Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

NGONO NDOA NA MAISHA YA UJANA

NGONO NA MAISHA YA UJANA

Elimu ya ngono ni muhimu sana kwa mtoto na watu wazima. Ningependa kushauri watu wazima wote wapate mwanga wa kufundisha somo hili kwa uzuri kabisa kulingana na mpango wa Muumbaji na kwa kulingana na ukweli uliofunuliwa tayari. Hapo ndipo tutaweza kuwasaidia watu, kwa kuwa wengi wameona aibu kufundisha yale ambayo Mungu anataka tuyaeleze inavyopasa. Shetani anataka kile ambacho Mungu alikitoa kwa ukarimu kwa mwanadamu kiwe kitu cha aibu na kiovu. Ngono ni zawadi ya Mungu iliyotolewa kwa wanandoa tu. Lakini mafundisho duni na ya uongo kuhusu ngono, yapo kwenye karibu kila kabila na jamii hapa duniani. Je, unayajua mafundisho ya ngono yaliyo mapokeo mazuri ya jamii yako? Unajua mafundisho ya barabarani ya kabila lako na yale yaliyo rasmi yanayohusu ngono? Tunadhani si vizuri mtoto wa chini ya umri wa miaka 18 kuanzisha urafiki wenye sura ya uchumba wa majaribio (Dating). Ni bora kuwe na uchumba wa wazi na wazazi wajulishwe. Moja ya hoja zinazotolewa kuhalalisha aina hii ya mahusiano ni kuwa vijana wanavutiwa na wenzao wa jinsia nyingine lakini wanalosahau ni kuwa Mungu aliweka hali hiyo ili nyumba zisimame na siyo njia ya kumfanya mtu kwenda dukani kumnunua mwenzake wa jinsia tofauti. Uchumba wa majaribio (Dating) ni kama mtu anayeenda dukani huku akiwa hana nia ya kununua bali kuangalia na kujaribisha. Hali hiyo huweza kuleta matokeo yasiyo mema, na wengine wanaweza wakakosa kueleweka na kukosa mtu ambaye angeoana nao baadaye.

WATOTO WAFUNDISHWE USAFI:

Nimesoma kitabu kizuri cha Josh Harris  kiitwacho “I Kissed Dating Goodbye” gharama ya kitabu hiki kwa watoto wetu ni kama dola moja kwa kilichotumika kwenye Internet. Kitabu kingine chenye ushauri juu ya kuachana na mazoea haya ya uchumba wa matazamio kinaitwa “Passion and Purity” kilichoandikwa na Elizabeth Elliot. Mara nyingi watoto wanakuwa na mihemko ambayo inakuwa shida kuimiliki. Mihemko ya watoto wa miaka 16 ni sawa na ile ya watu wazima, lakini je hawa watoto wanasaidiwaje? Uchumba wa majaribio siyo suluhisho. Watoto wetu wafundishwe usafi wa moyo, usafi wa mawazo na usafi wa matendo. Watoto wakiwa wadogo wazazi wanapaswa kuwafundisha mambo yanayoshabihiana na umri wao na kamwe wasitoe masomo ambayo ni juu ya kiwango chao. Watoto waangaliwe kwa makini wanapocheza peke yao michezo ya kujificha mashambani hasa kwenye mashamba ya mahindi. Hatuwezi kuacha watoto wawe pekee yao muda mrefu. Nilipofika Bunda niliona watoto waliokuja kucheza na watoto wetu na walikaa siku nzima na hakuna aliyewatafuta. Na wale watoto wadogo wa miaka minne mpaka sita, walianza kusema maneno machafu kwa wenzao wa miaka mitano. Kwa mfano yule mvulana alimwambia mtoto mwenzake wa kike wa miaka minne avue nguo.

WAZAZI TUWAFUNDISHE WATOTO WETU:
Watoto wana udadisi na ni sisi wazazi tunapaswa kuwafundisha vinginevyo wataenda kwingine kupata majibu. Utafiti unaonesha kuwa wakina baba wengi ni wazito kufundisha somo hili hata kwa vijana wao wa kiume. Na wengine wanapofundisha wanafundisha wakiwaambia vijana wao ni uhodari kutembea na msichana. Kwenye makambi watoto wangu wadogo wa kiume wa miaka tisa, walifuatwa na wasichana waliowaambia “tunataka uwe rafiki yetu wa kiume (boyfriend).” Bibi yao alikuwepo na kuwahimiza “Hivi ninyi hamtaki kuoa?” Rafiki yangu wa Afrika ya Kusini ana kijana wake wa miaka 12 anayehubiri vizuri. Wakitoka kwenye jukwaa anakuta na wanawake wanaomsubiri na maneno “Huyu ni binti yangu mchukue na umwoe nimekupa” wakiwa wanamaanisha kabisa wanachosema. Rafiki yangu alisema ilibidi nione aibu kwa kile wanawake wenzangu wanachokifanya cha kutaka kumwangusha mhubiri huyu kijana! Mambo yanayoonekana madogo madogo kama haya yanaweza kumwandama mtoto na kumfanya asishinde majaribu ya namna fulani maishani mwake. Nilikutana na mchungaji wa Kisabato aliyekuwa shoga (homosexual) na ambaye alioa tena baadaye. Kwenye tovuti yake anasema alianza tabia hiyo akiwa na miaka 3 huko mashambani akiwa na wafanyakazi wanaomsaidia baba yake. Aliendelea kukua na akaenda seminari, akaoa lakini bado akiwa anaendelea na tabia hii. Yeyé anashuhudia kuwa ingawa wengi wa walioathirika na tabia hii wanajitetea kuwa walizaliwa katika hali hiyo, bado wanaweza kuzaliwa mara ya Pili (even if we say we were born like this, we can be born again in Christ). Huduma yake inaitwa “Coming Out of Closet Ministry.”

WATOTO WA JINSIA TOFAUTI WATENGANISHWE:
Watoto wa jinsia ya kike na ya kiume wanapaswa kutenganishwa hata wakiwa kwenye umri wa miaka minne tu. Hali imekuwa mbaya sana siku hizi. Tumeshuhudia kwa macho yetu mambo ya kutisha yanayohusu watoto hivyo hatuwezi kuyafumbia macho tena. Ni kweli wote tumepungukiwa na utukufu wa Mungu ila hatuwezi kuacha watoto wakapata elimu hii kwa mtu mwingine bali kutoka kwetu wenyewe na baada ya kuhakikisha ni elimu inayotokana na Neno la Mungu. Wazazi wanapaswa kujivika kwa kujifunika vizuri hata wakiwa majumbani mwao maana inakuza heshima kwa watoto wao. Tusithubutu kuvaa nguo za kulalia mbele ya watoto wetu, huku tukitambua watoto wetu ni wakubwa. Ushauri mwingine ni kuwa watoto na wazazi wasilale pamoja, au kuoga pamoja. Niliona tukienda kuogelea kule shuleni Andrews watoto wangu wadogo wa miaka 9 walisema hatuendi tena kubadilisha nguo kule maana watu wazima wote wanatembea uchi bila nguo, na sisi watoto tunaogopa. Kweli si jambo jema mtu mzima wa miaka mingi inayofikia 50 aonwe utupu wake na watoto wadogo. Makanisa yetu yapaswa kufundisha mambo haya pia. Rafiki yangu wa San Francisco aliniambia taabu anayoipata na mgeni mmoja aliyemtembelea nyumbani kwake. Kwa kuwa maeneo ya huko yana matetemeko mengi, yanapotokea usiku mgeni huyo hutoka nje ya majengo bila hata ya nguo moja!

DHANA POTOFU ZIPIGWE VITA:
Mafundisho  mengine ya ngono hata yale yanayotolewa na  waumini wetu huwa ya kutisha sana.  Tumesikia baadhi yao kwa mfano wakisema kuwa kulala na aliye bikira kwa mwathirika wa UKIMWI kwaweza kumponya aliyeathirika na mengine mengi ambayo hatupendi kuyasema hapa wazi wazi. Ila utakaposoma tamaduni za zamani na za siku hizi, utagundua kuwa tendo la ndoa limehusianishwa na vitu vingi ambavyo Mungu hakuvisema. Mengi si ya kweli, japo yapo ambayo ni  kweli mfano tendo la ndoa wakati wa hedhi si kitu cha afya. Angalia kama mafundisho haya yanaendana na sayansi, usafi, afya, utu, na Maandiko. Mambo ya ngono yanahusiana sana na afya kwa namna nyingi kwa mfano uaminifu katika ndoa unalinda afya kwa namna nyingi. Mambo ya ngono yameleta vifo, magomvi na maradhi ya hisia, kujiua na kuuana. Tamaduni zingine pia zimeunganisha mambo ya ngono na ibada za giza. Naona kwenye magazeti na vitabu mambo mengi ya kutisha na nafikiri nawe ndugu msomaji umeyaona. Usiyarudie rudie mambo hayo kichwani mwako, bali ugeuze uso wako kwenye yaliyo bora. Hata kwenye Maandiko Matakatifu tunaona jinsi watu walivyokufa walipojihusisha na ibada za ngono. Siku moja walianguka watu 24,000 kwa ajili ya kujihusisha na ngono wakiwa na Nabii aliyeasi aliyeitwa Balaamu. Katika milima na chini ya miti wanaume na wanawake walijihusisha na mambo haya ya kuchukiza, wakawakiana tamaa wanaume kwa wanawake. Mambo haya yameangusha majemadari, na hivyo hatuwezi kuyaacha bila kuyazungumzia, bali tunapaswa kuyafundisha au kuyaweka pahali pake panapostahili. Tuchukue tahadhari kwa kuepuka kujitungia tungia katika mamabo katika uwasilishaji wa mada za aina hii.  

MATUMIZI SAHIHI YA NGONO:
Mungu ametupa mambo ya kutufurahisha (pleasure), kwa kuwa mkono wake wa kuume wa utoaji hutupatia mambo yafurahishayo. Kwa upande mwingine adui huwa  anabadilisha mambo ya Mungu kwa kuweka mambo yake, ambayo huleta furaha ya  kitambo kidogo tu kisha kufuatiwa na huzuni. Mungu aliumba ngono, na alitaka iwe tendo la kuleta furaha kati ya mume na mke. Mfalme Sulemani aliandika kitabu cha Wimbo ulio bora akizungumzia upendo huu ambao watu wa mashariki ya kati waliuzoea sana. Walipenda kitabu hiki kisomwe na watu wazima tu kwa vile kilisema mengi kwa undani. Vitabu vingine vya zamani kama kile cha Wakorintho kimesema kwamba kwa vile kuna uchafu mwingi wa uasherati kila mtu ni lazima awe na mke wake (au mume wake). “Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.” (1 Wakorintho 7:2). Na mtu aliyeoa mwili si wake ila ni wa yule aliyemwoa, au na aliyeolewa naye halikadhalika. Kila mmoja ana jukumu la kumfurahisha mwenzake, isipokuwa kwa wakati uliotengwa maalumu kwaajili ya kusali ili wana ndoa wasijiletee majaribu ya kutafuta kuridhishwa mahali pengine. Mausia haya yaonyesha ndoa na ngono vililenga kuleta uwajibikaji zaidi badala ya kuwa jukwaa la kudai haki. Wajibu wa kila mwanadoa ni kutafuta namna ya kuondoa deni lake kwa mwenzake na si namna ya kudai haki yake kutoka kwa mwenzake. Tendo hili si la kiboko au adhabu kwa mwengine. Kujali mwingine huongeza furaha ya ndoa. Na wale wanaomthamini Muumba na kuthaminiana huongeza kuridhika katika maisha yao ya ndoa na ngono.  Nafasi hii si ya kumlazimisha mwingine kufanya matakwa yako bali ya kujaliana na kutumikiana, kila mmoja akimjali mwenzake. Maisha ya usafi wa mwili na mazingira ni muhimu sana katika hatua hii. Juhudi ya kutosha ifanyike katika kuoga, kufua nguo, au kupiga mswaki na kadhalika. Wanaume wengine wamejiingiza kwenye ngono za kutisha ambazo ni za hatari zaidi (exotic sexual practices). Usimlazimishe mwenzi wako kufanya yatakayomkosesha raha. Mambo ya kulazimishana hayana nafasi kwenye upendo wa ndoa.

KURIDHIANA KATIKA NDOA:
Kuridhika kwako kwenye ndoa ni swala la uchaguzi. Kataa kumlinganisha mke au mume wako na magazeti, au mtu mwingie au filamu fulani fulani. Usimfundishe mwenzako kufanya mambo uliyoyaona kwingine hasa katika mambo yanayohusu ngono. Mambo ya kuigiza hayafai. Uwe mbunifu. Mfanye mwenzako ang’ae na aonekane mzuri. Mtafutie majina ya kumfanya atabasamu na kuona amefanikiwa kukupata. Mfalme Sulemani alisema ridhika na mke wa ujana wako. Hebu uridhike na mwili wake na umfurahie. Mwanamke pia afanye mume wake apende kuwa naye. Watu wengine wamekuja na nadharia za ngono za ajabu. Kwa mfano kuna bwana mmoja aliyeitwa Kellog. Huyu na mkewe walikuja na nadharia kwamba ngono ni kwa ajili ya kuzaa tu na baada ya hesabu ya watoto kutimia basi wanandoa hawapaswi kukaribiana tena. Nadharia kama hizi ni vyema umwambie mwenzi wako kabla ya ndoa ili ajiandae na isimletee shida baadaye hata kumsababishia kutoroka. Wanawake wengine wameleta nadharia za ajabu kwenye ndoa zao kutokea kwenye familia zao walikolelewa, kwamba tendo la ndoa ni kitu cha kustahimili, na wala si kitu cha kukuletea raha au starehe. Wengine huvumilia tendo hili kupitia unyanyasaji wa ngono, kubakwa, au ukatili uliotendwa na watu wa mbali au jamaa wa familia (incest). Wengine wamepata shida ya kupewa vilema wakiwa wadogo. Inasemekana zaidi ya wanawake milioni 100 wamekeketwa duniani. Wengine nilikutana wakiwa wametokea Ethiopia huku wakiwa wameshonwa sehemu ya uke. Inadaiwa ukeketaji hufanyika ili kuwazuia  wasifanye ngono na mtu yoyote hadi wakati wa ndoa. Sababu nyingine inayotolewa ni kuwa  watakapofanya ngono wasione raha yake, na hii itafanya watulie na kutokimbia kimbia huku na kule. Dai hili ni la unyanyasaji kwani katika Amri za Mungu uzinifu umekatazwa kwa wanaume na wanawake. Kama kuna kuzuia uzinzi basi kwa nini kusifanyike kwa jinsia zote? Tukumbuke kuwa sote tutasimama katika kiti cha hukumu siku moja na Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo atatuhukumu kila mmoja kutokana na matendo yetu. Tusisahau ya kuwa ingawa tunaokolewa kwa neema, lakini tutahukumiwa kwa matendo yetu. 

DHANA POTOFU KUHUSU NGONO:

Mambo haya mapotofu  yaweza kuleta madhara kwenye tendo hili (dysfunction). Wenye kufanya vitendo hivi wanahitaji zaidi ya maombi. Wanahitaji wataalamu wa kuwashauri. Kwa kawaida wengi hawaponi katika majanga haya ila kwa msaada kutoka nje. Washauri wengine wameingiza nadharia na mambo yao mengine yasiyofaa au yanayozidisha kutonesha vidonda.  Wanahitajika watakaosaidia majeruhi hawa kufurahia ngono kama ilivyokuwa imepangwa na Muumbaji wao. Kama umeamua uwe mwaminifu kwa mwenzi wako basi mwombe Mungu akupe uwezo. Kama umefanya makosa kwenye maisha yako ya ndoa, mwombe Mwenyezi Mungu msamaha na uanze upya. Hakuna aliye mkamilifu hivyo kukubali makosa si dalili ya udhaifu. Usishupaze shingo. Watu wengine wamesema ngono ni kwa ajili ya kupata watoto, na baada ya hapo hakuna haja ya wanandoa kukaribiana tena. Mifano ya watu wa namna hiyo ni Mke wa Kellog wa ‘Cereal’ na Mahatma Gandhi. Wao walikuwa na nadharia hii. Hawa hawakukaribiana baada ya kutimiza idadi ya watoto waliowahitaji.  Wenzi wapya wasilete nadharia kama hizi zisizofaa.  Katika ndoa zingine ni mwanamume tu ndiye mwenye uhalali wa  kumwambia mke cha kufanya. Ngono imewekwa kwa ajili ya kufanyika kwenye ndoa tu, na kwa hiyo isingepaswa kuwa jambo la kulionea kinyaa. Nje ya bustani tunaweza kuwa na maua mazuri, ila tukiyachimba na udongo wake tuyaweke kwenye zulia letu la sebuleni yakiwa na lile tope yatakuwa katika sehemu isiyo yake. Usitoe ile raha ya ngono ikawa peke yake bila ndoa. Ni kama vile tutake kupata raha ya ladha bila kumeza, kutafuna, na kuyeyusha. Yaani tunakula tupate ladha na kisha tunatema kile chakula. Ngono nje ya ndoa ni maigizo tu (performance) yanayomwacha mtu mpweke, tupu na mwenye baridi baada ya muda. Kuvunja sheria hii ni kama kukiuka masharti ya tabibu yatakayosalimisha maisha yako. Kutotii nguvu ya uvutano ina maana utaanguka, na si uvutano utakaopata shida. Serikali haipingi noti za bandia kwa vile ni mbaya, la hasha bali ni kwa vile si halisi kwa matumizi ya msingi ya kusaidia.

MAKUSUDI YA NGONO:
Mume na mke; wote waliumbwa kwa mfano wa Mungu. Wote wawili wanafanya mfano wa Mungu. Mungu aliyeumba mikono, na miguu ndiye aliyeumba viungo vyetu vya kiume/kike. Ashiki imeumbwa naye hata kabla ya Adamu kuanguka, ambapo kila kitu alichokiumba kilikuwa kizuri. Mungu hakuumba roho tu, bali na mwili pia. Sisi ni watu wa kiroho na kimwili pia. Ila ngono potofu ndiyo chanzo cha magonjwa ya mwili, hisia, roho, ambayo huumiza na kuharibu. Hivyo una uchaguzi baina ya ngono potofu na ile ambayo Muumba alitupatia. Watu wengi hata walio waumini hudhani kwamba wataonekana ni watu wa ajabu endapo hawatafanya ngono kabla ya ndoa na nje ya ndoa. Jumuiya, marika na vyombo vya habari huongoza katika kuwacheka watu hawa wanaoweka miili yao wakfu wasiichafue. Wao hupendekeza nguvu za ashiki (libido) zitumiwe wakati wowote na mtu yoyote kwa kadri anavyojisikia kama wanyama wafanyavyo. Huu ni utamaduni wa uovu uliokumbatiwa na mataifa ya zamani kama Wayunani na Warumi, ambao hatupaswi kuukubali. Leo hii watu wengi wana magonjwa ya kushindwa kufanya ngono (sexual dysfunction) kuliko zamani. Cha kustaabisha madawa ya kusaidia ngono yamekuwa mengi kama Viagra ila hayajasaidia kama watu wanavyofikiri. Hii ni kwasababu ya kujichafua na ngono haramu. Kwenye mataifa yanayoendelea  yasiyo na mambo mengi ya kileo watu wako salama zaidi miilini mwao kuliko wale wenye mabunifu mengi wanaoandamwa na shida nyingi. Utafiti waonyesha ngono ndani ya ndoa licha kuwa salama, ina kuridhika zaidi (satisfaction) kuliko nje ya ndoa.

NGONO NI KWA AJILI YA WANANDOA:
Vijana wengine hudai ngono ni kama vitamini ambayo usipoipata hutakuwa na makuzi mazuri, ambapo karibu asilimia 70% kwenye miji mingine walionyesha kujishugulisha na ngono nje ya ndoa kabla ya kufikia miaka 18. Mambo ya picha za ngono (ponografia) yametia fora zaidi katika kizazi hiki. Tungependa tujadili mengi juu ya mada hii ila pengine tujadiliane siku nyingine. Wiki iliyopita nilienda semina na swali likaulizwa kwa wanasemina kuwa mtu mwenye mazoea haya afanye nini kati ya kumwambia mkewe au mumewe au kukaa nayo kimya? Ilionekana wengine walijihisi hatia ila hawakutaka wazo la kumweleza yoyote (accountability), bali waliamini njia bora ni kumwambia Mungu tu. Hawa walipoteza nafasi ya kushinda katika jambo hili. Watu waliokuwa pale hata wachungaji walisema walikuwa na hiyo shida wakiwa wadogo sana. Mchungaji mmoja aliyekuwa na miaka 50 alisema alianza mazoea hayo akiwa na umri wa miaka 11 na mwingine alisema akiwa na miaka tisa. Hawa walisema kwamba hadi leo, wameifunga mitandao hiyo ili wasirudi kwenye njia waliyopitia zamani. Ni kama wanasema afadhali kwenda chongo mbinguni, kuliko kuendelea na mazoea hayo. Kuna watoto walitoka mchana shuleni,  wakielekea nyumbani kwao ambako walibaki wenyewe bila wazazi na huku wakiwa wamealika marafiki zao wa kufanya nao ngono. Hizi ni nadharia mbovu zinazoharibu watoto wetu. Mtu mmoja aitwaye Josh Mc Dowell alipofanya utafiti aligundua 28% hupata habari za ngono za mapema toka kwa marafiki zao, wakati 26% hupata kutoka kwenye filamu, 23% toka kwenye madarasa ya shule, na 22% toka kwenye runinga. Wajua runinga ina mafundisho gani kuhusu utakatifu wa ndoa na ngono? Kuna vpindi vingi vinavyofundisha mambo ya furaha ya ngono nje ya ndoa bila kutafakari madhara yake. Matokeo ya vipindi kama hivi ni kuwa kila siku wasichana wadogo huzaa nje ya ndoa (teen pregnancy). Hawa wanasumbuka na kuishi maisha ya umasikini, magonjwa ya zinaa kama ukimwi na kisonono. Vijana hawapewi habari kamili kuhusu ngono kwenye runinga. Vijana wengi wamepoteza amani na matumaini ya maisha yenye mafanikio. Wamepata makombo na kuumizwa mioyo.

NGONO SI KIPIMO CHA UPENDO:
Ngono isiwe kiini cha urafiki wa mapenzi kwa kuwa ngono inapokuwa kiini cha mapenzi, huzaa hasira, kutovumilia, ubinafsi, na wivu vinavyoweza kufanya mahusiano yasiwe na furaha. Mahusiano yaliyojikita kwenye ngono tu hukinai na matokeo yake ni kuachana. Kisa cha Amnoni kijana wa Daudi aliyemtamani sana msichana mwenye sura nzuri aitwaye Tamari, chatufundisha ukweli huu kwa kuwa alipofanya naye ngono chuki yake dhidi ya msichana huyo ikawa kubwa zaidi ya ule upendo aliokuwa nao awali hata kutaka kumwua. Kutotawala nafsi huweza kukuletea  kujidharau, kutojisamehe na hata kujichukia. Watu wamefanya majaribio ya ngono huru na wamegundua hakuna ngono huru. Ukikataa kufanya ngono zembe utafanya mtu akuthamini,  na hii tumeona kwenye ndoa za watu wa zamani. Kungoja mpaka tuseme “Ndiyo namchukua huyu mwanamke kuwa mke wangu/ au mwanamume kuwa mume wangu” ni muhimu sana. Hivyo wasichana wanaotaka wathaminiwe na wanaume waweke msimamo wa kutolala nao hadi ndoa itakapofungwa. Msifungue zawadi aliyowapa Mungu mapema, hiyo itawafanya muifurahie hiyo zawadi zaidi. Kwa wale ambao wameanguka, waombe msamaha na kujizuia kufanya tendo hili mpaka siku ya harusi. Itakuwa ni furaha na afya tele kwao. Watu hutoa matusi au kuapa kwa mambo mawili (Mungu na ngono). Vyote ni vitu vitakatifu. Kuna vitu vichache vitakatifu na hivi ni mojawapo. Je! Waweza kuorodhesha vingine? (Amri za Mungu, siku ya Mapumziko iliyoagizwa kwetu, Neno la Mungu, ndoa). Na ndiyo maana  hali ya furaha kwenye ndoa inazidi kupungua jinsi watu wanavyotumia tendo hili nje ya ndoa, furaha haikuongezeka bali imepungua na kuleta majonzi mingine. Uhuru wa kweli ni ngono kwenye mpango tuliopewa, maana wengi wamejichoma kwa maumivu mengi kwa uhuru waliofikiri wataupata kwa kufanya ngono nje ya ndoa. Ukitaka muziki mzuri huwezi ukapiga kinanda unavyotaka, eti tu kwa madai upo huru. Itakuwa makelele yasiyofaa. Hakuna jamii iliyo huru inayoendeshwa na tamaa. Jamii inayofanya hivyo itakuwa na minyonyoro ya utumwa. Katika katiba ya Mungu watu wasiotawala nafsi hawawezi kuwa huru kamwe. Mpaka pale watakapojifunza kutawala nafsi zao.   Mtu akiendelea na upotofu huu hujiona kama ametumiwa, hapendwi, hahitajiwi, ametelekezwa, na mzee.

KUOA NA KUOLEWA NI AGIZO LA MUNGU:
Wasichana wengine wamepata wanaume wa kuwaowa lakini wakakataa kuolewa lakini wakakubali kuzaa nao tu. Wanasema watakuwa huru zaidi kwa kutokuolewa. Hawajui kwamba kwa msimamo huo wanatoa mafundisho mapotofu kwa watoto wao wenyewe. Wanajifariji kwa kuwatambulisha wakisema eti “huyu ni mzazi mwenzangu” wakati kiuhalisia ni mtu anayefanya naye uasherati. Watu wengine wameenda mbali zaidi kwa kuharibu ndoa za wenzao. Wanachotakiwa kujua ni kwamba wanapaswa kuwa na wivu wa kuwa na waume zao wao wnyewe badala ya kuingilia ndoa ya watu wengine. Wanalopaswa kukumbuka mara zote ni kuwa hawaijui kesho yao itakavyokuwa. Kwa kuendeleza mazoea hayo, wanaweza kujikuta wakiwa viporo wao wenyewe kwenye ndoa zao, na wakati huo wivu utakuwa unawajaa watakapokuwa wakiwaona wenzi wao wa ndoa wakiwa na watu wengine. Ukweli uliothibitishwa ni kuwa, mtu mwenye wapenzi wengi, huwa hana upendo wa kweli. Maisha yake yamejaa utupu na utusitusi. Ni Mungu tu anayetoa furaha ya kweli na si ngono yenyewe peke yake. Yeye hutupatia sababu ya kuishi na maana ya maisha ambavyo hakuna awezaye kutunyanganya. Hakuna ulinganisho kati ya ngono kwa mpango wa Mungu na ngono huru ya Ibilisi.  Njia ya Mungu ndiyo bora kupita zote. Hakuna ngono salama itakayofanywa nje ya ndoa, maana ni jambo linaloingia kwa undani sana (intense) kwenye hisia za mtu. Nje ya ndoa ni kutumiwa tu, na kuharibiwa maisha.

KINGA YA MIMBA ISIYO SAHIHI:

Kutumia Kondomu si salama kama tunavyodhani. Maana kama hata baada ya kutumia kondomu mimba yaweza kuingia, kondomu ina uhakika wa kiasi gani kuzuia virusi vya ukimwi kuingia mwilini maana kirusi ni kidogo mara 450 kuliko mbegu za kiume. Wataalamu wanatuambia uwezekano wa kondomu kuzuia mimba ni asilimia 64-86% tu. Isije ikadhaniwa kwa kuwa karibu kila mtu anaitumia basi kondomu ni salama. Wengine huona aibu kutumia kondomu wanapojamiiana nje ya ndoa kwa kuwa dhamiri zao huwashitaki kwamba ni dhambi. Basi hiyo ingekuwa sababu tosha ya kuyaaga maisha hayo ya uchafu na kuingia katika maisha ya usafi. Mwaka 1989 shule ya Adam City High, ya Colorado ilifanyiwa majaribio ya watoto kupewa kondomu. Mwaka huo mimba za wanafunzi zilikuwa 58 kati ya 1000. Mwaka uliofuata wanafunzi waliofanya ngono kiholela na kupata mimba walikuwa 100 kati ya 1000.  Na takwimu zinaonesha kuwa takribani kila mwaka wasichana milioni nne hutoa mimba. Kutoa mimba si njia ya majira ya uzazi. Ni kuua. Je! Unaweza kumwua mtoto wako aliye wa miaka miwili? Au 20? Kwanini umwue huyu? Maneno ya Daudi katika Zaburi 139 yatuonyesha kuwa ubinadamu huanzia pale mimba inapotungwa. Programu za kulinda wasichana wasipate mimba zimepoteza tabia Njema. Kutofanya ngono nje ndiyo njia ambayo ina mafanikio kwa 100%. Hebu kila mtu afanye uasi kwa kukiuka ngono nje ya ndoa. Wengine husema tumeshaahidiana tutaona, ila asilimia kubwa hawapelekani kokote bali kubwagana na kuumizana vibaya.

HAKUNA NDOA YA MUDA:
Watu wanapojua kwamba mahusiano yao ni ya muda (temporary) hawawajibiki kikamilifu. Kuaminiana na kuheshimiana ambako ni kwa muhimu katika ndoa kunakosekana. Usitarajie kwamba mwanamume au msichana asiyejitawala au kujiheshimu aweza kuwa msaada kwako. Urafiki bila ngono ndiyo kipimo cha mtu atakayekuwa mwaminifu kwako na atakayekuwa na nidhamu ya ngono. Watu wasio kwenye ndoa hawana uwajibikaji. Wanaweza kung’oa nanga wakati wowote. Si watu wa kutegemewa hao kabisa. Ni bora ukaishi peke yako kuliko na watu kama hao. Baadhi ya watu husema hawajafikia umri unaofaa kuolewa, kwa kuwa hawana kazi, au wanaenda shule, au pengine wanadai hawajakomaa kimwili, lakini cha kushangaza watu hao hao wanafanya mambo yale yanayowastahili watu wazima walio kwenye ndoa zao. Kwa nini basi watu wajiingize kwenye ngono ya namna hii? Je ni kutojua? Je ni tamaa? Je ni upendo ulio na ulaghai ndani yake? Watu hawa wangefanya jambo la maana sana kama wangeendelea na shule au watafute kazi kama hawataki kuwajibika.

JIEPUSHE NA VISHAWISHI VYA NGONO:
Wengine wamejiingiza kwenye mahusiano ya ngono nje ya ndoa kwa sababu ya umalaya wa mapicha (ponografia na punyeto). Haya mawili yamesababisha watu wawe na wenzi wengi wa ngono (multiple patners). Epuka kuwa na mtu yoyote peke yenu, kwenye maficho, gizani, au kumsimulia mambo yatakayofanya hisia zenu zijenge tama za ngono. Washauri wengi wa ndoa wana hatari ya kuingia majaribu ya ngono nje ya ndoa wanaposimuliwa shida za watu. Wanaona wao wangekuwa wenzi bora, ili wawatulize watu hawa kwa mahaba. Ukimshauri mtu hakikisha una mwenzi wako au mtu mwingine wa kukulinda. Usidhanie umesimama; anguko laweza kukujia kwa ghafla usipochukua tahadhari. Japo sheria za kabila lenu zaruhusu kuchukua mke wa mtu mwingine ni makosa kwa mujibu wa sheria za Mungu kufanya hivyo. Tuzungumze na kutenda kama wale watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru. Mwanamke ama mwanamume asiyeoa au kuolewa huyu pia siku za usoni atakuwa mke au mume wa mtu mwingine. Ford mtengenezaji wa magari alipoulizwa siri ya ndoa yake kufikia miaka 50 alisema “stik to one model – Jikite kwa aina moja tu” Bila kujali umeoa au hujaoa, kamwe usiangalie runinga na mikanda inaonyesha ngono za ajabu, za kulawiti watoto wa kike na kiume, na zingine kwenye ponografia. Maana kwa kufanya hivyo, unashamirisha biashara haramu yenye uovu ndani yake, na pia unajiingizia mapepo kwenye mawazo yako ambao hapo baadaye itakulazimu kutumia juhudi kubwa yenye majuto kuwatoa. Kujilegeza kwa ngono (sexual promiscuity) kunatokana na uovu unaoendelea kama huu. Watu wengine wamesema kwamba matendo haya ya uovu hayaathiri jamii, na ya kwamba kujizuia kufanya ngono tuliyoumbiwa nayo ni kuwa mtu wa kale wa enzi za mawe. Baada ya muda watu waliojishugulisha na umalaya wa picha za ngono wataota sugu za ukatili, na hawataona kwamba wanawafanyia wengine ukatili. Wabunifu wa mitandao ya picha za ngono, wamegundua hii ni sumu ya kumaliza jamii, kwa kuongeza uharamia wa namna mbali mbali.

PONOGRAFIA NI JANGA:
Ponografia ni shambulio kwa ubinadamu na ukatili na uovu kwa wanawake na binadamu. Laana ya kujaamiiana ndugu wa karibu, na maradhi ya akili yameongezwa na zimwi hili. Waliotaka kuacha wameingia kwenye ulevi, wakitoka na kurudi tena wamewapa wake zao maumivu mengi. Kuona mambo haya kwenye runinga hata mara moja kwaweza kuleta ulevi wa ngono ulio kwenye urithi ambao mtu haujui. Watoto wengi wameingizwa kwenye mambo ambayo twaweza kusema yale maneno yaliyosemwa “Yoyote atakayefanya watoto hawa wadogo wafanye dhambi basi imempa afungiwe jiwe na kutupwa baharini ili azame, na afe kuliko aishi na kuangamiza wengi Jehanamu”. Watu wameenda jela kwa kuwalawiti watoto na kubaka watu, kutokana na kujihusisha na kuangalia mikanda mibovu katika umri wa utotoni. Familia zao zimepata shida nyingi. Wanawake wengi wameshindwa kuendelea kuwa pamoja na hawa waume zao kwa kuona wana uchafu usiofutika. Wanawake hawa wakawaona washauri watakaowasaidia mahusiano yao. Je! Wewe na mke wako au mume mnaangalia mikanda hii iliyoandikwa “watu wazima”, eti wakati watoto wameenda kulala? Acha kabisa, unapandikiza laana ambayo itakuwa vigumu kutoka nyumbani mwako. Mmoja wenu akisafiri anaendelea kuangalia vitu hivi na kukutana na wengine na kuendeleza uovu huu.

NDOA HAINA UZEE:
Lazima tujifunze mambo haya jinsi inavyotakiwa. Ndugu yangu mmoja anayetoka kanda ya ziwa, japo naye ni muumini, aliniambia mara kadhaa “Mwanamke ukifika miaka ya kuacha hedhi hupaswi kuendelea kufanya tendo la ndoa tena, kwa sababu kufanya hivyo kunaashiria kuwa una tamaa.” Yeye anashauri aliyefikia ukomo wa hedhi amwache yule mumewe apate wasichana wengine wadogo. Yeye aliyeamini hivyo alianza kulalamika mume wake alipoanza kutoka nje na kwenda kwa wasichana wadogo. Napenda kusisitiza, hakuna kitu cha namna hiyo. Kuacha hedhi ni mpango wa Mungu unaokusudia kumpunguzia mwanamke mambo ya kulea watoto. Mungu aliona mama akiwa mzee, ufanisi wa kulea mtoto unakuwa mdogo na hivyo akaweka huo ukomo na wala ukomo huo hauathiri tendo la ndoa. Mara nyingi wanawake wa rika hii hawana hofu ya kupata ujauzito, au kuahirisha safari kwa sababu ya kuhofia mambo yanayoendelea kila mwezi. Lazima tujielimishe vya kutosha kutoka chanzo sahihi cha ukweli yaani Maandiko Matakatifu. Mazoea ya kujenga hoja za maswala ya ndoa kwa kutegemea mapokeo au maoni ya watu wengi hayawezi kuwa salama. Maandiko Matakatifu yanathibitisha kuwa mwanamke aliyekoma kwenye hedhi si tu anaweza kujihusisha na tendo la ndoa bali hata kuweza kupata mtoto. Mfano mzuri ni wa Elizabeti na Sara ambao walipata watoto katika umri ulioenda sana wakiwa wamekoma katika hedhi. Kuna mambo ya msingi ambayo wengi mnaosoma mnayajua, ila nitayarudia kwa ajili ya vijana, maana kizazi hiki kimerukwa na mafundisho mengi ya jamii, na mara nyingi watu hupata habari zao kwenye mitandao, au marafiki badala ya chanzo cha kuaminika chenye uhakika na ukweli. Yale nitakayozungumza kwenye ukurasa huu ni kweli yote, kweli halisi na kweli tupu (absolute truth). Ni mambo ambayo kila binadamu anapaswa kujua, si kwa lengo la kujiongezea maarifa tu kuhusu maumbile yetu yanavyofanya kazi (anatomy and physiology), bali pia kwa kwa lengo la kuimarisha nia. Ni vyema ukayaingiza haya mawazoni mwako na kuyafanyia utafiti kwa kuyaweka kwenye vitendo.

MASWALA YA NDOA YASIONEWE AIBU:
Yale yahusuyo ngono ni sehemu mojawapo ya maisha yetu ya kila siku na si kitu cha kukionea aibu. Ni kitu cha aibu tu tunapokiuka sheria na kanuni zake. La muhimu ni kwamba sisi binadamu ni viumbe tulioumbwa tukiwa na viungo vyetu vya uzazi, au vya ngono, ambavyo wengine huviita sehemu za siri. Viungo hivi havikuwekwa usoni, au mikononi kwa sababu maalumu. Tunaweza kutembea barabarani na kumwonyesha mtu chanjo kwenye mikono yetu, nywele zetu tulivyokata au hata malengelenge mikononi baada ya kulima. Bali hatuwezi kumwonyesha mtu viungo vyetu vya siri (uke, uume, njia ya kutokea kinyesi, au hata matiti). Hivi kwa nadra tunaweza kuonyesha kwa wahudumu wa afya kama kuna shida fulani mfano mabadiliko ya rangi, ukubwa, mafundo, maumivu au jambo lisilo la kawaida kama muwasho, joto, au kutoka maji maji (discharge). Viungo vya siri vya mtoto pengine vyaweza kuonekana wakati akihudumiwa, ila mtu afikiapo miaka sita au saba anapaswa ajisetiri. Tabia ya mtu mzima kujifunua mbele ya watu si tabia njema hata kidogo (inappropiate). Kwa maelezo ya kina zaidi, Yeye mwenye kuviumba viungo hivi ameandika kwenye Torati ya Musa kitabu cha Walawi 18 na 20 jinsi ya kuenenda na viungo hivi. Kwenye maelezo hayo imefafanuliwa kuwa ngono ni kwa ajili ya wanandoa walio watu wazima tu. Torati yasema usifunue utupu wa ndugu yoyote kwenye familia awe ni dada yako, shangazi, mama, mjomba, au mkamwana (incest). Zamani Watoto wa Adamu na Hawa walioana kizazi kikiwa na nguvu, ila siku hizi kumekuwa na udhaifu na wengi wamekuwa na madhara ya kuzaa watoto walio na hitilafu au ulemavu fulani (inbreeding genes). Muumbaji aliweka sheria hizi ili kusaidia kuratibu mahusiano. Ni kweli Mungu ametupa uchaguzi, ila haina maana tukichagua machukizo basi sheria na kanuni zake zinaweza kutulinda. Tunachagua kwa uangamivu wetu wenyewe. Madhara yanayotokana na ukiukwaji wa kanuni hizi hayabagui, huwatokea hata wale wanaodhaniwa ni wakamilifu. Mambo haya yaliwapata watu wa zamani kama Rubeni mtoto wa Yakobo ambaye alirukia kitanda cha baba yake. Hata Ibrahim na Yakobo walioa wake wengi ikaleta shida, ila Isaka na Yusufu wao walinusurika na anguko hilo.

KAZI NA NDOA:
Mungu aliwaumba Adamu na Hawa akawaweka bustanini, si kukaa na kunywa juisi za nazi tu, bali kufanya kazi ili bongo zitumike. Hakuwaweka magorofani wakose cha kufanya na iwe rahisi wao kutoka nje ya mstari. Mungu hakumwumba Adamu na Haruni, wala Adam na Hawa na Rehema. Hakumwumba Adamu kisha akampa mnyama awe mwenzi wake bali binadamu mwenzake. Wote tumekosa na kupungukiwa na utukufu wa Mungu kwa maagizo ya Mungu ya aina mbali mbali, ila tuking’amua twapaswa tuache hiyo njia na kurudia mapito ya kwanza. Mwaka jana yasemekana watu milioni 2.2 wamekufa kwa magonjwa ya wanyama. Binadamu tulioumbwa kwa mfano wa Mungu tunapaswa kufuata kanuni za miili yetu. Mambo ya ngono si ya kufanyia mchezo, maana hayahusu uwezo wa mali, au mvuto, bali yanahusu zaidi afya; iwe ni ya kimwili, kiakili au ya kiroho. Wengi wameingia huzuni na kuugua kwa maumviu mengi kwa kutofuata mwongozo wa aliyeviumba viungo hivi vya uzazi na kutoa zawadi hii kwa binadamu. Watoto wetu tumewafundisha isivyo katika jambo hili tukawa kama wale waliotoa makafara yao kwa mungu wa Moleki na hivyo kuwaangamiza watoto. Wazazi hatuwezi kuwaambia watoto wasifanye mambo ya uchafu au zinaa wakati sisi tunayafanya. Mifano yetu ni mafundisho makubwa kwa watoto zaidi ya maneno yetu. Hata watoto wetu wakisoma vizuri na wakawa na maisha mazuri endapo hawatajua kumiliki jambo hili na badala yake kufanya tendo hili na watu, vitu, wanyama, mitandao au  wenyewe itafaya maisha yao kuwa magumu yenye kukosa furaha. Tumesema kuna nadharia nyingi kuhusu viungo vya siri kiasi kwamba ukisikia baadhi ya simulizi za makabila mengine masikio yatawasha! Watu wamejigundulia mavumbuzi mengi kiasi kwamba wanadhani kitu chochote chaweza kutumiwa kwenye viungo hivyo nyeti! Ni muhimu kutambua njia sahihi ya kuvitumia viungo hivyo kwa mujibu wa malekezo ya mtengenezaji mwenyewe (user manual). Viungo hivi havikuumbwa kwa uasherati au zinaa. Vilikuwa zawadi kwa wanandoa.

WAONE MATABIBU:
Masuala ya shida za kina mama au kina baba zihusuzo kizazi ni vyema kuwaeleza matabibu. Kwa wanawake mambo ya kukosa hedhi kwa muda mrefu, damu kutoka nyingi, kuchelewa kuvunja ungo, na kuugua kunakotokea wakati hedhi ya mwanamke imekata (menopause). Matatizo hayo kwa sehemu kubwa hivi sasa yanatibika na hii ni kutokana na utafiti uliofanywa kwa miaka mingi.  Mama mmoja tuliishi naye Michigan alipopata Menopause (hali ya kukoma hedhi) alianza kupatwa na maradhi ya akili, akawa mtu mgumu kuishi naye, ingawa alikuwa mama mwema sana. Alipoenda kwa Daktari alipewa dawa rahisi tu za Vitamin Bs, hali yake ikarudi kama kawaida. Wengine hupata joto na kusikia kama wanaungua, hasa katika nchi ambazo mazingira si ya asili. Wanawake wa Japani au Afrika wenye maisha rahisi na yasiyo na misongo sana wameonekana kuepuka kuwa wagonjwa wakati wa kukoma hedhi. Kwao inakuwa kama wanapitia kipindi cha kawaida cha maisha. Wanaume wamekuwa na shida ya tezi dume (prostate) kuvimba na kufanya mkojo usipite. Katika nchi zingine 70% ya wanaume waliofika miaka 80 wana shida hii. Haya yote yana ufumbuzi hivyo usiwe na hofu  kuyazungumza na tabibu wako, na kuendelea kujisomea ili kufahamu mengi zaidi yahusuyo maradhi yatokeayo katika utu uzima. Torati inasema mtu yoyote asilale na mwenzake wa jinsia moja naye, au na mnyama. Haya mawili yana athari moja na yakifanywa ni machukizo katika Torati au sheria ya Mungu. Mataifa mengi yamepinga mambo haya, japo machache yanaanza kuingia kwenye mtego, na hii ni dalili ya kufikia ukingoni. Machukizo ni mambo mabaya yasiyofaa ambayo unaweza kujisomea mwenyewe kwenye Torati ya Musa. Mtu anapaswa kufunua utupu wa mkewe au mumewe tu, na si vinginevyo. Mtoto anapozaliwa tu, karibu kila mtu hutaka kujua ni wa jinsia gani; wa kike au kiume. Zamani watoto wa kiume walithaminiwa sana, (katika baadhi ya jumuiya) kuliko watoto wa kike. Ilhali, watoto wa kike walithaminiwa sana kuliko watoto wa kiume katika makabila mengine, hasa kwa minajili ya malipo au mahari ambayo wazazi wangepata wakati mtoto huyu anapoolewa. Hivyo watu wengi huwa wanapenda kuwa na mchanganyiko wa wasichana na wavulana, hata kama uwezo huo anao Mwenyezi Mungu peke yake.

WATOTO WAPEWE MAFUNDISHO:
Kutokana na mambo ya siku hizi hatushauri watoto walale pamoja bila ya kupewa mafundisho yahusuyo via vyao vya uzazi. Watoto wengi wameshikana sehemu zisizofaa kwa udadisi ulio na uzushi waliopata toka kwa wenzao. Wazazi ni vyema kuwa na watoto wetu ili watuambie mambo, ila wakituambia tusistuke sana (freak) mpaka wanyamaze kwa kuhofia kueleweka vibaya. Wale wakina baba wanaokuwa karibu na wasichana wao wanawafanya kujitunza kwa maisha ya usafi, na wakina mama wanaokuwa karibu na watoto wao wa kiume wanawasaidia kujitunza kwa maisha ya usafi. Vijana wa kiume na kike wote wanatakiwa kuwa na maisha ya usafi. Sheria ya usafi si kwa wanawake tu, kwani viwango vya Muumba viko sawa, na viongozi au hata makuhani wa wanawake kwa hivyo kiongozi hawezi kudondosha viwango. Watoto wa umri wa miaka mitano hadi miaka sita huwa wanajiuliza maswali mengi. Moja ya maswali hayo ni juu ya wao walitoka wapi hasa. Wanauliza maswali mengi pia kuhusu tofauti za jinsia za watoto. Wanagundua kwamba wana tofautiana. Mtoto wa kike wa miaka minne alimuuliza mama yake, “Mbona Jonny ana kitu kirefu cha kukojolea na mimi sina?” Pia wanapenda kuuliza wao walitoka wapi hasa? Wakiona mnyama au kuku akimpanda mwingine anauliza, “ Hao wanafanya nini? Mbona anamuumiza mwenzake?”  Huu ni wakati mzuri wa kuanza kufundisha elimu ya kijamii, kwa kujibu kwa  kifupi tu maswali yanayoulizwa. Watoto wakiwa wadogo, mara nyingi wanafikiria kwamba tuliwatoa hospitalini, kwa vile wanaona picha zao wakiwa wadogo hospitalini, au wanasikia watu wakisema kwamba waliwaona walipozaliwa hospitalini. Kama mama aliyeelezea mtoto wake wa miaka mitano, (alipoomuuliza alitoka wapi), nadharia yote ya mfumo wa uzazi, na mtoto akabaki akishangaa, kisha akamwambia, “nilikuuliza hivi, rafiki yangu Daudi anatoka Musoma, sisi tunatoka wapi?”

WATOTO WANAPOANZA KUJUA:
Mtoto anapofikia umri wa miaka saba anakuwa amefahamu tofauti za maumbile ya msichana na ya mvulana.  Unaweza kuwaona wakishikashika sehemu zao za siri. Wakati mwingine wanaweza kuwashika wenzao makalioni au katika sehemu zao za siri, huku wakichekacheka. Hapa ni wakati mzuri wa mzazi kumweleza mtoto mambo ya mahusiano, maungo, maumbile na mambo mema yanayofaa kufanyika (aprópiate). Watoto wengine huuliza, mbona “wewe na baba mnalala chumba kimoja”. Mweleze vizuri tu, kutokana na umri wake. Ila cha muhimu ni usafi wa moyo na mwili (purity). Miaka tisa hadi kumi na mitatu ni miaka ya kujiandaa kwa ajili ya balehe (adolescence.) katika umri huu ingawaje viungo vya uzazi huwa bado havijakomaa, wasichana wanaweza kuanza kupata hedhi yao. Pia huanza kujadili wanayoyajua kuhusu ngono pamoja na rafiki zao. Wengi wanakuwa wamesoma shuleni kuhusu mfumo wa uzazi, na wana hamu ya kujua zaidi. Wanapofikia umri wa miaka 11 hadi 14, wengi wanakuwa wana habari kamili kuhusu uzazi na ngono. Wanakuwa na hisia zinazowafanya washangae na wasijue jinsi ya kuzitumia. Basi wanabaki wakitaniana tu kuhusu hisia zao. Vijana wengine hushangaa kwa nini wamechelewa kubadilika sauti au kukua kwa sehemu za mwili zinazohitaji mabadiliko kama sauti, mabega, matiti, maumbo nk. Kwa kawaida mfumo wa uzazi tofauti na mifumo yote mingine huwa haukosei, hata ukichelewa basi utapitia ukuaji wake kama kawaida hapo baadaye.

UMRI WA UJANA:

Umri hatari sana ni wa kati ya miaka kumi na mitano na kumi na minane. Vijana katika umri huu wana mvuto mkubwa sana kwa vijana wa jinsia tofauti (opposite sex). Wazazi na waalimu wanahitajika sana kuwapa vijana hawa mwongozo na elimu ya kijamii (sex education) kuhusu hisia zao, ambazo zinachemka sana wakati huu. Wanapokosa elimu hiyo katika umri huu mchanga, huchanganyikiwa wasijue jinsi ya kujizuia. Wasichana wanavutiwa na wavulana, na pia wavulana wanavutiwa sana na wasichana, ingawaje bado hawapendi kuonekana hadharani. Hivyo wakipata nafasi wakiwa peke yao wanaweza kuvuka mipaka kwa kufanya mambo yasiyofaa ili mradi wafanye majaribio na kukidhi haja ya hisia hizi. Inabidi watoto waambiwe kwamba hii ni hali ya kawaida ya kukua. Na kwamba Mungu alitupatia uwezo wa kujizuia na kusubiri hadi hapo tutakapokuwa tayari kuchagua  mmoja wa kuambatana naye katika ndoa. Mambo ya umalaya wa picha (ponografia) yamejaa sana kwenye simu na mitandaoni. Wachungaji maelfu kwenye utafiti (questioneer) wa evangelical walipoulizwa asilimia 54% walisema walihusika na jambo hilo. Watoto wamekuwa na vitu hivi, na wazazi wao hawakuamini, wakaanza kulaumu walimu. Mtoto wako umjuavyo na alivyo mara zingine ni tofauti sana. Uovu huu wa kileo, wa ponografia, punyeto, na ngono zingine za kutisha upo. Hivyo tuna sababu maalumu ya kusali, maana binadamu utakabilianaje na haya yote? Mungu aweza kutuonesha cha kufanya ila tusipate mshtuko sana mbele yao (do not freak) utakapokuta mambo haya yanatendwa na wale usiowatarajia.  Usioneshe mshtuko wa aina yeyote utakapogundua kuwepo kwa hali usiyoitarajia maana ukifanya hivyo, utafichwa mengi zaidi. Mambo mengine huenda yakahitaji kutoa tarifa kwa vyombo vya kisheria ili hatua za haraka za kunusuru maisha ya watoto zichukuliwe. Uwe rafiki zaidi ya polisi, maana ngono inaweza ifike kwenye hatua za kuua, kujiua, kufanya mambo kwa nguvu na mengineyo ambayo hatukuumbiwa binadamu tuyatende

NGONO ZA MAPEMA:
Ni vizuri vijana waambiwe hatari ya kujihusisha na mambo ya ngono mapema. Athari kubwa muhimu ni kwamba hiyo ni dhambi mbele za Mungu. Na hili tunalisema bila hofu kama Yusufu alivyothubutu kusema. Japo tu binadamu na tunakosea mara nyingi, lakini hiyo haimaanishi tuhalalishe dhambi, la! Tunapotenda dhambi tunamwomba Mungu atusamehe kwa kuwa tumevunja sheria na amri yake aliyoweka. Na kwanini ameweka? Ameweka ili kutulinda sisi na watoto wetu, na jamii yetu tusiingie kwenye maumivu mengi ya  hisia, mimba zisizo na uwajibikaji, kupata mimba na mtoto ambaye bado huna uwezo wa kumlea n.k. Dada mmoja wa miaka 28 alinidokezea kwamba kwenye dini yake hawakuambiwa wasilale na mwanamume kabla ya ndoa hivyo aliishi na mwanamume na wakawa na mtoto, na sasa katika hali ya majuto akawa ananiambia “Napenda mtu atakayenioa amkubali na mtoto wangu.” Kilichonishangaza ni kuwa naye alikuwa wa madhehebu ya kikristo. Alishindwaje kujua kuwa kujamiiana kabla ya ndoa ni tendo lililoharamishwa hata katika ukristo? Kwa kweli hata wale wapagani wanajua wazi kwamba ngono na mtu bila ndoa ni jambo ovu. Jamii zote duniani zinatambua kanuni hii, maana si rahisi uende mahali ukute wasichana na wavulana katika hali ya kawaida wakilala pamoja. Kwa kutumia tu akili ya kuzaliwa (instinct) kila mtu hujua kuwa hapaswi kuvua nguo mbele ya mtu mwingine wa jinsia tofauti au hata kulala naye. Kwa kuzoelea ngono, mtu unaweza kuambukizwa na magonjwa ya zinaa, yakiwemo ukimwi, ambao hadi sasa hivi hauna tiba. Mama usimpe binti yako dawa za kuzuia mimba, au kumfundisha kutumia mipira ya kondomu ili kuzuia mimba au magonjwa. Wazazi wengine, hasa mama wanawatafutia au kuwahimiza wasichana wao wawe na wachumba ili hali wakingali wadogo! Hii ni aibu kubwa, na uovu huu unaweza ukurudie kwa jinsi fulani kwako. Wengine waliofanya hivi, walisamehewa na Mungu ila hawakujisamehe wenyewe, na walipokosa kuzaa kwa bahati mbaya tu, walifikiri Mungu amewaadhibu, au hakuwasamehe kwa dhambi waliyomtendea, jambo ambalo mara nyingi huwa si kweli.

KUTOA MIMBA:
Uovu huu wa kutoa mimba utashusha hadhi yako na utakuwa mtumwa wa kutumia mwili wako kwa kujifurahisha  wewe mwenyewe kwa anasa na tamaa za kimwili. Enzi hizi za uhuru wa ngono (sexual freedom), watu wameichukulia ngono kama njia ya kutimiza haja tu kama vile mtu anavyokula baada ya kujisikia njaa, au mtu anapokunywa maji baada ya kujisikia kiu. Katika enzi hizi za teknolojia ya kubonyeza (press button) tu na kupata unachotaka, iwe ni hela, chai au kahawa imetufanya tufikirie kwamba, hata ukisikia tamaa ya mwili, badala ya kuutawala mwili na kujizuia, basi ni lazima ujiridhishe hapo hapo kwa kubonyeza tu. Hii ndiyo sababu nyingine kwa nini ubakaji umekithiri sana siku hizi. Watu hawajui kubembelezana na kuridhiana. Watoto wetu wafundishwe jinsi ya kuvaa. Kabla ya dhambi Adam na Hawa walivikwa utukufu wa Mungu. Ila baada ya hapo ilibidi watengenezewe mavazi. Kwa nini tunavaaa nguo? Ni agizo la Mungu kuficha utupu wetu, na kujikinga na hali ya hewa. Twapasa kuvaa katika namna ambayo hatutatuma ujumbe wa ngono kwa jinsia ile nyingine. Wasichana waelewe hili maana matokeo ya kile wanachofanya ni makubwa, na ndiyo wao wanajaribiwa na hili kuliko wanaume. Watoto wetu wa kike tuwafundishe kuvaa vyema toka wakiwa wadogo. Twasoma haya zaidi kwenye Torati ya Musa Kutoka 20:26. Kutembea bila nguo zinazofunika vyema ni dhambi, na aibu. Kuwa na utupu kunakaripiwa kwenye ufunuo 3:17. Ila Mungu anatupa uwezo wa kununua nguo. Tukijaribu kuvuta macho ya watu kwa mwonekano wetu wa utupu tunatia afya zetu hatarini. Kijana anapokuwa amefikia umri mzuri wa kutafuta mwenzi wa maisha, (mara nyingi vijana wanapata wachumba wanapokuwa vyuoni), ni vizuri pia wachumbiane katika hali ya kumcha Mungu na kujizuia hadi watakapooana.  Kitabu cha “I kissed dating goodbye” kinaelezea vizuri jinsi uchumba ulivyo mzuri ukilinganisha na urafiki wa mihadi ya mapenzi (courtship versus dating). Kijana aombe maradufu anapofikia umri huu wa kutafuta mchumba na Mungu, kwa wakati ufaao, atakupatia.

UCHUMBA SIYO NDOA:
Katika kipindi kimoja cha vijana, kijana mmoja alichangia akasema hakuna haja ya kungoja kama wameshahakikishiana na mchumba wake kwamba wataoana, na hasa kama wameshatambulishana kwa wazazi wa pande zote mbili. Kwa kumjibu mchungaji wake, alifungua Biblia na kusema, “Nitawasomea fungu fulani na ninawaomba mniambie linatoka katika kitabu na sura gani katika Biblia. Na fungu lenyewe linasema ‘Msizini, isipokuwa kama una uhakika mchumba uliyenaye mtaoana naye, na ya kuwa mmeshatambulishana kwa wazazi wa pande zote mbili….’”  Vijana wachache walishabikia wakaanza kutafuta kitabu na sura inayosema hivyo kwenye Biblia, lakini wengi waligundua wakasema kwamba hakuna fungu kama hilo kwenye Bilblia. Wote walifurahia ubunifu wa Mchungaji huyu na wakakubaliana kwamba watafuata mwongozo wa Mungu ulioko katika Biblia. Kuwa mchumba wa mtu ni kama mti kuwekewa alama kukatwa lakini bado haujakatwa. Mpaka siku ya arusi ndiyo unajua sasa huyo ni wako. Na hata siku ya harusi peke yake si uhakikisho kuwa utaoana naye maana tulishasikia wengine waliokataliwa mbele ya mimbari ya kufunga ndoa. Hebu Neno la Mungu lipewe uzito wake kwa kusisitiza kwamba ngono nje ya ndoa ni dhambi, hata kama inatendwa na vijana walio wachumba waliotambulishwa na wanaopendana kiasi gani. Shetani amedhalilisha ndoa, na hasa kushirikiana kimwili, limekuwa kana kwamba ni jambo la kawaida tu. Wasichana wengi wameachwa kwenye mataa, wakipigwa na butwaa. Imechukuliwa kama kukata kiu kwa kunywa glasi ya maji au soda. Au kula chakula unaposikia njaa, maana unachofanya ni kuangalia tu mgahawa ulio karibu unaingia na kuagiza chakula, unakula. Ukishiba unaenda zako. Kesho yake ukisikia njaa tena, utakula po pote tu, mradi ushibe, siyo lazima uende kwenye ule mgahawa uliokula jana yake. Hii ndiyo hali tunayoiona kwenye luninga na mitandaoni, kwamba uhusiano wa kimwili siyo lazima uwe wa kudumu, ni wa kujifurahisha kwa muda tu. Na mtu anaona raha zaidi anapokuwa na wenzi wengi.

JIHADHARI KABLA YA HATARI:
Wasichana wawe waangalifu kwa afya zao, wanapotembea usiku, na kujihusisha na watu waovu, maana kuna uwezekano wa kushikwa kwa nguvu (kubakwa). Mawasiliano yetu na watu yawe ya usafi, pia tusitume ujumbe usio sahihi aidha kwa maneno, mavazi, kuashiria, au kukonyeza. Maisha yanabadilika hata wanaume hubakwa siku hizi,  kutokana na dhambi au machukizo kuzidi duniani. Nilikutana na mama na mtoto wa kiume wakiwa kituo cha polisi siku moja ambaye mtoto wake wa miaka 10 alikuwa amebakwa. Haya yote si mambo mazuri na hatutaki yatutokee. Tunaishi ulimwengu wa dhambi, na ni vyema tuwe waangalifu tunavyoweza na kuomba Mungu atusaidie. Kulikuwa na kipindi ambacho kilikuwa kinaonyesha baba mmoja anatembea na mke wa kijana wake, na wote kijana na baba wakazaa na huyo binti, na wote wanajuana!!! Ubaya zaidi ni kuwa, wanaonyesha kwamba jambo hilo ni sawa kabisa, na hakuna shida wala madhara yo yote katika kulifanya. Pia kuna haya mazoea ya watu wengi, (nafikiria pia kutokana na luninga), kwamba wapendanao, lazima walale pamoja na kufanya ngono. Mtoto mmoja wa chekechea alikuja kushtaki akilia kwamba mwenzake amesema kwamba yeye ni rafiki (girlfriend) wa mvulana fulani mdogo kama yeye. Nikamuuliza, “kwani kuna ubaya gani, ukiwa rafiki wa fulani?” Akasema, “Mimi silali naye!” Jamani!! Nani aliwaambia hawa watoto wadogo kwamba ukiwa rafiki wa mvulana au msichana fulani ni lazima mlale naye? Haya ni mawazo ya mwovu shetani. Wakati fulani tulikuwa kwenye makambi mahali fulani, nikahudhuria kipindi cha vijana. Mhubiri wao akawa anawafundisha somo la kuwa safi (pure) katika ujana wao. Akawauliza, “Je, inawezekana vijana wa leo wajitunze (wawe pure) hadi waoe/waolewe?” Akaongezea swali la kutia changamoto sana, “Je, Yesu angezaliwa katika kipindi hiki, na malaika Gabrieli aje akitafuta msichana safi, bikra wa kumzaa Yesu, je, angepatikana?”  Wavulana wengi, kama siyo wote waliokuwepo walijibu kwa kuzomea, “HAPANAAA!” Wasichana wachache sana walijibu kwa aibu, “Ndio, tupoo.” Mhubiri akawashangaa wavulana akawauliza wanajuaje kwamba wasichana wengi leo siyo bikra, na ni nani wahusika wakuu? Wakabaki kuchekacheka tu.

TUKEMEE UASHERATI:
Wazazi wenzangu, hebu tukemee dhambi hii ya uasherati. Ni dhambi tu hata tukiipamba kwa lugha gani. Maandiko yasema wanzinzi wote hawataurithi ufalme wa Mungu. Tuwatie vijana wetu moyo kwamba inawezekana kuishi maisha matakatifu kama Yusufu. Haikuwa rahisi kwake kumkimbia mke wa Potifa, na kusema, “Nitawezaje kufanya uovu huu  na kufanya dhambi mbele za Mungu?” Huwa ninawauliza vijana wanaobisha kwamba siku hizi hawawezi kujizuia hadi siku ya kuoa, kwani enzi za zamani kulikuwa hakuna simu na internet, ilikuwa lazima watu waandikiane barua, ambayo ingemfikia mpenzi baada ya wiki kadhaa. Siku hizi ni ujumbe mfupi wa maneno (sms/text) tu na tayari mmeshaonana baada ya dakika chache kabisa. Huwa nawapa mfano wa Yusufu, kwamba naye alikuwa na hisia (emotions) kama wao, na alikuwa kijana kama wao. Si waoga wakimbiao, kijana Yusufu Mtumwa aliweza kukimbia wakati Samsoni jitu kubwa, Rais wa nchi aliangushwa chini na Delila. Waambie vijana wasifikiri wao ni imara hata wakijiweka kwenye majaribu wataepuka uchafu wa ngono, la hasha! Kama wanafikiri vile basi wajifunze kwa Suleimani ambaye pamoja na hekima yake aliangushwa, ama Daudi pamoja na kumpenda kwake mungu aliangushwa, ama kwa Samsoni ambaye pamoja na nguvu zake zote aliangushwa katika ngono.  Mambo mengine ya kuwafundisha watoto wanapoendelea kukua ni yanayohusu kujisisimua kwa kushika sehemu zao siri au punyeto (masturbation) na picha za umalaya (ponografia).  Haya yote yanathiri afya ya mtoto au mtu mzima, kwani siyo mpango wa asili wa binadamu, na huleta dhamira kushitaki na kuharibikiwa na ubongo kwa namna fulani. Kwa mpango wa Mungu ni dhambi pia, na kiafya ni madhara makubwa kwa  kuleta maradhi ya akili. Wengi wameharibikiwa maisha kwa mtindo huu wa siri, na watu wengi wameuidhinisha kwamba ni sawa na watoto waweza kufanya hivi. Usafi wa tabia, mawazo, kuoga na kubadilisha nguo za ndani ni muhimu sana kila siku. Watoto wafundishwe yahusuyo kupevuka na kuwa msichana au mvulana.

KIZAZI CHA WASIOJIZUIA:
Siyo kwamba hisia za watu wa zamani zilikuwa zimepungua  au zilikuwa kidogo kuliko zile za watu wa kisasa. Zote zilikuwa sawa. Tofauti ni katika hali ya kujizuia au kujikana nafsi (self control). Self control inahitajika katika nyanja nyingi za maisha, kama mavazi, vyakula, hasira n.k.  Danieli aliamua yaani aliazimia katika moyo wake kwamba “hatajinajisi na vyakula vya mfalme,”.  Siri iko katika uamuzi. Bahati mbaya sana wengi wetu tunaishi kama bendera, tunafuata tu upepo, hatuna maazimio yo yote katika maisha. Mungu alituumba ili tumtukuze Mungu kwa miili yetu, na kila tulitendalo, kwa nguvu za Mungu inawezekana wapendwa. Shetani ametufanya tuonee aibu kuwafundisha watoto wetu somo la ngono.  Hii inafanya wapate elimu ambayo si ya kweli, yaani ya uongo na kuharibu maisha yao.

Maisha ya ngono nje ya ndoa na kabla ya wakati ni mabovu na yenye kuharibu tabia na kicho kwa mambo ya kiroho katika maisha yote ya mtu. Nilipofanya hospitali ya wagonjwa wa maradhi ya akili kule Hagerdon, New Jersey mtu aliyetusimamia kazi alisema “asilimia 70 ya wale walio hapa wanahusika na ngono potofu”, yaani walikuwa wameharibiwa maisha wakiwa wadogo au vijana (abused) kwa namna fulani. Mtoto akifika miaka 10-12 lazima apate mafundisho ya undani zaidi, maana siku hizi watoto wa umri huo watakuwa wameshakutana na mengi mno (exposed), labda mtoto wako umfundishie nyumbani, na muishi katika jamii zenye uwezo kidogo, kila mtu ana nyumba yake mbali na kujitegemea, na tena msiwe na runinga au kompyuta au simu ziwe za nadra sana au tuseme uwe unachunga mambo haya sana, na usiwe na kibarua cha kukuweka mbali na wanao.

WATAHADHARISHE WANAO:
Mwambie mtoto kuhusu mpango wa Mungu kwa viumbe vyake vyote, vidogo na vikubwa. Mfano waweza kumsimulia mtoto wa miaka mitatu hivi “Sikiliza Haruni, Mungu ana mpango wake ambao ameandika kwenye kitabu chake kinachotufundisha sote, wadogo kwa wakubwa. Mungu ni muumbaji aliyeumba vyote, ametupa macho tuone, na anataka tufanye yaliyo sawa, ametupa masikio, mikono, miguu, na chakula ili kufanya miili yetu iwe na nguvu. Siku moja utakuwa mtu mzima, na yale ufanyayo sasa ndiyo yatakayowezesha kukua katika tabia bora mbele za Mungu. Kuna watoto na watu wengi ambao ni wazuri, bali kuna wengine ambao kwa kuonekana nje hawana tofauti na wazuri ila ni wabaya. Utawatambua kwa vitu watakavyokwambia ufanye.” “Wakati mtu haoni, au kusikia watakuuliza tuonyeshe sehemu yako ya siri au ya kukojolea. Ukisikia hivi, ujue ni jambo baya, hata akiwa rafiki yako. Je utaona kama ni mchezo kwa vile ni rafiki yako au utakimbia? Hakikisha unaniambia au unamwambia mtu mzima unayemwamini. Mara nyingine watakusifu, na wengine watakuja kama kondoo na kumbe ni mbwa mwitu. Anaweza kukwambia ukae kwenye mapaja yake na kukwambia maneno fulani maovu. Akikuambia nyamaza usiseme siri zetu, hakuna atakayekuamini, ujue ni kitu kiovu. Pengine aweza kukuahidi zawadi ili ashike sehemu zako za siri, au kukushika kwa nguvu. Anaweza kukwambia atakupa kitu fulani ili ufiche siri. Je utamkimbia na kuniambia mimi au mtu mzima unayemwamini? je adui akiwa ni kitabu cha picha za watu wasiovaa nguo, au picha mbaya, je utaziangalia hizo picha? Shetani ni mwovu, ataka kuharibu roho yako, ndiyo lengo lake, ila utakuwa nguzo ya  familia yako utakapokua.  Jinsi utakavyoongoza familia yako itatokana na unayoona na kuyakimbia kama ni maovu. Usikubali mtu akuvue nguo zako, upige makelele na useme kinachoendelea, usikae kimya “

MFUNDISHE NAMNA YA KUJIHAMI:
Mwambie apige makele endapo mtu anataka kumshika sehemu za siri. Je mawazo mabaya yakija kwako ufanyeje? Ni vyema uombe, mawazo machafu, matendo na maneno yasije kwako. Wale wanaopenda kulawiti watoto wana uzoefu (professional) wa shughuli hii. Mtoto wako akijua kwamba upo kumlinda na unamwamini anachosema atakuambia.  Watoto wako wanapaswa kujua kwamba wako huru kuja kwako saa yoyote.  Hawataelewa hili bila wewe kuwaambia, wapaswa kuwa na mawasiliano nao (communication).  Watu kama hao waweza kumfanya mtoto wako awe na woga, aibu au asiweze kujua la kufanya. Watajionyesha wao ni watu wakamilifu na wala hawawezi kufikiri hilo.  Wengi wao wana talanta ya kufurahisha watoto. Wanafurahi ukiwapa watoto wako kutunza.  Wanapenda kukupendeza na kukufanya uwaamini.  Waweza kutamani sana uwe na nafasi ya kufanya mambo fulani na kuwapa watu hawa watoto wako ila waharibu utoto wao na kuanza safari ya mavunjiko au mipasuko ya hisia na jamii.  Wanajua kufanya watoto wajisikie wana hatia na kwamba wao ndiyo waliyofanya uovu wao ukatokea.  Mzazi jifunze kuangalia na kusikiliza.  Weka wazi mawasiliano na mtoto wako. Rafiki yangu alisema mtoto wake wa miaka 10 alimwambia kwamba mvulana wa miaka 6 alikuja kumshika sehemu zake za siri na alipomwambia, kwanini anafanya vile? Alicheka tu. Mama yake alimwambia kwamba kuna milango ya ulinzi kwako. Mlinzi wa kwanza ni Mungu wako, mlinzi wa pili ni wewe mwenyewe, na ni vizuri umeniambia kwa sababu mimi ni mlinzi wako wa tatu. Ukiona kitu cha namna hiyo tena niambie ili twende kwa mzazi wa huyu mtoto pia.  Watu waovu wanaoharibu watoto  wanaangalia wale ambao wako karibu ya mikono yao (vulnerable). Wazazi wengi wanaogopa kujadili mada hii ya ngono, wakifikiri shida zitaondoka zenyewe na mtoto atajua mwenyewe. Wazazi wengine wanaficha mtu aliyemfanyia mtoto wao ubaya hasa kama ni jamaa yao, mwishowe mabomu ya kutisha hulipuka. Watu hawa waovu wanapenda uweke siri hii na wanaenda kumfanyia mtoto au mtu mwingine.   Tuvalishe watoto wetu wa kike kwa adabu na kwa uangalifu, ili watu hawa wenye mawazo magonjwa na mapotofu wasipate kuwarubuni watoto wetu. 

UMALAYA KWA WATOTO:
Umalaya kwa watoto unaongezeka duniani kwa ajili ya watu kama hawa. Watoto wako wakicheza hakikisha wamevaa vizuri, watoto wa kike wavalishwe kaptura ndani ya magauni yao. Wengi tunashangaa tunaposikia mambo ya kubaka watoto, na wala tusijue watu hao ni watu wa kawaida tunaokutana nao kila siku. Ni ndugu zetu na wengi tunaishi nao nyumba moja au mtaa mmoja. Mungu amehahidi hekima kwa wote wanaoulizia. Waovu hawa wanaishi maisha ya mafanikio na ya utulivu kwa vile hakuna mtu anawatolea taarifa ili wakamatwe.  Wanajiona salama kwa vile miaka inapita na wanaendela na haya na watu wanafichia siri zao. Wengine ni ndugu zetu wa karibu na tunaogopa wataenda jela japo wameharibu watoto wetu katika maisha yao yote.  Maisha ya watoto hawa kama si neema za Mungu yanakuwa na huzuni na matukio mengi mno yanayohusu hisia za kutojithamini, hisia za kujiua, kuchukia jinsia nyingine, kuchukia ngono hata baada ya kuoa/kuolewa na mengineyo.  Ni kweli kuna hukumu siku ya mwisho, ila hata sasa ukisikia yoyote anayeshugulika na uhalifu huu toa taarifa.   Yule anayechafua watoto anapofichuliwa nguvu zake zinavunjwa.  Kumbuka kumwambia mtoto wako kwamba unampenda na kutaka awe na usalama na mara zote akwambie chochote kile ambacho kinabidi kisememwe, na utakuwa tayari kusikiliza mara zote. 90% ya wahalifu wa namna hii ni wale walio karibu na mtoto, marafiki au familia. Jinsi ya kusaidia ni kuwaeleza vizuri kuhusu watu wabaya hawa na cha kusema wanapoambiwa “usiseme.” Mtoto afundishwe usafi wa mawazo, matendo na maneno. Watoto wengi wameuliza, Je, ni umri gani waweze kuwa na mahusiano ya jinsia nyingine? Kwa kweli hatushauri mahusiano na jinsia nyingine ya karibu, bali ya urafiki wa kawaida (general friend) mpaka mtu afike miaka 18 ndiyo afikirie uchumba. Na hata hiyo miaka 18 ni vyema kutumia mfumo wa uchumba (courtship) badala ya urafiki wa mapenzi unaoitwa “dating” na pia waweze  kujitegemea kimaisha. Hebu urafiki wa aina hii usiwe mafichoni, muda uchukuliwe kuombea vijana hawa, na vijana wajiombee, maana katika ndoa  mtu huharibu maisha mema au kujenga maisha mema.

FAIDA YA NDOA ZA KIAFRIKA:
Waafrika toka jadi walikuwa na uchumba unaongozwa na wazazi na wazee na kutoa mahari, hii ilifanya ndoa zetu kuwa imara. Mtoto hata wa miaka 8 aelezwe jinsi ya kuheshimu jinsia nyingine, kama wavulana kuheshimu wasichana kama dada zao, na kuwasaidia wajiweke safi kwa wenzi wao wa siku za usoni.  Mahusiano na jinsia nyingine si majaribu ya urafiki tu, bali ni kwa ajili ya ndoa. Kama hauna mpango wa ndoa usifanye urafiki wa majaribio ya dating. Kukumbatiana na kubusiana, kuna madhara yake, kiroho na hata kimwili.  Lazima kuwe na mipaka na jinsia nyingine: Huyu si mke au mume, vijana wangojee hadi waoane ndio wajuane kimwili. Hili si agizo letu, bali ni agizo la Muumba, na watafiti wa sayansi wameona wale ambao wanayaanza mambo hayo mapema na hata kuthubutu kuishi pamoja wakisema wanajaribu kama itawezekana wafaane, wameachana kwa zaidi ya 300% kuliko wale ambao walijitunza. Wengi wanafikiri kwa vile wataoana hivyo wana haki ya kufanya  yale wafanyayo wanandoa, wakagundua wamechelewa, na kwa majonzi na makovu mengi wamejuta! Ukitaka chimba haya zaidi kwenye kitabu cha “I kissed Dating Goodbye”, au Courtship vs dating by Dr Davis. Kufanya uchumba (engagement) ni kama mtu alitia alama mti, aje kuukata na ikapita miaka mia hakurudi tena. Je hatujaona hilo bado? Kila siku mawazo ya mtu yanabadilika, basi mtu asije akaachwa kwenye mataa na kubeba hatia ya dhambi au hata kiumbe kipya. Mitindo ya maisha na imani ikiainishwa pamoja yaleta watu kuridhika na amani ndani ya moyo wa mtu.

JITENGE MBALI NA MAJARIBU:
Siku hizi hatuna jambo au unyago, hebu vijana wafundishwe ili isionekane wanataka kukatazwa raha fulani bila sababu. Maandiko yasema kila kitu. Kumezuka siku hizi umalaya wa mapicha (ponografia) kwenye Kompyuta na ngono za ajabu ajabu za dotcom. Hizi zote ni uovu. Nchi zingine asimilia zaidi ya 50 ya watu hushugulikia hizi, na kuvunja ndoa zao. Umekuwa kama ulevi, kwa watu wazima na hata baadhi ya watoto wa chini ya umri wa miaka 18. Haya yote ni uovu, uwe wa picha au uwe wa halisi (3D). Epuka matangazo kwenye Kompyuta, utakapoona yanakuja yaruke. Weka kompyuta mahali kama sebuleni kila mtu aone kinachoendelea ili kupunguza uovu huu, maana umewateka wengi na hata kutekwa nyara kwa watoto wadogo kumetokea. Dunia imepauka ukilinganisha na yale Mungu ametutayarishia au kutupa kama zawadi. Jifunze kutofautisha yale ambayo ni mazuri tuliyopewa kama zawadi, na yale ambayo ni maovu ili ulinde afya yako. Usijiingize ubia na wale wanaotenda maovu. Hebu tujitoe kwenye hivi vitu na uchunge njia ziendazo moyoni. Jikite kwenye mambo yaliyo ya kweli,  yaliyo ya staaha, yaliyo ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, yaliyo na sifa njema, yaliyo na wema, yenye sifa nzuri, haya ndiyo uyatafakari.  Taifa haliwezi likaweka sheria eti mtu aache uovu wa ngono. La! Bali waumini wenyewe ndio wanatakiwa waamke na kuacha kuangalia mikanda, runinga, vitabu na yoyote yale ya uovu. Watu wengi hudai kuwa ni waumini ila kauli hiyo ni tofauti na yale wanayoweka kwenye bongo zao. Ikiwa waumini wa dini zote watakataa kununua mikanda, vitabu, au mambo kama haya yatakosa soko. Mambo haya yanaweza kufa tu usipoyapa lishe (starve to death). Usiweke mafuta ya taa kwenye moto huu. Ayubu alisema “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana?” (Ayubu 31:1). Macho na masikio yetu vyapaswa vilindwe ili tuwe na usafi. Runinga leo ina upuzi mwingi, ambapo watu waovu ndiyo mashujaa (heros). Nashauri endapo una ulevi wa kuangalia runinga hata kwa vipindi vyake visivyofaa iweke mbali na wewe au iuze, na tumia muda uliokuwa unaupoteza kwenye runinga kwa kufanya mengine yenye manufaa zaidi. Jifunze kushona, kupiga kinanda, au useremala. Wengine hudhani ni lazima watazame kila kilichopo kwenye runinga ili waelewe mambo yanayoendelea duniani kisha wachague. Chukua muda kujaza bongo yako na Neno la Mungu, ili uepuke dhambi hizi. Kama wewe ni kiongozi na una shida hizi unapaswa umshirikishe mtu atakayekusaidia kuwajibika ili usirudi tena kule Misri. Kama humjui mtu tuandikie tukukutanishe na watu watakaokusaidia.

PALILIA UPENDO:
Fanya juu chini ili familia yako, marafiki zako na wewe mwenyewe mwondoke kwenye hichi kifungo. Malaika na Mwenyezi Mungu nao pia watafurahi. Upendo si ngono, upendo ni kanuni toka kwa Mungu. Inakuja na upendo endapo inakuwa mahali pake. Endapo umesoma makala haya na badala ya kukuongezea matumaini imekukatisha tamaa nakusihi usikate tamaa.  Mungu yuko kwenye mchakato wa kukusaidia utoke kwenye utumwa ili utawale mwili wako, uwe na nidhamu na kujiheshimu na kuheshimu wengine. Kufanya yale Mwenyezi anayotaka ni kujitoa muhanga na si kitu cha kujilegeza. Upendo au mahaba ya kweli si upotofu, uzinzi au uchafu. Usiishi ukijipenda na kufanya makosa ukisingizia ni jinsi ulivyokuzwa au ulivyofanyiwa ubaya ukiwa mdogo, na sasa unalipiza na huwezi kutoka hapo. Uzinzi hauongezi furaha bali unapunguza. Endapo ndoa yako ina shida, usiende huko na huko, ikarabati, na tafuta msaada. Ukienda kwingine shida itakuwa pale pale. Mungu amefanya uwekezaji kwako, kwa Kukuumba kwa jinsi ya ajabu na kutisha. Wekeza kwenye ndoa yako pia. Mpende mwenzi wako mpaka kifo kiwatenganishe hata kama hastahili. Mungu naye anakupenda japo hustahili. Na kuna siku utapata matunda na upendo wa kweli kwa mwenzi wako. Upendo mara nyingi waleta huduma na kutunza wengine. Upendo wa ndoa waleta mtoto azaliwe na inahusisha kutunza na kuhudumia watoto. Upendo wa kweli hauna ubinafsi kwamba wewe ndiyo upate na kuridhika au kuwa na ubinafsi. Kile Mungu anatukataza tusifanye ni kwa ajili ya faida yetu, daima, ili tuishi maisha tele yenye furaha. Tukifanya upendo wa Mungu kuwa kanuni yetu, tunawekwa huru. Tunatolewa kwenye uhuru wa ngono na kupelekwa kwenye utajiri wa mahusiano unaofanya tuwe na kuridhika na upendo wa kweli unaopita uelewaji wa binadamu. Uchafuzi kwenye mwili ni mbaya zaidi ya uchafuzi wa mazingira. Kama umepoteza moto wa mapenzi kwenye ndoa yako anza kupalilia. Tunabadilisha hisia zetu kwa kubadilisha matendo au mienendo yetu.

MUNGU AWEZA KUTUSHINDIA:
Mungu aweza kututoa kwenye maisha ya uchafu na kutufanya tuwe vitu vya thamani kubwa tukimruhusu. Wazungu wana msemo “He can save from the uttermost and the guttermost”. Yaani aweza kutuokoa kutoka kwenye shimo kubwa la takataka tulilotumbukia la ngono potofu. Mungu ana mwisho mwema kwako hata kama umekuwa na talaka, unyanyasaji wa ngono, ulaghai, ulevi, ngono na jamaa wa karibu (incest). Atakutoa kwenye pipa la taka taka na pale senene au tunutu alipokula ataparudisha vizuri utakapomruhusu leo! Usingoje kesho, kesho. Dhahabu, mkaa na penseli inatokana na vinasaba vya ya hewa mkaa (Carbon.) Tofauti yake ni mpangilio. Leo Mungu aweza kupanga maisha yako ukimruhusu ukawa dhahabu badala ya mkaa. Kama umepoteza ubikira wako kwa kudanganywa au kwa kujiingiza kwenye maarifa yasiyofaa Mwenyezi Mungu ni msaada. Kama unatafuta upendo wa kweli na hujawahi kupendwa aidha na wazazi au mwenzi wako, usiwe na huzuni wala hofu. Mungu atanyosha mapito yako kwa namna wewe usiyoijua ila itakuleta furaha. 


Makala hii imeandaliwa na Grce Momadi – USA na kuhaririwa na Stephen Letta - Tanzania