Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

JINSI MUNGU ANAVYOTUPENDA

HAYA YAMETOKA WAPI?

Kila kitu kilichopo kina chanzo chake. Dunia hii tuliyopo nayo ina chanzo chake. Licha ya kuwepo taarifa mbalimbali za chanzo cha dunia yetu, taarifa ya kuaminika inasema chanzo cha dunia hii ni Mungu aliyeiumba miaka mingi iliyopita. Mungu huyu taarifa hizo zinaendelea kusema hana mwanzo. Hilo laweza kuonekana jambo la kushangaza na gumu kulielewa. Dunia hii ina mambo mengi yasiyoeleweka lakini ambayo ni kweli na halisi. Si wote tunaoelewa ndege kubwa zinavyopaa angani na namna meli nzito zinavyoelea baharini. Lakini kutojua zinavyofanya kazi, hakuzuii vyombo hivyo visiendelee kufanya kazi zake za kushangaza. Mungu yupo na ukweli kuwa hana mwanzo ni wa kweli kabisa.

MUNGU AWAPA UWEZO WANADAMU

Mungu hakuumba tu dunia hii tunayoishi aliumba pia dunia zingine zinazokaliwa na viumbe wengine. Katika dunia hii Mungu aliumba wanadamu, wanyama, na viumbe wengi wengine na vitu vya asili.  Lakini kwa namna ya pekee aliwaumba wanadamu tofauti na viumbe hawa wengine. Wanadamu aliwapa uwezo na uhuru wa kufanya uchaguzi. Mungu alifanya hivyo akitarajia kuwa mwanadamu angetumia uhuru huo vizuri. Lakini sivyo ilivyotokea. Mwanadamu alitumia uhuru huo kuchagua kisichofaa. Alichagua kufanya dhambi. Baada tu ya kutenda dhambi matatizo yote yalianza hapo. Leo tunakabiliwa na vifo, magonjwa, umaskini, ujinga na mengi mengine kutokana na dhambi.

MUNGU AMPATIA MWANADAMU NAFASI YA PILI

Mungu kwa kuwa anampenda mwanadamu alimpatia nafasi ya pili. Alimpa uwezo wa kutubia makosa yake. Msukumo huo wa kutubu huanzia moyoni mtu anapotafakari umbali alioenda katika kumkimbia Mungu. Wale wanaoitumia fursa hiyo vizuri hupona katika hali yao ya dhambi.  “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana.” Matendo 3:19. Pasipo Mungu hakuna awezaye kutubu. Luka 5:32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu. Matendo ya Mitume 5:31 Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Matendo ya Mitume 11:18 Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.

MUNGU AMPATIA MWANADAMU TOBA

Toba ya Mungu ni tofauti na toba bandia ya kibinadamu. Toba ya Mungu huanzia kwenye kutafakari wema wa Mungu. Warumi 2:4 Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? Wakati ile toba ya kweli husukumwa na wema wa Mungu, ile ya kibinadamu husukumwa katika kujutia matokeo ya dhambi. Haileti badiliko la moyo ila inajaribu kutafuta namna ya kukwepa matokeo ya dhambi.  2 Wakorintho 7:10 Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.

UMUHIMU WA TOBA YA KWELI

Toba ni hatua muhimu ya kwanza katika kutafuta tiba ya dhambi. Kama maabara inavyochunguza aina ya ugonjwa unaomsumbua mgonjwa ili daktari ajue dawa sahihi inayohitajika kuponya ugonjwa husika, ndivyo toba inavyomuandaa mdhambi kupata tiba yake. Mungu anazo njia nyingi za kuamsha toba kwa mwenye dhambi lakini iliyo maarufu ni Neno lake au Sheria yake. Mwanzo 3:9 Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Waebrania 4:12 Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Warumi 7:7 Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.

MUNGU AMSAIDIA MWANADAMU KULITAMBUA TATIZO

Neno la Mungu na Sheria ya Mungu hututia hatiani katika namna isiyotia shaka wala isiyokosea. Kama vitu hivyo visingekuwepo mwanadamu angeweza kutafuta njia mbadala ya kukwepa hatia. Ni jambo gumu kupingana na sauti ya Mungu inayotutia hatiani kwa kuwa ipo ndani katika dhamira zetu. Yohana 8:9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Warumi 2:15 Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea. Kushindana na sauti hiyo ni sawa na kuupiga mchokoo teke. Matendo ya Mitume 26:14 Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo. Hakuna mtu atakayekosa kuokolewa aliye tayari kushirikiana na Mungu.

MUNGU AMPA MWANADAMU MWONGOZO

Neno la Mungu na Sheria ya Mungu haiishii tu katika kutambulisha dhambi, bali pia huitambulisha tabia ya Mungu. Yohana 5:39 “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.” Huu ndiyo mtazamo chanya wa Neno la Mungu na Sheria ya Mungu. Havipo kwa ajili ya kuwatia watu hatiani tu. Bila kuwa na Maandiko Matakatifu na Sheria ya Mungu ni vigumu kujua tabia ya Mungu. Ni matarajio ya Mungu kuwa kwa kuiangalia Sheria na Maandiko Matakatifu mtu aweza kubadilishwa. 2 Timotheo 3:15 “Na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.”

MUNGU AMSAIDIA MWANADAMU KUKIKABILI KIFO

Mabadiliko yaliyotokea baada ya mwanadamu kuingia dhambini hayakukomea tu katika hali ya kujisikia hatia, bali hali ya kuikabili adhabu iliyokuwa imetangazwa na Mungu kabla ya dhambi kufanyika yaani adhabu ya kifo. “Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwanzo 2:17. Mwanadamu amekuwa akiishi katika hali ya hofu mara tu baada ya dhambi kuingia ulimwenguni. Yesu alikuja ili kumwondolea mwanadamu hali hiyo. Waebrania 2:15 “Awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.” Huu ndiyo utumwa wa mauti unaowakabili wanadamu wote. Hakuna wa kukwepa. “Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?” (Zaburi 89:48)

MUNGU AJITOA KUFA BADALA YA MWANADAMU

Adamu alipotenda dhambi hakufa siku ile ile, lakini hiyo haimaanishi kuwa hakufa. Kuna mambo mawili yalitokea. Alianza kufa taratibu siku ile ile aliyotenda dhambi na wakati huo huo kuna mwingine akichukua nafasi yake na kufa badala yake. Maandiko yanasema baada ya dhambi mwanadamu alianza kupungukiwa na utukufu. “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” Warumi 3:23. Huku kupungukiwa na utukufu wa Mungu ni kitendo kinachoendelea kikipunguza uwezo wa aliyeathirika na dhambi. Mwanadamu wa leo (miaka takribani 6,000 baada ya dhambi) amepungua sana kwa mwonekano, kimo, uzito, kinga za mwili na uwezo wa kushinda dhambi kuliko mwanadamu yule wa kwanza.