MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 1:1-26
- Kitabu cha kwanza cha mwandishi wa Matendo ya Mitume ambako aliandika yale Yesu aliyokuwa ameanza kufanya na kutenda ni kipi? Ubatizo wa Roho Mtakatifu unatofautianaje na ubatizo wa maji? Upi ni ubatizo muhimu? Je aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu hahitaji ubatizo wa maji? Ubatizo wa maji kidogo na wa maji mengi una tofauti yoyote? Je ubatizo wa maji mengi una shida gani na wa maji kidogo una shida gani?
- Je kuna haja ya kujua nyakati au majira ya kuja kwa ufalme wa Mungu? Kwa nini tarehe ya kutimia kwa jambo hili la kuja kwa Yesu kusimamisha ufalme wake limekuwa la siri? Kuna ubaya wowote wanadamu wakijua tarehe na saa ya kuja kwa Yesu? Mbona Maandiko yanatuahidi kwamba sisi hatumo gizani hata siku ile itukute bila kujua wala kujiandaa? (1 Wathesalonike 5:4)
- Kwa nini kupokea nguvu kulikuwa sharti la lazima kabla ya kwenda kuhubiri injili? Je, leo watu wanasubiri kupokea nguvu kabla ya kwenda kuhubiri injili? Watu wawili waliowapa wanafunzi maneno ya matumaini baada ya Yesu kupaa mawinguni walikuwa nani? Je Yesu ataapokuja ataonekana kama jinsi alivyoonekana wakati wa kupaa kwake? (Ufunuo 1:7) Kwa nini watu wengine husema Yesu atakuja kwa siri? (Mathayo 24:23-27). Ujumbe uliotolewa na wale watu wawili ulikuwa na umuhimu gani kwa wale wanafunzi?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 3:1-26
- Je, saa tisa ni saa ya kusali? Je, ni sahihi kumweka kiwete kwenye mlango wa hekalu ili aombe sadaka kwa watu wanaoingia humo? Je wale wanaowatembeza walemavu kwenye matoroli ili waombe fedha kwa watu wanawasaidia au wanawadhalilisha? Kanisa linapaswa kufanya nini kuwasaidia walemavu? Kwa nini Petro na Yohana walimwambia yule kiwete "tutazame sisi" badala ya kumwambia mtazame Yesu? Je kuna wakati imani ya mfuasi wa Kristo inapaswa kujengwa juu ya kiongozi wake wa kiroho? (1 Wakorintho 11:1 Wafilipi 3:17)
- Je, yule mlemavu alipata alichokitaka au alichohitaji? Je kuna wakati katika maisha tunaishia kupata tunachotaka badala ya tunachohitaji? Katika kujibu maombi yetu Mungu hutupatia tunachotaka au tuna chohitaji? (Waefeso 3:20). Nyayo na vifundo vya miguu ya mlemavu vilitiwa nguvu wakati Petro aliposema simama uende au alipomshika mkono wa kuume na kumwinua? Kuna nini kwenye mguso wa mwombaji wakati anapomwombea mgonjwa?
- Muujiza wa uponyaji uliotokea haukutokana na nguvu au utauwa wa Petro na Yohana. Kwa nini leo hatushuhudii miujiza hiyo kwa wingi kwa watu wa Mungu? Je, miujiza mingi inayofanyika leo inamtukuza Mungu au inawatukuza wanadamu? Je, kitendo cha kurukaruka hekaluni kilichofanywa na mlemavu aliyeponywa kilikuwa kinavuruga ibada? Je aliyeponywa anaweza kupangiwa namna ya kushukuru na kufurahi?
- Kumkana mtakatifu mwenye haki na kutaka wapewe mwuaji kulikofanywa na Wayahudi kulitokana na nguvu zao wenyewe au kulisukumwa na nguvu za giza na kutokujua? Mkuu wa uzima anawezaje kuuawa na ambao siyo wakuu wa uzima? Kwa nini asijitetee? Je tunapotenda dhambi tunatenda kwa kutokujua kwetu? Kwa nini Wayahudi hawakutambua kuwa Kristo alikuwa anapitia mateso yake kama kutimiza unabii uliotangulia kuandikwa?
- Kwa nini asiyemsikiliza Yesu ataangamizwa na kutengwa na watu wake? Kwa nini kutubu ni kwa lazima kabla ya dhambi kufutwa na kabla ya kuja nyakati za kuburudishwa. Nyakati za kuburudizhwa zinazotajwa hapa ni zipi? Kwa nini asiyemsikiliza Yesu ataangamizwa na kutengwa na watu wake? Kwa nini kutubu ni kwa lazima kabla ya dhambi kufutwa na kabla ya kuja nyakati za kuburudishwa. Nyakati za kuburudizhwa zinazotajwa hapa ni zipi? Je, unadhani unabii uliotabiri kuwa katika uzao wa Ibrahimu kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa umetimia?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 8:1-40
- Ilikuwaje Mungu aruhusu adha kuu kulipata kanisa la Yerusalemu hadi watu wote wakatawanyika? Kwa nini Mitume walibaki Yerusalemu bila kutawanyika? Je tukio hili lina mfanano wowote na mtawanyiko wa wajenzi wa mnara wa Babeli? Je kifo cha Stefano kilileta pigo kwa kanisa? Je Sauli alitambua kwamba analiharibu kanisa kwa kuwakamata waumini wake na kuwatupa gerezani? Je kosa la waumini hao lilikuwa nini? Kwa kufanya hivyo Paulo alitambua kwamba anamwudhi Yesu?
- Je kuna wakati makanisa makubwa yanatakiwa kutawanywa ili injili ipate kuenea? Ilikuwaje Filipo aende Samaria kuwahubiri Kristo hali ya kuwa Wayahudi na Wasamaria hawachanamani? Kwa nini watu wasiomjua Mungu kama Wasamaria walitakiwa kuwahubiriwa Kristo? Je kumhubiri Kristo kunalainisha sana mioyo ya wenye dhambi kuliko masomo mengine? Je mbinu hii inafaa kutumika leo kwenye maeneo mapya yasiyofikiwa na nuru ya injili?
- Ni nini kinachowaletea furaha watu wanapohubiriwa habari za Kristo? Kwa nini nguvu za giza haziwezi kustahimili wakati injili ya Kristo inapohubiriwa? Je kuna wakati uchawi hudhaniwa kuwa ni uweza wa Mungu yule mkuu? Jambo gani laweza kikutambulisha kuwa ule unaodhaniwa uweza wa Mungu ni uchwi? Je wapo watu leo wanaosikilizwa na wadogo na wakubwa kwa sababu ya miujiza yao ya kichawi inayoshaniwa ni uweza wa Mungu?
- Je ni salama kwenda kuhubiri maeneo yanayosifika kwa uchawi? Je mchawi anaweza kuongoka na kuacha uchawi? Je kuombewa kwa kuwekewa mikono kunamfanya mtu apokee Roho Mtakatifu? Je, ni vibaya kukitaka kipawa fulani kwa kukilipia fedha? Je leo kuna wanaojiita watumishi wa Mungu wanaogawa vipawa vya miujiza kwa kuwalipisha watu fedha? Je fikra ya kutaka kuwa maarufu katika huduma za kiroho ni fikra potofu anayopaswa mtu kuitubia?
- Watumishi wa leo huongozwa na malaika katika utendaji wao kama walivyokuwa wakiongozwa wale wa zamani? Je ni sahihi kufanya kazi ya uinjilisti bila kuongozwa na malaika? Je hao malaika wanaowaongoza watumishi wa Mungu hujitokeza kama malaika au kama wanadamu? Je kuna uwezekano wa kupinga mashauri ya malaika aliyetumwa kwako ili akuongoze? Je Mungu anapenda tuwe tunafanya kazi kwa kubahatisha au kwa kuelekezwa? (Matendo 16:14; Matendo 16:9).
- Je kuna watu wanaosoma Maandiko bila kuyaelewa wanaohitaji mtu wa kuwasaidia? Yupi anafaa kuanza naye kujifunza Maandiko kati ya yule anayesoma bila kuelewa au yule asiyependa Maandiko kabisa? Je kuna watu unaokutana nao wasiojua kile unachokijua na wanaotamani kuwa na mtu wa kuwasaidia? Kumhubiri Yesu ni kuelezea jinsi Yesu aliyotimiza mpango wa wokovu kwa wanadamu? Je hilo ni hitaji kubwa kwa wanadamu leo?
- Je njia rahisi ya kufungua darasa la kujifunza Biblia ni ipi? Darasa la Biblia laweza kuanzishwa ukiwa safarini? Je mtu aweza kuamua kubatizwa kwa somo moja tu au ni mpaka ayafahamu mafundisho yote ya Biblia? Je mtu aweza kubatizwa kwa kujifunza siku moja? Je ili mtu abatizwe ni watu wangapi kwa mujibu wa Biblia wanatakiwa kuridhia? Je ipo sababu inayoweza kumzuia mtu anayetaka kubatizwa kutobatizwa?
- Je mbatizwaji anaweza kubatizwa bila shemasi au mtu wa kushuhudia? Je kiapo kidogo wanachopewa wabatizwa kinachowataka wakiri kama wanamwamini Kristo kinatosha? Je ni lazima kila anayebatizwa abatizwe kwenye maji mengi? Je anayebatiza naye ni lazima awe majini? Kwa nini Mungu alimnyakua Filipo ili Towashi asimuone tena? Kwa nini mtu aliyebatizwa kwa maji mengi na baada ya kujifunza na kuamini huwa na furaha?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 9:1-43
- Watu wa Njia hii ni watu gani? Kwa nini waliitwa hivyo? Kwa nini ilikuwa lazima Sauli apewe barua na Kuhani Mkuu ili kwenda kuwakamata wanafunzi wa Bwana? Kwa nini Yesu hakumwadhibu Sauli kwa kuwaza kuwaua wanafunzi wake? Je kutiwa upofu kwa Sauli kule Dameski kulilenga nini? Je Mungu alikusudia kumtumia Sauli kulijenga kanisa alilokuwa analibomoa?
- Je Sauli alikuwa na hiyari ya kumtumikia Mungu au Shetani? Je kuna wakati Mungu akitaka kumtumia mtu kazini kwake humtengenezea mazingira magumu ili akubali kutumika kama ilivyotokea kwa Sauli na Yona? Kuna ukweli gani juu ya kauli kuwa adui mkuu wa kanisa ni lazima atoke kwenye kanisa? Kwa nini vita ya kidini huwa ni dini mbaya na ngumu kuimaliza?
- Je, ugaidi ni zao la vita ya kidini? Kwa nini watu wenye mwelekeo mmoja wa kidini hujikuta wakigombana? Je, kujihesabia haki huwa ni chanzo cha migogoro hiyo? Je ilikuwa rahisi kwa Anania kwenda kumkabili mtu aliyetumwa kuja kuwakamata kama wahalifu? Sauli alikuwa na tatizo kwenye macho ya kiroho zaidi kuliko kwenye macho ya kimwili? Je macho yake ya kimwili yalirejea katika ubora wake wa awali ua ndiyo mwiba aliolilia Mungu autoe maishani mwake? (2 Wakorintho 12:7-9).
- Je ilikuwa rahisi kumkubali Sauli kama mmoja wa wanafunzi wa Yesu? Je watu wenye misimamo mikali ya kidini waweza kuongoka na kuwa wanafunzi wa Yesu na kukiri kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu? Kwa nini kukiri kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu ni kigezo cha kuwa Mkristo? Hii inakuambia nini juu ya Wakristo wasioamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu?
- Kwa nini kuona kulitangulia kupokea Roho Mtakatifu? Sauli aliwatiaje fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski? Je ushuhuda wa aliyeongoka una nguvu gani kwa watu aliokuwa anashiriki nao hapo awali? Kwa nini Wayahudi walitaka kumuua Sauli? Kwa nini wanafunzi wa Yerusalemu walipata shida kuamini kuwa Sauli ameongoka kuliko wale wa Dameski?
- Je, unapokuwa umeongoka na watu wanatilia shaka uongofu wako unafanyaje? Je kuna umuhimu wa kuwa na watu wa aina ya Barnaba makanisani mwetu? Kwa nini Sauli alipendelea kufundisha kwa njia ya midahalo? Je, midahalo ina nafasi gani leo katika kufundisha Neno la Mungu? Unadhani ni kwa nini kanisa lilipata raha katika Uyahudi yote na Galilaya na Samaria? Je ilitokana na kujishughulisha na kazi ya injili?
- Unadhani makanisa yasiyo na raha (yenye migogoro isiyoisha) yameacha kufanya kazi ya injili? Je ni muhimu kwa maiti kuoshwa kabla ya kuzika? Kwa nini wajane walionekana kuumizwa na kifo cha Dorkasi kuliko watu wenine? Wajane wa leo wanapaswa kujifunza nini kwa wajane wa Yafa? Petro aliyemkana Yesu mara tatu aliwezaje kufanya muujiza wa kumponya mwenye kupooza kwa miaka 8 na kumfufua aliyekufa?
- Hii inakuambia nini juu ya uwezo wa Yesu wa kusamehe na kusahau yaliyopita? Je Yesu anaweza kuwatumia watu wake leo kufanya miujiza iliyofanywa na Petro? Maisha ya Dorkasi yalikuwa na msaada kwa watu hata Mungu akaruhusu kumfufua. Maisha yako yamekuwa mbaraka kwa watu hasa jirani zako? Unadhani ukifa leo watu watakukumbuka kwa ukristo wako au kwa matendo yako mema kwao?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 17:1-34
- Kwa nini Wakristo wa awali walikuwa wanakutana siku ya Sabato kwa ibada kwenye masinagogi ya Kiyahudi? Tofauti ya dini ya Kikristo na Kiyahudi ilikuwa ni ipi? Kwa nini Paulo alikuwa na kawaida ya kusali siku za Sabato hata alipojiunga na dini ya Kikristo? Kwa nini Paulo alipendelea kuendesha mafunzo yake kwa njia ya midahalo au mahojiano? Je njia hiyo inafaa kutumika leo?
- Ilikuwaje Wayunani walio wapagani walivutiwa na mahubiri ya Paulo wakati Wayahudi waliokabishiwa mausia ya Mungu walichukizwa na mahubiri ya mtume Paulo? (Warumi 3:1-2). Je kuna wakati vita baina ya Wakristo vyaweza kuwa vizito hadi kufikia hatua ua kuwatumia watu mabaradhuli walio adui wa Mungu kama majambazi na wachawi? Ukijua unakabiliwa na hatari ya namna hiyo unapaswa kufanyaje ili kuiokoa nafsi yako?
- Je ni lazima tofauti za kidini zilete machafuko na ghasia? Kwa nini Wayahudi walikerwa kusikia Yesu ni mfalme na kuonea fahari kuwa chini ya mtawala wa Kirumi Kaisari? Je Wakristo wa kanisa la awali waliupinduaje ulimwengu wote wa wakati huo? Kwa nini watu wa Beroya walisifiwa kuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike?
- Je, ni sahihi kupinga kila wazo jipya la kidini badala ya kuichunguza Biblia inasemaje kuhusu wazo hilo? Kuna faida gani ya kuwa na darasa la kujifunza Maandiko kila siku? Kwa nini kuna watu wanachukizwa sana Neno la Mungu linapohubiriwa? Kwa nini Paulo alichukizwa kuona mji wa Athene umejaa sanamu? Unadhani Paulo angetembelea leo baadhi ya makanisa na kukuta yamejaa sanamu angechukizwa? Sanamu zina ubaya gani?
- Je ni halali kufanya mahojiano ya Neno la Mungu sokoni kama alivyofanya Paulo? Kwa nini Neno la Mungu lilionekana kama upuuzi kwa Wayunani wa Athene? (1 Wakorintho 1:22-24). Faida na changamoto ya wasomi katika kupokea Neno la Mungu ni ipi? Je unadhani wasomi wanatakiwa kupelekewa Neno la Mungu kwa njia tofauti na wengine? Je unakubaliana na Paulo kuwa Waathene walikuwa watu wa kutafakari sana mambo ya dini? Unawatambuaje watu wanaotafakari sana mambo ya dini?
- Je ni kweli Paulo alikuwa amekuja kuwahubiri watu wa Athene Mungu waliyekuwa wakimwabudu pasipo kumjua? Je unapowapelekea watu nuru mpya ni muhimu kuanza na mambo wanayoyafahamu? Je ni muhimu kujua mambo watu wanayoyaamini ili kuona namna ya kuingiza yale wasiyoyaamini? Kama Mungu hakai kwenye hekalu zilizojengwa na wanadamu kwa nini Mungu aliagiza wamjengee hekalu? (Kutoka 25:8).
- Je Mungu ana hekalu alilolijenga yeye mwenyewe ambamo hupendelea kukaa? (1 Wakorintho 6:19). Kwa nini ni kawaida kukuta watu wakithamini mahekalu au nyumba za ibada walizozijenga wenyewe kuliko kumthamini mwanamke (hekalu la Roho Mtakatifu) lililojengwa na Mungu mwenyewe?Je mtu kuonea fahari kazi ya mikono yake badala ya kuonea fahari kazi iliyotendwa na Mungu ni udhihirisho wa kuwa na roho ya Mpinga Kristo? (2 Wathesalonike 2:3-4).
- Je kuna ushahidi gani kuwa mataifa yote ya dunia yalitoka kwa mtu mmoja? Kwa nini watu wa mataifa ya dunia wanatofautiana kwa mwonekano na rangi ikiwa walitoka kwa mmoja? Je ni Mungu aliyefanya mipaka ya makazi ya wanadamu? Je, ni muhimu kujua nyimbo zinazoimbwa na jamii unayokwenda kuihubiria? Je, wanaoabudu sanamu wanachukulia kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe vitu vilivyohongwa kwa ustadi na akili za wanadamu? Zamani za ujinga ambazo Mungu alijifanya kama hazioni ni zipi?
- Je Mungu aweza kumhukumu mtu asiyejua kosa lake? Mungu atauhukumu ulimwengu lini? Nani amewekwa na Mungu kuwa mhukumu wa ulimwengu na kwa nini? (Yohana 5:22; Matendo 10:38-43). Kwa nini habari za ufufuo na wafu ziliwafanya watu wa Athene kumfanyia dhihaka Paulo? Je kitendo kuahirisha kufanya maamuzi kilichofanywa na Waathene wakitaka kumsikiliza Paulo siku nyingine kilikuwa na hatari ya kupoteza nafasi ya kuokolewa?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 18:1-28
- Wahubiri wa injili wanaweza kufanya kazi zingine za kujikimu.kimaisha kama kutengeneza mahema? Kwa nini Paulo alikuwa anatoa hoja zake kila Sabato na siyo siku nyingine? Kwa nini ilikuwa muhimu kuwashuhudia Wayahudi kuwa Yesu ni Kristo? Je kukataa kuwa Yesu si Kristo ni sawa na kumtukana Mungu? Kwa nini kwa Wayahudi ilikuwa rahisi kukubali damu ya Yesu iwe juu yao kuliko kumkubali kama Kristo au aliyetumwa na Mungu?
- Kwa nini injili ilianzia kwa Wayahudi kwanza kabla haijaenda kwa Wamataifa? Watumishi wa Mungu wana uhakika gani wa usalama wao wakati wanapoihubiri Injili ya Yesu? Je utambuzi kuwa Mungu anao watu wenye hamu ya kusikia Neno kuna umuhimu gani kwa mhubiri wa injili anayepitia changamoto kwenye kazi yake? Je woga ni adui mkubwa wa wahubiri wa injili?
- Je unaponyamazishwa usiendelee kuhubiri ni kipi kinapaswa kutendwa? Je ni kunyamaza au kuendelea kuhubiri? Je Mungu leo bado angali anaongea na watu wake kwa njia ya maono usiku? Paulo alidaiwa anawavuta watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Je ni sheria gani hizo? Kazi ya kuwapitia waongofu wapya kwa lengo la kuwaimarisha ni la muhimu katika kupunguza kasi ya watu kurudi nyuma na kupotea?
- Je mtu aweza kuwa hodari wa kuhubiri injili lakini asijue kweli zingine za Biblia? Je mhubiri mwenye mafanikio anaweza kusahihishwa jambo na wasikilizaji wake? Je Roho Mtakatifu hatoshi kumkamilisha mhubiri wa Injili hata imlazimu kwenda kupata mafunzo chuoni? Je ukisikia roho inakuwaka ni sahihi kuomba nafasi ya kuhubiri?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 22:1-30
- Mtu mwenye jitihada kwa Mungu anatambulikaje? Je kuwa na jitihada kwa Mungu ni makosa? Kulelewa na mwalimu Gamalieli kulikuwa kunamwongezea sifa gani mtu? Pamoja na umaarufu wake wote Gamalieli alikuwa anakosea nini katika kuwafundisha watu? Kwa nini haikuonekana kama kosa kwa Myahudi kuwakamata, kuwafunga, na kuwaua Wakristo zamani za Sauli? Unadhani hali hiyo itajirudia wakati wa kufunga historia ya dunia? (Ufunuo 14:14-16).
- Je wakati akiwatesa Wakristo Sauli alikuwa anafahamu kama anamuudhi Kristo? Je ni halali kuwatesa watu mnaotofautiana imani? Kwa nini Sauli alianguka chini baada ya nuru kuu kummulikia pande zote? Anania alimtangazia Sauli uponyaji wa macho? Je unao upofu wa macho ya kiroho unaohitaji tiba? Je kuwafikiria wengine kuwa hawastahili Mungu ni upofu? Je aliye kipofu aweza kumuongoza kipofu mwenzake? (Matendo 26:16-18).
- Je Mungu anayo mambo yaliyoamriwa uyafanye kwa ufanisi wa kazi yako ambayo mtu fulani ameagizwa akuambie? Je kuna wakati umeshindwa kupokea maagizo hayo kwa kukosa kuwa na mawasiliano naMungu? Kama Mungu alikuwa na nafasi na mtu anayelitesa kanisa lake hata akaongoka na kuwa mhubiri wa injili unadhani anaweza kufanya hivyo kwa maadui wa leo wa injili?
- Je ni sahihi kumtakia mgonjwa upone badala ya kumuombea? Utajuaje kama umeitwa kwa kazi ya injili au kwa kazi ya uchungaji? Je Paulo aliyefundishwa na Gamalieli na aliyekuwa na jitihada kwa Mungu alistahili kubatizwa akiwa mtu mzima? Kubatiza watoto wadogo kulitoka wapi? Kwa nini ushahidi ni lazima uwe wa kuona au kusikia? Unapomshuhudia Kristo unashuhudia ulichoona au ulichosikia?
- Kwa nini ushahidi wa Sauli usingekubalika Yerusalemu? Kwa nini baada ya kujitetea Sauli alipigiwa kelele huku watu wakirusha rusha mavumbi juu? Je kuna wakati watu waliokosa hoja hufanya hivyo? Je kuna wakati badala ya kuwageuzia shavu jingine watesi wako unapaswa kudai haki zako kwa kutumia sheria zilizopo? Je Yesu anapenda tuteseke hata kwa mambo ambayo tunaweza kuepuka kwa njia ya kisheria au mazungumzo ya kidiplomasia?
MASWALI YA KUJADILI: MATENDO 23:1-35
- Je ni muhimu kwa mtumishi wa Mungu kujua vifungu vya sheria vinavyolinda haki zako? Je ilikuwa sahihi kwa Paulo kubishana na hakimu baada ya kuhisi haki haitendeki dhidi yake? Je ni halali kuwabishia viongozi wa dini? Paulo alijitambulisha kama Farisayo ili kuwafarakanisha maadui zake? Njia hii ya kuwafaraknisha maadui (devide and rule) inafaa kutumika na mtumishi wa Mungu dhidi ya adui zake awapo kazini?
- Je unadhani Paulo alihitaji ujumbe wa matumaini aliopewa na Mungu usiku kuwa yupo pamoja naye na asiache kazi ya kumshuhudia hata kama ina machungu? Je Mungu bado angali anatoa maneno ya faraja kama hayo kwa watumishi wake leo? Kwa nini jumbe nyingi za matumaini kwa watumishi wake Mungu huzitoa usiku? (Matendo 18:9).
- Je, ni sahihi kutumia nyakati za usiku pia katika kutafuta ķujua mapenzi ya Mungu? Je ni sahihi kuahirisha kupeleka injili maeneo yenye upinzani na kuelekeza kule kusiko na upinzani? Je kuna wakati waumini kutokana na tofauti zao za kidini au sera hufikia hatua ya kukaribia kuraruana hata ikabidi vyombo vya dola kuingilia kati? Je viongozi wa serikali wana haki ya kuingilia inapoonekana dalili kuna uwezekano wa kutokea uvunjifu wa amani?
- Je kuna nyakati waumini hula kiapo cha kumuua kiongozi wao wanayetofautiana naye? Je ipo haja ya viongozi wa kiroho kuwa makini na kujilinda na watu walio kwenye jumuiya zao za kidini wanaotafuta kuwadhuru? Unadhani kuwa karibu na watu ndiko kulikomsaidia Paulo kugundua njama za kumuua? Utajuaje kama mipango mizuri inayopendekezwa na watu walio karibu nawe ina hila ndani yake?