NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: EZRA 1:1-11
- Hakuna aliye madarakani ambaye Mungu hakutambua tangu awali kuwa angekuja kuwa madarakani. Dhana hiyo ina ukweli gani unapoangalia kuinuka kwa Koreshi mfalme wa Uajemi? Kwa nini Mungu alimtumia mtawala wa kipagani kuagiza mji wa Yerusalemu ujengwe tena? Je kwa matamko yake Koreshi alikuwa anakiri Mungu wa Yuda ni mkuu kuliko mungu wake? Iliwezekanaje basi kwa mungu mdogo kutawala raia wa Mungu mkubwa?
- Palihitajika Mungu kuamsha roho za Wayahudi ili wawe na ari ya kurejea Yerusalemu na kuujenga upya mji. Je hiyo inamaanisha kama Mungu asingeamsha mioyo yao wasingetamani kurudi nyumbani? Kama kurudi nyumbani kwa Wayahudi kulihitaji kuamshwa je kurudi kanisani kwa wale waliorudi nyuma au kutamani kwenda mbinguni kunahitaji kuamshwa na Mungu?
- Kujengwa upya kwa hekalu lililoharibiwa la mwili wako kunahitaji tangazo la mfalme wa mbinguni? (Zaburi 71:3). Je Yesu alitoa malipo gani ili hekalu lako lijengwe upya? (1Petro1:18-19; 1Kor. 7:23). Kuna mlingano gani kati ya kuondoka kwa Waisraeli utumwani Misri na kuondoka kwa Wayahudi utumwani Babeli? (Kutoka 3:20-22). Kwa nini Wamisri na Wakaldayo walikuwa tayari kuwasaidia watu wa Mungu mali za kwenda kuujengea ufalme wa Mungu? Unaiona hali hiyo ikijitokeza mahali ulipo?
- Je kulikuwa na umuhimu wowote kwa Koreshi kurejesha vyombo vya nyumba ya Bwana vilivyoporwa na mtangulizi wake kwenye hekalu la Yerusalemu? Je kulikuwa na haja gani ya kuhesabiana vyombo vinavyorudishwa? Je ni wakati gani Mungu alijidhihirisha ni mkuu zaidi wakati vyombo vyake vilipokuwa vinaporwa au wakati vilipokuwa vinarudishwa? Je, unao ushuhuda wowote wa namna mali yako au ya kanisa ilivyorejeshwa kwa namna ya kushangaza nawe ukamtukuza Mungu?
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 2:1-70
- Unadhani Mungu aliruhusu Wayahudi waende utumwani Babeli ili wakafundishe au wakafundishwe au yote mawili? Unadhani wanadamu baada ya kukaa kwenye dunia ya dhambi kwa takribani miaka 1,000 tumekuwa bora zaidi kuliko tulivyokuwa kabla ya dhambi? Je Mungu alipata faida yoyote kwa Wayahudi kukaa uhamishoni Babeli? Je Mungu anawachukuliaje wale wanaowalea watu wake walio kwenye mazizi mengine (vikundi vya dini) yanayopotosha ukweli wake? (Yohana 10:16).
- Unadhani kuhesabiwa kwa watu kulilenga kubaini wenye nasaba ya Yuda na wanaostahili kurudi Yuda? Kulikuwa na hatari gani kama wasingehesabiwa? Je mtu aweza kuwa na watumishi wa kike na wa kiume na hali yeye mwenyewe akiwa mtumwa? Kwa nini watumwa waliokuwako Babeli walianza kubaguana walipokuwa wanakaribia kurejea nyumbani? Unaona hiyo ikijitokeza kwenye kanisa lako?
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 3:1-13
- Kukusanyika pamoja kama mtu mmoja kunamaanisha nini? Unadhani ni nini kiliwashika hata wakakusanyika pamoja kama mtu mmoja? Kwa nini walitangulia kumtolea Bwana sadaka kabla hawajaweka msingi wa hekalu? Je ni kwa nini Koreshi aliendelea kuhusika na ujenzi wa hekalu la Yerusalemu?
- Kwa nini waliotoka uhamishoni walianza kumtolea Bwana sadaka siku ya kwanza ya mwezi wa saba? Kwa nini Yerusalemu panaitwa nyumbani kwa Mungu? Kwa nini watakaokombolewa wanatambuliwa kama watu wa nyumbani mwake Mungu (Waefeso 2:19)? Kwa nini kazi ya usimamamizi wa nyumba ya Bwana ilihitaji Walawi wenye miaka ishirini au zaidi?
- Kwa nini nyimbo za kusifu zinapatikana zaidi kwenye nyimbo zetu za vitabuni kuliko katika nyimbo za kwaya zetu za makanisani? Je kusifu kumepitwa na wakati? Kumhimidi Bwana kwa kupaza sauti na kupiga kelele kuna umuhimu gani katika uimbaji? Kwa nini kwenye ujenzi wa nyumba ya Mungu huwepo wale wenye kupaza sauti kwa furaha na wale wenye kupaza sauti kwa huzuni?
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 4:1-24
- Kwa nini adui wa Yuda na Benyamini walitaka kushiriki kazi ya ujenzi wa hekalu la Yerusalemu? Kwa nini kazi hiyo wasiifanye wenyewe wakati Yuda na Benjamini wakiwa hawajarudi toka uhamishoni? Hiyo inakufundisha nini juu ya watu usiowajua wanaotaka kukusaidia? Je ni salama siku zote kuwakubalia watu kama hao?
- Watu waliokuwa wamejitoa kusaidia kujenga hekalu waliwezaje kugeuka na kuanza kuwasumbua waliokuwa wanaendelea kujenga hata kuwadhoofisha? Mchumba anayegeuka kuwa adui mkubwa baada ya kukataliwa hiyo inaashiria alikuwa na upendo mwingi au hakuwa na upendo kabisa?
- Walioandika mashtaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu kwa nini hawakufanya hivyo mara tu walipoanza kujenga lakini wakasubiri hadi ujenzi ulipokuwa umeanza kushika kasi? Walioshitaki kuwa mji wa Yerusalemu unaojengwa ni mji mwasi walisahau kwamba watawala hao wa Uajemi ndiyo walioamuru kwamba ujengwe?
- Je haiwezekani kuwashawishi wengine kuwa wewe ni mtu mwema bila kwanza kuwapaka matope watu wengine? Tabia ya kujipendekeza kwa watawala na kuchongea wengine inatokana na nini? Ukipewa taarifa kuwa mtu fulani ni mbaya wako wajibu wako wa kwanza ni upi? Anayekwamisha kazi ya Mungu kwa tuhuma za uongo Mungu anamchukuliaje?
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 5:1-17
- Je ukijua haki yako ya kufanya unachofanya na kisha mtu asiye na mamlaka yoyote akakutishia uache kufanya utamsikiliza na kumtii? Je kuna nyakati katika maisha unastahili kuwa mbishi? Yesu aliposema akupigaye shavu la kuume mgeuzie la pili alimaanisha tuwe tayari kuonewa? Je viongozi wa Yuda na Yerusalemu waliposimamishwa kujenga kwa amri ya mfalme Artashasta walipaswa kufanya nini?
- Viongozi wa kiroho kama manabii walifanya sahihi kuwatia moyo viongozi kuendelea na ujenzi wa hekalu licha ya kusitishwa na mfalme Artashasta? Je, unadhani kuna wakati woga umekwamisha kazi ya Mungu? Kwa nini ujenzi wa nyumba nyingi za ibada unachelewa kukamilika?
- Waraka uliotumwa kwa mfalme Dario ulisaidia kueleza umuhimu na uhalali wa ujenzi wa hekalu unaoendelea Yerusalemu. Kama wanaoshitaki wanatambua nyumba inayojengwa Yerusalemu ni ya Mungu mkuu kwa nini wanahangaika kushindana naye? Je kuna wakati anayekuchongea hukusaidia kukusafishia njia?
NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: EZRA 6:1-22
- Utaratibu wa kutunza kumbukumbu ulikuwepo tangu zamani. Mwanadamu ana kawaida ya kusahau. Kumbukumbu zilisaidia kubaini ukweli juu ya uhalali wa ujenzi uliokuwa ukiendelea Yerusalemu. Utunzaji wa kumbukumbu husaidia katika kutatua migogoro.
- Haki ya mtu haiwezi kupotea lakini inaweza kucheleweshwa. Kuna wakati mchakato wa kutafuta haki huwa wa muhimu ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro uliodumu kwa muda mrefu. Utawala wa Babeli ulitaka kuonesha kuwa unathamini juhudi za watendaji wake katika kuutakia mema utawala wake na unajali pia haki za raia wake. Ubabe katika mazingira hayo usingeweza kuleta suluhu ya kweli.
- Kuna wakati waliotuhumu hujikuta wakipewa majukumu ya kuwahudumia waliowatuhumu na kuhakikisha wanafanikisha majukumu yao bila kubugudhiwa. Huo ndiyo wakati waliokupiga kibuti hukupigia saluti.
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 7:1-28
1, Kwa nini mwandishi ameielezea nasaba ya Ezra hadi kufikia kwa Haruni Kuhani Mkuu? Alikuwa anatafuta kuhalalisha kitu gani? Kabla hajaitwa kwa kazi ya ukuhani Ezra alikuwa amefanya maandalizi gani? Unadhani wanaotamani kufanya kazi ya Mungu kwa kudumu (on permanent basis) wanatakiwa kufanya maandalizi gani?
- Mwandishi alikusudia nini aliposema Ezra alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa? Ilikuwaje mfalme akamjalia Ezra matakwa yake yote hata yeye mwenyewe kuruhusu hazina yake kutumika kununua sadaka zinazohitajika kutolewa kwa madhabahu ya nyumba ya Mungu iliyopo Yerusalemu? Je fedha ya kupewa na mtawala wa kipagani yafaa kununulia sadaka? Je sadaka hiyo itapokelewa na Mungu?
- Safari ya Ezra kutoka Babeli hadi Yerusalemu ilichukua miezi mitano. Je umeiona Roho ya kujitoa ya Ezra? Unadhani kwa namna Ezra alivyokubalika kwa mfalme, angeomba apewe nafasi kubwa katika utawala wa Babeli asingepata? Unaweza kumfananisha Ezra na Yesu aliyejitoa kuja kuwatumikia ndugu zake walio duniani?
- Artashasta anajitambulisha kama mfalme wa wafalme. Je unadhani anatambua kuwa Mungu wa Wayahudi ndiye mfalme wa wafalme? Unadhani ni kwa nini anaamrisha kila neno litakaloamriwa na Mungu wa mbinguni na litendeke? Je mfalme Artashasta anatambua Mungu wa mbinguni ndiye Mungu wa Wayahudi? Unadhani watu wanamheshimu Mungu wako au wanamdharau?
- Je amri ya mfalme Artashasta ya kutaka wote wasiotaka kuzitenda sheria ya Mungu wa Ezra wauawe, au wahamishwe, au wanyang'anywe Mali zao, au wafungwe ilikuwa ya halali? Kama leo watawala wangeweka sheria kama hiyo kungekuwa na watu wasiomtii Mungu?Unadhani mfalme Artashasta alikuwa anampenda Mungu au alikuwa anamuogopa? (Ezra 7:23). Kipi sahihi kumpenda Mungu au kumuogopa?
- Je ilikuwa halali kwa mfalme Artashasta kutowalipiza kodi makuhani na watumishi wa kiroho? Kutokana na mchango wao katika kuituliza jamii unadhani ni busara kwa viongozi wa kiroho kutokatwa kodi kwenye mishahara au posho zao?
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 8:1-36
- Zoezi la Ezra la kuwahesabu watu kwenye mto unaotelemkia Ahava ulilenga nini? Kwa nini hakufanya ukaguzi wa watu kabla ya kuanza safari? Kwa nini idadi inahusu wanaume tu na haitaji wanawake? Umuhimu wa Walawi ulikuwa upi katika uhamisho huo hata ikabidi warudi kuwachukua? Je unadhani kuna watu ambao ni muhimu kuwa nao ili taasisi ya kidini itimize kwa ufanisi majukumu yake kwa Mungu na kwa jamii?
- Je kufunga kulikofanywa na watu wa uhamisho penye mto Ahava kulikuwa kwa lazima? Je kiongozi anaweza kuwaamrisha watu wafunge au jambo hilo linatakiwa mara zote lifanywe kwa hiari ya mtu? Ilikuwa busara kwa Ezra kutomwomba mfalme askari wa kuwalinda njiani huku wakiwa na mali nyingi za thamani? Je kuna wakati tunatakiwa kujizuia kuomba msaada ili kulinda heshima yetu na heshima ya Mungu wetu?
- Je ni usalama kuacha mali ya thamani mikononi mwa wasaidizi wako ili waisimamie? Utajuaje kama hawatakuwa na tamaa na kuanza kuitumia kwa matumizi yao binafsi? Unawazungumziaje wale wasiowaamini wasaidizi wao na hivyo kuhodhi mali zote za thamani wao wenyewe wakihofia kuwa wengine hawatakuwa waaminifu kama wao?
- Je ni usalama kuacha mali ya thamani mikononi mwa wasaidizi wako ili waisimamie? Utajuaje kama hawatakuwa na tamaa na kuanza kuitumia kwa matumizi yao binafsi? Unawazungumziaje wale wasiowaamini wasaidizi wao na hivyo kuhodhi mali zote za thamani wao wenyewe wakihofia kuwa wengine hawatakuwa waaminifu kama wao? Njia ipi ni sahihi katika kuthibiti wizi
- Mungu aweza kutuokoa na mkono wa adui na mtu mwenye kuvizia njiani hata kama hatuna silaha mkononi? Nini hutokea kwa adui pale mkono wa Mungu unapokuwa pamoja nasi? Je ni sahihi kuajiri mlinzi katika mazingira yanayoashiria kutokuwepo usalama au hiyo ni dalili ya kukosa imani kwa Mungu?
MASWALI YA KUJADILI: EZRA 9:1-15
- Hao wanaoitwa mashehe hapa ni nani? Mbegu takatifu haikutakiwa kuchanganyika na mbegu za watu wa nchi. Unazungumziaje mbegu ya binti wa nchi ya Ruth Mmoabu iliyochanganyika na mbegu takatifu na kuwepo kwenye ukoo mtakatifu ambapo Yesu alizaliwa?
- Kwa nini Ezra alishangazwa na taarifa kuwa makuhani wamewatwaa binti za watu na kuwafanya wake zao? Iliwezekanaje apitwe na tukio la makuhani kuoa binti wa nchi na aje kuzifahamu habari hizo baadaye sana? Unadhani makuhani hawa walikuwa wanajua unyeti wa kazi waliyopewa?
- Je kuna umuhimu gani wa kukunjua mikono mbele za Mungu wakati wa kuomba? Je, inawezekana shida tunazozipitia wanadamu zimelenga kutuonesha makosa yetu ili tutubu? Ezra anaposema Mungu ametupa msumari katika mahali pake patakatifu anamaanisha nini? Je kuziacha amri za Mungu kwaweza kuleta madhara gani kwa jamii ya wanadamu?
- Je kuoana na wanaotenda machukizo kwaweza kumkasirisha Mungu na kuleta maangamizo hata pasisalie mabaki au mtu wa kuokoa? Biblia inaposema siku za mwisho watu watakuwa wakioa na kuolewa kama wakati wa Nuhu inamaanisha watu wataoana bila kuzingatia maagizo ya Mungu? Je hali hiyo unaiona leo?