Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

KUUENDEA UZEE MWEMA

  

KUUENDEA UZEE MWEMA

Uzee unatajwa kuwa na changamoto nyingi za kimwili na hata kiakili kutokana na kushuka kwa viwango vya kinga ya mwili na kumbukumbu. Kwa sababu hiyo mchango wa wazee huonekana kuwa mdogo katika familia na katika kanisa na mara nyingi kuonekana mzigo au kero kwa wanafamilia. (Mhubiri 12:1-4) “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo. Kabla jua, na nuru, na mwezi, Na nyota, havijatiwa giza; Kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua; Siku ile walinzi wa nyumba watakapotetema; Hapo wenye nguvu watakapojiinamisha; Na wasagao kukoma kwa kuwa ni haba; Na hao wachunguliao madirishani kutiwa giza; Na milango kufungwa katika njia kuu; Sauti ya kinu itakapokuwa ni ndogo; Na mtu kusituka kwa sauti ya ndege; Nao binti za kuimba watapunguzwa.”

Mambo yanayochangia uzee mbaya

Uzee mwema hauji wenyewe bali huandaliwa. Maisha yenye mshikamano wa kifamilia na kuendelea kumtumainia Mungu na maisha yanayozingatia maadili na kanuni za afya ndiyo siri kubwa ya kuwa na uzee mwema. Ni jambo la kusikitisha kuumaliza mwendo vibaya kwa kumuacha Mungu na kuyarudia matapishi. (2 Timotheo 4:7-8) “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.” Wakati wa uzee watu wengi hujaribiwa kuwasahau wenzao waliohangaika nao katika kutafuta Maisha hasa pale wanapokuwa wamefanikiwa kiuchumi. (2 Petro 2:22) “Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.” Hali hiyo huwatesa sana Watoto ambao hukosa mwelekeo wa Maisha na msaada wa ushauri ili kuzifikia ndoto zao za Maisha.

Mambo yanayochangia uzee mwema

Biblia inawataja wazee kadhaa walioufikia uzee mwema. Kwa namna fulani Mungu anakusudia sote tuufikie uzee mwema. (Mwanzo 15:13-15) “Bwana akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, -watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema.” Pamoja na kurukaruka huku na huko, Ibrahimu alikufa katika uzee mwema. Mungu alitimiza ahadi yake. (Mwanzo 25:8) “Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake.”

Ibrahimu hakumwacha mkewe licha ya misukosuko ya kuzaa na Hajiri na kuchelewa kupata mtoto. (Mwanzo 23:1-2) “Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba ndio umri wake Sara. Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea.” Ibrahimu alikuwa na uwezo wa kiuchumi wa kuendeshea mazishi ya mke wake. (Mwanzo 23:17-20) “Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango iliyokuwamo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake. Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Na lile shamba, na pango iliyomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia.”

Uzee na ugane usikuzuie kuhudumia Watoto

Ibrahimu katika hali yake ya ugane alifanikiwa kumuozesha kijana wake Isaka. Kuondokewa na mwenzi wako kusihafifishe wala kukwamisha huduma unazotakiwa kuzitoa kwa Watoto wako. Wala dhana ya kuwa ukifiwa na mkeo ni lazima uoe haraka ili mambo yako yakuendee vizuri haipaswi kuchukuliwa kama sheria. (Mwanzo 24:1-4) “Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.”

Suluhisha migogoro ya familia kabla hujaumaliza mwendo

Migogoro ya kifamilia itafutiwe ufumbuzi kabla hujaumaliza mwendo. Pande zinazotofautiana ziletwe pamoja na kama mzazi aliwakosea Watoto asisite kuwaomba msamaha. Kumbuka kuwabariki wanao unapoona mwelekeo wa kutoendelea kuishi. (Mwanzo 49:1-2) “Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu.” (Mwanzo 49:22-29) “Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matwi yake yametanda ukutani. Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli, Naam, kwa Mungu wa baba yako atakaye kusaidia; Kwa mibaraka ya mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo chini, Mibaraka ya maziwa, na ya mimba. Mibaraka ya baba yako Imepita mibaraka ya milima ya kale, Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake.”

Wapatanishe wanao ukiwa hai

Kwa kadri inavyowezekana wapatanishe wanao waliokuwa kwenye ugomvi. Na kwa kadri itakavyowezekana walio nje ya familia uwalete nyumbani bado ukiwa hai. Hekima huhitajika katika kuwaleta nyumbani Watoto waliozaliwa nje ya ndoa. Watoto ambao si wa familia ambao walikuwa msaada kwa familia wapewe heshima na haki wanayostahili. (Mwanzo 25:8-9) “Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake. Isaka na Ishmaeli wanawe  wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre.” (Mwanzo 35:29) “Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika.”

Warithishe wanao utajiri wako

Watoto waliofiwa na wazazi hupata changamoto katika kujipanga na kuanza upya kimaisha. Wazazi wawawekee Watoto wao mali ya kurithi Mwanzo 25:5 Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo.” Hata hivyo urithi wa maana na udumuo ni tabia ya kujituma kufanya kazi uliyowajengea, na kuishi vizuri na watu. Urithi mwingine usioweza kufilisika ni elimu.

Jiandalie utakapomalizia mwendo

Ni jambo muhimu kuandaa mahali utakapomalizia uzee wako. Katika jamii nyingi mtoto wa kwanza wa kiume au wa mwisho wa kiume huandaliwa kuwatunza wazazi watakapokuwa wazee. Hata hivyo ni vema kumchagua yule mwenye mapenzi ya dhati na wazazi na yule ambaye mzazi mwenyewe anampendekeza. Mahali pa kumalizia uzee wenu pangekuwa makazi yenu yenye nafasi ya kufanya ufugaji na bustani na palipo Jirani na huduma za afya na za kiroho. Pale inapowezekana wazee wawe kwenye mpango wa bima ya afya ili matibabu yao yasikwame kwa kukosa fedha za kulipia gharama.

Watoto wakubaliane juu ya matunzo ya wazazi wao

Katika familia za Kiafrika wazee wanatunzwa na familia zao wakati katika nchi za wenzetu wazee hutunzwa katika vituo vya kulelea wazee. Utaratibu wa kuwalea wazee katika vituo maalum na watu wasio ndugu zao umelalamikiwa na wataalam wa afya na wa saikolojia kuwa unawafanya wazee hao kujihisi wapweke kwa kukosa upendo wa ndugu zao. (Mwanzo 47:12) “Naye Yusufu akawalisha babaye na nduguze na nyumba yote ya babaye, kwa kadiri ya hesabu ya watoto wao.”

Wazee wawe washauri wema

Wazee Pamoja na mapungufu yao ya kiafya ni hazina katika jamii wanazotoka. Wazee wanategemewa kuwa washauri wema wa jamii na uongozi uliopo madarakani. (Kutoka 18:13-17) “Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni.Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.”

Wazee walee ndoa changa

Wazee wakitumia uzoefu wao wanaweza kuwa msaada kwa kanisa na kwa uongozi kwa kupitia busara na imani zao huku wazee wa kike wakiwasaidia wanawake wenye ndoa changa au wanaotarajia kuingia kwenye ndoa ili wawapende waume zao. (Tito 2:1-5) “Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe.”

Wazee wastahiwe na kuheshimiwa

Wazee wanapokosea wasaidiwe kwa tahadhari kubwa ili kuepuka kuwavunjia heshima. Wazee wenzake waone namna ya kumsaidia badala ya viongozi vijana kujibebesha jukumu hilo gumu. (Mwanzo 9:20-25) “Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. Akasema,Na alaaniwe Kaanani;Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. (1 Timotheo 5:1) “Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu.”

Wazee wawe watu wa maombi

Wazee wana fursa nzuri ya kukumbuka njia yote ambayo Mungu amewaongoza na kumshukuru. Katika kuomba kwao wamkumbushe Mungu ahadi zake. Zaburi 71:9 Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.

Kufanya kazi ya Mungu na kujitunza kiafya huwafanya wazee kutozeeka. Mungu aweza kuurejesha ujana. Zaburi 103:5 Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai.” Zaburi 71:9 Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.” Zaburi 92:14 Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.