Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

YESU MLEZI WA FAMILIYA NA WATOTO

Kadri tunavyoukaribia ule mwisho hali ya mambo katika familia nyingi itakuwa mbaya kuliko jana na juzi. Yesu anailinganisha hali hiyo na hali iliyokuwepo nyakati za gharika na nyakati zile za Sodoma. (Luka 17:26-30) “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.”

Hata hivyo katika matukio hayo mawili yaliyotajwa ya gharika ya Nuhu na moto wa Sodoma waliookolewa walitokana na juhudi za kumtafuta Mungu katika familia zao. Yesu anaonesha katika nyakati kuelekea mwisho wa wakati kutaibuka vuguvugu katika familia litakalogeuza mtazamo uliozoeleka hadi mioyo ya baba iwaelekee watoto na mioyo ya watoto iwaelekee wazazi tofauti na ilivyo sasa. (Malaki 4:5-6) “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.” Vuguvugu hilo litahusika pamoja na mambo mengine kumuinua Yesu kama mlezi wa watoto, vijana, wanandoa, wajane, wagane, yatima, wagumba, walea pweke, matowashi, na wazee.

Ndoa, au familiya ililengwa pawe kitalu cha kukuzia upendo wa Mungu mahali ambapo mahitaji ya kila mmoja yanasikilizwa na kutimizwa. Familia ilikusudiwa kuwa makimbilio ya wanyonge waliokosa kusikilizwa kwingineko na mahali ambapo kusamehe na kusamehewa ni utaratibu wa hiyari wa kila siku. Familia ilikusudiwa kuwa kituo cha uinjilisti ambapo watu huambukizana uelewa kuhusu wokovu na ambapo hupeana mbinu za kuwafikia wengine kwa injili. (2 Wafalme 5:3) “Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.”

Umuhimu wa ndoa katika jamii

Maisha ya baadaye ya mtoto, kanisa, na jamii hutegemea malezi yanayotolewa kwa Watoto wa jamii husika. Malezi bora ni yale yanayomhusisha Yesu aliye mlezi bora wa familiya na yanayozingatia Kanuni za Kikristo za malezi.  (Zaburi 127:1) “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.” Mchango mkuu wa ndoa au familiya katika jamii ni malezi ya watoto wanaokulia katika hizo familiya. Matatizo ya mmonyoko wa maadili na ukosefu wa uadilifu unaoshuhudiwa katika jamii nyingi na hata kanisani hutokana na kuporomoka kwa mambo hayo katika ndoa na familia. Dini ya kweli hukuzwa nyumbani na kanisani ni mahali pa kwenda kusambazia kwa wengine ile aina ya ukristo mlionao nyumbani.  

Utabiri wa kuharibiwa kwa ndoa na familia

Yesu akitabiri nyakati tunazoishi alitamka jambo la kuhuzunisha kuhusu ndoa na familia. “Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” (Mathayo 24:38-39). Tahadhari tunayopewa ni kuwa kuoa na kuolewa kulikofanywa zamani hizo kukawakosesha watu kuokolewa ndiko kutakakowakosesha watu kuokolewa katika nyakati zetu. Tunapofikiria kuokolewa tufikirie kuokolewa na Watoto wetu. (Kutoka 10:9) “Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia Bwana sikukuu.” Kila aliyepewa nafasi ya kuleta mtoto duniani au aliyejipa jukumu la kulea mtoto ajiandae kutoa hesabu siku ya mwisho. (Yeremia 13:20) “Inua macho yako, Ee Yerusalemu, ukawatazame hawa wanaokuja kutoka kaskazini; liko wapi kundi lako ulilopewa, kundi lile zuri?”

Yesu aahidi kuponya familia

Mungu ana mpango wa kuileta pamoja familia yake iliyotengana kutokana na anguko la dhambi ambapo viumbe wa sayari zote wataishi pamoja tena kwenye makao ya amani. Mpango wa kurejesha familia zote pamoja unaanza kwa kuirejesha familia iliyosambaratika ya wanadamu pamoja. (Malaki 4:5-6) “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.” Huu ni unabii wa matumaini kuwa kwa namna Fulani Mungu anaenda kuingilia kati ugumu uliopo kwenye familia na kuleta maridhiano baina ya wanafamilia waliofarakana.

Idara ya Huduma za Familia

Huduma ya familia ndiye huyo nabii aliyetabiriwa kuleta roho ya maridhiano katika familia. Roho hii inaweka msisitizo wa kudumisha kupendana, kuvumiliana, kusameheana na kutega sikio kwa mahitaji ya kila mmoja katika familia. Idara hii inatoa huduma kwa wote wapatikanao katika familia bila kubagua au kupuuza mahitaji ya yeyote. Inahudumia Watoto, vijana, wanandoa, wajane na wagane, walea pweke, na wazee ili kuinusuru ndoa, kaya, na familia isipotee bali ikaokolewe siku ya mwisho. Jukumu la kitengo hiki ni kuanisha nafasi ya ndoa na familia katika ustawi wa watu, na katika kufanikisha wokovu wao. Elimu hii inayohusu ndoa na familia imekusudiwa kutolewa kila mara makanisani na viongozi wenye dhamana ya huduma za familia, na katika mikutano ya makambi na mikutano yote ya injili. Elimu hii inawalenga walio ndani na walio nje ya kanisa.  

Umuhimu wa watoto katika familia

Watoto huongeza furaha katika familia na kuwa nao ni mbaraka. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kujiweka katika mazingira ya kuwezesha upatikanaji wa watoto katika familia haukabiliwi na ugumu wowote ambao ungeweza kuepukwa. Ni jambo linaloumiza kujulishwa na wataalam wa afya kuwa uwezekano wa kupatikana kwa mtoto ni mdogo au haupo kutokana na uharibifu wa via vya uzazi tulipokuwa tunajaribu kutoa mimba au kama matokeo ya magonjwa ya zinaa tuliyoyapata siku za nyuma. (Zaburi 128:3) “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana. Bwana akubariki toka Sayuni; Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako; Naam, ukawaone wana wa wanao. Amani ikae na Israeli.”

Mungu anataka tuzae watoto

Mungu aliwaumba wanadamu kwa mfumo tofauti na wa Malaika ambao hawaoi wala hawazai watoto. Alikusudia dunia ijazwe na watu wanaotokana na mtu mmoja. (Matendo 17:26) “Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu.” Alipanga wanadamu wazae wanadamu wenzao kupitia ndoa ya mwanaume na mwanamke. (Mwanzo 1:28) "Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”

Dunia iliumbiwa watu

Dunia haikuumbwa ili isikaliwe na watu. Dunia iliumbwa ili ikaliwe na watu kwa idadi kubwa ya kutosha kwa sababu kwenye watu wengi ndiko kwenye maendeleo. (Isaya 45:18) “Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine.” Hii ndiyo maana wanadamu walipopinga mpango wa kutawanyika ili kuijaza nchi na kinyume chake kuanzisha uasi kwa kujenga mnara wa Babeli, aliwachafulia lugha na kuwatawanya ili litimie kusudi lake la kuijaza nchi. (Mwanzo 11:8) “Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.”

Mambo ya kuzingatia unapoleta watoto duniani

Mungu anataka watoto wazaliwe kwenye familia ya baba na mama wanaoishi pamoja kisheria na kwa ridhaa ya wazazi na taasisi ya kiroho inayotambulika. Watoto hao pia waweze kupatiwa huduma za kiroho, kimwili, na kijamii pamoja na maadili mema ya kuwafanya raia bora hapa dunia na raia wa mbinguni. Watoto wanaozaliwa nje ya utaratibu huo wana uwezekano wa kuwa laana badala ya kuwa mbaraka. (1 Timotheo 5:8) “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.”

Idadi ya watoto itokane na uwezo wa kuwahudumia

Ili watoto wayapate mahitaji hayo kwa uwiano unaofaa panahitajika mpango maalum unaoanisha waje lini, wapishane umri kwa umbali gani, na waje kwa idadi gani. Kazi ya kuijaza nchi itakamilishwa kwa kila familia kuchangia kiasi fulani cha idadi ya Watoto kulingana na uwezo wa familia husika. Familia moja peke yake haiwezi kuifanya kazi hiyo. Ikiwa uwezo wako wa kuwatunza watoto unaishia mtoto mmoja ishia kwa huyo mmoja. Kanuni ya msingi ni kuhakikisha hushindwi kuwatunza watoto wako. (Mithali 31:21) “Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.” Usilete Watoto duniani kwa matarajio ya kuhudumiwa na wengine.

Usihusike kuleta watoto watakaokuwa laana

Si kila anayezaliwa duniani amekuja akitimiza agizo la Mungu la kuzaa na kuongezeka. Mungu katika nyakati mbalimbali amekuwa akiwapunguza wale ambao wameonekana kuwa laana kuliko kuwa mbaraka kwa dunia. (Mwanzo 6:5) “Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.” Usizae watoto kwa ajali.

JADILI: Kipi bora kutoa mimba, kutumia vidonge vya kuzuia mimba, au kulea mtoto aliyekuja bila kutarajia?

Umri sahihi wa kuleta mtoto katika familia

Inashauriwa kuwa wanandoa wapya wasizae watoto mapema isipokuwa kama walichelewa kuoana. Kukawia kupata Watoto kunawapa muda wa kutosha kuzoeana na kufurahia maisha mapya ya ndoa. Hata hivyo wengine huona ni vyema kupata idadi ya watoto wanaowahitaji mapema ili wawe na muda wa kuwalea na kuwahudumia wakiwa na nguvu. Ili kuwasaidia kumudu majukumu ya malezi na kumsaidia mama kurudisha afya yake inashauriwa watoto wapishane umri wa kuanzia miaka mitatu. Kwa kadri inavyowezekana shughuli ya kuzaa watoto ifanyike mapema katika hatua za awali za ndoa ili kuepuka kuwa na watoto walio shule wakati mnapofikia umri wa kustaafu. Kuzaa katika umri mkubwa kunachangia matatizo kwa mtoto anayezaliwa na kuzaa katika umri mdogo kunachangia matatizo kwa mzazi na mtoto.

Msijichoshe ili kupata watoto wa jinsia fulani

Msijichoshe ili kulazimisha kupata Watoto wa jinsia fulani. Kama baada ya kujaribu mara kadhaa mtoto mumtakaye hajapatikana amueni kuridhika na hao mlionao.  Mungu anaweza kuwafanyia makubwa kupitia hao Watoto wa jinsia moja. Naomi alizaa Watoto wote wa kiume lakini akafaidika kupitia wakamwana wake. mke wa mwanao ni binti yako na mume wa binti yako nim toto wako wa kiume. Wapo waliotunzwa vizuri na watoto wao wa kike kuliko na watoto wao wa kiume na wapo waliotunzwa vizuri na watoto wao wa kiume kuliko na wa kike. Kinachohitajika ni kuwapatia mahitaji yao na kuwarithisha maadili mema. Hata hivyo leo wataalamu wanajua namna ya kuwawezesha wanandoa kupata mtoto wa jinsia wanayoitaka, waoneni wataalamu hao wawasaidie. 

Changamoto ya kupata watoto

Kusudi mojawapo la Mungu la kuanzisha ndoa ni kuunda taasisi ambayo ingehakikisha wanadamu wanaongezeka kwa njia ya mwanamke kushika ujauzito na kuzaa watoto. Mpango huo haujabadilika. Kwa bahati mbaya kutokana na dhambi, ndoa zingine zimekosa kupata watoto na hiyo imetokana na mke kushindwa kushika ujauzito ama kuharibika kwa mimba au watoto kufariki wakiwa wachanga. Matatizo ya mke kutoshika mimba au kuchelewa kushika mimba, hutokana na sababu za kibaolojia au kiafya na sababu za kisaikolojia zinazowahusu wanandoa wenyewe, ndugu zao, zinahusu mazingira, na zingine zikiwa hazijulikani sababu zake kwa usahihi.

Msaada wa kitaalamu

Wanandoa wenye changamoto ya kutopata Watoto wanahimizwa kuendelea kumtegemea Mungu, huku wakishauriana na wataalam wa afya na saikolojia. Matatizo yanayosababisha kutoshika ujauzito si lazima yatokane na mwanamke. Wakati mwingi matatizo hayo yameonekana kusababishwa na mume kutoa mbegu zilizo hafifu zisizoweza kushika mimba. Tatizo hilo linaweza kurekebishwa kirahisi kwa kubadili mtindo wa maisha kwa kadri utakavyoelekezwa na wataalamu. Wakati mwingine mimba kuharibika mapema yaweza kutokana aina ya damu au makundi ya damu ya wahusika kutoptana. Mara nyingine sababu za kutopata mtoto zaweza kutokana na utoaji mimba au magonjwa ya zinaa ambayo hayakupata tiba kamili.

Watoto hawahalalishi ndoa

Hata hivyo ndoa haihalalishwi na kuwepo kwa mtoto. Kukosekana kwa mtoto hakuifanyi ndoa kuwa haramu, hakuhalalishi kuachana, wala si kipimo cha kuwaweka wanandoa hao kwenye kundi la wadhambi, waliolaaniwa au wanaotiliwa shaka juu ya mwenendo wao. Ndoa isiyo na watoto ni ndoa halali kabisa kama ile yenye watoto. Mtu asijaribiwe kumwacha mkewe au mumewe au kuongeza mke wa pili kwa kuwa tu mke au mume aliyenaye hajampatia mtoto. (Mwanzo 18:6-11) “Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake.”

Mbaraka wa watoto wanaochelewa kuzaliwa kwenye ndoa

Mara nyingi watoto wanaozaliwa kwa kuchelewa baada ya wazazi wao kudhaniwa hawana uwezo wa kupata watoto, huwa mbaraka mkubwa kwa familia na jamii husika. (Waamuzi 13:2-5) “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.” Usikate tamaa huenda Mungu amepanga kukupatia mtoto atakayekuwa mbaraka.

Upendo waweza kuwa tiba

Mwanadamu anapokabiliwa na zahama uwezo wake wa kustahimili hushuka na hivyo kuhitaji uwezo wa wale wasio kwenye zahama. Msaada huo usipopatikana kwa wakati mtu aweza kufanya maamuzi yasiyofaa. Maamuzi hayo yasiyofaa huweza kutokana na kukerwa na masimango ya watu na kukosa uvumilivu kutokana na muda mrefu wa kusubiria. Hana na Sara walipata watoto baada ya vipindi virefu vya kungoja na kudhihakiwa. Sara alidhihakiwa na Hajiri mjakazi wake na Hana alidhihakiwa na mke mwenza. (Mwanzo 16:1-4) “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.”

Mke asiye na mtoto apewe upendeleo

Mke ambaye ni mwepesi kukata tamaa katika mazingira haya hupata utulivu wa mawazo wenye mchango mkubwa katika kuhuisha vichocheo vya ujauzito. (1 Samweli 1:4-6) “Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo.” (1 Samweli 1:8) “Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?”

Mungu na ratiba ya kupata mtoto

Sara na Hana katika wakati wa ratiba ya Mungu walipata watoto jambo linalothibitisha kuwa Mungu anatuwazia mema. Mungu hapendi kutesa watu ila huruhusu kila jambo litimie kulingana na ratiba yake. (Mwanzo 21:2) “Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.” (1 Samweli 1:20) “Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.”

Kuasili mtoto

Kukosa Watoto hakuwezi kuwa sababu ya kutokuwa na watoto unaowamiliki kama wako. Dunia hii imejaa watoto waliokosa wa kuwalea baada ya wazazi wao kufariki. Lingekuwa jambo sahihi zaidi kuchukua wa aina hiyo na kuwaasili kama Ibrahimu alivyofanya. Watoto wanaozaliwa nje ya ndoa mara nyingi wamekuwa chanzo cha migogoro katika familia, jamii na taifa. (Mwanzo 15:2) “Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.” Wale wenye Watoto nje ya ndoa huenda lingekuwa jambo bora kukubaliana kuwaleta hao watoto nyumbani ili warithi mali ambazo wana unasaba nayo.

JADILI: Watoto nje ya ndoa watambulishwe au wabaki huko huko bila kutambulishwa?

Vituo vya kulelea watoto yatima

Wengine wamepata baraka kubwa kwa kulea watoto yatima majumbani mwao au kwenye vituo vya watoto yatima au watoto waishio kwenye mazingira magumu. Kulea watoto wanaokutambua na kukupa heshima kama baba na mama uliyewaleta duniani kumeleta faraja kwa wengi. Haitoshi kutembelea vituo vya kulelea waishio kwenye mazingira magumu. Hebu tufikirie kufungua vituo vya kusaidia Watoto hao. (Mwanzo 12:5) “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.” (Kumb. 24:19) “Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako.”

JADILI: Kwa nini uanzishaji wa vituo vya kulelea watoto yatima imekuwa mtihani kwa Waadventista? Kipi bora kukaa na mtoto wa ndugu yako au na mtoto baki?

Malezi ni ya baba na mama

Mungu ameweka jukumu la kuzaa watoto kwa wanandoa wa jinsia tofauti. Kulelewa na walezi kunapunguza ule ukaribu waupatao watoto kutoka kwa mama zao waliowazaa. Wazazi na hasa mama ahakikishe ana wakati wa kutosha na mwanae mchanga. Ushoga unalenga kuzalisha watoto waliokosa upendo wa wazazi watakaoifanya dunia isiweze kukalika. (Zaburi 1:8) “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako.” Utaratibu unaopigiwa debe sasa wa kuwa na familia ya walezi wa jinsia moja hautoi fursa kwa mtoto kupokea malezi kutoka kwa mama na baba.  

Malezi huanza lini?

Malezi ya watoto huanza wakati mtoto akiwa bado tumboni. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mtoto hujifunza mwenyewe anapofikisha miezi kadhaa kabla ya kuzaliwa. Upo wakati mtoto aliye tumboni husikia kinachoendelea nje ya tumbo na hupokea mawasiliano kupitia mazungumzo, nyimbo, maombi na kadhalika. (Luka 1:44) “Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.” Huu ni udhihirisho wa kutosha kuwa kitoto kichanga kina uwezo wa kufanya mawasiliano na walio nje wakati kikiwa tumboni mwa mamaye. Mtoto aliye tumboni anahitaji kuzungukwa na mandhari yenye amani, tulivu, ikiwa na mazungumzo yenye amani, nyimbo za kiroho na maombi mengi. Ikiwa patakuwa na patashika ya magomvi wakati wa ujauzito kuna uwezekano wa magomvi hayo kumwathiri mtoto.

Kujiepsha na vyakula na vinywaji

Kitu kingine ambacho ni muhimu kwa makuzi ya mtoto akiwa tumboni ni chakula na vinywaji anavyotumia mama mjamzito. Watoto wanaozaliwa wakiwa na majukumu muhimu ya kubeba katika jamii lazima wakuzwe katika mazingira ya kuwaepusha na mazoea ya kula na kunywa vinayopingana na kanuni za afya. (Waamuzi 13:2-4) “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; Ndiyo maana mkewe Manoa aliagizwa.” Pombe, uvutaji sigara, na ulaji wa wanyama najisi unaofanywa na mama mjamzito, hudhuru afya ya mtoto tangu akiwa tumboni.

Mkinge mwanao

Kanisa linawahimiza wakina mama wajawazito na wenye vitoto vichanga kujiunga na madarasa ya watoto wakati wa vipindi vya shule ya Sabato ili kuwasaidia watoto wao waliojifungua na walio matumboni kupata mafunzo yao yanayowastahili. Mtoto azoezwe kuomba kabla ya kunyonya na kabla ya kulala hata wakati akiwa mchanga kabisa. Mtoto aendelee kuimbiwa nyimbo za kiroho na kumweka mbali na miziki yenye midundo mizito ya kidunia. Mama aliyejifungua asikawie bila sababu kumleta mtoto kanisani ili apate mafunzo yanayomhusu.

Kuwekewa mikono watoto

Kila inapowezekana mtoto afanyiwe huduma ya kuwekewa mikono mapema sana bila kusubiri hadi amekuwa mkubwa wa kutembea mwenyewe. Huduma ya kuwekewa mikono inafanywa kwa watoto wachanga ili kuwaimarishia ulinzi wao wa kiroho na kimwili. Siku ya kuwekewa mikono mtoto aandaliwe sadaka ya shukurani, picha za ukumbusho, na sherehe fupi. Picha za matukio mbalimbali ya mtoto katika hatua za ukuaji wake zihifadhiwe vizuri kwa ajili ya kumbukumbu yake atakapokuwa mtu mzima. Sambamba na kuwa na cheti cha ubarikio, ifanyike jitihada ya kuhakikisha mtoto anapata cheti chake cha kuzaliwa mapema. Wazazi wanapaswa kuzingatia maagizo wanayopewa wakati wa kuwekewa mikono watoto. Watoto wapewe kipaumbele katika kuwapatia lesson zao kila robo na wazoezwe pia kuendesha mijadala ya lesson nyumbani.

Watoto wapangiwe ratiba ya kazi

Watoto watahadharishwe kuwa makini na watu wanaowabembeleza kwa zawadi na kuwashika shika kwenye sehemu za miili yao hasa sehemu za siri. Usiwaruhusu watoto kulala kitanda kimoja na wageni wanaotembelea hapo nyumbani kwako hata kama ni ndugu wa karibu, maana wengine kwa kufanya hivyo walisababisha watoto wao kulawitiwa. Watoto wasipewe uhuru unaovuka mipaka. Wapangiwe ratiba ya mambo ya kufanya hata wanapokuwa likizo. Mama asifanye kazi zote za nyumbani bila kuwashirikisha watoto. Hata kama kuna msichana wa kazi asiwe wa kufanya kazi zote na watoto wakiwa hawajui hata kutandika vitanda vyao wenyewe.

Watoto wadogo waruhusiwe kucheza

Watoto wanahitaji kucheza michezo yao ya kitoto. Usiwazuie. Wakina baba wengi huwa si wavumilivu kwa michezo ya watoto ambayo huandamana na kuwepo kwa zana nyingi za mifano ya magari, wanasesere, kuchorachora ardhini na hata kwenye ukuta, kuchimba chimba vishimo na kadhalika, ambavyo kwa kiasi fulani huharibu mazingira. (Waefeso 6:4) “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.” (Wakolosai 3:21) “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” Ukali wa wazazi kama hao ndiyo uliowakimbiza baadhi ya watoto na sasa wapo mitaani wakiitwa watoto wa mitaani. Watoto wanahitaji kuoneshwa upendo.

Tambua mwelekeo wa mtoto

Tafsiri nyingine ya kumlea mtoto katika njia impasayo ni kutambua Mungu amewekeza kitu gani kwa huyo mtoto na kumwekea mazingira ya kukuza matamanio yake hayo tangu akiwa mtoto. Aliyezaliwa akipenda kusoma aelekezwe kwenye masomo ya darasani na aliyezaliwa akipenda ufundi aelekezwe kwenye masomo ya ufundi yanayohitaji vitendo zaidi kuliko nadharia. Huu ndiyo wakati wa kutambua mapungufu na vipawa alivyonavyo mtoto kimwili, kiakili, kihisia, na kijamii na kuchukua hatua za kurekebisha. Watoto wenye mwelekeo wa kutokuwa na nguvu za kiume huweza kutambulika katika umri huu kwa kupima hali ya uume wake asubuhi anapoamka au wakati anapokojoa. Mtoto aliye mzima huamka na uume uliosimama na anapokojoa mkojo huangukia mbali.

Mwelekeo huonekana mapema

Watoto wa kwanza wa Adamu na Eva na wa Isaka na Rebeka walitofautiana kwa mambo waliyokuwa wakiyapendelea. (Mwanzo 4:1-2) “Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.” (Mwanzo 25:27) “Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani.” Kupitia tabia hizi zinazojidhihirisha tangu mapema mzazi aweza kuweka msingi wa kuendeleza kile kilichoonekana kwa mtoto.

Usibeze maono ya watoto

Kwa bahati mbaya wazazi hubeza maono na maoni ya watoto wao juu ya kile wanachopendelea au vile ambavyo wangependa kuwa siku za usoni na kushinikiza wafuate kile wakipendacho wazazi. (Mwanzo 37:7-10) “Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?”

Msitofautiane katika kukuza maono ya watoto

Wakati fulani maoni ya wazazi juu ya namna bora ya kumlea mtoto na kumwandaa kushika majukumu yake ya siku za usoni huweza kutofautiana. (Mwanzo 27:6-10) “Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Enenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake.”

Licha ya kuwa Esau alikuwa mtoto wa kwanza wa kiume mwenye haki ya kuendeleza ukoo, mama yake alimuona anapungukiwa sifa ya mambo ya kiroho yaliyo muhimu kwa kazi hiyo tofauti na Yakobo. Baba aliangalia manufaa ya sasa ya mwanae wakati mama aliangalia manufaa ya baadaye ya mwanae na ya taifa zima la Israeli. Kauli yake ya siku za nyuma ilionesha asivyowekea umuhimu nafasi hiyo. (Mwanzo 25:32) “Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi?” Maisha ya baadaye ya Esau ni udhihirisho mwingine wa namna Esau asingeweza kuitendea haki nafasi hiyo ya kiroho. (Mwanzo 28:8-9) “Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake. Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao.”

Aina za malezi ya Watoto

Tabia ya mtoto hujengwa kutegemeana na yale anayojifunza kwa kuona na kwa kusikia kutoka kwa watu wanaomzunguka. Tabia ya mtoto pia hutokana na urithi kutoka kwenye vinasaba vya wazazi wake. Kuna aina mbili kuu za malezi ya watoto; malezi ya ukali na malezi ya kudekeza. Malezi ya ukali au ya kikatili ni yale yenye sheria nyingi na kali bila kuzingatia uwezo wa mtoto wa kuzitekeleza na usiotoa nafasi ya kuelimishana na majadiliano. Malezi haya ya ukali huandamana na adhabu kali zinazozidi uzito wa kosa na uwezo wa kustahimili wa anayeadhibiwa bali hutegemea kiasi cha hasira alichonacho mtoa adhabu. Huu unaitwa pia unyanyasaji wa watoto.

Malezi ya vitisho na ukatili

Malezi ya vitisho na ukatili havimpi mtoto uwezo wa kukuza kujiamini bali humfanya awe mwoga na asiye na hulka ya kuthubutu mambo maishani mwake. (Mwanzo 4:11-15) “Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.”

Mtoto aelekezwe kwa upendo na kwa maumivu

Mtoto aelekezwe kwa upendo na pale unapobidi kwa kutumia maumivu. Kazi hii ya kumwelekeza mtoto apaswacho kufanya na asichopaswa kufanywa katika umri wa awali wa mtoto kwa kawaida hufanywa na mama. (Mithali 29:15) “Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.” Tabia njema ya Timotheo ilichangiwa na malezi bora ya kiroho ya mama na bibi yake. (2 Timotheo 1:5) “Nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.”

Adhabu husaidia kujifunza

Adhabu humsaidia mtoto kujifunza. Katika malezi ya awali mtoto akiwa mdogo anahitaji kuadhibiwa maana ndiyo njia inayomsaidia kukumbuka kilicho kibaya na kizuri. Katika hatua hii adhabu inakusudia kubadili tabia isiyohitajika. Adhabu katika umri huu huchukua sura ya maumivu yanayotolewa kwake ili kumkumbusha kila anapotaka kurudia kosa juu ya maumivu atakayoyapata. Adhabu hapa hutumika kama kiongozi anayesimama karibu naye kumwepusha na matokeo yenye maumivu. Lakini pale adhabu inapomfanya mtoto kuwa sugu inapoteza lengo lake. (Mithali 23:13) “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu.”

Adhabu izingatie staha

Adhabu itolewe kwa staha na pale inapokuwa ni lazima kwa kipimo ambacho mmekubaliana huku ikibeba ujumbe wa upendo na si chuki au kukomoana. Adhabu isitolewe wakati mtoa adhabu akiwa na hasira. Kanuni ya utoaji wa adhabu inataka anayeadhibiwa asitiriwe asionekane akipokea adhabu na wenzake, alijue kosa alilotenda, na makubaliano yawe yamefanyika mapema kuwa kosa fulani litastahili adhabu fulani litakapotendwa, na adhabu yake lazima iwe na ukomo. (Kumb. 11:26-28) “Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.”

Badili mbinu ya kuadabisha mtoto

Adhabu inafaa kutumika katika umri wa utoto zaidi kuliko katika umri wa ujana ambapo mtu anajielewa. Katika hatua hii mazungumzo yenye ushauri na wosia hufaa zaidi kuliko utoaji wa adhabu. (Mithali 1:10) “Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.” Kila inapowezekana (na hasa mwenye kukosa anapoonyesha kutambua kosa lake na kulijutia), msamaha unastahili kutolewa. Wema wa wazazi ni chachu nyingine ya kuwafanya watoto wajutie makosa yao. (Luka 15:17-18) “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.”

Nyumbani pawe kituo cha makimbilio

Watoto wengi wanaoitwa wa mitaani ni wale waliokimbia ukatili waliokuwa wakitendewa nyumbani ama na wazazi wao au ndugu zao wa karibu. Tupafanye nyumbani kuwa kituo cha makimbilio ambapo hoja ya kila mmoja inapata nafasi ya kusikilizwa. Wekeni vikao vya mashauriano ambapo kila mwanafamilia ana fursa ya kutoa maoni yake bila hofu wala vitisho. (Zaburi 133:1) “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” (Mithali 13:10) “Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.”

Kudekeza Watoto

Namna nyingine ya malezi mabaya ni ile ya kudekeza watoto. Hii hufanywa kwa kuwaacha watoto wafanye kile wanachokifurahia bila kuwawekea mipaka wala kuwaadhibu wanapokosea. Udekezaji huonekana mara nyingi kwa watoto wenye changamoto za kiafya, waliozaliwa kwenye mazingira yaliyokuwa yanahatarisha uhai wao au wa mama zao, waliopewa majina ya watu wanaoheshimika katika ukoo, wenye kufanana na mzazi mmojawapo kwa mwonekano au tabia, mwenye maendeleo mazuri shuleni, anayesoma kwenye shule maalum, au aliyepatikana kwenye umri wa uzee. (Waebrania 12:6) “Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.”

Kupendelea Watoto

Watoto wa aina hii huondolewa kwenye majukumu yanayowahusu watoto wenzao, na hata wanapokosea hawaadhibiwi au hupewa adhabu nyepesi. Pakiwapo zawadi watoto hawa hupata upendeleo wa wazi unaowafanya wengine kuumia wakati wale waliopendelewa huringia wenzao kwa kule kutoadhibiwa kwao. 1 Timotheo 5:21 Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo. Unapompenda mtoto mmoja kuliko wengine unamweka huyo mtoto kwenye mazingira wa kuchukiwa na kudhurika. (Mwanzo 37:3) “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu.”

Watoto wa uzeeni wasidekezwe

Watoto wanaopatikana uzeeni au wajukuu wanaolelewa na babu na bibi zao wasidekezwe. Wajengewe msingi wa Maisha ya kujitegemea na kujisimamia katika Maisha ya baadaye. (Mwanzo 37:3-4) “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.” Ni heri ikiwa wazazi wameshindwa kulea mtoto waombe msaada wa wanajamii kuliko kumuache akue na tabia yake mbaya inayoweza kuja kuiathiri jamii hiyo.  (Kumbukumbu la Torati 21:18) “Mtu akiwa na mwana mkaidi, mshupavu, asiyetii sauti ya baba yake, wala sauti ya mama yake, nao wajapomwadhibu hawasikizi, ndipo babaye na mamaye na wamkamate, na kumpeleka kwa wazee wa mji wake, katika lango la mahali pake; wawaambie wazee wa mji wake, Huyu mwana wetu ni mkaidi, mshupavu, hasikizi sauti yetu; ni mwasherati, tena ni mlevi. Waume wote wa mji wake na wamtupie mawe, afe; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako; na Israeli wote watasikia na kuogopa.”

Watoto wa viongozi waadabishwe

Watoto wa viongozi ni kioo cha jamii. Makosa yao yana kawaida ya kuiathiri jamii nzima. Marudi kwa Watoto hawa yanapaswa kuwa ya wazi na yenye uzto mkubwa kulingana na kosa lililotendwa. Eli kuhani mkuu alishindwa kutoa adhabu kali kwa wanaer kwa sababu mtindo wa malezi aliokuwa anautumia ni ule wa upole na kudekeza. (1 Samweli 2:22-24) “Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa Bwana.” Kosa la Eli ni kulishughulikia kosa la Watoto wake kwa uzito mwepesi. Eli angeweza kuwasimamisha kutofanya kazi za hekaluni kwa muda au moja kwa moja. Eli aliwadekeza wanawe. Watoto wa viongozi au watu wenye ushawishi katika jamii wanapopotosha watu waonywe vikali ili wengine wasiige mfano wao, 1 Timotheo 5:20 Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.

Zawadi zitolewe kwa tahadhari

Kutoa zawadi kwa mtoto anayefanya vizuri kuliko wengine kuna faida ya kumuongezea hamasa ya kufanya vizuri zaidi katika siku za usoni au kudumisha mafanikio yake. Lakini utoaji huo wa zawadi ufanyike kwa tahadhari kubwa ili nia njema ya kuongeza hamasa isizae chuki kwa wengine wanaoburuza mkia. Mtoto asiyefanya vizuri kwa tabia na masomo huhisi maumivu kwa kushindwa kufikiwa matarajio ya wazazi wake. Hivyo kutotambua juhudi zake za kufikiwa mafanikio waliyofikia wenzake kutamfanya apate maumivu mara mbili. (Ezekieli 46:16) “Bwana MUNGU asema hivi; Mkuu akimpa mwanawe awaye yote zawadi, ni urithi wake, itakuwa mali ya wanawe; ni milki yao kwa kurithiwa.”

Usiwagombanishe wanao kwa zawadi

Kwa kuzingatia kuwa aliyefanya vizuri na aliyefanya vibaya wote ni wanao unapaswa kutomwacha mikono mitupu aliyeshindwa kufikia viwango. Mwandalie naye zawadi kwa mambo yale anayoyamudu kuliko wenzie au usitoe zawadi kabisa kwa wote. Kwa kawaida mtoto asiyefanya vizuri ndiye anayehitaji upendo mwingi zaidi kuliko wale wenye nafuu ili kumsaidia kubadilika. (1 Wakorintho 12:23) “Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.”

Fafanua sababu ya kutoa zawadi

Utoaji zawadi kwa ambaye hajafanya jema lolote waweza kuibua maswali kwa aliyestahili zawadi akiona kuwa haikuwa halali huyu mwingine kupewa zawadi. Hali kama hiyo itakapoibuka mzazi awe tayari kulitolea ufafanuzi. (Luka 15:28-32) “Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”

Ondoa uhasama kwa watoto ukiwa hai

Shida ya mfumo huu wa malezi ni kuleta uhasama unaoweza kupelekea watoto kupigana, kuuana na kusambaratisha familia. (Mwanzo 37:18-20) “Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”

Uhasama wa watoto wa Ibrahimu na Isaka

Wazazi wana wajibu wa kusuluhisha migogoro waliyoisababisha kwa watoto wao mapema kabla haijaota mizizi au kabla hawajaondoka duniani na kuacha mpasuko mkubwa katika familia. Watoto wa Ibrahimu na Isaka walikuwa na uhasama mkubwa. (Wagalatia 4:28-29) “Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.” (Mwanzo 27:41) “Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.”  

Waliohasimiana wapatanishwe

Inatia moyo kwamba Isaka na Ishmaili (Watoto wa Ibrahimu) na Esau na Yakobo (Watoto wa Isaka) ambao hapo awali hawakuelewana kiasi cha kutoleana maneno mabaya walifanikiwa kuondoa tofauti zao na kuelewana hata kufanikiwa kushiriki mazishi ya baba yao. (Mwanzo 25:8-9) “Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake. Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre.” (Mwanzo 35:29) “Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.”

Urithi bora kwa watoto

Urithi wa maana ambao wazazi waweza kuwaachia watoto wao ni tabia itakayowawezesha kukubalika katika jamii ya watu wastaarabu na kuwawezesha kuishi na yeyote hata asiye ndugu yake. Urithi mwingine muhimu ni ujuzi au elimu vinavyoweza kumpa ajira au kujiajiri au kupanua uwezo wake wa kufikiri na wa kufanya maamuzi. Hivi vina uhakika wa kudumu kuliko mali ambayo huisha na kuleta kutoelewana katika kuimiliki. Mtoto aliyezoezwa kupenda kazi na kutobagua kazi yoyote mradi inaweza kumwingizia kipato ana uhakika wa ajira na mafanikio katika Maisha. (Mithali 14:23) “Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.” Mtoto mwenye sifa njema atapendwa na kila mtu n ani rahisi kupendwa na watu na kusaidiwa atakapokuwa na changamoto. (Mhubiri 7:1) “Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.”

Mzoeze mtoto kuwa mcha Mungu na mchapakazi  

Yakobo alikuwa mchapakazi na mwaminifu kwa Mungu wakati alipotoka nyumbani kwake kwenda kuishi na mjomba wake. Licha ya kunyanyaswa na kudhulumiwa na mjomba yake mara nyingi, alifanikiwa sana kiuchumi kwa sababu ya bidii ya kazi na uaminifu wake kwa Mungu. (Mwanzo 30:27-30) “Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili yako. Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa. Akamwambia, Umejua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi wanyama wako walivyokuwa kwangu. Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi, Bwana akakubariki kila nilikokwenda. Basi sasa, nitaangalia lini mambo ya nyumba yangu mwenyewe?” Mtoto wako akiwa mchapakazi hatakosa ajira na hawezi kulala njaa.

Wazoeze Watoto kujitegemea na kupenda wa kwao

Wakati wa likizo wazoeze watoto wako kujifanyia wenyewe kazi za nyumbani za kufua, kuosha vyombo, bustani, kutandika kitanda na hata kupika. Imeonekana kuwa watoto wanaoishi majumbani mwetu kama wafanyakazi au ndugu wa familia hutoka hapo nyumbani wakiwa wamejua kujitegemea kuliko watoto wetu wanaozuiwa kufanya kazi za nyumbani. Watoto waliozoezwa kujitegemea kwa kazi za nyumbani, shambani, na mifugo hawataisahau kazi hiyo hata baada ya kuelimika au kufanikiwa kiuchumi. (Waebrania 11:24-25) “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo.” (Kutoka 2:15-17) “Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.”

Elimu isibague kazi za mikono

Kamwe elimu inayotolewa isingewanyima watoto wetu fursa ya kujifunza kazi za mikono, kujifunza mazingira watakayokwenda kuishi na namna ya kuyafanya kuwa bora zaidi. Elimu ya kweli ni ile inayozingatia kumjua Mungu, na kukuza uwezo wao wa kiakili na kimwili na inayowaandaa kwenda kuitumikia jamii waliyotoka. Musa alipata elimu ya namna hiyo kutoka kwa mama yake na kutoka vyuo vya Misri. Kanisa lina wajibu wa kuanzisha shule za kutosha zenye mwelekeo huo ili kubadili mtazamo hafifu juu ya elimu usiompa mtu fursa za kujiajiri na uwezo wa kufikiri namna ya kutatua matatizo ya watu wa kwao. Musa alipohitimu elimu yote ya Misri alienda kufanya kazi duni ya kuchunga kondoo wa mkwewe bila malipo. Wahitimu wakubali kufanya kazi hata kama si ile waliyoisemea kwa kuwa ndiyo inayopaikana wakati huo, (Kutoka 3:1) “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.”

Shule zenye maadili ya Waadventista

Ikiwa mzazi atakuwa mwaminifu kwa Mungu na kuwarithisha wanawe mambo yale ajifunzayo kwa Mungu kwa bidii, watoto hao hata kama hapo katikati wataiacha imani, wakifikia utu uzima kuna uwezekano wa kuirejea imani yao ya zamani.  Hakuna urithi wa maana anaowekeza mzazi kwa watoto kama elimu ya kumjua Mungu. Mzazi usikubali mwanao asome shule inayomnyima mwanao fursa ya kutunza Sabato kama ilivyoagizwa na Maandiko Matakatifu. Mtoto huyu hata kama atafaulu vizuri masomo yake, atakuwa amepungukiwa uadilifu. Wazazi wenye kuwathamini watoto wao watajitahidi kuwasisitiza kumheshimu Mungu na kusoma shule zenye maadili ya Waadventista. 

Watoto wajiunge na vyama vinavyowalea kiroho

Kanisa la Waadventista wa Sabato, limeweka utaratibu mzuri unaowahusu watoto. Idara ya shule ya Sabato ya Watoto, Idara ya Watoto, vyama vya Wavumbuzi na Watafutanjia na vyote hivyo ni vitengo ndani ya kanisa vinavyomuandaa vyema mtoto. Usiache kumhimiza mwanao kushiriki katika vitengo hivyo na kujitahidi kumtimizia mahitaji yake kama yanavyoelekezwa na vitengo hivyo. Watoto wanaokosa miongozo, makadi na sare za vyama vyao huumia na kukatishwa tamaa. Usiache mwanao aonekane kituko katikati ya wenzake.