Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

ZAKA NA SADAKA

ZAKA NA SADAKA

Zaka na sadaka ni utaratibu ulioanzishwa na Mungu kwanza kwa kusudi la kumsaidia mwanadamu mwenyewe kutambua kuwa mmiliki wa mali na vyote alivyonavyo ni Mungu na kwa kadri anavyotambua ukweli huo na kutii agizo la kutoa sehemu ya mali yake kwa Mungu ndivyo kwa kadri hiyo hiyo ataendelea kupokea mibaraka isiyo na idadi na isiyo na kikomo. Sababu ya pili ya kuanzisha utaratibu wa kurudisha zaka na kutoa sadaka ulilenga kuitegemeza kazi ya Mungu hapa duniani ambayo kwa sehemu kubwa inahusu matumizi ya fedha na mali.

Mungu hata hivyo angeweza kuifanya kazi yake hapa duniani bila kutegemea zaka na sadaka ya mwanadamu kwa kuwa yeye ana uwezo wa kufanya chochote bila msaada wa mwanadamu. Ayubu 26:7 “Yeye hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu.” Tena kumruhusu mwanadamu kushiriki katika kuifanya kazi yake hapa duniani ni upendeleo ambao mwanadamu hakustahili. Matendo ya Mitume 17:24-25 “Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote.”

Mungu ameruhusu wanadamu wahusike na kushiriki katika ujenzi wa ufalme wake hapa duniani kama sehemu ya maandalizi ya nafasi ya utawala wanayoandaliwa kuchukua baada ya dhambi kukoma katika makao ya milele. Moja ya sifa muhimu ya mtawala ni uwezo wa kujitawala. Ufunuo wa Yohana 2:26 “Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa.” Sisi tutakaoketi kwenye kiti cha enzi tunajaribiwa ili kuona kama tutalimudu jukumu hilo linalohitaji kujikana nafsi kukubwa. 1 Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.” Adamu na Hawa pale Edeni walishindwa kuamini kuwa kwa kutii agizo la Mungu wangekuwa salama wakajaribu kujitafutia usalama wa wakati ujao kwa kutamani kile walichozuiwa. Mungu anatupa nafasi ya pili baada ya Adamu kushindwa pale bustanini kwa kutupatia agizo la kurudisha Zaka na kutoa sadaka. Anatuagiza katika Waebrania 13:5 kwamba, “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”

KURUDISHA ZAKA

Zaka ni moja ya kumi ya mapato yako au ya mali yako yote. Kiwango hiki cha mali au fedha unapaswa kukirudisha kwa Mungu.  Kumbukumbu la Torati 14:22 “Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.” Zaka haitolewi kama inavyotolewa sadaka kwa sababu kadhaa. Zaka ni gawio la Mungu kutoka mapato yako na kiwango chake hakipungui wala kuzidi; siku zote hubaki kuwa asilimia kumi ya mali na mapato yako. Ili mali ipatikane ni lazima nguvu, maarifa, na muda vitumike. Na ni ukweli ulio wazi kuwa bila Mungu nguvu, maarifa na muda visingeweza kupatikana. Na kama mali tulizonazo zinapatika kwa kushirikiana na Mungu ni ukweli ulio Dhahiri kuwa Mungu ndiye mwenye mchango mkubwa katika mali tunazomiliki. Kumbukumbu la Torati 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Lakini pamoja na ukweli huo wote Mungu anahitaji gawio la asilimia kumi na sisi akituachia asilimia zote tisini kwa matumizi yetu. Hakuna mbia hapa duniani anayechangia asilimia kubwa katika upatikanaji wa mali na kuwa radhi kupokea asilimia kumi tu ya kinachopatikana isipokuwa Mungu.

Kutoa zaka ni kurudisha gawio linalomstahili Mungu kama mshiriki mkuu wa mafanikio yetu na ni njia pia ya kumsihi Mungu aendelee kuwa mshirika wa shughuli zetu za kiuchumi ili awe msaada pale changamoto mbalimbali zitakapoibuka. Malaki 3:11 “Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.” Mungu ameahidi kutusaidia kukabili changamoto za kiuchumi zinazoweza kukwamisha tusifikie malengo tuliyojiwekea ikiwa tutakuwa waaminifu katika kumrudishia zaka yake kwa wakati. Hakikisha kila kinachopatikana iwe fedha au mazao unatenga asilimia kumi kando kabla hujaanza matumizi yako mengine. Kama ni mshahara zaka yako itakuwa asilimia kumi ya Basic Salary au Gross Salary – yaani ule mshahara ule mshahara wote unaoupata kabla ya makato ukiwa pia umeigiza marupurupu mengine yaliyo nje ya mshahara wako ulioajiriwa nao – mfano overtime, nk.

Kutolea zaka kwenye mshara uliobaki baada ya makato mengine ni kumpunja Mungu gawio lake analostahili. Kutoa zaka kabla ya makato mengine ndiko kunakotambulika kama kutoa zaka kamili. Malaki 3:10 “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.” Mungu anawaahidi wale watakaotoa zaka kamili – yaani asilimia kumi ya mapato yao, kuwa ataizidisha ile mali au fedha waliyobakiwa nayo baada ya kutoa zaka kiasi kuwa itakidhi mahitaji yao yote na kubaki.

Ibrahimu alikuwa muumini wa utaratibu huu wa kutoa zaka. Waebrania 7:4 “Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara.” Kama matokeo ya kurudisha zaka kwa uaminifu Ibrahimu alibarikiwa sana na Mungu. Mwanzo 13:2, 6 “Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.” Hata leo wapo wengi waliobarikiwa kwa kufuata utaratibu wa kurudisha zaka kwa uaminifu. Wewe unaweza kuwa mmojawapo ukipenda.

Mungu anaruhusu tumjaribu katika swala hili la utoaji wa zaka. Anajua siku tutakapojaribu hatutaacha kutoa. Tutagundua kuwa “. . . Ni heri kutoa kuliko kupokea.” (Matendo 20:35). Wengi wamejikuta katika uhitaji mkubwa na umasikini wa kutisha kwa sababu ya kuzia zaka na sadaka. Wale wanaozuia zaka na sadaka Mungu anawaita wezi waliolaaniwa. Malaki 3: 8-9 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.”

Kiukweli wale wanaozuia zaka ya Mungu si tu kwamba wamekuwa ni wezi bali ni wanyang’anyi hasa. Ni wanyang’anyi kwa kuwa wizi hufanyika wakati ambao mwenye mali hajui kuwa anaibiwa. Hakuna wakati mwanadamu atamwibia Mungu kwa maana ya kuwa asijue kuwa unamuibia. Kile kitendo cha kutorudisha zaka kinafananinshwa na unyang’anyi unaofanyika mchana kweupe. Huwezi kufanya kitendo kama hicho kwa Mungu kisha uwe salama. Kwa hakika hali yako itakuwa sawa nay a mtu aliyelaaniwa na wazazi wake. Mambo yako hayataweza kusimama. Amosi 5:19 anasema mtu kama huyo, “Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.”

Lakini ukiwa mwaminifu wa kurudisha zaka Mungu anaahidi nini? Kumbukumbu la Torati 15:6 “Kwani Bwana, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao.” Kumbukumbu la Torati 28:12 “Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.”

MATUMIZI YA ZAKA

Mungu alipanga zaka itumike kama posho ya watumishi aliowachagua kutumika kwa kazi yake kwa mkataba wa kudumu. Hesabu 18:21 “Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania.” Katika Agano Jipya ambapo kazi ya ukuhani hufanywa na waumini wote, zaka hutumika na watumishi wa injili. 1 Wakorintho 9:13-14 “Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.”

Zaka hairuhusiwi kutumika kwa matumizi mengine. Pamoja na kuwa wale wanaopokea zaka wanapaswa kuitumia kiuhalali kama ilivyoelekezwa na kuishi maisha yaliyo mfano kwa wanaowaongoza, mtu asijichukulie jukumu la kuzuia kutoa zaka kwa kuwa Mungu atamhesabia mtu kama huyo hatia. Kama watu wote wangetoa zaka kwa uaminifu tusingekuwa na upungufu wa watendakazi na injili ingekuwa imeenea kila mahali. Warumi 10:14-15 “Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!”

Zaka inapokuwa kidogo wahubiri wanautumwa huwa wachache lakini ikiwapo ya kutosha ghalani watumishi wengi zaidi huajiriwa na kutumwa. Mungu anaposema “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu . . .” (Malaki 3:10) anamaanisha kwenye kanisa lake. Leo hii umeibuka utaratibu wa kujianzishia makanisa ya mifukoni yanayomilikiwa na familia au kinyume na utaratibu wa kitaasisi unaofuatwa na kanisa lililoundwa kwa kufuata taratibu zilizozoeleka. Wanaofanya hivyo hebu wajitathmini kama wamefuata kiusahihi agizo hili la Malaki 3:10.

UTOAJI WA SADAKA

Mungu ameagiza wanadamu watoe sadaka kama njia ya kuonesha shukurani zao kwa Mungu aliyewapa zawadi za namna mbalimbali. Kwa kawaida sadaka haina kiwango kama zaka bali mtu hutoa kadri alivyobarikiwa. Biblia inasema, “. . . Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi” (Luka 12:48.) Waisraeli waliagizwa kutoa sadaka za wanyama wakati wa Agano la Kale. Wanyama hao walitakiwa wawe wakamilifu wasio na kilema. Mambo ya Walawi 22:20 “Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu.” Sadaka hiyo ilikuwa inamlenga Yesu aliye Mwanakondoo wa Mungu achukuaye dhambi zetu. Leo sisi hatutoi tena sadaka ya wanyama maana Yesu alijitoa yeye mwenyewe awe sadaka. Waebrania 9:14 “basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”

Leo sadaka inayotolewa ni ya vitu na fedha. Luka 12:33 “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.” Kama ilivyo katika zaka, sadaka nayo inatakiwa itolewe kwa kiwango kinachofanana na mibaraka uliyopokea kinyume na hapo Mungu anakuchulia unamwibia. Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.” Hiyo inayoitwa dhabihu kwenye fungu hapo juu ni sadaka. Kumbe Mungu anajua kama sadaka unayotoa imefikia viwango vinavyostahili au la. Kimsingi anayetoa zaka kwa uaminifu huwa mwaminifu pia kwa utoaji wa sadaka.

Kiwango cha sadaka mara nyingi huwa juu zaidi ya zaka kwa ubora na kwa uwingi. Marko 12:41-44 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Hii ni lazima ilikuwa sadaka kwa maana kama ingekuwa ni zaka isingewezekana mwanamke maskini awe ametoa zaidi kuliko wale matajiri kwa kuwa zaka ni asilimia kumi ya mapato ya mtu. Kanuni ya kutoa sadaka ni kutoa kile kilicho bora katika vile unavyovimiliki. Hii ndiyo sababu Mungu alimtoa mwanawe wa pekee na Ibrahimu naye akamtoa Isaka mwanaye wa pekee kuwa sadaka. Hata Hana yule mwanamke tasa Mungu alipomfungua tumbo lake alimtoa mwanae Samweli sadaka. 1 Samweli 1:27-28 “Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.”

Waisraeli walikuwa wanatoa sadaka kwa kiwango kinachoanzia asilimia kumi ya mapato yao na kuendelea. Sadaka hii waliita zaka ya pili. Ili kuhimiza mikusanyiko ya watu kwa ajili ya huduma za kidini, sambamba ni kuwapatia maskini mahitaji zaka ya pili kutoka kwenye mapato yao ilihitajika. Kuhusiana na zaka ya kwanza, Bwana alikuwa ametangaza, “Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli . . .” lakini kuhusiana na zaka ya pili aliamuru, “Nawe utakula mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng'ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wako, daima.” Zaka hii au inayofanana nayo kifedha, zilitakiwa kwa miaka miwili ziwe zinaletwa pale hekalu liliposimikwa. Baada ya kutoa sadaka ya shukurani kwa Mungu na sehemu maalumu kwa kuhani, mtoaji alitumia kilichobaki kwa karamu za kidini ambapo Mlawi, mgeni, na yatima na mjane wangeshiriki . . .” (Welfare Ministry uk. 273)

Kutokana na nuru hiyo watu wa Mungu wanahimizwa kutoa sadaka sawa na zaka au kuzidi kidogo kulingana na jinsi mtu alivyobarikiwa. Kwa bahati mbaya takwimu za utoaji zinaonesha wengi wanathamini au wanahofu kutoa zaka zaidi kuliko kutoa sadaka. Mazoea haya yanayanyima makanisa mapato yanayohitajika kuendeshea shughuli za kikanisa. Shughuli za kikanisa zinazoendeshwa kwa sadaka za waumini ni kama kununulia samani, vitabu na vifaa mbalimbali vya idara na ofisi za kanisa pamoja na kugharimia shughuli za uinjilisti.

Hata hivyo sadaka inatakiwa itolewe kwa hiyari na moyo wa kupenda kwa kuwa ndiyo inayopima mahusiano ya mtoaji na Mungu wake. Zaburi 54:6 “Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema.” 2 Wakorintho 9:7 “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” Kutoka 35:5 “Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba.” Watu watakapotambua upendo ambao Mungu amewatendea maishani hawatasita kumtolea. Wana wa Israeli wakati mmoja walipoguswa wakatoa hadi vikazidi hata ikabidi viongozi wasitishe zoezi la utoaji. Kutoka 36:5-7 nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana aliagiza ifanywe. Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena. Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.

Kutoa sadaka hakuangalii utajiri wa mtu alionao bali kunatokana na mguso wa kiroho. Katika Biblia, watu wa Makedonia walitoa sana ingawa walikuwa watu maskini. 2 Wakorintho 8:1-3 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao.” Ukisubiri mpaka siku utakapofanikiwa sana kiuchumi ndipo utoe sadaka utasubiri sana. Unapaswa uishinde tamaa ya fedha na mali kwa kumheshimu Mungu. Mithali 3:9-10 “Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.”