Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WARUMI 8

UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI

SURA YA NANE

Kitabu cha Warumi sura ya nane kianaendelea kuelezea maisha ya ushindi anayoyapitia aliyehesabiwa haki kwa imani na ambaye anaukulia wokovu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. (Warumi 8:1) “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” Sura hii ina welekeo wa kuhitimisha mgogoro uliokuwa unajadiliwa kwenye sura ya saba iliyotangulia ambapo sheria ilionekana kuwa chanzo cha kukosekana kwa utulivu katika maisha ya mwanadamu mwenye asili ya dhambi na anayetawaliwa na sheria ya dhambi.

Katika sura ya nane hali hiyo imebadilika baada ya mafunuo yaliyoibuliwa mwishoni mwa mjadala uliokuwepo kwenye sura ya saba. (Warumi 7:24-25) “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.” Yesu alikuja duniani ili kumwokoa mwanadamu na mwili huu wa mauti au mwili wa dhambi.

Wokovu huu unafanyika ndani ya mwili wa mwanadamu kwa kuitiisha nia au akili inayotawala mwili kupitia kile kinachotajwa na Paulo kama sheria ya Roho wa uzima. (Warumi 8:2) “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Hii ni nguvu nyingine ya pili inayoanza kufanya kazi kwa mwanadamu mara tu baada ya mtu huyo kuhesabiwa haki kwa imani na kuanza kuukulia wokovu. Kama ambavyo sheria ya dhambi inaifanya akili ya mdhambi kuwa mateka (Warumi 7:23) vivyo hivyo sheria ya Roho wa uzima huifanya akili ya aliyehesabiwa haki na anayeukulia wokovu kuwa mateka wa Roho Mtakatifu.

Uthibitisho kuwa mtu amemgeukia Mungu na kwamba anaukulia wokovu ni kumilikiwa na Roho Mtakatifu. (Warumi 8:9) “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.” Roho Mtakatifu analetwa katika maisha ya mwongofu ili kuongoza maamuzi yake. Nia ya mwanadamu inapotawaliwa na sheria ya dhambi inakaribisha mauti lakini inapotawaliwa na sheria ya Roho wa uzima inakaribisha uzima na amani. (Warumi 8:6) “Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.”

Roho Mtakatifu ndiye mtawala mpya na mume wa mke aliyefiliwa na mume katili aitwaye sheria ya dhambi. Ni mume aliyekuwa hana huruma kwa makosa ya mkewe licha ya kujua kuwa udhaifu alionao umetokana na yeye kuimiliki akili yake. Mke huyu anapata mume mwelewa anayeshughulika udhaifu wake kwa kumpa msaada unaohitajika. (Warumi 8:4) “Ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.”

Maagizo ya torati ambayo hapo awali ilikuwa vigumu kutimizwa ndani yetu kutokana na udhaifu wa mwili sasa kwa ujio wa Roho Mtakatifu maagizo hayo yanatimizwa kirahisi. (1 Yohana 5:3-4) “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito. Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.”

Amri zinakuwa nyepesi kwa kuwa anayezifanya ziwe nyepesi ni Roho Mtakatifu anayetawala nia ya mwongofu. Mwongofu anaiacha kazi ya kuukulia wokovu chini ya uangalizi wa Roho Mtakatifu ambaye ametengeneza mazingira rafiki tofauti na yaliyokuwepo awali. Katika mazingira haya mapya mwongofu anapogundua mapungufu katika uwezo wa kutii maagizo anaomba msaada naye hupewa. (Yakobo 1:5-6) “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.”

Katika mazingira ya awali mtu alipojikuta hana uwezo wa kutii maagizo alijipunguzia mwenyewe ukali wa hayo maagizo au alihukumu wengine ili kupunguza uzito wa makosa yake au aliweka mkazo kwenye maagizo ya kawaida za kidini ili kuficha mapungufu hayo au alielekeza lawama kwa wengine. (Mwanzo 3:12) “Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” (Luka 18:11-12) “Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.”

Katika mazingira ya kuongozwa na Roho Mtakatifu kosa linaweza kusamehewa hata liwe kubwa kiasi gani na hata likirudiwa mara nyingi. (Isaya 55:7) “Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.” Hakuna hatia ya kudumu inayoondoa amani moyoni maana Roho Mtakatifu hutuombea kwa kuugua kwa niaba yetu. (Warumi 8:26) “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”

Jinsi Yesu ilivyomgharimu kutukomboa ni sababu nyingine inayotufanya tuwe mateka wa Roho Mtakatifu na watumwa wake wa hiyari. Tunajizuia kutenda dhambi si ili tufikiriwe kupewa haki na uzima ila ni kwa sababu tunatamani kumfurahisha bosi wetu mpya. (Wagalatia 6:14) “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.” Dhambi inakuwa kwetu jambo la kuchukiza kutokana na kile ilichomtenda rafiki yetu. (Warumi 8:10-11) “Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”

Miili yetu kuhuishwa ni kufufuliwa kutoka hali ya wafu. Yule mtu wa dhambi tuliyemuacha kaburini tulipokuwa tunabatizwa hawezi kuendelea kuonekana katika maisha yetu mapya. Maana mambo aliyokuwa anayapenda yule wa zamani ni tofauti na yale anayoyapenda huyu mpya. (2 Timotheo 2:4) “Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.” Yule aliyeokolewa kwa neema huona fahari kuishi sehemu iliyobaki ya maisha yake kwa ajili ya Kristo. (Wagalatia 2:20) “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”

Uzoefu mpya wa kuondokana na utumwa wa dhambi unaamsha shangwe isiyokoma moyoni huku hali hiyo ikiwastaajabisha wanaoshuhudia na kuwafanya kutamani kujua mengi zaidi juu ya muujiza huo. (1 Petro 4:4) “Mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana.” Uzoefu huo mpya kwa wengine utakuwa kero hata kufikia hatua ya kutukana huku kwa wengine ukiwa mbaraka. (2 Timotheo 3:12) “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.” (1 Petro 2:12) “Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”

Matendo ya mwili yaliyokuwa kawaida ya maisha ya awali kabla ya kuongoka sasa yanapungua na kuelekea kwisha kutokana na kazi inayoendelea ndani katika moyo au nia ya mwongofu inayotokana na Roho Mtakatifu. (Warumi 8:12-14) “Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.”

Kuishi maisha ya ushindi yatokanayo na usaidizi wa Roho Mtakatifu ni maamuzi ya hiyari. Baada ya kuanza maisha hayo mapya bado kuna uwezekano wa mtu kuchagua kuishi kwa kufuata mambo ya mwili. Kinachohitajika ni juhudi ya kuyafisha matendo ya mwili kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Kinachohitajika katika hatua hii ni mtu kutokubali udanganyifu uletwao na moyo. Moyo hupenda kuleta ushawishi kwa mwongofu kuwa amefikia hatua ya kutofanya dhambi kabisa wakati ambao hajaifikia hatua hiyo. (Ufunuo 3:17) “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”

Pale udhaifu wa kutamani matendo ya mwili unapoibuka na dhamira ikikuchoma kwa kuhisi hatia unatakiwa uitambue hali hiyo mapema na kuitolea taarifa kwa Yesu ili upate usaidizi. (Ufunuo 3:18) “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.” Dhahabu ilisafishwa kwa moto ni imani ambayo hukuzwa kupitia mchakato kutubu, kuungama, na kusamehewa dhambi. Kujificha kuwa huna dhambi hakuwezi kukuondolea hatia wala kukurejeshea amani. (Mithali 28:13) “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” (Zaburi 32:1) “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.”

Paulo anaibua dhana ya sisi kuwa watoto wa Mungu kama namna ya kuthibisha uhalali na uhakika wa wokovu wetu. (Warumi 8:14-17) “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.”

Mungu alituchagua tangu milele tuwe wana wake kwa njia ya Yesu Kristo. (Waefeso 1:5) “Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.” (Warumi 8:29) “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” Kusudi la kutufanya wanawe ni ili aturithishe. (Wagalatia 4:7) “Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.” Hata hivyo kule kufanywa kwetu wana kulikamilika wakati ule tulipopokea roho ya kufanywa wana kwa kuwa kila aliye na Roho wa Mungu huyo ndiye Mwana wa Mungu.

Swala la kutufanya warithi limekidhi vigezo vyote vya kisheria. Tumefanywa wana wa Mungu kwa njia ya Kristo na limethibitishwa na Roho wa Mungu kuwa tu wana na warithi halali. (Warumi 8:16) “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu.” Kana kwamba hiyo haitoshi swala la Mungu kuturithisha sisi lipo katika ahadi alizowapa Ibrahimu, Isaka, na Yakobo – baba zetu wa kiroho. (Waebrania 11:9) “Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.”

Ahadi ile ya kutufanya warithi ni ya uhakika kwa maana iliandamana na kiapo. (Waebrania 6:13-18) Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu.”

Maisha ya kuukulia wokovu hayana majuto, hofu, wala huzuni maana yamejikita juu ya ahadi za kuaminika na zisizo na shaka. Wana wa Mungu hawaishi tena kama watumwa bali kama wana wenye matumaini wakisubiri kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu na utimizo wa ahadi. (Warumi 8:18-23) “Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu.” Kumjua Mungu kunakuwa darasa lao la kila siku na kiini cha amani inayowazunguka pande zote.

Mwandishi wa kitabu cha Ayubu anatuhimiza kumjua Mungu na kutujulisha faida ya kufanya hivyo. (Ayubu 22:21) “Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.” Kama kuna sababu kubwa ya hali yetu ya kiroho kuwa kwenye viwango vya chini basi sababu kuu ni jitihada ndogo inayofanyika katika kutafuta kumjua Mungu. (Ayubu 36:26) “Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui; Hesabu ya miaka yake haitafutiki.” Mungu atakapokuja duniani atakuja kuwachukua waliomjua maana ndiyo watakaofaidi wenda kuishi naye mbinguni. Hosea anatuhimiza kuendelea kumjua Mungu. (Hosea 6:3) “Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.”

Katika jitihada za kumjua Mungu waongofu wapya hujishughulisha pia katika kuujua upendo wake wa ajabu. (Waefeso 3:17-19) “Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.” Upendo huo wa Mungu ukikaa moyoni kwa kuutafakari hufukuza hofu. (1 Yohana 4:18) “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.”

Kuhitimu katika kumjua Mungu na katika kutambua upendo wake wa ajabu kwa wanadamu humsaidia kila anayeukulia wokovu kustahimili kirahisi majaribu yanayomkuta. Hujipa matumaini kuwa Mungu hawatesi wanadamu bila kuwepo sababu. (Warumi 8:28) “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” Paulo wakati mmoja alimsihi Mungu amuondolee jaribu lililokuwa likimkabili lakini Mungu alikataa na Paulo akaridhika. (2 Wakorintho 12:7-9) “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”

Waongofu wanaoukulia wokovu huonea fahari kusifia udhaifu na mapungufu yao kuliko kujivunia yale waliyojaliwa na Mungu na ambayo hawakuhusika katika kuyafanya yatokee. (2 Wakorintho 11:30) “Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.” (1 Wakorintho 4:7) “Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea?” (1 Timotheo 1:15) “Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.” Majivuno si sehemu ya maisha ya anayeukulia wokovu. (Luka 18:13) “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.”

Wokovu wetu unapitia mchakato wa kuhesabiwa haki kupitia kifo cha Yesu hatua inayotuondolea adhabu ya mauti ya milele iliyokuwa inatukabili na kutuingiza kwenye uzima. Maandiko yanatuambia hatua hiyo ilikamilika pale msalabani Yesu aliposema IMEKWISHA. Lugha ya asili iliyotumika kulielezea neno hilo kwa lugha ya kawaida ni IMELIPWA KIKAMILIFU. Sisi hatuununui wokovu lakini Yesu aliununua maana alifanya malipo ya kifo kilichokuwa kinatukabili. (Ufunuo 5:9) “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa.”

Hatua ya pili inayofuata baada ya ile ya kuhesabiwa haki kwa kifo cha Yesu ni ile ya kutakaswa. Kutakaswa ni mchakato unaodumu katika kipindi chote cha maisha ya mwongofu nao hufikia hitimisho Yesu anaporudi kuja kuwachua watakatifu. Kasi ya mabadiliko katika mchakato huu hutegemea jinsi mwongofu anavyotoa ushirikiano kwa Roho Mtakatifu. Awamu ya tatu ya wokovu ni kutukuzwa. Hii inakamilishwa pale Yesu anapokuja kuwatunuku mwili wa utukufu wale waliovumilia hata mwisho.

Wakati fulani mchakato wote wa wokovu huwekwa katika awamu mbili. Awamu ya kuhesabiwa na kutakaswa huwekwa katika katika Kundi moja la kuhesabiwa haki na Kundi la pili huitwa kutukuzwa.  Lakini Habari njema ni kuwa kupitia mafunuo Paulo aliiona michakato hiyo ikiwa imekamilika tangu kuwekwa kwa misingi ya dunia. (Warumi 8:30) “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.” Mungu hana shaka na uwezo wake wa kutukamilisha ikiwa tutamruhusu afanye kile alichokusudia tangu milele. (Yohana 10:28-29) “Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.”

Tuna kila sababu ya kujivunia Yesu na kutamba na wokovu wetu kama kitu halisi kisicho na shaka kinachosubiri kudhihirishwa katika wakati ulioamriwa. Kwenye hukumu ya kuchuja wasiostahili inayoendelea kule mbinguni tunaye mtetezi mwenye hoja zisizoweza kupingwa na yeyote. (Warumi 8:33-34) “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”

Yesu ndiye hakimu, ndiye mtetezi, ndiye Mwanakondoo aliyechinjwa kwa ajili yetu kabla ya ulimwengu kuwako. Yeye ndiye anayelundikiwa mashtaka na shetani dhidi yetu. Shetani katika kutapatapa kwake anampelekea Yesu mashitaka dhidi yetu akisahu kuwa Yesu ni kaka yetu. (Waebrania 2:11) “Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake.” Yesu atapuuza mashitaka yake na kuyatupilia mbali. (Ufunuo12:10) “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”

Atahakikisha tunashinda kesi hiyo. (Warumi 8:37) “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Sura ya nane ya kitabu cha Warumi kinatuhakikishia kwa Ushahidi mwingi kuwa ushindi wetu ni hakika. (Warumi 8:38-39) “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Ni kusudi la Mungu watu wake wawe na uhakika wa kuokolewa kwao kama Shetani alivyo na uhakika wa kupotea kwake.

Unaokolewa si kwa sababu ulitenda chochote. Unaokolewa kwa sababu ulichaguliwa. Unaokolewa kwa sababu Mungu aliahidi kukuokoa. Unaokolewa kwa sababu Mungu aliamuru uokolewe. (Zaburi 71:3 Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.” Mungu asingeweza kuweka mpango ambao unategemea witikio wa mwanadamu asiyeaminika. (Zaburi 103:14) “Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”