Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

MASHAIRI YA MCHUNGAJI LETTA

KIZOTA NET EVENT, IWE YA MAFANIKIO

1. Kizota Net Eventi, hili ni kubwa tukio,
Tena ni tukio nyeti, liletalo shangilio,
Ni mwingine mkakati, wa mavuno si kilio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

2. Tupo kwenye harakati, za kuondosha kilio,
Shetani awekwe kati, na kukatwa masikio,
Tunampiga kibuti, na kumfukuza mbio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

3. Mahubiri haya nyeti, yakawe ni kimbilio,
Yakakupatie cheti, na mema mafanikio,
Yakuweke katikati, yakidhi matarajio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

4. Wapaswa kujizatiti, kabla ya siku hio,
Jiundieni kamati, kuliratibu tukio,
Na kuweka mikakati, ya kulipamba tukio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

5. Nawaomba wenyeviti, hamasisheni tukio,
Vile vipaza sauti, na kwaya na mapambio,
Mikeka na vile viti, viwe na mpangilio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

6. Mahubiri haya nyeti, yachome kila sikio,
Yakaingilie kati, maisha yenye vilio,
Yakimwinua kwa dhati, Yesu kama kimbilio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

7. Malekana mwenyekiti, liongoze shambulio,
Sisi twapiga magoti, kuombea kazi hio,
Wazo tunalisapoti, tumeshatoa ridhio,
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio

8. Kizota Net Event, nitakwenda itikio,
Kizota Net Event, siyo ya majaribio,
Kizota Net Event, hiyo inakuja mbio
Kizota Net Event, iwe ya mafanikio


USIILEWESHWE NA SIFA, SIFA MBAYA ZINAUA

1. Usileweshwe na sifa, sifa zitakuumbua,
Kuna siku utakufa, pasipo kujitambua,
Ninakupa taarifa, kwamba sifa inaua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

2. Sifa huleta maafa, unapojitutumua,
Maana mpenda sifa, anajifanya kujua,
Hukataa maarifa, na kukataa kukua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

3. Wale wapendao sifa, wanahisi kupungua,
Wanahisi kuna ufa, ambao unasumbua,
Hivyo wanaona sifa, ndiyo itayotatua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

4. Usipendelee sifa, Mungu atakuumbua,
Asitahiliye sifa, ni Mungu hilo tambua,
Unapopokea sifa, tatizo unalizua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

5. Usiwape watu sifa, maana utawaua,
Wataleweshwa na sifa, na kamwe hawatakua,
Sifa huleta maafa, unatakiwa kujua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

6. Kama unatoa sifa, zisiwe zinazoua,
Zisizoleta maafa, zinazoleta kukua,
Zinazojenga taifa, na kulifanya kukua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

7. Viongozi wenye sifa, taifa wanaliua,
Maana palipo ufa, watashindwa kupajua,
Wataambulia kufa, watakaowazindua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.

8. Anastahili sifa, yule anayetambua,
Kwamba siku moja sifa, itakuja muumbua,
Na akaacha misifa, pia kujitutumua,
Usileweshwe na sifa, sifa mbaya zinaua.



KAMA HAYANA UPENDO, MAISHA HAYA SI KITU.

1. Maisha haya si kitu, kama hayana upendo,
Maisha yawe na utu, ndipo hujaa uhondo,
Yasipothamini watu, si maisha ni uvundo,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

2. Maisha siyo ya vitu, maisha siyo mitindo,
Maana wingi wa vitu, huweka uzima kando,
Maisha kupenda watu, na maisha ni matendo,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

3. Kama unapenda watu, umeshauanza mwendo,
Kwani maisha ni watu, maisha siyo vishindo,
Kutokuwapenda watu, si maisha ni uvundo,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

4. Unapoonyesha utu, unachochea upendo,
Unawashawishi watu, kuiga wako mwenendo,
Vitu si muhimu katu, muhimu sana upendo,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

5. Nijapokuwa na vitu, lakini sina upendo,
Naonekana si kitu, sawasawa na marando,
Upendo ni kila kitu, upendo mwendo mdundo,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

6. Mmemsikia mtu, mwenye utajiri rundo,
Katoa talaka tatu, ndoa kaona uvundo,
Asikuambie mtu, ndoa yataka upendo,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

7. Maisha haya si vitu, maisha yataka pendo,
Unapothamini watu, huo ndiyo uzalendo,
Nini thamani ya vitu, pale pasipo na pendo?
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

8. Acha kuthamini vitu, zingatia sana pendo,
Na pia ujali watu, waonyeshe na upendo,
Acha kuchukia watu, ukatili weka kando,
Kama hayana upendo, maisha haya si kitu.

AWE WAKO PEKE YAKO, ASIWE WA WENZI WAKO

1. Awe wako peke yako, huyo ndiye mwenzi wako,
Asije ondoka kwako, akenda kwa mwenzi wako,
Mfuate aendako, kumuacha iwe mwiko,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

2. Yanasema Maandiko, huo ni ubavu wako,
Kakupa Muumba wako, usimchape viboko,
Akakupe burudiko, usiende kwingineko,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

3. Hilo ni chaguo lako, mpende huyo ni wako,
Mlaze kwenye tandiko, asije pata sumbuko,
Asiwe na mpauko, uso uwe na chereko,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

4. Asivae mipasuko, akashusha hadhi yako,
Au kuwa na minuko, hali hiyo iwe mwiko,
Kokote kule aliko, harufu njema iweko,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

5. Umtunze mtu wako, umpe madikodiko,
Apende mapishi yako, asipende ya wenzako,
Na alapo kwingineko, akumbuke pishi lako,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

6. Ajae moyoni mwako, na kwenye kauli zako,
Msifie kwa wenzako, wambie huyo ni wako,
Akupaye farijiko, sabuni ya roho yako,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

7. Mtii ni mume wako, aliyekutoa kwako,
Mlinzi wa nyumba yako, mleta mkate wako,
Kwake kumekuwa kwako, mstahi mume wako
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.

8. Mjali ni mwenzi wako, mpende ni tunu yako,
Mfurahishe mwenzako, asiwaze atokako,
Wasimbebe wenzako, ukapata hanagaiko,
Awe wako peke yako, asiwe wa wenzi wako.



MAMA SAMIA HASSANI, IONGOZE TANZANIA

1. Tumetoka msibani, Watanzania twalia,
Hatunaye maishani, Magu ametangulia,
Atatuongoza nani, hapa kwetu Tanzania,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

2. Shikilia usukani, sisi twakuangalia,
Walete wote nyumbani, nchi waliokimbia,
Nchi iwe ya amani, tusije kuangamia,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

3. Ipange safu makini, itayokutumikia,
Itayojua ni nini, kile unakusudia,
Achana na watu duni, wasije kuchafulia,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

4. Tunayo kubwa imani, juu yako mama Samia,
Wewe ni wetu rubani, nchi tumekuachia,
Iondoe tafrani, tuwe moja familia,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

5. Na kule mahakamani, nazo mahabusi pia,
Uwatoe watu ndani, wale wasio hatia,
Warudi uraiani, nchi kuipigania,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

6. Kaa nao wapinzani, ikiwa utaridhia,
Ujuwe ni jambo gani, wanalolalamikia,
Kuondoa uvutani usiotusaidia,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

7. Wakulima vijijini, wengine wanaumia,
Bei bado zipo chini, soko halijatulia,
Zungumza na jirani, tukauze nako pia,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.

8. Wafanyakazi nchini, nao pia wanalia,
Mishahara ipo chini, kapandishe japo mia,
Vijana waajirini, mana nao wanalia,
Mama Samia Hassani, iongoze Tanzania.



NCHI IMETIKISIKA KWA KIFO CHA MAGUFULI

1. Huzuni imetushika, hatulali na hatuli,
Watu wanahangaika, kwa maumivu makali,
Magufuli katutoka, inauma kweli kweli,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

2. Magufuli alitaka, tuweze kufika mbali,
Tuweze kuheshimika, kwa miradi mbalimbali,
Uhai umetoweka, nani atafanya hili?
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

3. Magufuli kaondoka, imetutoka akili,
Tuendako tutafika? Haya ni yetu maswali,
Ni kweli hataamka, amekwenda Magufuli,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

4. Watu wanahuzunika, kweli kifo kikatili,
Kuna wanaoanguka, katika tukio hili,
Na wafao kadhalika, inasikitisha kweli,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

5. Twatambua kwa hakika, uzito wa Magufuli,
Kinara wa Afrika, aliyetetea kweli,
Sasa amepumzika, tukubali hiyo hali,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

6. Mungu wetu mtukuka, tupunguzie maswali,
Tuliza yetu mizuka, tuupumzishe mwili,
Kisha uipe baraka, hii yetu serikali,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

7. Nani sasa atashika, kasi yake Magufuli,
Samia mheshimika, iongoze serikali,
Na bila kubabaika, nchi ifikishe mbali,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.

8. Mungu wetu mtukuka, utufundishe kwa hili,
Tujue kwa uhakika, kufa ni jambo la kweli,
Nayo siku ikifika, tulale katika kweli,
Nchi imetikisika, kwa kifo cha Magufuli.



KAMA UNATAKA MALI, ZINGATIA UWAKILI


1. Mtoto mwenye akili, aliitamani mali,
Akaja kumsaili, babaye Akilimali,
Akampa swali hili, “nitaipataje mali”?
Kama unataka mali, zingatia uwakili.

2. Mzee Akilimali, akalielewa swali,
Akakiri kuwa mali, ni muhimu kwelikweli,
Ila yataka akili, ili kuipata mali,
Kama unataka mali zingatia uwakili.

3. Akasema uwakili, zingatia jambo hili,
Uwakili ndiyo mali, sikia yangu kauli,
Kanuni ukizijali, hapo utapata mali
Kama unataka mali, zingatia uwakili.

4. Wakati ukiujali, utakupatia mali,
Kuzurura si halali, tumia muda vizuli,
Usicheze makamali, fanya kazi za halali,
Kama unataka mali, zingatia uwakili.

5. Fanya kazi ya halali, inayokupa ugali,
Iwe kazi ya ukuli, au kuuza asali,
Kazi ndiyo uwakili, ifanye upate mali,
Kama unataka mali, zingatia uwakili.

6. Fanya kazi kwa akili, isiyouchosha mwili,
Mana akili ni mali, isake kwa kila hali,
Watumiao akili, hao wana nyingi mali,
Kama unataka mali, zingatia uwakili.

7. Zisake kila mahali, fursa za kila hali,
Ufike hadi Kigali, ukiitafuta mali,
Uvivu katu si mali, uutupilie mbali,
Kama unataka mali, zingatia uwakili.

8. Ukishaipata mali, rudisha kwa mwenye mali,
Mpe mgao halali, yaani zaka kamili,
Na sadaka mbalimbali, zitoe upate mali,
Kama unataka mali, zingatia uwakili.



UMOJA KITU CHA HERI, ILA UWE WA UKWELI


1. Ninalianza shairi, kuzungumza ukweli,
Kuna jambo lenye shari, na utata kwelikweli,
Tena jambo la hatari, lahusishwa na ukweli,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

2. Ameianza safari, akenda kila mahali,
Watu akiwahubiri, wamrudie Jalali,
Eti ni jambo la heri, kwa pamoja tukisali,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

3. Umoja huo nakiri, hilo jambo la halali,
Ni jambo lenye fahari, na tamu kama asali,
Lakini ni la hatari, likipuuza asili,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

4. Umoja ule nzuri, utajali maadili,
Maandiko utakiri, wala hautakejeli,
Huku ukitafakari, ile Sabato ya kweli,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

5. Umoja huo hatari, usiposema ukweli,
Ukikosa ujasiri, kusonda ubaradhuli,
Uliofanywa kwa siri, tulipokosa akili,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

6. Wale wote wajeuri, waliokanyaga kweli,
Wakajaza utitiri, wa dini za udalali,
Tunawataka wakiri, na ndipo tuje kusali,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

7. Tusione ufahari, kuacha dini ya kweli,
Dini ya toka dahari, dini yenye maadili,
Siyo dini ya sayari, dini ya wapiga dili,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.

8. Dini moja naikiri, ni dini ile ya kweli,
Siyo huu utitiri, hautufikishi mbali,
Umoja huu si siri, utajaleta ajali,
Umoja kitu cha heri, ila uwe wa ukweli.



IKIWA UNANIPENDA ZITUNZE AMRI ZANGU


1. Hakika ninakupenda, kutoka moyoni mwangu,
Kokote ninakokwenda, wewe u karibu yangu,
Shetani akikuwinda, ama zake ama zangu,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

2. Pamoja na kukupenda, sikia kauli yangu,
Ninataka kukufunda, usiwe jeuri kwangu,
Usipende kuziponda, sheria ni mali yangu,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

3. Naomba nipe heshima, kama Muumbaji wako,
Na isiwe kwa lazima, bali kwa hiyari yako,
Nalo ulifanye hima, mana ni muhimu kwako,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

4. Kila nikikutazama, napata mashaka kwako,
Wautangazia uma, mimi ni rafiki yako,
Jambo linaloniuma, hutunzi kauli zako,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

5. Haushi kuzisema, katika vikao vyako,
Kwamba siyo za lazima, zimekoma na haziko,
Lakini mimi nasema, kukoma hizo ni mwiko,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

6. Amri tangu ujima, zilikuweko na ziko,
Zipo dunia nzima, siyo tu hapa kwako,
Sitaki hizo hujuma, sitaki utani wako,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

7. Kama wataka uzima, onyesha nidhamu yako,
Na mimi ninakupima, nijue akili yako,
Achana na kulalama, acha madharau yako,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.

8. Kama hauna heshima, usilaumu wenzako,
Wao wanaona vyema, kumtii Mungu wako,
Hivyo nawe nakutuma, uwaige wenzi wako,
Kama kweli wanipenda, zishike Amri zangu.



KUTOA ZAKA YA BWANA, KIPIMO CHA UKARIMU


1. Ni jambo la uungwana, tena ni jambo muhimu,
Twapasa kukumbushana, kwa kutumia kalamu,
Tusije laumiana, ya kwamba hukufahamu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

2. Kama wewe ni kijana, unafanya kazi ngumu,
Ni mtu wa kupambana, uvivu kwako ni sumu,
Unahitajika sana, jambo hili kufahamu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

3. Kama wewe msichana, tena uliyehitimu,
Unajaribiwa sana, kutokuwa mkarimu,
Unahitaji kupona, na moyo huo mgumu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

4. Zaka hiyo ni ya Bwana, usiile ni haramu,
Kaitenge mbali sana, usije iona tamu,
Utafilisika sana, zaka ya Bwana ni sumu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

5. Pato likipatikana, jambo la kwanza muhimu,
Itenge zaka ya Bwana, kwenye chombo maalumu,
Na uilete kwa Bwana, kwa furaha na nidhamu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

6. Moja ya kumi ya Bwana, wapaswa kuiheshimu,
Usije ukagombana, kisha upate wazimu,
Zingatia hilo sana, ishi maisha matamu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

7. Mungu kakupenda sana, hata wewe wafahamu,
Tangu enzi za ujana, angali anakukimu,
Nawe shukurani huna, zaka unamdhulumu?,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.

8. Baraka kila namna, huzipata wakarimu,
Mana hawana hiyana, Mungu hawamdhulumu,
Nawe nakusihi sana, Mungu wako muheshimu,
Kutoa zaka ya Bwana, kipimo cha ukarimu.



SIKU SITA FANYA KAZI, YA SABA UPUMZIKE


1. Heshima ya mtu kazi, kazi isiyo makeke,
Iwe kupika maandazi, fanya usinug’unike,
Mradi siyo ya wizi, ifanye uheshimike,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

2. Raisi wetu kipenzi, katika hotuba zake,
Amesema hapa kazi, tufanye tusibweteke,
Msemo huo wa kazi, naomba ukubalike,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

3. Ndugu yangu piga kazi, pambana hadi uvuke,
Acha mambo ya upuuzi, kusudi utajirike,
Lakini bada ya kazi, nenda ukapumzike,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

4. Unapoifanya kazi, Mungu wako mkumbuke,
Anayekupa pumzi, usimpige mateke,
Usifanye yako kazi, kwenye hiyo siku yake,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

5. Jumapili anza kazi, nenda ukachakarike,
Fanya bila utegezi, hadi sita zikafike,
Mwisho wa juma la kazi, na wewe upumzike,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

6. Unapoipenda kazi, ipende na miiko yake,
Alishasema Mwenyezi, hataki uathirike,
Usinogewe na kazi, heshimu agizo lake,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

7. Mungu alifanya kazi, kuumba dunia yake,
Mwisho wa juma la kazi, kaacha shughuli zake,
Akawaagiza wazazi, wafuate nyayo zake,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.

8. Kama utaacha kazi, ili ukapumzike,
Na kufanya kumbukizi, ya uumbaji wake,
Nakutamkia wazi, unazo Baraka zake,
Siku sita fanya kazi, ya saba upumzike.



SAUTI KUU NGURUMA NGURUMA WATU WAPONE


1. Sauti kuu ni mama, afundishaye wengine,
Ambaye amesimama, kuliko hao wengine,
Gazeti lenye heshima, lisomwalo na wanene,
Sauti Kuu nguruma, nguruma watu wapone.

2. Sauti Kuu ni duma, kimbia uonekane,
Ufike nchi nzima, kila pembe wakuone,
Utokapo kila juma, wakusomapo wapone,
Sauti Kuu nguruma, nguruma watu wapone.

3. Sauti Kuu tazama, waangalie wajane,
Watazame kina mama, wavute waonekane,
Waoneane huruma, maarifa wapeane,
Sauti Kuu nguruma, nguruma watu wapone.

4. Sauti Kuu koroma, koroma ujulikane,
Ufike kwa wakulima, nao pia uwakune,
Uwafundishe kulima, mazao mengi wavune,
Sauti Kuu nguruma, wakusomao wapone.

5. Sauti Kuu lalama, dhambi isionekane,
Iseme bila huruma, wadhambi watafutane,
Ili wabaki wazima, na Shetani watengane,
Sauti Kuu nguruma, ili wadhambi wapone.

6. Sauti Kuu lazima, taarifa tupashane,
Tupashe ya juma zima, yaliyojiri kwingine,
Na hata ya kule nyuma, hayo nayo uyanene,
Sauti Kuu nguruma, nguruma watu wapone.

7. Sauti Kuu sukuma, wasomi watazamane,
Tupe mada za heshima, na kamwe usitukane,
Watamani kukusoma, wala haya wasione,
Sauti Kuu nguruma, nguruma watu wapone.

8. Sauti Kuu daima, kwetu usikosekane,
Hakikisha kila juma, unakuja tukuone,
Wewe ni wetu uzima, wala hatuna mwingine,
Sauti Kuu nguruma, nguruma watu wapone.



SIKU YA SABA YA JUMA SIKU BORA YA IBADA


1. Leo nawapa shuhuda, kina baba kina mama,
Naomba mnipe muda, niwajuze ya uzima,
Jinsi nilipata shida, na kisha nikasimama,
Siku ya saba ya juma siku bora ya ibada.

2. Siku ipi ya ibada, aliyotupa Karima,
Swali lilinipa shida, nikaanza kuparama,
Nikahitaji msaada, nao haukuja hima,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

3. Kulikuwa na ibada, siku ya kwanza ya juma,
Kukawepo na ibada, siku ya sita ya juma,
Na pia kuna ibada, siku ya saba ya juma,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

4. Bada ya kupita muda, nikagundua zahama,
Ya kwamba hii ibada, imefanyiwa hujuma,
Mungu anayo ibada, siku ya saba ya juma,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

5. Ukweli wa hii mada, angalia kule nyuma,
Wakati anaiunda, dunia kwa juma zima,
Mungu alitenga muda, mwishoni mwa hilo juma,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

6. Akabariki ibada, akasema ni lazima,
Ifanywe na kina dada, watoto nao wazima,
Na izingatie muda, ifanywe kwa taadhima,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

7. Wakina kaka na dada, wakina baba na mama,
Tuiheshimu ibada, maana ni ya lazima,
Na tuzingatie muda, Mungu aliotutuma,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

8. Ibada inayo muda, nayo ni mwisho wa juma,
Ijumaa wake muda, siku inapoyoyoma,
Ufikapo huo muda, shughuli zinasimama,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada,

9. Msije fanya husuda, kuitunza ni lazima,
Kupuuza huo muda, ni kuukosa uzima,
Na kujiletea shida, zisizo za ulazima,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.

10. Si siku ya kawaida, siku ya saba ya juma,
Siku tupewayo muda, dhambi zetu kuungama,
Tuzilete zetu shida, na tutakuwa salama,
Siku ya saba ya juma, siku bora ya ibada.



SIKU KUMI ZA MAOMBI NA ZIKAWE ZENYE HERI

1. Tupo mwanzoni mwaka, tunaianza safari,
Moyoni hatuna shaka, mambo yapo ng’aring’ari,
Ila Mungu anataka, jambo hili tafakari,
Siku kumi za maombi, kazitumie vizuri

2. Hakikisha unafika,na unawahi vizuri,
Na upange kualika, maskini na tajiri,
Ili waje burudika, Yesu wanapomkiri,
Siku kumi za maombi, kazitumie vizuri.

3. Uache kuhangaika, au kuleta kiburi,
Utaja kuaibika, ukose mambo ya heri,
Acha pesa kuzisaka, kapokee mahubiri,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri,

4. Kama wataka Baraka, hizo ni zako tayari,
Kanisani ukifika, kamwe hutatahayari,
Ni nyingi zimefurika, kuzikosa ni hiyari,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri.

5. Kila unachokitaka, Mungu akupe kwa siri,
Kila unachokereka, nenda nacho ukakiri,
Kiandike na kuweka, kwenye chombo cha mimbari,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri.

6. Na shuhuda kadhalika, kazitoe kwa uzuri,
Na jinsi ulivyovuka, na kuzikwepa hatari,
Na ulivyofaidika, hadi ukapata gari,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri.

7. Tena utawakumbuka, na watu wako mahiri,
Hao utawaandika, majina yao kwa siri,
Kisha utawatamka, kwenye maombi ya siri,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri.

8. Mafungu utaandika, kisha kuyatafakari,
Ahadi za uhakika, nazo utazikariri,
Na ndipo utatamka, unapotaka kusari,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri.

9. Omba Roho atashuka, na kuondoa kiburi,
Omba utatakasika, na kusafisha dhamiri,
Omba na utaponyeka, hata magonjwa ya siri,
Siku kumi za Maombi, kazitumie vizuri.

10. Tamati nimeshafika, ombi langu tafakari,
Uache kurukaruka, jiandae kwa safari,
Siku kumi zikifika, kazitumie vizuri
Siku kumi za Maombi, na zikawe zenye heri.



CHUNGA SANA UTENDAYO, YASIMKWAZE NDUGUYO

1. Chunga uyatazamayo, na yale uyafanyayo,
Chunga pia usemayo, na mavazi uvaayo,
Yasije mvunja moyo, jirani ayaonayo,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

2. Watu wanakuamini, kuwa ni mtu wa dini,
Usiyependa matani, mwadilifu na makini,
Hapo kwenu mtaani, kukuiga watamani,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

3. Unapotoka nyumbani, kagua mavazi yako,
Yanatoa picha gani, kwako na kwa ndugu zako,
Kama ni mavazi duni, yatoe mwilini mwako,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo

4. Chunga unavyojipamba, usizidishe mikogo,
Usiwe kama washamba, wapakao mikorogo,
Usije jiremba remba, ukawa kama kinyago,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

5. Viduku navyo vya nini, nyoa kistaarabu,
Usinyoe kwa fasheni, zinazoleta aibu,
Mawigi na makatani, kichwani usijaribu,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

6. Lugha zako za kihuni, hizo si zaizi yako,
Na matusi ya nguoni, hatutarajii kwako,
Wewe ni mtu wa dini, matusi kwako ni mwiko,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

7. Uzinzi si fungu lako, huo usitajwe kwako,
Itunze heshima yako, timiza maono yako,
Wadhambi wakija kwako, washinde kwa Maandiko,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

8. Na pombe usitumie, ni mbaya inalewesha,
Mateja wasaidie, waache bangi kuwasha,
Kwa Yesu wakaribie, awafundishe maisha,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

9. Watu wanatumaini, kujifunza toka kwako,
Hivyo ukawe makini, hasa kwa tabia yako,
Usije vaa heleni, sikio si mali yako,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

10. Beti huu ni wa mwisho, nimekuasa mwenzangu,
Ufanye marekebisho, usije kukosa mbingu,
Maisha ya maonyesho, hayampendezi Mungu,
Chunga sana utendayo, yasimkwaze nduguyo.

 

MTAJI WA MASIKINI NI NGUVU ZAKE MWENYEWE

1. Maisha si lelemama, maisha ni kukazana,
Kama una afya njema, umshukuru Rabana,
Toka nyumbani mapema, na kuanza kupambana,
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwenyewe,

2. Nguvu ukiitumia, mali itakupatia,
Ila ukiihurumia, uvivu itakutia,
Uanze kujililia, na mwisho ukajifia,
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwenyewe.

3. Nguvu utafyatulia, tofali za kujengea,
Pia utazitumia, na mawe kusombelea,
Shamba utapalilia, mizigo utabebea,
Mtaji wa maskini, ni nguvu zake mwenyewe.

4. Kuni utajikatia, mkaa utachomea,
Usafi utafanyia, magari utaoshea,
Ulinzi utalindia, na pesa watakugea,
Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.

5. Nguvu utaitumia, kwa kazi za majumbani,
Na tena utatumia, kusomba taka sokoni
Mizigo ya abiria, utajitwisha kichwani,
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwenyewe.

6. Nguvu itazitumia, kufua nguo za watu,
Pia utazitumia, kung'arishia viatu,
Kaburi utachimbia, wanakozikiwa watu,
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwenyewe.

7. Vijana nawausia, tumieni nguvu zenu,
Mana Neno latwambia, nguvu ni fahari yenu,
Uzee ukiwadia, hazitakuwepo kwenu,
Mtaji wa maskini, ni nguvu zake mwenyewe.

8. Tumieni nguvu zenu, mjipatie ajira,
Acheni maringo yenu, mtajapata hasara,
Tambua fursa zenu, changamkia ajira,
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwenyewe.

9. Siku sita fanya kazi, Biblia inasema,
Si lazima za ujuzi, au zile za heshima,
Jamani kazi ni kazi, fanya acha kulalama,
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwnyewe.

10. Tamati natamatika, kalamu naweka chini,
Kazi unazozitaka, kama hazionekani,
Somba hata takataka, uwe na chakula ndani
Mtaji wa masikini, ni nguvu zake mwenyewe.

MUNGU NI MUNGU MMOJA, KATIKA NAFSI TATU.

1. Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu,
Hii ni muhimu hoja, haina utata katu,
Maelezo yanakuja, utajua kila kitu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

2. Kwa nini mwili mmoja, wanapooana watu,
Hilo halileti hoja, hoja ni kwenye watatu,
Hivyo hoja siyo moja, hoja ipo kwenye tatu
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

3. Ukiwa na ndizi moja, ukakata mara tatu,
Ndizi hiyo bado moja, au zimekuwa tatu?
Na kama bado ni moja, basi Mungu si watatu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

4. Na katika yai moja, wapata sehemu tatu,
Ute na ganda pamoja, na kiini ni cha tatu,
Hilo bado yai moja, siyo mayai matatu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

5. Hakuna nafsi moja, ipitayo hizo tatu,
Zote hufanya pamoja, hazifarakani katu,
Lifanywalo na mmoja, wafanya wote watatu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

6. Baba ni mtoa hoja, kuhusu wokovu wetu,
Aliyeruhusu kuja, Bwana na Mwokozi wetu,
Na ndiye atayekuja, kutupa urithi wetu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

7. Mwana ndiye alikuja, kulipa adhabu yetu,
Ndiye alikidhi haja, akawa kafara yetu,
Tukawa naye pamoja, akawa badala yetu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

8. Na Roho alipokuja, kunyosha tabia zetu,
Tukasikia faraja, ndani ya mioyo yetu,
Akaiamsha haja, ya kutubu dhambi zetu,
Mungu ni Mungu mmoja, katika nafsi tatu.

AMRI KUMI ZA MUNGU, ZIPO NA ZITAKUWEPO

1. Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo,
Zipo katika mawingu, na huko mbinguni zipo,
Ni tamu wala si chungu, zipo popote ulipo,
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.

2. Amri za Mungu zangu, na ni zako wewe hapo,
Zasonda tabia yangu, hunishika nitangapo,
Hiyo ndiyo dira yangu, isipokuwepo sipo,
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.

3. Amri ni taa yangu, yamulika niendapo,
Na tena mwalimu wangu, yanionyesha nilipo,
Zikiwemo ndani yangu, na dhambi pia haipo,
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.

4. Na hata Mwokozi wangu, amri azitajapo,
‘Amri hizo ni zangu’, alisema hapo hapo,
Hakusema za wazungu, ni zetu hadi ajapo,
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.

5. Amri hizo za Mungu, kwa hapo sasa zilipo,
Huwezi sema za Mungu, kwa sababu zipo zipo,
Kwani kama ni za Mungu, ya pili mbona haipo?
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.

6. Kinacholeta uchungu, ingawa ya nne ipo,
Imewekewa ukungu, sivyo ilivyokuwepo,
Eti kumwabudu Mungu, Sabato tena haipo?
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.


7. Ile ya kumi mwenzangu, utacheka usomapo,
Imegawanywa mafungu, ili kumi zitimupo,
Ile ilopigwa rungu, iweze fidiwa hapo,
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.


8. Amri Kumi za Mungu, ziache pale zilipo,
Sibadili ndugu yangu, usije pata kichapo,
Sifuate ya wazungu, kwamba amri hazipo,
Amri Kumi za Mungu, zipo na zitakuwepo.