Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

1 SAMWELI

MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 1:1-28   

 1. Mtu anaweza kujiuliza Elkana aliwezaje kuwa na wake wawili? Je jambo hili lilikuwa halali machoni pa Mungu? Matatizo yaliyojitokeza kwenye familia yake yanathibitisha kuwa haukuwa mpango wa Mungu? Tatizo la kukosa mtoto limeziumiza baadhi ya familia. Elikana alitumia njia gani unazozikubali katika kupunguza maumivu ya kukosa mtoto kwa mke wake?
 2. Mara nyingi Mungu alipolifunga tumbo la mwanamke asizae alilifungua baadaye kwa kumpatia mtoto aliyekuwa muhimu kwa familia, jamii, na kwa ulimwengu kama ilivyotokea kwa Hana. Unapata ujumbe gani wa faraja kutokana na ukweli huo? Unapokuwa na jambo nyeti unalotaka Mungu akutendee ni lazima uchukue hatua zisizo za kawaida. Hatua gani umevutiwa nazo ambazo Hana alizitumia kukabili changamoto yake ambazo ungependekeza kwa mtu anayepitia changamoto hizo?
 3. Kuhukumu wengine kwa jambo tusilo na hakika nalo ni kosa linaloumiza wale wanaotuhumiwa. Umehusika kwa namna gani kutafsiri vibaya vitendo vya wengine? Je umeitikia tuhuma hizo kama alivyofanya Hana? Hana alimtoa mwanawe kwa Mungu mara tu baada ya kuachishwa kunyonya. Umemtoa mwanao kwa Mungu mapema kiasi gani ili alelewe kiroho?
 4. Unadhani Hana alijisikiaje siku aliyopata mtoto? Je wakati ulipowadia Hana akachukua mimba' unaeleza ukweli kuwa kila jambo lina wakati wake?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 2:1-36   

 1. Maombi ya kushukuru ya Hana yamejaa sifa kwa Mungu juu ya uwezo wake wa kuokoa. Kwa nini maombi yetu mengi yamejaa mahitaji badala ya sifa na kushukuru? Kuna faida gani katika maombi ya sifa na shukrani? Kwa kulinganisha na kisa cha wakoma 10, kwa nini idadi ya wanaorudi ili kumshukuru Mungu huwa ni chache? Kwa nini kuna shuhuda chache katika mikutano ya kiroho kwenye makanisa leo hii?
 2. Wana wa Eli walifanya dhambi kwa kukiuka kanuni za utoaji sadaka kwa kujitwalia sadaka isivyostahili na kulala na wanawake. Dhambi hii ingalipo leo miongoni mwa watumishi wa Mungu? Iliwezekanaje Samweli asiige tabia hii mbaya kutoka kwa wakuu wake wa kazi? Hatua aliyochukua Eli baba yao na kiongozi wa kiroho dhidi ya tabia za watoto wao inaridhisha? Je ilikidhi matarajio ya waumini? Je ilikidhi matarajio ya Mungu?
 3. Kwa nini wakati fulani viongozi na waumini hukosa ujasiri kuchukua hatua dhidi ya wale wanaomkosea Mungu kanisani? Je Mungu anaridhishwa na hali hiyo? Je watumishi wa Mungu wanapofanya makosa katika utumishi wao ni halali kujitwalia nafasi ya Mungu na kuwahukumu kwa kutumia nguvu?
 4. Je Mungu ana mpango wa kuwashughulikia watumishi wabovu wa kiroho wanaowapotosha watu? Kwa nini mara nyingi anaonekana kukawia kuchukua hatua hizo?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 3:1-21 

 1. Iliwezekanaje Samweli kulala hekaluni tena karibu na sanduku (ndani ya vyumba vitakatifu) bila kuwa na hatia? Kwa nini inasemwa nyakati za ukuhani wa Eli neno la Mungu lilikuwa adimu? Je yaweza kuwa watu walikuwa hawahubiriwi neno ila mapokea na siasa? Hali hiyo ipo kanisani kwenu?
 2. Utatambuaje ikiwa mtu ameitwa na Mungu kwa kazi yake? Utawatambuaje wale wanaolazimisha wameitwa na Mungu kumfanyia kazi na kumbe wamejiingiza kwa nguvu kukidhi matakwa yao? Unazungumziaje wale wanaokataa kufanya kazi ya Mungu hadi wabembelezwe au hadi watumiwe wajumbe maalumu? Je ni dalili ya unyenyekevu?
 3. Mungu anamaanisha nini anaposema atatenda tendo katika siku za usoni ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha? Je ni kweli kuwa Eli hakuzuia laana isiwakute watoto wake? Huruma kwa mwenye makosa inaweza kuwa njia ya kumtafutia laana mtu huyo?
 4. Kwa nini uovu wa nyumba ya Eli ulikuwa hausafishiki kwa dhabihu wala kwa sadaka? Je kuna dhambi ambayo damu ya Yesu haiwezi kuitakasa? Je kuna wakati kama mtumishi wa Mungu unaweza kuogopa kuwaeleza watu ukweli kwa kulinda maisha yako au maslahi fulani?
 5. Waisraeli walitambua kuwa Samweli amewekwa na Bwana. Je leo kuna shida ya kutowatambua (kuwapa heshima wanayostahili) watumishi wa Bwana?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 4:1-22

 1. Unadhani nini kilikuwa chanzo cha Waisraeli kuwa dhaifu na kupigwa na adui zao? Uamuzi wa wazee kulileta Sanduku la Agano vitani lilikuwa sahihi na lilipata baraka za Mungu? Unadhani nini kingekuwa sahihi kufanyika baada ya kipigo walichopata vitani?
 2. Kosa la kubeba sanduku la agano kutoka chumba cha pili cha hekalu (ambako kuhani mkuu pekee alikuwa anaruhusiwa kuingia) kunatokana na dhambi walizotuhumiwa hapo awali ambazo hazikuwa zimeshughulikiwa? Kwa nini sanduku lilishindwa kufanya miujiza kama lilivyofanya wakati wa kuvuka mto Yordani?
 3. Kwa nini Mungu aliruhusu sanduku litwaliwe na Wafilisti na kuifanya miungu ya kipagani ionekane ina nguvu kuliko Mungu wa kweli wa Israeli? Je kifo cha Hofni na Finehasi kinaashiria kuwa makuhani hao watukutu walikuwa wanapokea malipo ya uovu wao?
 4. Je, Kuhani Mkuu Eli na mkwewe nao walikufa kwa sababu walikuwa wanawatetea makuhani hao waliojitwalia madaraka yasiyo wahusu   au kwa sababu ya kutambua kuwa Mungu ameliacha taifa la Israeli? Unajifunza nini kuhusu kisa hiki unachopanga kurekebisha ili kuepuka hasira ya Mungu dhidi yako na dhidi ya kanisa lako?

 
MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 5:1-12  

 1. Wafilisti waliamini miungu yao ndiyo iliyowawezesha kulitwaa sanduku la agano. Unadhani Mungu aliruhusu sanduku litwaliwe ili akadhihirishe ukuu wake dhidi ya miungu ya kipagani? Nini kilidhihirisha ukuu huo? Je inawezekana mwanadamu kumtetea Mungu anapoona anadhalilishwa? Mungu anapotegemea utetezi wa wanadamu badala ya kujitetea mwenyewe anakuwa amepoteza sifa za kuwa Mungu?
 2. Je kuwa na sanamu katika nyumba za ibada ni desturi ya dini za kipagani? Je sanduku la agano lililotekwa lilikuwa mbaraka kwa Wafilisti? Kwa nini? Wafilisti walikuwa na viongozi walioitwa mashehe. Je Wafilisti walikuwa Waislamu?
 3. Kwa nini sanduku la agano halikuleta madhara makubwa kwa Wafilisti vitani kama lilivyoleta lilipofikishwa kwenye miji ya Wafilisti? Mungu alitaka kuwafundisha nini Wafilisti na Waisraeli?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 6:1-21   

 1. Wafilisti hawakutaka kushindana na Mungu kama Farao na hivyo walikubali kuwa miungu yao imeshindwa na kuamua kulirudisha sanduku la agano. Kwa nini kwa miezi yote saba Waisraeli hawakufanya jitihada zozote za kulirejesha sanduku la agano? Unadhani toba ya Wafilisti ilipokelewa na Mungu?
 2. Kwa hatua hii ya toba na mipango ya kurejesha sanduku Wafilisti wanaonekana kuwa wa kiroho kuliko Waisraeli? Kama jibu ni ndiyo kwa nini na kama jibu ni hapana ni kwa nini? Ng'ombe ambao hawajafungwa nira na gari jipya lililobeba sanduku viliongoza msafara bila kukosea?
 3. Nini kiliwaongoza ng'ombe hao wanyonyeshao wasiliache sanduku na kurudi nyumbani kwenda kuwahudumia ndama wao? Kitendo cha kuwatoa kafara ng'ombe waliobeba sanduku kinadhihirisha ukatili kwa wanyama au kicho cha hali ya juu kwa Mungu wa mbinguni?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 7:1-17  

 1. Chini ya uongozi wa Samweli Israeli inashuhudia uamsho mkuu wa kiroho na matengenezo. Iliwezekanaje wakati huu waliwashinda maadui zao na kurejesha maeneo yaliyotekwa ingawa hawakuwa na sanduku la agano? Unadhani ni uamsho na matengenezo gani yanahitajiwa leo kanisani kwako?
 2. Kuna jambo gani maishani mwako linaloshuhudia kuwa hata sasa Bwana anakusaidia? Kwa nini Wafilisti walioonekana kama wametubu na kumkiri Mungu wa Waisraeli waligeuka na kupanga kuwashambulia tena Waisraeli? Hii inaeleza nini kuhusu tabia ya mwanadamu?
 3. Katika vita vya kiroho hatuhitaji kupigana kwa nguvu zetu maana Mungu ameahidi kutupigania. Unaamini kuwa kama ukiwa na imani Mungu aweza kuwasikilizisha sauti ya kishindo adui zako na kusababisha wakimbie?
 4. Je, unachukua nafasi ya kuwalilia kwa maombi watu wa Mungu walio katika dhiki kuu? Ikiwa Mungu alisikiliza kilio cha Samweli hawezi kusikiliza cha kwako?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 8:1-22  

 1. Kwa nini swala la Waisraeli kutaka kuongozwa na mfalme lilikuwa baya machoni pa Mungu. Kama viongozi hawafai ilitakiwa wachukue hatua gani muafaka? Kwa nini matendo mabaya yanayotendwa kwa viongozi wa kiroho Mungu anayachukulia kama yametendwa kwake?
 2. Kwa mujibu wa maelezo ya sura hii haifai kujichagulia kiongozi wa kukuongoza bila kumshirikisha Mungu. Unadhani ni njia gani sahihi ya kufanya ili usije ukachagua kiongozi atakayewaletea mateso badala ya baraka? Tamaa ya kutaka kuendesha mifumo ya maisha yetu kama wafanyavyo wale wasio na hofu ya Mungu ipo hata leo hii.
 3. Je kuna ubaya wa kuiga wafanyavyo maadui zetu? Kwa nini Israeli walichoshwa kuongozwa na Mungu? Kwa nini wakati fulani Mungu huruhusu kile tukiombacho hata kama kina madhara kwetu?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMWELI 9:1-27 

 1. Kupotea kwa punda wa Kishi babaye Sauli kunahusianaje na mpango wa Mungu wa kuwapatia Israeli? Je tunapokuwa tunahangaika kumpata kiongozi Mungu huwa ana mtu tayari aliyemuandaa? Kulingana na yale Sauli aliyofanya baadaye na alivyokufa vitani baada ya kugeukia umizimu na nguvu za giza unadhani lilikuwa chaguo sahihi la Mungu?
 2. Sauli kabla hajawa mfalme alikuwa mnyenyekevu pamoja na ukweli kuwa alikuwa nzuri kuliko watu wote. Kwa nini baada ya kuwa mfalme Sauli alipoteza hali hiyo? Watu wanaotabiri yaliyotokea na yatakayotokea (Waonaji au Manabii) walikuwepo nyakati za Sauli na kupitia kwa Samweli Sauli alitambua kuwa punda wameonekana. Je watu hao ni muhimu na wanapatikana hata sasa?
 3. Je dhana ya kuwalipa kwa huduma wanayoitoa kulingana na mawazo ya Sauli na rafiki yake ni sahihi kibiblia? Unaizungumziaje huduma kama ya marehemu pastor Godson wa Hedaru? Kuna haja ya kuwepo mtu atakayechukua nafasi yake?
 4. Kuna ukweli kuwa punda wale walipotea ili Sauli akutane na Samweli na kupewa ujumbe nzito kutoka kwa Mungu utakaobadilisha hatima ya maisha yake na maisha ya taifa la Israeli? Je kuna ukweli kuwa si kila baya linalotokea maishani mwako lina kusudi baya? Mwombe Mungu akusaidie kushukuru kwa kila jambo na kuacha kunung'unikia kila jambo maana lipo lililokusudiwa kukuletea mema.


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 10:1-27   

 1. Huko zamani mtu mmoja tu alikuwa anatosha kumtangaza kiongozi aliyechaguliwa na Mungu kuongoza jumuiya ya kidini (kanisa) tofauti na sasa ambapo kazi hiyo inafanywa na kibaraza cha uchaguzi. Utaratibu huu wa zamani una faida na hasara zip? Je utaratibu huo inafaa kurejewa?
 2. Je, kutiwa mafuta kulikofanywa kwa Sauli kunaweza kufananishwa na kuwekewa mikono kunakofanywa kwa wachungaji, wazee wa kanisa, na mashemasi leo hii? Kusudi la huduma hii ni nini? Je, kuna uwezekano wa kutambua kitakachotokea katika ratiba yako ya siku husika hata kama wewe si nabii? Je Mungu yupo tayari kufanya hilo kwa kila mtu?
 3. Ikiwa kila kinachotokea kilikuwa kimepangwa na Mungu nafasi ya mtu kufanya maamuzi yaliyo tofauti ipo wapi? Je mtu atawajibishwaje kwa kufanya yale yaliyopangwa na Mungu? Sauli alipoanza kutabiri manabii walishikwa mshangao na kuanza kumkejeli. Tunawatia moyo kiasi gani wale wenye karama tulizonazo na wanaotamani kufikia viwango vya utendaji tulivyonavyo?
 4. Sauli hakuwa na kiherehere cha kupenda uongozi au kujitangaza kama inavyotokea kwa baadhi yetu. Hata hivyo wapo wale ambao hawapokei kazi mpaka wabembelezwe. Unadhani Sauli alikuwa wa kundi gani? Unajifunza nini kutoka kwake? Hotuba ya Samweli kwa Waisraeli ilionrsha Mungu ameafikiana na sherehe ya usimikwaji wa mfalme wa kwanza8 wa Israeli?
 5. Je Mungu alikuwa amezira? Matamko yale yalikuwa ya laana au baraka? Kwa nini Sauli alipotambulishwa watu wote walipiga kelele za "mfalme aishi"? Waliridhika na nini kwa mtu huyu wa kabila ndogo ya Benjamini? Wale waliosema hawezi kutuokoa kwa nini wameitwa wasiofaa kitu? Ni kweli hawafai?


MASWALI YA KUJADILI: 1SAMUELI 11:2-15  

 1. Sifa ya kiongozi bora ni kuwa na uchungu na magumu yanayowakabili watu wako na kutafuta njia ya kuwatoa kwenye madhila hayo. Je hasira ni muhimu katika kufanikisha majukumu ya kiongozi? Kwa nini wazee walitoa majibu kwa mfalme wa Amoni aliyetishia kuwang'oa jicho la kuume watu wote wa Israeli bila kumshirikisha mfalme wao Sauli? Je walikuwa hawana imani naye?
 2. Waisraeli waliposikia taarifa za kung'olewa macho walilia sana. Je, kulia unapokuwa na matatizo kunatoa nafasi ya kupata ufumbuzi? Ushindi wa kwanza wa Sauli kama mfalme wa Israeli uliimarisha kukubaliwa kwake. Je Sauli alijiinua kwa ushindi huu au alimtukuza Mungu? Unapofanikiwa kama kiongozi sifa unazielekeza kwa nani?
 3. Je ushindi wako unathibitisha kuwa waliokuchagua hawakukosea au unathibitisha uwezo wa Mungu unaowainua wanyonge? Je watu wanaobeza uwezo wako katika uongoze unawatendeaje wanapokwamisha juhudi zako au unapokuwa umepiga hatua ya mafanikio? Unajifunza nini kuhusiana na namna Sauli alivyowatendea waliokuwa wanambeza?


MASWALI YA KUJADILI: 1 Samueli:12.1-25   

 1. Kufanya tathmini ya uongozi wako kama Samweli (1 Sam. 12:3-4) na Yesu (Mathayo 16:15-16) ni jambo linalosaidia kutambua mapungufu yako kwa lengo la kuyaboresha au kupima mafanikio yako. Unadhani jambo hilo lina msaada katika wakati wetu?
 2. Utaratibu wa kuachiana majukumu unataka kuwepo mwendelezo wa kazi bora zilizokuwa zinafanyika na kutengeneza mazingira bora ya kazi kwa anayeachiwa kijiti. Je katika mazingira unayoishi jambo hili linafanyika kwa ufanisi? Je kunakuwepo na makabidhiano yenye upendo na ari ya kumsaidia aliyepokea kijiti?
 3. Kwa nini Samweli aliamua kuwakumbusha Israeli matendo yote ya Mungu katika nyakati zilizopita katika hotuba yake wakati anakaribia kufa? Ahadi kwa Israeli kuwa "Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu" inasikikaje masikioni mwako wewe unayepitia sasa changamoto za maisha? Je waweza kuidai ahadi hiyo? Je, kuacha kuwaombea watu wa Mungu kwa mujibu wa Samueli ni dhambi?
 4. Unachukua nafasi gani kuwaombea watu wa Mungu maishani mwako? Wanadamu wa leo wamejiundia mifumo fulani ya kuliongoza kanisa la Mungu iliyojikita katika ukabila na ukanda ambapo hujenga misimamo ya kikanisa kutegemeana na tamaduni na mazoea ya makabila yao. Je, dhambi hii ni sawa na dhambi ya Israeli waliojichagulia mfalme na kumweka kando Mungu wa mbinguni? Jambo hili linahafifishaje kazi ya Mungu?
 5. Neno la mwisho la Samweli kwa Israeli ni kuwa "mkiendelea kutenda mabaya mtaangamia". Umelipokeaje onyo hili ambalo linakuja kwako leo. Utakuwa tayari kushirikiana naye ili kukomesha matendo ya dhambi maishani mwako?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 14:1-52  

 1. Kitendo cha Yonathani kuwavukia maadui zao Wafilisti bila kumjulisha mfalme Sauli kilikuwa kitendo cha kishujaa chenye nia ya kusaidia ufalme wa baba yake au kilikuwa kitendo cha uasi? Kitendo cha Sauli kutaka kumwangamiza Yonathani kilitokana na aibu ya kutoshirikishwa na maamuzi ya kushambulia Wafilisti na kutojibiwa kwa maombi yake au kulikuwa na nia ya kuzuia hasira ya Mungu isiwaangukie Israeli yote? Kwa nini Waisraeli walikataa mpango huo?
 2. Kwa nini Yonathani alikuwa tayari kuuawa? Alihisi kuwa ana hatia? Idadi ya watu haijalishi katika kuleta ushindi. Jeshi kubwa la Wafilisti lenye zana bora lilishindwaje na jeshi la watu wawili; Yonathani na mchukua silaha wake? Je sheria ya kuzuia watu wasile siku ya ushindi wa vita ilikuwa ni ya lazima?
 3. Je inafaa kufunga siku ya Sabato? Je ushindi dhidi ya Wafilisti waliowatia hofu Waisraeli ulitokana na Sauli, au Yonathani? Je ni sahihi kumkatalia mtawala anapoonesha dhamira ya kuonea baadhi ya raia wake hata kama kwa kufanya hivyo utakuwa unahatarisha maisha yako?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 15:1-35   

 1. Mungu anafahamu wakati ni njia bora ya kulipiza kisasi cha wale wanaotuonea. Kwa nini kwa kawaida mwanadamu huwa haruhusu Mungu alipize kisasi kwa niaba yake? Kwa nini Sauli aliona vigumu kukiri kuwa hakuitii sauti ya Mungu? Je angekiri asingesamehewa?
 2. Kwa nini watu wengi wanapofanya makossa hupenda waonekane walikuwa na nia njema? Kumleta Agagi mfalme akiwa hai Yerusalemu wakati aliagizwa amuangamize kulikuwa na faida kwa nani? Je tunapofanya kazi ya Mungu kuna uwezekano wa kutafuta sifa?
 3. Je ile mifugo ambayo Mungu aliagiza iteketezwe isingefaa kwa kutolea kafara? Unadhani ilikuwa inakidhi vigezo vya kafara? Je, kukataa neno la Mungu ni sawa na kumkataa Mungu? Kama Mungu si mwanadamu hata ajute (1 Samwel 15:29), ilikuwaje katika (1 Samwel 15:11), anasema najuta kumtawaza Sauli kuwa mfalme?
 4. Je kunahitajika ujasiri kuwakabili watu waliozoea kulitesa kanisa la Mungu? Je watu hao wanahitaji huruma yoyote? Mungu aliagiza Waamaleki wauawe kutokana na ubaya waliowafanyia Waisraeli huko zamani. Je ujumbe huu una faraja ye yote kwako wewe unayeonewa sasa na Mungu kuonekana kana kwamba hachukui hatua ye yote?
 5. Kwa nini kuangamizwa kwa Waamaleki kuliandamana na kuharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo hata vile vyenye matumizi katika maisha? Huu si uharibifu wa mali? Unadhani kwa nini Sauli alimwacha Agagi hai wakati alitakiwa amwangamize? Alimuonea huruma? Kutofikia kwetu mafanikio ya juu katika nyanja mbalimbali kunaweza kuwa kunatokana na kutozingatia maagizo ya Mungu?
 6. Ni mazoea au mahusiano gani ya dhambi ambayo hujayaacha yanayohatarisha hali yako ya kiroho? Kwa nini Sauli alisema 'nimeitimiza sauti ya Mungu' wakati akijua hajafanya hivyo? Kwa nini baadaye alikiri na kusema 'nimefanya dhambi kwa kuihalifu amri ya Bwana'?
 7. Je ni vizuri kwa kiongozi kufanya maamuzi kwa lengo la kufurahisha watu? Ni nini hatari ya kufanya hivyo? Kwa nini kuasi kunalinganishwa na dhambi ya uchawi na ukaidi unalinganishwa na  ukafiri? Je unaweza kufanya vitu vya maendeleo kwa taasisi unayoiongoza na bado ukaonekana hufai?
 8. Je Sauli alikuwa na toba ya kweli? Kwa nini alichana vazi la kuhani? Ilitakiwa afanye nini kama kuhani alionesha kutaka kuondoka wakati yeye akiwa bado anahitaji msaada wake? Ni mambo gani umepanga kuyaangamiza ambayo yamekuwa yakizuia ukuaji wako kiroho? Je unahitaji msaada wa Mungu kuyaangamiza?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 16:1-23 

 1. Ikiwa kiongozi ameonekana kutoyamudu majukumu yake inafaa kumuondoa kabla ya muhula wake? Je kufanya hivyo hakuwezi kuhatarisha maisha ya yule anayejaribu kumuondo? Je ushauri kuwa mfalme Sauli anahitaji mtu wa kumpa tiba ya kiroho itakayomsaidia kumweka sawa kiafya ulikuwa sahihi? Je, Sauli alikuwa anasumbuliwa na kichaa, mapepo, au msongo wa mawazo?
 2. Je hii kazi mpya ya Daudi iliyompeleka ikulu ilikuwa fursa ya kujifunza utawala na maisha kama maandalizi ya kazi yake katika siku za usoni? Sauli aliendelea kufanya kazi ya Mungu huku amekataliwa na nafasi yake kupewa mtu mwingine? Kuna uwezekano wa leo kuwepo watu wanaodhani wanamfanyia Mungu kazi na kumbe walishakataliwa kitambo?
 3. Kwa nini Daudi hakuingia ikulu mara tu baada ya kutawazwa? Daudi alijisikiaje kufanya kazi ya kumtumbuiza mfalme wakati akijua yeye ndiye mfalme aliyetawazwa na anayekubalika na Mungu? Daudi alipata kibali kwa Mungu na kwa mfalme Sauli bila jitihada za wazi za kujipendekeza au kutafuta fursa hizo kama inavyofanywa na watu wengine? Ni nini siri ya kukubalika kwake?
 4. Viongozi wanahitaji washauri wema watakaowasaidia kuhimili mikiki mikiki ya uongozi inayoweza kuwapatia msongo watakaomshauri cha kufanya ili kulinda afya yake? Je huduma hiyo inafanyika kwa ufanisi katika taasisi za kidini na taasisi zinginezo? Je, machapleini wenye mafunzo ya huduma hii wanapewa kipaumbele? Kwa nini uteuzi wa Daudi na kutiwa mafuta kwake kulifanywa kwa kificho na kwa kutunga sababu za uongo? Nini kingetokea kama ingefanyika kwa wazi?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 17:1-58 

 1. Kwa nini maneno 'nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane isipokuwa kijana mdogo asiye na jukumu lolote katika jeshi. Je mfalme Sauli na Abneri mkuu wake wa majeshi walizipokeaje kejeli hizo? Je ni wakati gani unatakiwa kumtetea Mungu na wakati gani anatakiwa ajitetee mwenyewe?
 2. Kwa nini kaka zake Daudi walijaribu kumkatisha tamaa mdogo wao Daudi asifikirie kupambana na Goliath? Waliridhika na dharau wanayofanyiwa Israeli, walitaka kuokoa maisha ya mdogo wao, au walimwonea wivu? Wajibu wa raia mwema kwa kiongozi aliyekata tamaa ni upi? Je, ni kukaa kimya, kumsema pembeni, au kumtia moyo?
 3. Jina la Bwana laweza kuwa silaha vitani? Daudi alijuaje kuwa katika vita ile angeibuka mshindi? Yule ambaye Mungu amemuandaa kuleta ushindi kwa familia, kanisa, na kwa taifa anaweza asishawishi watu kwa mwonekano. Mtu kama huyo anatakiwa afanye nini ili wenzake wajue yeye ndiye chaguo la Mungu?
 4. Unadhani ushindi wa Daudi uliwafurahisha watu wote wa Israeli. Tahadhari gani unatakiwa kuchukua baada ya Mingu kuruhusu ushindi kupitia kwako?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 18:1-30  

 1. Kwa nini Yonathani hakuona umaarufu wa Daudi kuwa tishio kwa nafasi yake ya mrithi wa kitu cha ufalme? Je aliridhika Daudi awe maarufu kuliko yeye? Kwa nini Daudi anaonekana kufanikiwa kwenye kila eneo alilotumika? Hii ni kwa sababu Mungu alimpendelea au kwa kuwa alijituma na kutumia fursa vizuri?
 2. Je wanawake walioimba walijua sifa wanazompa Daudi zinamchonganisha na mfalme Sauli? Je busara ilihitajika katika kumsifu Sauli? Unapokuwa na kiongozi anayependa yeye tu ndiye asifiwe mnafanyaje? Je ilikuwa sahihi kwa Daudi aliye maskini na asiyekubalika kwa mfalme kumuoa binti wa mfalme?
 3. Ukipendwa na binti kutoka familia tajiri na wewe ni maskini utafanyaje? Je utaratibu wa kutoza mahari kwa namna ulivyofanywa na Sauli na namna unavyofanyika leo ni sahihi? Kwa nini mfalme alimuogopa Daudi ambaye ni raia asiye na madaraka ye yote na kwa nini Daudi hakumuogopa Sauli?

 

MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUEL 18:1-30 


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 19:1-24  

 1. Ungejihisi vipi kuwa na rafiki anayekusema vizuri kwa adui zako na aliye tayari kukujulisha njama zinazopangwa kinyume chako? Unafanyaje kuwa na marafiki wa jinsi hiyo? Je kipi kinakupatia maadui zaidi kati ya kutenda mema na kutenda mabaya? Kwa nini watu wengine wanapomchukia mtu kile wanachofikiria ni kumuua tu?
 2. Je kuua kunaweza kuwa ufumbuzi wa usumbufu wanaoupata kuhusu mtu huyo? Kwa nini Mikali mkewe Daudi na binti wa Sauli alikubali kuhatarisha maisha yake kwa kumuokoa Daudi na kumdanganya baba yake. Je upendo wa mume na mke una nguvu kuliko upendo wa mtu na wazazi wake?
 3. Kwa nini Samueli baada ya kushitakiwa na Daudi juu ya vitendo vya Sauli na nia yake ya kutaka kumuua hakwenda kwa Sauli kumuonya kama alivyokuwa akifanya huko nyuma? Kwa nini kila jitihada za kumkamata Daudi zilipokuwa zinagonga ukuta hazikumshitua Sauli kuwa Daudi hakuwa na hatia na ya kwamba haukuwa mpango wa Mungu afe?
 4. Kwa nini Sauli tofauti na wenzake wengine wote alitabiri akiwa amelala uchi mchana kutwa na usiku kucha? Unadhani ilikuwa sahihi kwa kiongozi kumuandama raia wake asiye na hatia bali anayeonekana kuwa tishio kwake?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 20:1-42  

 1. Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Unazungumziaje urafiki wa Yonathani na Daudi? Unaye rafiki wa namna hiyo maishani? Yesu aliyatoa maisha yake ili mimi na wewe tupone. Je una mpango wa kumfanya rafiki yako wa kudumu?
 2. Utafanyaje ukigundua ndugu zako wanafanya njama za kumwangamiza rafiki yako ili kulinda nafasi yako ya ajira? Utafanyaje utakapogundua watu fulani wanaojifanya wanakupenda sana kumbe wanapanga njama juu yako?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 21:1-15   

 1. Unadhani Daudi alijihisi vipi kuona kuna kiongozi anayetambua umuhimu wake na mchango wake kwa taifa? Je kuna haja ya kumtambua na kujaribu kumhifadhi kiongozi asiyekubalika na kiongozi mkuu kwa chuki binafsi zisizo na maslahi kwa taasisi yenu? Je Daudi na wenzake (ambao hawakuwa makuhani) walikuwa na sifa ya kuila ile mikate ya wonyesho?
 2. Pakiwa na mtu aliye katika hatari ya kufa kwa kukosa chakula naweza kumpa mikate iliyobaki kwenye Meza ya Bwana? Kujitenga na wanawake (kutotenda ngono) ilikuwa sharti mojawapo la kushiriki ibada inayohusisha mikate ya wonyesho. Je hii ni kumaanisha wanawake ni najisi? Je sheria hii ipo leo au imekoma?
 3. Upanga wa Goliati ulihifadhiwa kama kumbukumbu za kihistoria kwa ajili ya vizazi vijavyo. Unadhani tunafanya jitihada za kutosha kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria za kanisa letu? Nini kifanyike ili kumbukumbu hizo zisipotee? Je katika kukabiliana na adui kuna wakati mbinu ya Daudi ya kujifanya kichaa huwa ni ya lazima?
 4. Yesu aliposema kuweni wapole kama huwa na werevu kama nyoka alimaanisha hiki alichokifanya Daudi. Ukiwa vitani na ukajivika majani ili adui asikutambue utakuwa unafanya dhambi ya kudanganya?


MASWALI YA KUJADILI: 1 SAMUELI 22:1-23  

 1. Daudi aliwakumbuka wazazi wake hata katika kipindi anachopitia machungu na magumu katika maisha kama Yesu alivyomkumbuka Mama yake pale msalabani. Umefanya nini kuwapatia wazazi unafuu wa maisha? Au unangoja siku mambo yako yatakapokaa vizuri? Kwa nini Daudi alipata waungaji mkono wengi kiasi hicho?
 2. Je ni kwa kuwa alikuwa mtu wa watu au waliomuunga mkono walikuwa wanatofautiana na Sauli? Kuwepo kwa Sauli madarakani kunawanufaishaje watu wa kabila lake la Benjamini? Hali hiyo ya viongozi kupendelea watu wa makabila yao bado ingalipo leo. Je inasaidia kuchochea maendeleo au kuyarudisha nyuma?
 3. Je ilikuwa sahihi kwa Ahimeleki - kuhani mkuu kutoa upanga na chakula kwa Daudi na watu wake bila kumjulisha au kutaka ushauri wa mfalme Sauli? Je hukumu aliyopewa na mfalme ilikuwa ya haki na kwa maslahi ya nchi? Ni nani kati ya Doegi aliyetii amri ya mfalme ya kuua makuhani na askari walinzi waliokataa kutii agizo la mfalme aliyekuwa ametenda jema machoni pa Mungu?
 4. Utatambuaje amri ya mkuu inayostahili kutiiwa na ile isiyostahili? Je Doegi atakuwa na hatia kwa kutekeleza agizo la mkuu? Je Ahimeleki kuhani mkuu alikufa kifo cha kishujaa au cha kizembe na cha usaliti? Je uzembe wa Daudi umechangia kifo hicho?