Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

2 NYAKATI

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 2:1-18 

  1. Kudhamiria kujenga nyumba kwa jina la Bwana ni kudhamiria kutojitwalia utukufu unapoitegemeza kazi ya Mungu. Waliojenga mnara wa Babeli walitafuta kujifanyia jina (Mwanzo 11:4) matokeo yake Mungu aliwatawanya (Mwanzo 11:8). Utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume (Mathayo 6:3). Msifanye wema wenu machoni pa watu; kusudi mtazamwe na wao (Mathayo 6:1). Mungu hapokei wema unaotendwa kwa lengo la kujinufaisha.
  2. Mungu anastahili mambo makubwa kwa kuwa Yeye ni Mkubwa. Chochote kinachomhusu Mungu kinapaswa kuwa katika viwango bora. Ndiyo maana sadaka ya wanyama ilitakiwa kuwa isiyona kilema (Walawi 22:20). Utaratibu wa kumtolea Mungu mabaki hauakisi ukuu wake. Mungu anapaswa kupewa kile kilicho bora zaidi.
  3. Watu hupewa mtawala anayelingana nao. Mungu akiwapenda watu huwapatia mtawala aliye bora (2 Nyakati 2:11). Mtawala aliyeletwa na Mungu hujali watu. Hushughulika kuinua viwango vya maisha yao katika nyanja zote. Faraja yake ni kuona watu wake wanafikia maisha ya njozi zake.
  4. Mtawala bora hujenga mahusiano na majirani zake. Hakuna ubaya kutumia huduma au bidhaa ya jirani iliyokatika viwango bora kuliko vya kwako. Bure ni aghali hivyo ni heri kutumia gharama ili uwe na bidhaa na huduma bora zaidi.
  5. Kiongozi mwema hutambua vipawa vya ambao hawapo chini yake na kuvitumia kufanikisha majukumu yake. Hatasita kuvitumia eti kwa vile havitokani na watu wake. Kilicho muhimu kwake ni kufanikiwa kwa kazi yake. Hapa duniani hakuna anayejitosheleza kwa kila kitu. Ujuzi usiokuwa nao unajifunza au unauazima kwa walionao. Kitu chako kizuri si lazima kiwe kimefanywa na wewe. Hata kikifanywa na wengine bado ni chako.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 3:1-17 

  1. Watu wanaomheshimu Mungu humjengea nyumba ya ibada yenye hadhi. Nao huona fahari kutoa mali zao kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu. Ikiwa kila kitu kwenye hekalu kilifunikwa kwa dhahabu, sakafu na kutau za nyumba ya Mungu zapaswa kufunikwa kwa namna bora. Mungu aweza kudharauliwa ama kuheshimiwa kutokana na mwonekano wa jengo la ibada.
  2. Mwili ni hekalu la Mungu. Unahitaji kusetiriwa na kupambwa kwa namna inayompa Mungu utukufu (1 Timotheo 2:9). Mungu anapendekeza tujipambe kwa tabia ya Kristo ambayo hufunika wingi wa dhambi zetu (1 Petro 4:8; 1 Petro 3:3-4).

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 4:1-22 

  1. Mifano ya ng'ombe aliyoitengeneza Sulemani ilikuwa sanamu za ng'ombe. Mwanadamu akijitengenezea sanamu huwa ni dhambi (Kutoka 20:4). Mungu akimuagiza mwanadamu kutengeneza sanamu huwa si dhambi (Hesabu 218). Mungu hafungwi na sheria. Hashitakiwi na yeyote kwa lolote analolifanya. Yeye mwenyewe ni sheria.
  2. Kazi ya kusanifu mpangilio wa hekalu la Mungu ulifanywa na mtaalamu kutoka nchi ya ugenini. Dhana hapa ni kuwa nyumba hiyo ni kwa ajili ya mataifa yote (Isaya 56:7). Ujenzi wa nyumba za ibada usingefanywa kwa kubagua walio nje. Wapewe nafasi ya kushiriki kwa kuchangia chochote walichonacho maana ni nyumba yao pia.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 5:1-14 

  1. Ujenzi wa hekalu la Mungu na samani zake visingekuwa na thamani yoyote bila kuchinja ng'ombe na kondoo. Wanyama hao waliwakilisha kafara ya Kristo. Huduma zote za hekaluni zilimlenga Yeye. Mwanadamu hawezi kufanya na kufanikisha lolote bila msaada wa damu ya Yesu. Yesu ndiye Mwana-Kondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu. Vyombo vya hekalu vyenye thamani kubwa ya madini vilisafishwa kwa damu ya wanyama lakini sisi tulio wenye thamani kubwa zaidi tunasafishwa kwa damu ya thamani ya Kristo (1 Petro 1:18-19).
  2. Sanduku la Mungu hatimaye lilipandishwa na kuingizwa hekaluni salama. Mara hii hakukuwa na kifo kilichotokea maana kila kitu kilienda sawa na maagizo ya Mungu. Kwa kila jambo kuna majira yake (Mhubiri 3:1-8). Usikate tamaa kwa kuwa kuna jambo halijatimia kwa namna uliyokusudia. Wakati wa Mungu ulikuwa haujafika. Vuta subira Mungu ana mpango na wewe.
  3. Uimbaji hekaluni katika Agano la Kale ulifanywa na kikundi cha makuhani na familia zao tofauti na leo. Namba ya waimbaji ilikuwa kubwa kuliko Idadi ya kwaya nyingi za leo. Uimbaji ulipofanyika vizuri kwa kukidhi vigezo utukufu wa Mungu ulijaza hekalu. Ala za muziki kadhaa zilitumika vikiwemo vinanda, vinubi, na matowazi lakini vyote vilitengeneza sauti moja isiyopishana. Mtu alipowasikiliza waimbaji alisikia sauti moja kutoka kila sauti. Sauti za aina moja zililingana na kuleta muafaka. Uimbaji leo unapaswa kuzingatia vigezo ili utukufu ujaze hekalu la mwili kila wimbo unapoimbwa.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 6:1-42 


NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 7:1-22 

  1. Zamani hizo ilikuwemo namna ya kutambua kama maombi yako yamejibiwa. Moto ulishuka kutoka mbinguni na kuiteketeza kafara. Tunatakiwa kuomba kama tunaotarajia kupokea majibu ya Mungu. Tupange hoja (Isaya 43:26; Isaya 41:21; Wafilipi 4:6-7). Mungu hatawanyima kitu chema wale waendao kwa ukamilifu (Zaburi 84:11).
  2. Mungu alikuwa na utaratibu wa kuwatokea watu usiku pale anapokuwa na taarifa anazotaka kuwapa. Utaratibu huo haujabadilika. Hata leo wale anaopenda kuwapa taarifa muhimu huwatokea ndotoni (Mathayo 2:13). Mungu amekuwa akisema nasi ndotoni lakini tumekuwa ama hatukumbuki ndoto hizo ama tunashindwa kujua tafsiri zake. Mungu hatafanya jambo lolote bila kuwafunulia watu wake siri hiyo (Amosi 3:7).
  3. Kujinyenyekesha, kuomba, kuutafuta uso wa Mungu na kuziacha njia mbaya za dhambi humfanya Mungu kutega sikio, kusamehe watu hao dhambi zao, na kuiponya nchi yao. Kujinyenyekesha ni kwa muhimu kwa kuwa roho ya kiburi hufunga aina zote za mawasiliano na Mungu (Ayubu 35:12). Sifa ya mtu aliye mkamilifu ni kutokuwa na kiburi (Zaburi 19:13).
  4. Mungu huchukizwa mwanadamu anapojiamulia kuiabudu miungu isiyo na sifa za kuabudiwa. Mungu anayestahili kuabudiwa ni lazima awe amemuumba na amemkomboa mwanadamu (Ufunuo 4:11; Ufunuo 5:9). Mungu ana wivu anapoona viumbe wasio na sifa wakiabudiwa (Torati 32:21).

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 8:1-18 

  1. Mfalme Sulemani hakuwapa upendeleo makabila matano yaliyoandamnana na Waisraeli lakini akampendelea binti Farao wa Misri. Hii ni 'double standard'. Yaani kufanya jambo kwa kanuni inayokinzana na kile ulichofanya awali. Huu ni udhaifu ambao huwapata wanadamu wengi hasa walio watawala. Mungu hana upendeleo (Matendo 10:34; Warumi 2:11; 1 Timotheo 5:21).
  2. Sulemani alikuwa mtawala aliyejua kuwasimamia walio chini yake. Kuyafahamu wanayopaswa kufanya walio chini yako na kuhakikisha kuwa yanafanyika ni wajibu wa kiongozi bora. Kazi za walio chini zikilala aliyelala anaweza kuwa ni yule anayezisimamia. Ili kuepusha kulaumiana mpe mwongozo wa kile anachotakiwa kukifanya aliye chini yako - Majukumu ya Kazi (2 Timotheo 2:2; 1 Timotheo 3:15).
  3. Chuki na mifarakano huleta magomvi na kudumaza maendeleo. Sulemani alitumia diplomasia zaidi kuliko nguvu kupatana na maadui zake waliomzunguka. Waliokuwa maadui wa baba yake wakawa washirika wake wa maendeleo. Kuna wakati wa kukomesha chuki na kuleta maridhiano ya kifamilia na kitaifa. Mafanikio ya miundombinu aliyoijenga Sulemani kwa sehemu kubwa inatokana na misaada ya wale ambao hapo awali walikuwa maadui wa taifa.

NILICHOJIFUNZA NA KUGUNDUA: 2 NYAKATI 9:1-31

  1. Sheba ilikuwa himaya ya kifalme iliyokuwa inaongozwa na mwanamke katika eneo ambalo leo linafahamika kama Ethiopia. Hii inaonesha kuwa wanawake wa Kiafrika walikuwa na uwezo wa uongozi tangu zamani. Uongozi wa malkia wa Sheba ulikuwa umepiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwa ulikuwa unamiliki manukato, dhahabu na vito vya thamani. Nchi za Afrika chini ya utawala wa mwanamke hapo zamani zilikuwa zinatoa misaada na zawadi kwa nchi za Mashariki ya mbali. Hatujachelewa Afrika inaweza kuwa na mafanikio makubwa yavkiuchumi huenda kwa kuwatumia zaidi wanawake.
  2. Hakuna dhambi wala ubaya kujifunza kwa waliofanikiwa. Kinachotakiwa ni kutoruhusu kiburi na majivuno. Maarifa yanatafutwa tena kwa gharama kubwa (Methali 4:13,7), wala usizitegemee akili zako mwenyewe (Methali 3:5). Taifa, taasisi za kidini, familia, na mtu mmoja mmoja zilizo maskini zikiwekeza kwenye elimu na ujuzi, ipo siku zitakuja ondokana na umaskini wa kipato na utegemezi.
  3. Maneno matupu hayana uwezo wa kushawishi kama matendo. Badala ya kutumia muda mwingi kujitangaza ulivyo mzuri jihusishe kwa kufanya mambo yasiyo ya kawaida yanayobariki watu katika jamii yako. Matendo yana nguvu kuliko maneno. Chema chajiuza na kibaya chajitembeza. Tuhakikishe taasisi zetu za elimu, afya, na vyombo vya habari na mwonekano wa majengo yetu vinavutia waliotuzunguka hata watamani kuja kujifunza kwetu. Inawezekana kama tukidhamiria.
  4. Ukitoa nawe utapokea. Ukizuia utabaki na ulivyonavyo tu na hata huenda vikapungua (Luka 6:38; Mithali 11:24-25). Waafrika walikuwa wakarimu tangu zamani. Wakoloni waliutumia vibaya ukarimu wetu tukatawaliwa na kuwa maskini. Bado hatujachelewa tunaweza kuamka. Tuanze ukarimu kwa kumpa Mungu kile tulichonacho na kwa kuitegemeza kazi yake. Sulemani na baba yake Daudi walitegemeza kazi ya Mungu kwa mali zao nao wakawa matajiri. Ethiopia ndiyo nchi pekee ya Kiafrika ambayo haikuwahi kuwa koloni la wageni. Tukatae umaskini kwa kuwa wakarimu.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA:  2 NYAKATI 10:1-19 

  1. Mwishoni pa utawala wenye hekima wa Sulemani paliingia watu wawili wasio na sifa za uongozi. Hawakujifunza chochote kutoka kwa mtangulizi wao. Tofauti na Daudi ambaye alimwandaa Sulemani, inaonekana Sulemani hakumwandaa mrithi wake. Watu wengi wenye kipaji cha akili hawana bahati ya kushuhudia akili hiyo kwa watoto wao.
  2. Inaelekea mfalme Sulemani alilifanya zito kongwa la watu wake. Alikuwa mbabe. Hakutoa uhuru wa maoni kwa watu wake. Lakini mtoto wake angalau aliwauliza raia wake wanachotaka. Alipendelea ushauri wa vijana wenzake kuliko wa wazee. Kuna wakati vijana hawaamini wazee.
  3. Wazee wanapendekeza kwa mfalme kijana awe mwema, awapendeze na kuwaambia maneno mazuri raia wake. Inashangaza kuwa wazee hawa hawakuweza kumsaidia Sulemani asilaumiwe katika utawala wake. Washauri wengi wana kawaida ya kutoa ushauri kwa kupima mtazamo wa mpokeaji.
  4. Mfalme Rehoboamu hakusikiliza sehemu kubwa ya maoni ya raia wake. Baada ya kuona maslahi yao hayazingatiwi na mtawala mpya wakaasi. Wakati fulani uasi wa watawaliwa hutokana na uasi wa Watawala. Taifa la Israeli likapasuka vipande viwili wakati makabila 10 yakaunda ufalme wa kaskazini na makabila mawili yakaunda ufalme wa kusini.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 11:1-23 

  1. Huwezi kukataa ushauri kila wakati. Hatimaye Rehoboamu alikubali ushauri wa mtu wa Mungu. Muda na mali ambavyo vingetumika kwa vita vikatumika kujenga miji 15 na kuimarisha ulinzi. Ni muhimu kupima kama kuna ulazima wa kuzua au kukuza mgogoro unaoweza kuepukwa.
  2. Ndugu wanapotofautiana si lazima wapigane. Upande mmoja unaweza kukubali kutokubaliana na maisha yakaendelea. Madhara ya ndugu kugombana ni makubwa kuliko kusameheana. Mtu anaweza kumchagua rafiki lakini hawezi kumchagua ndugu.
  3. Kuna wakati wa ndugu kutengana kwa faida ya mahusiano (Mwanzo 13:7-9). Hiyo inatoa fursa kwa wenye nia ya kudumisha mambo bora yaliyokuwa yanatendeka kabla ya kutofautiana. Makuhani ambao hawakupokelewa na ufalme wa kaskazini walikuja kutumika kwenye ufalme wa kusini. Hata kama kuna kutofautiana kusiwahusishe wale ambao kimsingi hawahusiki na ugomvi.
  4. Rehoboamu alionesha udhaifu katika maswala ya uundaji wa familia. Alioa wake 18 na masuria 60 na sehemu kubwa ya wake zake ni watoto wa ndugu zake. Alilenga kuwa na watoto wengi ili awatawanye katika nchi zote za Yuda na Benyamini. Mbinu hii ilikuwa ya kibinadamu zaidi. Hatuzai watoto ili kujiongezea ulinzi.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 12:1-16 

  1. Kwa kawaida wanadamu wengi humuacha Mungu pale wanapofanikiwa. Ukifika wakati ambao hujisikii fahari kujivunia mahusiano yako na Mungu unakaribia anguko lako. Kiri kuwa mafanikio yako yametokana na Mungu. Haitakugharimu kitu, bali utaendelea kuinuka hadi vileleni. Kuacha Torati ni kuacha maagizo ya Mungu. Ni kuchagua kutembea gizani.
  2. Kumwasi Mungu kunakaribisha mashambulizi kutoka kwa adui. Ulinzi uliokuwepo unaondolewa na inakuwa rahisi kushambuliwa na adui wasiohesabika (Waefeso 6:12).
  3. Miji iliyotumia muda na raslimali nyingi kuijenga ilitwaliwa. Bima halisi ya mali zetu ni Mungu. Yeye hufanya kituo akiwalinda wamchao (Zaburi 34:7). Mungu anatutaka tumtolee mali zetu ili zipate ulinzi wa kuaminika (Mathayo 6:19-20).
  4. Mungu anapompenda mtu humuonya mara kwa mara. Rehoboamu alionywa alipotaka kufanya vita na makabila ya kaskazini. Alionywa tena alipomuacha Mungu. Mara hii Rehoboamu na wazee wa Yuda walitii tena. Maisha ya kuukulia wokovu ni safari ya kuanguka na kuinuka tena. Kilicho muhimu ni kukubali kosa. Kukubali kosa ni ukomavu. Huleta wokovu na uponyaji.
  5. Mwanadamu ni mtumwa wa hiari. Ama atachagua kumtumikia Mungu ama atachagua kumtumikia Mungu na Shetani. Wote ni utumwa. Mungu ana utumwa wenye faida (Warumi 6:16). Waliochagua kumtumikia Mungu hawatajuta.
  6. Uzembe katika kufuatilia maagizo ya Mungu kumewagharimu watu wengi. Umakini katika mambo ya kiroho unahitajika. Wale walioanza na Mungu wahakikishe wanamaliza naye. Vinginevyo miisho kama ya Rehoboamu itawahusu.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 13:1-22 

 


NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 14:1-15 


NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 15:1-19 

  1. Mungu huwa pamoja na watu wakati hao watu wanapomhitaji Mungu. Naye huwaacha wanapokuwa hawamhitaji. Mwanadamu anamuhitaji zaidi Mungu kuliko Mungu anavyomhitaji mwanadamu. Mungu anampenda mwanadamu zaidi kuliko mwanadamu anavyopenda Mungu. Mungu angekuwa na tabia ya kulazimisha kupendwa wanadamu wote wangempenda Mungu. Mtu aliyelazimishwa kupenda hajui kupenda. Mungu anapenda wanaojua kupenda.
  2. Maisha yasiyo na Mungu na yasiyoongozwa na mafundisho ya Mungu hayana amani ya kweli. Yamejaa mfadhaiko usiokoma. Hata hivyo Mungu hawi mbali na wanaomtafuta (Matendo 17:27). Maana yeye hapendi mtu apotee (2 Petro 3:9).
  3. Watu wasio na mazoea ya kujipa moyo wanapokabiliwa na changamoto hulegea sana. Hukosa nguvu za kusonga mbele. Hukata tamaa na kutoamini kama kile wakifanyacho chaweza kuleta matunda. Huchukia kazi zao na hujichukia wao wenyewe. Mungu anawafariji watu wa aina hiyo kuwa wasikate tamaa (Zaburi 27:14; Zaburi 31:24; 1 Kor. 15:58).
  4. Ujumbe wa matumaini unahitajika sana kwa waliokata tamaa. Hunenepesha mifupa (Mithali 15:30). Ni kama Sega la asali (Mithali 16:24). Watu wengi hupoteza maisha na kuishi maisha yaliyojaa msongo kwa sababu ya kukosekana watu wa kutia moyo. Hata ukihitaji kumsahihisha mtu msahihishe ukimuonesha anavyoweza kutumia uwezo mdogo alionao kubadilisha hali ya mambo. Muoneshe pia jinsi Mungu wake anavyomuwazia mema (Yeremia 29:11).
  5. Dhambi inachosha. Dhambi inatumikisha. Watu wakishachoshwa na dhambi huagana nayo mchana kweupe (Ezekieli 12:3-4). Moja ya vitendo vya kijasiri ni kumkataa Shetani. Na Shetani anajua wanao mkataa kwa kumaanisha kuwa huwa hawarudi nyuma. Siku ya Shetani kuachwa peke yake huwa ya huzuni kwake lakini ya furaha kwa mateka aliyeachiwa huru. Mkimbieni Shetani naye atawakimbia (Yakobo 4:7).

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 16:1-14 

  1. Hofu humfanya mtu amkimbilie mwanadamu kwa msaada na kumtelekeza Mungu mwenye nguvu zote. Hofu huondosha kumbukumbu zote za matendo makuu Mungu aliyokutendea huko nyuma. Hofu hukuza kidogo kikaonekana kikubwa. Hofu hupata nafasi mtu anapomsahau Mungu. Mungu anapendekeza tumtumaini Yeye tunapokabiliwa na nyakati ngumu (Kumb. 31:8; Kumb. 7:18; Kumb. 20:1; Ezekiel 2:6; Ezekiel 3:9; Yoshua 1:9; 2 Wafalme 6:16; Isaya 41:10, 13; Yeremia 1:8).
  2. Mungu hatulii akitafuta watu wanaomtumainia ili awatie nguvu na kuwapigania. Mungu ni mtetezi wa wanyonge (Ayubu 19:25). Anatambua kwamba watu wanyonge wanahitaji msaada wake na hivyo huwahi kwenye eneo la tukio ili awape msaada. Lakini badala ya kumkimbilia Yeye ili wasiaibike, wao huwakimbilia wasio na uwezo na ambao huwahadaa kwa kuwapa matumaini ya uwongo (Ayubu 8:18; Yeremia 17:18; Zaburi 71:1; Kumb. 18:10).
  3. Rafiki mwema ni yule anayekuambia mapungufu yako. Wanadamu wana kawaida ya kutowapenda marafiki wanaowaambia mapungufu yao na kuwakumbatia wanaowapa sifa za uongo. Sikiliza kila ushauri. Uwe na ujasiri wa kukiri makosa. Ukikiri hutakufa bali utaiokoa nafsi yako na mabaya zaidi. Assa alipuuza ushauri wa mwonaji akaishia kubaya. Manukato yanayoletwa baada ya kifo hayana thamani kama ule ushauri uliotolewa ungefanyiwa kazi. Hata maiti

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 17:1-19 

  1. Mtu anapokwenda kulingana na taratibu zilizoelekezwa katika kuongoza taasisi ya kidini Mungu huwa pamoja naye. Mungu huepusha magumu ambayo yangeweza kutokea. Mambo yanapokuwa hayaendi kama inavyotarajiwa ni wakati wa kuchunguza kanuni zilizowaletea mafanikio waliokutangulia na kuzifuata. Ni rahisi kupoteza dira ya taasisi lakini ni jambo linalohitaji ujasiri kurejesha dira hiyo inapohusika.
  2. Kumtafuta Mungu ni kufanya matengenezo ya kiroho. Matengenezo ya kiroho huandamana na kurejea kwenye mafundisho yaliyojengwa juu ya Neno la Mungu. Upo wakati katika historia ambapo kanisa lilifanya matengenezo hayo. Wanamatengenezo wale walifaulu kurejesha mafundisho ya msingi ya Biblia ikiwapo ibada ya siku ya saba ya juma. Hata hivyo Ukristo kwa sehemu kubwa unakumbatia mapokeo ya wanadamu yanayohitaji matengenezo makubwa.

MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 18:1-34 


MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 19:1-11 

  1. Yehoshafati alifanya kosa la kuwasaidia waovu na kuwapenda wamchukiao Bwana. Je, hiyo ina maana ya kuwa haitupasi kuwapenda waovu? (Mathayo 5:54). Kwa nini kama Yehoshafati alifanya kosa la kumsaidia Ahabu mfalme wa Israeli hakuadhibiwa au kuuawa vitani badala yake alirudi nyumbani kwake salama?
  2. Ilikuwa ni kawaida kwa wafalme wa Yuda na Israeli kuamuru waonaje waadhibiwe pale wanapotoa matamko ya hukumu kwa watawala wao. Ilikuwaje Yehu hakukutwa na dhahama kama hiyo?
  3. Moja ya sababu zilizofanya Yehoshafati asiadhibiwe kwa makosa yake ni wema alioutenda kwa kuondoa maashera. Je matendo mema yanafuta matendo mabaya? (Waefeso 2:8-9). Mara nyingi haki za watu zinaporwa na wale waliowekwa kusumamia haki hizo. Kuna umuhimu gani kwa utengamano wa nchi kuhakikisha haki za raia zinalindwa?
  4. Kuwepo kwa sheria zinazolinda haki za watu si kwa muhimu ikiwa wasimamizi wa haki hizo si waadilifu. Ni njia gani zinazopendekezwa hapa ili kuhakikisha wasimamizi wa sheria wanatenda haki?

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 20:1-37 

  1. Taarifa za kufadhaisha huweza kumfanya mtu amtafute Mungu kwa bidii. Tena kwamba Waamori ambao kwa asili ni ndugu wakishirikiana na mataifa mengine mageni wanakuja kuwashambulia (Mwanzo 18:30-38). Mfalme akaliongoza taifa kwenye toba. Mtawala makini hufanya tathmini ya nguvu na mapungufu aliyonayo. Na akibaini hawezi Kustahimili huutafuta uso wa Bwana.
  2. Toba ya kweli ni chimbuko la ushindi. Yehoshafati alipojitambua hawezi lolote mbele ya adui zake ndipo alipopata ushindi. Tunakawia kupata ushindi kwa kutojitambua kuwa tu wanyonge vipofu na uchi (Ufunuo 3:17-18; 2 Korintho 12:10; Yohana 15:5).
  3. Mungu hukumbushwa ahadi zake. Katika nyakati za dhiki kuu ndizo nyakati za kumkumbusha Mungu alichoahidi alichowahi kukutendea siku za mafanikio yako. Mungu ni mwaminifu kutimiza maagano. Kama aliahidi atatenda. Yeye mwenyewe ameagiza tumkumbushe (Isaya 43:26; Zaburi 50:15; Kumb. 8:7-8; Zaburi 89:34; 1 Kor. 10:13; 1 Thes.5:24; 2 Thes 3:3).
  4. Ndugu aweza kugeuka adui. Waamoni na Wamoabu ambao kwa asili ni ndugu na Yuda wanaungana na mataifa ya kigeni kushambulia ndugu zao ambao waliwatendea mema siku za nyuma. Adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake (Mwanzo 19:30-38; 2 Nyakati 20:10-11; Mathayo 10:36; Marko 6:4; Zekaria 13:6).
  5. Vita si yetu. Hakuna wakati Mungu ameacha kupigana kwa ajili yetu. Tutakapotambua vita dhidi ya dhambi na dhidi ya shetani si yetu tutapunguza hofu na mfadhaiko unaotupata maishani. Kama Mungu angeiacha hii vita mikononi mwetu tungekuwa tumeangamia kitambo. Mungu ameinunua vita hiyo na amekuwa akipigana kwa niaba yetu tangu tulipoanguka dhambini. Kwa kuwa vita ni yake na ushindi unaopatikana ni wake pia (Samweli 17:47; Kutoka 17:8-13; Kutoka 14:14; Warumi 8:31; 2 Wafalme 6:14-18; Mathayo 6:25-34; Isaya 37:15-20).
  6. Nyimbo zaweza kutumika kuleta ushindi vitani. Nyimbo zilizoimbwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu huondoa hofu na kuongeza ujasiri na kuleta kitisho kwa adui. Nyimbo inaimbwa wakati wa furaha na wakati wa huzuni. Nyimbo inayomwinua Yesu ina uwezo wa kutibu magonjwa yaliyoshindikana. Imba hadi milango yako ya gereza ifunguke (Matendo 16:25-26; Isaya 23:16, Zaburi 47:7; Kutoka 15:20-21;

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA:  2 NYAKATI 21:1-20 

  1. Hofu ya kuondolewa kwenye madaraka yaweza kuibua chuki kwa wale wenye uwezekano wa kuchukua nafasi yako hata kudhamiria kuwaua. Kuwapo kwa watu wanaokupa changamoto ni jambo lenye afya kwa anayejiamini. Kwa asiyejiamini hali hiyo humletea msongo wa mawazo msongo ambao huendelea kumsumbua hata baada kuwaangamiza aliodhani ni adui zake. Mara nyingi wale wanaowindwa ili wasije kuchukua nafasi zinazogombaniwa huwa ni watu wema wasio na hatia. Mwisho wa watu hao wenye chuki huwa mbaya na mara nyingi hawafaidi matunda ya nafasi walizokuwa wanazigombea.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 22:1-12 

  1. Wakina mama hutajwa majina yao wakati visa vya kusikitisha vya watoto wao vinaposimuliwa. Wakina mama wana mchango mkubwa katika ujenzi wa tabia za watoto wao. Wao ni marafiki wa karibu wa watoto wa kiume kuliko ilivyo kwa baba. Uovu wa Ahazia mfalme wa Yuda ulichangiwa na ushauri mbaya wa mama yake. Watoto huharibika ama kwa kudekezwa ama kwa kufanyiwa ukatili. Mama anaweza kutumia vizuri ukaribu alionao kwa watoto kwa kuwajengea maadili mema. Mmonyoko wa maadili tunaoushuhudia leo huenda ukawa umetokana na wakina mama wengi kutotimiza wajibu wao kama walezi (Zaburi 22:6; Mithali 10:1; Kumb. 4:9; Kumb. 6:7; 2 Wafalme 2:4; Ayubu 1:5; Mathayo 14:6-8; 2 Timotheo 1:5).
  2. Kuna hasara katika kujiweka karibu na watu au matukio fulani fulani maishani mwako. Kumshirikisha Mungu katika maamuzi mbalimbali unayofanya maishani mwako kwaweza kukuepusha na majanga yaliyokusudiwa watu wengine. Usifungiwe nira na watu wasiomheshimu Mungu utapata malipo machungu. Ahazia asingejiungamanisha na Yoramu mwana wa Ahabu huenda asingepoteza maisha kwa kifo cha kijinga (Luka 9:60; 2 Kor. 6:14; Waamuzi 14:3; Mithali 13:20; Yakobo 4:4; 1 Timotheo 6:9).
  3. Auwaye kwa upanga atauawa kwa upanga. Mungu ni mwamuzi wa haki atakayemlipa kila mtu kulingana na anachostahili. Watawala hukabiliwa na hukumu mbaya kutokana na uonevu walioufanya wakiwa madarakani. Ahazia aliuawa kama yeye alivyowaua kikatili ndugu zake wasio na hatia. Tujifunze utawala wa kiutumishi wa Yesu. Waliomdhihaki aliwaombea msamaha na wala hakutisha watu. (Ufunuo 13:10; Mathayo 7:2; Luka 23:33-34; 1 Petro 2:23).
  4. Ingawa kwa asili wanawake ni wenye huruma wapo walio wakatili kupindukia. Athalia, mama wa Ahazia ni mfano wa wanawake hao. Aliangamiza wajukuu zake wote ili asiwepo wa kurithi ufalme. Mwanamke akijiruhusu kutumika na Shetani anaweza kufanya mengi ya kuimarisha utawala wake na akiamua kumtumikia Mungu hufanya mengi ambayo hata wanaume hawawezi kufanya. Yehosheba ni mfano wa wanawake hao ambaye kwa ujasiri mwingi na kwa kuhatarisha maisha yake alimficha miongoni mwa wana wa mfalme katika kipindi ambacho mama yake alishika utawala wa nchi kimabavu. Mwanamke katili kama Athalia anafananishwa na Kanisa lililoasi jinsi lilivyowaua watakatifu katika kipindi cha zama za giza. Kanisa hilo limehusika katika kuleta mafundisho mengi ya uongo na kupotosha ukweli (Yoshua 6:17, Yohana 4:28-30; Marko 16:1-4; Ufunuo 16:6; Ufunuo 17:6; Ufunuo 18:20).

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 23:1-21 

  1. Madaraka yanayotwaliwa kimabavu hayawezi kuwa na mwisho mwema. Mtu aliyeingia madarakani bila kufuata utaratibu anaowatawala huwa katika huzuni na hali hiyo haichochei maendeleo. Wakati fulani yanahitajika maamuzi magumu kurejesha hali ya mambo katika utaratibu uliozoeleka. Hili haliwezi kufanyika kwa matakwa ya mtu. Kurejea kwenye mapito ya zamani kunahitaji msaada wa Mungu (Yeremia 6:16).
  2. Mtu asiyefaa asiendelee kuwepo madarakani. Anaifanya taasisi anayoiongoza kukosa mwelekeo. Jambo hilo linahitaji tahadhari lisije likazua maafa makubwa zaidi na kuwagawa watu. Vyombo vya ulinzi ama vikao vya maamuzi vikubali kutumikia umma badala ya kutumikia maslahi ya watu wachache. Walio madarakani wana nafasi kubwa ya kusimamia mabadiliko ya kitaasisi kwa maslahi ya walio wengi. Yehoyada ni mfano wa watu hao.
  3. Hakuna haja ya kupambania nafasi ya uongozi. Kama unadhani ilikuwa ni halali yako kuipata muda utasema. Kila kitu kina majira yake na wakati wa Mungu ukifika umefika. Usijipambanie acha wengine wakupambanie. Yoashi ni mfano wa watu ambao hawajipambanii. Yehosheba alimficha kwa miaka sita na Yehoyada aliandaa mapinduzi ya amani ya kumuweka madarakani. Haki ya mtu haipotei.

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 24:1-27 

  1. Ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kutengeneza nyumba ya Mungu waweza kufanyika kwa kuwaendea watu majumbani mwao kama ilivyofanyika Yuda. Kuwaendea watu nyumbani kunajenga mahusiano ya karibu zaidi kati ya watoaji na wapokeaji. Sadaka hii ilitolewa na wote bila kumuacha yeyote. Sadaka hii ilikuwa ya kudumu ikitolewa kila mwaka. Ukusanyaji wa sadaka hii na ujenzi wa nyumba ya Mungu ulitakiwa uwe wa kasi. Hapa lipo jambo la kujifunza kwa makanisa yenye miradi ya ujenzi.
  2. Kiongozi aliye madarakani anapaswa ajitambue kwamba amewekwa na Mungu. Asionee wala kumpendelea yeyote. Hata waliomchagua na kumfanyia kampeni hawapaswi kupuuza maagizo yake. Yoashi hakumwogopa kumsuta Yehoyada kwa kushindwa kusimamia maagizo yake. Kiongozi asiyefanya hivyo huzalisha watu wazembe (Warumi 13:1-3; Warumi 13:7; 1 Timotheo 5:17).
  3. Kuwa na utaratibu wa kudumu wa kutoa sadaka maalum ya ujenzi wa nyumba ya Mungu kwenye kasha maalum linalowekwa mlangoni ulisaidia nyakati za mfalme Yosia. Hapa hata wale wageni wanaotembelea waweza kuacha mbaraka wao wa mchango wa jengo. Kiongozi ni yule mwenye maono na ushawishi kwa anaowaongoza ili wafikie maono hayo huku wakifurahia. Watu hawapaswi kufanya majukumu yao kwa ajili ya Mungu huku wakinung'unika (2 Kor. 9:7; 1 Nyakati 29:6-9).
  4. Wazee na wastaafu wasaidiao walio madaraka kwa ushauri mwema na kusimamia mabadiliko muhimu katika hali ya utulivu wanastahili heshima wanayopewa wafalme wa nchi. Wastaafu wenye uzoefu wa kutosha na walioisimamia kazi vyema katika siku za utumishi wao watambulike na kupewa heshima stahiki. Wawe msaada kwa walio madarakni. Na kwa wale wenye nguvu bado wapewe nafasi za kutumika.
  5. Kuwa na eneo maalum la kuzikia wafalme wa Yuda kulikuwa na faida kwa vizazi vijavyo kutopoteza kumbukumbu ya watu muhimu katika taifa. Kanisa leo likipenda linaweza kufanya hivyo kwa viongozi wake wanaofariki.
  6. Fedha inayobaki baada ya kazi iliyokusudiwa kukamilika inatakiwa irudishwe ilikochukuliwa ili ifanyiwe matumizi mengine. Utaratibu wa kujilipa fedha iliyobaki unahesabiwa kama kumuibia Mungu. Dhambi hii inaligharimu kanisa na taifa.
  7. Madaraka yanalewesha kama pombe. Yoashi aliyeanza vizuri alifika mahali akalewa madaraka. Akakubali kusujudiwa. Watu wanaosujudia wanadamu hawashindwi kusujudia miungu. Yoashi akakosa heshima ya kifalme. Akazikwa kikawaida. Hiyo ndiyo miisho ya watu wanaojikweza.

MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 25:1-28 


MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 26:1-23 

  1. Uzia akajitia nia amtafute Mungu na alipomtafuta Mungu akamfanikisha. Kuna uhusiano gani kati ya kumtafuta Mungu na mafanikio? Kujitia nia ni kufanyaje? Kama mtu anajisikia hana nia ya kumtafuta Mungu tatizo linakuwa wapi? Mtu kama huyo Mungu anamsaidiaje?
  2. Je magomvi yasiyoisha ya kubomoleana miji na majumba kati ya Israeli na Palestina yanayoendelea leo wameyarithi kutoka vita vilivyopigana hapo zamani? Je Mungu ameshindwa kukomesha vita hiyo ya ndugu wenye asili moja?
  3. Je Mungu anachangia kuwepo kwa vita hizi? Je vita hii inaweza kufananishwa na vita ya kudumu kati ya Roho na mwili? (Wagalatia 5:17; Wagalatia 4:22-23).
  4. Uzia alijenga mabirika mengi ya maji maana yeye alipenda kulima. Je kilimo na ufugaji unaokwenda sambamba na upatikanaji wa maji ya kuaminika wakati wote vyaweza kumkomboa mtu au taifa kutoka kwenye utegemezi wa kiuchumi?
  5. Je ili ufanikiwe kwenye kilimo ni lazima ukipende? Mtu anayefanya shughuli asiyoipenda anaweza kufanikiwa? Kama kazi unayoipenda haipatikani ufanye ile usiyoipenda? Unadhani kuchagua kazi ya kufanya ndiyo sababu inayofanya watu wengi wasifanikiwe leo?
  6. Je kilimo na ufugaji vina uwezo wa kutoa ajira na kuondosha tatizo la vijana wengi wanaomaliza vyuo kukosa ajira? Mfalme Uzia alisaidiwa mno ajabu hata akapata nguvu. Unadhani mfalme Uzia alifanya tahadhari ya kutosha katika kulipanga na kuliandaa jeshi lake ili kuwaepushia vifo vinavyoweza kuepukika askari wake?
  7. Mitambo ya vita aliyobuni ililenga nini? Unaona matumizi ya taaluma na elimu katika mipango yake? Kuna faida gani ya kuwa na kiongozi mwenye maono na anayethamini taaluma? Kiongozi asiuyejua na kuchunga mipaka ya kazi yake ana hatari gani katika utekelezaji wa majukumu yake na ustawi wa taasisi anayoiongoza?
  8. Je, nani ana mamlaka ya juu kuhusu masuala ya ibada kati ya kiongozi wa dini na kiongozi wa eneo husika? Je, ni halali kwa kiongozi wa serikali kulazimisha walio chini yake kufanya ibada?

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA:  2   NYAKATI 27:1-9 

  1. Habari za Yothamu ni fupi sana lakini zipo upande wa chanya. Kitu muhimu si urefu wa kipindi ulichotumika bali ni alama ulizoacha katika kipindi cha utumishi wako. Alijua mipaka ya kazi zake na hakufanya ili aonekane. Alimjua aliyemtumikia.
  2. Nguvu yetu inategemea jinsi tunavyozitengeneza njia zetu kwa Mungu. Mungu yupo tayari kutusaidia kutengeneza njia zetu kwa kuwa sisi wenyewe hatuna uwezo huo (Zaburi 40:2; Zaburi 73:2; Zaburi 119:133; Zaburi 140:4; Yeremia 10:23).

MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 28:1-27 

  1. Ahazi alianza na uasi moja kwa moja tofauti na watawala waliomtangulia walioanza vizuri na kuharibu baadaye. Ibada kwa Mungu wa mbinguni haikuwa rahisi kwa watawala kuliko ibada kwa Baali. Walipenda kumwabudu mungu baali. Ni vigumu kumtenganisha na kitu au mtu anayempenda. Mungu ndiye pekee awezaye kujenga uadui huo (Mwanzo 3:15; Warumi 7:17).
  2. Kama Mungu anakiri kabisa kuwa Ahazi ni mtu wake kwa nini anaruhusu kutiwa mikononi mwa mfalme wa Shami na wa Israeli na kupigwa sana? Mungu anapokuruhusu kumwadhibu ampendaye hufanya hivyo kwa maumivu makali. Wengi hujisahau kuwa makosa yale yale wayahukumuyo ndugu zao nao hufanya hayo hayo pia (Warumi 2:3).

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 29:1-36 

  1. Hezekia alianza kipindi cha utawala wake kwa kuwarejesha watu madhabahuni. Huduma zilizokuwa zimekoma zikafufuliwa. Matengenezo ya kweli huanza na ibada. Ibada iliyokoma nyumbani kwako huu ndiyo wakati wa kuifufua. Nunua Biblia, Nunua kitabu cha Nyimbo, nunua na Mwongozo wa Kujifunza Biblia.
  2. Kuna nyakati ambazo watu hugeuzia mbali nyuso zao na makao ya Bwana kumpa maungo tu. Wengine huwapeleka watoto wao kanisani wenyewe wakibaki nyumbani. Na wengine huja ibadani bila sadaka. Mambo hayo yanahitaji matengenezo. Mungu anawatarajie watu hao watambue umuhimu wake maishani mwao. Mungu akiwa wa kwanza maishani mwako atavifanya vingine vyote kushika nafasi ya kwanza.
  3. Wale ambao Mungu amewachagua kuwa viongozi wa kiroho wameitwa ili kumtumikia Mungu. Kila wakifanyacho wahesabu kuwa wanakifanya kwa Mungu na si kwa wanadamu. Wanamtumikia Mungu aliyeziumba mbingu na nchi. Hii ndiyo heshima ya juu zaidi awezayo kupewa mwanadamu.
  4. Upo wakati wa kuweka upya agano lako na Mungu. Unapoona mambo yako hayaendi kama ilivyotarajiwa. Wakati mikosi inapokuandama. Huu ndiyo wakati wa kujitathmini na kujitakasa. Kujidhili kwa namna hiyo kwaweza kuepusha mabaya mengi na kufungua ukurasa mpya wa maisha.

NILICHOGUNDUANAKUJIFUNZA: 2 NYAKATI 30:1-27 


NILICHOGUNDUANAKUJIFUNZA: 2 NYAKATI 31:1-21 

  1. Kama watu wangeleta matoleo nyumbani mwa Bwana, wangekula na kushiba, na kusaza tele, kwa kuwa Bwana angewabariki watu wake. Kuzuia mali ya Mungu kumetuzuilia mibaraka (Mithali 11:24). Mungu ameweka utaratibu wa matoleo ili atunufaishe sisi (Mithali 28:25).

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA: 2 NYAKATI 32:1-29 

  1. Ni muhimu kuzuia mianya ambayo adui anaweza kuitumia ili kukushinda. Kutojiandaa kushinda ni kujiandaa kushindwa. Ushindi hupatikana katika hatua za maandalizi. Unakusanya taarifa za kutosha za adui. Unapima uwezo wako. Kisha unabuni mkakati wa kumsambaratisha adui yako
  2. Hamasa kwa wapambanaji wa mstari wa mbele ni ya muhimu. Wapambanaji hujengewa uwezo kwa kutiwa moyo na kutendewa wanavyostahili. Vitendea kazi si muhimu kuliko upendo wanaooneshwa. Ni lazima wajione kuwa bora na muhimu. Ni lazima wafurahishwe mioyo yao.
  3. Lazima sisi tulio wapambanaji tutambue kuwa tunapigana kwa ajili ya nani na kwa nini? Ni lazima tutambue tumepata upendeleo kuwemo kwenye taasisi tuliyopo. Tutambue kuwa aliye upande wetu ni mkuu kuliko aliye upande wa adui. Tutambue kuwa katika mapambano haya hakuna kushindwa. Aliye upande wetu hajawahi kushindwa.
  4. Tambo katika vita ya kiroho na katika vita yeyote ile ni za muhimu (1 Wafalme 18:27). Kuzomea adui na kushangilia timu yako ni mambo yasiyoweza kutenganishwa. Hakuna namna ya kutukuza uwezo wa adui. Uwezo wa adui unapotukuzwa na unapoongelewa sana una kawaida ya kupunguza kiwango cha ujasiri.
  5. Historia ya ushindi ina nafasi katika kuandaa mazingira ya ushindi. Lakini siyo kila ushindi wa siku za nyuma wa adui waweza kuwa kigezo cha kumhofia. Ushindi wake waweza kuwa umetokana na kuwashinda wenye viwango vya chini. Adui wa kuhofiwa ni yule aliyewashinda watu wa kiwango chako au walio zaidi yako. Hata hivyo ushindi hautegemei sana historia. Hutegemea hali ya mshindani wako ilivyo siku ya tukio. Ushindi wa adui yako katika siku za nyuma hauwezi kuwa sababu ya wewe kushindwa. Hata Goliati mwenye historia ya kushinda alipigwa na kijana mdogo Daudi (1 Samweli 17:4-51).
  6. Wale wanaowashutumu watumishi wa Mungu kwa kuwasingizia uongo wanajitafutia maangamizo. Hawawadhalilishi viongozi na taasisi wanayoisimamia tu bali wanamdhalilisha Mungu mwenyewe pia. Kulilinganisha kanisa la Mungu lenye kufuata misingi ya Maandiko na makanisa yenye kubeba mapokeo ya wanadamu ni udhalilishaji kama ule uliofanywa na Senakerubi. Wanaotambua heshima ya Mungu watakapoomba wadhalilishaji hao watajikuta mahali pabaya.
  7. Kuna uwezekano wa Mungu kumtajirisha sana sana mwanadamu. Mungu hapendi tuwe maskini. Umaskini wetu waweza kuwa umetokana na sisi kutomtumainia au kushindwa kuitawala ile mali. Mungu hutajirisha utajiri udumuo na usio na majuto (Yakobo 1:17; Kumb. 8:18; Mithali 8:18; 2 Kor. 9:8). Tatizo la watu ni kutafuta utajiri kwa kutegemea akili zao wenyewe (Mithali 23:4; Wafilipi 4:19), na kuitumainia hiyo mali (1Timotheo 6:17; 1Timotheo 6:10).

MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 33:1-25 

  1. Je anayeanza kutawala akiwa na miaka 12 anapata wapi uzoefu wa kuongoza watu? Je ni nani alikuwa anaamua wawe viongo? Je, ni wao wenyewe na mfumo wa utawala uliopo au wanawekwa na wananchi? Wapo wanaodhani mfumo wa kidemokrasia haufai katika kuongoza nchi changa. Unaichukuliaje hoja hiyo ukifananisha na mfumo usio wa kidemokrasia uliokuwa ukiongoza Yuda na Israeli zamani hizo?
  2. Je watawala wanahitaji kuwekewa masharti wasiyopaswa kukiuka mara waingiapo madarakani? Kwa nini hapakuwa na mwendelezo wa yale mema yaliyofanywa na watawala wa vipindi vya nyuma? Je kiongozi akiasi ni lazima wafuasi wake wote waasi?
  3. Mungu ana uwezo wa kubashiri na kufanya uganga lakini Manase alitaka huduma hizo kutoka vyanzo vilivyopigwa marufuku? Inakuwaje mwanadamu anapoteza imani kwa Mungu na kuweka matumaini yake kwa mwanadamu mwenzake?
  4. Namna pekee kwa baadhi ya watu yakuwafanya watambue kuwa Mungu ni Bwana ni kwa kuwaingiza kwenye tanuru la mateso. Kwa nini ni vigumu kwa mwanadamu kuwa mnyenyekevu hadi ateswe kwanza?
  5. Kiongozi aliyeasi akitubu anaweza kurejeshwa kwenye nafasi yake ya awali? Kwa nini Mungu alimrejeshea nafasi yake ya ufalme baada ya kutubu? Je, Shetani angetubu kama Manase angerudishiwa nafasi yake mbinguni?
  6. Manase, tofauti na wafalme wengi waliomtangulia, alianza vibaya na kumaliza vizuri. Iliwezekanaje kwa mfalme kunyenyekea na kuanza matengezo ya toba bila kuona kuwa tendo hilo ni la kujidhalilisha? Je unaweza kumwita Manase shujaa kwa kitendo chake hicho? Kwa nini Manase anasemwa kwa mabaya zaidi kuliko kwa mazuri?

NILICHOGUNDUA NA KUJIFUNZA:  2 NYAKATI 34:1-25

  1. Umri mdogo wa mfalme Yosia haukuwa kikwazo cha yeye kushindwa kufanya vizuri katika majukumu yake. Hoja zinazotolewa na baadhi yetu juu ya kushindwa kwao kunakosababishwa na umri wao mdogo kazini zinathibitishwa na Yosia kuwa hazina mashiko. Katika uchanga wake wa umri na kazi alianza kumtafuta Mungu. Umri haumzuii Roho Mtakatifu kukufanya mkamilifu na uliyekomaa.
  2. Kutokwenda kushoto wala kulia ni kusimamia kanuni na miongozo iliyopo bila kuyumba. Taasisi nyingi zinaanguka kwa kukosa wasimamizi thabiti kama Yosia. Mungu anajua wakati atakaowaleta viongozi wa aina hiyo kuongoza kazi yake. Tumwombe Bwana wa mavuno atume watendakazi shambani mwake.
  3. Kubomoa machafu yaliyokuwepo kwenye uongozi uliotangulia kabla yako ni jambo linalohitaji ujasiri. Wengine hatua kama hiyo huilinganisha na kufukua makaburi hivyo huiepuka. Mambo yanayohitaji kubomolewa yanaweza yasionekane katika sura ya ubaya lakini ambayo yamerudisha nyuma kasi ya ukuaji wa kazi. Mipango mibovu na watu waliokuwa kwenye ajira kimakosa na kusababisha hasara kwa taasisi ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kubomolewa. Ubomoaji huu ingawa huleta maumivu huzaa matumaini mapya ya maendeleo.
  4. Utawala mpya unapoingia mara nyingi hukutana na uhaba wa fedha za kugharamia uendeshaji. Katika hali hiyo mikakati ya upatikanaji wa fedha kwa haraka kukidhi mahitaji huwa ni ya lazima. Uongozi usio na mkakati endelevu wa vyanzo vya mapato vya kuaminika una uwezekano wa kushindwa kabla haujaanza. Kama kuna eneo linalohitaji umakini mkubwa kulisimamia ni utunzaji wa mali na fedha. Matengenezo ya kweli ni lazima yaguse usimamizi wa fedha.
  5. Jamii inayojiepusha na maonyo na makatazo ya Mwenyezi Mungu inatembea gizani kwa kuwa itakuwa na upungufu mkubwa katika mambo yahusuyo maadili. Mafanikio ya taifa, taasisi au mtu binafsi yanategemea inavyolipatia kipaumbele swala la usomaji wa Neno la Mungu na uinjilisti. Neno la Mungu linapswa kulindwa kwa gharama yoyote wakati wowote (Yoshua 1:8; Wakolosai 3:16).

MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 35:1-27 

  1. Mojawapo ya mambo muhimu aliyofanya Yosia ni kumfanyia Bwana Pasaka huko Yerusalemu. Pasaka ina umuhimu gani katika kufanya matengenezo ya kiroho? Pasaka inayotukumbusha kafara ya Yesu msalabani inasaidiaje kutupatia ushindi dhdi ya maadui zetu?
  2. Je watumishi wa Mungu wanahitaji kutiwa moyo ili kutekeleza majukumu yao? Kwa nini watiwe moyo ikiwa wana wito wa kazi waifanyayo? Je na wale watumishi wa Mungu wanaolipwa nao wanahitaji kutiwa moyo? Ni madhara ya kazi pale kiongozi asipowatia moyo wasaidizi wake?
  3. Mnatumia vigezo gani kanisani kwenu kutambu kuwa pasaka (Meza ya Bwana) mliyofanya ilikuwa ya mafanikio? Unadhani ni kwa nini baadhi ya watu wanapuuza kushiriki Meza ya Bwana. Kuna faida gani kanisa zima likishiriki Meza ya Bwana. Kufanikiwa kwa Meza ya Bwana kunatokana na juhudi za Mashemasi au Wazee wa Kanisa na Mchungaji? Je Meza ya Bwana kanisani kwenu imewasaidia washiriki kuwa wanyenyekevu na wenye mshikamano zaidi?
  4. Kwaya zina mchango gani katika kuifanya Meza ya Bwana kuwa ya kipekee. Uimbaji wa kicho unaovuta hisia za waabuduo kwa Mungu aliye juu umekuwa wa kawaida kanisani kwako? Unadhani kuvaa majoho kunawatambulisha waimbaji kama wahudumu wa ibada kuliko ilivyo kwa mavazi mengine yasiyo majoho? Mwonekano wa majoho unawapunguziaje majaribu waimbaji na watazamaji wao?

MASWALI YA KUJADILI: 2 NYAKATI 36:1-23 

  1. Utawala wa Yehoahazi ulitawala kwa muda mfupi wa miezi mitatu ambapo Misri ilitumia udhaifu huo kujitwalia mali kwa njia ya kodi. Je iliwezekanaje Misri bara lililodhaniwa la giza liitawale Yuda taifa linaloongozwa na Mungu? Je kuna uwezekano leo kanisa likiongozwa na watu waliochomekwa na maadui zao?
  2. Kwa nini Nebukadreza hakutamani fedha bali alilenga kuvichukua vyombo vya nyumba ya Bwana ili vikatumike kwenye hekalu lake huko Babeli? Wageni wanaweza kuvutiwa na jambo gani katika ibada yako wanachoweza kukipeleka kwenye ibada zao? Kwa nini uchukuaji wa vyombo haukufanyika kwa mara moja bali kwa awamu tatu?
  3. Mfalme Sedekia hakujinyenyekeza mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha Bwana. Unadhani anguko la wafalme wa Yuda lilitokana na kutowasikiliza manabii wa Mungu? Ni kwa kiasi gani kanisa leo limezingatia nuru iliyotolewa na mtumishi wa Mungu Ellen G. White? Je kuna mahali mtumishi huyo wa Mungu amelionya kanisa hilo la masalio au Laodikia kukutwa na hukumu ya Mungu lisipotii na kutubu?
  4. Je kumwasi mfalme Nebukadreza kulikofanywa na mfalme Sedekia kulikuwa jambo sahihi? Machoni pa Mungu nani alikuwa bora zaidi kati ya Sedekia na Nebukadreza? Je Mungu aweza kumtumia mtawala wa kipagani kumtia adabu mtumishi anayeongoza taifa lake takatifu?
  5. Je Mungu anaporuhusu watu wake kuchukuliwa utumwani na wengine kuuawa kama ilivyotokea kwenye utawala wa Sedekia huwa anakuwa na huruma nao? Mungu akijiridhisha kuwa mtu wake haonyeki huchukua hatua gani? Je ikiwa Mungu atagundua kuwa upendeleo aliokufanyia huuthamini aweza kuondoa huo upendeleo kwako na kuukabidhi kwa wengine? Je unadhani Yuda walitambua ukweli huo?
  6. Kwa nini Mungu aliruhusu hekalu lake takatifu kuteketezwa na mfalme wa kipagani wa Wakaldayo? Je mtoto wako asipothamini mali ulizomrithisha waweza kumnyang'anya na kumpa mtu meingine?