Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

TUZUNGUMZIE UCHUMBA

TUZUNGUMZIE UCHUMBA

Uchumba ni hatua ya mpito kuelekea kuoana. Watu wawili wa jinsia tofauti wakikubaliana kuishi pamoja kama mume na mke katika siku za usoni huanzisha mahusiano yanayoitwa uchumba. Uchumba si ndoa. Katika uchumba mahusiano ni ya kirafiki yasiyohusisha kujamiiana. Uchumba ni hatua ya msingi ya ndoa. Makosa yakifanyika katika uchumba yanaathiri ndoa. Kwa hiyo ni muhimu kufanya maamuzi kwa makini katika uchumba. Huu ndiyo wakati ambao mtu huweza kudhani vyote ving’aavyo ni dhahabu wakati vipo vinavyong’aa ambavyo si dhahabu kabisa.
Mjue unayemchumbia

Unataka mchumba wa namna gani?

Eneo muhimu na linalohitaji umakini wakati wa kufanya uchumba ni aina ya mtu unayemchumbia. Lazima ujiridhishe kuwa unayechumbiana naye ndiye hasa chaguo la moyo wako na anakidhi vigezo vya maisha unayokusudia kuishi huko mbeleni. Ni lazima akuvutie ndiyo hilo ni muhimu. Maana haikubaliki kuoa au kuolewa na usiyempenda. Wakati wa kufunga ndoa swali moja linaloulizwa kwa kurudiarudia na kwa kubadilisha maneno ni lile linalotaka kufahamu kama mchumba uliyemchagua ulimchagua mwenyewe kwa hiari na utakuwa tayari kuishi naye siku zote na katika hali zote. Swali hilo wengine wamekuwa wakilijibu kirahisi bila kuzingatia mantiki yake. Muhimu sana kujiridhisha kama unayemchumbia unampenda.
Pima upendo wake

Upime upendo:

Lakini muhimu zaidi ni kujua upendo ulio nao kwa mchumba wako ni wa kweli ama wa bandia. Upendo wa kweli unadumu. Upendo wa kweli hauvutiwi na mali na mwonekano peke yake. Ni dhahiri kuwa wavulana wengi huvutiwa na mwonekano kabla ya kitu kingine, wakati wasichana wengi huvutiwa na mafanikio ya mvulana na wakati fulani sura yake. Hivi si vitu vibaya lakini havipaswi kuwa vipaumbele. Kwa nini? Uzuri na mali huwa vinaisha na kama upendo ulikaia juu ya hivyo si nao utaisha. Muungano wa ndoa ulikusudiwa uwe wa kudumu si wa majaribio. “Akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. (Mathayo 19:5-6) Kwa hiyo sifa za waoanaji pia ni lazima ziwe za kudumu si za mpito. Jiulize unampenda mchumba wako kwa dhati au kwa msisimko tu?

Mwalike Mungu akusaidie:

Kuchagua mchumba anayefaa ni mtihani unaowakabili wanadamu wote. Kutokana na ugumu na unyeti wa jambo hili Mungu ametoa ahadi kwa wote wanaotafuta wachumba kuwa atawasaidia. “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” (Mithali 19:14) Mke mwema au mume mwema hapatikani kwa uchaguzi wa kibinadamu peke yake. Wala hapatikani kwa kuchaguliwa na wazazi au viongozi wa dini. Mume ama mke mwema hutoka kwa Mungu. “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.” (Yakobo 1:17).

Usidanganyike:

Kwa nini Mungu amejichukulia jukumu hili la kuwachagulia wanadamu wachumba? Je, ana kusudi la kuwanyima uhuru wao wa kuchagua wampendaye? La, hasha. Mungu anajua kuwa maamuzi yetu ya kibinadamu yanaharibiwa na uwezo hafifu wa mioyo yetu katika kupima mambo. Mioyo yetu ni midanganyifu. “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” (Yeremia 17:9) Ni rahisi mwanadamu kudanganyika kuwa unapenda au unapendwa wakati kiuhalisia sivyo ilivyo. Kuna wengi wamelizwa na wachumba wao. Wavulana wamelizwa na wasichana nao wamelizwa. Baada ya kupotezeana muda kwa ahadi tamu tamu wamekuja kuachana ghafla jambo lililoleta maumivu ya kutisha. Wengi katika hatua hiyo wamekiri hawakuwajua vizuri wachumba wao. Na wengine waliachwa hata na wachungaji! Mchumba mzuri hatokani na kazi anayofanya bali na jinsi alivyo.

Usitegemee wanadamu:

Usitegemee wanadamu katika kufanya maamuzi hasa yanayohusu uchumba. “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.” (Yeremia 17:5). Mtu anayekufaa wewe alishaandaliwa na Mungu kitambo wakati ukiwa huna taarifa yoyote. Kabla wewe hujazaliwa na yeye hajazaliwa. Hata mke wa Adamu aliandaliwa, yeye Adamu akiwa usingizini. “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.” (Mwanzo 2:21-22)

Washirikishe watu wanaoaminika:

Kutafuta mchumba ni kazi inayostahili kushirikisha watu lakini siyo kuwategemea watu. Isaka alipotaka kuoa alimshirikisha baba yake. “Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.” (Mwanzo 24:2-4).

Washirikishe wazazi:

Wazazi wana nafasi katika kutoa ushauri juu ya yule utakayemuoa au utakayeolewa naye. Lakini hawapaswi kulazimisha mawazo yao. Mwisho wa yote atakayeoa ndiye anayefanya uchaguzi wa mwisho. Ingawa Isaka hakushiriki katika mchakato wa kuchagua lakini aliridhia chaguo alilofanyiwa na mtumishi wa baba yake. Na Rebeka naye ingawa alimkubali Isaka wakati hajamuona, bado alipokutana naye aliridhika kutoka moyoni mwake. “Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.” (Mwanzo 24:64-67)

Washirikishe viongozi wa kiroho:

Hakuna tofauti sana kama leo mzazi, au kiongozi wa kiroho atamwita mvulana au msichana kushauriana naye swala la uchumba hasa akihisi muda umefika na pengine unakaribia kupita ili kujiridhisha kama anafahamu wajibu unaomkabili? Si wote wanaofahamu nini wafanye na wafanyeje wakati umri wa uchumba unapokuwa umetimu. Wengine wamekiri kabisa kuwa wameshindwa kujua vigezo, wengine wameshindwa kujua akikutana na msichana amwambieje, wengine wameshindwa kufahamu dalili za mvulana ama msichana anyempenda na kwa kukosa kuzijua stadi hizo wamepoteza wachumba na kuchelewa kuoa ama kuolewa. Wazazi na viongozi wa kiroho wasilikwepe jukumu hili. Wakutane na vijana wao na wawape ushauri wa namna ya kufanikisha mchakato wa uchumba. Pamoja na ushauri wanapaswa kuwaunganisha na Mungu mwenye majibu ya kuaminika juu ya changamoto zao.

Vigezo na masharti:

Kuoa na kuolewa kunawahusu wote waliofikia umri unaostahili jambo hilo na wenye vigezo vingine muhimu vinavyohitajika katika kuoa na kuolewa. Kwa majaliwa ya mwenyezi Mungu karibu watu wote huwa na vigezo vya kuoa na kuolewa. Vigezo hivyo ni pamoja na uwezo wa kukidhi majukumu na kutoshelezana katika ndoa. Dhambi imesababisha baadhi ya wanadamu kupoteza uwezo wa kutoshelezana katika ndoa. Hawa pamoja na kufikia umri unaostahili hawawezi kushughulika na uchumba. Paulo ni mfano wa watu hawa. “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” (1Kor. 7:8-9).

Ukomavu wa akili na viungo:

Kuchumbia si jambo la kitoto linahitaji waliokomaa akili na viungo. Wakati fulani kuchumbia kunahitaji kufikia kiwango fulani cha kujitegemea kwa ama kuwa na kazi ya kuajiriwa ama kujiajiri ili kuweza kujikimu kimaisha. Hata hivyo kutokuwa na ajira hakuzuii mchakato wa uchumba kuanza ikiwa wahusika wamejibainisha kuwa wamekomaa akili na viungo. Kukomaa kiakili kinahusisha uwezo wa kujitambua wewe ni nani, unataka kufikia malengo gani maishani, na mpango kazi unaotembea nao sasa ili kufikia malengo hayo. Katika mpango kazi kutaonekana lini unataka kuoa ama kuolewa, lini utaanza mchakato wa uchumba, unataka ndoa yenye watoto wangapi, lini unafikiria kufikia ukomo wa kuzaa, na mipango yako mingine ya kujiendeleza kielimu na kiuchumi.

Dalili za kutokomaa:

Kushindwa kujibu maswali haya muhimu kutaashiria kuwa mhusika hajakomaa kiakili na hivyo hajawa tayari kwa mchakato wa uchumba. Kutokomaa kwa akili kutadhihirika pia kwa njia ya mhusika kutoweka bayana ni yupi hasa anampenda na vigezo anavyotumia. Wapo wanaouchimbia kila msichana anayevutiwa naye na wako wanaochumbiwa na kila mvulana aliye maarufu. Na wengine hufikia hatua ya kuwa na wachumba zaidi ya mmoja kwa wakati. Akili iliyokomaa na iliyotulia haiwezi kufanya mchezo huo. Ina malengo sahihi, yenye mikakati sahihi na vigezo sahihi. Akili iliyokomaa na iliyotulia haikurupuki kufanya uteuzi wa mchumba bila kufikiria. Na akili iliyokomaa na iliyotulia haitoi taarifa zote za uchumba wake kwa kila aliye rafiki yake. Akili iliyokomaa inajua kutunza siri.

Tabia za kitoto:

Akili iliyokomaa na kutulia hutumia fedha kwa uangalifu. Mwenye akili iliyokomaa hatapanyi fedha ili kuhadaa watu kuwa fedha siyo tatizo kwake wakati ukweli ni kuwa fedha yenyewe pengine ni ada ya shule na hali ya nyumbani kwake ni duni. Mwenye akili iliyokomaa hana sababu ya kuazima mavazi ili kuwahadaa watu kuwa yeye ana uwezo wa kubadili mavazi wakati hali yake ya uchumi ni duni. Mwenye akili iliyokomaa anamjua anayemtaka na yupo tayari kumsubiri. Hata vikwazo vikitokea atasimama naye. Hakatishwi tamaa changamoto zinapojitokeza. Hata akikataliwa haoni vibaya kurudi tena na tena huku akisukumwa na dhamira inayomhakikishia kuwa yule anayemkataa ndilo chaguo la Mungu kwake.

Ziishi ndoto zako:

Mwenye akili iliyokomaa haogopi kufanya jambo lenye manufaa hata kama machoni pa vijana wenzake litaonekana linamshusha. Kwake jambo la muhimu ni lile linalomwongezea uwezo wa kiuchumi ama kielimu. Kijana aliyekomaa kiakili anajua kudunduliza kila anachopata. Anauangalia wakati ujao na anatafuta mbinu za kuukabili. Kijana mwenye akili zilizokomaa anaziishi ndoto zake. Haishi kwa ajili ya leo tu. “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.” (Mhubiri 11:9)

Ukomavu wa akili:

Akili iliyokomaa ni kigezo muhimu sana katika kuanzisha uhusiano wa uchumba. Kukomaa kwa akili si lazima kuendane na umri wa mtu. Wapo ambao akili zao hukomaa mapema kuliko umri wao. Na wapo ambao akili hukawia kukomaa tofauti na umri wao.  Kwa hiyo kigezo cha ni umri upi unafaa kunza mchakato wa uchumba itategemea sana akili ya mchumbiaji na mchumbiwa. Hata hivyo kwa kawaida umri unaotarajiwa mtu azungumzie uchumba ni kuanzia miaka 24. Inaweza kuwa mapema kidogo kuliko hapo au miaka michache mbele. Umri huo unashabihi mtu aliyesoma bila kukwama kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu. Katika umri huo akili ya kawaida huwa imefikia hatua za kuanza kukomaa. Ndoa zilizo mapema sana au mbele sana ya umri huo hukabiliwa na changamoto za mwili kutokuhimili mikiki ya uzazi ama mwili kufikia ukomo wa kuzalisha watoto.

Ukomavu wa kimwili:

Ukomavu wa mwili ni kigezo kingine muhimu katika kuamua ni lini mchakato wa uchumba uanze. Moja ya majukumu makubwa ya ndoa ni mwanamke kuzaa watoto na mwanaume kuhangaika kutafuta riziki kwa ajili ya familia. “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” (Mwanzo 3:16) “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” (Mwanzo 3:17-19).

Usioe na kuolewa mapema:

Mwanamke anayeolewa na kuzaa mapema anahatarisha afya yake kwa kuwa viungo vyake vinakuwa havijakamilika kuweza kuhimili mikiki mikiki ya kujifungua. Wengi ama hufa ama kupata maradhi au kusababisha matatizo kwa watoto wanaozaliwa wakati wa kujifungua. Wazazi wenye tabia ya kuwaoza watoto wao wangali wadogo waache mila na utaratibu huo maana unawanyima watoto wao haki ya kufurahia ndoa. Ukomavu wa viungo huenda sambamba na usalama wa viungo vyenyewe – na hasa viungo vya uzazi. Viungo vya uzazi vikitunzwa vyema huwa salama wakati wa uchumba lakini visipotunzwa huathirika kwa njia ya maambukizo na hatima yake ni kupata ulemavu wa kudumu au maradhi yasioyoponyeka. Maradhi kama ya saratani ya shingo imegundulika kuwa huweza kusababishwa na kujamiiana katika umri wa utotoni. Kanuni ya msingi kwa wavulana na wasichana ni kutoyachokoza mapenzi mpaka wakati muafaka utakapofika. “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe” (Wimbo Ulio Bora 2:7)

Wazazi washauriane na watoto wao:

Wazazi wana wajibu muhimu wa kuwalea watoto wao katika maadili ili waje kuingia katika majukumu ya ndoa kwa mafanikio. Pamoja na kuwapa maadili mema wanapaswa kushauriana nao kwa upendo na kusikia maoni yao hasa wanapokaribia umri wa kuoa na kuolewa. Wasiwachukulie kama ni watoto wasio na uwezo wa kujadili mamabo yanayowahusu. Wazazi wengine wamelaumiwa kwa kutumia fursa ya mabinti zao kuolewa kwa kuwachagulia wachumba wa kuwaoa kinyume cha matakwa yao. Mara nyingi vigezo vinavyoangaliwa ni uwezo wa kiuchumi (mahari) au kabila la muoaji kuliko sifa zingine za msingi. Huo ni ubinafsi unaoangalia faida ya wazazi pekee bila kuzingatia matakwa ya waoanaji. Hilo halipo sahihi na linapaswa kurekebishwa. Vijana wanaooana kwa shinikizo la wazazi huanza vibaya ndoa yao na uwezekano wa ndoa hiyo kudumu au kuwa yenye furaha ni mdogo.

Wazazi wasilazimishe mawazo yao:

Wapo na wazazi wengine wanaowaozesha vijana wao wa kiume kwa haraka ya kupata mjukuu. Kijana muoaji anaendelea kuishi kwa wazazi na mkewe na kupangiwa shughuli za kufanya na wazazi wake. Hilo nalo haliko sawa. Ndoa ni taasisi inayojitegemea ikiwa na serikali yake na haipaswi kuingiliwa katika maamuzi yake ya kila siku. “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” (Mwanzo 2:24). Ndoa za utotoni na zenye kulenga kujinufaisha kwa upande wa wazazi bila kuzingatia maoni ya waoanaji zinakiuka haki ya msingi ya wanandoa na ni chanzo cha migogoro mingi ya ndoa. Wazazi tujielekeza katika wajibu wetu wa kuwa washauri tu kwa watoto na si kulazimisha mawazo yetu. Pia tuendelee na jukumu la kuwaombea watoto wetu ili Mungu awape hekima katika maamuzi ya jambo hili nyeti. Wale ambao wameweka juhudi ya kutosha katika kuwaombea watoto wamevuna mafanikio.

Tatizo la ndoa zilizochelewa:

Tatizo la ndoa za utotoni linaonekana kuanza kutoweka na tatizo jingine limeanza kuja kwa nguvu. Tatizo linaloonekana kuja kwa nguvu kwa sasa ni la wavulana na wasichana wanaokawia kuoa na kuolewa. Limeanza kuwa jambo la kawaida kuona wavulana na wasichana wenye miaka 35 hadi 45 ambao hawajaoa na kuolewa. Baadhi yao hata hawajui wataoa na kuolewa lini. Kwa sehemu haya ni matokeo ya vijana kuwa katika masomo kwa muda mrefu ama kutafuta kujiimarisha kwanza kiuchumi kabla hawajachukua hatua hii nyeti.

Kukosa uaminifu:

Lakini nyuma ya madai hayo kuna uwezekano mwingine wa mambo yasiyofaa yanayoendelea kwa baadhi ya vijana hawa. Yapo madai kuwa wapo vijana wanaoendelea kujamiiana wakati wanaendelea na masomo na hata baada ya kumaliza masomo na hivyo hawaoni haja ya kuoa na kuolewa kwa sasa. Madai haya yakiwa ya kweli basi kuna janga linalozijia familia za vijana hawa pindi watakapoamua kuoa na kuolewa. Itakuwa vigumu sana kwao kuvunja mazoea hayo wakiingia kwenye ndoa zao. Tunawashauri vijana kujiepusha na mazoea hayo ya kujamiiana kabla ya ndoa. Mahusiano ya mvulana na msichana yazingatie ushauri Mungu anaoutoa kwao. “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.” (1 Wakorintho 7:1).

Ukomavu wa kiroho:

Sifa nyingine muhimu ili mtu awe na uhalali wa kuingia kwenye mchakato wa uchumba ni kuwa na ukomavu wa kiroho. Ukomavu wa kiroho hapa nakusudia kiwango cha kutosha cha kumwelewa Mungu na ahadi zake. Mungu ni mdau mkubwa katika mchakato wa kutafuta mchumba. Mungu hajihusishi tu na maswala ya uchumba peke yake bali anajihusisha na mafanikio yako yote katika maisha haya ya sasa na yale ya milele. “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (1 Petro 5:7)  Mungu anataka ufanikiwe katika mambo yote unayoazimia kuyafanya maishani. Hana mpango wa kukukwamisha bali kukusaidia. Anakuwazia mema si mabaya. Katika kitabu cha Yeremia anasema; “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yeremia 29:11)

Mtegemee Mungu:

Kutambua kuwa hupo peke yako katika mapambano yoyote yale ni jambo linaloongeza hamasa ya kusonga mbele kwa mafanikio. Katika kutafuta mchumba Mungu ameahidi kusaidia. Lakini Mungu hatasaidia ikiwa hajaombwa kufanya hivyo. Usitegemee akili zako mwenyewe. “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” (Mithali 3:5). Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kushinda vishawishi vya dhambi kwa nguvu zake mwenyewe. Paulo anaieleza hali hiyo anapowaandikia warumi. “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.” (Warumi 7:18-19)

Usikate tamaa:

Vijana wanaosumbuliwa na majaribu na walioangushwa katika majaribu hayo, Yesu anawaalika waje kwake. “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” (Mathayo 11:28). Anaahidi kuwasamehe kabisa na kuwapa nguvu mpya. “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.” (Isaya 43:25). Jambo muhimu ukisamehewa ni kuamini kuwa upo huru. Mungu akikusamehe hakumbuki. Na ukisamehewa unaanza ukurasa mpya wa matengenezo. Hurudii matapishi. Unasonga mbele. Mtu aliyekomaa kiroho anatambua kuwa uwezo wa kutenda mema hautokani na uwezo wake. Ni neema ya Mungu. “Ee Bwana, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:230)

Mungu ni rafiki yako:

Mungu ametuchagua wanadamu tuwe marafiki zake pamoja na kutambua udhaifu wetu. “Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.” (Yeremia 31:3). Na pamoja na kushindwa kwetu mara nyingi Mungu anaahidi kuwa hatatuacha. Mungu akiahidi kitu kwako habadilishi. Aliwaahidi uzao wa Ibrahimu ahadi na ametimiza. “Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” (Mwanzo 28:15). Moja ya mambo ambayo Mungu amewaahidi wanaotaka kuoa na kuolewa ni kuwapatia wenzi wa maisha. “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” (Mithali 19:14). “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” (Mwanzo 2:22-23)

Ujue mpango wa maisha yako:

Kila binadamu aliyekuja duniani ana mpango maalumu ambao Mungu amekusudia autekeleze kwa manufaa yake mwenyewe, kwa manufaa ya wanadamu wenzake, na kwa utukufu wa Mungu. Ili kufanikisha kutekeleza mpango huo Mungu amewekeza kwa kila binadamu uwezo wa kutekeleza mpango huo. Jukumu la binadamu ni kutambua mpango ambao Mungu ameukusudia kwake na uwekezaji ambao Mungu amefanya kwake ili kufanikisha mpango wenyewe. Tunapotambua mpango wa maisha yetu na kutambua nay ale Mungu alitupatia kufanikisha mpango wa maisha yetu, na kuwa tayari kushirikiana naye katika kufikia malengo hayo ndipo tunapoweza kufikia mafanikio makubwa sana maishani.

Mungu ni kocha wako:

Moja ya maeneo ambayo Mungu anataka ufanikiwe ni katika mpango wa ndoa. Ndoa na familia ni msingi wa kujenga jamii iliyo bora na yenye mafanikio. Mungu alitoa ndoa kama zawadi kwa mwanadamu kwa sababu alijua anahitaji ndoa – anahitaji kuwa na mwenzi wa maisha mwenye kumtosheleza pale alipopungua. Ndoa ni kama timu ya mpira ambapo mafanikio huja kwa wachezaji wa nafasi mbalimbali wanaposhirikiana. Na kama ilivyo katika timu ya mpira wachezaji wa nafasi mbambali huchaguliwa na kocha wa timu. Hivyo Mungu anakuchagulia mwenzi wa maisha utakayeshirikiana naye kuleta ushindi wa timu yenu ya ndoa. Lakini shetani aliye adui mkuu wa wanadamu akitaka kuvuruga mafanikio ya wanadamu aliishambulia ndoa na juhudi zake za sasa zinatishia kuisambaratisha kabisa ndoa yenyewe.

Wengine walio kwenye soko la uchumba:

Kuna watu wamefiwa na wenzi wao wa maisha na sasa ni wajane. Wanajiuliza waoe na kuolewa tena ama la. Kuna wale walioachika na waume zao au wake wao. Nao wanajiuliza tuone na kuolewa tena au la. Kuna wale wale ambao walizalishwa na kisha kutelekezwa nao wanajiuliza waolewe au wabaki wazazi wanaolea watoto peke yao (single parents) au la. Kuna wale ambao umri umeenda sana kiasi wanshindwa kujitambulisha upande wa vijana au upande wa wanandoa. Hizi ni changamoto ambazo lazima zitafutiwe majibu. Tunawahimiza hata wale ambao si vijana lakini wanahitaji wachumba kutumia fursa iliyopo kupata wachumba kwa kadri Mungu atakavyowaelekeza.

Mungu atakusaidia:

Mungu anajua hali mbalimbali wanazopitia wandamu na ana mpango wa kuwasaidia. Ikiwa Mungu ana mpango wa kukusaidia naomba usikate tamaa. “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” (Isaya 41:10). Wajane ambao wanajisikia kutaka kuoa na kuolewa tena wanashauriwa kufanya hivyo bila kusita. “Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.” (1 Timotheo 5:14). Na wale walioachika na ama kutelekezwa baada ya kuzalishwa nao waolewe. “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” (1Wakorintho 7:8-9).

Usiishi na uchungu moyoni:

Wazazi wanaolea watoto peke yao wanaweza kudhani hawahitaji tena kuolewa kutokana na machungu waliyoyapitia huko nyuma lakini huo siyo utatuzi. “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” (Waefeso 4:26) Wanachotakiwa ni kuchukua hatua za kusamehe na kujisamehe wenyewe na kuendelea na maisha. Kusamehe ni njia sahihi ya kuondosha uchungu moyoni. “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” (Waefeso 4:31) Maisha ili yakae vizuri yanahitaji timu ya mwanaume na mwanamke wanaoishi kama wanandoa. Matatizo yaliyotokea katika ndoa ya zamani si lazima kuwa yatatokea katika ndoa utakayofunga tena. Ukidumisha roho ya msamaha utaishi maisha ya amni. “Mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”  (Waebrania 12:15).

Kuchumbia ni haki ya kila mwenye vigezo:

Tunapozungumzia uchumba tunazungumzia makundi yote. Wale vijana ambao hawajazaa wala kuoa na kuolewa, wale ambao waliwahi kuzaa bila kuolewa na kuoa, wale ambao wamefiwa na kuachika, na wale ambao wanadhani wanaweza kuishi bila ndoa kutokana na kuendelea kulea machungu waliyoyapitia huko nyuma – hawa wote wanayo fursa ya kuchumbia wakitaka. Tatizo linalowakuta wengi kudhani kitendo cha kujitambulisha kuwa unahitaji mchumba ni aibu. Kuchumbia hakuna aibu yoyote. Ni haki ya kila mtu.  Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kuwepo watu wanaoratibu mipango hii ya uchumba. Viongozi wa kiroho na wazazi wa watoto wasilikimbie jukumu hili maana ni lao

Kutojamiiana kabla ya ndoa:

Ni jambo bora kuoa na kuolewa na aliye bikira. Lakini dunia hii iliyojaa changamoto watu wenye sifa hiyo si wengi kama ambavyo ingetarajiwa. Hii na kwa sababu ya wengine kupitia changamoto fulani fulani za maisha. Jambo la muhimu ni kujua kisa kilicho nyuma ya kila mwenye tabia hiyo na kuona kama alijutia kosa hilo kuliko kuendelea kumhukumu tu. Wapo walioingizwa katika kuzalishwa katika mazingira yaliyokuwa magumu na wanajutia hali hiyo. Hawa wanaweza kuwa wachumba wazuri kama wale walio bikira na hata wakati mwingine kuwazidi.

Usitelekeze uliowaharibia maisha:

Ni wachache sana kati ya wale wanaopenda kuoa mabikira ambao wao wenyewe ni mabikira – yaani wamejitunza katika ujana wao. Na kwa hiyo sababu za kupenda kuoa mabikira zisiwe za ubinafsi. Iwe na wewe pia kweli ulikuwa mwaminifu. Ubinafsi mwingine ambao usingefaa uwepo ni ule wa kuwaharibia mabinti kadhaa usichana wao kwa kuwazalisha na halafu wakati wa kuoa unawaacha na kutafuta aliye bikira. Huo ni ubinafsi mbaya. Ikiwa kwa bahati mbaya ulimzalisha binti au ulimwingilia kwa kumuahidi kumuoa ni lazima utimize ahadi hiyo kwa kumuoa huyo huyo na si mwingine. Idadi ya watoto wa mitaani inayozidi kuongezeka inachochewa na idadi inayoongezeka ya wanaume wanaozalisha bila kutunza watoto wao au kuwaoa wazazi wa hao watoto. Ni jambo lenye uchungu mkubwa kukuta aliyeahidi kukuoa akikutelekeza na kuoa mwingine na huku pengine akikuachia ujauzito. Wengine wamejaribiwa kunywa sumu ili wafe au kutoa mimba na kuishia kuharibu kizazi chao.

Zikimbie tamaa za ujanani:

Hata hivyo ni vizuri wasichana wakajitunza katika ujana wao. Wapo waliofanya hivyo na Mungu awabariki. Si jambo rahisi linahitaji kujitambua na kuishi katika ndoto zako. Ikiwa utaamua ni jambo linalowezekana. Tambua kusudi la kuja kwako hapa duniani ni nini? Je, ni kutumika kama chombo cha kuburudisha wengine ambao mwisho wa yote wanakutupa kama kitu kisicho na thamani? Je, Mungu ana jambo gani ambalo anataraji kulitimiza kwa kuwepo kwako hapa duniani? Je ungetaka uwe mama wa watoto wa jinsi gani? Ukitafakari hayo na kisha ukaomba msaada kwa Mungu hakika Mungu atatimiza ndoto yako. “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.” (2 Timotheo 2:22) Biblia imejaa mifano mingi ya wasichana mashujaa wa jinsi hiyo. “Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.” (Mwanzo 24:15-16) 

Sifa muhimu kuliko zote:

Tabia ndiyo kigezo muhimu katika kuchagua mchumba anayefaa. Tabia hueleza yote kuhusu hali ya mhusika. Tabia hueleza kama mtu anajitambua au bado yupo usingizini. Tabia hueleza kama mtu anamjua Mungu na kumuogopa ama hana dira ya maisha. Tabia hufunua hali ya mtu kama ni mtu anayetegemea neema ya Mungu katika kufikia ukamailifu ama ni mtu asiyekubali makosa. Tabia hufunua hali ya mtu kama anaweza kuchukuliana na hali zote za maisha zinazoletwa na kupanda na kushuka kiuchumi, kiafya, kimahusiano, na kadhalika au ni mwepesi wa kukata tamaa na kutelekeza mambo yanapogeuka kuwa magumu. Tabia ninadhihirisha kama mtu anajua kupenda na gharama za kupenda au anasukumwa na misisimko na hamu ya kukidhi matamanio ya mwili tu. Tabia ndiyo kitu muhimu katika mchakato wa kutafuta mchumba.

Mchumba mwenye mahusiano na Mungu:

Jiulize, Je, mtu ninayetaka kuoana naye ana mahusiano gani na Mungu wake. Anamtambua kama ndiye chanzo cha mafanikio yake na anajua kile Mungu alichowekeza kwake na mpango anaotarajia autimize maishani? Na je, yeye anaishi katika huo mpango wa Mungu na anashirikiana naye ili kuufanikisha? Na je, anajua kuwa Mungu atamuwajibisha kwa kutoishi kulingana na mpango na uwekezaji alioufanya kwake? Ikiwa hana uelewa juu ya jambo hili muhimu huyo hajakidhi kigezo cha uchumba. Anahitaji kuendelea kusubiri ili hali yake ya kiroho ikomae. “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.” (Mhubiri 11:9). Mhubiri anaposema “ukaziendee njia za moyo wako anamaanisha ukaishi kulingana na mpango wa maisha ulio nao. Ni lazima ujihoji ulikuja duniani kwa kusudi gani. Swali hilo litakuelekeza katika kutambua mambo amabyo Mungu amewekeza kwako na ambayo alitaka uyatumie kwa kuokoa na kubariki wengine na kunpa yeye utukufu.