Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

GABRIEL MBWANA

Gabriel Hassan Mbwana (1933-1994)

Gabriel Hassan Mbwana alizaliwa mwaka 1933 na Hassan Mbwana na Nanguma Chali katika kijiji cha Sangana, Kata ya Chome, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Alikuwa mtoto wa tano kati ya watoto saba.

Elimu:

Mbwana alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi ya Kati ya Gwang'a iliyokuwa inaendeshwa na madhehebu ya Kiluteri kati ya 1940 na 1941 kisha akahamia Shule ya Kati ya Suji Mission ambako alimalizia darasa la saba. Alipobatizwa, alibadilisha jina lake kuwa Gabriel kutoka jina la awali la Mroki. Mwaka 1948 alikwenda Shule ya Sekondari ya Ikizu na baadaye akajiunga na Chuo cha Ikizu ambako alipata mafunzo kwa miaka miwili katika kozi ya uinjilisti wa walei. Baada ya kozi yake ya uinjilisti wa walei, alianza kufanya kazi ya ualimu huko Utimbaru, wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Mnamo Januari 1955, Gabriel Mbwana alimuoa Orupa Nangasu Yona na kwa pamoja walijaliwa kupata watoto sita: Geoffrey Mbwana (makamu wa mwenyekiti wa Konferensi Kuu), Yona, Guheni, Grace, Cliver na Justine. Kuanzia 1957 hadi 1960 Mbwana na familia yake waliishi katika Chuo cha Waadventista cha Bugema (sasa Chuo Kikuu cha Bugema) huko Uganda ambapo alisoma diploma katika programu ya mafunzo ya uchungaji.

Uchungaji

Kazi yake ya kwanza baada ya kuhitimu ilikuwa mwaka 1961 mkoani Tabora ambako aliwahi kuwa mchungaji wa mstari wa mbele. Ili kuendeleza ujuzi na utaalamu wake katika kazi ya Mungu, aliomba kujiunga na Chuo cha Kumbukumbu ya Spicer nchini India ambako alisomea shahada ya kwanza ya elimu ya dini kuanzia mwaka 1981 hadi 1985. Alipomaliza shahada yake ya kwanza alijiandikisha katika programu ya shahada ya uzamili iliyomchukua miaka mingine miwili na kuhitimu mwaka 1987.

Aliporejea nyumbani, aliteuliwa kuhudumu kama mkurugenzi wa idara ya Huduma Binafsi na Shule ya Sabato katika Tanzania General Field. Mabadiliko yalipofanywa katika uongozi wa fildi, alichaguliwa kuwa mwenyekiti. Kisha aliteuliwa kama mkurugenzi wa Sauti ya Unabii. Mwaka 1991 aliteuliwa kuwa mwinjilisti wa Union Misheni ya Tanzania, nafasi ambayo ilimlazimu kusafiri sana ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kampeni, semina na makongamano mbalimbali ya uinjilisti. Alipokuwa akihudumu katika wadhifa huu aligundulika kuwa na saratani ya tumbo aliyopambana nayo hadi Mei 1994 alipolala usingizi wa mauti. Alizikwa katika kijiji alichozaliwa cha Sangana.