UONGOZI NA UKUAJI WA KANISA
Mungu alianzisha kanisa ili kiwe kituo cha kuzalisha watakaorithi ufalme wa mbinguni. Lengo ni kuwafikia watu wote. (Marko 16:15) “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.” Watakaokolewa watakuwa wengi kulingana na idadi ya malaika walioasi. (Luka 13:23-24) “Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.” (Ufunuo 7:9-10) “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.”
Mungu anasubiri tuifikie idadi hiyo kubwa ya watu. Idadi hiyo itatimia kwa kuzingatia ubora. Ubora kwa upande wa waumini unaotokana na ubora katika viongozi wanaowaongoza. Mungu hahitaji tu idadi kubwa bali anahitaji watu wenye ubora yaani (Quantity and Quality). Ili kupata watu wengi na wenye ubora anahitaji pia kupata viongozi wengi na wenye ubora. (Mathayo 9:37-38) “Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”
Watenda kazi wenye ubora hupatikana kutoka kwa Bwana kama ambavyo mke mwema mtu hupewa na Bwana. (Mithali 19:14) “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” Mungu alishawaandaa watu wa kuliongoza kanisa lake. Hawa ni watu wenye mapungufu lakini wanaofundishika na wenye kiu ya kujifunza. (Kutoka 18:17-18) “Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.” (Mathayo 16:23) “Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
Usikatae kazi ya Mungu. kukataa kazi kwako ni hasara. Ipokee na kumuomba Mungu akufundishe naye hatakuangusha. Jifunze kwa waliotangulia na wenye uzoefu huku ukijisomea vitabu na kuhudhuria semina. Unapokosolewa usikasirike wala kuzira. Mwombe Yesu ashushe kiburi chako. Jifunze kutambua silika na tabia za waumini wenzako ili kuepuka kukwazika. Wale wenye uzoefu wawaonee huruma wachanga na kuwaimarisha. (Luka 22:31-32) “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.
Kanisa ni lazima lipimwe ili kutambua kama linakua au la. (Marko 4:8) “Nyingine zikaanguka penye udongo ulio mzuri, zikazaa matunda, zikimea na kukua, na kuzaa, moja thelathini, moja sitini, na moja mia.” (Yohana 15:16) “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.”