Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

SIMULIZI ZA WATANGULIZI

SIMULIZI ZA WATANGULIZI WETU

Simulizi hii muhimu imeandaliwa na Mchungaji Jocktan Kuyenga, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Konferensi ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, ambaye sasa ni marehemu na inahusu historia ya Kanisa la Waadventista wa Sabato katika sehemu za kati, mashariki, kusini na magharibi mwa Tanzania.

MWANZO WA UINJILISTI KATIKA TGF:

Kupanuka kwa kazi ya injili katika Tanzania General Field (TGF) kulikuwa kwa kasi katika kipindi cha Mchungaji Dobayas (Dobias). Mchungaji Dobias aliyeitwa mwinjilisti wa Union ya Tanzania, kwanza alipelekwa Kibidula kutumika kama Meneja wa Shamba, (Farm Manager.) Kazi ya Farm Manager hakuipenda sana, ndipo akaanza mpango wa kutuma wainjilisti katika maeneo mapya kutoka sehemu kadhaa za Tanganyika. Programu ya Mchungaji Dobias ilizalisha wainjilisti waliotumika kama wamishenari wazalendo, ambao walitumwa sehemu mbalimbali za eneo la TGF, wakiwemo wafuatao:-
1. Lameck Mulungu-Njombe
2. Alhpaxad Katogi-Malinyi
3. Rayphord Bulenga-Mpwapwa

Kutokea Dar Es Salaam ambako kazi ilianza kiutume katika maeneo ya kusini Mashariki na kati mwa TFG ya zamani, yaonekana kulikuwepo na mtaa mmoja mkubwa uliochukua mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, na Singida kisha kuelekea mikoa ya kusini ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Lindi na Mtwara. Eneo hili lilikuwa kubwa, lenye changamoto kuhudumiwa na mchungaji mmoja, pamoja na kwamba alikuwa na msaada wa wainjilisti wa vitabu au wainjilisti wa kujitolea.

Katika kukabiliana na changamoto ya ukubwa wa eneo uliaanzishwa mtaa wa kusini chini ya uongozi wa Mchungaji Joshua Kamenya Kajula, (sasa marehemu) wenye makao makuu Mbeya mwaka 1972. Mchungaji Yohana Lusingu akaingia katika mtaa huu mpya na Mchungaji Kajula akaendelea hadi Songea. Kazi iliendelea vizuri kusini, huku nyumba kadhaa zikinunuliwa na Mchungaji Dobias katika miji mbalimbali kama vile Masasi, Lindi, Kilosa, Tukuyu, Kyela, na kwingineko zikatumika kama makazi na mahali pa ibada.

Mkakati huu ulikuwa na udhaifu wake. Kiongozi wa mkakati huu alishikilia madaraka mkononi mwake kwa maana kwamba aliweza kumwachisha kazi mtenda kazi kwa wakati wowote hata bila kungojea uamuzi wa baraza. Matokeo yake wahubiri hawa wa kujitolea walirudishwa nyumbani. Hata hivyo injili iliendelea kwa nguvu kwa misingi ya imani zaidi.

Mchungaji Elingoth alishikilia uongozi wa T.G.F baada ya Mchungaji Henning aliyeitwa kwenda Makao Makuu ya Kanisa Ulimwenguni (GC) kama Mkurugenzi wa Uchapishaji. Baada ya hapo kazi ilkuwa na kupanuka kutoka mashariki, sehemu ya katika ya Tanganyika, kusini hadi magharibi.

Mchungaji Dobias alichaguliwa kuwa President baada ya Elingoth. Kipindi hiki kilikuwa na migogoro ya uongozi sehemu nyingi. Na hivyo baada ya Mchungaji Dobias kubadilishwa kutoka katika uongozi, Mchungaji Gabriel Mbwana alichaguliwa kusimamia T.G.F.