MASWALI YA KUJADILI: YONA 1:1-17
- Je unadhani Mungu ana mpango wa kuokoa majiji ya leo kama alivyokuwa na mpango wa kuliokoa jiji la Ninawi? Ni nini kilichomvutia juu ya jiji la Ninawi? Je ilikuwa rahisi kwa Yona kwenda kuokoa wenyeji ambao walikuwa adui wa nchi yake? Je ni sahihi kukataa kazi ya Mungu ikiwa unajua hutaifanya inavyotakiwa?
- Kwa nini Yona anakuwa tayari kutumia gharama kukimbia jukumu alilopewa na Mungu kuliko kutumia gharama kuitikia wito wa Mungu? Kwa kitendo hicho Yona alistahili kuitwa Nabii wa Mungu?
- Kwa nini Yona alipokataa kazi ya Mungu, Mungu alivuruga mpango wake wa kukimbilia Tarshishi? Je matatizo yanayokupata yanaweza kuwa yametokana na kukataa kazi ya Mungu?
- Je ilikuwa sahihi kwa nabii wa Mungu kukumbushwa kuomba kwa Mungu wake na wafanyakazi wa melini? Je kuna wakati wateule huonyesha udhaifu wa kiroho kuliko wale waliotumwa kwenda kuwaokoa? Je kuna wakati ulimwengu huingia matatizoni kutokana na wateule wa Mungu kukataa kutimiza wajibu wao?
- Je, umewahi kukuta mtu mwenye wito wa kichungaji lakini akifanya kazi iliyo kinyume na wito wake? Umefanya nini kumsaidi aingie kwenye wito wake? Je inawezekana kujitambua kuwa una wito wa kichungaji?
- Je waliomtupa Yona baharini walikuwa wanamwonea huruma Yona, walikuwa wanaionea huruma kazi ya Mungu, au walikuwa wanajionea huruma wenyewe? Kitendo hicho kinafananishwa na kufanya nini leo?
MASWALI YA KUJADILI: YONA 2:1-10
- Yona aliwezaje kumwomba Mungu akiwa ndani ya Samaki? Je, Mungu anaweza kusikia sauti inayomwomba kutoka tumbo la Samaki? Kumlilia Bwana kwa sababu ya shida yako ni sawa na kumwomba? Utajuaje kuwa sasa ninamlilia Bwana? Je, ni Yona aliyejitosa vilindini au ni Mungu aliyemtosa?
- Katika hali iyo ya kutisha ya kukaa tumboni mwa nyanumi Yona alipataje ujasiri wa kumkumbuka Mungu wake? Kwa nini tunapopitia hali numu kama hizo za majaribu tunakosa ujasiri wa kumgeukia Mungu ili kupata ukombozi? Je tunahisi Munu ametuacha?
- Mungu alimwambia nini yule Samaki hata akamtema Yona pwani? Je Mungu alimbembeleza au alimwamuru? Je kuna kifungo kigumu Mungu asichoweza kukufungua? Je shetani ana uwezo wa kumzuia Mungu asikutoe kwenye kifungo alichokufunga?
MASWALI YA KUJADILI: YONA 3:1-10
- Kwa nini hatimaye Yona alikubali kwenda Ninawi kuhubiri kile Mungu atakachomwamuru? Je kuna watu ambao hawawezi kufanya kazi ya Mungu hadi waadhibiwe?
- Je kuna uwezekano leo wa kuendesha mahubiri katika mji mkubwa kama wa Ninawi ukiwa peke yako? Je muujiza wa Yona kukaa tumboni mwa samaki kwa siku tatu ulichangia watu kumuamini?
- Je kuna wakati tumesita kufanya kazi ya Mungu kwa kudhania kuwa watu tunaowaendea watakataa kupokea ujumbe? Witikio wa watu wa Ninawi unatufundisha nini kuhusu dhana hiyo?
- Viongozi wa kijamii na watawala wana nafasi gani katika kusaidia kuenea na kupokelewa kwa ujumbe wa wokovu? Kuna umuhimu au ubaya gani katika kushirikiana na viongozi hao kwenye kazi ya Mungu?
- Je kuna uwezekano wa yale mapigo yaliyotabiriwa siku za usoni kwa wasiomtii Mungu kubadilishwa na yasitokee kama tunavyohubiri sasa?
MASWALI YA KUJADILI: YONA 4:1-11
- Kwa nini Yona alichukizwa na kitendo cha Mungu kuwasamehe Waninawi? Je, hakupenda waokolewe? Je, aliona aibu unabii wake kutotimia? Au alitaka Mungu ashauriane naye kwanza kabla hajawasamehe? Je alijiona kuwa anastahili kuliko Waninawi? Yona alipokubali kuifanya kazi ya kuhubiri aliikubali kwa moyowote au kwa shingo upande?
- Kitendo cha Yona kutamani kufa kwaweza kuchukuliwa kuwa ametenda dhambi ya kuua tayari? Je kama Yona angejiua angepokelewa mbinguni? Kwa nini Mungu huongea lugha ya upole anapoongea na watu waliokasirika? (Mwanzo 4:4-7). Kama Mungu alimponya Yona katika hali yake mbaya ya kuwakiwa jua kwa nini hakuona kulikuwa na haja ya Mungu kuwaokoa Waninawi katika hali yao mbaya ya dhambi?