NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: NEHEMIA 1:1-11
- Nehemia alikuwa mtumishi wa Mungu na mtumishi katika ofisi ya mfalme wa Babeli mwenye uchungu na kazi ya Mungu. Akiwa kama mnyweshaji wa mfalme alikuwa akifuatilia madhila yanayowapata watu wa Mungu. Wapo wanaotambua kuwa wapo kwenye nafasi walizopo ili kulisaidia kanisa la Mungu. Na hawaoni hofu au unyonge kujitambulisha kama watu wa Mungu.
- Kuna nyakati kazi ya Mungu yaweza kurudishwa nyuma sana kutokana na hila za Shetani na vibaraka wake. Taarifa za kubomolewa kwa kuta zinaumiza mioyo ya wale waliojituma kufanya kazi ya Mungu kama zinavyouma taarifa za ufujaji au upotevu wa fedha za kanisa. Katika mazingira hayo watu waaminifu wa Mungu hujiuliza Mungu wa agano yu wapi? Kulia na kulalamika pekee hakuwezi kutosha. Panahitajika maombi ya kufunga na ya dhati.Unapokuwa na matatizo katika kuendesha kazi ya Mungu usikae nayo bila kuwajulisha wadau wenye mzigo wa kazi kwa mashauriano na ufumbuzi. Matatizo yavkanisa hayapaswi kuatamiwa na wachache kana kwamba ni yao peke yao. Kwa kadri inavyowezekana yapelekwe panapohusika na hatua zichukuliwe haraka. Kazi ya Mungu itafanikiwa zaidi pale uwazi unapotawala.
- Wale watumishi wanaofurahi kulicha jina la BWANA wanapaswa kuamka na kumkumbusha Mungu ahadi zake juu ya kanisa lake linalodhulumiwa kila kukicha. Wanapaswa kuliamsha kanisa kwa toba ya mambo ya hovyo yaliyomkasirisha Mungu yaliyotendeka siku zilizopita ili Mungu awe tatari kutembea tena na kanisa lake. Bila toba ya dhati kuna mambo hayataweza kubadilika.
MASWALI YA KUJADILI: NEHEMIA 2:1-20
- Mwezi wa Nisani ni mwezi gani kwa leo? Kwa nini uliitwa mwezi wa Nisani? Je kuonyesha huzuni wakati wa kumhudumia mfalme ni tabia inayokubalika? Je huzuni ya moyo yaweza kuzuilika isionekane nje? Maisha yanapokuwa yamekunyookea unawachukuliaje ndugu zako wanaoendelea kuteseka? Ni nani wenye nafuu kati ya wale wanaoteseka wakiwa wametoka nchi ya utumwa na wale wanaoishi raha mstarehe wakitumika kwenye nchi ya utumwa?
- Nehemia anahuzunika kwa kuwa mji ulio mahali pa makaburi ya baba yake unakaa ukiwa na malango yake yameteketezwa. Makaburi yana umuhimu gani ikiwa waliozikwa ndani yake hawajui neno lolote? Au alikuwa analenga nini kusema hivyo?Malango ya mji huo yalikuwa na umuhimu gani? Jambo gani linalowakilisha uwepo wa Mungu ambalo likiondolewa linakuacha mpweke?
- Kama watumishi wa serikali na walio kwenye ajira zingine wangetumia mahusiano mazuri na waajiri wao kurekebisha matatizo yanayozikumba jumuiya zao za kidini hali ya jumuiya hizo ingekuwa bora kuliko ilivyo leo? Kwa nini wanahofu kufanya hivyo?
- Je msaada wa mfalme kwa Nehemia ulitegemea mahusiano yake na mfalme au ulitegemea mkono mwema wa Mungu uliokuwa juu yake? Kwa nini Nehemia alikagua uharibifu wa mji majira ya usiku? Na kwa nini hakutaka kwenda na watu?
- Ikiwa kuna watu hawataki nyumba yenu ya ibada ijengwe kwenye eneo lao mnafanyaje? Na ikitokea wakaibomoa baada ya kuijenga mtawachukulia hatua gani? Je mnaweza kumuomba Mungu awalaani watu hao?
NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: NEHEMIA 3:1-32
- Hapa duniani si kwetu. Hata kama tunaishi maisha yaliyo bora kuliko wenzetu wengi bado hapa ni nchi ya ugenini. Shauku yetu kubwa inapaswa kuwa kwenye mji ule Mungu aliotuandalia. Mji ambao tutaishi na baba zetu wa imani Adamu, Ibrahimu na manabii wa zamani pamoja na Mungu mwenyewe. Mji ambao mwenye kuujenga na kuubuni ni Mungu mwenyewe (Waebrania 11:10; Wafilipi 3:20; Waefeso 2:19)
- Mungu anatupa fursa ili tuzitumie kusimamisha na kuimarisha ufalme wake duniani. Fursa hizo zisitufanye tujisikie kuwa bora kuliko wengine au kujiondoa katika madhila yanayowapata waumini wenzetu. Kuna wakati msaada wetu kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo na watawala yanaweza kusaidia kuondoa changamoto za kazi ya Mungu kwenye eneo tulilopo. Esta na Nehemia ni mifano mizuri ya watu waliotumia fursa zao kuimarisha na kuitetea kazi ya Mungu.
- Ni muhimu kujitambulisha imani yako mahali unapofanyia kazi mapema iwezekanavyo ili kiongozi au mwajiri wako aelewe misimamo yako. Pamoja na kujitambulisha ni muhimu pia maisha yako yashuhudie kile unachoamini. Uaminifu wako kwa Mungu wako mara nyingi huwa kichocheo cha wakuu wako wa kazi kukuamini na kukutekelezea madai na maombi yako (Esta 4:1-17).
- Ni muhimu kujionea mwenyewe changamoto za kazi ya Mungu kwa kutembelea eneo la tukio na kufanya tathmini ya matengenezo yanayohitajika bila kutegemea maelezo ya watu. Wengine wamejikuta wakisaidia miradi hewa ambayo misaada iliyotolewa iliishia mifukoni mwa watu. Kuna wakati msaada ili ufikie kinachokusudiwa unapaswa usimamizi wa mtoaji. Na inakuwa muhimu hivyo hasa pale msaada unapokuwa umeupata kutoka michango ya wadau au wakuu wako wa kazi. Kutoa misaada kuendane na kuisimamia.
MASWALI YA KUJADILI: NEHEMIA 4:1-23
- Je ni halali kuwaombea laana wanaodhihaki kazi ya Mungu? Je ukijenga nyumba ya ibada kwa viwango vya chini waonao wana haki ya kufanyia dhihaka? Je hapo kosa litakuwa la kwao au lako wewe uliyejenga chini ya kiwango?
- Moyo wa kufanya kazi unachochewa na nini? Je watu waliokata tamaa wanaweza kuwa na moyo wa kufanya kazi? Je watu wenye moyo wa kufanya kazi wanahitaji msimamizi au mtu wa kuwasukuma? Mahali unapoishi unaona huo moyo wa kufanya kazi?
- Wakati unapofanya kazi ya Mungu na kusikia woga huwa unakumbuka kuwa Bwana ndiye mkuu mwenye kuogofya? Wanaume wanatakiwa kuwapigania wake zao, pamoja na watoto wao wa kike kwa wa kiume. Je mwanaume alipewa jukumu hilo kwa kuwa ana nguvu kuliko mwanamke? Kwa nini mwanamke asijipiganie mwenyewe? Je wajane wanapiganiwa na nani?
- “Mungu wetu atatupigania.” Kwa nini Mungu anaahidi kuwapigania watu wake? Je haoni kwa kufanya hivyo Shetani anaweza kulalamika kuwa anaingilia ugomvi usio wake? Kama Mungu ndiye anayewapigania wanadamu wana sababu ya kuhofia kushindwa?
MASWALI YA KUJADILI: NEHEMIA 5:1-19
- Je ni halali kuwatoza riba waumini wenzako? Unapomkopesha ndugu yako asiye na uwezo wa kulipa unakuwa umemsaidia au umemtwisha mzigo mzito? Inatokeaje ndugu wa familia moja mkapishana pakubwa katika kipato? Je kuna uwezekano wa kuondoa tofauti kubwa ya vipato kati ya ndugu?
- Je ni halali kuwaita makafiri watu wasiomjua Mungu? Je kafiri ni mtu asiyemjua Mungu au asiyeamini kama wewe unavyoamini? Ukiitwa kafiri kwa kuwa huamini kama anavyoamini mwenzako una sababu ya kukasirika?
- Je umaskini wa kipato waweza kutokana na mifumo isiyo ya haki dhidi ya wanyonge iliyopo kwenye jamii? Unadhani riba kubwa zinazotozwa na mabenki na bei ndogo zinazotolewa na wanunuzi wa mazao zinaweza kuwa chanzo cha umaskini wa kipato?
- Je inawezekana kufanya kazi ya serikali na huku ukiwa mwaminifu kwa Mungu wako na kwa serijali yajo na ukiwa msaada kwa waumini wenzako? Je kuna wakati viongozi wa serikali wa kuteuliwa na wa kuchaguliwa huweka sheria kandamizi kwa nia ya kujilimbikizia mali na kuwaumiza raia? Je kuna uwezekano wa kuwa na maendeleo bila kutoza kodi?
MASWALI YA KUJADILI: NEHEMIA 6:1-19
- Unadhani Nehemia alikataa kwenda kuonana na Sanbalati na Geshemu kwa sababu ya kuhofia maisha yake au kwa sababu ya umuhimu wa kazi aliyokuwa anaifanya? Je ni halali kukataa au kukubali wito kutoka kwa wafanyakazi wenzako ikiwa unajua kuwa wana nia ovu juu yako?
- Je ni rahisi kumtambua mwenye hila? Kwa nini wenye nia ovu hupenda kubuni uongo na kuufanya uaminike kama ukweli? Unadhani ni kwa nini Shetani anaitwa baba wa uongo? Uongo unamsaidiaje Shetani kufanikisha malengo yake?
- Utajuaje kama ushauri unaopewa na watu wako wa karibu una nia njema na siyo sehemu ya njama ya kukuangamiza? Adui gani ni mbaya zaidi kati ya yule anayekuchekea na yule anayekununia?
- Shetani akishindwa kukuogofisha kwa kutumia vitisho atatumia hila ili utende dhambi na kukukosesha na Mungu wako. Unaiona hali hiyo katika kisa cha Nehemia na adui zake? Unawafahamu watu walioajiriwa au kukodishwa ili waharibu maisha yako? Je ukiwafahamu utawachukia au utawapenda?
NEHEMIA 7:1-73
MASWALI YA KUJADILI: NEHEMIA 10:1-39
- Unadhani kulikuwa na umuhimu gani kila mwenye maarifa na akili wa jamaa yote Yuda kujitenga na jamaa yote ya nchi kwa viapo na laana? Je unadhani vile viapo vya ubatizo hutolewa kwa uzito kama huo wa nyakati za Nehemia? Je kiapo cha kutowaoza binti zao kwa wamataifa na kutowatwalia wana wao binti za wamataifa kilikuwa na umuhimu gani wakati ule? Je kiapo hicho ni cha muhimu hata leo?
- Kwa nini kununua chakula kulikataliwa siku ya Sabato wakati chakula ni hitaji muhimu kwa wanadamu? Je katazo hilo linawahusu watu wa Mungu waishio leo? Je ni kitu gani kinachoweza kuwa halali kununua siku ya Sabato?
- Utaratibu wa kuleta malimbuko ya ardhi (mazao) na wazaliwa wa kwanza wa mifugo ulikomea wapi? Je katika kukamilisha kauli ya Mungu Kwanza isingependeza kuleta malimbuko yetu kanisani mwaka kwa mwaka? Utaratibu wa kuleta mazao na mifugo ya zaka kanisani unafaa kufanyika hata leo badala ya kuleta fedha tu kama inavyofanyika kwa sasa?
NEHEMIA 11:1-36
NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: NEHEMIA 13:1-31
- Waamoni na Wamoabi walikuwa ndugu wa damu na Waisraeli kupitia kwa Lutu (Mwanzo 19:31-38). Mtu anaweza kuwa ndugu yako wa damu lakini akashindwa kukusaidia unapopitia wakati mgumu kwa roho yake mbaya. Undugu si kuzaana wala kulingana; undugu ni kufaana. Kila ubaya tunaoufanya kwa ndugu aliyehitaji huruma yetu kumbukumbu yake inatunzwa mbiguni. Tuwe na tahadhari.
- Uwezo wa kutambua wenye nia haupo kwa watu wote. Kuna watu wamejikuta matatani kwa kuwakaribisha au kuwashirikisha watu wasiowatakia mema. Watu hao hutumia udhaifu wa viongozi waliopo au mwanya ulioachwa na kiongozi aliye makini. Hapa tunajifunza kuwa makini na yule unayekasimu madaraka yako kwake. Kama si mkomavu wa kutosha usikae mbali naye kwa muda mrefu.
- Kama ukusanyaji wa zaka na sadaka hautasimamiwa kikamilifu utendaji wa watumishi wanaotegemea matoleo hayo utaathirika sana. Mitaa mikubwa na idadi kubwa ya washiriki wanaohudumiwa na mchungaji mmoja ndiyo sababu nyingine ya kushuka kwa hali ya kiroho. Juhudi kubwa inahitajika katika kusimamia na kuhimiza utoaji kunusuru vyombo vyetu vya habari na shughuli za uinjilisti kwa ujumla.
- Kujali kupita kiasi shughuli za kiuchumi kumesababisha baadhi ya waumini kutozingatia ibada za katikati ya juma na za mwisho wa juma. Katika Luka 21:24 Yesu anatutahadharisha kuepukana na hayo. Tusisumbukie sana maisha hadi kumsahau Mungu na kuanza kuvunja Sabato (Mathayo 6:25-28).
- Swala la kuchagua mwenzi wa maisha halipaswi kufanywa kwa kutegemea akili za kibinadamu. Hata Suleimani mwenye hekima katika jambo hili alifulia. Mungu ameahidi kutusaidia (Methali 19:14). Tena imeshauriwa kutooana na mtu mwenye misimamo inayokinzana ya imani. Watoto husumbuka sana wasijue wafuate dini gani kati ya baba na mama. Kilinde kizazi kijacho kwa kuzingatia ushauri huu.