii kwa wazazi? Kwa nini Esau alijitwalia wake wengi tena kutoka usio na maadili ya kiroho kama ya wazazi wake? Baada ya hatia ya kufanya udanganyifu kwa baba yake na hila ya kuchukua mibaraka ya kaka yake Yakobo alihitaji faraja na uthibitisho kuwa Mungu bado yungali pamoja naye. Je ndoto aliyoota akiwa anaenda kwa mjomba wake ilimletea faraja hiyo? 
 2. Unajisikiaje unapohisi Mungu amekusamehe dhambi zako? Kwa nini Mungu alimtia moyo Yakobo wakati alikuwa amefanya hila? Je wakati wa kuchagua mchumba unapaswa kuwa na taswira jinsi maisha naye yatakavyokuwa huko mbeleni? Ahadi kuwa atakuwa na uzao utakaoenea pote aliipokeaje Yakobo wakati hata mke mwenyewe alikuwa hana?
 3. Je ni sahihi kuweka nadhiri katika maisha ya leo? Je umewahi kumuahidi Mungu kumtole fungu la kumi la mapato yako ikiwa atakufanikisha? Je hili linafaa kwa wale wanaotafuta kazi? Je, kipi kinatakiwa kitangulie kati ya kutafuta kazi na kutafuta mchumba? Je Yakobo alianza na kimoja au alienda na vyote? Ni sahihi kufuata mfano wake kwa maisha ya leo?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 29:1-35

 1. Jamii ya Kiyahudi ambayo Maandiko Matakatifu yanasema wokovu unatoka kwao (Yoh. 4:22) ni jamii ya wafugaji. Unadhani wafugaji walikuwa na nafasi kubwa ya kuupokea wokovu kwa kuwa umeandikwa katika mazingira wanayoyafahamu? Kwa nini kwa sehemu kubwa wapo nyuma katika kuupokea wokovu? Unadhani changamoto ipo kwa wapokeaji au wapelekaji wa ujumbe?
 2. Sifa mojawapo ya mvulana anayetaka kuoa ni ujasiri katika kutetea haki za wanyonge hasa wanawake na watoto. Unaiona sifa hiyo kwa Yakobo. Mvulana anayetaka kujamiiana kabla ya kukuoa ana huruma na wewe? Je ni muhimu mvulana aoneshe uwezo wa kukutunza kwa kulipa mahari kwa wazazi wako?
 3. Kubusiana katika uchumba ni jambo la hatari lisipofanyika kwa tahadhari.  Je busu linalofanyika watu wote wakiona kama lile la Yakobo lina hatari kama lile lifanyikalo kwenye faragha? Je busu takatifu unalielezeaje? (2 Wakorintho 13:12). Kwa nini mtu unayempenda hupati shida kumhudumia? Ni sahihi kwa mchumba wa kike kumhudumia mchumba wa kiume?
 4. Je upendo sahihi kwa mtoto wa dada yako ni kumtumikisha bila kumlipa chochote kando ya chakula na malazi au unatakiwa kumlipa mshahara? Je wale wanaokaa na watoto wa ndugu zao bila kuwasaidia kujitegemea wanawaharibu au wanawatendea wema?
 5. Unauonaje utaratibu ambao mwenye kuoa ndiye anayepanga mali ya kutoa kwa mzazi wa binti? Unazungumziaje madai ya wavulana wanaotaka kuoa bila kutoa chochote? Uongo ambao Yakobo alimfanyia baba yake naye alifanyiwa na mjomba wake. Je kulikuwa na kitu ambacho Mungu alitaka Yakobo ajifunze?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 30:1-43

 1. Mungu anasikia kilio cha wanawake walio kwenye ndoa wanaohitaji mtoto. Ukweli huo unakuhasishaje kuendelea kuombea jambo hilo? Je, kuna ukomo wa kuliombea jambo hilo? Je umri mkubwa ni kikwazo kwa Mungu kuweza kumpatia mtu mtoto? (Mwanzo 21:2; Luka 1:37). Je, mume au mke aweza kumwajiri vipi mwenzie? Unapofanya upendeleo kwa malengo maalum kwa mwenzi wako huko ni kumuajiri? Wakati hayo yanafanyika lengo huwa ni nini?
 2. Je kuna aibu yoyote kwa mwanamke aliye kwenye ndoa kukosa mtoto? Je wajibu wa mume kwa mke wa aina hiyo ni nini? (1 Samweli 1:3-8). Je wajibu mke huyo kwa Mungu wake nini? (1 Samweli 1:10-11). Je kuna uwezekano wa kudhulumiwa na ndugu wa damu tena mlio katika Imani moja? Njia sahihi ya kutatua mgogoro huo ni nini? Kwa kuangalia mfano wa Yakobo unakubaliana na dhana kuwa ndugu au watu wa imani hufanya kazi kizembe wanapoajiriwa?
 3. Kuna uhusiano gani kati ya fimbo alizozichomeka Yakobo kwenye visima vya kunywea maji na mimba walizoshika Wanyama hao? Huu uliotumika hapa ni uchawi, sayansi, au nguvu za Mungu kwa njia ya maombi? Yakobo alimlalamikia mkwewe kumdhulumu mshahara wake. Je wapo wanaodhulumu mshahara wa ndugu zao wa damu au wa Imani kwa visingizio mbalimbali? Njia aliyotumia Yakobo kutafuta haki yake haikuwa ya dhuluma?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 31:1-55

 1. Mafanikio huongeza idadi ya maadui hata miongoni mwa ndugu zako. Unaiona hali hiyo katika kisa hiki cha Yakobo? Je kushindwa kwako kuendelea maishani ni lazima kutokane na mafanikio ya wengine? Kuna wakati mambo yasipokuendea vizuri ni kwa sababu Mungu ameandaa mafanikio yako mahali pengine? Je kuna wakati katika maisha ambapo kurudi nyumbani huwa ni suluhisho la changamoto unazopitia?
 2. Mahusiano ya baba mkwe na mama mkwe huweza kuharibika hasa mnapoishi pamoja. Je katika mazingira kama hayo suluhisho huwa ni nini? Kati ya Mama mkwe na Baba mkwe ni nani huwa mkorofi zaidi? Nini siri ya Naomi kuwa na mahusiano mazuri na mkwewe Ruthu? Je ni sahihi kuendelea kufanya kazi kwa mtu anayekudhulumu au kukupunja mshahara wako? Iliwezekanaje kwa mtu anayedhulumiwa kuwa na mafanikio ya kiuchumi yanayomtia wivu tajiri yake?
 3. Je ni sahihi kumweleza mumeo au mkeo dhuluma na uonevu unaotendewa na Baba mkwe au mama mkwe? Je ni sahihi kumkabili Baba mkwe au mama mkwe wewe mwenyewe juu ya uonevu anaokutendea? Je wazazi wanaopokea mahari wanatakiwa kurudisha kwa mabinti zao sehemu ya mahari hiyo kwa kuwapa zawadi siku yao ya ndoa? Je kutumia mahari kukwamua mradi wako binafsi uliokuwa umekwama ni halali na kisha ukose zawdi ya kutoa kwa binti yako ni halali?
 4. Kwa nini Raheli alimwibia Baba yake vinyago? Kwa nini Labani alitaka kuondoka bila kuaga? Je alimshirikisha Mungu katika uamuzi huu? Kama katika msako ule Yakobo angeonekana na mali za wizi angeweza kupoteza yote aliyoyahangaikia kwa miaka 20 na hata kupoteza maisha yake. Je uaminifu kwa tajiri yako au Baba mkwe wako anayekunyanyasa na kukudhulumu unalipa?
 5. Je Raheli alikuwa mshirikina ndiyo maana aliiba vinyago vya baba yake? Je kiroho Lea alikuwa bora zaidi kuliko Raheli? Je ndugu wana uwezo wa kumaliza migogoro yao ya kifamilia na ndoa bila kulazimika kuifikisha mahakamani au kanisani? Kwa nini mara nyingi jambo hilo halifanyiki? Unadhani Labani alikuwa anawapenda binti zake na kuwatakia mema?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 32:1-32

 1. Malaika wa Mungu wana kawaida ya kupeleka taarifa njema na taarifa mbaya kwa wanadamu. Malaika aliokutana nao Yakobo wanafanana vipi na malaika waliomtembelea Ibrahimu nyumbani kwake? Je Yakobo alipata faraja yoyote kuhusiana na malaika wale?
 2. Kuna mambo maishani mwako haywezi kwenda sawa hadi umeungamiana na yule uliyemkosea. Je wazo la Yakobo la kutaka suluhu na kaka yake aliyemdhulumu lilitokana na kutambu ubaya wa kosa lake au ulitokana na kuona hatari ya nduguye kulipiza kisasi?
 3. Yakobo alionesha ubinafsi kwa kuwatanguliza wanawe mbele ili wakabiliane na adui na yeye akikaa nyuma alipodhani pana usalama zaidi? Je alimshirikisha Mungu kwenye kuandaa mpango huo au aliendelea kutegemea akili zake tu? Ubinafsi kama huu unauona ukifanywa leo na wazazi?
 4. Unapokuwa na maombi yaliyojaa hofu ni muhimu kumkumbusha Mungu ahadi alizowahi kukuahidi ili zikutie nguvu? Je ni muhimu kumwambia Mungu kuwa naogopa au nimeshindwa kwenye maombi yako ikiwa hiyo ndiyo hali halisi au hayo ni maombi ya mtu asiye na imani ambayo Mungu hapendi kuyasikia?
 5. Je zawadi zaweza kutumika kukupatanisha na uliyemkosea? Je njia mojawapo ya kupunguza uhasama na maskini waliokuzunguka ni kuwagawia sehemu ya yale Mungu aliyokubariki?
 6. Yakobo alibaki peke yake usiku mahali alipodhani ni salama zaidi kwa maisha yake lakini hapo ndipo alipokutana na mtu aliyepigana naye mieleka hadi kunakucha. Jambo hili linatufundisha nini kuhusu kumtegemea Mungu na kuacha kutegemea akili zetu?
 7. Je kuna wakati katika maisha unahitaji kumenyana na Mungu mieleka katika maombi? Je ni sahihi kuendelea kuombea jambo hadi litakapojibiwa vile unavyotaka? Kwa nini ilikuwa ni lazima yule malaika ambariki ndipo Yakobo aweze kumuachia?
 8. Unapokusudia kuacha maisha ya zamani ya dhambi kwa kubatizwa ni muhimu kuachana na majina yanayobeba dhana za maisha ya dhambi kama alivyofanya Yakobo? Unatamani kuacha uongo au dhambi nyingine kama alivyofanya Yakobo?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 33:1-22

 1. Esau na Yakobo walipokutana baada ya kupoteza kwa muda mrefu walikumbatiana wakalia. Unadhani ni hisia gani zilizowasababishia kulia? Unadhani ni kitu gani kilichosababisha Esau kubadilisha msimamo wake wa awali wa kulipiza kisasi? (Mwanzo 27:41). Kwa nini Yakobo hakutaka kujiinua mbele ya kaka yake Esau kwa mafanikio aliyoyapata huko alikokwenda kutafuta maisha na badala yake alikiri mafanikio hayo yametokana na Mungu? Kwa nini huwa vigumu kwa baadhi yetu kumpa Mungu urukufu kwa mafanikio yetu? 
 2. Kwa nini Yakobo alitumia juhudi nyingi kumshurutisha ndugu yake Esau kupokea zawadi alizomletea? Vipi kama asingepokea zawadi hizo hiyo ingemaanisha nini kwa Yakobo? Yakobo anadhihirisha kuwa na roho ya huruma kwa wanyama na watu sifa ambayo ni muhimu kwa kiongozi wa kiroho. Je huruma kwa unaowaongoza ni sifa ya lazima kwa viongozi wa aina yoyote hata wa serikali? Madhara ya kiongozi asiye na huruma ni nini?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 34:1-31

 1. Kuna msemo usemao watoto wakiwa wadogo hutukanyaga miguu lakini wakikua hutukanyaga mioyo. Unaiona hali hiyo kwa Dina Binti wa Yakobo? Je kitendo alichofanya Dina kilitia doa dini ya baba yake na kumwaibisha Mungu? Mwenye makosa katika tendo lile ni Dina au mkuu wa nchi? Upendo hauna macho unapenda yoyote bila kujali itikadi, utaifa, au hali ya kiuchumi. Utajisikiaje Binti yako anapopendwa na mkuu wa nchi ila mwenye itikadi tofauti na ya kwako?
 2. Kwa Nini Yakobo alikawia kuwaambia wanawe juu ya tukio la Dina kubakwa? Utakapojua Binti yako au mvulana ana mahusiano na wapagani utachukua hatua gani? Kuna njia mbili kuu za kuharibu tabia za watoto; ama utawafanyia ukatili au utawadekeza. Unaiona tabia gani kwenye malezi ya Dina? Kijana asiye wa imani moja na wewe anapompa ujauzito binti yako naye akitaka kuja kujitambulisha kwako akiwa na wazazi wake Ili amuoe binti yako utampokea?
 3. Je ni sahihi kumpa sharti la kujiunga na Imani yako kijana wa Imani nyingine anayetaka kumuoa Binti yako? Akikubali kubadili dini atakuwa amefanya hivyo kwa kumpenda Binti au kwa kuipenda Imani? Watawala wa Shekemu waliwaingiza matatani raia wao kwa kuwasilisha makubaliano yaliyofanyika yakificha ukweli halisi wa mambo. Unaiona hali hiyo kwa baadhi ya watawala wetu wa kisiasa na viongozi wa dini? Kwa Nini makosa ya watu wachache yanawagharinu watu wengi wasio na hatia?
 4. Unadhani hatua iliyochukuliwa na kaka zake Dina ya kuwaua wenyeji wa nchi Ile Yakobo aliafikiana nayo? Je watoto wale kwa kitendo hicho walionesha kutokuwa na nidhamu kwa baba yao? Je adhabu iliyotumika kuwaadhibu watu wa nchi Ile kutokana na kumdhalilisha dada yao ilikuwa inatoa fundisho juu ya ubaya wa kubaka au ilivuka mipaka? Ukiona dada yako anadhalilishwa utachukua hatua gani?
 5. Kwa nini wanaume wa taifa lile hawakutoa pingamizi kwa viongozi wao kuwa kuacha utamaduni wao wa kutotahiriwa ni aghali zaidi kuliko kuchukua fedha ya kwenda kununua hiyo mifugo na kutolea mahari? Je kuna uwezekano mikataba mingine inayoyalemea mataifa ya Kiafrika inatokana na kulipa adhabu ya makosa ya wakuu wa nchi? Yakobo hakujua kuwa alikuwa na binti mwenye tabia za ukahaba na wavulana wajeuri wanaoweza kuua kwa panga. Je unaweza kuwa mzazi  uliye mcha Mungu usiyejua tabia mbaya za watoto wako?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 35:1-29

 1. Wajibu wa kwanza kabla ya kufanya ibada ni kuungamiana makosa na dhambi naa kuondoa tofauti zetu. Je unafanya jitihada gani kuondoa tofauti zenu kabla hamjaenda kuabudu hapo nyumbani na mahali kwingineko? Je wanaofanya ibada huku wakiwa hawasemeshani ibada yao inapokelewa? Kwa nini ibada ya Mungu haipatani na ibada ya sanamu? Ni sanamu gani tunatakiwa tuziweke kando leo tunapoenda ibadani?
 2. Je nyumba ya Yakobo ni kielelezo bora cha nyumba ya Kikristo ikiwa ilikuwa na binti na wavulana ambao hawakuwa mfano bora na kulikuwa na ibada ya sanamu iliyokuwa inaendelea hapo na pete na vikuku? Nyumba yako ni mfano wa nyumba hiyo? Kwa nini Mungu bado alikuwa anaitembelea nyumba hiyo na kuipa ushauri wa kiroho na kuihakikishia kuwa atakuwa pamoja nayo?
 3. Je inafaa kuwavua heleni, na mikufu au kuwazuia wanaokuja wakiwa wamevaa nguo fupi ibadani? Kwa nini Mungu aliendelea kumkumbusha Yakobo ahadi ya kuwa atakuwa na uzao utakaokuwa mbaraka kwa ulimwengu? Unadhani alikuwa anamtabiria kuzaliwa kwa taifa la Israeli au kuzaliwa kwa Yesu?
 4. Ule upatanisho walioufanya Yakobo na kaka yake Esau uliwawezesha kuendesha mazishi ya Baba yao pamoja bila ugomvi wowote. Unadhani ilikuwa rahisi kushirikiana tena wako aliyekudhulumu haki yako? Je Esau alikuwa na roho ya msamaha na huruma kwa mdogo wake? Unajifunza nini ukizingatia leo hii kuna ndugu Wakristo wa tumbo moja wasiopatana? Reuben alithubutuje kulala na mama yake mdogo Bilha? Je walizoeana kwa kuwa rika lao limekaribiana? Kwa kuwa huyo mama hakubakwa inaelekea alijirahisi kwa huyo mtoto? 
 5. Unawalindaje watoto wako wakubwa wa kiume na wanawake waliopo nyumbani mwako wasio na tabia njema na wenye mwonekano wa kutamanisha na utani usiofaa? Kwa nini Yakobo haonekani kutoa kauli yoyote juu ya tukio hilo hadi wakati wa karibu na kufa kwake? (Mwanzo 49:1-4). Wanaume wanaooa mabinti wadogo baada ya kufiwa na wake zao wanatengeneza mazingira ya majaribu kwa vijana wao wakubwa?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 36:1-43

 1. Esau ni mfano wa watu waliopoteza fursa ya kuokolewa kwa kutumia vibaya uchaguzi wao. Unadhani wapo watu wenye uwezekano wa kupoteza wokovu kutokana na uchaguzi mbovu wa wenzi wa maisha? Kuna msemo ndugu wakikaa pamoja hawaishi kugombana. Kwa nini ndugu hupenda kufombana badala ya kupendana? 
 2. Je kutengana wakati fulani la ugomvi wa mara kwa mara? Je mtu aweza kubarikiwa hata kama amemwacha Mungu? Unadhani kwa nini Esau alikuwa na mali nyingi? Unajisikiaje ndugu yako mliyelelewa pamoja katika misingi ya kidoni anapoacha imani na kufuata desturi za kipagani? Je, ni mbinu gani zinatakiwa kutumika kumbadilisha mtu kama huyo?
 3. Waedomu ni uzao wake Esau na ni matokeo ya mzazi aliyepokea injili baadaye akarudi nyuma kiimani. Unawaona wapi waliorudi nyuma kiimani katika siku zijazo. Watarudi kanisani au watakuwa jamii kubwa itakayoleta upinzani kwa kanisa?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 37:1-36

 1. Je, ni sahihi kumpa zawadi mtoto wako anyefanya vizuri kwa tabia na majukumu mengine anayopewa huku ukijua wenzake pale nyumbani wanamchukia? Je, ni wazo zuri kuonyesha au kueleza mafanikio yako mbele ya watu wanaokuchukia au wanaokudharau? Kwa nini? Kwa nini Yusufu alichukiwa na ndugu zake? Pamoja na ndoto zake na tabia yake nzuri ya kutoshiriki uovu wao huenda alichukiwa pia kwa kuwa ni mtoto wa mama mdogo?
 2. Nani waliokuwa wanajaribu kuzuia ndoto ya Yakobo isitimie na kwa sababu gani? Je unadhani ni rahisi kuzuia kilichopangwa na Mungu? Unadhani ulikuwa uamuzi wa busara na wenye usalama kwa Yakobo kumtuma Yusufu akawapelekee chakula kaka zake huku akijua kuwa walikuwa wakimchukia.
 3. Ikiwa kusema ukweli kunakuongezea maadui je kujitenga na wanaofanya ubaya ili usiwaone kunaweza kuwa suluhisho? Kwa nini Reuben na Yuda walishindwa kumuokoa ndugu yao Yusufu asiuzwe utumwani ingawa walikuwa na nia njema ya kumuokoa?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 38:1-30

 1. Kwa nini Yuda alienda kuoa Mkaanani? Je, madhila yaliyomkuta ni kwa sababu ya kuoa kinyume cha utaratibu? Unajifunza nini kuhusu roho ya kuhukumu watu katika mambo ambayo hata wewe mwenyewe unayashiriki?
 2. Kwa nini ni rahisi kuona kibanzi kilicho katika jicho la mwenzako wakati wewe una boriti jichoni mwako? Njia aliyotumia Tamari kujipatia uzao ilikuwa sahihi? Njia aliyotumia Onani kuzuia mimba ilikuwa sahihi?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 40:1-23

 1. Kuna wakati Mungu huongea kwa ndoto. Je, utaratibu huo ungali hata leo? Je, kila ndoto ina ujumbe kutoka kwa Mungu? Unatofautishaje ndoto ya kawaida na ile ambayo Mungu anatoa ujumbe maalumu kwako? Je, tofauti ya mtafsiri wa kweli wa ndoto na mbabaishaji ni ipi? Kazi ya Huduma magerezani imesifiwa na Yesu mwenyewe (Mathayo 25:36). 
 2. Je, unachukua nafasi kuwahudumia walio magerezani kwa kuwatembelea na kuwapa ushauri? Je, hudhani kwamba ushauri wako unaweza kuwasaidia baadhi yao kutoka kifungo cha dhambi au kifungo cha gereza? Je, umewahi kumtendea mtu mema na alipofanikiwa akakusahau? Ulijisikiaje? 
 3. Je, unadhani ni kwa nini watu wanapofanikiwa huwasahau waliowasaidia katika mafanikio yao? Yusufu alitambua kuwa aliuzwa isivyo halali na ametupwa gerezani isivyo halali, kwa nini uelewa huo haukumfanya amsahau Mungu wake aliyeonyesha kutomsaidia?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 45:1-28

 1. Unadhani nduguze Yusufu (ukiondoa Benjamin) walikuwa na hofu gani baada ya kugundua Yusufu yu hai na anataka aonane na baba yake? Kwa nini Yusufu hakulipiza kisasi kwa ndugu zake waliomuuza utumwani walipokuja kuhemea chakula kwake? Damu ni nzito kuliko maji inadhihirishwaje katika kisa hiki? Kilio cha Yusufu kinadhihirisha nini juu ya ndugu zake? 
 2. Kwa nini wengine wakifanikiwa huwasahau watu wa nyumbani kwao? Ukweli kuwa Mungu aliruhusu Yusufu auzwe ili kuja kuwahifadhia watu chakula unatuambia nini kuhusu matatizo tunayoyapitia? Je, waliomuuza Yusufu hawana hatia kwa kuwa Mungu alipanga Yusufu aje awahifadhie watu chakula? 
 3. Wema wa Farao kwa nduguze Yusufu unadhihirisha kuwa Yusufu alikubalika. Nini siri ya kukubalika na watu hata katika nchi ya ugenini? Agizo la Yusufu kwa ndugu zake kwamba wasigombane njiani lilikuwa linaashiria kuwa Yusufu alihisi nini kwa ndugu zake? Nini kilifanya moyo wa Yakobo ukazimia na nini kilifanya moyo wake ukafufuka?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 46:1-34

 1. Unadhani Yakobo alijisikiaje kutokewa tena na Mungu katika ndoto akimhakikishia kuwa pamoja naye katika maisha yaliyoonekana kama ya kutangatanga na safari zisizo na mwisho? Unadhani Yakobo alitambua kuwa mafanikio ya mwanawe Yusufu yalitokana na uwezo wa Mungu na siyo uwezo wa mwanawe peke yake?
 2. Jamii ya Yakobo aliokuja nao Misri walikuwa sabini. Ukubali wa hao watu wote kumfuata Yakobo unakueleza nini juu ya uhusiano aliokuwa nao na watu wa nyumbani kwake? Au walikubali kumfuata kwa kuogopa wasije kufa njaa? Je, unao ushawishi wa kiasi gani kwa watu wa nyumbani mwako? Je, mtu mwenye nguvu ya kiuchumi ana nguvu gani katika familia zetu?
 3. Kitendo cha Yusufu kwenda kumlaki baba yake kinaonesha alivyokuwa na heshima kwa baba yake licha ya kuwa na madaraka makubwa. Je, ni kwa nini baadhi ya watu wakiwa na madaraka hupunguza heshima kwa waliowazidi umri? Kitendo cha yusufu kuwatahadharisha ndugu zake juu ya mila za Wamisri wasiopenda ufugaji zinaonesha jinsi alivyothamini tamaduni za watu wengine. Je, unajifunza nini juu ya kuheshimu tamaduni na Imani za watu wengine hata kama haziko sahihi kimaandiko?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 47:1-31

 1. Yusufu aliwatambulisha nduguze kama wafugaji na wacha Mungu hata Yakobo akaweza kumuombea Farao. Kwa nini baadhi ya Wasabato hawajitambulishi siku ya kwanza ya kuanza masomo au kazi kuwa kwa imani yao hawatsoma au kufanya kazi siku za Sabato? Kwa nini wakuu wa shule na waajiri wengine hawataki kutambua haki hiyo ya kisheria wakati wengine huitambua? Je ni sahihi kuwapendelea ndugu zako unapokuwa madarakani au kwa kutumia madaraka yako? Je Yesu amefanya upendeleo gani kwako ambao hukustahili?
 2. Kuwa na mahusiano mazuri na mkuu wako wa kazi kuna faida gani? Je unadhani Yusufu alikuwa na mahusiano mazuri na bosi wake Farao? Kwa nini alishindwa kuwa na mahusiano mazuri na ndugu zake? Je kuwa na mahusiano mazuri na wakubwa zako kazini kwaweza kuwatengenezea ndugu zako ajira? Kwa nini Yusufu alikataa kuwapa Wamisri chakula cha bure wakati aliweza kuwapa ndugu zake chakula na kuwarudishia fedha yao? 
 3. Je watoto wanaoomba kuchangiwa ili waende kambi lao la watoto wanatakiwa wapewe bure fedha hiyo au wafanyishwe kazi? Kwa nini kwa kawaida wakulima wengi hushindwa kujiwekea akiba ya mazao na matokeo yake kukosa hata mbegu ya kupanda msimu ujao? Mpango wa kutoa kwenye mapato sehemu ya tano ambayo ni sawa na asilimia 20 ni sawa na utaratibu wa kutoa kwa mpango unaohimizwa na kanisa la Waadventista? Je wanaotoa kwa mpango wana uhakika wa mapato yao kutotindika? 
 4. Kama kila muumini kanisani kwako angetoa 20% kanisa lingekuwa na mafanikio gani? Kwa nini Israeli alimpa agizo la atakakozikwa Yusufu ambaye hata hakuwa mzaliwa wa kwanza? Je alimpendelea Yusufu kwa kuwa ndiye aliyemtunza katika uzee wake au kwa kutii ndoto ya Yusufu ambayo hapo awali hakuiamini? Ni jambo muhimu kuwatunza wazazi katika uzee wao ili kurefusha umri wao wa kuishi? Unadhani Yusufu alilifanya hilo kwa Baba yake?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 48:1-22

 1. Yusufu anaposikia baba yake anakaribia kufa anapeleka watoto wake ili wabarikiwe. Unafanya jitihada gani kupata baraka za wazazi wako kabla hawajafa? Wazee wenye umri na wenye kuijua vyema historia ya tulikotoka ni hazina. Kizazi cha sasa kinafanya jitihada kupata hazina hiyo sasa kabla haijatoweka kabisa?
 2. Efraimu na Manase watoto wa Yusufu waliingizwa katika orodha ya watoto wa Yakobo ili kukamilisha idadi ya kabila 12 za Israeli. Unadhani ni kwa nini Yakobo alifanya hivyo? Kwa nini Yusufu alitaka kuingilia kati utowaji wa mibaraka ya baba yake kwa watoto wake Efraimu na Manase? Unadhani ni kwa nini Yakobo alikumbusha tukio la kufiwa Raheli kwa mwanae Yusufu? Hii inaonesha jinsi alivyompenda Raheli na jinsi kifo hicho kilivyomwachia jeraha la kudumu?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 49:1-33

 1. Je, ni wajibu wa mzazi kuwajulisha watoto yatakayowapata siku za mwisho? Je maneno ya mwisho ya mzazi yana mchango gani katika kuyaongoza maisha ya mtoto? Je, ni vizuri kutamka laana kwa mtoto? Mtoto wa kwanza kuzaliwa anatarajiwa kuchukua nafasi gani katika familia? Kwa nini watoto wengi wa kwanza wameshindwa kufikia matarajio ya wazazi? Je, kosa alilolifanya Reubeni halikuwa na uwezekano wa kusameheka kwa baba yake? Je lilitosha kumuondolea sifa ya mzaliwa wa kwanza? 
 2. Wanadanu wote watakaokombolewa watapewa hadhi ya kuwa wazaliwa wa kwanza. Unadhani wanastahili sifa hiyo? (Waebrania 12:22-23). Je kile alichofanya Yuda kumtetea mdogo wake Benjamini na baba yake na kujitoa ili a achukue adhabu iliyomstahili mdogo wake (Mwanzo 44) kilichangia kumpandisha hata likawa ndiyo kabila linalotoa viongozi? Je, uongozi unasomewa au uongozi unawahusu wazaliwa wa kwanza au huwa mtu anazaliwa nao? ( Zaburi 89:27). Je, wapiga mishale gani unaowakumbuka maishani mwako waliokutenda machungu lakini bado uliendelea kusimama? 
 3. Ili kuiokoa familia na kutimiza makusudi ya Mungu maishani wakati fulani huwa ni lazima kujitenga mbali na familia na marafiki zako na kwenda kuishi uhamishoni kama Yusufu? Je ni vizuri kuwa na mazoea ya kuwaombea watoto wako baraka? Je baraka unazowatamkia watoto wako zina uwezekano wa kuwapata? Je, ni lazima ukifa ukazikwe kwenye eneo walikozikiwa wazazi wako? Kwa nini baada ya kumaliza hotuba yake kwa wanawe Yakobo alifariki. Je alijua kuwa saa yake ya kuondoka duniani imefika?


MASWALI YA KUJADILI: MWANZO 50:1-26

 1. Je, ni sahihi kuiangukia maiti na kuibusu kutokana na kushikwa na uchungu wa kufiwa na upendo kwa marehemu? Je kubusu maiti na kuiaga ni kukubaliana na dhana potofu kuwa aliyekufa bado yu hai? Je kuihifadhi maiti kwenye jeneza la thamani ni dalili ya upagani na matumizi mabaya ya raslimali? Je kuihifadhi maiti isioze inaendana na mafundisho ya dini? Kwa nini watu humaliza msiba baada ya siku arobaini? Je kuliliwa sana msibani ni dalili kuwa ulipendwa na watu au ulipendwa na Mungu? Kitu gani kiliwafanya Wamisri wamlilie Israeli kwa siku sabini?
 2. Je, kujiandalia maziko kwa kutayarisha kaburi lako na sanda ukiwa hai ni njia ya kuwapunguzia waliobaki mzigo wa gharama au ni uchuro na kujitabiria kufa? Yakobo au Israeli alizikwa kwa heshima ya kitaifa mazishi yake yakihudhuriwa na wazee wote wa ikulu na wazee wote kutoka nchi ya Misri tofauti na pacha mwenzake Esau. Je hiyo inatokana na yeye Yakobo kumpa Mungu kipaumbele maishani mwake au ni upendeleo kutoka kwa mwanae Yusufu? Je unauona uwezekano wa kuzuka mgogoro mkubwa Katika familia ya Yakobo kama Yusufu asingetumia hekima na busara kuumaliza? 
 3. Je unauona umuhimu wa wazazi kumaliza migogoro ya watoto wao kabla hawajafa? Je unakubaliana na mbinu waliyotumia kaka zake Yusufu kuumaliza mgogorro huo? Katika kila jambo baya analotendewa mcha Mungu kwa nia ovu Mungu huligeuza jambo hilo hilo kuleta matokeo mema kwa watu wengi. Unaiona hali hiyo katika kisa cha Yusufu? Je kisa cha Yusufu kimekuongezea ari ya kutokata tamaa unapotendewa mabaya na kutolipiza kisasi? Yusufu bado anajitambua kuwa ni muumini wa tumaini lililowekwa na Mungu kwa wazazi tofauti na watu wengine ambao wakipata madaraka makubwa husahau mambo ya dini. 
 4. Nini kilimsaidia Yusufu kubaki mwaminifu kwa Mungu wake licha ya kuwa na madaraka makubwa? Yusufu aliagiza mifupa yake ibebwe wakati wana wa Israeli watakapokuwa wanaondoka Misri kuelekea Kaanani. Unadhani agizo hili lilikuwa na umuhimu wowote? Unadhani wana wa Israeli kwa kutii agizo hili (Kutoka 13:19; Yoshua 24:32) walionesha kumkubali Yusufu kama kiongozi wao wa kiroho? Kubeba mifupa ya marehemu ili kwenda kuizika nyumbani kama walivyofanya Waisraeli inatofautianaje na inalinganaje na desturi ya kuhamisha msiba inayofanywa na baadhi ya makabila hapa nchini?