Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

WALAWI

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 1:1-17

  1. Kwa nini mtu alipotaka kumtolea Mungu sadaka alitakiwa kutoa katika wanyama wake wa mifugo? Kwa nini mnyama aliyetakiwa kutolewa kwa sadaka ya kuteketezwa alitakiwa awe mume mkamilifu? Ukamilifu wa Wanyama hao ulikuwa unapimwaje? Kwa nini mkono wa mtoa sadaka ulitakiwa kuwekwa kichwani mwa sadaka ya 5nini?
  2. Kwa nini ilimwagwa kwenye madhabahu na makuhani? Kwa nini watoa sadaka wengine waliruhusiwa kutoa sadaka ya njiwa badala ya Wanyama? (Walawi 5:7,11). Hii inakufundisha nini kuhusu nia ya neema ya Mungu kuwafikia watu wa daraja zote? Katika mazingira haya kuna ambaye atanyimwa wokovu?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 2:1-16

  1. Kwa nini sadaka yya unga iliyobaki walipewa Haruni na wanawe kwa matumizi ya kawaida? Je, kitendo hicho kiliwafanya washirika wa dhambi iliyosababisha sadaka ikatolewa? Je, kupitia utaratibu huo malipo ya makuhani yalitegemea sadaka iliyotolewa? Hali hiyo bado ingalipo hata leo? (1 Wakorintho 9:1). Chumvi iliyokuwa inawekwa kwenye sadaka zilizokuwa zinatolewa iliwakilisha nini? (Mathayo 5:13; 2 Wafalme 2:21; Ayubu 6:6).

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 3:1-17

  1. Kwa nini sadaka za utumbo, ini, na figo pamoja na mafuta yanayozunguka viungo hivyo zilipoteketezwa kwa moto vilileta harufu ya kumpendeza Mungu? Kwa nini leo tunatakiwa tuitoe miili yetu kuwa dhabihu iliyo hai? (Warumi 6:19; Warumi 12:1).
  2. Katika ibada zetu leo, je, kuna nafasi ya kusherehekea neema ya Mungu kama familia moja mbele za Bwana? Je, Kanisa linatumiaje meza ya Bwana kama mahali pa ushirika wa amani, si hukumu tu?

 

 

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 4:1-35

  1. Mtu anafanyaje dhambi isiyo ya kukusudia? Kuhani aliyetiwa mafuta na atendaye dhambi analetaje hatia juu ya watu? Kwa nini ngombe wa sadaka ya dhambi achinjwe na aliyetenda dhambi na asichinjwe na kuhani?
  2. Damu iliyokuwa inanyunyizwa na kuhani mbele ya Bwana mara saba ilikuwa inaashiria nini? Kuhani katika Agano la Kale alikuwa anampatanisha mdhambi na Mungu wake kwa kupokea sadaka kutoka kwa anayetafuta upatanisho. Je leo wanaohitaji kuponywa na changamoto za kimaisha hawahitaji kuleta sadaka kwa watumishi wa kiroho?
  3. Mtawala aliyetenda dhambi aliweza kutambuliwa na kufanyiwa maombezi. Leo hii mtawala anatambulikaje kuwa ametenda dhambi n ani nani humfanyia maombezi?je dhambi ya mtawala yaweza kuwaathiri raia anaowaongoza?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 5:1-19

  1. Mtu huhesabiwa kuwa ana hatia pale alitambuapo kosa lake na si kabla ya hapo. Je leo wale wazivunjao amri za Mungu bila kujua wanakosea watahesabiwa haki au watahesabiwa hatia?
  2. Kwa nini mtu asiyemudu sadaka ya kondoo alikuwa anaruhusiwa kuleta makinda mawili wa njiwa? Je, ni sahihi kuwapangia watu viwango vya sadaka kulingana na uwezo wao? Je ni sahihi kuweka kiwango sawa cha sadaka na michango kwa watu wote?
  3. Unga wa sadaka uliobaki baada ya upatanisho ulikuwa wa kuhani kwa ajili ya matumizi yake binafsi. Je sadaka inayoletwa kwa ajili ya maombezi inapaswa kuliwa na watumishi wa kiroho?
  4. Zamani watu walitoa pesa (shekeli) ili kusamehewa dhambi. Je, leo makasisi wana uhalali wa kupokea malipo kwa dhambi wanazoungamiwana waumini wao?

 

 

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 6:1-30

  1. Ni nini madhara ya kudanganya katika biashara na katika mahusiano kwa ujumla? Je, jamii zilizofanikiwa kuondokana na udanganyifu zilifikiaje hatua hiyo? Mtu mwenye utu anajisikiaje anapojaribiwa kudhulumu wengine? Je watu waaminifu wanachukiliwaje katika jamii yenu? Wanaonekana mashujaa au watu waliochelewa?
  2. Ni kwa vipi kila kitu kitakachogusa nyama ya sadaka kitakuwa kitakatifu lakini kila chombo cha udongo ambacho hiyo nyama ilipikwa ndani yake kitavunjwa? Tofauti kati ya sadaka ya dhambi na ya hatia ni ipi?
  3. Je, tunaweza kumkaribia Mungu kwa sala bila kwanza kuomba msamaha au kurekebisha majeraha kwa watu wengine? Katika jamii yetu ya leo, ni wapi tunahitaji kusikia mwito wa marejesho?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 7:1-38

  1. Kwa nini kushiriki sadaka ya amani ni tendo la ibada na si tukio la kawaida la kijamii? Je, tunawezaje kushiriki Meza ya Bwana leo kwa moyo wa heshima kama ilivyokuwa katika sadaka za Walawi? (Mathayo 26.26 -30 1 Wakorintho 11.17 - 34).
  2. Kwa nini ibada ilihitaji utakaso na usafi? Je Mungu anataka tumsogelee tukiwa hatuna dhambi au anataka tufanye toba kabla ya kumkaribia?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 8:1-36

  1. Kwa nini wana wa Haruni na wa kabila la Lawi pekee walioruhusiwa kuhudumu katika nafasi ya ukuhani? Kuwekwa wakfu kabla ya kuanza kazi ya Mungu kuna umuhimu gani? Kila mnyama aliyetolewa kafara na kila kuhani aliyehudumu kwenye hema takatifu alimwakilisha Kristo aliye kuhani na Mwanakondoo wa Mungu azichukuye dhambi za ulimwengu. Kwa nini ashike nafasi zote muhimu za huduma za hekaluni?
  2. Kwa nini watu wengine wasio makuhani walitakiwa kukutana mlangoni pa hema na siyo ndani ya hema? Kama utaratibu wa Agano la Kale ungeendelea kufuatwa watu waliotakiwa kuingia nyumba za ibada wangekuwa makuhani wa kabila la Lawi pekee?
  3. Kwa nini utaratibu wa utoaji kafara wa Agano la Kale haukuendelezwa baada ya Yesu kuja? Je huduma za utoaji kafara kwenye hema takatifu zilikomeshwa kwa sababu hazikuwa na ubora? Kama Mungu alijua zisingekuwa na ubora kwa nini alizianzisha?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 9:1-24

  1. Kipi kina usumbufu zaidi katika kutayarisha kati ya sadaka ya wanyama na sadaka ya fedha? Maagizo ya kuleta sadaka ya wanyama ingetolewa leo ingekuwa na upinzani zaidi? Nani atalipa gharama ya wanyama walioliwa katika kutoa kafara iliyoagizwa na Mungu? Kitendo hiki cha kuua wanyama wasio na hatia kwa ajili ya kutoa kafara hakiendi kinyume cha haki za wanyama?
  2. Shughuli kubwa ya makuhani wa Agano la Kale ilikuwa kufanya upatanisho kati ya wenye dhambi na Mungu waliyemkosea. Je leo huduma ya kuombea wenye dhambi ili wapatanishwe na Mungu wao inafanywa na nani? Je Padre, Shehe, au mchungaji anaweza kufanya kazi hiyo?

. Je ukuhani wa Agano Jipya unahusu kusamehe dhambi za watu? Huduma hiyo ya ukuhani wa Agano la Kale leo inafanywa na nani? Kwa nini huduma hiyo haiandamani na kutoa kafara za wanyama?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 10:1-20

  1. Kwa nini moto waliouwasha Nadabu na Abihu umeitwa moto wa kigeni? Kwa nini moto waliouwasha wenyewe uliwaangamiza? Kwa nini Mungu aliruhusu jambo hili liwatokee watumishi wake aliowaweka wakfu kwa kazi takatifu? Unajifunza nini juu ya unyeti wa kazi za kiroho kama uchungaji, uzee wa kanisa, na ushemasi zinazohusisha kuwekwa wakfu kwa kuwekewa mikono?
  2. Kunyamaza kwa Haruni baada ya jibu la Musa kunaashiria nini? Je kitendo cha Mungu kuwaua watumishi wake watukutu kilisaidia kuwafundisha makuhani wengine na waumini juu ya utakatifu wa Mungu na upendo wake? Je Mungu alifurahia tukio hilo? Makuhani walikatazwa kuyararua mavazi yao. Kwa nini Kuhani Mkuu aliyekuwa anashughulikia kesi ya Yesu alirarua mavazi yake? Hakujua kufanya hivyo ni kosa? (Mathayo 26:65).
  3. Kwa nini makuhani hawakuruhusiwa kuacha wazi nywele za vichwa vyao? Kukatazwa kwa makuhani kunywa divai au kileo chochote kunaonyesha jinsi Mungu asivyokubaliana na unywaji wa pombe? Je viongozi wa dini wanaotetea unywaji wa pombe wanalielewaje fungu hili? Je waumini inawapasa kuomboleza kwa majanga yanayomkuta kiongozi wao wa kiroho hata kama yalimpata kwa uzembe wake?
  4. Je kuwafundisha waumini juu ya Amri na Sheria za Mungu ni mojawapo ya wajibu wa viongozi wa kiroho? Je, ni halali kwa viongozi wa kiroho kutengewa chakula tofauti na waumini wao? Je, ibada ya kisasa inaweza kuwa na “moto wa kigeni”? Iko wapi hatari yake leo? 
  5. Je, kuna haki za viongozi wa kiroho ambazo waumini hawapaswi kuzidai? Wachungaji wanapojitenga na waumini wao wakati wa kula chakula kwenye makambi ni halali au ni ubaguzi? Ni kwa njia gani tunaweza kujifunza hofu ya Mungu bila kuingiwa na hofu ya kuhukumiwa?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 11:1-47

  1. Je, tofauti ya chakula safi na najisi inafundisha nini kuhusu maisha yetu ya kila siku? Tunawezaje kuhifadhi usafi wa moyo na maisha yetu katika mazingira yaliyochafuliwa kiroho? Kwa nini Mungu aliwachagulia Waisraeli wanyama wafaao kuliwa? (Mwanzo 1:26-30)
  2. Kungekuwa na ubaya gani kama wangejichagulia wenyewe? (Warumi 1:23-28). Agizo la vyakula vinavyofaa kuliwa na visivyofaa liliwahusu Waisraeli pekee au linawahusu wanadamu wa vizazi vyote? (1 Wakorintho 10:31).
  3. Ikiwa wanyama wamewekewa utaratibu ili walao nyasi wasile nyama na walao nyama wasile nyasi unadhani mwanadamu aliyeumbwa kwa sura ya Mungu ameachiwa uhurru wa kula atakacho kama wengine wanavyodai? (Luka 21:34). Je, ni kweli kuwa Yesu aliondoa sheria ya wanyama najisi alipovitakasa vyakula vyote? (Marko 7:19)
  4. Je, unadhani ulaji usio na mipaka ni chanzo kingine cha maradhi yawapatayo wanadamu siku hizi? Kwa nini nguruwe anaonekana kuwa kikwazo cha watu wengi katika kuacha kula wanyama najisi? Je walao wanyama najisi kama nguruwe na panya watafanyiwa nini na Mungu siku ya mwisho? (Isaya 66:17).
  5. Paulo anapowaagiza Wakolosai kuwa mtu asiwahukumu kwa vyakula (Wakolosai 2:16) alikuwa anamaanisha kuwa maagizo ya vyakula najisi yamepitwa na wakati na si ya lazima tena? Kama wanyama wasio safi hawafai kwa kuliwa kwa nini waliingizwa Safinani? (Mwanzo 7:2).

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 12:1-8

  1. Unajisi wa siku saba wa mwanamke aliyejifungua mtoto wa kiume unatokana na nini? Kwa nini siku za unajisi kwa ajili ya kujifungua mtoto wa kike zilikuwa nyingi zaidi? Kwa nini baada ya siku saba unajisi huo huondoka? Kwa nini mtoto wa kiume aliweza kutahiriwa baada ya kufikisha umri wa siku nane? Kwa nini tohara ilihusu watoto wa kiume tu? 
  2. Je Yesu pia alitahiriwa? Jekutahiriwa kulikuwa mbadala wa ubatizo? (Wagalatia 6:15). Kama kutahiriwa kulikuwa kunawakilisha ubatizo na kuzaliwa upya kwa nini Yesu alibatizwa baada ya kutahiriwa? (Mathayo 3;13-15). Ilikuwa muhimu kutoa sadaka ya shukrani kwa ajili ya kupata mtoto wakati wa Agano la Kale. Je unaona muhimu wa sadaka hiyo wakati huu?
  3. Ni hatari gani zinamkabili mtoto anayezaliwa na mama anayejifungua zinazotosha kumshukuru Mungu mzazi anapojifungua salama? Je siku 60 au 66 baada ya mama kujifungua ni kipindi kinachotosha kwa nume kukutana na mkewe kimwili? Je, mzazi atatakiwa apangiwe kiwango cha sadaka ya shukrani au apange kulingana na uwezo wake?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 13:1-59

  1. Kazi ya Kuhani Mkuu ilikuwa kutambua kama mtu ana ukoma au la. Huduma hii ilikuwa na umuhimu gani kama haikuweza kumponya mgonjwa? Ukoma katika nyakati za Agano la Kale ulifananishwa na nini na kwa nini?
  2. Kwa nini mwenye ukoma alitambulika kuwa najisi? Kuchoma vazi la mwenye ukoma kulilenga nini? Unazungumziaje hali ya mwenye dhambi inayoambuliwa kwa mwonekano wake? Leo mwenye dhambi anatambulika kwa mwonnekano wake?
  3. Kama sote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu kuna haja ya kuwaona wengine kuwa wadhambi zaidi yetu? Je Mungu anatuona tuna nafuu kuliko wengine kama sisi tunavyoonana?
  4. Je, kuna tofauti gani kati ya kutengwa kwa sababu ya ugonjwa na kujitenga kwa ajili ya uponyaji wa kiroho? Leo hii, ni nani anayeweza kuwa "kuhani" anayesaidia watu kugundua hali zao na kusimama nao hadi wapate utakaso?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 14:1-57

  1. Pigo la ukoma ulikuwa uthibitisho wa nje kwamba mwenye ukoma ni mdhambi anayestahili kutengwa na makazi matakatifu ya Mungu pamoja na watu wa Mungu. Hata hivyo kulikuwa na nyakti za kupona ukoma na kurejea kwenye makazi kama kawaida. Kwa nini Mungu alianzisha utaratibu huu? Je, hiyo inatufundisha kuwa dhambi hata kama imetuchakaza sana ina mwisho?
  2. Ingawa zoezi la kutengwa na jamii baada ya kugundulika una ukoma lilikuwa chungu na la kufedhehesha sana, furaha ilikuwa kubwa siku ya kurejeshwa kundini baada ya kupona ukoma. Unadhani tutakaporejea mbinguni baada ya miaka 6,000 ya dhambi furaha yake itafanana na mkoma aliyepona anayeruhusiwa kujiunga na jamii? Una ujumbe gani wa matumaini kwa mdhambi aliyekata tamaa?
  3. Kwa nini Mungu mwenye uwezo wote asiizuie dhambi isitokee kuliko kukabili hasara na gharama kubwa Kufanikisha uhai wa viumbe wake na ya Mwanae kama alivyofanya? Kuhani aliyekuwa anamkagua mwenye ukomo alikuwa anaharisha maisha yake kwa kumshikashika?
  4. Kuna wakati mtumishi wa Mungu hufanya kazi katika mazingira hatarishi ambayo hawezi kuepukana nayo? Je wakati wa Korona ungetakiwa umbatize mgonjwa aliyeomba kubatizwa ingekuwa sahihi kufanya hivyo? Je, tunawezaje kusaidia wale waliotengwa kijamii wapate urejesho wa kweli? Kuna watu wangapi leo ambao wako “nje ya kambi” wakisubiri kuhani awatembelee?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 15:1-33

  1. Kisonono ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya kujamiiana na wapenzi wengi. Kwa kuweka sheria ya kuwatenga wenye kisonono Mungu alikuwa anaonesha kuwajali watu wake au kuwabagua? Kanuni hii inakubalika kiafya?Je sheria hii ingefuatwa leo ingepunguza au kutokomeza kwa kiasi kikubwa magonjwa ya zinaa?
  2. Je kutokwa na mbegu za kiume kwaweza kumfanya mtu najisi? Kwa nini mwanamke aliye kwenye siku zake alihesabiwa najisi? Utaratibu huu ungefuatwa leo hii ungeathiri kwa kiasi gani huduma zinazowahusu wanawake kanisani? Kwa nini kutoka damu ya unajisi, shahawa, na usaha wa kisonono kulihitaji kutoa sadaka ya upatanisho?
  3. Je usafi wa mwili una mchango gani katika kutuepusha na maradhi na kukamilisha ibada? Je usafi katika kuingiliana kimwili waweza kuwaepusha wanaojamiiana na maradhi?
  4. Je, ni wapi katika maisha ya jamii yetu tunaweza kuona kifo kikitembea bila kificho? Je, tunajua jinsi ya kuwasaidia wale walioguswa na kifo—kimwili au kiroho—warudi kwa Mungu aliye Uhai? Je mwili ulio mchafu unakidhi vigezo vya kuwa hekalu la Roho Mtakatifu?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 16:1-34

  1. Mbuzi wa Azazeli aliyesindikizwa jangwani na kutelekezwa huko anawakilisha nani? Dhambi zilizokuwa zinapelekwa kwenye hema takatifu ziliondolewa mwisho wa mwaka na Kuhani Mkuu. Dhambi tunazoziungama kila siku zinaenda wapi? Kama zinaenda mbinguni ina maana mbingu kwa sasa imechafuka kwa sababu ya dhambi zetu? 
  2. Kama mtu hakuungama dhambi zake kabla Kuhani Mkuu hajaenda kufanya upatanisho nini kilimtokea mtu huyo? Kama Kuhani Mkuu angekuwa na dhambi ambayo haijaungama angekutwa na nini huko kwenye huduma yake? Unadhani kabla ya kuongea na Mungu wetu tunahitaji upatanisho na kuungama dhambi?
  3. Je dhambi zangu kabla hazijandolewa kwenye hekalu la mbinguni na kukabidhiwa Shetani ninaweza kudai kuwa nimesamehewa na Mungu? Je siku ya upatanisho Waisraeli walikuwa wakiendelea kuungama dhambi zao au walitakiwa kuwa kimya? Kwa nini Mungu alipanga sadaka ya dhambi hata kwa Kuhani Mkuu? Je, kuna maana gani kwa jamii yetu leo ya kuwa na siku ya toba ya pamoja?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 17:1-16

  1. Utaratibu wa kutoa sadaka kwa majini ambao Mungu aliwazuia Waisraeli kuendelea nao ulikuwaje? Je shetani naye hupokea sadaka? (1 Wakorintho 10:20). Kwa nini Mungu aliwazuia Waisraeli kuleta sadaka zao kwenye lango la hema takatifu kwa makuhani?
  2. Je sadaka aitoayo mtu kwa wahitaji bila kuifikisha kanisani ina uzito saw ana ile ifikishwayo kwanza kanisani? (Malaki 3:10). Je kuna uwezekano kwa wanadamu kufanya uasherati na majini? Katika viungo vyote vya ndege na Wanyama vitolewavyo kama sadaka ya upatanisho kwa nini damu inapewa uzito mkubwa?
  3. Kwa wale walao nyama wametakiwa kumwaga damu yote kabla ya kuitumia nyama hiyo. Unadhani zoezi hilo ni la muhimu hata leo kiroho na kiafya? Unadhani ulaji wa nyama ambao umedaiwa kuwa chanzo cha maradhi wakati huu ni kwa muhimu sana kwa afya zetu?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 18:1-30

Kulala na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke kumetambulika kama ni machukizo kwa Mungu. Unadhani kwa nini desturi hiyo imerudi kwa nguvu sana wakati huu kiasi cha kuwarubuni vijana na Watoto wetu kwa fedha? Hii inaashiria dunia inaelekea wapi? (Luka 17:28).

Je tabia za kujamiiana na wanyama au ndugu wa karibu au wanaoacha matumizi ya asili ya mwanamke zinazofanywa na mataifa yaliyoendelea kiuchumi ni Ushahidi kuwa mambo hayo hayana ubaya au ni kuwa mataifa hayo yanapitiwa na laana ya Mungu nay a kuwa hizo nchi zimekuwa najisi? (Warumi 1:21-28).

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 19:1-37

  1. Mungu anaposema mtazitunza Sabato zangu alikusudia hizo Sabato wazitunze hadi lini? Je kutunza Sabato kunamaanisha nini? Nyumba za ibada zilizosheheni sanamu zinakwenda kinyume cha maagizo ya Mungu? Kutia kwazo mbele ya kipofu na kumlaani kiziwi kumekatazwa. Je, jamii za kidini zinapaswa kuwa mfano bora katika kuhudumia watu hao wenye mahitaji maalum?
  2. Kupendelea na kuonea watu ni kinyume cha mapenzi ya Mungu. Je mtu wa Mungu anapasawa kukemea matendo hayo hata kama yanafanywa na watawala? Kuishi na kinyongo kwa ajili ya mtu aliyekukosea au kukudhulumu kumekatazwa. Unafanyaje ili kuondokana na kinyongo na mtu ambaye hakubali kuwa ulimkosea?
  3. Kunyoa denge na kuandika alama miilini ni kawaida inayopendwa sana na vijana iliyo kinyume na mapenzi ya Mungu. Kwa Wamakonde waliochora nyuso zao walionekana washamba lakini hawa wanaochora mwili mzima wanaonekana wajanja?
  4. Biblia imezuia kuwaendea wenye pepo na waaguao. Wale wanaoenda kwenye nyumba za ibada wakiwa wazima na kuanguka kwa mapepo baada ya kukutana na wanaojiita watumishi watakuwa waliwaendea wenye pepo?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 20:1-27

  1. Kwa nini mtu alalaye na mke wa mjomba wake adhabu yake ni kutozaa mtoto. Watoto wanaozaliwa kutokana na mtu kulala na dada au mama yake atakuwa katika mazingira gani kiakili, kiroho na kisaikolojia?

2, Mabinti wa Lutu walizaa na baba yao na kupatikana uzao ambao baadaye uliunda taifa la Wamoabu na Waamoni. Unadhani tabia hii Watoto walijifunzia wapi wakati baba yao aliwatetea kuwa hawamjui mume bado? (Mwanzo 19:8). Je maisha ya Sodoma yalichangia tabia hii ya mabinti zake?

  1. Je watoto wetu wanaweza kuwa wameanza tabia mbaya ya ngono bila wazazi kujua? Je nini kifanyike kuwalinda Watoto wetu? Kwa nini makosa ya kukosa maadili yalihukumiwa kwa kifo cha kupigwa mawe? Kwa nini rehema haikuwepo kwa makosa hayo?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 21:1-24

  1. Kwa nini sadaka inaitwa chakula cha Mungu? Kwa nini kuhani mkuu hakuruhusiwa kuingia kwenye maiti wala kuruhusiwa kumuoa mjane au aliyeachwa na mumewe bali bikira? Je, sheria hiyo bado ingali ina nguvu hata leo? Kwa nini makuhani hawakutakiwa kuwa na kilema? Hii ilikuwa inaakisi nini? (Waebrania 9:13-14).
  2. Desturi ya kunyoa upaa, kunyoa pembe za ndevu, na kuchanja chale kwa ajili ya kufiwa ilikatazwa katika torati. Je wakristo wanapolazimishwa kufanya hivyo kwenye misiba na viongozi wa mila wafanyeje hasa pale inapotafsiriwa kutoshiriki mila hizo ni kuonyesha kutomthamini aliyekufa au kujitenga na ukoo?

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 22:1-33

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 23:1-44

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 24:1-23

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 25:1-55

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 26:1-46

 

MASWALI YA KUJADILI: WALAWI 27:1-34