MASWALI YA KUJADILI: 1 YOHANA 1:1-10
- Kwa nini kusema kwamba hatuna dhambi ni kujidanganya wenyewe? Je moyo unashiriki kwa kiasi gani katika udanganyifu huo? Neno la Mungu linatusaidiaje kujitambua kuwa tuna dhambi? Hilo lililokuwako tangu mwanzo na lililokuwako kwa Baba ni nini? Kwa nini Yesu anaitwa uzima?
- Kuwapelekea watu habari njema ya wokovu kunaletaje furaha kwa wapelekaji pia? Kwa nini nyakati fulani wapelekao habari njema huonekana wasio na furaha? Je, furaha itaendelea kudumu kwa wapelekao habari njema hata pale habari hiyo inapokataliwa au watakapotendewa vibaya? (Mathayo 5:12).
- Kwa nini dhambi nyingi hufanyika gizani? Kama Mungu ni nuru ni nani aliumba giza? Biblia inaposema kuna matendo ya giza na ya nuru inamaanisha nini? Kwa nini damu ya Yesu yatusafisha dhambi yote pale tunaposhirikiana sisi kwa sisi na tunapoenenda nuruni?
MASWALI YA KUJADILI: 1 YOHANA 2:1-29
- Kipi rahisi kati ya kutenda dhambi na kuomba msamaha? Je wanaojitanabaisha kuwa hawatendi dhambi huwa wepesi wa kukiri makosa na dhambi? Kwa nini inakuwa hivyo? Kwa nini Yesu Kristo pekee ndiye mwenye uhalali wa kutuombea?
- Kwa nini kushika amri ni dalili inayowatambulisha wale wanaomjua na wanaompenda Yesu? (Yoh. 14:15) Kwa nini kudai unamjua Yesu na huku huzishiki amri zake kunafaninishwa na kusema uongo?
- Kwa nini ni vigumu kumpenda Mungu na huku unaipenda dunia? Unaiona dalili za watu wa Mungu kuipenda dunia hasa katika siku hizi za mwisho? Nini kifanyike kuzuia hali hiyo isiendelee?
MASWALI YA KUJADILI: 1 YOHANA 3:1-24
- Kuitwa kwetu mwana wa Mungu kunaandamana na upendeleo upi ambao hapo awali hatukuwa nao? Je hadhi ya Yesu ya kuitwa Mwana wa Mungu inafanana na hadhi yetu ya kuitwa wana wa Mungu?
- Dhambi inatafsiriwa kama uasi au kama ilivyo katika lugha ya kiingereza "Lawlessness" ambayo kwa tafsiri rahisi ni hali ya kutokuwa na sheria. Je ni kweli kuwa dhambi haiwezi kuwepo kama hakuna sheria? (Warumi 7:7). Je Biblia inaposema hatupo chini ya sheria inamaanisha hatuwajibiki kutii sheria?
- "Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi." Unadhani shida ipo wapi kwa wale Wakristo wanaoendelea kutenda dhambi. Paulo alipokuwa anasema "ndani yangu halikai jambo jema" alikuwa anazungumzia uzoefu wa Mkristo au wa mtu ambaye hajamjua Kristo? (Warumi 7:18).
- Tunathibitisha upendo wetu kwa binadamu pale tunapoutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Neno "kuutoa uhai" hapo linawakilisha kitendo gani?
MASWALI YA KUJADILI: 1 YOHANA 4:1-21
- Kwa nini tunatahadharishwa kutoamini kila roho? Unatumia njia gani kuzijaribu hizo roho ili kubaini ukweli? Nini sifa za manabii wa uwongo na manabii wa kweli? Kwa nini kila Roho inayokiri Kristo alikuja katika mwili imetokana na Mungu? Sifa za Mpinga Kristo ni zipi? Huyo aliye ndani yao anayemzidi huyo aliye katika ulimwengu ni nani?
- Kigezo cha kumtambua aliyezaliwa na Mungu na anayemjua Mungu ni nini? Roho ya upotevu ina kawaida ya kutosikia. Unadhani kutosikia huku kunatokana na nini? Je inawezekana sisi wenyewe kupendana kama hatumpendi Mungu? Je inawezekana kumpenda Mungu kabala hatujapokea upendo kutoka kwake?
- Kwa nini kulifahamu pendo la Mungu hakutoshi ni mpaka uliamini pendo hilo? Kwa nini pendo lililokamilika ndani yetu linatupa ujasiri siku ya hukumu? Kwa nini pendo lililokamilika huitupa hofu nje?
MASWALI YA KUJADILI: 1 YOHANA 5:1-21
- Kwa mujibu wa 1Yohana 5:3, kumpenda Mungu ni lazima kuandamane na kuzishika amri zake. Amri hizo tunazoagizwa kuzishika ni zipi?
- Warumi 8:7 inakuambia ile nia ya mwili haiitii sheria ya Mungu wala haiwezi kuitii. Nini kimefanya sheria (amri) katika 1Yohana 5:3 iwe si nzito? Je wanaofundisha na kujizoeza kutii amri za Mungu ni adui wa Mungu? (Mathayo 5:19).
- Kwa mujibu wa 1Yohana 5:12 ni kuwa yeye amwaminiye Mwana yaani Yesu anao uzima wa milele. Je wale wasiomwamini Yesu hawawezi kuwa na uzima wa milele. Kama Yesu ametajwa kwenye Kuraani mara nyingi kuliko mtume Mohamadi (SAW) hiyo inaashiria Mungu alitaka Waislamu wamuamini Yesu ili waokolewe?
- Utajuaje kuwa unachoomba kipo kulingana na mapenzi ya Mungu? Je kuna wakati unaomba jambo na huamini kuwa utalipata? Utafanyaje kubadilisha hali hiyo?