Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

YAWAPASAYO WANANDOA

Ndoa ni makubaliano ya kimkataba ya kuishi pamoja; yanayofanywa kati ya mwanaume (ambaye katika mkataba huu hutambulika kama mume) dhidi ya mwanamke (ambaye katika mkataba huu hutambulika kama mke) wanaokubaliana kuishi pamoja hadi mauti itakapowatenganisha. Makubaliano haya ni ya kudumu yanayozuia kuachana na ndiyo maana yakaitwa pingu za maisha. Kuoana kunapitia mchakato wa kuacha, kuambatana, na kuwa mwili mmoja; mchakato unaoendelea katika kipindi chote wanandoa hao watakapokuwa pamoja. (Mwanzo 2:24) “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Hatua hizi tatu ni za muhimu ili ndo iwe vile Mungu alivyoikusudia kuwa. Wanaoachwa wakati wa kupitia mchakato huo ni wazazi, ndugu wengine wa karibu, na marafiki. Kuacha kunahusu pia kuacha mazoea mengine yanayoweza kumuudhi mwenzi wa maisha na hivyo kuathiri uhusiano unaoanzishwa.

Kuacha kunakusudia kupisha mahusiano mapya

Kuacha hapa kunakusudia kupunguza ukaribu na watu wengine unaoweza kuhafifisha mahusiano mapya ya ndoa yanayoanzishwa. Kuacha, kuambatana, na kuwa mwili mmoja kunaenda kinyume na mazoea ya dhambi na ubinafsi ambayo mwanadamu amezoea kuyaishi. Kutokana na ukweli huo wanadamu wanapotaka kuanzisha maisha ya kudumu ya kuacha, kuambatana na kuwa mwili mmoja, hutakiwa kupeana viapo vitakavyowafunga kila mmoja kwa mwenzake.

Viapo vya ndoa

Wanandoa wanapounganishwa hutoa viapo vya ndoa. Kwenye viapo hivyo huahidiana kupendana, kufarijiana, kuheshimiana, kutunzana, na kutokuwa na mume, au mke mwingine katika kipindi watakachokuwa hai. Katika viapo hivyo kila mwanandoa huahidi kumtendea mema mwenzake hata kama mzingira yatabadilika. Viapo hivyo vinapoheshimiwa mchakato wa kuacha, kuambatana na kuwa mwili mmoja hufanyika kwa ufanisi mkubwa na mahusiano hukua kwa kasi inayotarajiwa. Viapo huwatayarisha wanandoa kuanza maisha mapya ambayo hawajawahi kuyaishi hapo kabla. (Zaburi 45:10) “Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.” 

Wakati wa kufunga ndoa mchungaji humuuliza Bwana arusi: “Je, unamkubali mwanamke huyu kuwa mke wako uliyemuoa kihalali, na kuishi naye katika hali takatifu ya ndoa kama ilivyoamriwa na Mungu? Je, utampenda, na kumfariji, na kumheshimu, na kumtunza, katika ugonjwa na katika afya; na kuwaacha wengine wote, ukidumu na yeye tu siku zote mtakazoishi?” Kama Bwana arusi anamkubali atajibu: “Ndiyo, namkubali.”

Kisha mchungaji humuuliza Bibi arusi: “Je, unamkubali mwanamume huyu kuwa mume wako aliyekuoa kihalali, na kuishi naye katika hali takatifu ya ndoa kama ilivyoamriwa na Mungu? Je, utampenda, na kumfariji, na kumheshimu, na kumtunza, katika ugonjwa na katika afya; na kuwaacha wengine wote, ukidumu na yeye tu siku zote mtakazoishi?” Kama Bibi arusi anamkubali atajibu: “Ndiyo, namkubali.”

Ndipo Bwana arusi atamshika mkono yule bibi arusi nao watafuatisha maneno yanayosemwa na mchungaji kama ifuatavyo: “Nawasihi watu wote waliopo hapa, washuhudie kwamba mimi (majina yote—fulani fulani bini fulani) nakutwaa wewe (majina yote—fulani binti fulani) uwe mke wangu halali wa ndoa; niwe nawe na kuambatana nawe tangu sasa hata siku zote, katika hali njema na katika hali mbaya, latika utajiri na katika umaskini, katika ugonjwa na katika afya, nikupende na kukutunza, mpaka mauti itakapotutenganisha kulingana na amri takatifu ya Mungu; na katika mambo hayo nakupa ahadi yangu.”

Ndipo Bibi arusi naye atafuatisha maneno yanayosemwa na mchungaji kama ifuatavyo: “Nawasihi watu wote waliopo hapa, washuhudie kwamba mimi (majina yote—fulani fulani bini fulani) nakutwaa wewe (majina yote—fulani binti fulani) uwe mume wangu halali wa ndoa; niwe nawe na kuambatana nawe tangu sasa hata siku zote, katika hali njema na katika hali mbaya, latika utajiri na katika umaskini, katika ugonjwa na katika afya, nikupende na kukutunza, mpaka mauti itakapotutenganisha kulingana na amri takatifu ya Mungu; na katika mambo hayo nakupa ahadi yangu.”

Matarajio ya taasisi inayojitosheleza

Ndoa inakusudia kuunda taasisi imara inayokuza upendo wa Mungu kwa wanafamilia, taasisi imara ya kiuchumi inayojitosheleza kwa mahitaji, na kituo kikuu cha uinjilisti na uongoaji wa roho. Watu wanaoitembelea familia iliyokidhi vigezo hivyo vitatu hutarajia kushuhudia upendo uliotamalaki unaoifanya familia hiyo ionekane kama mbingu ndogo na mahali pa kutamanika kuishi. Hutarajia kushuhudia kuwepo kwa mgawanyo wa majukumu na ushirikiano katika utendaji unaochochea ukuaji wa kiuchumi na maendeleo. Hutarajia kushuhudia pia maisha yanayomwakilisha Mungu kwa njia ya ukarimu, ibada, ushuhudiaji, na viwango vya juu vya kujitoa katika kuitegemeza kazi ya Mungu.

Nyumbani kwa Ibrahimu ni mfano mzuri wa taasisi ya ndoa iliyojikita katika ibada, shughuli za kiuchumi na uinjilisti.  (Mwanzo 13:1-6) “Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai; napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la Bwana hapo. Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.”

Ibrahimu alitambua kuwa msingi wa familia imara ni kumfanya Mungu kuwa wa kwanza kwa kila jambo. (Kumb. 6:5-9) “Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.” Kumtegemea Mungu kwa dhati huwawezesha wanafamilia kuyafikia makusudi hayo makuu matatu ya ndoa kwa mafanikio makubwa.

Kiongozi wa familia

Mungu amekusudia mume awe kiongozi au kichwa cha familia. (Waefeso 5:23) “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.” Ili mume amudu majukumu ya kuwa kichwa cha nyumba na kuwa Mwokozi wa mwili (nyumba), anapaswa kumtambua na kumtegemea aliyemweka kwenye nafasi hiyo na aliye juu yake kwa madaraka. (1 Wakorintho 11:3) “Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.” Mume hawezi kufanikiwa kutekeleza majukumu na viapo vyake vya ndoa, bila kutegemea msaada kutoka kwa Kristo anayemwakilisha. Akijenga mahusiano ya karibu na Yesu atajua kujishusha na kuwatendea mema watu wa nyumbani mwake na hasa mke wake. (Mithali 3:27) “Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.”

Mume aliye kichwa cha nyumba humpigania mkewe kwa gharama yeyote wala haitarajiwi mume amfanye mkewe kuwa chanzo cha mapato yake au mlinzi wake anapohisi kukabiliwa na hatari. Wala haitarajiwi mume amshambulie mke kwa matusi na vichapo. Vijana wa kiume wa kizazi hiki wameonekana kukumbwa na hatari hii ya utegemezi kwa wake zao na kushindwa kuishughulisha akili katika kutafuta kutatua changamoto za maisha hasa za kiuchumi. Ibrahimu alipoteza sifa hii muhimu ya mume aliye kichwa cha nyumba alipoomba mkewe Sara amkingie kifua pale atakapomtambulisha kama dada yake na si mke wake halisi huku akihofia kuuawa. (Mwanzo 26:7) “Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso.” Kuwa kichwa cha nyumb ani pamoja na kumlinda mkeo.

Waume wasilewe Madaraka

Madaraka yana tabia ya kulewesha. Mtu anayepewa Madaraka na Mungu ni lazima ajue miiko na mipaka ya madaraka hayo na kuepuka kuyatumia vibaya kwa kukandamiza wengine au kwa kujinufaisha. Mume anatarajiwa kuwa daraja la watu wa nyumba yake kuvuka na kufikia magoli na ndoto zao za maisha kwa mafanikio. Ni lazima ajue mahitaji ya watu wake na kuona namna bora ya kukidhi mahitaji hayo. (Mwanzo 33:13-14) “Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng'ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote. Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri.” Kuwa kichwa cha nyumba ni pamoja na kuwalinda watoto na wote ‘walio wadogo’ walio chini ya himaya yake. (Mathayo 25:40) “Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.

Ndoa ya watu wa jinsia moja

Haukuwa mpango wa Mungu wanandoa wawe wa jinsia moja. (Kumb. 23:17 “Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.” Hawa ambao Biblia inawataja hapa kama mahanithi kwa lugha ya kiingereza wameitwa” Sodomites” ikimaanisha mashoga. Ndoa za watu wa jinsia moja zimekatazwa na Maandiko Matakatifu kwa kuwa si mpango wa Mungu na zinatokana na wanadamu kuwakiana tamaa na si kweli kuwa ni udhaifu ambao watu wengine wanapaswa kuutambua na kuukubali. (Warumi 1: 26-27) “Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.” Hivyo ndoa ni ya wawili wa jinsia mbili tofauti mwanaume akiitwa mume na mwanamke akiitwa mke.

Ushauri mwema wa wanawake

Mwanamke anafaa zaidi kuwa mke kuliko mwanaume kwa kuwa ushauri wake unamfaa zaidi mume kuliko ule wa mwanaume mwenzake. Mungu amekusudia mke awe mshauri mkuu wa mume, akimsaidia kutimiza majukumu yake ya kuisimamia nyumba. (Mithali 31:26) “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.” Nyuma ya waume waliofanikiwa kwa kawaida huwapo mke anayeshiriki kikamilifu katika kutimiza majukumu yake ya kushauri. (2 Wafalme 4:9-10) “Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.” Wanaume wanaopuuza ushauri wa wake zao kwa sababu umetolewa na mwanamke wana hatari ya kupewa ushauri unaopotosha kutoka kwa wazazi na rafiki zao.

Mke mmoja anatosha.

Mungu anayemfahamu mwanaume vizuri na kile anachokihitaji, anatambua kuwa mwanaume anahitaji mke mmoja na si zaidi ya hapo. Ndiyo maana hapo mwanzo uhitaji wa mwanamke ulipojitokeza Mungu alimpatia Adamu msaidizi mmoja na si zaidi ya hapo. (Mwanzo 2:18) “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” Mungu anajua pia kuwa mke anahitaji kuwa na mume aliye wake peke yake na si mume wanayeshirikiana kummiliki wanawake wengi. (1 Wakorintho 7:2) “Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.”

Ndoa ni ya wawili

Ndoa ilikusudiwa iwe ya watu wawili; yaani mume na mke, ambapo mume angetokana na jinsia ya kiume na mke angetokana na jinsia ya kike. (Mathayo 19:4-5) “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?” Ndoa ya watu zaidi ya mmoja ni mavumbuzi tu ya wanadamu lakini haikutokana na mpango wa Mungu. Mtu wa kwanza kwenye Biblia kuwa na wake wengi ni Lameki. (Mwanzo 4:19) “Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.” Lugha ya kujitwalia iliyotumika inaashiria yalikuwa maamuzi yake yaliyosukumwa na tamaa.

Wake wengi na changamoto za kuwatosheleza

Mume mwenye kuoa wake wengi hushindwa kugawa upendo kwa wake zake katika kiwango kinacholingana na hivyo kuibua malalamiko kwa mke au wake wanaohisi kunyimwa upendo. (Mwanzo 29:30) “Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine.” Wanawake walioolewa kwa mume mmoja huwa na magomvi yasiyoisha yanayoweza kusababisha migogoro ya ndoa na hata kupelekea kumchanganya mume. (Mwanzo 16:5-6) “Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. Bwana na ahukumu kati ya mimi na wewe. Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake.”

Wake wengi walimgeuza mwenye hekima

Wake wengi wana kawaida ya kumuelemea mume katika kufanya maamuzi na hivyo kumgeuza kutoka kwenye msimamo aliokuwa nao awali. (1 Wafalme 11:3) “Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.” Kama mwenye hekima aliweza kugeuzwa moyo nitakuwa vipi wanaume wa kawaida watakapooa wake wengi? Wake wengi wana kawaida ya kumtoa mtu kwenye mahusiano na Mungu wake. (1 Wafalme 11:4) “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”

 

 

Migogoro ya watoto wa mama tofauti

Tatizo jingine la kuwa na wake wengi ni migogoro ya urithi inayozuka kwa watoto waliozaliwa kwa mama tofauti. (Waamuzi 11:1-2) “Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine.”

Mume asiitelekeze familia yake

Wanaume hudhani wana wajibu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto za watu wote wanaofahamiana nao wanaohitaji msaada hapa duniani. Mume asijihisi kuwajibika zaidi kuongoza familia aliyozaliwa nayo au ukoo wake au hata taasisi ya kidini anayoisimamia, au watu wanaomzunguka, na kusahau wajibu uliowekwa mabegani mwake wa kuisimamia familia yake. (1 Timotheo 5:8) “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” Wajibu wake katika familiya ya kwao na ukoo havipaswi kumuondoa kwenye wajibu wake wa msingi kwa familia hata kama yeye ni mtoto wa kwanza wa familia hiyo au anayetegemewa sana katika ukoo. Hapaswi kuyaacha madaraka ya kuongoza nyumba kwa wazazi wake au mlezi wake hata kama mzazi au mlezi huyo ni wa kiroho sana au amehusika katika kumfikisha kwenye kiwango cha mafanikio aliyonayo.

Wazazi wawaachie watoto wao wa kiume

Wazazi wawaachie watoto wao wa kiume kusimamia mambo ya familia zao wenyewe baada ya kuoa wakitambua kuwa watoto hao sasa wamekua na wanahitaji kukuza uwezo wa kupambanua jema na baya na kufanya maamuzi ya kusimamia nyumba zao. Wasijisikie kuendelea kuwajibika kwa makosa ya (Yohana 9:19-21) “Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa? Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.”

Wazazi wawaachie uhuru mabinti zao walioolewa

Hata binti aliyeolewa asiingiliwe katika maamuzi yake. Apewe uhuru wa kujiamulia mambo yanayomhusu yeye na mume wake. (Mwanzo 24:54-59) “Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. Ndugu yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende. Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi Bwana amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda. Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake.”

Wazazi wasiwatelekeze watoto walio kwenye ndoa changa

Wazazi, walezi, na rafiki wanayo nafasi ya kushauri kutokana na uzoefu walio nao kwenye ndoa lakini hawapaswi kushinikiza ili ushauri wao utekelezwe. Mashauri hayo yapitie kwenye vikao vya mashauriano vya mume na mke kwa ajili ya kuchambuliwa, kujadiliwa, na kutolewa maamuzi. Ushauri usipozingatia vipaumbele vyenu na kwenda kinyume na utaratibu wenu mtautupilia mbali na kuendelea na mipango mliyojiwekea. Ni makosa kuwa na mipango ya kifamilia isiyomhusisha mume au mke. Tena ni makosa kwa mmoja wa wanandoa kutoa msaada mkubwa kwa walio nje ya familia bila mwenzi wake kushirikishwa au kujulishwa.

Mume ana wajibu wa kuitunza familia yake

Ili mume awe kichwa hasa cha nyumba anapaswa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa chakula, mavazi na mahitaji mengine ya muhimu kwa mkewe na kwa familia nzima. (Waefeso 5:28-29) “Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.” Mume anapaswa kuwa mpambanaji anayeilisha familia yake. Asiyetangulia kukidhi mahitaji yake akiyasahau ya watu wake. Furaha yake daima iwe ni kuwaona watu wa nyumbani mwake wakionea fahari kuwepo kwenye familia anayoiongoza. Kudhulumu jasho la mke au watoto kwa kutowashirikisha matumizi ya mapato ya familia ni chanzo kikuu cha mifarakano katika ndoa na chanzo pia cha kuporomoka kiuchumi kwa familia. (Mithali 31:30-31) “Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa. Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.”

Mke anayependwa humsaidia mumewe kukidhi mahitaji ya nyumbani

Mke anayependwa kwa dhati amwonapo mumewe akihangaika kuipatia familia na yeye mwenyewe mahitaji yao ya msingi hamwachi akihangaika peke yake bali hujiunga naye katika kuipambania familia. (Mithali 31:19-25) “Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia. Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake. Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu. Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani. Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi. Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi. Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao.”

Mungu humchagulia mtu mwenzi kulingana na mahitaji

Kazi ya kuchagua mwenzi wa maisha hufanywa na Mungu mwenyewe kwa kuwa hakuna anayeweza kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa zaidi yake. (Mwanzo 2:18, 21-23) “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”  Hii ni kwa sababu Mungu anamfahamu kila mtu alivyo na atakavyokuwa siku za usoni na ni nani anayeweza kuendana naye kama wakiishi pamoja. (Yeremia 1:5) “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.” Kwa kawaida Mungu huwaleta pamoja watu wanaoweza kutembea kwa masikilizano katika safari ya maisha. (Amosi 3:3) “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?” Mungu hawezi kuwaleta kuishi pamoja watu waliofaraka maana ndoa ni kwa ajili ya waliopatana.    (Zaburi 133:1) “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.”

Hakuna mwanandoa aliyekamilika

Kila mwanamke aliyezaliwa ili aolewe huzaliwa duniani akiwa amekamilika katika kukidhi mahitaji na mapungufu ya mumewe mtarajiwa lakini akiwa hajakamilika katika kila kitu. Hali ni hiyo hiyo pia kwa mwanaume. Mwanamke au mwanaume huletwa na Mungu kwenye ndoa kwa kusudi la kukidhi yaliyopungua kwa mwenzake. Mungu alitambua kuwa Abigaili atakidhi mapungufu ya mumewe Nabali. Kwa upande mwingine Nabali alikuwa na utajiri ili pengine kukidhi upungufu wa utajiri wa Abigaili. Hata hivyo Nabali alikuwa tajiri, asiye na adabu kwa watu, na Abigaili mkewe alikuwa mwenye akili njema na mzuri wa uso kama Maandiko yasemavyo. (1 Samweli 25:2-3) “Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.” Hawa waliweza kuchukuliana mapungufu yao hadi mmoja wao aliposhikwa na umauti.

Urithi wa kwanza kutoka kwa Mungu

Mke na mume ni urithi uliotukuka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mungu anaweza asikupe mali lakini akakupa mke au mume mwenye busara atakayekuwa mbaraka kwa Maisha yako. (Mithali 19:14) “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Kila mwanaume na mwanamke ana jambo fulani ambalo Mungu amewekeza kwake ambalo likitumika vyema huwa mbaraka kwa mwenzie na jamii inayowazunguka. Adamu alithibitisha kuwa alikuwa mume mwenye busara kwa kukamilisha kazi ya kwanza aliyopewa na Mungu kwa ufanisi mkubwa. (Mwanzo 2:20) “Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye.” Je, unadhani maisha yako yamegusa maisha ya watu wengine kwa kiasi gani?  Je, unadhani umetimiza kwa kiwango gani kusudi la Mungu la kukuweka mahali ulipo? Adamu alipewa kazi ya kuwapa majina viumbe ambao Mungu alikuwa hajawapa majina. Lakini yeye akajiongeza hadi kutoa jina hadi kwa kiumbe ambaye Mungu alishampa jina tayari.  (Mwanzo 2:21-23) “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” Unadhani mke au mume uliye naye amekuongezea thamani yako kiasi gani? Kama ungeambiwa umpatia jina linalofanana na thamani aliyoongeza kwenye Maisha yako ungempa jina gani? Ungetumia lugha ya Adamu au ya Sulemani? (Mithali 31: 29) “Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.”

Mchakato wa kuhitaji mwenzi utokane na msukumo wa ndani

Mchakato wa kumpata mwenzi wa Maisha huanza na kukamilika pale mwenye uhitaji akiwa hatambui kinachotokea. (Mwanzo 2:21-22) “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.” Mungu humleta mwenzi aliyekuandalia ukiwa usingizini. Akili zako zina mchango mdogo sana katika jambo hili nyeti. Wakati ukiwa unaomba na kufunga huku moyo ukikusukuma kuangalia kila kona ndipo Mungu hukuletea yule uliyemngoja sana.

Mwenzi huja ili kutosheleza yaliyopungua

Mwenzi wa maisha huja akiwa amebeba yale yaliyopungua kwa mwenzi mtarajiwa. (Yeremia 31:22) “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.” Kumlinda hapa imetumika kukidhi yale yaliyopungua kwa mwanaume. Kuna tofauti kubwa kati ya mwanaume na mwanamke katika utendaji wao. Mwanamke ana uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja bila kutingwa tofauti na mwanaume. Mwanamke ana uwezo wa kukumbuka mambo madogo madogo yaliyo ya muhimu kuliko mwanaume na wakati huo huo mwanamke huendeshwa na hisia zaidi kuliko kanuni.

Fanya bidii kujua tabia za watu wako

Mojawapo ya jukumu la muhimu la wanandoa wanaoishi pamoja ni kufahamiana tabia. Mtu yeyote unapomfahamu tabia huwa ni rahisi kuishi naye. Kwa kawaida tabia za wanadamu zimetofautiana. Zipo zile zinazoweza kurekebishika kirahisi na zile ambazo kurekebishika kwake huchukua muda mrefu au hushindikana. Mfano, tabia ya kucheka kwa sauti kubwa au kupiga miayo kila wakati, tabia ya kutafuna chakula kwa kutoa sauti na bila kufumba mdomo, tabia ya kupandisha makamasi, tabia ya kuweka vidole puani, tabia ya kuweka mikono nyuma au mifukoni unapoongea, tabia ya kukoroma unapolala, tabia ya kufikicha masikio kwa vidole na tabia nyingi nyingine kama hizo mtu huzaliwa nazo na hubadilika kwa shida sana.  

Chukuliana na tabia za watu

Njia ya kuepuka migongano isiyo ya lazima katika familia na katika jumuiya ya watu ni kuwajua sana watu hao na tabia zao. Mtu unayemjua alivyo hawezi kukusumbua.  (Mithali 27:23) “Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe zako.” Unatakiwa uwajue hao watu kwa kuwa kwa namna fulani Mungu amekupatia uwaongoze, kama mchungaji alivyopatiwa mifugo aisimamie na kuiongoza salama. Kuchukuliana mizigo ni kutambua udhaifu wa mwenzako na kuwa tayari kuuvumilia. (Wagalatia 6:2) “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.” Yesu aliweza kuwasamehe watesi wake kwa sababu aliwafahamu asili yao na kinachowaongoza kutenda kile walichokuwa wanatenda. (Luka 23:34) “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.”

Tabia nne za wanadamu

Tabia nyingine ya kupenda kutawala na kuwatumia wengine, au tabia ya kuongea sana hata kukosa usiri, au tabia ya kuwa na misimamo isiyotaka kubadilika, au tabia ya unyamazifu uliovuka mipaka ni tabia pia zilizo ngumu kubadilika na ambazo kwa namna fulani watu wamezaliwa nazo. Wataalamu wamezigawanya tabia za wanadamu katika makundi makuu manne. Kundi la Koleriki, kundi la Melankoli, kundi la Sanguini, na kundi la Flagmatiki.

Koleriki

Koleriki wanapenda watu wa kundi lao zaidi wenye ujasiri, kusimamia kazi, kujitoa mhanga, kufanya kazi kupita kiasi, na kuthamini kazi kuliko watu, na watu wenye hasira za haraka. Hawa ni viongozi wenye njozi. Wakidhamiria kufanya jambo lazima watatimiza hata kama ni kwa njia ya kuumiza watu. Hawa ni mabingwa wa kutatua matatizo lakini ni watu wanaopenda sifa pia.

Melankole

Melankoli wanapenda kufanya mambo kwa kufuata utaratibu waliojiwekea na hupendelea kuweka sheria na kuzisimamia, ni watunzaji wazuri wa kumbukumbu, na si wepesi wa kupokea mabadiliko, na wana asili ya kupenda usafi. Ni wabunifu, wazuri katika kuweka mipango ya baadaye, wabunifu, na watu wanaofikiri sana.

Sanguini

Sanguini ni wepesi kufanya maamuzi bila kufikiria matokeo. Hutoa ahadi wasizo na uwezo wa kuzitimiza. Wanajua kuchangamsha, wepesi kulia na wepesi kucheka na hupenda kucheka kwa sauti ya juu. Wepesi kusamehe na kusahau hawatunzi mambo moyoni. Wanazoeana na watu kirahisi. Wanashughulika zao na sasa kuliko kesho. Wanajua kuwahamasisha wengine lakini wanakata tamaa kirahisi. Wanapenda kushindana na michezo na ni wasimuliaji wazuri wa visa.

Flagmatiki

Flagmatiki ni wakimya na wapenda amani. Ni wasikilizaji wazuri na wapatanishi. Wavumilivu wa usumbufu wanaofanyiwa na wenzao ila wakichoka kuvumilia hawana kurudi nyuma. Huchelewa kufanya maamuzi na hupendelea kuficha hisia zao za ndani

Kumpenda mtu wa jinsia tofauti

Mungu aliasisi ndoa ili kiwe chuo kidogo cha kujifunza tabia yake ya upendo. Hapa Mungu aliwaweka watu wawili wa jinsia tofauti ili wajifunze kusomana na kupendana huku wakiendelea kuakisi tabia yake ya upendo wa Agape. Kwenye ndoa ndipo mahali watu hukosana mara nyingi na kusameheana mara nyingi pia. Katika kukosana na kusameheana huko ndipo upendo kati yao unapoimarika. Ndoa ya mwanaume na mwanamke ni kivuli cha ndoa baina ya Kristo na kanisa lake; mume akimwakilisha Kristo na mwanamke akiliwakilisha kanisa. (2 Wakorintho 11:2) “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” Kwenye ndoa ndiko ambako Kristo humletea mwanamke bikira (yaani asiye na mume mwingine) mume mmoja wa kuolewa naye. Mwanamke anayekwenda kwa mwanamke mwenzie ili aolewe naye au mwanaume anayekwenda kwa mwanaume mwenzie ili aolewe naye hajafuata mpango wa Mungu wa ndoa. 

Ndoa chuo cha mafunzo

Ndoa inakuwa chuo cha kujifunza kupendana kwa kuwa mume anatoa huduma ya kumpenda na kumheshimu mkewe na mke anatoa huduma ya kumstahi na kumtii mumewe. (Waefeso 5:33) “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.” (1 Petro 3:7) “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” Mume hampendi na kumheshimu mkewe kwa sababu kuna kitu anachotarajia kupokea kutoka kwake wala mke hamtii na kumstahi mumewe kwa sababu kuna kitu anachotaraji kulipwa na mumewe. Wajibu huu unafanyika kwa sababu kuna agano la kutendeana wema waliloagizwa na Mungu. (1 Yohana 4:11) “Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.” (1 Wathesalonike 4:9) “Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.” Upendo ambao Mungu amewafundisha wanandoa kupendana ni upendo wa hisia na upendo wa kanuni. 

Upendo wa hisia inaowakilisha hisia

Upendo wa kanuni una tabia ya kudumu na kustahimili kuliko upendo wa hisia. Katika hatua ya awali Adamu alipoletewa Hawa alimpenda kwa upendo wa hisia kutokana na mwonekano wake na namna alivyomuondolea upweke. Lakini upendo huo uliyumba na kupoteza nguvu yake mwanamke huyo alipotenda dhambi hata kudiriki kumshitaki na kumkana mkewe mbele ya Mungu. (Mwanzo 3:12) “Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Huyu ni mke yule yule aliyemfanyia tambo siku alipoletewa na Mungu akidai ni nyama katika nyama zake na mifupa katika mifupa yake.

Upendo wa hisia hutegemea thamani ya anayependwa

Upendo wa hisia ni upendo unaomthamini mtu anapobaki na thamani ile ile ya awali iliyofanya apendwe. Kilichowasaidia kuendelea kuishi pamoja bila kuachana baada ya hayo kutokea ni upendo wa kanuni ule ule unaomfanya Yesu aendelee kutupenda sisi wanadamu hata baada ya kuwa tumemkosea. (Warumi 5:8) “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” Upendo wa hisia ni wa muhimu maana unafurahia yale mazuri aliyonayo mwenzako bila hofu au kuona aibu. Ni upendo unaoonyesha hisia za ndani ambazo mwenzako anahitaji kuzishuhudia kutoka kwako. (Mithali 3:27) “Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.” Hata Mungu anahitaji kuonyeshwa upendo huu wa hisia. (Zaburi 18:1) “Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana.” (Malaki 1:6) “Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani?”

Upendo wa Agape udumuo

Aina ya upendo ambao Mungu anatupenda unazidi ule upendo wa hisia. Mungu anatupenda kwa upendo wa kanuni uitwao Agape. Upendo huu hauchuji wala kukoma hata pale hali ya mambo inapobadilika na kuwa isiyofaa. (Warumi 8:35, 38-39) “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Upendo huu hautafuti mambo yake wenyewe, wala kutafuta kujinufaisha kutoka mazuri aliyonayo unayempenda. (1 Wakorintho 13:4-5) “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; Upendo huu hutafuta kunufaisha wengine kwa hasara yake.”

Upendo utokao juu huongeza thamani

Anayependa kwa upendo wa kimbingu yaani wa agape hafanyi hivyo kwa matarajio ya kupokea kitu kutoka kwa mwenzie bali hufanya hivyo ili kumuongezea thamani aliyeagizwa kumpenda. Upendo wa wanandoa unafanana na upendo wa Ruthu kwa mama mkwe wake ambaye alikuwa mtu wa kabila jingine na ambaye hakutarajia kunufaika naye kwa lolote kwa kuwa alikuwa maskini na asiye na mtoto wa kiume ambaye angetarajia kuolewa naye. (Ruthu 1:16-17) “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.”

Maagano katika viapo vya ndoa

Viapo wanavyopeana wanandoa siku ya ndoa vinapima na kuthibisha kama wanapendana. Wanandoa wasiopendana kwa dhati ndoa yao si halali na kudumu kwake ni kwa mashaka. Kupenda ni kujitolea kutumikia furaha ya mwingine kwa hiyari na bila manung'uniko. Ni kuwa tayari kumpenda, kumheshimu, kumfariji, na kumtunza mtu mmoja zaidi ya wengine wote na kubaki na huyo tu siku zote za uhai wako.  Kupenda kwa namna hii kunatokana na wito ambao mtu huupokea kutoka kwa Mungu ambao atapaswa kuutolea hesabu siku ya mwisho. Unapompenda mtu huoni gharama kutumika kwa ajili yake wala huwezi kuhesabu mabaya anayokutendea. Pamoja na kuwa unayempenda lazima awe anakuvutia, bado sababu ya kumpenda inavuka mvuto wake. (Mwanzo 29:20) “Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda.”

Majukumu ya ndoa yanahitaji karama

Kuoa au kuolewa kunahitaji wito, karama na majaliwa ya Mungu kwa sababu ya yale mazito ambayo kila mwanandoa anatakiwa kumtendea mwenzake. Wapo binadamu wanaosikia msukumo wa kuoa na kuolewa na wapo wale wasio na msukumo huo kwa kadri walivyojaliwa na Mungu. (1 Wakorintho 7:7-8) “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.” Mwanadamu hawezi kuyatimiza kwa ufanisi na kwa ukamilifu yale yanayohitajika katika ndoa kama ambavyo hawezi kumudu kuishi bila kuoa na kuolewa asipokuwa amejaliwa na Mungu. Ni lazima awe na karama iliyowekwa na Mungu ndani yake. (Mathayo 19:10-11) “Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.” Katika ndoa, mume anatakiwa kumpenda mke kwa upendo ambao Kristo alilipenda kanisa. Kristo alilipenda kanisa kwa upendo unaoongeza thamani siyo ule unaovutiwa na thamani. (Waefeso 5:25-27) “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.”

Shabaha ya mume kwa mkewe

Lengo la Kristo la kulipenda kanisa (mimi na wewe) ni kuondosha mapungufu yanayotufanya tusifikie ubora ambao Mungu aliukusudia tuwe nao. (Waefeso 2:10) “Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.” Shabaha ya mume ya wakati wote ni kuona makunyanzi, ila, na mawaa yote katika tabia ya mkewe yanaondoka kwa msaada wa upendo atakaouonyesha kwake. Baada ya jitihada zake hizo zinazoshirikisha upendo wa Mungu wa agape, mume anatarajia kumuona mkewe akiwa amesafishika na kutakasika kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kwa maombi, na kwa msaada wa Neno la Mungu na amefikia hatua inayomletea Mungu utukufu. Mume hampendi mkewe kwa sababu ya uzuri wake pekee, bali hufanya hivyo kwa kutii agizo la Mungu la kumpenda asiyependeka, asiye na shukrani, na asiyekamilika ambaye Mungu amempa kwa lengo la kumsaidia kuondokana na mapungufu hayo.

Kupenda na kutii ni agizo la Mungu

Mke anatakiwa kumtii mumewe kwa utii ambao kanisa humtii Kristo. (Waefeso 5:22) “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.” Kanisa humtii Kristo kwa kuwa halina mwingine liliyeahidi kumtii kuliko Yeye. Mke humtii mume kwa kuwa halina mpango wa kumtii mwingine ambaye hajajitoa mhanga kwa ajili yake kama mume aliyenaye. Utii wa kweli unatokana na kumwamini yule unayemtii. Mume awe my anayeaminika katika kauli na matendo yake ili kumjengea mkewe mazingira ya kumwamini na kumtii. (Matendo 7:37-39) “Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye. Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi. Mtu huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao wakarejea Misri.”

Kumtii mume kama kumtii Bwana

Mungu anawataka wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana. (Waefeso 5:22) “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.” Kumtii mume kama kumtii Kristo kuna maana ya kutokuwa na mtu mwingine unayefikiria kumsikiliza zaidi ya mumeo. Ni kuyatoa kabisa maisha yako chini ya usimamizi wa mtu unayemuamini sana kuwa hatakusaliti wala kukutelekeza. Mke aliyemshiba mumewe na kujitoa kabisa kwake atasema kama walivyosema wanafunzi wa Yesu wakati baadhi ya wafuasi wake walipomkataa. (Yohana 6:66-68) “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena. Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.”

Sara mfano wa wanawake watiifu

Sara ni mfano wa wanawake waliowatii waume zao kama kumtii Bwana. (1 Petro 3:6) “Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote.” Hii haimaanishi kumfanya mume kuwa Mungu bali kumpa heshima ya juu kuliko apewayo mtu yeyote katika familia kwa kuwa yeye anamwakilisha Mungu katika familia. Hatuoni mahali popote Sara aliposhindana na mumewe. Alipomwambia waondoke nyumbani kwa waende kule Mungu atakapomwonyesha alitii bila maswali. (Waebrania 11:8) “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.” Alikuwa tayari kumsaidia mumewe kupata mtoto kwa njia ya mjakazi wao ili tu ahadi ya Mungu ya kumpatia Ibrahimu mtoto itimie (ingawa jambo hili halikuwa sahihi kwa Mungu). (Mwanzo 16:2) “Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai.”

Wanawake watii huwaamini waume zao

Kanisa hutii kila linaloagizwa na Kristo likiamini kuwa Yeye anayetoa agizo hilo ana nia njema na kanisa na ndiye atoaye uwezo wa kulitii agizo hilo. (Mwanzo 28:15) “Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” Mke huamini kuwa, mume wake hawezi kumwangusha au kumtelekeza baada ya jitihada alizofanya kwa ajili yake na ahadi alizotoa siku ya kuolewa kwake jambo linalombidisha kutii maagizo magumu kutoka kwa mume huyo. (2 Wakorintho 5:14) “Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote.”

Kumtii mume kwa kila jambo

Inahitaji karama na wito kumtii binadamu mwenzako kwa kila jambo au kwa kiwango unachomtii Mungu wa mbinguni hasa inapotokea huyo unayetakiwa kumtii ana mapungufu kama yako. (Waefeso 5:24) “Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.” Kumtii mume katika kila jambo ni agizo linalolenga kuepusha mtafaruku unaotokana na kumbishia mumeo mbele ya watu kwa kuwa unahisi ametoa maelekezo na maagizo yasiyofaa. Agizo lisilofaa kwa mke mwerevu hupokelewa kwa ajili ya utekelezaji lakini kabla halijatekelezwa mke huyo hutafuta nafasi nzuri ya faragha ya kumshauri mumewe asitishe agizo hilo kutokana na athari zake kiwa litatekelezwa. Mke mwenye busara atafanya ushawishi unaobainisha kasoro za agizo la mume ili zirekebishwe kabla ya utekelezaji. Mke anayefahamu uwezo wake wa kushauri hatasita kutii maagizo ya mumewe ili kumlindia heshima yake mbele ya watu akijua namna atakavyomshauri kuachana na wazo hilo potofu hapo baadaye. (Mithali 11:14) “Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.” (Mithali 2:6) “Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.”

Kutotii waume huchochea magomvi

Wanaume wengi wana kawaida ya kuhisi wamedharauliwa pale maagizo yao yanapopingwa vikali na wake zao mbele za watu. Hali hiyo huwafanya wengine hasa wale wenye silika ya kutotaka magomvi kutotoa maagizo mengine kwa kuhofia kuumbuliwa tena na wake zao. Kwa wale wenye silika ya kutotaka kushindwa hali hiyo huikabili kwa kuonyesha ukali na ubabe na wakati mwingine hata kuzusha ugomvi.  Mwanaume anayeamua kuwa mbogo au kutotoa maagizo kwa kuhofia ugomvi hushindwa kutimiza vyema majukumu yake kama mume. Na hiki ndicho Mungu anachokiepusha anaposhauri wake wawatii waume zao kwa kila jambo. (Mithali 15:18) “Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.”

Mke asiwe mtumwa wa mume

Lakini isidhaniwe kuwa utii wa mke kwa mumewe unalenga kumfanya mwanamke awe mtumwa kwa matakwa ya mumewe au apoteze uhuru wake. Mwanamke anayo thamani inayolingana na mwanaume kwa kuumbwa na kwa kukombolewa.  (1 Wakorintho 7:23) “Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu.” Biblia inasisitiza mwanamke ana nafasi sawa na mwanaume mbele ya Mungu. (Wagalatia 3:28) “Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.” Mwanamke aliumbwa kwa mfano wa Mungu kama ambavyo mwanaume pia aliumbwa kwa mfano wa Mungu. (Mwanzo 1:27) “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”

Ukomo wa mke kumtii mumewe

Biblia inaweka ukomo wa mwanamke kumtii mume. (Wakolosai 3:18) “Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.” Mke asikubali kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na mumewe. (Esta 1:10-12) “Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake.” Mke asikubali kutii maagizo yanayodhalilisha utu wake au yanayomuondolea utii wake kwa Mungu wake. asikubali kutii maagizo yanayomzuia Kwenda ibadani au kumtolea Mungu zaka na sadaka. Atumie ushawishi wake na si mabavu kumsihi na kumshawishi mumewe ili aruhusiwe kumwabudu Mungu wake.

 

Utii kwa mume asiyelijua Neno

Utii wa mke kwa mume asiyelijua Neno au asiyemtii Mungu ni dawa bora ya kulainisha moyo wa mume huyo na kubadilisha mtazamo wake. (1 Petro 3:1) “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno.” Kosa moja linalofanywa na wale walioolewa na waume wasiolijua Neno ni kuwalazimisha kubadili msimamo wao wa imani kinguvu badala ya kuwashawishi kupitia utii wao. Hakuna sababu ya kulazimisha kuachana na mume asiyelijua Neno kama anaridhika kukaa na mke anayeliamini Neno na anampa uhuru wa kuabudu. (1 Wakorintho 7:13) “Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.”

Majukumu ya mume katika ndoa

Kando ya upendo na utii unaowapasa wanandoa pia yapo majukumu yampasayo mume na mke. (Mwanzo 3:17-19) “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; [kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Katika laana hii panaonyeshwa pia majukumu ya mume na mke katika nyumba. Mume ana jukumu la msingi la kuilisha na kuivalisha familia yake. (Waefeso 5:28-29) “Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.” Kama ambavyo Kristo ana wajibu wa kulilisha na kulitunza kanisa lake ndivyo na mume alivyo na wajibu wa kuilisha na kuitunza familia yake. Kwa kuwa yeye ni kichwa cha nyumba ana wajibu wa kutafuta mahitaji ya watu wa nyumbani mwake akishirikiana na mkewe.

Majukumu ya mke katika ndoa

Mke ndiye hubeba ujauzito kwa miezi tisa na kujifungua kwa uchungu na mateso mengi. Pale kujifungua kwa kawaida kunapokosekana hulazimika kufanyiwa upasuaji ambao kwa wengine huishia katika kupoteza maisha yao au ya mtoto au ya wote wawili. (Mwanzo 3:16) “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Pamoja na jukumu la kuzaa, kuelimisha Watoto, kusimamia shughuli za nyumbani na kumshauri mumewe, mke analo jukumu la kuchangia mapato ya nyumbani. (Mwanzo 31:16) “Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.” Mke mwenye busara hatamwacha mumewe ahangaike peke yake katika kutafuta mahitaji ya nyumbani. Atajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali au utoaji huduma halali ili kuongeza kipato cha familia.

Msaidie mwenzako majukumu

Katika ndoa ya wanaopendana majukumu ya mume huweza kufanywa na mke na baadhi ya majukumu ya mke huweza kufanywa na mume. Mume aweza kufanya shughuli za upishi na usafi wa nyumbani au hata kubaki nyumbani na kulea watoto wakati mke akitimiza majukumu muhimu ya kuiingizia familia kipato. Hali kadhalika mke aweza kufanya wajibu unaomhusu mume baada ya kubaini uzembe wa mumewe au baada ya kubaini kuwa ameelemewa. Kuendeleza mashindano au kukomoana hakuwezi kuisaidia familia bali kutaididimiza. Betisheba alijibebesha majukumu ya mumewe mzembe na kumkabili mfalme Daudi kwa ujasiri na kwa hekima ya kimbingu ili kuinusuru familia. (1 Samweli 25:23-25) “Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.”

Kuambatana kunakomaza upendo

Biblia inashauri wanandoa kuambatana pamoja daima kila inapowezekana kila mmoja akihudumia furaha ya mwenzake. (Zaburi 133:1) “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” Usiridhike kutembea bila mwenzako, kula bila mwenzako, au kulala bila mwenzako. Mume na mke wanatakiwa kuishi kama watoto mapacha wakichekeshana, wakipeana michapo, na hata kutaniana, huku wakijikumbushia michezo yao ya utotoni ya kutekenyana, kukimbizana na hata kubusiana. Isaka na Rebeka licha ya nafasi yao kubwa katika taifa la Israeli walikuwa wanapata muda wa kufanya hayo. (Mwanzo 26:8) “Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe.” Msiruhusu Watoto, ndugu na rafiki wapunguze ukaribu wenu. Kaeni pamoja mkiwa kanisani, kwenye usafiri wa umma, na kwenye matukio ambayo mmealikwa.

Kusifiana hukuza upendo

Wajibu mwingine wa mume mwenye busara ni kusifu uzuri wa mkewe na kumpa majina yanayobeba sifa hizo kwa lengo la kukuza upendo. Usione aibu kumwita mkeo majina yanayobeba uzuri wake kama baby, au honey, au Sweetheart, au barafu ya moyo, au nyongo mkalia maini. Wanawake kwa asili wanapenda kusifiwa. (Wimbo Ulio Bora 1:15) “Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua.” Kwa kuwa mume ni kichwa cha nyumba yafaa apewe sifa zinazomstahili kwa makuu anayowatendea watu wa nyumbani mwake. (Zaburi 147:1) “Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.” Msifie mumeo au mkeo mbele ya watu wa nyumbani mwako hata mbele ya wakwe na mawifi ukielezea mazuri anayokutendea. Katika wakati wenu wa faragha na hata mbele ya watu mara kadhaa msifie mwenzio ili mwenzako atambue thamani yake na kupata hamasa ya kufanya vizuri zaidi. Hakikisha sifa zako zinakuwa za kweli ambazo hazina unafiki ndani yake na zisizo na lengo la kurahisisha upatikanaji wa kitu unachokihitaji kutoka kwake. Mtambulishe kwa marafiki kwa fahari kubwa ukimuita yale majina yenu mnayoitana mkiwa nyumbani.

Sifa za Sulemani

Sulemani alikuwa na namna ya kumsifu mke wake. (Wimbo Ulio Bora 4:1-5) “Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua, Nyuma ya barakoa yako. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi. Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya, Wakipanda kutoka kuoshwa, Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati ya o.Midomo yako ni kama uzi mwekundu, Na kinywa chako ni kizuri; Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, Uliojengwa pa kuwekea silaha; Ngao elfu zimetungikwa juu yake, Zote ni ngao za mashujaa. Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Nyuma ya barakoa yako. Ambao ni mapacha ya paa; Wakilisha penye nyinyoro.”

Kutawala mazungumzo

Kuna kanuni za kuzingatiwa na wanandoa zinazosaidia kutawala mazungumzo ili yalete furaha na yasilete magomvi. (1 Wakorintho 15:33) “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.” Kanuni ya kwanza inawataka wanandoa kujizoeza kuongea maneno yanayojenga na yanayoimarisha mahusiano kwa sababu ndoa inahitaji kupaliliwa kwa maneno matamu ya kupongezana, kutiana shime, na kushiriki maumivu na kuonyesha staha. (Wakolosai 4:6) “Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” Wataalamu wa mawasiliano wanapendekeza maneno Matano kama maneno yaliyojaa neema. Haya yanaposemwa mara nyingi katika mazungumzo ya wanandoa huimarisha mahusiano na kujenga hamasa ya kufanya vizuri zaidi. Maneno hayo ni NAKUPENDA, ASANTE, POLE, SAMAHANI, na NAOMBA. Maneno hayo yakitolewa katika mkao sahihi wa sauti, na katika lugha sahihi ya mwili huzuia magomvi na kuponya maumivu kirahisi na kwa mafanikio makubwa.

Kuzeni lugha ya kupongezana

Lugha ya kupongezana itawale mazungumzo ya wanandoa. Kanuni hapa ni kutafuta mazuri aliyonayo mwenzako na kuyasema mara nyingi. (Isaya 41:6-7) “Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu. Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.” Si lazima kila jambo baya lililotokea lisemwe. Mengine yapotezeeni na kama ni lazima kuyasema yasemwe kwa lugha ya upendo ukimhurumia yule aliyekosea. (Wakolosai 3:13) “Mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” Wajibu uliotendwa kwako na mwenzio unapaswa kulipwa kwa neno la shukrani. Neno asante limeonekana kubeba ukubali wa huduma iliyotolewa hasa linapotamkwa kwa mkao sahihi wa sauti na mkao sahihi wa mwili. (1 Wathesalonike 5:18) “Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.”

Kuzeni lugha ya kuhurumiana

Lugha ya kuhurumiana kwa wanandoa hupunguza maumivu na kuondoa upweke anaojikuta nao mtu aliyeumizwa. Kwa kawaida binadamu anahitaji sana watu wake wa karibu anapokutana na changamoto za maisha ili wamsaidie kuona mlango wa kutokea na kurejea kwenye maisha ya kawaida. Neno sahihi lisilo na gharama lakini lenye matokeo bora katika nyakati hizo ni pole hasa inapotolewa katika mazingira yanayowakilisha uhalisia. (Luka 6:36) “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.” Kusikitika kwa ajili ya jambo baya lililomtokea mwenzako ni dalili ya upendo wa kweli. Mwanandoa asipuuzie maumivu ya mwenzake kwa kutoonyesha kujali. Hata kama zimekuwepo tofauti zozote wakati wa majanga tofauti hizo ziwekwe kando na kushughulikia kumrejesha aliyefikwa na janga katika hali ya kawaida. (1 Petro 3:8) “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu.”

Dumisheni moyo wa kujutia makosa

Hakuna aliye mkamilifu katika ndoa na hata katika Maisha ya kawaida ya wanadamu. Hata yule anayemlaumu mwenzake leo, kesho anaweza kufanya kosa lile lile au hata lililo kubwa zaidi. Kitu cha muhimu kwa wanandoa ni utayari wa kusameheana. Kutokubali kosa huja kutokana na hali ya mtu ya kutojikubali. Mtu asiyejikubali anahisi kuonewa kila anapojulishwa kosa lake. Huyu hufanya juhudi kubwa kukanusha makosa anayonenewa ili kupunguza hali yake ya kujihisi duni anayoihisi moyoni mwake. Njia sahihi ya kuondokana na uduni anaojihisi mtu huja kwa kukiri makosa anayowafanyia watu. Kujutia makosa ni kuhuzunikia kosa ulilolitenda, na hiki ni kipawa kutoka kwa Mungu. (2 Wakorintho 7:10) “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.”

Adamu na Abigaili katika kujutia kosa

Adamu alionyesha ugumu katika kutambua kosa lake na kulijutia. (Mwanzo 3:12) “Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Abigaeli anaonyesha mfano bora wa mwanamke anayejua kushuka na kuomba msamaha kwa mwanaume aliyekasirika. Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. (1 Samweli 25:23-24) “Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.” Bila Yesu kuingia ndani ya moyo ni vigumu kwa binadamu kujutia makosa yake. (Matendo 5:31) “Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.”

Dumisheni lugha ya staha

Lugha ya staha ni ile inayomtambua mwenzako kuwa anastahili kutambuliwa utu wake na kupewa heshima anayostahili. Biblia inaposema mume na ampe mkewe heshima inalenga lugha ya staha katika kuomba huduma au kitu kutoka kwake. Waliolelewa kwenye mfumo dume mara nyingi wamekuwa wakijikwaa katika jambo hili. Wanapohitaji huduma au kitu kwa mkewe hukidau kwa nguvu na kwa lugha isiyo na staha jambo linalomfanya mwanamke ajione duni. Kumwita mkeo we mwanmke si lugha ya staha. Na kusema nataka badala ya naomba pia si lugha ya staha. Naomba au nakuomba ni lugha ya staha inayotengeneza mazingira ya kupewa kitu au huduma unayoihitaji kirahisi hasa pale inapotolewa katika mkao wake halisi. “1 Samweli 25:28 Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako, kwa kuwa hakika Bwana atamfanyia bwana wangu nyumba iliyo imara, kwa sababu bwana wangu anavipiga vita vya Bwana; tena uovu hautaonekana ndani yako siku zako zote.”

Dumisheni amani nyumbani

Hakikisheni mianya yote inayoweza kuharibu amani yenu nyumbani imezibwa. Mianya hii inayoweza kuharibu amani nyumbani mara nyingi huja kwa njia ya mazungumzo. (Waefeso 4:29) “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.” Neno lililo ovu ni lile lenye matokeo mbaya kwa yule unayemnenea. Wanadamu wanatambua maneno yanayoumiza mtu anapotamkiwa. Matusi ni mojawapo ya maneno yanaomiza. Maneno yanayotolewa kwa kejeli na dharau nayo yana tabia ya kuumiza na kuchochea ghadhabu. (Mithali 15:1) “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.” Unapohisi kutamka neno ovu, lisilofaa na linaloumiza mwombe Mungu uwezo wa kulizuia. (Zaburi 141:3) “Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.” Ni watu wachache wanaoweza kustahimili neno liumizalo na wasikasirike au kuanzisha ugomvi. Gharama ya kuumaliza ugomvi ulioanzishwa na neno liumizalo ni kubwa kuliko kuzuia neno hilo lisitoke mdomoni. (Mithali 17:28) “Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.”

Msiruhusu magomvi nyumbani kwenu

Amani nyumbani ndiyo ndiyo hitaji kuu la wanandoa hata kuliko mali na fedha. (Mithali 17:1) “Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.” Mahali penye amani panaruhusu ustawi wa kila aina. Gharama ya kuirejesha amani baada ya kupotea ni kubwa kuliko kuzuia isipotee. Watu wengi wameshindwa kurejea kwenye ndoa waliyokuwa wakiifurahia kwa sababu ya kuhofia kukutana tena na hali ya kukosa amani waliyoishuhudia kabla ya kutengana kwa muda. (Mithali 25:24) “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.”

Usiruhusu huzuni moyoni

Nyumbani panapaswa kuwa mahali bora ambapo kila mwandoa anapafurahia. Amani huanzia moyoni. Moyo uliochangamka ni chanzo kikuu cha amani nyumbani. (Mithali 17:22) “Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.” Mawazo yaliyojaa huzuni na majuto huleta uchungu moyoni. Uchungu huo hupelekea kumchukia mwenzako na hata kufika hatua ya kumnunia, kumtukana na kumpiga. Mungu anawashauri waume kutokuwa na uchungu na wake zao. (Wakolosai 3:19) “Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.” Uchungu hauwapati tu wanaume kwenye ndoa hata wanawake wanaweza kuwa na uchungu na waume zao kwa yale magumu wanayowatendea au wanayohisi kuwa wanawatendea. (Waefeso 4:31) “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.”

Kununiana kusipewe nafasi

Usitunze uchungu moyoni kwa mambo mliyokoseana. Wala usipange kulipiza kisasi kwa kununa au kuzira kutoa huduma inayohitajika au kuzira kupokea huduma iliyotolewa. Maandiko yanakataza wanaume kuwa na uchungu na wake zao. (Wakolosai 3:14-16) “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” Usiwe na donge limekukaa tangu asubuhi hadi jioni. Tabia ya kununiana na kutosemeshana kati ya wanandoa inakuza ugomvi ambao kama ungemalizwa mapema na kwa hekima ingewaacha huru. Mnapofanya hivyo mnamkaribisha shetani katikati yenu.

Kuthibiti hisia za kuonewa

Ugomvi hutokea kutokana na kutofautiana misimamo au kuhisi kuwa unaonewa, unadharauliwa, au unadhulumiwa haki yako jambo ambalo haupo tayari kulikubali. Hali hiyo inaibua hasira na uwezo wa kujitawala au kufanya maamuzi sahihi unapotea. (2 Timotheo 2:24-26) Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.” Hasira ni zawadi tuliyopewa na Mungu ambayo huleta matokeo bora inapotumika vizuri. (Waefeso 4:26) “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” (Wakolosai 3:19) “Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.”

 

Zuieni magomvi yasitokee

Ili nyumbani pafae kuwa kituo cha uinjilisti na taasisi imara ya kiuchumi panapaswa kudumisha utengamano na amani. Amani huja kwa kuhakikisha haja na haki za kila mwanafamilia zinasikilizwa na kutimizwa kwa kadri itakavyowezekana. Kusameheana kufanyike jambo la kawaida sana mtu anapokiri kukosea au kughafilika. Maneno ya kuudhi au yasiyo ya kiungwana yanayotolewa kwa lengo la kumuumiza mwenzako yaepukwe na kila mwanafamilia. Hata wazazi wasijione huru kutamka neno la kuumiza kwa watoto wao badala yake lugha ya kiungwana itumike.  Jizuie kumtukania mwenzi wako mama yake au baba yake au kusema ulemavu au udhaifu ulio nyumbani kwao. Hata kama mmetofautiana kiasi gani jizueni kutukanana. Tabia ya kutukanana haiwastahili watu waungwana kama nyie. Watu wastaarabu huwa hawatukanani. Tusi au neno liumizalo huchochea ghadhabu.  (Matendo 26:27-29) “Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.”

Kugombana kunaondoa ufahamu

Ghadhabu au hasira huchochea ugomvi. Mtu mwenye hasira huhisi kuonewa, na kudharauliwa na ili kuikataa hali hiyo hupandisha hasira. Hasira ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenyewe ana hasira. Tofauti ya hasira ya Mungu na mwanadamu ni kuwa ya Mungu ina busara ndani yake kuliko ya mwanadamu.  (Mwanzo 49:7) “Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali, Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma. Nitawagawa katika Yakobo, Nitawatawanya katika Israeli.” Mwanadamu akishikwa na hasira ufahamu wake unashuka viwango. Unapokabiliana na mtu mwenye hasira hatua ya kwanza unayotakiwa kuchukua ni kushusha hasira yake. (2 Timotheo 2:24-26) “Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; Akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”

Pima kauli yako kabla ya kujibu

Ugomvi unaamuliwa na mwenye kujibu kauli ya uchokozi. Unaweza kulipuuza neno la kuumiza lililotamkwa kwa kumchukulia mtoa kauli kama mtu asiye sawa. (Mithali 26:20) “Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.” Hali kadhalika neno la kuumiza linapokutana na jibu la upole hupoteza nguvu yake na ugomvi huzuiwa. (Mithali 15:1) “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.” Uandaye moyo wako kupokea hata yasiyopendeza na kuutengenezea mazingira ya kutoumia. Maneno yaumizayo hutoka kwa yule adui akiwatumia watu unaowafahamu na unaowathamini. Hapa lengo la Shetani ni kukutoa kwenye hilo jema unalokusudia kufanya na kukuchochea kulipiza kisasi. Unapaswa kuwa mtu wa kiroho ili kuikabili hali hiyo. (Waefeso 6:16) “Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.” Kauli ya ukali na iumizayo inapokutana na jibu la upole vita inakuwa imezuiwa. Mtu muhimu katika kuuchochea au kuumaliza mgogoro kwenye mazungumzo ni yule mwenye kutoa jibu. (1 Petro 3:15 “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.”

Kunyamaza ni jibu

Wakati mwingine ili kumpa muda wa kutafakari mwenye kutoa kauli inayoumiza busara ni kutojibu lolote. (Mithali 11:12) “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.” Kunyamaza baada ya neno linaloumiza kutolewa kunakusudia kumpa yule mtoa kauli fursa ya kujitafakari. Wengine katika kukaa kimya waliweza kurejewa na fahamu zao na kugundua makosa yao. (Marko 15:3-5) “Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.”

Kusikiliza kwa makini huepusha ugomvi

Wakati mwingine ugomvi huzuka kutokana na kutosikiliza kwa usahihi kilichosemwa au kuelewa tofauti kilichozungumzwa. (Mithali 18:13) “Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.” Ni rahisi mtu kuhisi ametukanwa kwa kuwa alisikia kitu kinachofanana na tusi kwenye kauli iliyotolewa jambo linalotokana na mazoea ya kutoa lugha ya matusi aliyonayo mwenzake.  Wakati mwingine kile kinachodhaniwa ni matusi kinatokana na tafsiri ya msikilizaji na wala si tafsiri ya mtoa kauli. Ili kuepusha ugomvi kuzuka inashauriwa mwenye kuhisi kutukanwa aombe kupewa ufafanuzi juu ya kauli iliyotolewa ili ajiridhishe kama lilikuwa tusi au la. Biblia inatushauri tuwe wepesi wa kusikia kwa maana ya kuwa tuwe na hakika kama tulichosikia ndicho kilichokusudiwa na msemaji. (Yakobo 1:19) “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika.”

Msitafute mabaya kwa mwenzako

Matatizo mengi ndani ya nyumba huja pale mnapotafuta mabaya kutoka kwa mwenzako. (Mithali 17:13) “Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.” Usitafute mabaya ya mwenzako kwa nia ya kumuumbua, kumkejeli au kumkosesha amani. Usitafute kujua kama nyuki wanauma kwa kuwarushia mawe kwenye mzinga. Kupenda kunahitaji nidhamu. Kupendana kunaendana na kustahiana. (Waefeso 5:33) “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.” Mnapokuza mambo mazuri yale mabaya hutafuta mlango wa kutokea yenyewe.

 

 

Vikao vya usuluhishi

Vikao vya usuluhishi vinahitajika mapema sana baada tu ya kutofautiana. Usuluhishi kwa kadri itakavyowezekana ufanywe na wawili waliokosana badala ya kushirikisha watu wengi. Usiwe na mazoea ya kupeleka kwa mjumbe au kiongozi wa dini, kila aina ya ugomvi unaotokea. Jaribuni kuyasuluhisha mambo hayo ninyi wenyewe mkitegemea hekima ya Mungu naye atawasaidia. (Waefeso 4:26) “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” Makosa yanapodundulizwa kuna hatari ya kushindwa kuyasuluhisha siku yatakapojadiliwa. Hata hivyo usuluhishi huo ufanyike wakati ninyi wote mkiwa mmetulia na si wakati ambao kila mmoja au mmoja wenu ana hasira. (Wagalatia 6:1) “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.”

Msuluhishi awasaidie kuona hatari

Lakini kama mmeshindwa kufikiwa muafaka mwalikeni mtu mnayemwamini awasimamie. Msuluhishi hatakiwi kuegemea upande mmoja na kile anachofanya siyo kuwaamulia njia ya kutatua tatizo au kumtambulisha mwenye makosa bali kuwasaidia kuona namna ambavyo wangeweza kuepuka mgogoro usitokee na kuwauliza wanapendekeza nini kifanyike. Msuluhishi atumie muda wa kutosha kusikiliza kuliko kuongea ili abaini mapema tatizo lilipo. Awaoneshe hatari za kuendelea na mgogoro na kuwathibitishia kuwa tatizo lao siyo jipya katika maswala ya ndoa na kwamba wasidhanie kutofautiana kwao siyo ishara kuwa Mungu hakupanga waishi Pamoja kama mume na mke. Awasaidie kuzingatia kusema yote yaliyojiri kwa lugha ya kiungwana isiyo na lengo la kumdhalilisha mwingine.

Kukiri makosa kunakomesha magomvi

Kama utakuwa bingwa wa kusukumia wengine makosa yako hiyo haitakuletea amani ya kweli. Utakanusha, kwa viapo na ushahidi bandia na kufanikiwa kushawishi watu lakini amani ya moyoni itakosekana. Na kukosekana huko kwa amani kutakufanya ufanye makosa mengi zaidi na kukosana na watu wengi zaidi. Njia sahihi ni kutafuta amani ya moyoni kwa njia ya toba ya kweli. (Zaburi 32:1-2) “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.” Mungu anatutaka tuwe na amani na watu wote. Huwezi kuwa na amani moyoni kama huna amani na wenzako.  (Warumi 12:18) “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.”

Kuungama kusiwe na kona kona

Kusamehe kunarahisishwa na namna upande uliokosea unavyokiri kosa na kuomba kuhurumiwa. Lakini kusamehewa si lazima kutokane na na namna upande wa pili unavyolipokea kosa. Kusamehe kunaweza kutangulia hata kabla upande wa pili haujakiri kosa. Yesu alipowasamehe waliokuwa wakimsulubisha hakufanya hivyo kwa sababu wakosaji walionyesha toba kwa makosa yao. (Luka 23:34) “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.” Watu wengine hukosa ujasiri wa kukiri moja kwa moja makosa yao na huona nafuu kukiri kwa kuonyesha vitendo vya kujirudi kama kuanza kubadilisha tabia zinazolalamikiwa au kwa kutoa zawadi. Na wengine badala ya kusema samahani hutumia lugha za kujaribu kulinda hadhi zao kwa kusema yaishe. Toba na ungamo la kweli haikwepi lawama au kuogopa gharama. Inanyoka na kukiri kuwa kosa lilifanyika. (Zaburi 51:3-4) “Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.”

Anayekiri kosa asemehewe

Mara nyingi sababu ya msingi ya kukosekana kwa mahusiano na mawasiliano mazuri nyumbani ni kukosekana kwa roho ya msamaha. Yesu anapendekeza kwetu. (Luka 17:3-4) “Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” Amani ya kweli haiwezi kuwepo mioyoni mwa watu wasiosamehe. Kusamehe kwa sehemu kubwa kunaleta nafuu na msaada kwa yule anayesamehe kabla hakujaleta nafuu kwa anayesamehewa. Kusamehe kunadhihirisha kuwepo kwa moyo mkuu unaoweza kutawala hisia. Wengine kwa kukosa kusamehe wamejikuta wakitenda makosa ya jinai ya kuua, kupiga, kutukana na hata kupeana talaka. Mbaya zaidi roho ya kutosamehe imewasababishia wengine maradhi kama ya shinikizo, msongo, vidonda vya tumbo hata mapepo na wendawazimu. Talaka ni hatua ya mwisho baada ya jitihada zote za kuwapatanisha wanandoa kushindwa. Ikiwa kiini cha tatizo ambacho ni kutosamehe kinakuwa hakijatafutiwa ufumbuzi, talaka peke yake haiwezi kuwa suluhisho la kudumu. 

Taasisi imara ya kiuchumi

Ndoa ilikusudiwa iwe taasisi imara ya kiuchumi. Hali ya Uchumi yaweza kuwa imara Ikiwa kutakuwako amani na masikilizano. Mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa na kuafikiwa mapema katika ndoa ni mambo yahusuyo pesa. Pesa ni kitu kinachoweza kuleta furaha au huzuni kutegemeana na kiwango chenu cha kujitoa kila mmoja kwa mwenzake na kiwango chenu cha uongofu. Biblia inatuthibitishia kuwa fedha ni mbaraka inapotumiwa vyema na mpango wa Mungu katika ndoa ni kutufanikisha kiuchumi. (Mhubiri 10:19) “Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, Na divai huyafurahisha maisha; Na fedha huleta jawabu la mambo yote.” (2 Wakorintho 9:8) “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.” Lakini tofauti na mtazamo wa wengi katika kizazi hiki Mungu hupitishia utajiri na baraka zake kwa njia ya kazi za mikono yetu. (Waefeso 4:28) “Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.”

 

Mke na mafanikio ya familia

Mke amebeba baraka za familia na anapotendewa isivyostahili huwa chanzo kikuu cha kuwepo kwa myumbo wa kiuchumi na kukosekana kwa utengamano nyumbani. (1 Petro 3:7) “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” Mungu anaweza kuzuia baraka zote Ikiwa mke ananyanyasika. Mke anayepewa heshima na mumewe hujisikia kuwa salama na usalama na kupendwa ndicho kitu cha kwanza anachokihitaji mwanamke kutoka kwa mumewe. Mume asiwe na mashaka na mkewe au kuwa na wivu unaopitiliza. Mume anayemwamini mke wake humfanya mkewe kujiamini zaidi na kufanya shughuli zake kwa uhuru na mafanikio makubwa. “Mithali 31:10-11) “Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.”

Mgawanyo wa kazi

Mama wa nyumbani ana mchango sawa na yule afanyaye kazi za kujiriwa au za kujiajiri. Hata hivyo mama asiridhike kufanya kazi moja tu. (Mithali 31:13) “Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.” (Mithali 31:19) “Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.” (Mithali 31:22) “Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.” (Mithali 31:24) “Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.” (Mithali 14:23) “Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.” (Tito 1:11) “Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.” Je kuna kazi ambazo Mkristo hapaswi kuzifanya hata kama zinamletea mapato? Je, kuuza baa, kuuza majeneza, na udalali? Je inafaa mke afanye biashara zinazomfanya asafari mara kwa mara?

Je ni lazima kujua pato la mwenzako?

Wanandoa wanaopendana kwa dhati watajulishana mapato yao na miradi yao waliyoifungua na mahali ilipo. (2 Wafalme 4:9-10) “Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.” Ili kuepuka kuwa na matumizi ya hovyo wanandoa watapanga bajeti Pamoja na kuchagua mmojawapo kuwa mtunzaji wa fedha. Mtunzaji wa fedha awe ni yule mwenye nidhamu ya pesa.

Je ni halali kutomshirikisha mkeo mapato?

Mke na Watoto wana haki ya kunufaika na mapato ya kazi ya baba wa familia au kwa kazi waliyofanya kwa pamoja kama familia. (Mithali 31:20-31) “Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa. Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.” (Mithali 31:11) “Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.”Siri ya mafanikio ya kiuchumi ni kupanua vyanzo na wigo wa mapato na kubana matumizi yasiyo ya lazima. Siri nyingine ya mafanikio ya kiuchumi ni kuongeza maarifa na vitendea kazi vya kurahisisha uzalishaji wa huduma au bidhaa.

Je ni sahihi kwa mke kusaidia mahitaji ya nyumbani kwa mapato yake?

Mke mwenye upendo wa kweli anao wajibu wa kusaidia mahitaji ya nyumbani kwake kwa kununua vitu vyenye gharama nafuu na vitu vyenye gharama kubwa kutegemeana na kipato chake. (Mithali 31:27) “Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.” (Mithali 31:16) “Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.” Mume asibweteke kwa sababu amepata mke anayemsaidia kwa kuwa huo ni wajibu wake yeye aliye kichwa cha familia.

Je ni sahihi kutomshirikisha Mungu kwenye mapato ya familia?

Familia nyingi zilizofanikiwa kiuchumi zimekiri kuwa kumshirikisha Mungu katika mipangokazi yao na kumshirikisha katika mgawanyo wa mapato yao imekuwa siri kubwa ya mafanikio yao. (Kumbukumbu la Torati 8:18) “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Yakobo alikuwa na mpangokazi wake alioukabidhi kwa Mungu ambapo aliahidi kutolea Mungu moja ya kumi ya mapato yake endapo kama angemfanikisha. (Mwanzo 28:20-22) “Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

Je kusaidia wahitaji kunatajirisha?

Kusaidia wahitaji na kuitegemeza kazi ya Mungu huongezea mibaraka kwa familia. (Luka 6:38) “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” (Mithali 31:20-21) “Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake. Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.” Jambo la kuzingatia ni kuhakikisha ukarimu huo unatendwa kwa moyo mkunjufu bila kuwaumbua waliosaidiwa. (2 Wakorintho 9:7) “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.”

Kuachana huleta maumivu

Moja ya vitu vilivyozoeleka sana leo kwa wanadamu na ambacho Mungu anakichukia  sana ni wanandoa kuachana au talaka. (Malaki 2:16) “Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.” Kuachana ni jambo lenye maumivu makali kwa sababu waliooana walipoambatana walishikamana kama karatasi mbili zinazounganishwa kwa gundi ya maji. Baada ya kukauka huwa vigumu kuzitenganisha bila kusababisha madhara pande zote. Hivyo ndivyo walivyoachana wanavyopitia maumivu.

Mkaribisheni Yesu

Ndoa na familia nyingi zinaathiriwa na magomvi ya mara kwa mara. Magomvi hayo huweza kufikia kiwango cha kutovumilika. Na inapofikia hali hiyo kutengana kwa muda kunaweza kuwa suluhisho. Hata hivyo suluhisho la kudumu ni kukaa chini na kuondoa tofauti. Sababu kubwa ya kuwepo kwa migogoro ni kumfungia nje yeye aliye mwanzilishi wa ndoa. Njia sahihi ya kuondoa tofauti hizo ni kumkaribisha Yesu mioyoni mwetu.  (Yohana 15:5) “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” Zamani kulikuwa na maandishi unayoyakuta katika nyumba nyingi yenye maneno, YESU NDIYE MKUU WA NYUMBA HII, MSIKILIZAJI WA MAZUNGUMZO YETU. Maandishi hayo yalienda wapi?

Rasimisheni ndoa zenu

Unapoanza na Mungu kwenye maisha ya ndoa mibaraka yake huwa tele nyumbani. Wale ambao mlitoroshana na mnaendelea kuishi bila ndoa nawashauri mkabariki ndoa zenu au kama vipi mkafungie serikalini ili zitambuliwe kisheria. Wengine mnaishi bila ndoa na bila ridhaa ya wazazi. Hiyo ni mbaya zaidi. Unatarajiaje kunyookewa na maisha wakati mnaishi kwa kificho kiasi hicho? Wale mnaoishi bila (ridhaa) kujitambulisha kwa wazazi nawashauri hebu nendeni mkawaone wazazi mpate baraka zao.

Msiishi kwa majaribio

Kuishi kama watu mnaofanya majaribio kwenye ndoa ni jambo lisilofaa kabisa. Moja ya matatizo ya kisheria utakayoyapata (hasa wewe mwanamke) siku mumeo atakapofariki utakuwa na wakati mgumu kuwashawishi ndugu wa marehemu kuwa wewe ni mjane na mrithi halali wa mali na watoto. Hata wale waliofunga ndoa zao serikalini kanisa linawapa fursa ya kuja kubariki ndoa hizo kanisani. Na kwa wale walioanza kuishi pamoja bila cheti cha ndoa nao wanaalikwa kuja kubariki ndoa zao na kuzirasimisha kwa kuwapatia cheti cha ndoa kinachotambulika kisheria.

Imarisheni mambo ya kiroho

Ili Mungu aendelee kukaa na wewe uliye kwenye ndoa, ni lazima umtengenezee mazingira ya kumwalika. Someni Neno lake pamoja. Ombeni mnapoamka na mnapolala na wakati wa chakula. Tengeni muda wa kufanya kazi ya Mungu kwa kutembelea majirani zenu na kujifunza nao kile ukijuacho kuhusu Mungu. Muwe mawakili wema kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kutumia vema wakati, na kuitegemeza kazi ya Mungu kwa mali zako, talanta zako, na muda wako, na mwisho kuhudhuria kwa uaminifu semina na mikutano ya kiroho.

Ombeni pamoja

Kuomba pamoja huweza kutatua changamoto za ndoa katika hatua ya awali. Kwenye maombi yenu msionyeshe kushindani au roho ya kujihesabia haki. Wafilipi 4:6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Yakobo 5:16 Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.

Shuhudieni pamoja

Kusaidia wengine kulielewa Neno la Mungu huweza kuondoa roho ya ugomvi. Muda unaotumia kujifunza Neno unaimarisha hali yako ya kiroho. (Matendo ya Mitume 18:26-28) “Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.” Matendo ya Mitume 17:11 Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. (Matendo 16:30-34) “Kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.”

Zoezi la kuambatana

Mungu alikusudia kuwe na matukio kadhaa yanayowaweka karibu wanandoa ili iwe kinga yao kwa mashambulizi ya adui. Ili kuimarisha kuambatana inashauriwa kuwepo siku ya kutambua huduma ya baba, huduma ya mama, huduma, ya Watoto, na huduma ya mfanyakazi wa nyumbani. Siku hiyo zawadi iandaliwe na kila mmoja atoe ushuhuda alivyobarikiwa na mhusika. Pale itakapowezeka majirani waalikwe kwenye tukio hilo litakaloandamana na mlo wa Pamoja ambapo mhusika atakuwa anawahudumia watu akiwa kwenye vazi la mpishi. (Mithali 31:29) “Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.”

 

Tundikeni picha yenu ukutani

Picha kubwa ya ndoa yenu iwepo sebuleni kila siku ikiwakumbusha mlivyounganishwa na ifikapo tarehe mliyofunga ndoa mfanye sherehe ya kujipongeza mkibandika picha za ndoa yenu sebuleni na kujikumbusha matukio kadhaa ya siku hiyo. Mtafanya hivyo siku ya kumbukizi ya kuzaliwa. Kwenye kumbukizi ya ndoa mwaweza kuwa na mtoko ambapo mtabeba chakula chenu na Kwenda kukilia sehemu tulivu huku mkiangalia uumbaji wa Mungu.

Ambatana na mwenzio

Ambatana na mwenzio kila inapowezekana hasa kwenye matukio ambayo wanandoa wamealikwa na muwe mnazungumza muda wote. Siku hizo vaeni mavazi yanayowatambulisha. Ukiitwa mbele kuwasalimu watu au kutoa maelezo Fulani nenda na mke wako. Ukiwa umealikwa kuendesha tukio fulani usisahau kumtambulisha mke wako. Ukipewa nafasi ya kuahidi jambo au kutoa shukrani mpatie hiyo nafasi mke wako. Kwa njia hiyo mtakuwa unaupalilia upendo wenu na Mungu atawafundisha kupendana. (1 Wathesalonike 4:9) “Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.”

Mungu anachukia kuachana

Kwa hali ilivyo kwenye ndoa leo inatia shaka kama upendo wa jinsi hii bado upo kwa kuwa viwango vya kuachana vinaongezeka. Kanisa ni lazima lifanye jitihada ili kupunguza kasi ya kuachana. (Malaki 2:16) “Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.” Hata hivyo kuachana kunaweza kuruhusiwa katika mazingira ambayo uhai wa mmojawapo upo hatarini, ama kuna tuhuma za uzinzi ambazo aliyetendwa ameshindwa kuzivumilia. (Mathayo 19:8) “Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.”

Kutoshelezana kimapenzi

Mungu aliweka tendo la ndoa kwenye ndoa ili wanandoa wakamilishe mchakato wa mawasiliano na mahusiano, na kutoshelezana kimapenzi. Tendo hili linapaswa kuanza baada ya kupata kibali cha kuishi pamoja kama mume na mke na si kabla ya hapo. Kibali hicho hutolewa na wazazi, kiongozi wa ukoo. Kingozi wa kidini, ama kiongozi wa serikali.  (Wimbo Ulio Bora 3:5) “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.” Uhalali wa tendo la ndoa ni kwenye ndoa peke yake.

Tendo la ndoa lilikusudiwa liwaletee furaha wanandoa wote wawili bila mmoja kujikuta akimpunja mwenzie. Hii ni huduma ambayo kila mmoja hutafuta kukamilisha furaha ya mwenzake kwa kujitoa kwa ajili yake.   (Mhubiri 4:11) “Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto?” Huo moto ni zile hisia wazipatazo wanandoa pale kila mmoja wao anapokuwa amefikia kilele cha utoshelevu wa tendo lenyewe. Hicho kilele cha utoshelevu huleta hisia za furaha zinazoelekeana na hali iliyotajwa kwenye Wimbo Ulio Bora kama kuzimia kwa muda. (Wimbo Ulio Bora 2:5) “Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera, Kwa maana nimezimia kwa mapenzi.”

Haki ya tendo la ndoa

Maisha ya wanandoa yamejaa matukio mengi ya tendo la ndoa. Tendo la ndoa hufanywa pale mmoja wa wanandoa au wote wawili wanapolihitaji. Haikuwa mpango wa Mungu kuwa ndoa isiwe na tendo la ndoa. Hali hiyo ya kutokuwa na tendo la ndoa inakubalika pale mmoja wa wanandoa anapokuwa hawezi kutoa huduma hiyo kutokana na changamoto za muda au za kudumu zilizomkuta na kamwe haikutokana na hali ya maumbile. Wale wasioweza kutoa huduma ya tendo la ndoa wanashauriwa kutooa au kutoolewa.   (1 Wakorintho 7:3) “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.” Haki inayotajwa hapa ni haki ya tendo la ndoa.

Kila mwanandoa ana haki ya kupata tendo la ndoa na mwenzake kila anapohitaji isipokuwa kama mazingira ya mwenzake au ya mahali walipo hayaruhusu. Mazingira kama ya ugonjwa, uchovu, njaa, au kuwepo kwenye siku zake na mengine kama hayo, si rafiki kwa tendo la ndoa. Mke au mume hana haki ya kumyima mwenzie tendo la ndoa kama njia ya kushinikiza madai fulani au kulipiza kisasi.  Tendo la ndoa likitumika huwa chanzo cha kuleta suluhu kwenye migogoro iliyokuwa inakaribia kuibuka na kupunguza maumivu waliyokuwa wanayapitia wanandoa kutokana na matukio fulani fulani yaliyowakuta. Hata hivyo tendo hili linapofanyika bila kiasi huwa chanzo cha matatizo. (1 Wakorintho 7:5) “Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” Ili kuepuka kukosa kiasi wanandoa wanaweza kujiwekea utaratibu wa wakati gani wakutane kwa tendo la ndoa ili kuwa na muda wa kutosha wa kutimiza majukumu mengine.

Tendo la ndoa linahitaji maandalizi

Tendo la ndoa linahitaji kuandaliwa kwa umakini ili lifikie utoshelevu unaohitajika. Licha ya kupangiwa wakati ufaao kufanyika linahitaji pia faragha ya kutosha na kutokuwa na usumbufu unaopunguza viwango vyake ya utoshelevu. (Waebrania 13:4) “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” Malazi ya wanandoa hasa wakati wanaposhiriki tendo la ndoa yanapaswa kuwa safi, yakiwa kwenye chumba kinachotunza faragha yao, mahali penye kuvutia na pasiporuhusu kuonekana na walio nje wala pasiporuhusu sauti za ndani kusikika nje. Mwanamke ana wajibu wa kupafanya chumbani kuwa mahali penye harufu nzuri na pa kuvutia wakati wote. (Mithali 7:16-18) “Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.” Harufu mbaya huzuia kufurahia tendo la ndoa.

Kunyimana

Kunyimana tendo la ndoa si lazima kutokane na mmojawapo wa wanandoa kumkatalia mwenzie tendo la ndoa. Wanandoa wanaweza kuwa wanashiriki tendo la ndoa kila wakati bado katika nyakati hizo zote mmoja akawa ananyimwa ule utoshelevu ambao ulikuwa haki yake aupate. Mara nyingi wahanga wa jambo hili ni wanawake. Wanawake wanahitaji kuandaliwa ili washiriki kikamilifu kwenye tendo la ndoa. Hisia za wanawake huanzia kwenye vichocheo au homoni wakati hisia za wanaume huja kutokana na macho kuona maumbile ya ndani ya mwanamke. (2 Samweli 11:2-4) “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.”

Lugha na vitendo vya upendo

Mwanamke anahitaji mawasiliano ya kina yaliyojaa upendo na kujali ili kuamsha hamu ya tendo la ndoa. Mawasiliano hayo yawe kwa vitendo na maneno. (Wimbo Ulio Bora 4:7) “Mpenzi wangu, u mzuri pia pia, Wala ndani yako hamna ila. Bibi arusi, njoo pamoja nami toka Lebanoni, Pamoja nami toka Lebanoni. Shuka kutoka kilele cha Amana, Kutoka vilele vya Seniri na Hermoni; Kutoka mapangoni mwa simba, Kutoka milimani mwa chui. Umenishangaza moyo, umbu langu, Bibi arusi, umenishangaza moyo, Kwa mtupo mmoja wa macho yako, Kwa mkufu mmoja wa shingo yako. Jinsi zilivyo nzuri pambaja zako, umbu langu, Bibi arusi, ni nzuri kupita divai; Na harufu ya marhamu yako Yapita manukato ya kila namna.”

Utulivu wa mawazo

Mwanamke anayesifiwa kwa mazuri anayofanya anaongeza kiwango cha amani moyoni mwake na kuondoa msongo unaoweza kuathiri kiwango cha hisia ya tendo la ndoa. (Mithali 17:1) “Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.” Tendo la ndoa linafananishwa na karamu. Tendo hili linapofanywa bila kuwepo utulivu wa mawazo linakuwa kero badala ya kuwa mbaraka. Magomvi huzuia utulivu unaohitajika kwenye tendo la ndoa. (Waefeso 4:31) “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” Pale magomvi yanapoibuka kwa wanandoa hatua za hekima za kuutatua ugomvi huo haraka zichukuliwe ili pamoja na mambo mengine yasiathiri utoshelevu wa tendo la ndoa la wanandoa hao. (Waefeso 4:26) “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” Tendo la ndoa linapofanywa bila utulivu wa mawazo kwa kuwa mmoja wa wanandoa aameumizwa kwa kauli au kitendo ambacho hakijapata muafaka ni sawa na ubakaji.

Kukumbatia

Miguso ya mwili ina mchango wa kuamsha hisia na kumwandaa mwanandoa kwa tendo la ndoa. Miguso hiyo huanzia kwenye nywele kichwani hadi unyayoni. Miguso ya mdomo huitwa busu na miguso ya mikono huitwa kushikana mikono na kukumbatia. (Wimbo Ulio Bora 2:6) “Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, Nao wa kuume unanikumbatia!” Kukumbatia na kubusu ni kwa muhimu kwa wanandoa si tu katika kujiandaa na tendo la ndoa bali katika kuimarisha mahusiano yao. Waumini wanapokusanyika kwa ibada huwa na muda wa kusalimiana kwa mikono wakati wa kuanza ibada na wakati wa kumaliza ibada. Makanisa ya awali yalikuwa na utaratibu wa kusalimiana kwa busu takatifu. (Warumi 16:16) “Salimianeni kwa busu takatifu. Makanisa yote ya Kristo yawasalimu.” Kuna ukaribu unaojengwa kwenye miguso ya namna hii.

Upendo unawakilishwa na mguso

Upendo unawakilishwa na mguso pale yule anayejidhania kuwa asiyefaa anapoguswa na yule anayemthamini sana. (Mathayo 8:3) “Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.” Halikuwa jambo la kawaida kwa mtu asiye na ukoma kumgusa mwenye ukoma nyakati za Yesu. Yesu kwa kumgusa mkoma alitaka kupeleka ujumbe kuwa hambagui mwenye ukoma hata kama kwa kufanya hivyo alikuwa anahatarisha afya yake na usalama wake kutoka kwa Wayahudi ambao wangemhesabu kuwa najisi. Je, unaona kinyaa kumgusa mkeo au mumeo kwa sababu ya kuogopa watu au kwa kuhisi kuwa utajidhalilisha? Mguso wako wa upendo utamuongezea thamani mwenzako na kuleta utulivu moyoni.

Mguso usiohitajika

Wakati fulani mguso unaweza kufanywa pasipohitajika. Mjulishe mwenzako mahali miguso inapohitajika. Nawe jifunze kwa mwenzako na kutoka kwa wataalam wa maswala ya ndoa maeneo ambayo miguso inahitajika zaidi katika mwili wa mkeo au wa mumeo. Kugusa pasipohitajika ni kero na matumizi mabaya ya maandalizi ya tendo la ndoa. Kugusa kunakohitajika huamsha hisia kali za mapenzi. (Ruthu 1:8-9) “Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. Bwana na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia.”

Mawasiliano

Mawasilino ni mchakato wa kushirikishana mawazo, maoni, na hisia kwa njia mbalimbali. Watu huweza kuwasiliana kwa sauti zilizobeba maneno au zisizobeba maneno, kwa maandishi, kwa lugha ya mwili, kwa mkao wa sauti, au kwa kukaa kimya. Kuna hatua tatu ambazo mawasiliano hupitia. Mawasiliano huanzia kwenye mawazo, kisha kupitishwa kwenye njia iliyochaguliwa kupitishia mawazo, na hatua ya tatu ni ya mlengwa kupokea ujumbe uliokusudiwa. Hatua hizi tatu zinapokamilika kwa ufanisi ndipo tunapoweza kusema mawasiliano yamekamilika. Hata hivyo ujumbe uliokusudiwa unaweza usimfikie mlengwa kutokana na kikwazo cha lugha, kushindwa kutafsiri kwa usahihi maneno yaliyotumika, kushindwa kusikiliza kwa umakini sababu ya kutovutiwa na mazungumzo au kutumia muda wa kusikiliza kujiandaa kujibu. Wataalamu wanasema mawasiliano yanaundwa kupitia njia kuu tatu ambazo ni maneno, mkao wa sauti, na lugha ya mwili isiyotumia maneno wala mkao wa sauti huku maneno yakibeba 7% ya ujumbe, mkao wa sauti ukibeba 38% ya ujumbe na lugha ya mwili isiyotumia maneno na mkao wa sauti ikibeba 55% ya ujumbe.

Mawasiliano katika tendo la ndoa.

“Kuwasiliana ni kuonyesha upendo na ukubali wetu kupitia namna tunavyosikiliza, tunavyozungumza, na tunavyothaminiana.”[1] Tendo la ndoa ni hatua ya ndani zaidi ya kufanya mawasiliano kati ya mume na mke. Hapa ndipo wanandoa wanaposhirikishana hisia, mawazo, maoni, furaha na huzuni zao kwa lugha ya upendo kila mmoja akijiacha wazi kimwili na kiakili bila kuona aibu. (Mwanzo 2:25) “Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.” Kwa kawaida mwanadamu ameumbwa na haya. Anaweza kufanya jambo linaloleta haya kwa mtu yule anayemwamini na anayemtegemea. Lugha anayoongea mwanaume au mwanamke kwa mwenzi wake anaposhiriki tendo la ndoa ni kuwa nakupenda, nakuamini, na nakutegemea kiasi cha kuwa tayari kukukalia uchi. Hii ni hatua ya juu ya mwanamke kujifunua kwa mumewe ndiyo maana Biblia ikalifananisha tendo hili na kumjua mke. (Mwanzo 4:1) “Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.”

Ibada ya tendo la ndoa

Tendo la ndoa linapofanyika kwenye ndoa huchukuliwa kama ibada. (1 Wakorintho 7:5) “Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” Sala ni ya muhimu kabla na baada ya tendo la ndoa. Ni ya muhimu kabla kwa sababu ya kuwasilisha kwa Mungu changamoto ambazo mngependa Mungu aziondolee mbali mnaposhiriki tendo hilo. Changamoto kama za kushindwa kupata mtoto, changamoto za kushindwa kumfikisha mwenzio kileleni, changamoto za upungufu wa nguvu za kiume, changamoto za kushika mimba wakati ambao hamuhitaji kushika mimba, na changamoto za kuwahi kufika kileleni. Uwasilishaji wa changamoto hizo (kama upo) waweza kuandamana na shukrani kwa zawadi ya tendo hilo linaloongeza furaha ya ndoa na linalothibitisha ukarimu wa Mungu kwa wanadamu. (2 Wakorintho 4:15) “Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.” Hii ni fursa pia ya kumshukuru Mungu kwa kuwapa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa uwezo ambao wengine hawajapewa na kuomba awajalie kutovuka mipaka ya viungo vilivyoidhinishwa kwa tendo la ndoa. (Warumi 1:21, 26-27) “Kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.”

Maboresho na kupongezana

Baada ya kila huduma ya tendo la ndoa kufanyike maboresho na kupongezana. Kila mmoja ampongeze na kumshukuru mwenzake kwa huduma aliyopokea na kuelekeza maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho. Kusiwe na kuambiana uongo au kugombezana katika kufanya tathmini hii. Yule ambaye amempunja au kumnyima mwenzake akubali kuwa anaondoka na deni ambalo atatakiwa kulilipa mechi itakaporudiwa. (Wakolosai 3:9-10) “Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.” Miongoni mwa maboresho kwa mume na hata mke ni kuongezewa vyakula au mimea inayoimarisha nguvu zake za kiume na hamu ya tendo la ndoa na kumrejeshea virutubisho vilivyotumika.

Mimba zisizohitajika

Ili kuepuka mimba zisizotarajiwa wanandoa wanashauriwa kutumia njia salama na za kuaminika za kuzuia mimba. Kama itakuwa lazima kutumia vidonge uamuzi huo uchukuliwe baada kuwaona wataalam wa afya na kujiridhisha kuwa vidonge hivyo havitakuwa na madhara kwa mtumiaji. Matumizi ya kondomu kwa wanandoa yanapunguza maana halisi ya tendo la ndoa na kukaribisha dhana ya hatia. Hata hivyo kondomu nyingine zimeonekana kutokuwa na uwezo wa kuzuia mimba kutokana na kuwa na matundu au kuchomoka wakati wa tendo lenyewe.

Matumizi ya kalenda katika kuzuia mimba

Kwa kadri itakavyowezekana wanandoa watumie kalenda kuzuia mimba zisizohitajika. Kama mzunguko wa mwanamke si wa kubadilika badilika siku kumi baada ya kumaliza siku zake huwa ni za hatari kwa maana ya kuwa na uwezekano wa kushika mimba. (2 Samweli 11:4-5) “Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.” Baada ya muda huo kuna uwezekano mdogo wa kushika mimba maana yai la mwanamke halina tena uwezo wa kutunga mimba.