MASWALI YA KUJADILI: MARKO 5:1-43
- Unadhani ujio wa Yesu kwenye nchi hii ya Wagerasi kulilenga kuja kukutana na mtu huyu mwenye pepo? Watu wa nchi yake walifanya jitihada gani kumsaidia mtu huyu? Kauli kuwa hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga tena inaashiria kukata tamaa kumsaidia? Kwa nini kuponywa kwake hakukupokelewa kama tukio lenye faraja? Je walithamini nguruwe kuliko binadamu? Kuna hali hiyo ya kutothamini ubinadamu leo kwa sababu ya kukumbatia mali au vyeo?
- Je kutoa mapepo ni karama ya watu fulani tu au mtu yeyote aweza kuifanya? Kuna haja ya kukimbia ili kujisalimisha na mweye mapepo? Je wanafunzi walifanya vema kukimbia na kumwacha Yesu na mwenye pepo aliye uchi peke yake? Je ni sahihi kwa Yesu kumuuliza mwenye pepo jina lake nani? Jina alilolitaja lilikuwa la mwenye pepo au la Shetani aliyemmiliki?
- Kwa nini Yesu alikataa kufuatana na aliyeponywa mapepo? Muda gani unahitajika kupita ili muongofu mpya kupewa kazi kanisani? Ili uwe mhubiri nzuri unahitaji kupata semina kwanza? Je ushuhuda wa maisha yako waweza kuhubiri kuliko 'mahubiri yako'? Unaweza kufanya nini baada ya kuthibitishiwa na madaktari kuwa ugonjwa wako hauna tiba? Unapaswa kufanya nini ili Yesu atibu ugonjwa wako ulioshindikana? Kwa nini ugonjwa wa yule mwanamke umeitwa msiba?
- Je mtu huponywa na Mungu au huponywa kwa imani aliyonayo kwa Mungu? Kwa nini mwanamke aliyeponywa aliingiwa na hofu na kutetemeka baada ya kugusa pindo la vazi la Yesu? Kwa nini Yesu alichagua watu wa kufuatana naye wakati anaenda kunfufua Binti Yairo? Je watu wasio na imani wana tatizo gani kwenye kumuombea mgonjwa?Kwa nini Yesu hakukatishwa tamaa na watu waliomcheka? Waliotolewa nje kabla ya kuombewa kijana walikuwa na kosa gani?
MASWALI YA KUJADILI: MARKO 6:1-56
- Kwa nini Yesu alikuwa anafudisha katika Sinagogi siku za Sabato? Kwa nini watu wa kwao walishangazwa na mafundisho na miujiza ya Yesu? Kwa nini kijijini kwake Yesu alitambulika kama Seremala na mtoto wa Mariamu? Je kulikuwa na dharau yoyote katika majina hayo? Je, kuendelea kumwita Yesu Mwana wa Seremala ni kumdhalilisha au kumstahi? Ungekuwa umezaliwa tumbo moja na Yesu ungemtambua kama Mwana wa Mungu?
- Je kudharauliwa na watu wanaokufahamu kunahalalisha kutoendelea kufanya huduma ya miujiza ya kuponya watu? Je huko siyo kuzira? Je, kutoa pepo wachafu kunahitaji uwe umepewa amri ya kufanya hivyo na Yesu? Kwa nini wanafunzi walikatazwa kuvaa kanzu mbili? Kukung'uta mavumbi kulimaanisha nini? Huduma ya kupaka mafuta ina umuhimu gani katika kuombea wagonjwa?
- Unadhani nani anahusika katika kuuawa kwa Yohana Mbatizaji? Je ni Herode, ni mke wake, ni Binti yake, au ni askari aliyetumwa? Je kuna uwezekano wa watawala kuwapoteza au kuwaangamiza wanaowatia hofu ili kufurahisha familia zao? Mungu alikuwa wapi kuzuia kuuawa kwa Yohana Mbatizaji? Je kumsema mtawala kuwa amekosea ni kukosa adabu au ni kutimiza Sheria? Je kwa kufanya hivyo Yohana Mbatizaji hakuwa anajiingiza kwenye siasa za nchi?
- Wajibu wa Mkristo ni upi kwa watawala wanaokiuka maadili? Je ni kuendelea kuwaombea au kuwakemea? Je kazi ya Mungu inahitaji kuitolea taarifa? Je, kuna haja ya kupata muda wa mapumziko kwa kazi ya Mungu? Kwa nini Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake kupanda mashuani? Kwa nini Yesu alipendelea kuomba mlimani peke yake? Kwa nini alipotembea juu ya maji alitaka kuwapita wanafunzi wake? "Wote waliomgusa walipona" inakufundisha nini?
MASWALI YA KUJADILI: MARKO 7:1-37
- Kwa nini wanafunzi wa Yesu walidaiwa kula kwa mikono najisi? Kwa nini wanaofundisha maagizo ya wanadamu huku wakipinga Amri za Mungu wanatajwa kama waaomwabudu Mungu bure? Kwa nini kimtiacho mtu unajisi ni kile kimtokacho na si kile kimwingiacho?
- Kwa nini Yesu alimwambia mwanamke Myunani aache watoto washibe kwanza? Kwa nini Yesu katika kumponya kiziwi ilibidi atie vidole masikioni mwake? Efatha maana yake nini?
CHAGUA JIBU LILILO SAHIHI: (kila swali marks 20).
- Unadhani hoja inayoshindaniwa kwenye Marko 7:1 – 23 ni
(a). uhalali wa kula vyakula najisi (b) uhalali wa kula chakula kisicho najisi kwa mikono isiyonawiwa hadi kwenye kiwiko (c) Kosa lililofanywa na wanafunzi wa Yesu la kula vyakula najisi vilivyokatazwa kwenye torati.
- Wayahudi:
(a) Waliacha amri za Mungu na kushika mapokeo ya wanadamu.
(b) Waliacha mapokeo ya wanadamu na kushika amri za Mungu.
(c) Walishika mapokeo ya wanadamu na amri za Mungu.
- Yesu kabla ya kumponya kiziwi..........
(a) Alimtemea mate usoni mbele za watu
(b) Alitema mate akamgusa ulimi
(c) Alimwambia Efatha maana yake Achia.
- Kilichomfanya Yesu kumponya binti wa mwanamke Mfoinike aliyekuwa na mapepo ni pale huyo mwanamke aliposema:
(a) Lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.
(b) Mtoe pepo katika binti yangu
(c) Si vizuri kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa
- Wanafiki kwa mujibu wa sura ya saba ya Marko ni wale:
(a) Wanaomheshimu Mungu kwa midomo ila mioyo yao ipo mbali.
(b) Wanaokataa kula nguruwe wakati alihalalishwa na Yesu.
(c) Wasionawa mikono mpaka kiwiko.
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 8:1-38
✅1. Yesu aliwaita wanafunzi akawaambia
(a) Wawatawanye mkutano waende zao nyumbani.
(b) Kwa kuwa wanafunga watazimia njiani.
(c) Nawahurumia mkutano kwa kuwa hawajala siku tatu.
✅2. Yesu alipovunja mikate 5 na kuwapa watu 5,000 wanafunzi walichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? (a) 12 (b) 7 (c) 5
✅3. Yesu alipovunja mikate 7 na kuwapa watu 4,000 wanafunzi walichukua makanda mangapi yamejaa vipande?
(a) 12 (b) 7 (c) 5
✅4. Yesu alipomuuliza kipofu aliyemwekea mikono unaona nini alijibu,
(a) Naona watu wanatembea
(b) Naona miti inatembea
(c) Naona watu kama miti, inakwenda.
✅5. Yesu alipowauliza wanafunzi wake vile watu wanavyomwita walisema yeye ni
(a) Yohana Mbatizaji (b) Eliya (c) Mmojawapo wa manabii (d) Majibu yote hapo juu ni sahihi.
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 9:1-50
✅1. Jambo lililowasumbua wanafunzi kuelewa ni:
(a) Musa na Eliya walitokea wapi na walienda wapi
(b) Nguo za Yesu zilifuliwa na nani
(c) Kufufuka katika wafu maana yake nini?
✅2. Wanafunzi wa Yesu walishindwa kutoa pepo maana hawakuwa wameruhusiwa na Yesu.
(b) Walishindwa kutoa pepo kwa kuwa hawakuwa na imani.
(c) Walishindwa kutoa pepo kwa kuwa hawakuwa na mavazi yanayometa-meta.
✅3. Baba wa mtoto mwenye pepo alionyesha (a) Kuwa na imani thabiti isiyoyumba. (b) Kuwa na imani iliyopungua na inayohitaji kujaziwa (c) Kuwa ni mbishi na anayetaka sifa.
✅4. Wanafunzi wa Yesu waliogopa kumwuliza (a) Kuhusu habari za kuuawa na kufufuka kwake. (b) Namna alivyomponya mwenye pepo. (c) Kilichosababisha wao kushindwa kutoa pepo.
✅5. Wanafunzi waliona mtu anayefanya miujiza ambaye hafuatani nao (a) Wakamkataza asifanye miujiza (b) Wakamfundisha namna ya kufanya miujiza (c) Wakamwonea wivu.
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 10:1-52
✅1. Je ni halali mtu kumwacha mkewe?
(a) Ni halali. Ndiyo maana Musa aliruhusu waachane.
(b) Si halali. Maana alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe.
(c) Si halali. Ila kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya wanadamu Musa aliruhusu waachane na Mungu akaridhia.
✅2. Yesu alichukizwa
(a) Kuletewa watoto wadogo ili awaguse
(b) Watoto kukemewa na wanafunzi wake.
(c) Kuletewa watoto wadogo ili awabatize.
✅3. Yesu alimjibuje aliyemuuliza cha kufanya ili arithi uzima wa milele?
(a) Auze alivyo navyo awe maskini.
(b) Ashike Amri zote 10 za Mungu.
(c) Amepungukiwa upendo kwa binadamu wenzake.
✅4. Yesu alipoulizwa "ni nani awezaye kuokoka" alijibu.
(a) Ni yule ategemeaye uwezo wa Mungu.
(b) Ni yule aliyeacha vyote akamfuata.
(c) Ni yule aliye wa mwisho hapa duniani.
✅5. Yule mwombaji kipofu aliposikia kuwa Yesu anamuita
(a) Alianza kupaza sauti yake na kusema Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.
(b) Alitupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.
(c) Alisema nataka nipate kuona.
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 11:1-33
✅1. Wanafunzi wa Yesu walipokuwa wanamfungua mwana-punda ‐------- wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda?
(a) Baadhi ya watu waliosimama huko
(b) Wapita njia
(c) Wenye mwana-punda.
✅2. Yesu aliuendea mtini asubuhi ili achume tini maana
(a) aliona njaa
(b) alikuwa na hamu na tini
(c) haukuwa wakati wa tini
✅3. Yesu alisema yoyote myaombayo mkisali aminini ya kwamba
(a) mtayapokea nayo yatakuwa yenu.
(b) Baba yenu aliye mbinguni atawasamehe ninyi makosa yenu.
(c) yatajibiwa sawasawa na mapenzi ya Mungu.
✅4. Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi?
(a) mbinguni
(b) kwa wanadamu
(c) haijulikani
✅5. Mambo aliyokuwa akiyatenda Yesu alikuwa akiyatenda kwa mamlaka gani?
(a) kwa mamlaka ya Mungu
(b) kwa mamlaka ya wanadamu
(c) kwa mamlaka ya Shetani.
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 12:1-44
✅1. Mwenye shamba alikuwa akituma watumwa kwa wapangaji wa shamba ili
(a) wakakague maendeleo ya shamba
(b) wakarithi shamba
(c) wakapokee matunda ya mizabibu
✅2. Wakulima walimuua mtoto wa mwenye shamba
(a) kwa sababu aliwachokoza
(b) kwa sababu alikuwa mrithi wa shamba
(c) kwa sababu alitaka kuwatoa shambani
✅3. Baada ya mtoto wake kuuawa na wakulima mwenye shamba
(a) atawaachia shamba lake wale wakulima
(b) atalikodisha shamba lake kwa wakulima wengine
(c) atamkabidhi mwanae shamba lake
✅4. Musa aliruhusu kurithi mke wa marehemu ili
(a) kumsaidia kuzaa watoto
(b) kumpunguzia machungu
(c) kumsaidia asiwe malaya
✅5. Yesu alimsufu mjane aliyetia sandukuni senti mbili kuliko matajiri waliotia pesa nyingi kwa sababu
(a) mjane alizipata pesa zake kwa shida
(b) mjane alikuwa ametoka kufiwa
(c) mjane alikuwa ametoa vyote alivyonavyo
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 14:1-72
✅1. Waliotafuta njia ya hila ya kumkamata na kumwuua Yesu walikuwa
(a) Viongozi wa Serekali ya Kirumi
(b) Wakuu wa Makuhani na Waandishi
(c) Viongozi wa dini.
✅2. Watu walilaumu kitendo cha mwanamke aliyempaka Yesu mafuta kwa sababu
(a) Mwanamke yule alikuwa malaya
(b) Mafuta yale yalikuwa na thamani kubwa.
(c) Mafuta yale yangeweza kuuzwa kwa dinari 300 na zaidi na kupewa maskini.
✅3. Wakuu wa makuhani walipopata habari kuwa Yuda amekubali kumsaliti Yesu
(a) Walimkanya sana asifanye hivyo
(b) Wakafirahi sana wakaaodi kumpa fedha
(c) Walimwendea Yesu wakimwonya juu ya mpango wa Yuda.
✅4. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akawaambia nendeni mjini nanyi mtakutana na
(a) Mwanaume amechukua mtungi wa maji.
(b) Mwanamke amechukua mtungi wa maji
(c) Kundi kubwa la watu wanakuja kunilaki.
✅5. Ingawa Yesu alijua atasalitiwa na kuuawa bado alimpa ole anayemsaliti kwa sababu
(a) ameyatekeleza hayo kwa tamaa zake na hajatumwa na Mungu.
(b) muda wake ulikuwa haujafika
(c) hakumshirikisha
✅6. Nao walipokwisha _________ walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.
(a) kusali
(b) kula
(c) kuimba
✅7. Yesu alipowaambia wakeshe wasije wakaingia majaribuni alitaka
(a) waombe angalau kwa saa moja pamoja naye
(b) wajiandae kumtetea mara atakapokamatwa
(c) wajiandae kukimbia
✅8. Yuda Iskariote aliwapa ishara gani wale wakamataji ili kumtambulisha Yesu?
(a) Jogoo kuwika mara tatu.
(b) Kumbusu
(c) Kuanguka kifudifu.
✅9. Kuhani mkuu alirarua nguo zake kwa kuwa Yesu alikuwa amejitambulisha
(b) kama Mwana wa Mungu.
(a) kama Kuhani mkuu
(c) kama mfalme wa ulimwengu.
✅10. Yule aliyemtambua Petro kama ni mwanafunzi wa Yesu alikuwa
(a) kijakazi wa Kuhani Mkuu.
(b) askari wa Kirumi
(c) mfalme Herode
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 15:1-47
✅1. Wakuu wa Wayahudi waliwataharakisha mkutano waombe wafunguliwe Baraba badala ya Yesu. Baraba alifungwa kwa kosa gani?
(a) Alikuwa amemsaliti Yesu
(b) Alikuwa amefanya fitina na kufanya uuaji.
(c) Alikuwa amehoji kwa nini Warumi wawatawale Wayahudi.
✅2. Pilato alimfungulia Baraba kutoka gerezani kwa kuwa
(a) ni kawaida ya serikali ya Kirumi kumfungulia mfungwa mmoja aliyeombwa na raia wakati wa sikukuu
(b) alikuwa raia mwenye sifa njema kuliko Yesu
(c) alikuwa amejutia kosa lake na kujirekebisha
✅3. Pilato alipowauliza makutano ni ubaya gani Yesu ametenda wao walijibu_______
(a) Anawadhulumu watu mali zao
(b) Anakufuru kwa kujifanya kuwa yeye ni Mungu.
(c) Msulibishe
✅4. Wakamleta mpaka mahali paitwapo __________ yaani Fuvu la kichwa.
(a) Golgotha
(b) Getsemane
(c) Kalvari
✅5. Waliomsujudia Yesu baada ya kupigwa mijeledi na kutemewa mate walifanya hivyo
(a) ili kumpunguzia maumivu
(b) ili kumtambua kuwa ni mfalme wa Wayahudi
(c) ili kumdhihaki
✅6. Baada ya Yesu kuelemewa na uzito wa msalaba na kuanguka nao mara kadhaa askari wa Kirumi
(a) wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita aitwaye Simoni Mkirene aubebe.
(b) wakauchukua msalaba na kuuweka kwenye gari linalokokotwa na farasi.
(c) wakaufunga msalaba kwa kamba ili Yesu aukokote.
✅7. Baada ya Yesu kusulubiwa msalabani wapita njia walitikisa vichwa vyao wakisema,
(a) jiponye nafsi yako ushuke msalabani
(b) mtu huyu hakuwa na hatia yoyote
(c) Yesu Mwana wa Daudi tuokoe
✅8. Eloi, Eloi, lama sabakthani maana yake
(a) Mungu wangu, Mungu wangu, niokoe.
(b) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
(c) Mungu wangu, Mungu wangu, naiweka roho yangu mikononi mwako.
✅9. Aliyetamka "hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu wakati wa kufa kwa Yesu alikuwa nani?
(a) mmojawapo wa wafungwa walisulibishwa na Yesu
(b) Pilato
(c) Akida
✅10. Mtu aliyeingia kwa Pilato na kuuomba mwili wa Yesu ili akauzike alikuwa nani?
(a) Wanawake waliofuatana naye huko Galilaya ili kumtumikia
(b) Akida wa jeshi la Kirumi
(c) Yusufu wa Arimathaya
MASWALI YA KUCHAGUA: MARKO 16:1-20
✅1. Siku Yesu aliyofufuka inaitwa:
(a) siku ya kwanza ya juma
(b) siku inayofuata baada ya Sabato kuisha.
(c) Jumapili
(c) A, B na C, hapo juu ni sahihi.
✅2. Sabato ni siku
(a) iliyo kabla ya siku ya kwanza ya juma
(b) iliyo kabla ya Jumapili
(c) ya Jumamosi
(d) A, B, na C hapo juu ni sahihi.
✅3. Yesu alifufuka
(a) siku ya kwanza ya juma
(b) siku ya saba ya juma
(c) siku ya Ijumaa Kuu
✅4. Mariamu Magdalene aliwafikishia wenzake habari za kufufuka kwa Yesu na kuwakuta wakiwa
(a) wamelala usingizi
(b) wanaomboleza na kulia
(c) wanaomba na kusali
✅5. Waombolezaji waliposikia habari kuwa Yesu yu hai na ameonekana
(a) walifurahi na kumtukuza Mungu
(b) walijawa na hofu kubwa
(c) hawakusadiki
✅6. Ipi kauli sahihi ya Yesu
(a) Aaminiye na kubatizwa ataokoka
(b) Asiyeamini akabatizwa ataokoka
(c) Aaminiye bila kubatizwa ataokoka
✅7. Kijana aliyevaa mavazi meupe waliyemkuta kaburini aliwaambia "enendeni mkawaambie wanafunzi na _________ ya kwamba awatangulia kwenda ________.
(a) Yohana, Galilaya
(b) Mariam, Yerusalemu
(b) Petro, Galilaya
✅8. Walioambiwa watashika nyoka na hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa ni kina nani?
(a) Wanafunzi wa Yesu
(b) Waaminio
(c) Waliokwenda kaburini siku Yesu alipofufuka
✅9. Baada ya kufufuka Yesu aliwaagiza wanafunzi wake waende ulimwenguni wakaihubiri Injili
(a) kwa kila kiumbe
(b) kwa wanadamu wote
(c) kwa nyumba ya Israeli
✅10. Yesu alipopaa mbinguni alienda
(a) kuketi mkono wa kuume wa Mungu.
(b) kuandaa makao ya watakatifu
(c) kufanya sherehe ya kukamilisha kazi ya ukombozi