TAMBUA HADHI YAKO
Tunaishi katika ulimwengu unaoonekana kwa macho ya nyama. Kando ya huu ulimwengu unaoonekana kwa macho ya nyuma upo ulimwengu mwingine ambao unahitaji ufunguliwe macho ili uweze kuuona. Mtumishi wa nabii Eliya kwa kutumia macho ya nyama Aliona jeshi kubwa la adui likiwa limewazingira lakini hakuliona jeshi la Mungu wa mbinguni lililowakinga kwa kuwa lilikuwa katika ulimwengu wa roho usioonekana kwa macho ya nyama. (2 Wafalme 6:1-14) “Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili. Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli? Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala. Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani. Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote.”
(2 Wafalme 6:15-17) “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.”
Kisa hiki kinatufundisha kuwa yanayotendeka katika ulimwengu huu wa kawaida yanaweza yasiakisi yale yanayotendeka katika ulimwengu wa roho. Wakati hadhi na uthamani wetu katika ulimwengu wa kimwili vikihujumiwa na kutwezwa hadhi yetu katika ulimwengu wa roho ni vya viwango vya juu na vinavyotukuzwa sana. Hadhi yetu katika ulimwengu wa roho haipo chini kama inavyoonekana katika ulimwengu wa kimwili kwa sababu ya kile kilichofanywa na Yesu. (Waefeso 1:3-5) “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.”
Tumebarikiwa kwa baraka zote za rohoni kwa kuwa Mungu Baba alitangulia kutuchagua sisi kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu ili tuwe watakatifu wasio na hatia na ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo. Mambo hayo mawili yanatupa haki na hadhi inayofanana ni ile aliyonayo Kristo. Kwa kitendo cha Yesu Kristo kufa na kufufuka kimetuinua kutoka hadhi ya chini tuliyokuwa nayo na kutuingiza katika viwango vinavyozidi vile vya Malaika. Kristo anapoinuliwa ni ubinadamu umeinuliwa kwa kuwa Yeye aliyefanyika mwanadamu akitokea katika Uungu hawezi kupewa nafasi yeyote ya juu inayozidi ile aliyokuwa nayo.
Yesu alikuja duniani kuuinua ubinadamu na kuurejesha ulipokuwa kabla ya dhambi. Lakini kwa kuwa Mungu alimchagua mwanadamu na kumpa hadhi ya kuwa mwana wake kwa mfano wa Yesu Kristo amemwinua kupita pale alipokuwa kabla ya dhambi kwa kumshirikisha utukufu wote wa Kristo. (Wafilipi 2:5-10) “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi.”
Katika ulimwengu wa roho mwanadamu anapewa hadhi ile ile aliyopewa Kristo aliposhinda pambano lake dhidi ya Shetani. Mwanadamu kabla hajaanguka dhambini alikuwa akiishi katika ulimwengu wa roho ndiyo maana hawakujiona kuwa wapo uchi maana walivikwa vazi la utukufu. (Mwanzo 2:25) “Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.” Lakini mara tu walipotenda dhambi wakafumbuliwa macho na kutoka katika ulimwengu wa roho na kuanza kujionea yaliyomo kwenye ulimwengu wa mwili. (Mwanzo 3:7) “Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.”
Adamu na Eva walipaswa kufunguliwa macho ili kuingia kwenye ulimwengu wa mwili kama ambavyo na sisi tunapaswa kufumbuliwa macho ili tuingie kwenye ulimwengu wa roho. (Waefeso 1:18-23) “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”
Tunahitaji macho yetu yatiwe nuru ili kujua utajiri wa utukufu wa urithi katika watakatifu (yaani sisi) jinsi ulivyo na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo. Mambo hayo mawili ambayo hakuna viumbe wengine walionayo yanatuongezea hadhi katika ulimwengu wa roho na kutufanya viumbe tusioweza kutwezwa au kuhujumiwa na nguvu zozote za giza. Kristo alipofufuliwa katika wafu aliwekwa mkono wa kuume katika ulimwengu wa roho na jambo ambalo amelifanya pia kwetu tuliomwamini. (Waefeso 2:6) “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.”
Katika ulimwengu wa roho sisi tuliomwamini Kristo tumeketishwa pamoja naye mkono wa kuume wa Mungu Baba. Hiyo ni kumaanisha tunayo mamlaka yote dhidi ya nguvu za kuzimu na nguvu za giza. Mkono wa kuume wa Mungu unasifika kwa kuwa na uweza wa kutenda maajabu. (Zaburi 98:1) “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.”
Sisi tuliofufuliwa Pamoja na Kristo hatupaswi kuishi kama tusiojua hadhi yetu tukitishwa na nguvu za adui ambaye uwezo wake upo chini sana kuliko uweza wetu. Kumbuka shetani ana uwezo lakini sisi tuna uweza ambao unapatikana kwa Mungu peke yake. (Wakolosai 3:1) “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.”
Paulo mara nyingi alitambulisha jambo hili kama siri ambayo watakatifu walitakiwa kuifahamu na kuikumbatia. (Waefeso 3:7-10) “Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho.”
Utajiri wa Kristo usiopimika unahusisha madaraka makubwa aliyonayo Yeye na wale wanaomwamini katika kulinganisha na madaraka ya mamlaka na falme zingine katika ulimwengu wa roho. Yesu aliposulubiwa pale msalabani alizodondosha mamlaka hizo na kuziaibisha vibaya. (Wakolosai 2:14-15) “Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” (Wakolosai 2:13-15) “Alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. Juu ya msalaba Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.”
Yesu alidhihirisha uwezo wake juu ya tawala za pepo wabaya katika ulimwengu wa roho na ulimwengu wa giza. Sisi nasi tunapambana na mamlaka hizo hizo na ili tuzishinde twapaswa kutambua hadhi yetu katika ulimwengu wa roho. (Waefeso 6:12) “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”
Hadhi yetu ambayo shetani anaihofu ni ile ya kuitwa Mwana wa Mungu. Cheo hicho kimebeba mamlaka kubwa yenye uweza wa ajabu ambayo shetani anaihofia sana. (Marko 3:11) “Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” (Warumi 8:29) “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.” (1 Yohana 3:1) “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.”
Unayo hadhi ya kuitwa Mwana wa Mungu tena mzaliwa wa kwanza. Katika ulimwengu wa roho hii ni hadhi ya juu sana iliyo juu ya mamlaka zingine zote za duniani na katika ulimwengu wa giza. zote. (Zaburi 89:27) “Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.” (Waebrania 2:6-8) “Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake.”
Miongoni mwa mambo ambayo Mungu anakutuma kwa walio gizani bad oni kutangazia Habari hii njema juu ya mamlaka waliyonayo katika ulimwengu wa roho. Tamba sasa na Yesu ukitambua hadhi yako katika ulimwengu wa roho. (Matendo 26:16-18) “Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako; nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.”
Makala hii imeandaliwa na Mchungaji Stephen Julius Letta wa Kanisa la Waadventista wa Sabato, Dar es Salaam, Tanzania. 14/10/2025.