Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WARUMI 7

UCHAMBUZI WA KITABU CHA WARUMI

SURA YA SABA

Kitabu cha Warumi sura ya saba kinaendelea kuzungumzia mahusiano ya mtu anayeukulia wokovu na matakwa ya sheria au torati. Ni ukweli usiopingika kuwa kuna mgogoro unaohitaji utatuzi kati ya mwanadamu mwenye mwili wa dhambi na madai ya sheria na torati. Mtu wa dhambi hawezi kustahimili mbele ya sheria. (Warumi 7:9-10) “Nami nalikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa. Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti.” Sheria haiwezi kutulia mpaka madai yake yatimizwe kikamilifu. (Warumi 2:13) “Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.”

Biblia imetoa hitimisho kuwa hakuna mwenye mwili wa dhambi awezaye kukidhi madai ya sheria kikamilifu. (Warumi 8:7) “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” Suluhisho pekee katika mazingira haya ni ama madai ya torati yaondolewe au mwanadamu mwenye mwili wadhambi aodolewe. Biblia inapendekeza kutoweshwa kwa mwili wa dhambi kama hitimisho la mgogoro huu. Kabla Yesu hajaja kutuoa tulikuwa tumeolewa na torati na dhambi. Yesu aliviondoa vyote viwili yaani dhambi na torati. (Warumi 8:3) “Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili.”

Yesu aliihukumu dhambi maana yake aliusulubisha mwili wa dhambi uliokuwa ukitumikishwa na torati ili kupisha mwili unaotawaliwa na sheria ya uzima iliyo kinyume na sheria ya dhambi na mauti. (Warumi 8:2) “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Utu wa kale au mwili wa dhambi ulisulubishwa ili kupisha mwili mpya unaotawaliwa na sheria ya uzima. (Warumi 7:2-3) “Kwa maana mwanamke (mwili wa dhambi) aliye na mume (sheria ya dhambi) amefungwa na sheria kwa yule mume wakati (mwili wa dhambi) anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, (mwili wa dhambi na sheria ya dhambi) amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, (sheria ya dhambi)  kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe (sheria ya dhambi na mwili wa dhambi) akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine (Kristo).”

Yesu alimuua mume wa kwanza wa mwanadamu mwenye mwili wa dhambi ambaye Paulo anamuita sheria ya dhambi au ile dhambi moja iliyo chimbuko la yeye kushindwa kutenda mema anayotamani kuyatenda. (Warumi 7: 15-20) “Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.”

Paulo anaweka wazi kuwa hastahili kulaumiwa kwa kushindwa kuwa mtii wa sheria maana si yeye atendaye dhambi bali ni ile dhambi iliyo ndani yake ambaye ndiye mume Kristo aliyekuja kumsulubisha ili apate fursa ya kumuoa huyo mjane aliyefiliwa na mume wa kwanza. Yesu hawezi kutawala katika mwili unaotawaliwa na mume mwingine. (Warumi 7:22-23) “Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.”

Hapa kuna sheria ya Mungu na sheria ya akili ambayo imefanywa mateka na ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo. Mgogoro unaanzishwa na akili au nia iliyotekwa na sheria ya dhambi ifanyayo kazi katika viungo vya mwili na kupelekea mwili kupingana na torati na maagizo yote ya Mungu. (Yakobo 4:1) “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?”

Yesu ili kuleta suluhisho aliuondoa mwili unaoongozwa na akili au nia iliyotekwa na sheria ya dhambi na kuondosha pia madai ya torati ambayo aliyatimiza alipojitoa kufa msalabani. (Warumi 8:7) “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Waefeso 2:15-16) “Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba.” (Wakolosai 2:14) “Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani.”

Watu wawili waliofanywa mtu mpya mmoja ndani ya Kristo ni yule aliyemwamini Yesu na kuumbiwa moyo mpya anayeendelea kuukulia wokovu akiwa na asili mbili; asili ya uzima inayotokana na nia yake wakati huu kuthibitiwa na uwezo wa Roho Mtakatifu pale anaporuhusiwa kuifanya kazi yake na asili ya dhambi pale nia inapothibitiwa na sheria ya dhambi kama matokeo ya mwanadamu kutotoa ushirikiano kwa Roho Mtakatifu. (Wagalatia 5:16, 24) “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili, Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.”

Baada ya Yesu kuifia torati pale msalabani mahusiano yetu na torati yamebadilika. (Warumi 7:6) “Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.” Mabadiliko yaliyofanyika si ya maagizo ya torati. Maagizo ya torati yanabaki vile vile lakini kilichobadilika ni njia inayotumika katika kutii maagizo hayo. Hali iliyotupinga ambayo sasa tumeshaifia ni mwili ule wa dhambi uliokuwa unaongozwa na nia ifanyayo kazi kupitia sheria ya dhambi. Kwa sababu haikuwa sahihi kwa torati ambayo kwa asili ni ya rohoni ishikwe na mwili unaotawaliwa na sheria ya dhambi. (Warumi 7:14) “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.”

Katika hali ya zamani ya andiko wana wa Israeli waliahidi kuwa hayo yote Mungu aliyoamuru katika torati watayatenda kwa kutegemea mwili unaotawaliwa na sheria ya dhambi jambo ambalo halikufanikiwa kwa kuwa walishindwa kushika hayo maagano kwa kuwa neno lile waliloahidi kutenda liligeuka kuwa adui wao likawaua. (Waebrania 8:9-10) “Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana. Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.”

Katika hali mpya sheria zilizokuwa zimeandikwa kwenye mbao za mawe na kwenye torati zitaandikwa mioyoni na kwenye nia zao. Hawatahitaji kukumbushwa maana Roho atakuwa ndani yao akiwakumbusha. Hawatazitii ili kufurahisha watu au kujaribu kununua wokovu maana Yesu alishawanunulia wokovu tayari. Hawatazitii ili kujiinua mbele ya wengine na kujihesabia haki kwa kuwa wanayo haki ya Kristo tayari na yale mema wanayotenda hayatokani na wao bali ni matokeo ya kazi inayofanywa na Roho Mtakatifu. (Wafilipi 2:13) “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”

Ni vigumu kumtii asiyekupenda au usiyempenda. Torati au sheria ilikuwa haijafunua vya kutosha jinsi Mungu alivyogharamika katika kumpenda mwanadamu hasa katika zoezi la kumtafuta alipotenda dhambi. Msalaba ulikuja kuainisha kwa kina upendo huo wa Mungu kwa mwanadamu. Kupitia Roho Mtakatifu tunajulishwa jinsi Yesu alivyotatua vikwazo vyote vilivyokuwa vinatuzuia kumtii Mungu na kuhesabiwa haki. Roho Mtakatifu anatufunulia jinsi sasa inavyowezekana kumtii Mungu kwa kuwa msukumo hautakuwa katika kujitafutia haki au kutafuta sifa bali kuonyesha shukrani kwa wema wa Mungu.

Katika hali ya mwili torati huzalisha dhambi kwa sababu mwili wa dhambi daima hupenda kufanya kile ulichokatazwa kufanya. Lakini katika hali ya roho mwili hufurahia kumpendeza Bwana wake aliyemtoa kwenye vifungo vya utumwa wa dhambi. (Warumi 7:5) “Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao.” Kuijua sana torati na matakwa yake hakumfanyi mwenye mwili wa dhambi kupata unafuu katika kuishika hiyo torati kwa sababu ya kupungukiwa uwezo wa kuitii.

Kuelewa matakwa ya sheria na torati ni kumjua Mungu mwenyewe mtoa sheria. Kwa sababu kumjua Mungu kunakurahisishia kufahamu kile alichokuagiza. Waisraeli walijua torati kuliko kumjua Mungu. Wakaweka msisitizo katika kuhusiana na torati ambayo haina urafiki na mdhambi wakaacha kuweka msisitizo katika kuhusiana na Mungu mwenye kuwaonea huruma. Wakati huu wa Agano Jipya msisitizo ni wa kumjua Mungu na Yesu Kristo ili kutujengea mahusiano yasiyo na mgogoro na sheria. Ni kosa kudhani kuwa torati au sheria kupitia mabadiliko haya vimebatilishwa. (Warumi 7:7) “Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.”

Sheria au torati inabaki na umuhimu wake ule ule wa kutambulisha dhambi na hakuna hata kipengere kimoja kilichofutwa kama yalivyo madai ya watu wengine. (Mathayo 5:17-19) “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” (Warumi 7:12) “Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema.”

Kuna watu wanaoishangilia injili ya Yesu kuwa imewaletea ukombozi kutoka utumwa wa kutii sheria na torati. Kwa sehemu fulani dhana hii ni sahihi hasa kuhusiana na maagizo ya torati hasa yale yaliyokuwa kivuli cha mambo yajayo ambayo yalikomea pale msalabani. (Wakolosai 2:16-17) “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” Kwenye torati kulikuwa na vinywaji vilivyoagizwa kutumika kwenye ibada za kutoa kafara. (Hesabu 28:31) “Zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, mtasongeza wanyama hao (watakuwa wakamilifu kwenu), pamoja na sadaka zake za vinywaji.”

Sadaka zingine za vyakula ni kama huo unga na mikate vilivyotumika kwenye ibada za makafara pamoja na wanyama na ndege. (Hesabu 15:20) “Katika unga wenu wa kwanza wa chenga-chenga mtasongeza mkate uwe sadaka ya kuinuliwa; vile vile kama mfanyavyo sadaka ya kuinuliwa ya sakafu ya kupuria nafaka, ndivyo mtakavyoiinua.” Mambo haya hayana nafasi tena katika Agano Jipya kwa kuwa Kristo aliye pasaka wetu amekwisha kuchinjwa. (1 Wakorintho 5:7) “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.”

Kawaida hizi za kutoa sadaka za vinywaji na unga ziliendelezwa na Wayahudi hata baada ya Yesu kufa pale msalabani ndiyo maana Paulo aliagiza watu wasihukumiwe kwa kutoendelea kufuata desturi hizo. Ni tofauti kabisa na tafsiri inayotolewa na wengine kwamba agizo hili la Paulo linatoa kibali cha watu kula Wanyama najisi na vinywaji kama pombe vilivyokatazwa na Biblia. Pia sheria nyingine iliyokuwepo kwenye torati na iliyokuwa kivuli cha mambo yajayo ni sabato za tarehe zilizo tofauti na sabato inayotokea kila ifikapo siku ya saba ya juma yaani Jumamosi.

Katika kitabu cha Walawi Mungu anaainisha sikukuu zitakazoandamana na ibada kwa mwaka. Sabato ya siku ya saba ya kila juma imetofautishwa na sabato zingine kwa kuwa hii si kivuli cha mambo yajayo maana imekusudiwa iwe ya milele. (Walawi 23:2-3) “Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za Bwana, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu. Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa Bwana katika makao yenu yote.”

Baada ya kuainisha sabato ya kila mwisho wa juma Paulo anaorodhesha sabato zingine za tarehe zilizokuwa zinalenga pumziko ambalo Yesu atalitoa kwa ulimwengu atakapoyatoa maisha yake ili kuwakomboa wanadamu. (Walawi 23:4-8) “Sikukuu za Bwana ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi. Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.”

Kulikuwa na sabato iliyokuwa inasherehekewa kila ifikapo siku ya kwanza ya mwezi wa saba wa Kiyahudi ambayo haikuangalia kama imeangukia siku gani tofauti na ile sabato ya majuma. (Walawi 23:23-24) “Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu.” Sura ya 23 ya kitabu cha Walawi inazitaja sabato hizo kwa mapana na hizo ndizo sabato ambazo Paulo aliwaambia waumini wenye asili ya Kiyahudi wa Kolasi kutoendelea kuziadhimisha.

Tafsiri kuwa agizo hilo lilizuia sabato iliyoagizwa kwenye amri ya nne inayoadhimishwa kila ifikapo siku ya saba ya juma imepotoshwa na haipaswi kuzingatiwa. Sabato hiyo ya siku ya saba ya juma iliagizwa ili kukumbuka uumbaji na ukombozi sababu ambazo hazijabadilika. (Kutoka 20:8-11) “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (Ezekieli 20:12) “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.”

Ni dhahiri kuwa sheria haina uwezo wa kumuokoa mwenye dhambi. Msaada peke utolewao na sheria kwa mdhambi ni kumtambulisha alivyo mwenye hatia na mwenye dhambi mbele ya sheria na kumtahadharisha kama hatachukua hatua za kurekebisha hali yake hiyo atakabiliwa na mauti. Hata kama huu hauonekani kuwa msaada wa maana kwa kuwa hautoi wokovu unamsaidia mwanadamu kuondokana na mazoea yake ya kujihesabia haki kwamba yeye ni mwenye haki.

Mwanadamu mwenye asili ya dhambi na anayetawaliwa na sheria ya dhambi wakati wote sheria inamsonda kama ni mwenye dhambi. (Warumi 7:7b) “. . . Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani.” Moyo wa mwanadamu ni mdanganyifu kwa kuwa humzuia mdhambi asijitambue kuwa ni mwenye dhambi. (Yeremia 17:9) “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” Adamu alipotenda dhambi moyo wake wa dhambi ulimzuia asijitambue kuwa yeye mwenyewe ndiyo chanzo cha dhambi aliyotenda. (Mwanzo 3:12) “Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.”

Hata hivyo sheria haiishii katika kututambulisha tulivyo wenye dhambi bali inatutahadharisha tusijaribu kuitii kwa kutumia ujuzi wetu maana hakuna mdhambi awezaye kuitii sheria ya Mungu bila kusaidiwa na Mungu mwenyewe. (Warumi 3:19) “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu.” Lakini msaada wa mwisho ambao sheria hutoa kwa mdhambi ni kumpendekezea wenda kwa Kristo ili apatanishwe na sheria na kupewa uwezo wa kuitii. (Wagalatia 3:24) “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.”