Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

JUMA LA FAMILIYA

MASOMO KWA AJILI YA JUMA LA FAMILIA
Ikiwa hukufanikiwa kupata masomo ya juma la familia la mwaka huu waweza kutumia haya hapa. Mungu akubariki
 
Siku ya kwanza, February 11, 2017
Ndoa ya Kikristo na Msalaba – Sehemu ya kwanza
Somo hili limetayarishwa na Elaine na Willie Oliver
Fungu Kuu: Luka 9:23-24
“Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.”
 
Maisha ya kujikana nafsi.
Andiko la Luka 9:23-24 linaorodhesha maneno ya Yesu ya kusikitisha: “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.”
 
Muktadha wa Luka 9 unamkuta Ysu akiwa na wanafunzi wake huku akidhihirisha uwezo wake dhidi ya mapepo na magonjwa, akiwatuma hao wanafunzi kwenda kuhubiri habari njema ya injili na mwisho kupata uzoefu wa utume huo, ndipo Yesu akafanya muujiza wa kuwalisha watu zaidi ya elfu tano katika viunga vya mji wa Bethsaida.
 
Baada ya ombi la upatanishi, Yesu anarudi katika majadiliano na mitume wake na kuwauliza kile watu wanachosema kumhusu yeye. Swali hili lilichochewa na kile ambacho Herode aliuliza mapema katika sura hii. Watu wengine walikuwa wakihoji kama huyo Yesu ndiye Yohana mbatizaji ambaye amefufuka kutoka katika wafu, na wengine walidhani kuwa pengine ni Elia. Hata hivyo yeye alikuwa anataka kujua kuwa mitume walimdhania yeye kuwa ni nani na kwamba wao walisemaje kumhusu. Petro kwa kujibu hilo swali alisema “Ni Kristo wa Mungu”
 
Mazungumzo kati ya mitume na Bwana wao yaliwapeleka katika uhalisia wa kutafuta sababu ya Yesu kuja hapa duniani. Mazungumzo haya kimsingi yalihusu kuweka wazi kuwa uwezo wa mitume umetokana na Yesu kwa jinsi yalivyoshuhudiwa kwa namna ya ajabu katika kulisha lile kundi kubwa la watu. haikuwa ni kwa sababu ya faida binafsi au kwa namna ya kujisifu bali ilikuwa ni kupeleka ujumbe kwa ubinadamu uliopotea kwamba Mungu yupo upande wao na kwamba anajishughulisha na haja zao za kila siku. Zaidi ya haya, upeo wa kusudi la Yesu kuja duniani ulikuwa ni kuteseka na kufa ili kuwezesha uhai kuendelea, pia wao kama mitume wake nafasi yao ingekuwa pale pale.
 
 
Changamoto katika ndoa
Ndoa zina nafasi kubwa katika Maandiko Matakatifu. Katika kitabu cha Mwanzo, ndoa inajitokeza kama taasisi ya mwanzo kuanzishwa na Mungu katika uumbaji wa mwanamume mmoja na mwanamke mmoja. Katika kitabu cha Ufunuo, ndoa imetumika kama mfano ili kujadili uhusiano kati ya Mungu na watu wake. Katika sura ya pili ya Injili ya Yohana, Yesu anaonekana akifanya muujiza wa kwanza katika ndoa kule Kana ya Galilaya. Swala kuwa ndoa inajitokeza mwisho wa wiki ya uumbaji, linapendekeza kile ambacho Mungu alidhamiria kiwe kwa ajili ya wanadamu. Na hapa tunapokuta sherehe ya ndoa inajitokeza mwanzo wa huduma ya Yesu hapa duniani inadhihirisha jinsi swala zima la ndoa linavyochukuliwa na mbingu.
 
Changamoto moja kubwa katika ndoa ni kuwa Mungu alidhamiria kuwa ndoa iwe ni uhusiano utokanao na muunganiko wa kudumu kati ya mwanamume na mwanamke. Katika Mwanzo 2:24 Biblia inasema: “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Yesu akijadiliana na Mafarisayo kuhusu uwezekano wa talaka alinukuu Mwanzo 2 alipotamka katika Matayo 19:4-6: “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”
 
Ni nini kinafanya ndoa iwe ni changamoto? Kwa nini itawaliwe na mawazo ya talaka? Ndoa nyingi zinazoanza na shamra shamra na vifijo kwa sherehe kubwa mara nyingi zinaishia katika masikitiko miaka kadhaa, miezi michache au hata wiki kadhaa baada ya siku ya ndoa.
 
Muda mfupi uliopita tulipokea swali kutoka kwa mtu katika moja ya safu za magazeti tunayoandika. Swali lenyewe ni hili:
“Sikufikiri hili lingeweza kutokea kwangu, lakini nimejikuta bila furaha katika ndoa yangu. Mimi na mke wangu hatuwasiliani vema, na inapobidi inakuwa ni kwa kushambuliana kila mmoja akipaza sauti na hivyo kuchochea mivutano tu. Haionekani kama kuna mapatano, na matakwa yetu yametofautiana kabisa kiasi kwamba tunaafikiana katika mambo machache sana. Je, uhusiano usiopikika kama huu utadumuje? Uhusiano wetu hauna afya kwa watoto wetu. Siamini kama Mungu anatazamia kwamba niendelee kukaa katika uhusiano usio na furaha kama huu. Wewe unafikirije?”
 
Swali zuri hili, au siyo? Wengi walio katika ndoa wanauliza swali hili kwa sauti au wakati mwingine kimya kimya. Tunajiuliza kuwa ni nini kilichotokea kwa ule ukaribu na msisimko uliokuwa dhahiri kabla ya ndoa, ambao wakati mwingine ulikuwa ni kama unadhalilisha ndugu na marafiki hasa wawili wapendanao wanapoonesha hadharani.
Kinachotokea ni kuwa watu wanapochumbiana na kukutana, mara nyingi hisia chanya zinavutana na zile hasi. Kwa upande mwingine katika ndoa hisia chanya zinapingana na zile hasi. Hii ndio inafanya kwa sehemu kubwa ndoa ni changamoto. Kama wenye dhambi sisi kwa asili tu wabinafsi. Huwa tunapenda maoni yetu wenyewe, na kwa kweli huwa tunataka kila kitu kiende vile tunavyotaka. Biblia inasema katika Isaya 53:6 kuwa “Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.”
 
Inachukua wiki chache au miezi baada ya kulewa upendo katika mwezi wa asali (honeymoon), ndipo wanandoa wanapoanza kukosa uvumilivu na kuwaona wenzi wao kama kero. Kila mmoja anageukia upande wake
 
 
Siku ya Pili – February 12, 2017
Ndoa ya Kikristo na Msalaba – Sehemu ya pili
 
Chaguzi katika ndoa
Mungu aliumba ndoa kwa ajili ya furaha yetu. Ili ndoa na maahusiano mengine yastahimili, ni lazima kufuata kanuni alizotoa Mungu. Katika Wagalatia 5:22-23 Biblia inatamka: “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
Hebu tafakari kuhusu haya mafungu. Ikiwa kanuni hizi (au tunda hili) zinafanya kazi katika mahusiano yetu – hasa katika ndoa – huku kuna tofauti za maoni, matashi, vionjo n.k. kuleta uzoefu unaozaa tunda analosema Paulo kutatuweka katika hali ya kushughulikia tofauti zetu kwa upole na wema badala ya hasira, chuki na ukali.
Hatuna ndoa mfano katika Biblia ila ile ya Adam na Hawa kabla ya anguko, zingine zote hazikuwa kamilifu. Ili tuwe na ndoa ya Kikristo ni lazima tuchague kuwa katika ndoa ya Kikristo ambayo inafanya kazi tu pale tunapotumia tunu za kiroho tulizopewa na Mungu katika Biblia. Kuchagua ndoa ya Kikristo ni kama kuchagua kuwa Mkristo. Huu ni uamuzi ambao lazima tuufanye kila siku, kama vile kula chakula au kupumua ili tubakie hai, wenye afya, na imara. Ili ndoa ibakie na mng’ao na kuendelea kuwa hai, wale walio katika ndoa lazima wailee ndoa yao la sivyo itafubaa na kufa.
 
Kufanya chaguzi zilizo nzuri katika ndoa, ni kuchagua kuweka katika uzoefu mashauri yaliyopo kwenye Waefeso 5:15-17 yanayosema: “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.” Pia katika Mithali 1:5 yanayosema: “mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.”
 
Ellen White anatoa mashauri kuhusu uhalisia wa ndoa na chaguzi ambazo wenzi lazima wafanye ili kuimarisha muunganiko wao kama ifuatavyo:
“Huba au upendo unaweza kuwa dhahiri kama kioo na wa kupendeza kwa usafi wake lakini unaweza ukawa hauna kina kwa sababu haujajaribiwa na kupimwa. Mfanye yesu kuwa wa kwanza na wa mwisho na bora kuliko vitu vyote. Mwangalie kwa uthabiti ndipo upendo wako kwake utakuwa wa kina na imara kadiri unavyopimwa na majaribu, kadiri upendo wenu kwa kila mmoja unavyokuwa na kuimarika”
 
 
Wajibu katika ndoa
Wajibu ni msingi unaokidhi na kuleta afya katika ndoa. Ni uamuzi ambao kila mwana ndoa anatakiwa kuufanya ikiwa anahitaji kubaki akiwa ameoa au ameolewa. Ndoa ya Kikristo kwa muktadha huu sio mfano wa ndoa wanazoingia na kubakia katika mvutano wa muda mrefu. Kila mmoja ni lazima aamue upeo wa mawasiliano ambao utaandamana na upeo wa maridhiano katika ndoa hiyo.
Ndoa kama uhusiano mwingine wowote katika maisha zina changamoto za mabadiliko. Mara nyingi tunasema hakuna ndoa iliyo kamilifu kwa sababu hakuna watu wakamilifu. Kwa hiyo hatuwezi kusema ukamilifu ni neno jingine la wajibu. Hata hivyo ni lazima wajibu uwepo ili ndoa iwe hai kama vile tu hewa inavyohitajika ili uhai uendelezwe.
 
Mtafiti wa familia na ndoa aitwaye Scott M Stanley anapendekeza aina mbili za wajibu: ule wa kujitoa na wa shuruti wenye mipaka. Wajibu wa kujitoa ni kama kuwajibika kwa hiari katika mradi fulani au kwa mtu fulani. Wajibu huu unaonesha hitaji au tamanio la mtu na utashi katika kuhakikisha kuwa kitu fulani kinatokea au kinafanyika. Kwa upande mwingine wajibu wa shuruti ni kama sharti ambalo lazima litimizwe kiasi kwamba kama halikutimizwa inaweza kuonekana kama balaa vile.
 
Wakati wajibu wa kujitoa ni kama mvuto fulani unaokuvuta kusonga mbele, ule wa shuruti ni kama nguvu fulani inayokusukuma kutoka nyuma. Wajibu wa kujitoa unafanya kazi katika maelezo ya Paulo katika 1 Wakorinto 13:4-8 akisema:
“Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; Bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.”
 
Kila uhusuiano wa ndoa unahitaji aina mbili hizi za uwajibikaji. Kadiri uwajibikaji wa kujitoa unvyoongezeka ndivyo uwajibikaji wa shuruti unavyohitajika na hivyo kuongezeka kwa upeo wa maridhiano katika ndoa. Nyakati ambazo uwajibikaji wa kujitoa unapopungua, ule wa shuruti utawawezesha wanandoa kuvuka katika bonde la uvuli wa uhusiano ambalo mara nyingi linajitokeza katika ndoa. Hata hivyo kila mmoja wa wanandoa anatakiwa kuwajibika kwa kujitoa kwa haraka iwezekanavyo ili kwamba ndoa iwe kama ushauri wa EGW ulivyo, yaani “mbingu ndogo hapa duniani…”
 
Hitimisho
Wote tunafurahia chakula! Na pale tunapodhamiria kuwa na kiasi sio kwa kile tunachokula tu, bali jinsi tunavyokila, ni kweli pia kwamba tunafurahia kula aina fulani ya chakula kuliko wengine, na hata kukila mara nyingi kuliko kingine.
Tunapoamua kula aina fulani ya chakula – ni aina gani hiyo ya chakula – baada ya kuwa barabarani kwa siku kadhaa na baadaye kujikuta nyumbani, huo ndio wakati wa kudhihirisha ubora wa ndoa zetu. Hiki ndicho kipimo kikuu cha kuonesha uzoefu wa kile tunachohubiri na jinsi tulivyo karibu na Yesu na kubakia karibu naye.
Ukweli ni kwamba ndoa ya Kikristo inaweza tu kuwa ya Kikristo pale ambapo sisi kama mitume wa kweli tutabeba misalaba yetu na kumfuata Yesu katika hali ya kujikana nafsi na kuwa kama Yeye katika kila namna. Kuwa tu mshiriki wa kanisa aliyebatizwa haitoshi kuwezesha ndoa zetu kuwa zenye afya na imara.
 
Kutambua kwamba ili uwe mwanafunzi wa Yesu kunamaanisha kuwa umejiorodhesha ili utumike katika kuhudumia badala ya kuhudumiwa; na unatafuta kile unachoweza kutoa badala ya kile unachoweza kupokea, hii ndiyo siri ya kuwa na ndoa iliyojawa na uwajibikaji wa kujitoa ambao unamwakilisha Yesu Kristo bila aibu.
Panapokuwa na zahama katika ndoa, maana yake ni kuwa kuna zahama ya kiroho, bila kujali umehusika katika masomo mangapi ya Biblia au ni watu wangapi umewaongoza katika ubatizo. Hata hivyo unapoitizama ndoa yako katika nuru ya msalaba, utaichukulia kwa hiari katika mtindo kama wa Kristo, ndipo utakapopata uzoefu wa furaha inayotokana na kumwamini Yesu ili akufanyie kile ambacho hauwezi kufanya peke yako. Hii ndiyo aina ya ndoa itakayokuwa pambo kwa mwenzi wako na kwa watoto wako na kwa kila mmoja utakayegusana naye katika mduara wako wa mvuto.
 
Kadiri unavyokusudia katika moyo wako leo kubeba msalaba wako, ni ombi letu kwamba ndoa yako ipitie uzoefu wa uwezo ubadilishao na kuleta furaha, amani na upendo. Kwa maneno ya wimbo wa Yohana Hugh McNaughton (aliyeishi kuanzia 1829 hadi 1891),
 
UPENDO NYUMBANI
Katika kibanda kuna furaha, panapokuwa na upendo nyumbani; chuki na wivu haviwezi kukasirisha. Panapokuwa na upendo nyumbani, waridi huchanua chini ya miguu yetu, bustani zote za ulimwengu zinatema utamu, zikifanya maisha yawe ni furaha kabisa. Panapokuwa na upendo nyumbani, upendo unakuwa ndiyo namna ya kuishi, panapokuwa na upendo nyumbani, panakuwa na mwisho mzuri wa mvutano, panapokuwa na upendo nyumbani, kila mmoja anajitoa kwa mwenzake kama zawadi, kiapo cha hiari kkupenda na kutegemeza, manukato yaponyayo kila ufa, panapokuwa na upendo nyumbani, hasira hutulizwa na misongo kukoma, panapokuwa na upendo nyumbani; watoto wanajifunza kuishi kwa amani, panapokuwa na upendo nyumbani; panakuwa na ujasiri wa kuifikia neema, na kukutana na mtu usiyemjua uso kwa uso, na kutafuta mahali pa suluhu, panapokuwa na upendo nyumbani; hakuna swali usiloweza kuuliza, panapokuwa na upendo nyumbani, tunashiriki furaha mahali pa kazi au pa michezo, panakuwa na ujasiri kukabili siku, kutambua kuwa upendo utaonesha njia, panapokuwa na upendo nyumbani.
 
Itikio:
Upendo nyumbani, upendo nyumbani; kutambua kuwa upendo uaonesha njia, panapokuwa na upendo nyumbani.
Ombi letu ni kuwa tunapofikia mwisho huu, Mungu na awabariki.
 
 
Siku ya Tatu – February 13, 2017
Mpango wa Mungu kwa wazazi na waoto – sehemu ya kwanza
Somo hili limetayarishwa na Elaine na Claudio na Pamela Consuegra
Fungu kuu: Mithali 4:10
“Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi.”
 
Utangulizi
Biblia ni kama ramani ya barabara, na Mungu ametupatia ramani hii ili tupate mwelekeo ulio bora kutuwezesha kufaulu kufika salama mahali alipotutayarishia. Mwisho wa barabara hiyo hapa duniani ni familia nzuri na yenye afya.
 
Yesu alituambia katika Yohana 10:10 kuwa, “…mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Mungu anaridhika kuona uhusiano wa familia zetu ukiwa imara na wenye afya. Lakini bado kunakuwa na talaka – hata kanisani. Vitendo vya udhalilishaji vinaendelea kutendeka – hata katika makusanyiko ya Waadventista wa Sabato.
Wazazi bado wanakabiliana na changamoto na watoto wao. Kuna wazazi wanaoamua kutoa mimba. Pia kuna watoto wanaopitia udhalilishaji wa hali ya juu. Katika nchi nyingine watoto wanawashtaki wazazi wao, na pia tuanasoma hadithi za watoto kuwaasi na kuwabishia wazazi wao.
 
Mtume Paulo anaelezea hali ya dunia nyakati za mwisho akisema, “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;” 2 Timoteo 3:1-4
 
Kadiri tunavyopitia orodha hii, tunatambua tabia hasi zinazoelezea mahusiano ya dunia yetu hii. “Wenye kiburi, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani,, waiowapenda wa kwao, wasiosamehe, wakaidi.” Je, haya siyo tunayoyaona yakifanyika katika familia nyingi leo hii?
Ni dhahiri pia kuwa sio kwenye familia za watu wasiomjua Mungu tu, inatokea katika familia za watu wenye kawaida ya kwend kanisani kila mara. Baada ya Paulo kuandika orodha hii akielezea hali ya watu nyakati za mwisho, anaongezea maneno yafuatayo: “wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.” 2 Timoteo 3:5
 
Paulo anasema watu wa dini, au watu wa kanisani watakuwa na uzoefu huu kati yao. Ndiyo maana ni muhimu kwamba usiwe tu mtu wa dini, lakini uwe mtu wa kiroho. Mtu wa dini ni yule ambaye anatimiza majukumu ya kidini; lakini anafanya hivyo tu kwa nje. Mtu wa kiroho ni yule ambaye anaamini kutoka moyoni na yule ambaye mwonekano wake wa nje wa kidini unatokana na ushawishi wa ndani ya moyo wake. Na hii inadhihirika kutokana na tunavyoshirikiana kila mtu na mwenzake kama wazazi na watoto.
Ili kutusaidia kama watu wa kiroho, Biblia imetupatia miongozo kadhaa ya mahusiano. Hizi ni amri zinazodhamiriwa kutusaidia kujenga mwongozo wa msingi na mwonekano wa msingi wa kuishi katika mahusiano na wengine. Hii miongozo ya mahusiano tunaipata ikiwa imetapakaa katika maandiko matakatifu katika vipengele kadhaa. Baadhi ya vipengele hivyo vinahusu uhusiano kwa ujumla katika upana wake na baadhi vinalenga watu wa aina fulani katika mahusiano mahususi kwa mfano wenzi waliooana, wazazi, watoto, majirani, au marafiki.
 
Mfano wa kipengele cha mwongozo wa mahuhsiano kwa ujumla katika upana wake ni kanuni kuu iliyoelezewa katika Matayo 7:12 “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.”
 
Kuna miongozo kadhaa inayohusu jinsi wazazi na watoto wao wanavyoweza kuhusiana. Hebu tuangali miongozo mine katika hiyo mingi inayoelezewa:
1. Watoto wawaheshimu wazazi wao
Mwongozo mmojawapo unaojulikana kwa watoto unatokana na amri kumi, katika nusu ya pili ya hizo amri inayoshughulikia mahusiano. Amri ya kwanza katika nusu hii ya pili ya amri inasema “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.” (Kutoka 20:12)
Mtume Paulo anadokeza jambo la muhimu kwamba “…amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,” (Waefeso 6:2) Waheshimu baba yako na mama yako! Kuwaheshimu baba yako na mama yako kuna maana gani? Tunafanyaje ili kukamilisha hilo?
 
Tunawaheshimu baba zetu na mama zetu kwa kuonesha heshima kwa maneno yatu na matendo yetu na kuwa na nia ya dhati kutoka ndani ya kuthamini nafasi zao.
Neno la Kiyunani linaloelezea ‘kuheshimu’ lina maana ya “kumchukulia mtu kwa heshima ya juu, kumthamini au kumuenzi”
[HAPA UNAWEZA KUTOA HADITHI ITAKAYOKUWA KAMA KILELEZO CHA KANUNI HII]
 
Turudi tena kuangalia, ni kwa jinsi gani unaweza kuwaheshimu baba yako na mama yako? Sulemani yule mtu mwenye hekima aliwaasa watoto kuwaheshimu wazazi wao kama tusomavyo katika Mithali 1:8; 13:1; 30:7
Ingawaje tunaweza tusiwe chini ya mamlaka ya wazazi wetu moja kwa moja, bado hatuwezi tukapuuzia amri ya Mungu ya kuwaheshimu. Hata Yesu, ambaye ni Mungu Mwana, aliwaheshimu wazazi wake wa hapa duniani kama tusomavyo katika Luka 2:51, “…naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.” Pia baba yake wa mbinguni kama tusomavyo katika Matayo 26:39 “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”
 
Basi tutakuwa tunafuata mfano wa Kristo tunapowatendea kwa heshima na kwa namna ambayo tungetenda tunapomkabili Baba yetu wa mbinguni. (Tizama pia Waebrania 12:9 na Malaki 1:6). Uwaheshimu kwa matendo na mwenendo (Marko 7:6), heshimu matakwa yao yaliyotamkwa na yale ambayo hayakutamkwa kama Sulemani asemavyo katika Mithali 13:1 “Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo”
EGW anadokeza kuhusu amri hii na kusema, “Ni wajibu katika utoto, ujana, umri wa kati na kwa wenye umri mkubwa. Hakuna kipindi cha maisha ambapo mtoto anaondolewa wajibu wa kuwaheshimu wazazi wake. Jukumu hili nyeti linamfunga mtoto yeyote awe wa kiume au wa kike, na hii ni mojawapo ya sharti la kuishi maisha marefu katika nchi ambayo Mungu atawapa waaminifu” (White, 1952, uk. 292)
 
Mchungaji aitwaye Mark Driscoll alishiriki hubiri, “Kuheshimu maana yake ni kutoa heshima, kujikabidhi, au kujitoa.” Maana yake hasa ni kuonesha upendo na kujali na kuvutiwa na wazazi. Heshima ni kitu kinachoanzia ndani ya moyo na kudhihirika nje. Unapokuwa na heshima moyoni, inadhihirika kwa maneno yako.
2. Watoto kuwatii wazazi wao
Mwongozo wa pili unahusu jinsi watoto wanavyohusiana na wazazi wao. Waefeso 6:1 panasema: “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.”
[HAPA TENA UNAWEZA KUTOA HADHITHI YA UTII KWA WAZAZI]
 
Wazazi wanawatakia mema watoto wao. Wanapowaonya au kuwazuia kitu fulani, hufanya hivyo kwa ajili ya wema na mafanikio yao. EGW anatoa tamko anapoandika kuwa:
Sababu moja kubwa inayosababisha kuwepo kwa maovu mengi katika dunia leo hii ni kwa sababu wazazi wamejaza fikra zao na mambo mengine kuliko yale yaliyo muhimu – jinsi ya kujizoeza katika kazi ya kuwafundisha na kuwaelekeza watoto wao kwa uvumilivu nja za bwana. Ingewezekana pazia kuondolewa, tungeona kwamba watoto wengi waliopotoka wamekosa mivuto mizuri iliyozembewa na wazazi wao. Kwa wazazi hakuna kazi iliyo muhimu kiasi cha kuwazuia kuwapa watoto wao muda wao wote ambao ni muhimu kuwafanya waelewe maana ya kutii na kumwamini bwana kikamilifu.” White, 1952
 
Asili na matokeo ya utii kwa wazazi ni muhimu kiasi kwamba Biblia imeyaorodhesha. Kati ya hayo matokeo tunakuta:
• Wakolosai 3:20 “Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana.”
• Waefeso 6:1 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.”
• Mithali 1:8 “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,”
Maagizo ya kwanza mawili yanatupa maelekezo yaliyo dhahiri ya namna watoto wanavyoweza kuhusiana na wazazi wao. Kuwaheshimu, kuwatii, ni kanuni za msingi kabisa katika maagizo haya mawili.
 
 
Siku ya Nne – February 14, 2017
Mpango wa Mungu kwa wazazi na watoto – sehemu ya pili
3. Wazazi kuwafundisha watoto wao.
Biblia haitoi maagizo upande mmoja tu – jinsi watoto wanavyotakiwa kuhusiana na wazazi wao, bali pia jinsi wazazi wanavyopaswa kuhusiana na watoto wao. Agizo la tatu linapatikana katika kitabu cha Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” Kwa sehemu kubwa fungu hili limeleta mkanganyiko na kutokuelewana kwa wazazi wakati mwingine. SDA Commentary inapanua upeo wa uelewa kwa kusema:
 
Wazazi wengi wamechukulia hili fungu kama kibali cha kuwalazimisha watoto wao kufuata taaluma au fani wanazofikiria au kuona zinafaa. Kwa kufanya hivyo wameleta masikitiko na huzuni kwao wenyewe kwa kuwa watoto wanapokua mara nyingi huenda kinyume kabisa na matarajio ya wazazi. Fungu hili linawaasa wazazi kujifunza njia ambazo watoto wao wanatazamiwa kuwa wa msaada kwao wenyewe na kwa wengine pia kwa namna itakayowaletea furaha. Kituo halisi kilichochaguliwa na mbingu kwa ajili ya mwanadamu katika maisha kinaamuriwa na uwezo wake. Mungu amepanga mahali kwa kila mwanadamu katika mpango wake mkuu.
 
Kisha mungu pia amemsheheni mwanadamu na uwezo unaohitajika ili kujaza nafasi fulani katika maisha haya. Kwa sababu hiyo uchaguzi wa nini mtu afanye katika maisha yabidi uwe sawa sawa na hitaji la mtu mwenyewe. Jitihada za wazazi na za mtoto yabidi zielekezwe katika kugundua aina ya kazi ambayo mbingu imepanga. Uvuvio unaeleza kuwa fungu hili linawaagiza wazazi “kuelekeza, kuelimisha na kukuza” lakini ili kufanya hivi, “ni lazima wao wenyewe waelewe njia ambayo mtoto anapaswa kuiendea” Nichol, 1977
Wakati mwingine wazazi wanawataka watoto wao wafuate nyayo zao. Mwalimu anataka mwanae naye awe mwalimu, mwanasheria naye anataka binti yake awe mwanasheria. Daktari anataka mwanae naye awe daktari, fundi seremala naye vivo hivyo. Wazazi wanaweza kuwasukuma watoto wao kuwa kile wanachotaka wawe, lakini hatuna uwezo wa kufanya hivyo.
 
Inawezekana katika mchakato huo wakazima njozi na matakwa ya baadaye ya watoto wao. Hii ni kwa sababu watoto wana haiba tofauti, talanta, na utashi ambavyo vinaweza kuwa tofauti na wazazi wao. Mwisho wanaweza kuishia katika kuchanganyikiwa kwa sababu wameshindwa kuendeleza kile walichotamani.
Kama wazazi tunahitaji kuelewa kwamba wajibu wetu wa kwanza na wa muhimu ni kuwaongoza watoto wetu kwa Mungu. Hiki ndicho kiwe kiini cha malezi yote badala ya kuwasukuma watoto katika tasnia tunayopendelea kama wazazi. Hapa chini kuna sehemu ya maandiko iitwayo Shema kwa kiyahudi inayokaririwa kila asubuhi:
“Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, bwana ndiye mmoja. Nawe mpende bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.” (Kumbukumbu la Torati 6:4-7)
 
Mtume Paulo anaongeza kuwa “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.” Waefeso 6:4 Mlee mtoto wako kupitia mfano wako mwenyewe. Kama gari moshi lilivyo na kichwa (injini) na mabehewa yote yanafuata kile kichwa, watoto wako watakufuata popote unapowaelekeza. Hivyo waongoze kwa mfano mzuri. Wafundishe kwa uvumilivu, upole na upendo mwingi.
 
Wafundishe kuwa na elimu iliyo bora ya uelewa wa Biblia. Wafundishe kufanya maombi kuwa ni tabia ya kila siku. Wafundishe kuhudhuria katika huduma za kanisani kila mara na kujishughulisha na maisha ya huduma kanisani. Wafundishe kutegemeza kanisa kwa muda wao, talanta zao, na hazina zao.
 
Wafundishe watoto wako kuwa watiifu kwa Mungu na kwa wazazi wao. Wafundishe kuzungumza kwa uaminifu. Fundisha watoto wako kumfahamu Mungu na kumwamini, kumpenda na kumshiriki na wengine, na mwisho wafundishe kuishi kwa ajili ya Mungu.
 
4. Wazazi kutokuwachokoza watoto wao.
Katika Agano Jipya, kuna agizo la mwisho tutakaloangalia.
“Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” (Wakolosai 3:21). Paulo aliyaandika haya maneno kwa kanisa la Kolosai, lakini aliwaandikia pia Waefeso maneno kama haya haya: “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.” (Waefeso 6:3). Katika nukuu za machapisho ya Ellen G. White kwenye kitabu kiitwacho “Child Guidance” EGW anadokeza dondoo muhimu kuhusu agizo hili la Biblia: akielekeza katika maneno yaliyotumiwa na Paulo kwa kanisa la Efeso, anatoa mfano wa jinsi wazazi wanavyowachokoza watoto wao kwa kusema:
 
“Mara nyingi tunavuka mipaka kwa kuwachokoza watoto badala ya kuwashinda. Nimewahi kumwona mama mmoja akimnyang’anya mtoto kitu mkononi kilichokuwa kinamfurahisha. Mtoto hakufahamu sababu ya kunyang’anywa na kwa hali ya kawaida ya kibinadamu alijisikia kuwa amedhalilishwa. Ndipo ugomvi ukafuata kati ya mzazi na mtoto, na adhabu ilihitimisha tukio hilo kwa jinsi ilivyoonekana kwa nje. Lakini nina uhakika mgogoro huo uliacha jeraha ndani ya fikra changa za yule mtoto ambalo ni vigumu sana kuliondoa. Huyu mama hakufikiria matokeo ya kile alichofanya na akatenda bila hekima. Jinsi alivyoshugulikia swala hilo kwa ukatili ilimsumbua yule mtoto na kwa tendo jingine kama hilo hisia hizo zinaamshwa na kuimarishwa.” (WHITE, 1954)
 
Wakati mwingine wazazi wanatumia muda mwingi wakitafuta makosa ya watoto wao katika kila jambo wanalofanya. Hebu sikiliza haya maneno:
“Hauna haki ya kuleta kiwingu juu ya furaha ya watoto wako kwa kutafuta makosa na kukuza vijikosa vidogo ili kupata sababu ya kugombeza. Kosa halisi na lioneshwe kwa ubaya wake na kukemewa kwa uimara wote, na njia itafutwe kuhakikisha kuwa halitokei tena. Hata hivyo watoto wasiachwe katika hali ya kukata tamaa bali kwa kiasi fulani na watiwe moyo kuwa wanaweza kuwa bora zaidi na kuteka tena ukubali wa mzazi. Watoto wanaweza kuwa wanatamani kufanya vizuri au wanaweza kudhamiria ndani yao kuwa watiifu, wanahitaji kusaidiwa na kutiwa moyo.” (WHITE, 1954, UK. 259)
 
Ninayapenda maneno hayo ya mwisho: “Watoto wanaweza kuwa wanatamani kufanya vizuri, au wanaweza kudhamiria ndani yao kuwa watiifu, wanahitaji kusaidiwa na kutiwa moyo.”
Tunawatia moyo kutafuta namna ya kutumia muda kusoma sura ya 48 ya kitabu hicho mahali ambapo EGW anatuambia kama wazazi tusiwe wakali sana katika jinsi tunavyowatia nidhamu watoto wetu. Tusiwalaani na kuwafaya waone huzuni kwa ajili ya matendo yetu.
 
Hitimisho
Kuna maagizo mengi ndani ya Biblia yanayofundisha jinsi ya kuhusiana na wenzi wako kama wazazi na watoto. Leo tumeangalia mambo manne:
Kwa watoto Biblia inasema (1) “Waheshimu baba yako na mama yako” na (2) “uwatii wazazi wako” Kwa wazazi, Biblia inasema (“Mlee mtoto wako” na “Msiwachokoze”
Mungu anatamani kwamba tuwe na mahusiano yaliyo chanya, mazuri, na yenye afya na watoto wetu. Anataka tuakisi uhusiano tulio nao naye.
[HAPA TENA UNAWEZA KUTOA HADITHI PENGINE HATA YA KWAKO MWENYEWE KATIKA KUHITIMISHA SOMO HILI]
Kuna hadithi ya mtu ambaye alikuja nyumbani kutoka kazini usiku, akiwa amechoka na kusumbuliwa huko alikotoka. Kufika akakuta mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano anamsubiri mlangoni. Maongezi yao yalikuwa kama ifuatavyo:
KIJANA: “Baba, naomba nikuulize swali”
BABA: “Swali gani mwanangu?”
KIJANA: “Baba, unalipwa kiasi gani kwa saa?”
BABA: “Hiyo haikuhusu, kwa nini unauliza maswali kama hayo?” aliuliza kwa hasira
KIJANA: “Nilitaka tu kufahamu. Naomba uniambie, unalipwa kiasi gani kwa saa?”
BABA: “Ikiwa ni lazima ufahamu, ninalipwa dola 30 kwa saa.”
KIJANA: “Ahaa!” huyu mtoto akaitikia huku ameinamisha kichwa chake.
KIJANA: “Baba, naomba uniazime dola moja”
Baba yake alikasirika, huku hasira ikidhihirika katika sauti yake alimwambia kijana, “Ikiwa ndio sababu iliyokufanya uulize maswali ili uazime fedha ukanunue ki-mdoli cha kijinga au mambo mengine ya kipuuzi, ondoka mbele yangu na nenda moja kwa moja hadi chumbani kwako kalale sasa hivi.”
 
Kale kakijana kaliondoka kimya kimya na kwenda chumbani kwake huku kakifunga mlango nyuma yake. Baada ya yule mzazi kutulia, alianza kufikiria upya. Pengine kuna kitu hasa ambacho yule mtoto alitaka kununua kwa kutumia dola moja aliyoiomba kwani alikuwa hana kawaida ya kuomba pesa.
Basi akaenda hadi penye mlango wa chumba cha mtoto wake na kumuuliza
“Umelala mwanangu?”
“Hapana baba nipo macho” alijibu kijana.
“Nimekuwa nikifikiria, pengine nimekuwa mchungu kwako, lakini hii hapa dola uliyotaka”
Yule mtoto akaamka akakaa huku akitabasamu:
“Ooh, Asante sana baba” alishangilia, kisha akapitisha mkono chini ya mto wake na kutoa bulungutu la noti za dola moja moja na kuunganisha na ile baba yake aliyompa. Mzazi wake alipoziona na kugundua kuwa mwanawe alikuwa tayari ana fedha, alikasirika tena.
Yule mtoto akazihesabu tena taratibu kisha akamwangalia baba yake. Maongezi yakaendelea kama ifutavyo:
“Kwa nini ulitaka fedha ikiwa ulikuwa unazo zingine?”
“Kwa sababu zilikuwa hazitoshi, lakini sasa zinatosha.” Alijibu kijana.
“Baba sasa nina dola 30, hivi… ninaweza kununua lisaa limoja katika muda wako? Tafadhali uje nyumbani mapema kesho, ningependa tule chakula cha jioni pamoja”
Yule mzazi akatekewa, mara akapitisha mkono wake mabegani mwa yule mtoto, akamkumbatia, na kumwomba msamaha. Wazazi hebu tuwapende watoto wetu na kuwafundisha badala ya kuwachokoza. Tutenge muda kwa ajili yao.
Watoto wa umri wote, hebu wapendeni wazazi wenu na kuwaheshimu huku mkiwatii katika Bwana.
Hebu mahusiano yenu siku zote na yawe ya kuheshimiana, kupendana, na kujaliana huku kila mmoja akijifunza kutoka kwa mwenzake.
Amina.
 
 
Siku ya Tano – February 15, 2017
Kujenga ndoa na Familia – Sehemu ya Kwanza
Somo hili limetayarishwa na Trafford Fischer
Fungu Kuu: Nehemia 4:14
“Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho;”
 
Agano la Kale linaorodhesha matukio kadhaa ya wafalme wa Babeli na wale wa Uajemi kuchukua wakazi wa Yerusalemu kama mateka. Hatufahamu majina ya wote ambao walilazimishwa kuyaacha makazi yao ila vijana Danieli, Shadraki, Meshaki na Abednego waliochukuliwa na Nebkadreza mfalme wa Babeli pamoja na mateka wengine. Nehemia alichukuliwa na mfalme wa Uajemi na kupelekwa Shushani.
 
Tunafahamu pia kuwa hawa waliotajwa hapa walichaguliwa kuwa viongozi katika jumuiya yao mpya ingawaje walikuwa watumwa tena mateka. Haijulikani hili lilitendekaje na ni kwa nini bali Nehemia alichaguliwa kuwa mnyweshaji wa Mfalme. Yawezekana kabisa kuwa mfalme alimwona kama mateka mwaminifu.
Siku moja mmoja wa ndugu zake Nehemia aitwaye Hanani ambaye alikuwa bado anaishi Yerusalemu aliwasili Shushani pamoja na watu wengine kumtembelea Nehamia. Nehemia akawauliza mambo yalivyo huko nyumbani Yerusalemu, taarifa walizompa hazikuwa nzuri. Wakajibu na kusema, “Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto.” (Nehemia 1:3)
 
Nehemia aliupenda Yerusalemu, na hivyo taarifa hizi zilimhuzunisha. Alikaa chini na kulia, na kuomboleza siku kadhaa, kisha akafunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni. Nehemia hakuwahi kuonekana mwenye huzuni mbele ya mfalme. Aliporudi katika utumishi wake, mfalme alimwambia: “Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.” (Nehemia 2:2)
 
Mfalme alikuwa na utambuzi wa hali ya juu, kipawa cha ajabu – kuweza kutambua mtu anapokuwa na huzuni na kumtia moyo au kushiriki huzuni yake. Mara nyingi tunashikika na mahangaiko ya hapa na pale kiasi kwamba hatugundui hata mtu anapokuwa na maumivu. Kwa haraka haraka tunampita tu bila hata kutambua maumivu aliyo nayo. Tunasema tu ‘mambo?’ na kupita bila kuulizia hali yake au kumtathimini mtu kwa kumwangalia machoni, au mikunjo usoni, au hata machozi yakimlengalenga. Tunahitaji kumwomba Mungu atusaidie tuwe kama mfalme wa Uajemi – kuwa na silika ya kuwaambia wale walioumizwa – ‘mbona una huzuni, na haionekani kama u mgonjwa – yawezekana una jambo moyoni,’ na kumpatia faraja au msaada upasao.
 
Kwa hofu na kutetemeka, Nehamia akamwambia mfalme jinsi mambo yalivyo huko Yerusalemu, na mfalme akamuuliza kuwa angependa amfanyie nini. Nehemia akajibu kwamba angependa kurudi na kuujenga Yerusalemu. Ni jambo la kushangaza kwamba mfalme alimruhusu na kumwambia arudi kama alivyoomba na kufanya vile alivyotaka. Zaidi ya ruhusa, alimpatia Nehamia barua zilizoelekezwa kwa viongozi wa kiserikali katika majimbo yale zikihakikisha usalama wake kwa kuagiza apewe viongozi wa jeshi lake ili kumlinda. (Nehemia 2:6-10)
 
Kwa hiyo Nehamia akaondoka kuelekea Yerusalemu na baada ya siku tatu akachukua watu watatu akaambatana nao kwenda kukagua mji. Akagundua kuwa taarifa alizoletewa na ndugu zake wa uhamishoni zilikuwa sahihi kabisa. Kuta zilikuwa zimepasuka, na sehemu zingine zilikuwa zimeanguka kabisa. Malango yalikuwa yamechomwa na yakawa hayafai. Lakini Nehamia hakukatishwa tamaa na hali aliyoiona, bali alijipanga na kuingia kazini. Aliwaita wazee viongozi wa mji na kuwaambia, “Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena.” (Nehemia 2:1). Wale viongozi wakaitikia, na kwa hali hiyo akaingiza familia zote kujiunga katika kazi ya kujenga kuta za mji. Awamu kwa awamu wakiondoa uchafu na kurudishia mawe wakajenga ukuta.
 
Katika sura ya 3 ya Nehemia tunakutana na orodha ndefu ya wale walioingia katika ujenzi huo kulingana na uongozi wao. Tunaambiwa Eliashibu, kuhani mkuu, pamoja na nduguze makuhani, wakalijenga lango la kondoo; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake; mpaka mnara wa Hamea wakalitakasa, mpaka mnara wa Hananeli; wana wa Hassena wakajenga lango la samaki; Uzieli mwana wa Harhaya mmoja wa mafundi wa dhahabu akajenga sehemu iliyofuata; na Hanania mmoja wa mafundi wa manukato nao wakaujenga Yerusalemu.
 
Katika Nehemia 3:2 Shalumu anatajwa kuwa mwana wa Haloheshi akida wa nusu ya jimbo la Yerusalemi naye akajenga sehemu iliyofuata akisaidiwa na mabinti zake. Huu kwa kweli ulikuwa ni mradi wa familia, “Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema” (Nehemia 2:18). Nehemia anasema, “Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.” (Nehemia 4:6)
 
Kuna jambo la kusisimua hapa kuhusu kufanya kazi pamoja kama familia katika shughuli au mradi wa pamoja, na hasa tunapofanya kazi “kwa mioyo yetu yote.” Familia zinaweza kuungana pamoja katika huduma kwa jamii na kuhudumia kwa upendo na neema na hivo kuleta tofauti kwa wengine na kujenga hali imara ya umoja wa kifamilia. Mtu mmoja aitwaye Albert Schweitzer alisema, “Sijui hatima yenu itakuwaje, lakini jambo moja nililo na uhakika nalo ni kuwa, wale ambao watakuwa na furaha kati yenu ni wale watakaokuwa wametafuta na kuelewa jinsi ya kuhudumia wengine.”
 
Na mwingine aitwaye John Wesley anaongezea agizo hili la ajabu kwa kusema: “Tenda mema uwezayo kutenda, kwa kila namna uwezayo, kwa kila njia iwezekanayo, kila mahali unapoweza, na kwa watu wote unaoweza mradi unao uwezo wa kutenda hivyo.”
Makanisa yetu yatashamiri pale familia zote zitakapofanya kazi pamoja kanisani “kwa mioyo yao yote.” Wakati fulani mshiriki mmoja aliniambia kwamba hakuwa na furaha na kanisa lake. Akasema kanisa lilitakiwa kufanya zaidi kwa ajili ya wahitaji waliopo katika jumuiya. Mimi nilimwambia, “Ni familia gani katika kanisa lako unaofikiria wangefanya zaidi kwa ajili ya jumuiya yenu?” Alinitazama kwa mshangao, ndipo nikamuuliza tena kuwa, “Ni familia gani unafikiri zingefanya kazi zaidi?” Alifikiria kwa muda kidogo kisha akatabasamu na kusema, “Nadhani natakiwa kufanya zaidi.” Kanisa ni “familia ya familia nyingi.”
 
Kanisa letu leo ni matokeo ya familia kadhaa zilizo pamoja. Kanisa sio kitu fulani ambacho hakituhusu tunachoweza kulalamikia kuhusu mapungufu fulani. Ni familia kubwa iliyounganisha familia moja moja. Ndiyo sababu tunatakiwa kutenga muda na nguvu zetu katika mahusiano na kuwajibika kikamilifu ili kuimarisha na kuneemesha ndoa zetu na hatimaye familia zetu. Tukiwa na ndoa zilizo imara na zenye afya, tutakuwa na kanisa imara na lenye afya. Hili ni jambo tunalotakiwa kufanya “kwa mioyo yetu yote.”
 
Naam, ujenzi wa ukuta wa Yerusalemi uliendelea kwa mafanikio na msisimko hadi hapo Sanbalat na Tobia na baadhi ya wenyeji katika jumuiya ile waliposikia habari za ujenzi huo. Hao watu hawakufurahia kile walichokiona. Hawakutaka ule mji kurudia hali yake ya awali tena. Walijiona salama zaidi pale ule mji ulipobakia magofu, kwa hiyo wakaanza tafrani. Wakawasumbua wajenzi na kuwakatisha tamaa kwa kauli za kukosoa na kukashifu kile walichokuwa wakifanya. Tobia Mwamoni alisema, “…Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.” (Nehemia 4:3). Wajenzi wakaingiwa ha hofu na kukatishwa tamaa. Na hasa swala la usalama wao likapewa kipaumbele, Nehemia akalichukua hili kwa uzito na kuamua kulishughulikia (Nehemia 4:10-12)
 
Sasa angalia katika sura ya 4 mstari wa 14; “Nikatazama, nikaondoka, nikawaambia wakuu, na mashehe, na watu wengine waliobaki, Msiwaogope; mkumbukeni Bwana, aliye mkuu mwenye kuogofya, mkawapiganie ndugu zenu, na wana wenu, na binti zenu, na wake zenu, na nyumba zenu. ”
 
Mkumbukeni Bwana
Nehemia anawajibu kwa namna iliyo bora kwa mashaka yao: “Mkumbukeni Bwana, aliye mkuu na mwenye kuogofya.” Hatumwabudu Mungu aliye mnyonge asiyeweza lolote. Sisi sio wafuasi wa uvumi fulani tu wa upepo au mfano wa miungu, wala hatumtumikii Mungu tusiyemjua. Mungu wetu ni mkuu na mwenye kuogofya na sisi ni mboni za jicho lake; wana wa kike na wa kiume ambao ni wapotevu na akituona kwa mbali anakimbia na kutukumbatia na kutukaribisha nyumbani (Luka 15:20). Yeye sio Mungu aliye mbali, au hakimu katili, mtawala mwenye upendeleo anayetoa kwa wachache kwa kuangalia usoni. Mungu wetu ni mkuu na mwenye kuogofya, naye amewekeza ndani yetu kama watu wake.
 
Siku ya Sita – February 16, 2017
Kujenga ndoa na Familia – sehemu ya pili
Somo hili limetayarishwa na Trafford Fischer
 
Pigania mahusiano yako
Sasa sikia kile Nehemia anachowaambia watu. Baada ya kuwaelekeza kwa Mungu mkuu mwenye kuogofya, anasema, “…mkawapiganie ndugu zenu, na wana wenu, na binti zenu, na wake zenu, na nyumba zenu.” (Nehemia 4:14)
Nehemia aliwaambia wtu ‘Mungu wetu ni mkuu na mwenye kuogofya.’ Hivo kaeni mtizame, wala msifanye chochote. Je, uchukulie maisha kama kawaida ukimwachia Yeye! La, hasha! Hivi sivyo tulivyosoma katika fungu hilo. Anasema, “…mkawapiganie ndugu zenu, na wana wenu, na binti zenu, na wake zenu, na nyumba zenu.”
 
Katika matukio kadhaa ndani ya Maandiko, Mungu anawaita watu wake kusimama na kuona uwezo wake katika utendaji. Alimwambia Musa katika Kutoka 14:13, 14 “Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.” Lakini katika matukio mengine Mungu aliwataka watu watende. Yesu alipoponya watu, aliwataka kufanya jambo: “…Simama, jitwike godoro lako, uende”
Nehemia alikuwa akiwaambia watu kuwa huu ni wakati wa kuwa makini. Hii ni zahama! Tunahitaji kusimama kwa ajili ya familia zetu na kufanya kila liwezekanalo ili kuwalinda. Haitafaa kitu kuzurura hapa tu na kutegemea tumaini fulani, ni wakati wa kutenda.
 
Nakumbuka nikiwa mtoto mara nyingi mama yangu aliniambia, “Usisimame hapa tu, tafuta kitu cha kufanya.” Nehemia aliziambia familia kuingia kazini. “Msisimame hapo na kuanza kuogopa mkitetemeka; tambueni kuwa Mungu wenu ni mkuu mwenye kuogofya, hivo ingieni kazini.”
 
Nilipokuwa kijana, nilijiunga na vijana wengine wane pamoja na kaka yangu kwenda na mtumbwi kutalii kwa siku tatu kwenye mto uliokuwa umepinda pinda na kujawa na magogo. Tulitakiwa kuwa waangalifu kwa hatari za kukwama katika magogo hayo na kuharibu mtumbwi au maisha yetu. Mmoja wa rafiki zangu alikaa mbele kabisa na wajibu wake ulikuwa ni kutahadharisha pale anapoona au kuhisi hatari. Bahati mbaya sio kila wakati aliona magogo, wakati mwingine tulijikuta tumeingia na kunasa katika magogo. Na ilipotokea hivyo aliingiwa na wasiwasi na kunyamaza kimya.
 
Nehemia hakutaka hilo litokee, hivyo aliwatahadharisha watu wake kwani hakutaka watu wake washtukizwe wala wafikirie wako peke yao. Aliwaasa kuwa haukuwa wakati wa kusimama tu, bali ulikuwa ni wakati wa kuwajibika kwa kushirikiana kama familia.
 
Jenga na Kulinda
Tukiangalia katika sura ya 4 mistari ya 16 na 17: “Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda. Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;”
Walijenga kwa mkono mmoja, na kwa mkono mwingine walishika silaha kwa ajili ya ulinzi. Mkakati wa Nehamia ulikuwa rahisi lakini thabiti – ‘Jenga’ na ‘Linda’. Hajielekezi katika kujenga tu huku akiacha watu katika hali ya hatari, wala hatumii rasilimali alizo nazo katika kulinda tu huku akiishi katika magofu. Anajenga, na kulinda.
Uhusiano Unaoporomoka
 
Katika jumuiya yetu kuna ndoa nyingi na familia ambazo ni kuta zinaporomoka na malango yaliyoungua. Bahati mbaya katika makanisa yetu pia kuna wanandoa wanaohisi kuwa ndoa zao zinaporomoka na wanajitahidi kwa pamoja kuzuia na kuhakikisha zinabaki katika umoja. Familia zinaweza kuhisi kama malango yanayokaribia kudondoka kwa sababu bawaba haziwezi kuhimili. Kama familia za Mungu – familia ambazo zinaishi na kumtumikia Mungu mkuu, mwenye kuogofya – ni lazima tufanye kazi pamoja na kupigania kile tunachoamini kuwa ni muhimu. Tunahitaji kutathmini desturi na tamaduni zetu kwa uangalifu na tusiruhusu kukandamizwa kwa umbo la dunia nyingine. Tunahitaji kuamua ni mabadiliko gani tunaweza kuishi nayo na ni mabadiliko gani hatuwezi kuishi nayo. Tunahitaji kuamua kuwa ni wapi tuchore msitari na kuweka msimamo wetu. Haiwezekani tukaelea tu huku tumefumba macho tukitumaini mema yatatufuata. Kuna ukweli katika msemo wa zamani usemao: “Samaki aliyekufa anaelea kuelekea kule mto unakoelekea, ni yule aliye mzima anayeweza kugoelea kinyume na mwelekeo wa maji”
 
Ndoa zilizopewa umbo na Mungu
Sura mojawapo ya wenzi walio katika ndoa na familia anayoina Mungu inapatikana katika kitabu cha Waefeso. Paulo anasema: “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.”
 
Uhusiano wa ndoa ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa watu wake. Wenzi walio katika ndoa wanaonesha tamko kwa ulimwengu kuhusu kiwango cha upendo wa Mungu kwetu. Hii ni changamot kubwa tunayopewa leo sisi wote wenye ndoa tulio kanisani. Mungu ametamka wazi kuwa ndoa kati ya mwanaume na mwanamke inatakiwa iwe ni tamko lenye nguvu kwa watu wote kwamba Mungu anawapenda watu wake kama tunavyopendana. Lisingekuwa jambo zuri kama watu wangechukuliana kwa jinsi tunavyopendana na kusema, “Yawezekana Mungu anawapenda watu wake kwa kina!”
 
Paulo anawatia moyo watu wa kanisa la Efeso na kuwahimiza wawapende wake zao, na kuwahimiza wanawake kuwaheshimu waume zao. “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.” (Waefeso 5:33). Hakuna dokezo kuwa wanaweza kuvunja uhusiano huo mambo yanapokuwa magumu au kuyaona kama yanashindikana kiasi kwamba hayawezi tena kujengwa upya na kuneemeshwa. Paulo anaingiza kanuni ya uhusiano wa kuridhiana: wanaume lazima wawapende wake zao, na wanawake lazima wawaheshimu waume zao.
 
Kanuni ni hiyo hiyo kwa watoto pia. Paulo anasema, “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.” (Waefeso 6:1). Hii inapendekeza kuwa wazazi lazima watengeneze mazingira ya kuheshimiwa. Kisha anasema, “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.” (Waefeso 6:4). Akiwaandikia Wakolosai anasema, “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” (Wakolosai 3:21). Kwa watoto ina maana ya kwamba wanahitajiwa kufanya kila liwezekanalo ili kutokuwa wakorofi na kuwapa wazazi hali ngumu.
 
Utafiti unaendelea kuonesha mguso wenye nguvu upatikanao katika ndoa iliyo imara na familia yenye furaha katika nyanja nyingi za maisha. Ndoa zenye furaha na familia zenye afya zinchangia kuboresha afya za wenzi walio katika ndoa na wengine wanaowahusu kama watoto, na kuongeza ustawi na miaka ya kuishi. Inachangia pia katika ubora wa maisha, kupunguza magumu kwa watoto walio mashuleni, kupunguza matatizo yanayoandamana na utumiaji wa pombe na madawa ya kulevya na mwisho inapunguza matatizo ya kitabia kwa vijana walio katika rika ya balehe.
 
Tunaitwa kujenga na kulinda ndoa zetu na familia zetu. Tunahimizwa kupigana kwa ajili ya ndugu na dada zetu, wazazi wetu, na hata nyumba zetu. Huu ni mwito wa tarumbeta kutuita tuwekeze katika familia zetu bila kujali maelezo au hata sura zake. Familia moja inaweza kuwa tofauti na familia nyingine. Baadhi yenu wanaweza kuwa wamepitia katika mabadiliko katika familia ambayo pengine hamkuwahi kuyawazia. Baadhi yenu yawezekana mmepoteza wenzi na kwa kweli mnawakosa kwa namna isivyoelezeka. Wengine mnaweza kuwa na wanafamilia ambao hamuwi nao tena katika duara la maisha ya familia. Wengine labda mmejikuta ni upande mmoja wa wazazi (single parents) au ni mababu na mabibi. Kwa hali yoyote ile bado wote ni walezi wa wale mnaogusana nao. Baadhi yenu yawezekana mna njozi za kuwa na familia mkitazamia kuanza mapema iwezekanavyo huku wengine wanafurahi tu kuwa jinsi walivyo na hawaoni haja ya kuingia katika uhusiano wa kudumu. Wito kwetu wote ni ule ule, “Jenga na linda”.
 
Ni lazima tudhamirie kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha uhusiano wetu unaboreshwa. Hebu tuweke kila jitihada kuhakikisha tunajenga na kulinda kwa namna ambayo Mungu angependa wawe.
Kwa wale waliooana kuna ujumbe kutoka kwa Hart na Morris (2003); “Kudumu katika ndoa na kuhakikisha inadumu linaweza kuwa jambo la kubahatisha au la hatari, lakini itakuwa zaidi ya hivyo ikiwa utaamua kuikimbia ndoa yako. Kuchagua kujaribu tena kunakuweka katika hali ya kuweza kudhuriwa kirahisi, lakini itakuwa zaidi ya hivyo ukijiachia katika dimbwi lisilokuwa na ulinzi… Kulea hisia za ukaribu na kufanya kazi kuwezesha ustawi wa uhusiano kunawezekana, bila kujali ndoa yenu ilikuwa na hali mbaya kiasi gani.” Mungu atasikia kilio kitokacho kwenye moyo mpweke ulioumizwa. Atakutana nawe pale ulipo.
 
Maandiko yanaweka wazi kabisa kwamba yawezekana mahusiano yetu yakaonesha kutaka kuvunjika, hiyo ni sehemu ya siku yetu, yanaweza pia kuonesha taswira ya upendo wa Mungu usiokoma kwa kuwa chini ya neema na kutiwa moyo na Mungu mwenyewe.
Hitimisho
 
Ni changamoto kubwa kwetu Wakristo. Ni changamoto kubwa kwetu kama watu wa Mungu – kujifunza kuwa wakweli na kupenda kwa dhati katika ulimwengu ambao hauna upendo wala ukweli. Kujifunza kumtia moyo mwenzi wako na kumthibitishia hilo katika ulimwengu huu uliopungua kutiana moyo na kutegemezana; kufahamu maana ya kupenda na kupendwa; kufahamu nini maana ya kuwa rafiki na msiri wa moyo wangu; kujua namna ya kutafuta njia mpya za kujenga daraja na wengine wanaoakisi upendo wa Mungu kwa ulimwengu huu. Isingekuwa vema kama mahusiano yetu, ndoa zetu, na familia zetu vyote vingekuwa imara na kurudia ubora wake pale tafrani zinapojitokeza ili tuweze kuwaambia kina Sanbalat na Tobia kwamba tunadhamiria kuendelea kuwepo na kudumu kufanya hivyo?
 
Kwa kuhitimisha, mashauri ya Sulemani mwenye hekima yanatuasa, “Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha; Kama mtu angetoa badala ya upendo Mali yote ya nyumbani mwake, Angedharauliwa kabisa.” (Wimbo ulio Bora 8:6, 7). Ni matumaini yangu kuwa hakuna kitu kitakachoweza kuzimisha upendo mlio nao kwa Mungu mkuu, mwenye kuogofya, na kwa wenzi wenu kila mmoja.
 
Hebu upendo huu usije ukaondolewa na kitu chochote kile.
Siku ya Saba – February 18, 2017
Utume, Tumaini na Uponyaji – sehemu ya kwanza
Somo hili limetayarishwa na Peter N. Landless
Fungu Kuu: Matayo 9:35-37
 
“Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.”
 
Kila baada ya sekunde 40 maisha yanakoma, mara nyingi katika mazingira yasiyo na matumaini. (Shirika la Chakula la Kimataifa, 2014). Takwimu hizi na zitushtue na kutuleta katika uhalisia na hasa tunapotambua kuwa wengi wa hao ambao maisha yao yanakoma wakati mwingine kwa kujiua ni wale wenye umri kati ya miaka 19 na 29. Kukosa matumaini hakuheshimu uhai, na kwa sehemu kubwa kwa vijana. Je, hili linakushangaza? Mjue ya kuwa yule mwovu amewalenga vijana wetu msidha kwamba mashambulizi yake yatapungua kadiri tunavyokaribia ule mwisho. Sehemu nyingi vijana wetu wanapomaliza masomo yao na kufuzu vyuoni, bahati mbaya jambo la kusikitisha ni kuwa wanafuzu kanisani pia.
 
Mawazo haya yalijaa fikra zangu tulipokuwa katika kikao cha Shirika la Afya Duniani kwenye chumba cha mikutano kilichofanyika kwa siku mbili tukijaribu kutafuta jinsi ya kupata ufumbuzi wa kupunguza tatizo la kujiua hasa kwa vijana. Mawazo yangu yalikimbia huku na huku nilipokuwa ninatazama fursa zinazotolewa na kanisa kwa kutekeleza mpango mtambuka wa huduma ya afya (Comprehensive Health Ministry-CHM). Mpango huu ukiwa na upana kama unavyojieleza unalenga ukamilifu wa kimwili, kiakili, kiroho, kijamii, na kimhemko au kihisia, lakini pia kila huduma inabeba jumla ya ustawi – inaleta mantiki na ni sahihi. Ukamilifu huo ni wa msingi na unajenga kitako cha kuifikia jamii, utume, huduma na shughuli nzima ya kanisa la Mungu.
 
Ndipo macho yangu yalipoelekea katika vibao vya utambulisho wa kila mjumbe. Kulikuwa na wawakilishi wa nchi mbali mbali, vyuo vikuu, taasisi mbali mbali na mashirika yasiyo ya kiserikali, nikaona kulikuwa na shirika moja tu la dini – Kanisa la Waadventista wa Sabato! Hii ni heshima kubwa sana, na wajibu mkubwa pia fursa nzuri ya kushiriki na watu maarufu na makundi yaliyojikita katika kutatua hili tatizo muhimu. Tulipoanza kupitia swala hili, kukatokea hali ya kutokufurahisha. Hoja ya afya, tumaini, ustawi wa kiakili na kihisia au kimhemko, huduma na utume ni mambo ambayo yanaingiliana kiasi kwamba hauwezi kuyatenga. Unapotoa dhamana ya kuyajadili kwa dhehebu moja tu - kanisa la Waadventista wa Sabato – hasa tatizo la ustawi wa kiakili ambalo katika mpango wa miaka mitano (2015 – 2020) ndio sababu kubwa ya mapungufu ya afya duniani.
 
Hii ilikuwa ni fursa ya pekee na wajibu mkubwa, yaani kila kanisa liwe kitovu cha elimu ya afya, na kila mshiriki awe mmisionari wa afya – kwa upana wake – yaani kimwili, kifikra, kiroho, kihisia na kijamii.
 
Yesu ndiye ni kielelezo cha ubinadamu, Tabibu Mkuu, Mponyaji mkuu, Chimbuko la tumaini. Katika kushughulikia agizo la muhimu kwa upana wa Huduma ya Afya, EGW aliandika kiunabii akielekeza kuwa:
“Ninaona kwamba huduma ya uponyaji itakuwa ndiyo upenyo mkubwa, kupitia kwayo, nafsi zilizojeruhika zinaweza kufikiwa. Muunganiko kama wa Kristo, yaani mwili na kazi kama ya Kristo kwa ajili ya roho, ndiyo tafsiri sahihi ya injili.” (White, 1902, ukurasa 14, 15)
 
Dunia ya leo inatumia lugha ifuatayo:
“Kuzuia magonjwa kunaweza kuimarishwa kwa kuhimiza vigezo vinvyolinda kama uhusiano binafsi ulio imara, mfumo binafsi wa imani, na mikakati chanya ya kushugulikia mambo.” (Taarifa ya shirika la afya duniani (who) – Preventing Suicide uk. 8)
Nilisikia umuhimu wa kuondoa unyanyapaa wa afya ya akili na kila kinachohusiana na ustawi wa kihisia; ni lazima tuongee kwa uhuru kuhusu maswala haya kwa namna ambayo sio ya kukashifu wala kuhukumu. Nilisikia maneno kama kujali, huruma, tumaini; maneno ambayo yanaelezea utume wetu na vipengele muhimu vinavyokosekana katika mapendekezo mengi yanayoshughulikia mahitaji ya mwanadamu. Mungu aepushe kwamba haya yasije yakakosa katika utume wa kanisa la Waadventista wa Sabato, kwa sababu bila haya, utume wetu haujakamilika na lazima utashindwa.
 
Yesu ambaye ni kielelezo cha mwanadamu, alionesha huduma hii kwa ukamilifu wake kwa kukumbatia ubinadamu wote. Ninatekewa na matukio ya ajabu ambapo Yesu alikutana na watu mbali mbali wa nyakati zake. Kila alipokutana na mtu, maongezi yake yalisisitiza na kuelekeza katika hali ya kiroho, na mara nyingi hasa pale muujiza wa uponyaji ulipotendeka. Sisi pia mara nyingi tunaelezea kutendeka kwa miujiza inayohusiana na afya zetu. Yesu pia alishughulikia hali ya akili na hisia - hasa kwa kudhamiria. Katika kitovu cha huduma yake ya uponyaji alitamka pia kusamehewa kwa dhanbi na kuondolewa udhalimu wote. Huduma ya Afya kwa upana wake haiwezi kuachanishwa na ujumbe wa wokovu.
 
Utume wa Kristo ulikuwa kuponya wagonjwa, kuwatia moyo waliokata tamaa, kutangazia wafungwa kufunguliwa kwao. Kazi hii ya urejeshwaji inatakiwa kufanyika kwa wahitaji, na wale wanoteseka kwa mateso mbali mbali. Mungu anatuita sio kwa ukarimu wetu tu, bali kwa uso mchangamfu na maneno ya matumaini, hata kule kumshika mtu mkono kwa kumtegemeza. Tafuta namna ya kumpunguzia maumivu mmojawapo wa hao wadogo. Wengine ni wagonjwa waliokata tamaa, hebu warudishie ile nuru ya jua katika maisha yao. Zipo roho zilizopoteza matumaini, zungumza nao, omba nao, waombee. Wapo wale wanaohitaji mkate wa uzima, wasomee kutoka katika Neno la Mungu. Kuna magonjwa mengine ambayo hakuna dawa inayoweza kuyaponya, omba kwa ajili ya haya na kuyaleta kwa Yesu Kristo. Na katika kazi yote unayofanya kumbuka kuwa Kristo atakuwa pale kuweka mvuto katika mioyo ya watu.
 
“Hii ndiyo aina ya umisionari inayotakiwa kufanyika. Angaza nuru ya jua ndani ya chumba cha mgonjwa anayeteseka. Fundisha wale wasio na kitu jinsi ya kupika. Atalisha kundi lake kama mchungaji, kwa chakula cha muda, na chakula cha kiroho.” (White, 1898, ukurasa 105)
 
Yesu alichoka. Je kuna yeyote kati yenu anayejikuta hivyo? Kati kati ya mahangaiko haya ya kila siku, umewahi kusoma maneno yaliyoandikwa katika sura ya 4 ya Yohana?
“Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.” (Yohana 4:6)
“Akiwa amechoka kwa sababu ya safari yake.” Maelezo haya pengine yanastahili kwa wengi waliopo hapa kuliko tunavyoweza kukubali. Ninatiwa moyo kufikiria kuwa Yesu naye alichoka wakati fulani. Kuchoka kwake labda kulisababishwa na hisia za kujali kuhusu kukosekana kwa matumaini katika sayari hii kwa namna ambavyo hali ya changamoto zilizopo ndani na nje ya kanisa wakati mwingine zinaleta hali ya kuchosha.
 
Ndipo mwanamke Msamaria akaja kuchota maji kisimani. Mitume walikuwa wameenda pengine kwenye duka la vitabu vya Kisabato (ABC) kununua chakula kwa ajili ya safari – wakijielekeza katika mahitaji halisi. Yesu anaanza kuongea na huyu mwanamke Msamaria kwa kumwomba maji ya kunywa. Najaribu kupiga picha ya mshangao wa mwanamke huyu anapomuuliza Yesu kuhusu usahihi wake kumwomba maji akiwa mwanamke Msamaria. Anakuja kisimani nyakati hizi kukwepa macho ya wanakijiji wenzake yanayohukumu. Tambua ya kuwa alikuwa tayari anabeba furushi la huzuni za kihisia, na hatia ambazo kwa kweli zilipunguzwa kwa mwenendo wa wengine (na hasa kwa mwenendo wake mwenyewe)
Yesu anashirikiana naye umuhimu wa wokovu na kumdhihirishia kwamba Yeye ni Maji ya Uzima na ndiye wokovu wenyewe.
 
Wanajibizana kwa kifupi kuhusu ni wapi ibada ya kweli inapofanyika: “Katika mlima huu” au Yerusalemu. Yesu anamfunulia ukweli wa kina na kumweleza ibada ya kweli – kuwa ni katika roho na kweli.
Anajidhihirisha kwake kwamba ndiye Masihi. Mara tu, mtume wanarudi, lakini – ingawaje wanashangaa kwamba anaongea na mwanamke Msamaria – hawaulizi swali lolote. Umewahi kujiuliza kwamba ni kwa nini mdadisi Petro alijizuia asitamke neno la kurekebisha? Napenda kufikiri kwamba kadiri mitume walivyokaribia eneo la tukio wakishangaa na pengine kuwaza kuwa hatendi vema,
 
Yesu aliwaangalia kwa mtazamo, ule unaofahamika kwa wazazi, watoto na hata kwa wanandoa. Mtazamo ambao wakati mwingine unapeleka ujumbe kuliko maneno. “Wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?” (Yohana 4:27)
 
Wanampa chakula, hasikii njaa tena wala kuchoka kwa sababu anapata kutosheka katika kutimiza na kutegemeza utume. “Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.” (Yohana 4:34)
Mitume wanashangaa! Yesu alivunja mipaka ya desturi, dini, kabila na hata jinsia, akahudumia wahitaji kwa huruma na hata roho zilizokuwa na hatia. Kalamu ya uvuvio inatuambia kuwa, “Mkono wa ajabu ulikuwa unafungua kurasa za historia ya maisha ya yule mwanamke Msamaria zikimdhihirishia kile ambacho alitumaini kukificha milele.” (White, 1808, uk. 187). Aliukubali wokovu; akakimbia kurudi mjini, akashawishi wengine kuja kumwona Yesu, nao wakabarikiwa kwa ushuhuda wake kwa siku mbili zaidi.
Alidhihirisha kuwa ni mmisionari mzuri kuliko mitume wa Yesu. Matokeo yake yalikuwa mbaraka mkubwa mkamilifu na kwa upana wake – Huduma ya Afya kwa Upana wake.
 
“Tumefikia wakati ambapo kila mshiriki wa kanisa lazima aingie katika umisionari wa ‘huduma ya uponyaji.’ dunia ni nyumba ya wagonjwa iliyojawa na wahanga wa magonjwa ya kimwili na ya kiroho. Watu wanaangamia kila mahali kwa kukosa maarifa na kweli tulizokabidhiwa. Washiriki kanisani wanahitaji kuamshwa ili watambue wajibu wao wa kutoa kweli hizi.” (White, 1855, vol. 7, uk. 62)
 
Siku ya Nane – February 18, 2017
Utume, Tumaini na Uponyaji – sehemu ya pili
 
Huduma ya uponyaji: Petro na Yohana
Hebu njoo nami katika uzoefu wa Petro na Yohana wanapoweka katika utendaji na kutekeleza utume na Huduma ya Uponyaji katika Upana wake, kwa jinsi walivyojifunza kutoka kwa Yesu. Tunasogea haraka hadi Matendo sura ya 3 na ya 4, Petro na Yohana wanaelekea hekaluni kupitia ‘Lango la Uzuri’ saa tisa mchana. Kuna mtu ambaye ni kiwete tangu alipozaliwa. Kila siku analetwa na kuwekwa langoni pale ili apate kuomba kwa wanaoingia hekaluni. Macho yake yanakutana na macho ya Petro na Yohana na anaomba pesa. Unajua ilivyo unapokabiliwa na omba omba.
 
Unaweza kugeuza macho yako, kama yule farisayo na ukageukia upande mwingine. Petro anaitikia kwa maneno ambayo yamekuwa ya kawaida kwake, - lakini kabla ya hayo maneno anasema “Tuangalie” naye anawaangalia kwa tumaini la kupata fedha. Maneno yanayofuata yanamkatisha tamaa, “Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho…” tumaini likaanza kurudi. Umeshawahi kupitia uzoefu huu? Unapohitaji fedha au kitu fulani, yule anayekupa anageuza mchezo! Hata hivyo hadithi haikuishia hapa.
 
“Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.” (Matendo 3:6-8) Tambua kwamba huduma ya uponyaji ndio mkono wa kuume wa ujumbe wa Injili. Yule mtu akasimama, akatembea, akarukaruka na kumtukuza Mungu. Mtu ambaye hakuwahi kutembea tangu kuzaliwa, sasa anaruka ruka, ni badiliko kubwa.
 
Watu walipoona, Mafarisayo walipoona, wakaanza kuuliza maswali – wanayatenda haya kwa uwezo wa nani; imetokeaje? Petro yule aliyemkana Yesu akawajibu kwa ujasiri kufuatia agizo alilopewa kuwa “Lisha kondoo wangu”. “…kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote.” (Matendo 3:16)
Mwili, akili, roho, jamii, hisia, vyote vinashughulikiwa katika tukio hili. Ndipo Sanhedrin nao wanaanza kujihusisha na tukio hili. “Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya?” (Matendo 4:7). Peteo akiwa amejawa na Roho Mtakatifu alijibu:
 
“Kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.” (Matendo 4:9-10)
Na hapa ndipo penye siri – kuongezeka kutoka katika kitendo cha uponyaji wa mwili, akili na roho:
“Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” (Matendo 4:11, 12)
 
Hakuna jina jingine ila jina la Yesu katika huduma ya familia, elimu, vijana, chaplensia, watoto, uchapishaji, afya, au huduma nyingine yoyote – hakuna jina jingine kuliko la Yesu – ambaye ndiye kitovu, msingi, wa kwanza na wa mwisho!
Lakini hebu angalia mwitikio wa watu, Sanhedrin na wengine wote,,,
“Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” (Matendo 4:13)
 
Je, watu watashangaa, kupigwa butwaa, kuridhika, kufurahi au kushtushwa kwamba tumekuwa na Yesu – bila kujali mada au changamoto? Je, watashangaa kwamba Roho wa Mungu anawezesha kanisa lake kuwa katika muunganiko pamoja na mitizamo inayopishana? Tambua kwamba kuna tofauti ndogo, unaweza kukosea kwa kutofautisha maneno kama “Umoja ni nguvu” au “Nguvu ni umoja” kuna tofauti! Hebu Mungu aepushe kukosea kwa maneno na tubakie katika njia kuu. Swali kuu ni kuwa “nimekuwa na Yesu kweli?”
 
Petro na Yohana wanakamatwa, mitume wengine wanaungana kuwaombea, na wanaachiwa. Watakatifu endeleeni kuomba ili mpango wa “Huduma ya Uponyaji kwa Upana wake” na utume vitiwe nguvu na maombi na kuneemeshwa kwa ombi hili, “Wawezeshe watumishi wako kunena Neno lako kwa ujasiri. Nyoosha mkono wako kuponya na kufanya miujiza, ishara na maajabu kupitia katika jina la Mtakatifu wako Yesu Kristo (Matendo 4:30). Na mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
Maisha yetu pia na yatikiswe, tujawe Roho Mtakatifu, tunene Neno la Mungu kwa ujasiri!
 
Bwana atawafanikisha katika kazi hii (umisionari wa huduma ya uponyaji), kwa sababu injili ni uweza wake Mungu uletao wokovu inapounganishwa katika uzoefu wa maisha ya kila siku, na unapoishi. Muunganiko wa kazi ya Kikristo kwa ajili ya mwili wa Kristo, na kazi ya Kikristo kwa ajili ya roho ndiyo tafsiri iliyo sahihi ya injili.” (White, 1902, uk. 14, 15)
 
Huduma ya Afya kwa Upana wake, ikiponya (kwa ujumla katika uvunjifu wake), na utume vimeungana kwa namna isiyokwepeka. Utaona dhana ya huduma inayojumuisha mbinu ya Kristo ya huduma katika kuwafikia watu.
Hii mbinu itaonekanaje? Itaonekana kama vile Yesu amekuwapo (au yupo) ndipo hali na maisha kwa ujumla itabadilika.
Ni utume na huduma – sio mbinu tu; inawafikia watu wa ndani na nje – kwa wahitaji wa aina zote, kwa ukamilifu na kuzuia msukumo wa mtindo wa maisha; inatoa mwendelezo wa kujali kwa ujumla kimwili, kiakili, kiroho, kihisia, na kijamii. Tumeanza kitu ambacho hatuwezi kukisitisha – hadi hapo Yesu atakapokuja tena. Maranatha.
Hitimisho
 
Tukiungana katika maombi, tukitiwa moyo na Roho Mtakatifu, kudai ahadi na jina la Yesu, huku tukifahamu kwamba hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo, na ambaye tunamtumikia, na anayetutia nguvu na kutupa tumaini na uponyaji katika utume huu. Hebu na tuelekeze usikivu wetu kwake kadiri tunavyosonga mbele. Sio kushangaa kwa umahiri wa kuongea au ubishi katika kuvutana, ila kwa sababu tumekuwa na Yesu na tunaundwa tuweze kuleta matumaini na uponyaji kwa wale waliovunjika mioyo katika sayari hii iliyochoka ikilalama kutazamia kurudi kwake kuliko karibu.
 
Mungu na atubariki na kutuongoza katika utume wetu huu ili tuweze kuleta matumaini na uponyaji, kwa jina la Yesu, Amina