Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

MARAFIKI WA YESU

MARAFIKI WA YESU KRISTO

Hakuna mtu mwenye hasara kama yule ambaye hajamfanya Yesu kuwa rafiki yake. Yesu ndiye pekee mwenye urafiki wa kweli na wanadamu. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13). Yesu aliutoa uhai wake kwa jili ya rafiki zake. Kwa ajili yako na yangu. Ni kweli kuwa kipimo cha juu cha upendo wa kibinadamu kipo katika kutoa. Lakini kutoa kunapohusu uhai wa mtu huwa ni jaribu gumu zaidi. Yesu alithibitisha upendo wake kwa binadamu kwa kujitoa mwenyewe kuwa fidia ili sisi tusiangamie. “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.” (Yohana 10:11)

Yesu alitulipia deni la dhambi kwa kifo chake pale msalabani. Deni la dhambi lilikuwa kubwa kwetu kiasi cha kutoweza kulilipa. Mtume Yohana alifunuliwa jambo hilo katika njozi na alilia sana alipokosekana mtu wa kulilipa deni hilo. “Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama. Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.” (Ufunuo 5:4-5). Gharama yake haifananishwi na dhahabu wala fedha.  “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.” (1 Petro 1:18-19)

Ujio wa Yesu duniani takribani miaka 2,000 iliyopita ulikuwa kwa kusudi la kuja kulipa fidia hii kwa makosa yaliyotendwa na wanadamu ambayo adhabu yake ilikuwa ni mauti ya milele. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Marko 10:45). Alikuja kutuwekea dhamana na kutumikia adhabu yetu. Hakuona faida ya yeye kuwa mbali na rafiki zake. Ingawa alikuwa Mungu kwa vigezo vyote hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa kitu cha kumzuia asiwasaidie rafiki zake. “Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” (Wafilipi 2:6-8)

Adhabu ya mauti haikuwa rahisi maana ilikuwa inasimama badala ya mauti ya milele itakayowapata wanadamu wote watakaokataa kuokolewa – yaani kutengwa kabisa na uso wa Mungu. Ndiyo sababu Mtume Paulo anaiita mauti hiyo kuwa ni mauti kuu. “Aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa.” (2 Wakorintho 1:10). Aliyekuwa katika tukio lile asingedhani kuwa aliyekuwa anateswa na kuuawa alikuwa anafanya hivyo kwa makosa yasiyomhusu. “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” (Isaya 53:4-5)

Hakuwa katika hali ya kutamanika alipokuwa katika hatua za kutukomboa. Isaya anasema; “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.” (Isaya 53:2-3.) Maisha ya Yesu yalikuwa kama ya mtuhumiwa aliyehukumiwa kifo. Alikuwa na hakika kuwa maisha yake hapa duniani yatahitimishwa na kifo cha aibu cha kutundikwa msalabani na wale aliowaumba na aliokuja kuwakomboa.

Hali hiyo ya huzuni ilizidi kuongezeka kadri alivyokuwa anakaribia saa yake atakayotiwa mikononi mwa wauaji wake. Akiwa kwenye bustani ya Getsemane ambako wauaji wake walipanga kuja kumkamata na huku giza likiwa limeingia alisikika akiwaambia wanafunzi wake; “. . . Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.” (Mathayo 26:38)
Wakati mmoja alijaribiwa kufikiria kuahirisha mpango huu wa kulipa fidia ya wenye dhambi kwa kuomba utaratibu fulani ufanyike utakaokuwa mbadala wa ule uliopo wa kuwaokoa wanadamu. Adhabu ya wokovu wa wanadamu ilionekana kubwa mno kwake. “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.” (Marko 14:35). Jibu alilopewa kwa ombi hilo ni kuwa mpango huo hauwezi kubadilishwa kwa sababu ukibadilishwa mwanadamu ataangamia milele. Yesu hakustahimili kuona wanadamu wanaangamia. Alikubali kuendelea na mpango wa kutuokoa. Yesu alivumilia yote hayo kwa sababu alitupenda.

Yesu alikufa mahali pa kila mmoja wetu akipigiliwa misumari mikononi na miguuni. Alama hizo za misumari zitaendelea kubaki mwilini mwake katika umilele wote hata baada ya dhambi kutokomezwa kama ukumbusho wa gharama ya kuokolewa kwetu. Katika makazi yale ya kudumu ambako waliokombolewa wataishi na viumbe ambao hawajawahi kuanguka dhambini Yesu ataonekana tofauti kwa sababu ya makovu yake, na itasababisha maswali mengi kwa wale wasiokijua kisa hiki. “Na mtu atamwambia, Je! Jeraha hizi ulizo nazo kati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni jeraha nilizotiwa katika nyumba ya rafiki zangu.” (Zekaria 13:6). Yesu anajisikia fahari kubaki na alama hizo kwa kuwa zinatambulisha kuwa wanadamu waliokombolewa ni rafiki zake wa karibu sana. Amua kufanya urafiki na Yesu.

Kufanya urafiki na Yesu ni jambo muhimu tena ni la maana sana. Ni jambo la maana kwa kuwa Yesu si kama wale marafiki wengine wasioaminika, wanaoweza kukutelekeza. “. . . Kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.”  (Waebrania 13:5). Yesu ameahidi kuwa pamoja nasi hata mwisho. “. . . Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:20).

Lakini kumbuka watu wawili hawawezi kudumu katika mahusiano pasipo kupatana. “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? (Amosi 3:3) Nawe ili uwe rafiki wa Yesu unatakiwa kupatana naye. Kupatana na Yesu ni rahisi. Utatakiwa kuamini kila anachosema. “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.” (Yohana 15:14). Ibrahimu alikuwa rafiki wa Yesu. Alipoambiwa amtoe mwanawe wa pekee Isaka awe kafara hakusita bali alitii kwa imani. “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu. . .” (Waebrania 11:17). Marafiki wa Yesu huwa watii hata pale maagizo yanapokuwa magumu kuyatekeleza. Yesu mwenyewe amesema kuwa sisi hatuwezi lolote, bila msaada wake. “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” (Yohana 15:5) Anapotuagiza chochote anatupatia na uwezo wa kutii maagizo yake. Hivyo usisite kuja kwa Yesu kwa kuogopa maagizo yake. Yeye mwenyewe atarahisisha utii huo badala ya kuwa mzigo litakuwa jambo jepesi liletalo furaha. “. . . Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.” (Luka 18:27)

Njia bora ya kudumisha mahusiano yoyote yale ni kuwasiliana. Yesu ameweka utaratibu wa kuwasiliana na rafiki zake. “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” (Wafilipi 4:6). Yesu anataka rafiki zake wawasiliane naye bila kikwazo chochote. Ili kuwasiliana na Yesu huhitaji kujua lugha fulani maalumu. Mweleze haja yako kwa lugha yoyote haja hizo zitamfikia. Na kwa hiyo kipimoja cha kujua kuwa ulikuwa unawasiliana na Yesu ni pale ambapo baada ya kuomba unaweza kukumbuka haja ulizomweleza Yesu. Ukikuta baada ya maombi hujui ulikuwa unamwambia nini Yesu mawasiliano hayo hayakumfikia Yesu na hukuwa unataja haja yoyote. Wale wanaotaka kudumisha urafiki wao na Yesu ni lazima wazingatie agizo hili. Ni lazima wajue wameomba nini.

Yesu anataka utumie lugha ya mawasiliano inayotumika kuwasilisha hoja. “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” (Isaya 43:26). “Maombi si ugomvi bali ni mazungumzo kati ya marafiki wanaopendana. Yesu anasema; Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo”. (Isaya 41:21). Jambo la pili muhimu katika maombi ni imani. “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” (Waebrania 11:6). Kuna mambo amabyo Yesu yeye mwenyewe ametuahidi. Hivyo usioneshe hali ya kusita sita au mashaka unapomkumbusha mambo hayo. Amini kwamba atatenda. Yesu anasema; “Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.” (Marko 11:23).

Imani hukuzwa kwa kusoma Neno la Mungu. Kama huna mazoea ya kusoma Neno la Mungu anza sasa. Utashuhudia imani yako ikiongezeka. “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” (Warumi 10:17). Mashaka katika maombi ni kikwazo kikubwa sana cha kujibiwa maombi yako. “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.” (Yakobo 1:6-7)

Jambo jingine linaloweza kukukosesha Baraka zako kwa Mungu ni kuomba kwa kumtegemea mwanadamu mwenzako. “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” (1 Petro 5:6-7). Maandiko hapa yanatuambia hatuna sababu ya fadhaa zetu kuwatwisha wanadamu wenzetu. Yesu mwenyewe anatualika tumtwishe fadhaa zetu zote. Hakuna mwenye kujishughulisha na matatizo yetu zaidi ya Yesu. Wakati wa Agano la Kale dhambi zilikuwa zinamfikia Mungu kwa njia ya makuhani. Katika Agano Jipya Yesu mwenyewe aliye kuhani mkuu anazichukua dhambi zetu. Hatuhitaji mtu mwingine wa kati kati wa kutuombea kwa Mungu. “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu.” (1 Timotheo 2:5). Usimwambie mwanadamu mwenzako siri zako eti kwa madai kuwa anakuombea kwa Mungu. Wale wanaotaka kudumisha urafiki wao na Yesu ni lazima wazingatie agizo hili. Ni lazima wajue wanaomba kwa nani.

Jambo jingine muhimu katika kudumisha mawasiliano na Yesu ni kujua namna ya kuongea naye. “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” (Mathayo 6:5-6). Marafiki wanapozungumza hawapayuki. Kule kupayuka ni kama kutaka kujionesha au sifa. Unatafuta sifa ya nini? Mungu si kiziwi hadi umpigie kelele zote hizo. Mungu hapigiwi kelele. Kupiga kelele si dalili ya kumheshimu bali inapelekea kumvunjia heshima. “Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu?” (1 Wakorintho 14:23). Wale wanaotaka kudumisha urafiki wao na Yesu ni lazima wazingatie agizo hili. Ni lazima wajue kuongea kwa adabu na Mungu.
Tutakapokutana tena tutazidi kuangalia marafiki wa Yesu wanavyopasa kuwa. . . Mungu akubariki sana.