MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 1:1-27
- Kwa nini baada ya kufa kwake Sauli mtu alimwendea Daudi na kumsujudia? Je ilikuwa lazima taarifa za kifo cha Sauli zimfikie Daudi? Unadhani Daudi alizipokeaje taarifa za kifo cha Sauli na Yonathani? Ukisikia adui yako amekufa unahuzunika au unafurahia? Kwa nini mleta taarifa alikuja kwa Daudi akiwa na taji iliyokuwa kichwani mwa Sauli? Je alikuwa anakusudia kumrahisishia kujitangaza kuwa ndiye mfalme mpya wa Israeli?
- Je Daudi alimtilia shaka mleta habari hata akamuuliza ulijuaje Sauli na mwanae Yonathani wamekufa? Mleta taarifa hakutumwa na mtu kuleta taarifa zile zilizosababisha kifo chake. Je, angejua kwamba zingemletea madhara angezileta? Utajuaje kama habari unayompelekea mkubwa wako itamfurahisha ama haitamfurahisha? Unaiona hali ya kujipendekeza kwa wakubwa kwa mleta taarifa huyu? Je kuna wakati uchawa waweza kumletea madhara mtu?
- Daudi anamwita Sauli shujaa. Je, ushujaa wa Sauli ni upi? Ni vizuri kuwasema vizuri viongozi wa watu hata kama katika uongozi wao wameonyesha udhaifu mkubwa? Kwa nini Daudi aliuita upendo wa Yonathani kwake kama upendo wa ajabu uzidio ule wa mwanamke? Je kati ya mwanaume na mwanamke ni yupi anayependa zaidi?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 2:1-32
- Kawaida ya Daudi ya kumuuliza Mungu ushauri kabla hajatenda jambo inatokana na nini? Alitumia njia gani kupata majibu ya maswali yake? Je katika zama hizi za maendeleo ya sayansi ipo haja ya kufanya hivyo? Kwa nini Abigaili bado anatajwa kama mkewe Nabali? Je kutajwa kwa wake zake wawili kunaashiria mchango wao katika ushindi ambao Daudi alikuwa akiupata?
- Kufa kwa Sauli hakukumaliza utawala wake. Je ili kumaliza utawala huo palihitajika maridhiano au mapambano? Je marishiano yakishindikana huwa lazima kuwe na mapambano? Kwa nini Mungu hakuruhusu Daudi kuingia madaraka kwa amani bila kuhitajika kumwaga damu?
- Wazo la uwakilishi tunaliona katika vita ya kujipima ubavu iliyofanywa na vijana 12 kutoka kila upande. Unadhani kulikuwa na haja ya kuwa na vita ya namna hiyo? Je wanaomwakilisha Kristo wakishindwa ni Kristo ameshindwa? Je Asaheli alikufa kizembe au kishujaa? Kwa nini alikataa maridhiano na kupoteza maisha ila bosi wake Yoabu alikubali maridhiano na kuepusha vifo zaidi? Je ushauri wa Abneri ulikuwa wenye maana?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 3:1-39
- Upo wakati wa wewe kustawi na adui yako kuendelea kudhoofika. Unadhani wakati wako wa kuimarika na adui yako kudhoofika utafika? Ili kufanya wakati huo ufike unahitaji kumtumainia Mungu? Ni kweli kuwa wakati wa Mungu ukifika huwa umefika?
- Ishboshethi mwana wa mfalme Sauli alimkemea Abneri jemedari wa jeshi la baba yake kwa kutembea na mke (suria) wa baba yake. Je utetezi wa Abneri kuwa alistahili kujizawadia baada ya kazi ngumu ya kuitetea familia yao ulikuwa sahihi? Je dhambi inapotendwa na mtu mkubwa mtu mdogo ana nafasi ya kuikemea?
- Daudi anatoa sharti la maridhiano na Abneri wa jeshi la Sauli la kuletewa mke aliyemuoa kwa gharama ya mahari ya govi 100 za Wafilisti. Je Daudi alikuwa na uhalali wa kurudishiwa huyo mke? Kwa nini mume wa Milka alimsindikiza mkewe huku akilia?
- Abneri alifanya jitihada za kuwashawishi watu wake wamkubali Daudi kuwa mfalme. Kwa nini mtazamo wake ulibadilika hivyo baada ya Sauli kufa? Je viongozi wa aina hii walio tayari kupoteza ushindi ili kudumisha amani wanahitajika katika jamii zetu?
- Daudi alikuwa na nia ya maridhiano lakini wasaidizi wake hasa Yoabu hawakuridhia maana alitaka kulipiza kisasi. Unadhani Daudi alifanya jitihada za kutosha kuwashawishi wasaidizi wake waridhie maridhiano? Kwa nini Daudi alilia sana kwa ajili ya kifo cha Abneri?
- Unadhani kilichomliza zaidi ni kumkosa Abneri kwa kuwa angekuwa msaada katika kuwaunganisha Waisraeli au kutokana na aina ya kifo alichokufa?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 4:1-12
- Wimbi la kushindwa lilikuwa limeikumba Israeli wakati wasaidizi na washauri wa Sauli walipokuwa wanamalizana wenyewe baada ya kifo chake. Je Mungu alikuwa ameikataa Israeli? Je alikuwa analipiza kisasi kwa niaba ya Daudi? Mefiboshethi alipata ulemavu kwa kudondoka kutoka kwa yaya wake baada ya kupokea taarifa za kifo cha za Sauli na Yonathani. Unadhani mtoto wa Yonathani alistahili hali hiyo baada ya baba yake kufanya wema wote juu ya Daudi mtumishi wa Mungu?
- Je, walioleta taarifa za kifo cha Ishboshethi aliyekuwa kinyume cha maridhano ya taifa la Yuda na Israeli walikuwa na upendo wa kweli na Daudi au waliķuwa wambea? Kwa nini Daudi alikuwa kinyume na waliokuwa wanamletea taarifa mbaya za viongozi wa taifa? Alitaka kuleta fundisho gani kwa raia wake?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 5:1-25
- Kauli ya kabila zote za Israeli kwa Daudi wakisema; "sisi tu mfupa wako na nyama yako" huashiria kuwepo kwa mahusiano ya karibu sana kati ya mtawala na watawaliwa. Hali hii inapokosekana kwenye jamii zetu ni nani wa kulaumiwa? Daudi aliwezaje kuwaongoza Israeli watoke nje na ķuingia ndani wakati wa utawala wa Sauli? Je kuna uwezekano mtu fulani akawa faraja kwa raia au wanafamilia wakati wa mtawala katili?
- Daudi alitiwa mafuta na Samweli awe mtawala wa Israeli, ilikuwaje akawekewa mikono tena ya kuwa mfalme na wazee wa Israeli? Daudi alijipatia ushindi mkuu kwa vita alizopigana akiwa na taifa la Israeli na zile alizopigana nje ya nchi na kuwa na wafuasi wengi hata akiwa hajafikisha miaka 30.
- Hii inakuambia nini juu ya uwezo wa vijana kuongoza jumuiya za kidini na serikali za kidunia? Daudi alijenga mahusiano bora na majirani hata mfalme wa Tiro akamjengea nyumba. Mahusiano mema na wale tunaodhani ni adui zetu yanasaidiaje? Je ilikuwa halali mfalme wa nchi kujengewa nyumba na mtawala wa kigeni?
- Daudi licha ya mafanikio yake katika maeneo mengi alikuwa na udhaifu na wanawake. Je kitendo chake cha kuoa wake wengi na masuria kinahalalisha ndoa ya mitara? Je kupenda wanawake ni mojawapo ya majaribu yanayowakabili watawala na viongozi hata sasa?
- Kwa nini Mungu hakumchukulia hatua Daudi kwa kitendo chake cha kuoa wake wengi? Au hii ndiyo maana ya kusema, "zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu." (Matendo 17:30)
MASWALI YA KUJADILI 2 SAMWELI 6:1-23
- Hatua ya kwanza ya utawala wa Daudi ni kulirejesha Sanduku la Bwana katika nyumba yake Yerusalemu. Kwa nini Mungu aliruhusu sanduku lake kukaa mikononi mwa mataifa ya kipagani kwa muda wote huo? Kwa nini alisubiri hadi Sauli afariki? Kwa nini Uza alipogusa gari lililobeba sanduku la Agano alikufa lakini mfalme Nebukadneza wa Babeli alipotumia vyombo vitakatifu kunywea pombe hakufa pale pale?
- Sanduku la Agano lilikuwa na umuhimu gani kwa Mungu na kwa Wa israeli?Kuimba na kucheza kuliwezaje kukubalika wakati wa kurejesha Sanduku la Agano? Kwa nini kuimba na kucheza kwenye ibada huwa ni jambo lisilokubalika? Je ujio wa Sanduku la Agano ulipokelewaje na mfalme na raia wake baada ya kifo cha Uza? Je ni sahihi kuwasaidia mashemasi kuandaa meza ya Bwana kama wewe siyo shemasi?
- Wakati wengine wakilalamikia kazi ya Mungu kuwatia hasara wengine wamekiri kubarikiwa kwa kufanya kazi ya Mungu. Je, kunung'unika wakati wa kufanya kazi ya Mungu kwaweza kuchelewesha mibaraka ya Mungu? Je ni halali kujituma kwa kazi ya Mungu hadi watu wako wa karibu kama mke na mume wakakudharau?
- Je, ukiwa kiongozi wa nchi ukahitaji ubatizo utazamishwa kwenye maji mengi kama Yesu alivyobatizwa au itabidi utafutiwe utaratibu maalum ili usiaibishe cheo chako? Unadhani kauli ya Mikali mke wa Daudi na binti wa Sauli iliyolaumu kitendo cha Daudi cha kuonesha maungo yake mbele ya vijakazi ilikusudia kumpa Mungu utukufu au kumdhalilisha mfalme?
- Jibu la Daudi lilikuwa na fundisho kwa mkewe Mikali na kwa wote walioisikia laumu ile. Je, unadhani Daudi alifanikiwa kwa kauli na kwa vitendo kuwaonyesha wahudhuriaji wa hafla ile kuwa yupo Mungu astahiliye kuheshimiwa kuliko yeye mfalme wa Israeli? Je viongozi wote wangefanya hivyo kungekuwa na ustawi mkubwa kuliko walionao leo?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 7:1-29
- Mungu huwafanikisha wanadamu ili waweze kuitegemeza kazi yake. Kwa nini watawala na viongozi wengine wakiingia madarakani hawafikirii kuinua hali ya taasisi na maeneo wanayoyasimamia badala yake hufikiria kujinufaisha wao na jamaa zao? Kipaumbele cha Daudi kilikuwa kwa kazi ya Mungu au maslahi yake binafsi?
- Kutokana na yale Daudi aliyokuwa anayapitia ungeweza kudhani kuwa Mungu alikuwa pamoja naye? Je unaweza kujiona una mikosi kwa matukio yakupatayo na kumbe ikawa njia ya kukufikisha kwenye kilele cha mafanikio? Wakati Daudi akitamani kumjengea Mungu nyumba ya ibada Mungu anamtokea Daudi na kuahidi kumjengea nyumba. Kama Mungu anaweza kutujengea nyumba kwa nini asijenge nyumba yake mwenyewe?
- Kuonesha nia ya kuitegemeza kazi ya Mungu kwaweza kumfungulia mtu baraka? Kuitegemeza kazi ya Mungu kunahitaji kibali chake. Kwa nini kuna watu hawapewi kibali cha kuitegemeza kazi ya Mungu? Je ni sahihi kujisikia umependelewa unapoifanya kazi ya Mungu?
- Kuna wakati Mungu humuita mtu katika nafasi ya uongozi ili afanye maandalizi ya kile kitakachokamilishwa na mrithi wake. Kwa nini watu huwa wagumu kuwaachia warithi wao mipango na hazina ya kufanikisha majukumu katika kipindi kijacho? Kwa wanaorithi mikoba ya uongozi hawaendelezi mazuri waliyorithi kwa watangulizi wao?
- Inaonekana Daudi licha ya mapungufu yake kadhaa alijua kuchukuliana na Mungu wake na kubarikiwa sana naye. Unatakiwa kufanya nini ili kushiriki mibaraka ya Mungu kama Daudi?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 8:1-18
- “Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.” Ni mazingira gani yanahitajika ili Mungu ampe mtu kushinda kila anakokwenda? Daudi aliviweka wakfu kwa Bwana mali alizoziteka vitani. Hii inaweza kuwa mojawapo ya siri ya ushindi wake kila alikoenda? Daudi alionekana kuwa katili kwa mataifa ya kigeni na kuhukumu kwa haki juu ya watu wake? Hii ni kanuni muhimu ka kiongozi wa kiroho?
- Unadhani nini kilimwongoza Daudi kuwafanyia hukumu na haki watu wake wote? Je kipindi cha kuandamwa na mfalme Sauli kilimfinyanga na kumwandaa kuwa mtawala mwema? Je, kiongozi wa watu ni yule anayeheshimiwa au anayeogopwa? Unadhani Sauli aliheshimiwa au aliogopwa?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 9:1-13
- Unafanya nini kuwaenzi waliokutangulia kwenye wadhifa ulionao na kwa marafiki waliochangia mafanikio yako? Je unakubaliana kuwa njia bora ya kumkumbuka rafiki aliyetangulia mbele ya haki ni kuwatunza aliowaacha nyuma na hasa watoto wake? Unawatendea nini waliokuwa madarakani kabla yako?
- Je unatambua mchango wao au unawapoteza katika ramani wasiendelee kutajwa? Je watu hao wanaweza kuwa mwiba kwa uongozi wako? Wema hauozi ni kauli inayothibitìka kwa wema ambao Yonathani alimtendea Daudi wakati wa uhai wake. Je Mefiboshethi alistahili kula chakula kwenye meza ya mfalme? Je ni kweli kuwa baba yake asingempa Daudi kipaumbele huenda hiyo ikulu ingekuwa yao na baba yake angekuwa mfalme?
- Wakati fulani wastaafu au wajane na yatima hunyimwa stahiki zao kwa sababu ya kulipiza kisasi juu ya yale wao au jamaa zao waliyotenda wakiwa madarakani. Je ni halali kufanya hivyo au si halali? Je kati ya kusaidiwa chakula na kurudishiwa shamba upi ni msaada wa maana zaidi?
- Je wenye ulemavu wanasaidiwaje katika jamii yako? Wanapewa upendeleo maalum? Je huo ni upendeleo au ni haki yao? Je kula meza moja na mwenye ulemavu kulikuwa kunaidhalilisha ikulu? Siba ni mfano bora wa wasaidizi wa nyumbani wenye upendo wa dhati. Unadhani wasaidizi wa nyumbani mwako wanaowajali sana watoto wako wanastahili kutendewa nini? Je mshahara peke yake unatosha?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 10:1-19
- Daudi akiwa na nia njema ya kujenga mahusiano na jirani zake anakutana na mkwamo baada ya washauri wa mtawala jirani kutafsiri vibaya nia yake. Unadhani migogoro mingi hutokea kwa njia ya kutafsiri vibaya kauli na vitendo? Nini kifanyike kuepusha kauli na vitendo vyako kutafsiriwa vibaya? Unadhani wakuu wa wana wa Hanuni walikuwa na nia njema na bwana wao?
- Je kulikuwa na ulazima wowote wa kuwadhalilisha wajumbe wa Daudi kiasi kile? Dharau na kudhalilishana huchangiaje kuvunjika kwa mahusiano? Migogoro mingi inayogharimu maisha ya watu na mali zao ingeweza kuepukwa kama watawala wangetumia diplomasia zaidi katika kuitatua kuliko matumizi ya nguvu. Je unaiona vita baina ya Israeli na mataifa yanayowazunguka ilikuwa ya lazima?
- Je kuna ukweli kuwa mara nyingi raia huumia kutokana na kiburi cha viongozi wao? Je ni lazima watu wapigane kwanza ili watu waheshimiane na amani ya kweli iweze kupatikana? Je kama Daudi angepuuza dharau waliyofanyiwa wasaidizi wake vita hii ingeepukwa? Je hapa ndipo pa kutumia kanuni ya "Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu."? (Luka 6:29)
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 11:1-27
- Wakati wa faragha usio na jambo maalum linaloshughulisha mwili na akili ni mazingira yanayotumiwa na mwovu kuwaletea majaribu watumishi wa Mungu. Unadhani Daudi angeenda vitani angekutana na jaribu la Bath-sheba? Unadhani kisa hiki kilikuwa na umuhimu wowote wa kuandikwa? Ni nani mwenye makosa kati ya Daudi aliyekuwa darini na mwanamke aliyekuwa anaoga eneo linalomfanya aonekane na aliye darini?
- Madaraka yanalewesha usipojua namna ya kuyatumia. Je ilikuwa halali kwa Daudi kuwatumia walio chini yake kwa kutumia madaraka aliyonayo ili kufanikisha maslahi yake binafsi? Je wajumbe waliotumwa kwenda kumchukua Bath-sheba walikuwa na uwezo wa kumsaidia mfalme asifanye dhambi hiyo? Kwa nini mke wa Uriah hakuwa jasiri wa kukataa kufanya uzinzi na mfalme hali akijua tendo hilo ni dhambi?
- Daudi alijisikiaje askari wake mwaminifu alipokataa kwenda kulala na mke wake wakati jeshi likiwa vitani? Alijihisi hatia moyoni? Je waumini wasipojishughulisha kufanya kazi ya Mungu kuna uwezekano wa Shetani kuwapa shughuli ya kufanya? Kama wanaume wanavutwa kirahisi kufanya ngono kwa kuangalia maungo ya mwanamke je, wanawake wanapaswa kujisetiri kwa kuvaa nguo za adabu ili kuwanusuru wanaume au wanaume wapambane wao wenyewe na hali yao?
- Je inawezekana kumwangalia mwanamke mzuri usimtamani? (Ayubu 31:1). Watawala wanahusika na vifo vya wasaidizi wao wanaotofautiana nao kwa mtazamo. Unadhani kulikuwa na namna ambayo Uria angeepuka kifo kilichompata? Je Yoabu alifanya wajibu wake kutekeleza mauaji ya Uria? Je, kosa la Uria ni nini? Je Uria anahesabiwa kuwa alikufa kama shujaa au alikufa kizembe?
- Je Uria aliponzwa na uzuri wa mke wake, uzembe wa mke wake, au uaminifu wake? Je Bath-sheba aliumia kwa kuwa mumewe amekufa vitani au kwa kuwa amekufa kutokana na mahusiano yake na mfalme? Je, ni rahisi kiasi gani wasaidizi kujua maovu yanayotendwa na wakuu wao? Je wasaidizi wanaojua uovu unaotendwwa na viongozi wao hunufaikaje kama matokeo ya kujua huko?
- Je unadhani viongozi wa aina ya Daudi wana uwezo wa kukemea maovu yanayotendwa na wasaidizi wao? Je kulikuwa na sababu yoyote kwa Daudi kumtwaa mjane wa Uria kuwa mke wake? Unadhani kuolewa na mfalme kulileta faraja yoyote kwa Bath-sheba?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 12:131
- Je panahitajika umakini katika kumfanya mtu atambue kosa lake? (Wagalatia 6:1) Je, watu wenye ushawishi katika jamii wanaonywa kwa namna iliyo sawa na wengine? Je kila maonyo ni lazima yafanyike kwa faragha? (1 Timotheo 5:20). Je, nabii Nathani alikuwa anahatarisha maisha yake kwa kwenda kumjulisha mfalme dhambi yake?
- Unapohisi kusita kwenda kumwambia mtu dhambi yake unapaswa kufanya nini? Je kazi ya kuwaambia watu makosa yao inahotaji karama kutoka kwa Mungu au ni kazi ambayo yeyote anaweza kuifanya? Kwa nini Daudi hakuchukua mmoja wa wake zake ili kukidhi hisia zake na badala yake akaenda kuchukua mke wa mtu mwenye hadhi ya chini kuliko yake?
- Nini kinathibitisha kuwa aziniye hana akili? (Mithali 6:32). Kwa nini wenye dhambi huwa wasio na huruma na wenye dhambi wenzao? Kwa nini hasira wanayoionesha kwa wenye dhambi wenzao hawaionyeshi kwao wanapofanya dhambi ile ile? Ni kweli kuwa Mungu ndiye aliyempa Daudi wake aliokuwa nao? Je, adhabu ya Mungu kwa Daudi ilikuwa ya kikatili au inayostahili?
- Je Mungu akiruhusu wake wa Daudi walale na jirani yake wa kiume huo hauwezi kuwa udhalilishaji kwa hao wanawake? Kwa nini waadhibiwe wao kwa kosa la mume wao? Je msamaha wa haraka wa Nabii Nathani kwa Daudi ulitokana na toba ya dhati ya Daudi isiyo na konakona? Je mtu anayekiri makosa yake anaweza kusamehewa kwenye kanisa lenu au nyumbani kwenu?
- Kwa nini Daudi hakuondolewa kwenye nafasi yake ya ufalme kutokana na dhambi aliyofanya? Yoabu ni mfano mzuri wa watumishi wasiotafuta kujitwalia sifa au utukufu bali hutaka mkubwa wake aonekane ndiye aliyefanya hilo jema. Aliwezaje Yoabu kumpa Daudi upendeleo wa kushinda na kutukuzwa mbele ya watu wote hali akijua bosi wake anatuhumiwa kwa uzinzi?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 13:1-39
- Mpango wa Amnoni kumbaka Dada yake ulifadhiliwa na rafiki yake Yonadabu ambaye alionekana kumuonea huruma anavyoteseka kwa ajili ya Tamari. Marafiki wana nafasi gani katika kuwashawishi watu kutenda dhambi? Kwa nini wanaowashawishi watu kutenda dhambi huonyesha kama wanawahurumia? (Mwanzo 3:1). Unadhani Yonadabu ni rafiki wa kweli?
- Watu wengi hubakwa au kulawitiwa na jamaa zao wa karibu au na wachumba zao kwa sababu ya kutotambua mitego waliyowekewa na nia ovu za watu hao. Je ni mazingira gani huwa si salama kwa mtu kuwepo na mtu wa jinsia nyingine? Ni viashiria gani vinaweza kukutambulisha hatari ya kuingiliwa kimwili? Je kubakwa kwa Tamari kulitokana na uzembe wake au makosa ya Baba yake?
- Kwa nini Amnoni hakusikiliza kilio na ushauri wa Tamari dada yake alipomsihi wasitende dhambi ya uzinzi? Je kufanya ngono kabla ya kuoana ni dhambi? Je Amnoni angeomba kumuoa Tamari Daudi angemkubalia? Kwa nini baada ya wavulana kulala na wasichana huwaruka na kuwachukia kuliko hapo mwanzo? Ule upendo wa awali huenda wapi? Kwa nini wanapowapa ujauzito hukataa kuwaoa?
- Licha ya kukasirika kwa taarifa ya Amnoni kumbaka dada yake Tamari Daudi hakumchukulia hatua yoyote Amnoni. Unadhani ni kwa nini Daudi hakuchukulia dhambi hii kwa uzito unaostahili? Absalomu alikusudia kulipiza kisasi kwa Amnoni sababu ya kumbaka dada yake Tamari. Unadhani hatua aliyochukua Absalomu ya kumuua Amnoni ingeweza kuepukwa kama Daudi angelisimamia vyema tatizo lililosababishwa na Amnoni?
- Ugomvi wa watoto unapaswa kuamuliwa na watoto wenyewe au na wazazi wao? Je Daudi alinusa uwezekano wa kutokea kwa mauaji alipokataa kuhudhuria sherehe iliyoandaliwa na Absalomu? Je alichofanya Absalomu kilikuwa sahihi? Unadhani Yonadabu alijisikiaje baada ya kifo cha Amnoni aliyemsababishia kufanya dhambi iliyopelekea kifo chake? Je ni sahihi kumuita Yonadabu kama ndumila kuwili anayejipendekeza kila upande?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 14:1-33
- Mgogoro unapoacha kushughulikiwa kwa wakati kwenye ngazi ya familia huweza kukua na kulisumbua taifa zima. Unaiona hali hiyo katika nyumba ya Daudi? Kwa nini Daudi anaonekana kutaka kuchukua hatua kali kwa Absalomu lakini hakufanya hivyo Amnoni alipokosea? Je anahofia ushawishi alionao Absalomu kwa watu au amezinduka usingizini?
- Kiongozi wa kiroho anapokuwa na mgogoro na familia yake unaotishia kuleta mpasuko kwenye jumuiya ya kidini ni nani anastahili kuchukua hatua za kuwapatanisha na kuepusha mpasuko? Je hatua aliyochukua Yoabu ilikuwa sahihi? Kwa mara nyingine tena matumizi ya kisa yanasaidia kufikisha ujumbe kwa mfalme bila kusababisha madhara kama ilivyokuwa kupitia Nabii Nathani. Je kumshawishi mtu kunahitaji matumizi makubwa ya akili au kunahitaji ushawishi wa Roho Mtakatifu?
- Je kisa chaweza tumiwa na Roho Mtakatifu kumsaidia mtu kufanya maamuzi? Ni nini maana ya kuwa na busara kama nyoka na kuwa na upole kama hua? (Mathayo 10:16; 1 Wakorintho 9:19-23). Je inawezekana kutunga kisa ili kufikisha ujumbe au visa vyote vinatakiwa kuwa halisi na si vya kutunga? Mambo gani ya kuzingatia katika visa vya kutunga? Je, ni sahihi kukata mawasiliano na mtoto kwa miaka miwili kwa makosa aliyokutendea?
- Je anatakiwa kufanya nini mtoto anayetamani kukutana na baba yake aliyemkosea ili kurejesha mahusiano? Kati ya baba aliyekosewa na mtoto aliyemkosea baba ni nani anayehitaji usuluhishi zaidi? Kwa nini mara nyingi mahusiano ya baba na vijana wao wa kiume huwa katika mivutano? Je kuna wakati watoto wa kiume hasa wanaosifiwa na watu kwa uzuri au wenye vipaji maalum huwadharau baba zao? Ni umri gani wenye tatizo hilo hasa?
- Kwa nini vijana wakubwa wa kiume hung'ang'ania kutaka kukaa na wazazi hata kama umri unawaruhusu kujitegemea? Yoabu na yule mwanamke 'mwenye akili' walihatarisha maisha yao kwa kuchukua hatua za kumpatanisha mfalme Daudi na mwanae Absalomu.
- Je hasara ya kuchomewa mashamba ilikuwa ya lazima au ilitokana na kutokamilisha kazi aliyoianza kwa uzembe? Je kuchomewa mashamba kulisaidia kuharakisha mapatano ya Absalomu na baba yake? Je unadhani yule mwanamke anastahili kuitwa mwenye akili?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 15:1-37
- Je kupenda madaraka ya kiroho ambayo Mungu hajakupatia ni dhambi? Je ukiingilia majukumu ya watu wengine unaodhani hawawahudumii watu ipasavyo ni vibaya? Kama nikihisi watu hawatendewi ipasavyo wajibu wangu ni nini? Je mtu anaweza kujifahamu mwenyewe kuwa ana uwezo wa kuhudumia watu vizuri zaidi kuliko wale waliopo madarakani?
- Absalom alikuwa mtoto mwongo aliyewadanganya rai ana mfalme Daudi baba yake. Unadhani hii ni mojawapo ya tabia zilizompelekea kukumbwa na majanga na kifo cha aibu katika siku za usoni. Kwa nini watu waongo na wenye hila huwa na wafuasi wengi? Itai Mgiti alikuwa na upendo wa dhati na mfalme Daudi maana alikataa kutoandamana naye. Nani mwingine alikuwa na upendo kama huu katika Biblia?
- Kwa nini Daudi aliagiza sanduku lirudishwe Yerusalemu? Mzazi anapolia huku akiwa amevua viatu kwa sababu ya vitendo vya uasi vya mwanae huwa na uwezekano wa kumletea mikosi mtoto huyo? Unadhani kitendo cha Daudi kumkimbia mwanae Absalomu na kuiacha ikulu haina ulinzi wowote ilikuwa sahihi?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 16:1-23
1. Je ni kweli kuwa Mungu alikuwa amemwagiza mlaani Daudi au ni roho ya kiungwana aliyokuwa nayo Daudi ya kutotaka kuhukumu watu? Ni halali kwa raia kumtukana au kumlaani mtawala hata kama unadhani amekudhulumu? Unapoadhiriwa mbele ya watu na raia wako unapaswa kuitikia hali hiyo kwa kufanya nini? Je, ni wajibu wa raia mwema kumlinda na kumtetea mtawalaasidhalilishwe na watu?
2. Unapokuwa kwenye vita ya kulilia madaraka ni vyema kumwachia vita hiyo Mungu ili akupiganie au upigane wewe mwenyewe? Je ni kweli kuwa makosa mengi yafanywayo na watawala yanatokana na ushauri mbovu wa washauri wao? Je ni sahihi kwa mtawala kupima ushauri anaopewa na kuukataa ule unaopotosha? Je kitendo cha Absalomu kuzini na wake za baba yake ulikiuka maadili na kumuondolea sifa ya kuwa mtawala wa Israeli?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 17:1-29
- Absalomu analiona shauri la kumuua baba yake kuwa ni jema. Unapogundua mwanao anakuchukia kwa kiwango cha kutaka kukuua unafanyaje? Kwa nini wanaogombea vyeo mara nyingi huwa na roho ya kuondoa uhai wa wenzao? Ushauri unaweza kupotosha au kusaidia kufanya maamuzi sahihi. Mara nyingi Daudi alifanya maamuzi kwa kushauriana na Mungu kwa nini Absalomu anayetamani kukalia kiti cha ufalme anatafuta ushauri kwa watu?
- Utajuaje kama ushauri unaopewa ni wa kuhatarisha maisha yako au la? Utakuwaje na uhakika kama unayemweleza siri zako hatazifikisha kwa adui yako? Unadhani kwa mwanzo huu wenye kutia shaka Absalomu angeyamudu madaraka ya ufalme aliyokuwa akiyatafuta kwa udi na uvumba? Kwa nini Daudi alikuwa na bahati ya kujulishwa mikakati ya adui zake? Je alikuwa anakubalika kama kiongozi sahihi aliyewekwa na Mungu au watu walikuwa wanajipendekeza?
- Ahithofeli alijinyonga baada ya ushauri wake kupuuzwa, ushauri ambao aliamini ungeokoa maisha ya Absalomu na kumwangamiza mfalme Daudi. Unadhani alikuwa na sababu ya msingi ya kujiua? Mtu anayejiua amekata tiketi ya kwenda motoni au anaweza kwenda mbinguni? Je kuna namna yoyote ya kumsaidia anayetaka kujiua? Je anayejiua anastahili kufanyiwa mazishi ya Kikristo?
- Shobi na Makiri wanawakilisha watu wanaotambua huduma ya kiongozi wa kiroho hata kama wao si wanufaikaji wa karibu wa huyo kiongozi. Hii inakufundisha nini juu ya mpango wa kutambua huduma ya wachungaji? Je unaona mahali popote Daudi akiwaagiza hao watu kiwango cha kutoa au vitu wanavyotakiwa kutoa? Zawadi kama hizo zinamsaidiaje kiongozi anayepitia changamoto mbalimbali za maisha?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 18:1-33
- Kuchagua viongozi wa ngazi za chini kunasaidiaje uongozi wa juu? Viongozi wa ngazi za juu wasiposhirikiana au kuwathamini viongozi wa ngazi za chini kuwepo kwa viongozi hao wa chini kuna tija yoyote kwa taasisi husika? Je kiongozi mmoja mwenye karama ya uongozi hatoshi kuongoza taasisi hata ahitaji viongozi wadogo? Kiongozi hujisikiaje pale anaowaongoza wanapotambua thamani yake na kuwa tayari kumlinda?
- Inatokana na nini mtu kuona bora afe yeye kuliko kiongozi wake? Je viongozi wetu wanastahili kuwa kwenye mazingira salama zaidi kuliko sisi tunaoongozwa? Je ni anasa kwa kiongozi kutembelea gari linalohakikisha usalama wake zaidi? Je Daudi alionesha udhaifu wa kudekeza watoto alipoomba makamanda wamtendee kwa upole mwanaye Absalomu aliyekuwa amelisumbua sana taifa au alionesha upendo wa kweli ambao wazazi tunatakiwa tuuoneshe kwa watoto wetu wakorofi?
- Unadhani makamanda walilipokea vizuri agizo hilo la mfalme? Kwa nini Yoabu hakuzingatia maelekezo ya mfalme ya kutomgusa Absalomu licha ya kukumbushwa na askari aliye chini yake? Je yapo mambo ambayo si lazima uyatekeleze kwa maslahi ya taasisi hata kama yanatoka kwa kiongozi wako uliyeapa kumtii? Kwa nini Ahimasi aling'ang'ania kupeleka ujumbe ambao hata hivyo hakuweza kuufikisha?
- Je alikuwa anatafuta umaarufu? Je unafanya hicho unachofanya kwa sababu ya kutafuta umaarufu au unahisi ni wajibu ambao Mungu amekupa ili kusaidia watu? Watu wanaopenda kushindana kazini kama Ahimasi wana mchango wowote wa maana kwa taasisi mnayoitumikia? Unadhani Yoabu alikuwa amelenga kumsababishia Mkushi kifo kwa kumpelekea Daudi taarifa za kifo cha mwanaye kipenzi?
- Je kupeleka habari mbaya kunahitaji umakini? Maelezo ya utangulizi ya Mkushi yalimsaidiaje Daudi kupokea taarifa za msiba wa Absalomu? Kitendo cha Daudi kumlilia Absalomu aliyeleta madhara makubwa kwa taifa kilikuwa sahihi? Kuna uhalali gani wa kithiolojia wa kumlilia marehemu katika namna kama ya kuongea naye kama alivyofanya Daudi? Je huo ni mchakato wa kawaida wa kisaikolojia wa kumsaidia mwombolezaji kupona? Unaweza kumtuhumu Daudi kuwa alikuwa anaongea na mfu kinyume cha hali halisi ya wafu?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 19:1-43
- Je kulikuwa na haja yoyote kwa jeshi la Daudi kwenda vitani ikiwa hakutaka Absalomu auawe? Kwa nini kama lengo ni kumuacha Absalomu salama hakumuita kwa mazungumzo? Je siku ya ushindi wa jeshi la nchi ulipaswa kugeuzwa kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa? Je ni sahihi kuwa mfalme Daudi kwa kitendo cha kugeuza ushindi wa kitaifa kuwa maomboleza alikuwa anadhihirisha kuwa anawapenda wamchukiao na anawachukia wampendao?
- Je Yoabu alistahili kumshambulia mfalme kwa maneno makali au alikosa staha kwa bosi wake? Kama kiongozi Daudi hakutakiwa kusahau jukumu lake la kufariji raia wake katika hali ya huzuni iliyolishika taifa. Je inawezekana kufariji wengine wakati ambao wewe mwenyewe unahitaji kufarijiwa? Je inawezekana kwenda kuwaona walio kifungoni na kuwavika walio uchi wakati ambapo mimi mwenyewe niko uchi na nimefungwa na Shetani? (Mathayo 25:36).
- Kanuni muhimu ya kusamehewa bila kujali ukubwa wa kosa ni kutambua kosa lako na kulijutia. Unadhani Shimei alistahili kusamehewa? Je kuna dhambi yoyote ambayo wewe, Mungu, au kanisa lako haliwezi kusamehe? Kwa nini? (Isaya 1:18). Mfalme Daudi alifanikiwa kurejesha mahusiano na waliokuwa wafuasi wa Absalomu na wale waliomkosea yeye binafsi. Nini kilisaidia kufanikisha jambo hili? Ni moyo wake wa kusamehe au uwezo wake wa kupanga hoja? Ni ipi namna bora zaidi ya kushughulika na adui zako? Je kusamehe ni dalili ya ukomavu?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 20:1-26
- Watu wanaohamasisha uasi mara zote huwa ni watu wasiofaa? Au unadhani Sheba aliitwa mtu asiyefaa kwa sababu gani? Na kama ni mtu asiyefaa kwa nini watu walifuata ushauri wake? Daudi alihitaji uwepo wa Amasa katika wakati aliokuwa anamhitaji lakini akakaa zaidi ya muda aliopewa. Kwa nini katika nyakati za kukataliwa huhitaji uwepo wa watu wake wa karibu? Licha ya nyakati kadhaa Yoabu kutotimiza.
- Maagizo ya Daudi kama alivyotaka anaonekana kumsaidia sana katika nyakati zake za kukata tamaa. Je Mungu aweza kuwa msaada wa kuaminika wakati wengine wanapokuwa wamekuach? Kwenye kisa cha leo tumeona mtu asiyefaa na mwanamke mmoja mwenye akili. Unadhani wanawake ni wazuri katika kushauri? Je ushauri wa mwanamke mwenye akili ulikuwa na msaada kwa taifa? Je wanawake wakitumika vizuri wanaweza kufanikisha mapambano dhidi ya Shetani aliye adui wa wanadamu wote?
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 21:1-22
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 22:1-51
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 23:1-39
MASWALI YA KUJADILI: 2 SAMWELI 24:1-25