Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

KUVIISHI VIAPO VYA NDOA

Ndoa ni makubaliano ya kikataba ya kuishi pamoja kati ya mwanaume na mwanamke kama mume na mke hadi mauti itakapowatenganisha. Makubaliano haya ni ya kudumu na ndiyo maana yanaitwa pingu za maisha. Wanandoa hawa wanatakiwa kupitia mchakato wa kuacha, kuambatana, na kuwa mwili mmoja mchakato ambao unawahitaji kutumia maisha yao yote kuweza kuukamilisha. (Mwanzo 2:24) “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Wanaoachwa katika utaratibu huu siyo wazazi tu, bali hata ndugu wengine wa karibu, rafiki, na mazoea mengine yasiyo na afya katika uhusiano unaoanzishwa. Kuacha hapa kunakusudia kupunguza ukaribu unaoweza kuathiri mahusiano yenu mapya.

Viapo vya ndoa

Wanandoa wanapounganishwa hutoa viapo vya ndoa ambavyo huahidi kuviishi siku zote watakazokaa pamoja. Viapo hivi vinapokiukwa husababisha matatizo makubwa katika ndoa. Katika viapo hivyo kila mwanandoa huahidi kumtendea mema mwenzake hata kama mzingira yatabadilika kwa kutambua kuwa kila mmoja wao anahitaji kupendwa, kufarijiwa, kuheshimiwa, kutunzwa, na kujenga mahusiano ya karibu kuliko mengine yote.

Kisha mchungaji atamuuliza Bwana harusi: “Je, unamkubali mwanamke huyu kuwa mke wako uliyemuoa kihalali, na kuishi naye katika hali takatifu ya ndoa kama ilivyoamriwa na Mungu? Je, utampenda, na kumfariji, na kumheshimu, na kumtunza, katika ugonjwa na katika afya; na kuwaacha wengine wote, ukidumu na yeye tu siku zote mtakazoishi?” Bwana arusi atajibu: “Ndiyo, namkubali.”

Kisha mchungaji atamuuliza Bibi arusi: “Je, unamkubali mwanamume huyu kuwa mume wako aliyekuoa kihalali, na kuishi naye katika hali takatifu ya ndoa kama ilivyoamriwa na Mungu? Je, utampenda, na kumfariji, na kumheshimu, na kumtunza, katika ugonjwa na katika afya; na kuwaacha wengine wote, ukidumu na yeye tu siku zote mtakazoishi?” Bibi arusi atajibu: “Ndiyo, namkubali.”

Ndipo Bwana arusi atamshika mkono yule bibi arusi nao watafuatisha maneno yanayosemwa na mchungaji kama ifuatavyo: “Nawasihi watu wote waliopo hapa, washuhudie kwamba mimi (majina yote—fulani fulani bini fulani) nakutwaa wewe (majina yote—fulani binti fulani) uwe mke wangu halali wa ndoa; niwe nawe na kuambatana nawe tangu sasa hata siku zote, katika hali njema na katika hali mbaya, latika utajiri na katika umaskini, katika ugonjwa na katika afya, nikupende na kukutunza, mpaka mauti itakapotutenganisha kulingana na amri takatifu ya Mungu; na katika mambo hayo nakupa ahadi yangu.”

Ndipo Bibi arusi naye atafuatisha maneno yanayosemwa na mchungaji kama ifuatavyo: “Nawasihi watu wote waliopo hapa, washuhudie kwamba mimi (majina yote—fulani fulani bini fulani) nakutwaa wewe (majina yote—fulani binti fulani) uwe mume wangu halali wa ndoa; niwe nawe na kuambatana nawe tangu sasa hata siku zote, katika hali njema na katika hali mbaya, latika utajiri na katika umaskini, katika ugonjwa na katika afya, nikupende na kukutunza, mpaka mauti itakapotutenganisha kulingana na amri takatifu ya Mungu; na katika mambo hayo nakupa ahadi yangu.”

Taasisi inayojitosheleza

Ndoa ni taasisi inayojitosheleza yenye lengo la kukuza upendo wa Mungu baina ya wanafamilia na walio nje ya familia, kuwa kituo cha uinjilisti, na kuunda taasisi imara ya kiuchumi. Mungu amekusudia mume awe kiongozi (kichwa cha familia). (Waefeso 5:23) “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.” Mungu amekusudia pia mke awe mshauri mkuu wa mume, mtekelezaji na msimamizi wa shughuli za nyumbani, na mwelimishaji mkuu wa watoto. (Mithali 31:26) “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.” (Mithali 31:27-29) “Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu. Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema, Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.” (Mithali 6:20) “Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako.”

Katika mazingira hayo haipo haja ya nyumba kuongozwa na baba mzazi au mama mzazi au kiongozi wa ukoo au marafiki. Hao wanakaribishwa tu kutoa ushauri ambao kabla ya kuutekeleza mtakuwa na nafasi ya kuujadili peke yenu na kuutolea uamuzi. Ushauri usipokuwa na tija au unapoingilia uhuru wenu mtautupilia mbali na kuendelea na mipango mliyojiwekea. Ni makosa kuwa na mipango ya kifamilia isiyomhusisha mume au mke. Tena ni makosa kwa mmoja wa wanandoa kutoa msaada mkubwa walio nje ya familia bila mwenzi wako kushirikishwa au kujulishwa.

Mungu huchagua mwenzi kulingana na mahitaji

Kazi ya kuchagua mwenzi wa maisha hufanywa na Mungu mwenyewe. Hii ni kwa sababu Mungu anamfahamu mtu atakayeweza kuendana nawe vizuri zaidi kuliko wewe mwenyewe unavyoweza kumfahamu.  (Mwanzo 2:18, 21-23) “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.” Mungu anajua mtu akufaaye kuwa mwenzi wa Maisha na kwa wakati wake atamleta kwako. (Mithali 19:14) “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Lakini ili Mungu akuletee huyo aliyekuandalia inakupasa kumuomba wala usikate tamaa. (Luka 18:1) “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.”

Mwenzi hutosheleza yaliyopungua

Mwenzi wa maisha huja akiwa amebeba yale yaliyopungua kwa mwenzake. (Yeremia 31:22) “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.” Kuna tofauti kubwa kati ya mwanaume na mwanamke katika utendaji wao. Mwanamke ana uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja bila kuchoshwa tofauti na mwanaume. Mwanamke ana uwezo wa kukumbuka mambo madogo madogo yaliyo ya muhimu kuliko mwanaume na mwanamke anaendeshwa na hisia zaidi kuliko kanuni.

Chukulianeni mizigo

Mojawapo ya jukumu la muhimu la wanandoa wanaoishi pamoja ni kufahamiana tabia. Mtu yeyote unapomfahamu tabia huwa ni rahisi kuishi naye. Kwa kawaida tabia za wanadamu zimetofautiana. Zipo zile zinazoweza kurekebishika kirahisi na zile ambazo kurekebishika kwake huchukua muda mrefu au hushindikana. Mfano, tabia ya kucheka kwa sauti kubwa au kupiga miayo kila wakati, tabia ya kutafuna chakula kwa kutoa sauti na bila kufumba mdomo, tabia ya kupandisha makamasi, tabia ya kuweka vidole puani, tabia ya kuweka mikono nyuma au mifukoni unapoongea, tabia ya kukoroma unapolala, tabia ya kufikicha masikio kwa vidole na tabia nyingi nyingine kama hizo mtu huzaliwa nazo na hubadilika kwa shida sana. Migogoro mingine inaweza kusababishwa na tofauti zinazoletwa na makundi haya. Njia ya kuepuka hiyo migongano ni kuchukuliana. (Wagalatia 6:2) “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”

Tabia nne za wanadamu

Tabia nyingine ya kupenda kutawala na kuwatumia wengine, au tabia ya kuongea sana hata kukosa usiri, au tabia ya kuwa na misimamo isiyotaka kubadilika, au tabia ya unyamazifu uliovuka mipaka ni tabia pia zilizo ngumu kubadilika na ambazo kwa namna fulani watu wamezaliwa nazo. Wataalamu wamezigawanya tabia za wanadamu katika makundi makuu manne. Kundi la Koleriki, kundi la Melankoli, kundi la Sanguini, na kundi la Flagmatiki.

Koleriki

Koleriki wanapenda watu wa kundi lao zaidi wenye ujasiri, kusimamia kazi, kujitoa mhanga, kufanya kazi kupita kiasi, na kuthamini kazi kuliko watu, na watu wenye hasira za haraka. Hawa ni viongozi wenye njozi. Wakidhamiria kufanya jambo lazima watatimiza hata kama ni kwa njia ya kuumiza watu. Hawa ni mabingwa wa kutatua matatizo lakini ni watu wanaopenda sifa pia.

Melankole

Melankoli wanapenda kufanya mambo kwa kufuata utaratibu waliojiwekea na hupendelea kuweka sheria na kuzisimamia, ni watunzaji wazuri wa kumbukumbu, na si wepesi wa kupokea mabadiliko, na wana asili ya kupenda usafi. Ni wabunifu, wazuri katika kuweka mipango ya baadaye, wabunifu, na watu wanaofikiri sana.

Sanguini

Sanguini ni wepesi kufanya maamuzi bila kufikiria matokeo. Hutoa ahadi wasizo na uwezo wa kuzitimiza. Wanajua kuchangamsha, wepesi kulia na wepesi kucheka na hupenda kucheka kwa sauti ya juu. Wepesi kusamehe na kusahau hawatunzi mambo moyoni. Wanazoeana na watu kirahisi. Wanashughulika zao na sasa kuliko kesho. Wanajua kuwahamasisha wengine lakini wanakata tamaa kirahisi. Wanapenda kushindana na michezo na ni wasimuliaji wazuri wa visa.

Flagmatiki

Flagmatiki ni wakimya na wapenda amani. Ni wasikilizaji wazuri na wapatanishi. Wavumilivu wa usumbufu wanaofanyiwa na wenzao ila wakichoka kuvumilia hawana kurudi nyuma. Huchelewa kufanya maamuzi na hupendelea kuficha hisia zao za ndani

Chuo cha kujifunzia upendo

Mungu aliumba ndoa ili kiwe chuo kidogo cha kujifunza tabia yake ya upendo. Kwenye ndoa ndipo mahali ambapo watu hukosana mara nyingi na kusameheana mara nyingi pia. Ndoa ya mwanaume na mwanamke ni kivuli cha ndoa baina ya Kristo na kanisa lake; mume akimwakilisha Kristo na mwanamke akiwakilisha kanisa. Kinachowaunga pamoja wanandoa ni upendo wa hisia na upendo wa kanuni. 

Upendo wa Kanuni unadumu

Katika hatua ya awali Adamu alipoletewa Hawa alimpenda kwa hisia kutokana na namna alivyokuwa anavutia na alivyomuondolea upweke. Lakini upendo huo uliyumba alipoenda dhambi na akadiriki kumshitaki kwa Mungu. (Mwanzo 3:12) “Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Kilichowasaidia kuendelea kuishi pamoja bila kuachana baada ya hayo kutokea ni upendo wa kanuni ule ule unaomfanya Yesu aendelee kutupenda pamoja na kuwa tumemkosea.

Majukumu ya ndoa yanahitaji karama

Kuoa au kuolewa ni karama kwa sababu yale ambayo kila mwanandoa anatakiwa amtendee mwenzake. Mwanadamu hawezi kuyatimiza kwa ufanisi yale aliyoapa siku ya kuoana kwao asipokuwa na karama itokayo kwa Mungu. Mume anatakiwa kumpenda mke kwa upendo ambao Kristo alilipenda kanisa. Kristo alilipenda kanisa kwa upendo unaoongeza thamani siyo unaovutiwa na thamani. (Waefeso 5:25-27) “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.”

Kupenda na kutii ni agizo la Mungu

Mume hampendi mkewe kwa sababu ya uzuri wake pekee bali anatii agizo la Mungu la kumpenda asiyependeka, asiye na shukrani, na asiyekamilika aliyemchagulia kwa lengo la kumkamilisha ili asiendelee kuwa na mapungufu. Mke anatakiwa kumtii mumewe kwa utii ambao kanisa humtii Kristo. Kanisa hutii kila linaloagizwa na Kristo likiamini kuwa Kristo hawezi kuagiza kisichofaa au kisichotekelezeka. (Mithali 31:10-11) “Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.” Inahitaji karama kumtii binadamu mwenzako kwa kila jambo tena kwa kiwango unachomtii Mungu hasa ukizingatia huyo unayetakiwa kumpenda ana mapungufu kama yako. (Waefeso 5:24) “Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.” (Waefeso 5:22) “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.” Kimsingi wanandoa wote wawili wanatakiwa kupendana maana hata ule utii anaotakiwa mke kumfanyia mume wake unatokana na upendo kwa kuwa hata kanisa humtii Kristo kwa kuwa linampenda. (Yohana 14:15) “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”

Kupenda ni wito

Viapo wanavyopeana wanandoa siku ya ndoa vinapima na kuthibisha kama wanapendana. Wanandoa wasiopendana kwa dhati ndoa yao si halali na kudumu kwake ni kwa mashaka. Kupenda ni kujitolea kutumikia furaha ya mwingine kwa hiyari na bila manung'uniko. Ni kuwa tayari kumpenda, kumheshimu, kumfariji, na kumtunza mtu mmoja zaidi ya wengine wote na kubaki na huyo tu siku zote za uhai wako.  Kupenda kwa namna hii kunatokana na wito ambao mtu huupokea kutoka kwa Mungu wito ambao mtu atautolea hesabu siku ya mwisho. Unapompenda mtu huoni gharama kutumika kwa ajili yake wala huwezi kuhesabu mabaya anayokutendea. Pamoja na kuwa unayempenda lazima awe anakuvutia, bado sababu ya kumpenda inavuka mvuto wake. (Mwanzo 29:20) “Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda.”

Upendo huongeza thamani

Anayependa kwa upendo wa kimbingu hafanyi hivyo kwa matarajio ya kupokea kitu kutoka kwa mwenzie bali hufanya hivyo ili kumuongezea thamani aliyeagizwa kumpenda. Upendo wa wanandoa unafanana na upendo wa Ruthu kwa mama mkwe wake ambaye alikuwa mtu wa kabila jingine na ambaye hakutarajia kunufaika naye kwa lolote kwa kuwa alikuwa maskini na asiye na mtoto wa kiume ambaye angetarajia kuolewa naye. (Ruthu 1:16-17) “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.”

Majukumu ya mume

Kando ya upendo na utii unaowapasa wanandoa pia yapo majukumu yampasayo mume na mke. (Mwanzo 3:17-19) “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; [kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Mume ana jukumu la kuilisha na kuitunza familia yake. (Waefeso 5:28-29) “Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.”

Majukumu ya mke

Mke ndiye hubeba ujauzito kwa miezi tisa na kujifungua kwa uchungu na mateso mengi. Pale kujifungua kwa kawaida kunapokosekana hulazimika kufanyiwa upasuaji ambao kwa wengine huishia katika kupoteza maisha yao au ya mtoto au ya wote wawili. (Mwanzo 3:16) “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Pamoja na jukumu la kuzaa, kuelimisha Watoto, kusimamia shughuli za nyumbani na kumshauri mumewe, mke analo jukumu la kuchangia mapato ya nyumbani. (Mwanzo 31:16) “Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.”

Msaidie mwenzako majukumu

Katika ndoa ya wanaopendana majukumu ya mume huweza kufanywa na mke na baadhi ya majukumu ya mke huweza kufanywa na mume. Hiyo itatokana na kuelemewa majukumu kwa mwenzako ama kuwepo kwa uzembe na ujeuri kwa mwenzako. Kushindana au kukomoana hakuwezi kuisaidia familia bali kunaididimiza. (1 Samweli 25:3) “Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.”

Betisheba alijibebesha najukumu ya mumewe na kumkabili mfalme Daudi kwa ujasiri na hekima ya kimbingu. (1 Samweli 25:23-25)  “Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.”

Ambataneni

Kuambatana na kuwa Pamoja daima mkiwa na nia moja na kila mmoja akihudumia furaha ya mwenzake. Zaburi 133:1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Usiridhike kutembea bila mwenzako, kula bila mwenzako, kulala bila mwenzako. Mume na mke wanatakiwa kuishi kama Watoto mapacha mkichekeshana, mkongeleshana, hata kutaniana, huku mkifanya michezo yenu ya kushikana shikana. (Mwanzo 26:8) “Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe.” Msiruhusu Watoto, ndugu na rafiki wapunguze ukaribu wenu, kaeni Pamoja mkiwa kanisani, ndani ya basi, na kwenye matukio ambayo mmealikwa.

Sifianeni kukuza upendo

Kazi ya mwanaume ni kusifu uzuri wa mwanamke na kumpa majina yanayobeba sifa hizo. Usione aibu kumwita mkeo baby, au honey, au Sweet, au barafu ya moyo, au nyongo mkalia maini. Wanawake kwa asili wanapenda kusifiwa. (Mithali 31:29) “Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.” Msifie mumeo au mkeo mbele ya watu wa nyumbani mwako hata mbele ya wakwe na mawifi ukielezea mazuri anayokutendea. Katika wakati wenu wa faragha na hata mbele ya watu mara kadhaa msifie mwenzio ili mwenzako ajisikie vizuri. Hakikisha sifa zako zinakuwa za kweli ambazo hazina unafiki ndani yake. Mtambulishe kwa marafiki kwa Fahari kubwa ukimuita yale majina yenu mnayoitana nyumbani.

Sifa za Sulemani

Sulemani alikuwa na namna ya kumsifu mke wake. (Wimbo Ulio Bora 4:1-5) “Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua, Nyuma ya barakoa yako. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi. Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya, Wakipanda kutoka kuoshwa, Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati ya o.Midomo yako ni kama uzi mwekundu, Na kinywa chako ni kizuri; Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, Uliojengwa pa kuwekea silaha; Ngao elfu zimetungikwa juu yake, Zote ni ngao za mashujaa. Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Nyuma ya barakoa yako. Ambao ni mapacha ya paa; Wakilisha penye nyinyoro.”

Maneno mabaya yasitoke vinywani

Ndoa inahitaji kupaliliwa kwa maneno matamu ya kupongezana, kutiana shime, na kushiriki maumivu na kuonyesha staha. (Waefeso 4:29) “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.” (Wakolosai 4:6) “Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” Wataalamu wa mawasiliano wanapendekeza maneno Matano kama maneno yaliyojaa neema. Haya yasikosekane katika mazungumzo yenu ya kila siku. Maneno hayo ni NAKUPENDA, ASANTE, POLE, SAMAHANI, NAOMBA. Maneno hayo yakitolewa katika mkao sahihi wa sauti, na katika lugha sahihi ya mwili huzuia magomvi na kuponya maumivu kirahisi na kwa mafanikio makubwa.

Dumisheni amani nyumbani

Hakikisheni mianya yote inayoweza kuharibu amani yenu nyumbani imezibwa. Kumbukeni shetani hafurahishwi kuona nyumba zikiwa na amani. (Waebrania 12:14-15) Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.” Gharama ya kuirejesha amani ni kubwa kuliko kuzuia isipotee. (Mithali 25:24) “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.”

Msigombane

Nyumbani ndiyo mahali bora ambapo wanafamilia wote hupfurahia. Msipendelee kugombana kwenye familia yenu paonekane kama kilabu ya pombe au kituo cha polisi. (Waefeso 4:31) “Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” Ugomvi hutokea kutokana na kutofautiana misimamo au kuhisi kuwa unaonewa, unadharauliwa, au unadhulumiwa haki yako jambo ambalo haupo tayari kulikubali. Hali hiyo inaibua hasira na uwezo wa kujitawala au kufanya maamuzi sahihi unapotea. (2 Timotheo 2:24-26) Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.” Hasira ni zawadi tuliyopewa na Mungu ambayo huleta matokeo bora inapotumika vizuri. (Waefeso 4:26) “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” (Wakolosai 3:19) “Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.”

Zuieni magomvi nyumbani

Ili nyumbani pafae kuwa kituo cha uinjilisti na taasisi imara ya kiuchumi panapaswa kudumisha utengamano na amani. Amani huja kwa kuhakikisha haj ana haki za kila mwanafamilia zinasikilizwa na kutimizwa kwa kadri itakavyowezekana. Kusameheana kufanyike jambo la kawaida sana mtu anapokiri kukosea au kughafilika. Maneno ya kuudhi au yasiyo ya kiungwana yanayotolewa kwa lengo la kumuumiza mwenzako yasitolewe na mwanafamilia yeyote hata wazazi. Jizuie kumtukania mwenzi wako mama yake au baba yake au kusema ulemavu au udhaifu ulio nyumbani kwao. Hata kama mmetofautiana kiasi gani jizueni kutukanana. Tabia ya kutukanana imepitwa na wakati. Watu wastaarabu huwa hawatukanani. Tusi au neno liumizalo huchochea ghadhabu. (Mithali 15:1) “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.”

Kugombana kunaondoa ufahamu

Ghadhabu au hasira huchochea ugomvi. Mtu mwenye hasira huhisi kuonewa, na kudharauliwa na ili kuikataa hali hiyo hupandisha hasira. Hasira ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenyewe ana hasira. Tofauti ya hasira ya Mungu na mwanadamu ni kuwa ya Mungu ina busara ndani yake kuliko ya mwanadamu.  (Mwanzo 49:7) “Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali, Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma. Nitawagawa katika Yakobo, Nitawatawanya katika Israeli.” Mwanadamu akishikwa na hasira ufahamu wake unashuka viwango. Unapokabiliana na mtu mwenye hasira hatua ya kwanza ni kushusha hasira yake. (2 Timotheo 2:25-26) “Akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”

Pima kauli kabla ya kutamka

Usiwe mwepesi wa kusema kila unachokijua bali jua kile unachotamka na matokeo yake. Vita nyingi za matumizi ya silaha kali kali na zinazogharimu mali na Maisha ya watu zilitokana na maneno yaliyotolewa bila kupima athari zake. (1 Samweli 25:10) “Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake!” (1 Samweli 25:21-22) “Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.” Mwombe Mungu akusaidie kuzuia maneno yanayoweza kuharibu amani na kuahirisha hasira. (Zaburi 141:3) “Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.” (Isaya 48:9) “Kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.”

Pima kauli yako kabla yakujibu

Ugomvi unaamuliwa na mwenye kujibu kauli. (Mithali 26:20) “Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma.” Halikadhalika neno la kuumiza linapokutana na jibu la upole hupoteza nguvu yake na ugomvi huzuiwa. (Mithali 15:1) “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.” Na wakati mwingine ili kumpa muda wa kutafakari kauli yake usiwe mwepesi wa kujibu lolote. (Mithali 11:12) “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.” (Mithali 17:28) “Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.” (Marko 15:4) “Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki!”

Vikao vya usuluhishi

Vikao vya usuluhishi vinahitajika mapema sana baada tu ya kutofautiana. Usuluhishi kwa kadri itakavyowezekana ufanywe na wawili waliokosana badala ya kushirikisha watu wengi. Usiwe na mazoea ya kupeleka kwa mjumbe au kiongozi wa dini, kila aina ya ugomvi unaotokea. Jaribuni kuyasuluhisha mambo hayo ninyi wenyewe mkitegemea hekima ya Mungu naye atawasaidia. (Waefeso 4:26) “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka.” Makosa yanapodundulizwa kuna hatari ya kushindwa kuyasuluhisha siku yatakapojadiliwa. Hata hivyo usuluhishi huo ufanyike wakati ninyi wote mkiwa mmetulia na si wakati ambao kila mmoja au mmoja wenu ana hasira. (Wagalatia 6:1) “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.”

Msuluhishi awasaidie kuona hatari

Lakini kama mmeshindwa kufikiwa muafaka mwalikeni mtu mnayemwamini awasimamie. Msuluhishi hatakiwi kuegemea upande mmoja na kile anachofanya siyo kuwaamulia njia ya kutatua tatizo au kumtambulisha mwenye makosa bali kuwasaidia kuona namna ambavyo wangeweza kuepuka mgogoro usitokee na kuwauliza wanapendekeza nini kifanyike. Msuluhishi atumie muda wa kutosha kusikiliza kuliko kuongea ili abaini mapema tatizo lilipo. Awaoneshe hatari za kuendelea na mgogoro na kuwathibitishia kuwa tatizo lao siyo jipya katika maswala ya ndoa na kwamba wasidhanie kutofautiana kwao siyo ishara kuwa Mungu hakupanga waishi Pamoja kama mume na mke. Awasaidie kuzingatia kusema yote yaliyojiri kwa lugha ya kiungwana isiyo na lengo la kumdhalilisha mwingine.

Kukiri makosa kunakomesha magomvi

Kama utakuwa bingwa wa kusukumia wengine makosa yako hiyo haitakuletea amani ya kweli. Utakanusha, kwa viapo na ushahidi bandia na kufanikiwa kushawishi watu lakini amani ya moyoni itakosekana. Na kukosekana huko kwa amani kutakufanya ufanye makosa mengi zaidi na kukosana na watu wengi zaidi. Njia sahihi ni kutafuta amani ya moyoni kwa njia ya toba ya kweli. (Zaburi 32:1-2) “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.” Mungu anatutaka tuwe na amani na watu wote. Huwezi kuwa na amani moyoni kama huna amani na wenzako.  (Warumi 12:18) “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.”

Kusamehe kunarahisishwa na namna upande uliokosea unavyokiri kosa na kuomba kuhurumiwa. Lakini kusamehewa si lazima kutokane na na namna upande wa pili unavyolipokea kosa. Kusamehe kunaweza kunatangulia hata kabla upande wa pili haujakiri kosa. Yesu alipowasamehe waliokuwa wakimsulubisha hakufanya hivyo kwa sababu wakosaji walionyesha toba kwa makosa yao.

Kusamehe dawa ya magomvi

Ni kweli kuwa mawasiliano na mahusiano mabaya yamechangia kuondoa amani nyumbani. Lakini sababu ya msingi ya kukosekana kwa mahusiano na mawasiliano mazuri nyumbani ni kukosekana kwa roho ya msamaha. Yesu anapendekeza kwetu. (Luka 17:3-4) “Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” Amani ya kweli haiwezi kuwepo mioyoni mwa watu wasiosamehe.

Msamaha ni kwa faida ya anayesamehe

Kusamehe kwa sehemu kubwa kunaleta nafuu na msaada kwa yule anayesamehe kabla hakujaleta nafuu kwa anayesamehewa. Kusamehe kunadhihirisha kuwepo kwa moyo mkuu unaoweza kutawala hisia. Wengine kwa kukosa kusamehe wamejikuta wakitenda makosa ya jinai ya kuua, kupiga, kutukana na hata kupeana talaka. Talaka haitatui tatizo bali inalikuza na kuwaingiza kwenye shida na mgogoro wasiohusika na ugomvi huo yaani watoto.

Taasisi imara ya kiuchumi

Ndoa ilikusudiwa iwe taasisi imara ya kiuchumi. Hali ya Uchumi yaweza kuwa imara Ikiwa kutakuwako masikilizano. Mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa na kuafikiwa mapema ni mambo yahusuyo pesa. Pesa ni kitu kinachoweza kuleta furaha au huzuni kutegemeana na kiwango chenu cha kumuelewa Mungu. Biblia inatuthibitishia kuwa fedha ni mbaraka inapotumiwa vyema na mpango wa Mungu katika ndoa ni kutufanikisha kiuchumi. (Mhubiri 10:19) “Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, Na divai huyafurahisha maisha; Na fedha huleta jawabu la mambo yote.” (2 Wakorintho 9:8) “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.” Lakini tofauti na mtazamo wa wengi katika kizazi hiki Mungu hupitishia utajiri na baraka zake kwa njia ya kazi za mikono yetu. (Waefeso 4:28) “Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.”

Mke na mafanikio ya familia

Mke amebeba baraka za familia na anapotendewa isivyostahili huwa sababu ya kuwepo kwa myumbo wa kiuchumi na kukosekana kwa utengamano nyumbani. (1 Petro 3:7) “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” Mungu anaweza kuzuia baraka zote Ikiwa mke ananyanyasika. Mke anayepewa heshima na mumewe hujisikia kuwa salama na usalama na kupendwa ndicho kitu cha kwanza anachokihitaji mwanamke kutoka kwa mumewe. Mume asiwe na mashaka na mkewe au kuwa na wivu unaopitiliza. Mume anayemwamini mke wake humfanya mkewe kujiamini zaidi na kufanya shughuli zake kwa uhuru na mafanikio makubwa. “Mithali 31:10-11) “Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.”

Mgawanyo wa kazi

Mama wa nyumbani ana mchango sawa na yule afanyaye kazi za kujiriwa au za kujiajiri. Hata hivyo mama asiridhike kufanya kazi moja tu. (Mithali 31:13) “Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.” (Mithali 31:19) “Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.” (Mithali 31:22) “Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.” (Mithali 31:24) “Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.” (Mithali 14:23) “Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.” (Tito 1:11) “Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.” Je kuna kazi ambazo Mkristo hapaswi kuzifanya hata kama zinamletea mapato? Je, kuuza baa, kuuza majeneza, na udalali? Je inafaa mke afanye biashara zinazomfanya asafari mara kwa mara?

Je ni lazima kujua pato la mwenzako?

Wanandoa wanaopendana kwa dhati watajulishana mapato yao na miradi yao waliyoifungua na mahali ilipo. (2 Wafalme 4:9-10) “Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.” Ili kuepuka kuwa na matumizi ya hovyo wanandoa watapanga bajeti Pamoja na kuchagua mmojawapo kuwa mtunzaji wa fedha. Mtunzaji wa fedha awe ni yule mwenye nidhamu ya pesa.

Je ni halali kutomshirikisha mkeo mapato?

Mke na Watoto wana haki ya kunufaika na mapato ya kazi ya baba wa familia au kwa kazi waliyofanya kwa pamoja kama familia. (Mithali 31:20-31) “Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa. Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.” (Mithali 31:11) “Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.”Siri ya mafanikio ya kiuchumi ni kupanua vyanzo na wigo wa mapato na kubana matumizi yasiyo ya lazima. Siri nyingine ya mafanikio ya kiuchumi ni kuongeza maarifa na vitendea kazi vya kurahisisha uzalishaji wa huduma au bidhaa.

Je ni sahihi kwa mke kusaidia mahitaji ya nyumbani kwa mapato yake?

Mke mwenye upendo wa kweli anao wajibu wa kusaidia mahitaji ya nyumbani kwake kwa kununua vitu vyenye gharama nafuu na vitu vyenye gharama kubwa kutegemeana na kipato chake. (Mithali 31:27) “Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.” (Mithali 31:16) “Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.” Mume asibweteke kwa sababu amepata mke anayemsaidia kwa kuwa huo ni wajibu wake yeye aliye kichwa cha familia.

Je ni sahihi kutomshirikisha Mungu kwenye mapato ya familia?

Familia nyingi zilizofanikiwa kiuchumi zimekiri kuwa kumshirikisha Mungu katika mipangokazi yao na kumshirikisha katika mgawanyo wa mapato yao imekuwa siri kubwa ya mafanikio yao. (Kumbukumbu la Torati 8:18) “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.” Yakobo alikuwa na mpangokazi wake alioukabidhi kwa Mungu ambapo aliahidi kutolea Mungu moja ya kumi ya mapato yake endapo kama angemfanikisha. (Mwanzo 28:20-22) “Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

Je kusaidia wahitaji kunatajirisha?

Kusaidia wahitaji na kuitegemeza kazi ya Mungu huongezea mibaraka kwa familia. (Luka 6:38) “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” (Mithali 31:20-21) “Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake. Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.” Jambo la kuzingatia ni kuhakikisha ukarimu huo unatendwa kwa moyo mkunjufu bila kuwaumbua waliosaidiwa. (2 Wakorintho 9:7) “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.”

Kuachana huleta maumivu

Moja ya vitu vilivyozoeleka sana leo kwa wanadamu na ambacho Mungu anakichukia  sana ni talaka. (Malaki 2:16) “Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.” Kuachana ni jambo lenye maumivu makali kwa sababu waliooana walipoambatana walishikamana kama karatasi mbili zinazounganishwa kwa gundi ya maji. Baada ya kukauka huwa vigumu kuzitenganisha bila kusababisha madhara pande zote. Hivyo ndivyo walivyoachana wanavyopitia maumivu.

Msitafute mabaya kwa mwenzako

Matatizo mengi ndani ya nyumba huja pale mnapotafuta mabaya kutoka kwa mwenzako. (Mithali 17:13) “Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.” Usitafute mabaya ya mwenzako kwa nia ya kumuumbua, kumkejeli au kumkosesha amani. Usitafute kujua kama nyuki wanauma kwa kuwarushia mawe kwenye mzinga. Kupenda kunahitaji nidhamu. Kupendana kunaendana na kustahiana. (Waefeso 5:33) “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.” Mnapokuza mambo mazuri yale mabaya hutafuta mlango wa kutokea.

Msinuniane wala kuzira

Usitunze uchungu moyoni kwa mambo mliyokoseana. Wala usipange kulipiza kisasi kwa kununa au kuzira kutoa huduma inayohitajika au kuzira kupokea huduma iliyotolewa. Maandiko yanakataza wanaume kuwa na uchungu na wake zao. (Wakolosai 3:19) “Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.” Usiwe na donge limekukaa tangu asubuhi hadi jioni. Tabia ya kununiana na kutosemeshana kati ya wanandoa inakuza ugomvi ambao kama ungemalizwa mapema na kwa hekima ingewaacha huru. Mnapofanya hivyo mnamkaribisha shetani katikati yenu.

Mkaribisheni Yesu

Ndoa na familia nyingi zinaathiriwa na magomvi ya mara kwa mara. Magomvi hayo huweza kufikia kiwango cha kutovumilika. Na inapofikia hali hiyo kutengana kwa muda kunaweza kuwa suluhisho. Hata hivyo suluhisho la kudumu ni kukaa chini na kuondoa tofauti. Sababu kubwa ya kuwepo kwa migogoro ni kumfungia nje yeye aliye mwanzilishi wa ndoa. Njia sahihi ya kuondoa tofauti hizo ni kumkaribisha Yesu mioyoni mwetu.  (Yohana 15:5) “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” Zamani kulikuwa na maandishi unayoyakuta katika nyumba nyingi yenye maneno, YESU NDIYE MKUU WA NYUMBA HII, MSIKILIZAJI WA MAZUNGUMZO YETU. Maandishi hayo yalienda wapi?

Rasimisheni ndoa zenu

Unapoanza na Mungu kwenye maisha ya ndoa mibaraka yake huwa tele nyumbani. Wale ambao mlitoroshana na mnaendelea kuishi bila ndoa nawashauri mkabariki ndoa zenu au kama vipi mkafungie serikalini ili zitambuliwe kisheria. Wengine mnaishi bila ndoa na bila ridhaa ya wazazi. Hiyo ni mbaya zaidi. Unatarajiaje kunyookewa na maisha wakati mnaishi kwa kificho kiasi hicho? Wale mnaoishi bila (ridhaa) kujitambulisha kwa wazazi nawashauri hebu nendeni mkawaone wazazi mpate baraka zao.

Msiishi kwa majaribio

Kuishi kama watu mnaofanya majaribio kwenye ndoa ni jambo lisilofaa kabisa. Moja ya matatizo ya kisheria utakayoyapata (hasa wewe mwanamke) siku mumeo atakapofariki utakuwa na wakati mgumu kuwashawishi ndugu wa marehemu kuwa wewe ni mjane na mrithi halali wa mali na watoto. Hata wale waliofunga ndoa zao serikalini kanisa linawapa fursa ya kuja kubariki ndoa hizo kanisani. Na kwa wale walioanza kuishi pamoja bila cheti cha ndoa nao wanaalikwa kuja kubariki ndoa zao na kuzirasimisha kwa kuwapatia cheti cha ndoa kinachotambulika kisheria.

Imarisheni mambo ya kiroho

Ili Mungu aendelee kukaa na wewe uliye kwenye ndoa, ni lazima umtengenezee mazingira ya kumwalika. Someni Neno lake pamoja. Ombeni mnapoamka na mnapolala na wakati wa chakula. Tengeni muda wa kufanya kazi ya Mungu kwa kutembelea majirani zenu na kujifunza nao kile ukijuacho kuhusu Mungu. Muwe mawakili wema kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kutumia vema wakati, na kuitegemeza kazi ya Mungu kwa mali zako, talanta zako, na muda wako, na mwisho kuhudhuria kwa uaminifu semina na mikutano ya kiroho.

Ombeni pamoja

Kuomba pamoja huweza kutatua changamoto za ndoa katika hatua ya awali. Kwenye maombi yenu msionyeshe kushindani au roho ya kujihesabia haki. Wafilipi 4:6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Yakobo 5:16 Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.

Shuhudieni pamoja

Kusaidia wengine kulielewa Neno la Mungu huweza kuondoa roho ya ugomvi. Muda unaotumia kujifunza Neno unaimarisha hali yako ya kiroho. (Matendo ya Mitume 18:26-28) “Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.” Matendo ya Mitume 17:11 Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. (Matendo 16:30-34) “Kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.”

Zoezi la kuambatana

Mungu alikusudia kuwe na matukio kadhaa yanayowaweka karibu wanandoa ili iwe kinga yao kwa mashambulizi ya adui. Ili kuimarisha kuambatana inashauriwa kuwepo siku ya kutambua huduma ya baba, huduma ya mama, huduma, ya Watoto, na huduma ya mfanyakazi wa nyumbani. Siku hiyo zawadi iandaliwe na kila mmoja atoe ushuhuda alivyobarikiwa na mhusika. Pale itakapowezeka majirani waalikwe kwenye tukio hilo litakaloandamana na mlo wa Pamoja ambapo mhusika atakuwa anawahudumia watu akiwa kwenye vazi la mpishi. (Mithali 31:29) “Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.”

Tundikeni picha yenu ukutani

Picha kubwa ya ndoa yenu iwepo sebuleni kila siku ikiwakumbusha mlivyounganishwa na ifikapo tarehe mliyofunga ndoa mfanye sherehe ya kujipongeza mkibandika picha za ndoa yenu sebuleni na kujikumbusha matukio kadhaa ya siku hiyo. Mtafanya hivyo siku ya kumbukizi ya kuzaliwa. Kwenye kumbukizi ya ndoa mwaweza kuwa na mtoko ambapo mtabeba chakula chenu na Kwenda kukilia sehemu tulivu huku mkiangalia uumbaji wa Mungu.

Ambatana na mwenzio

Ambatana na mwenzio kila inapowezekana hasa kwenye matukio ambayo wanandoa wamealikwa na muwe mnazungumza muda wote. Siku hizo vaeni mavazi yanayowatambulisha. Ukiitwa mbele kuwasalimu watu au kutoa maelezo Fulani nenda na mke wako. Ukiwa umealikwa kuendesha tukio fulani usisahau kumtambulisha mke wako. Ukipewa nafasi ya kuahidi jambo au kutoa shukrani mpatie hiyo nafasi mke wako. Kwa njia hiyo mtakuwa unaupalilia upendo wenu na Mungu atawafundisha kupendana. (1 Wathesalonike 4:9) “Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.”

Mungu anachukia kuachana

Kwa hali ilivyo kwenye ndoa leo inatia shaka kama upendo wa jinsi hii bado upo kwa kuwa viwango vya kuachana vinaongezeka. Kanisa ni lazima lifanye jitihada ili kupunguza kasi ya kuachana. (Malaki 2:16) “Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.” Hata hivyo kuachana kunaweza kuruhusiwa katika mazingira ambayo uhai wa mmojawapo upo hatarini, ama kuna tuhuma za uzinzi ambazo aliyetendwa ameshindwa kuzivumilia. (Mathayo 19:8) “Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.”