HAKI KWA IMANI
Haki kwa mani ni mpango au utaratibu wa Mungu wa kuwapatia haki wanadamu wasio na haki kwa kuwalipia adhabu ya mauti ya milele waliyoistahili, kuwarejeshea uwezo wa kutenda mema walioupoteza, na kuwarejeshea utukufu walioupoteza baada ya anguko la dhambi. Hii ndiyo haki ambayo Kristo aliwahimiza watu wote kuitafuta kwa bidii. (Mathayo 6:33) “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Wanufaikaji wakubwa wa haki hii ni wale wanaojitambua jinsi wasivyostahili na adui wakubwa wa haki hii ni wale wasiokubali kiurahisi hali yao ya dhambi. (Mathayo 9:13) “Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Yesu pekee ndiye aliye mwenye haki kwa kuwa Yeye hajawahi kutenda dhambi. (1 Petro 2:22) “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.” (Mathayo 27:19) “Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake.” (Mathayo 27:24) “Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.”
Wanadamu wengine wote huitwa wenye haki kutokana na haki waipokeayo kutoka kwa Kristo. (Warumi 3:10) “Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja.” (Warumi 3:26) “Apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.” (Wafilipi 3:9) “Tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani.”
Utaratibu huu unakinzana kabisa na ule utaratibu mwingine unaopendelewa na wanadamu wa kujipatia haki kutokana na jitihada za kibinadamu ambao badala ya kumtukuza Mungu unamtukuza mwanadamu anayeubuni na kutekeleza mpango wenyewe. Hii ndiyo haki waliyoifuata Waandishi na Mfarisayo ambayo Yesu aliikemea sana. (Mathayo 5:20) “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” (Warumi 10:3) “Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.”
Fundisho la haki kwa imani limepata ugumu wa kueleweka kutokana na kuzidiwa nguvu na dhana ya kujihesabia haki liyoibuliwa na kubuniwa baada ya mwanadamu kutenda dhambi kwenye bustani ya Edeni. Baada ya anguko la dhambi mwanadamu (1) alipoteza uwezo wa kutenda mema (2) alipoteza uwezo wa kuitambua hali yake ya dhambi (3) alijihesabia haki juu ya sababu sahihi za kuwepo kwa hali hiyo na (4) alijibunia njia ya kuondokana na hali hiyo.
(Mwanzo 3:7-12) “Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo. Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Dhambi inapofusha macho mtu asione makosa yake au asione ukubwa wa makosa yake. Upofu huo huja pale mtu anapoamua kujitoa ufahamu au kujizima data baada ya dhamira yake kumshitaki kuwa yu mwenye hatia. Mtu atendapo dhambi dhamira yake humpa taarifa juu ya kosa lililofanyika na matokeo yake na hivyo kumuondolea amani. (Zaburi 38:1-7) “Ee Bwana, usinilaumu katika ghadhabu yako, Wala usiniadhibu kwa ukali wa hasira yako. Kwa maana mishale yako imenichoma, Na mkono wako umenipata. Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu. Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno. Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu. Nimepindika na kuinama sana, Mchana kutwa nimekwenda nikihuzunika. Maana viuno vyangu vimejaa homa, Wala hamna uzima katika mwili wangu.”
Hatia moyoni huleta maumivu kama ya mshale unaochoma. Wakati mtu anapohisi hatia moyoni Mungu hufanya bidii kumshawishi mtu huyo atubu na kuungama dhambi yake kama njia sahihi ya kuondokana na hali hiyo. (Warumi 4:7-8) “Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.” Huwezi kusitiriwa dhambi kwa kuikanusha au kwa kusukumia sababu za kuwepo kwake kwa watu wengine huku wewe ukijiweka mbali na uhusika kama alivyofanya Adamu na kama wafanyavyo watu wengi. Mtunga Zaburi anatambua umuhimu wa kuungama na kutubia dhambi ili kuondokana na hatia moyoni. (Zaburi 51:1-4) “Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu. Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima. Nimekutenda dhambi Wewe peke yako, Na kufanya maovu mbele za macho yako. Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo, Na kuwa safi utoapo hukumu.”
Ujasiri huu wa kuungama na kutubu dhambi hauji kwa juhudi au kwa akili za kibinadamu. Ni uwezo utolewao na Mungu kwa yeyote mwenye kutambua wema wa Mungu kwake. (Matendo ya Mitume 5:30-31) “Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.” (Warumi 2:4) “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?” uwezo wa kutubu ni zawadi itokayo kwa Mungu. Adamu hakupaswa kumfikiria na kumlaumu Mungu kuwa ndiye aliyemsababishia kufanya dhambi kwa kuwa eti alimletea mke aliyemshawishi kufanya dhambi.
Wema uwavutao wenye dhambi kutubu
Upo wema uwavutao wenye dhambi kutubu. Huu ndiyo wema uliomvuta Mwana mpotevu kutubu na kurudi kwa baba yake. Mwana Mpotevu alipotafakari wema wa baba yake ndipo alipopata ujasiri wa kwenda kuungama na kutubu dhambi zake. (Luka 15:17-19) “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.”
HAKI NI NINI
Haki ni kiwango kinachomfanya mtu kustahili. Mfano ili mtu astaili kumwona Mungu anapaswa kufikiwa viwango vya utakatifu vilivyowekwa. (Waebrania 12:14) “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao.” Hali kadhalika kuingia uzimani kunahitaji mtu awe katika kiwango cha haki kinachokubalika. (Mathayo 25:46) “Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.” Kwa hiyo hapo tumeona wenye haki wana stahili zao na wasio na haki nao wana stahili zao. Stahili za wenye haki ni kutuzwa zawadi njema na stahili ya wasio na haki ni kupewa adhabu.
MWENYE HAKI NI NANI?
Kwa tafsiri ya Nehemia mwenye haki ni yule aliyetenda yaliyo kweli na yaliyo mema. (Nehemia 9:33) “Lakini wewe u mwenye haki, katika hayo yote yaliyotupata; maana wewe umetenda yaliyo kweli, lakini sisi tumetenda yaliyo mabaya.” (Mwanzo 4:6-7) “Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Kwa hiyo namna pekee ya kutambuliwa kama u mwenye haki ni kutenda mema yaliyoagizwa kwa ukamilifu. Unapotafakari hali ya mwanadamu hasa kuhusiana na kutii maagizo ya Mungu unagundua kuna mapungufu makubwa katika kufikia kiwango cha haki ambacho ni utakatifu. Kama kuwa na haki ni kuwa na kiwango cha utakatifu alichonacho Mungu mwandishi wa kitabu cha Ayubu anaona huo kama mlima mrefu usiweza kupandwa. (Ayubu 9:2) “Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?”
MWANADAMU AWEZA KUWA MWENYE HAKI?
Ugumu huu wa mwanadamu kuweza kutenda mema na hivyo kufikia kiwango cha utakatifu unaohitajika unatokana na asili ya uovu aliyonayo mwanadamu mwenyewe. (Ayubu 15:14) Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki? (Zaburi 53:3) “Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.” (Mhubiri 7:20) “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.” (Yeremia 13:23) “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”
KUHESABIWA HAKI KUNAFANYIKAJE?
Kuhesabiwa haki ni jitihada za Mungu za kumkomboa mwanadamu asiyeweza kujikomboa kutoka kwenye shimo aliloHaki kwa Imani hutekelezwa kupitia awamu tatu zijulikanazo kama kuhesabiwa haki, kutakaswa na kutukuzwa. Wakati mwingine awamu hizi tatu huwekwa katika makundi ya awamu mbili kuu ambazo ni kuhesabiwa haki na kutakaswa.
KUHESABIWA HAKI
Kuhesabiwa haki kunakofanywa na Mungu kwa mwanadamu kunatokana na kushindwa kwa jitihada za mwanadamu za kujihesabia haki. Mwanadamu alipoanguka dhambini alidanganyika kudhani bado anao uwezo wa kutenda mema. Uwezo huo ulikuwa umeondoka kama ulivyokuwa umeondoka uwezo wa Samsoni. (Waamuzi 16:18-21) “Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”
Kuendelea kulazimisha kutenda matendo mema ya haki wakati uwezo wenyewe wa kutenda mema umeondoka ni kujichosha ambako huishia kuzalisha matendo yasiyokubalika yaliyo chini ya kiwango. (Isaya 64:6) “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.” Matendo ya mwanadamu hayakubaliki kwa sababu yamezalishwa na mwili uliopotoka ndiyo maana yanaitwa matendo ya mwili. Wayafanyao matendo hayo yasiyotokana na Roho Mtakatifu wanaitwa watu wa mwilini. (1 Wakorintho 3:1-4) “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu?”
Matendo yawezayo kumpatia mtu haki ni lazima yawe yametendwa na mtu wa rohoni. Mtu wa rohoni ni yule ambaye licha ya kuwa na asili ya mwanadamu amepokea uwezo kutoka kwa Mungu wa kuzalisha matendo mema yawezayo kumpatia haki mbele za Mungu na hata kuwapatia haki wengine wasioweza kufikia viwango vyake. (Yohana 1:12-14) “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Tito 3:4-7) “Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.”