Seventh-Day Adventist Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

JUMA LA FAMILIA

 

FAMILIA YA KIKRISTO

JUMAPILI

Hakuna mahali muhimu kwa binadamu kama nyumbani. Ndiyo maana kuna msemo wa kiingereza usemao “EAST OR WEST, HOME IS BEST” yaani iwe mashariki au magharibi nyumbani ndipo mahali bora zaidi. Usalama wa jamii huanzia nyumbani. Juhudi za kuleta amani ya kweli katika jamii na katika makundi ya watu kama kanisani ni lazima ianzie kwenye familiya. Jamii nyingi leo zinalalamikia kumomonyoka kwa maadili kwa kuwa familia zimeyumba. Familia zikipotea jamii yote ni lazima ipotee.

Yesu alipokuwa akiangalia ndoa katika siku tunazoishi, aliiona misingi yake ikiyumba. “Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” (Mathayo 24:38-39). Leo watu wanaoa na kuolewa bila utaratibu wa Mungu. Tunashuhudia ndoa za jinsia moja. Tunashuhudia watu wengi wakiishi bila ndoa. Tunashuhudia magomvi ya kutisha katika ndoa. Tunashuhudia watoto wakikimbia familia zao na kuishi kwenye mitaani kwenye majiji kama watoto wa mitaani. Mambo haya yanatuambia kuwa jambo fulani ni lazima lifanyike kuiokoa familia.

Maandiko yalitabiri kuwepo kwa juhudi zitakazosimamiwa na Mungu mwenyewe, za kuiokoa familia katika siku za mwisho. “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya. Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana.” (Malaki 4:5, 6). Mafungu haya yanatupa matumaini kwamba, mahusiano yaliyoharibika nyumbani yatarejeshwa kwa msaada wa Mungu. Kutakuwa na mahusiano mazuri baina ya wazazi na watoto, na kutakuwa na mahusiano mazuri baina ya mume na mke tofauti na ilivyo sasa. Kwa kusudi hili Idara ya Huduma za Familia ilianzishwa. Idara hii inalenga kuboresha mahusiano nyumbani, na kuifanya familia kituo cha wokovu; mahali watu wanapoandaliwa kuwa wanafunzi wa Yesu wakiukulia wokovu na kujishughulisha na uongoaji wa roho. 

Utume wa kanisa hauwezi kufanikiwa bila kuigusa familiya, kwa kuwa jitihada za uinjilisti katika miji mikuu ni lazima zilenge kufanyia uijnilisti familia zilizo kwenye miji hiyo. Uzoefu unaonesha wengi waliojiunga na kanisani walikuja kupitia mivuto ya familia. Wanafamilia wenyewe hupeana taarifa za wokovu kwa njia ya mivuto yao au masomo yaendeshwayo hapo nyumbani na mialiko kwenye matukio ya kiroho kama ndoa, sabato za wageni na mikutano ya injili. Mama White anasema “Familia moja iliyopangiliwa vizuri, na yenye nidhamu nzuri huzungumza mengi kuhusu Ukristo kuliko mahubiri yote yanayoweza kuhubiriwa.” (Adventist Home uk. 32). Hebu tuzifanye familia zetu kuwa vituo vya wokovu.

TAFSIRI SAHIHI YA NDOA

Kwa kawaida familia inafanywa na watu wawili yaani mume na mke. Hata hivyo si lazima wakati wote familia iundwe na watu wawili. Familia yaweza pia kuwa ya mtu mmoja ambaye hajapata mwenzi wa maisha au mmoja ambaye ameondokewa na mwenzi wa maisha. Familia yaweza kuwa na watu zaidi ya wawili. Familia yaweza kuwa na watoto au jamaa wa karibu au isiwe nao. Hata hivyo watoto na jamaa wengine siyo wanaohalalisha kuwepo kwa familia kwa sababu hata familia isiyo na watoto bado inatambulika kuwa ni familia na ndoa kamili. Watoto ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Kwa kawaida familia huanza kwa ndoa. Ndoa ni agizo la Mungu kwamba wanadamu wanapofikia umri wa kuoa na kuolewa wakiwa wamekidhi vigezo vingine vyote vya ndoa wanapaswa kuingia kwenye mahusiano ya ndoa. “Akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja” (Mathayo 19:5) ndoa kama ilivyokusudiwa na Mungu ilikuwa ya watu wawili; mwanaume na mwanamke. Lakini leo kutokana na mavumbuzi ya wanadamu kumekuwepo pia ndoa ya mume mmoja na wake wengi, ndoa ya mwanaume kwa mwanaume mwenzake na mwanamke kwa mwanamke mwenzake. Mavumbuzi haya na mengineyo mengi yaliyo kinyume cha Maandiko Matakatifu (maelekezo ya Mungu) yamesababisha kuongeza kwa migogoro katika ndoa na katika jamii husika.  

Lakini mtu anaweza kujiuliza tunapozungumzia ndoa ama familia tunamaanisha nini hasa? Mungu hakumpatia mwanadamu kibali cha kujitafutia tafsiri ya ndoa kama aonavyo yeye mwenyewe au kujibunia utaratibu katika kuanzisha taasisi hii ya ndoa. Pamoja na kumpatia mwanadamu uhuru wa kuchagua kufanya apendacho kati ya kumtii au kumwasi, Mungu alimzuilia mwanadamu uhuru wa kujiamulia aina ya ndoa aitakayo, mwenzi wa maisha amtakaye, aina ya ibada aitakayo, na aina ya chakula atakachokula. Katika mambo hayo yote Mungu ndiye anayehusika kumchagulia mwanadamu kutokana na mambo hayo kuwa nyeti kwa maisha yake. Mungu aliyeanzisha ndoa ndiye mwenye tafsiri sahihi ya neno ndoa na ndiye ajuaye utaratibu unaofaa kufuatwa mtu anapokusudia kuunda taasisi ya ndoa. Tafsiri sahihi ya ndoa ni ile inayotolewa na Maandiko Matakatifu (Biblia). “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” (Mwanzo 2:18). 

Mawazo potofu kuhusu ndoa

Wapo wanaodhani ndoa ni muunganiko wa watu wawili wanaopendana bila kujali wawili hao ni wa jinsia tofauti au la na kama ndoa yao itakuwa ya kudumu au ya muda kitambo. Kutokana na tafsiri hiyo, wapo wanaodhani ndoa ni muunganiko wa watu wawili wa jinsia tofauti wanaopendana na ambao wameamua kuishi pamoja kama mume na mke kwa maisha yao yote hadi mauti itakapowatenga, na wapo wanaodhani ndoa ni muunganiko wa mume mmoja na idadi ya wake atakaoweza kuwahudumia n.k. Mungu hakuliacha jambo hili katika utata huu tunaoushuhudia. Biblia imesema waziwazi, “Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.”(1 Wakorintho 7:2). Na tena Yesu anasisitiza “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja” (Marko 10:6-8). Ni mawazo potofu kabisa kudhani kuwa ndoa inaweza kuwa ya zaidi ya watu wawili.

Kuijaza nchi

Dunia hii iliumbwa ili ikaliwe na watu. "Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine." Isaya 45:18. Mungu alikusudia kuijaza nchi kwa watu watakaozaliwa kutoka kwenye ndoa ya mume na mke, na ndiyo maana aliamuru mwanaume na mwanamke waunde ndoa. Mume na mke wasipokuwa na hitilafu zinazozuia kutungwa kwa mimba wana uwezo wa kupata watoto na hivyo kutimiza agizo la Mungu linalowataka wazae. “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:28) Jukumu hilo haliwezekani kwa ndoa ya watu wa jinsia moja inayopigiwa debe sana katika kizazi hiki. Kwamba mwanaume kwa mwanaume ama mwanamke kwa mwanamke wanaweza kuunda ndoa na familia; ni wazo potofu linalopingana na mpango wa awali wa Mungu kuhusu ndoa.

Umuhimu wa ndoa katika jamii

Umuhimu wa ndoa au familia katika jamii hauna cha kulinganishwa. Jamii yoyote isiyo na ndoa au familia zilizo imara itakuwa jamii isiyo imara pia kwa kuwa uimara wa jamii kwa kawaida huanzia kwenye ndoa au familia. Matatizo ya mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa uadilifu unaoshuhudiwa katika jamii nyingi unatokana na kuporomoka kwa mambo hayo katika ndoa na familia. Yeyote anayetaka kuidhuru jamii ni kazima aanzie jitihada zake hizo katika ngazi ya ndoa na familia. Na tunaliona hili kupitia jitihada zinazofanywa na adui mkuu wa ndoa yaani Shetani. Yeye ameilenga ndoa na familia kama mahali pake pa kuanzia katika kuiharibu jamii ya wanadamu. Anafahamu kuwa atakapofaulu kuihujumu ndoa na familia atafanikiwa kirahisi zaidi kuiangusha jamii, taifa, na ulimwengu mzima.

Kwa kutambua ukweli huo kanisa la Waadventista wa Sabato liliunda kitengo cha Huduma za Familia katika kila ngazi ya kanisa ili kuzilinda familia dhidi ya mbinu chafu za yule mwovu. Idara hii inatekeleza jukumu lake hilo kupitia utoaji wa elimu ya familia kwa njia ya semina za wakati wa makambi na kwenye mikutano ya hadhara, mafunzo ya familia kwenye kanisa mahalia (hasa kupitia masomo maalumu ya juma la familia yanayoandaliwa), kupitia warsha za kujenga mahusiano ya ndani ya familia, na kupitia ushauri nasaha kwa vijana, wanandoa watarajiwa, walio kwenye ndoa, na wajane.  Kanisa lisilotilia maanani huduma hii linajiangamiza lenyewe “Moyo wa jumuiya, wa kanisa, na wa taifa ni kaya. Ustawi wa jamii, mafanikio ya kanisa, na kufaulu kwa taifa vinategemea mvuto wa nyumbani.” (Adventist Home uk. 15). 

1. Je, kanisani kwenu mnapata elimu ya Huduma za familia kama inavyostahili?

2. Je, makundi yote ya wanafamilia yanapewa umuhimu ulio sawa katika kupewa elimu ya huduma za familia? Ni makundi gani mara nyingi yanasahauliwa?

3. Unadhani sehemu kubwa ya migogoro iliyopo kanisani imetokana na hali ya mahusiano yasiyoridhisha kwenye familia

4. Imekusudia kufanya nini ili kuboresha mahusiano katika familia yako na familia ya kanisa lako?

 

JUMATATU

Umri unaohusika na ndoa

Si kila aliye mwanaume na mwanamke anakidhi vigezo vya kuoa au kuolewa. Ili mtu aonekane amekidhi vigezo vya kuoa au kuolewa ni lazima awe amefikia umri unaomwezesha kujitegemea na aliye tayari kwa jukumu la uzazi. Kutokana na vigezo hivyo mwenye sifa ya kuoa au kuolewa ni lazima awe amepita rika ya watoto na yupo rika la vijana akielekea utu uzima. Katika nchi nyingi wanatambuliwa kuwa na haki ya kuoa na kuolewa huanzia miaka 18 kwa wasichana na miaka 20 hivi kwa wavulana.

Lakini ili kuwa katika nafasi nzuri ya kuepuka madhara yatokanayo na ndoa za utotoni inashauriwa vijana waanze kufikiria kuoa na kuolewa baada ya miaka 25 muda ambao kwa wengi waliokuwa masomoni ndipo wanahitimu chuo kikuu. Msichana anayeolewa mapema sana anahatarisha afya ya uzazi kutokana na changamoto nyingi za uzazi zitokeazo siku hizi. Kuwahi kuoa pia kuna changamoto zake kwani kuna maandalizi ambayo yanakuwa hayajakamilika na ni ya muhimu yakamilike kabla ya ndoa. Majukumu hayo ni pamoja na kujua wapi mtaanzishia familia yenu (makazi) na njia za kujikimu kwa maisha kwa kuzingatia kuwa mara tu mtu akiingia kwenye ndoa hapaswi tena kutegemea wazazi kwa mahitaji yake ya msingi kama chakula, malazi, mavazi, matibabu nk.

Kama matokeo ya dhambi, wapo wanaojikuta wakiwa na viungo vya uzazi vyenye mapungufu. Hawa watahitaji ushauri nasaha na kama tatizo lao litathibitika kuwa halina ufumbuzi basi watashauriwa wasioe wala kuolewa isipokuwa kama atapatikana mtu atakayekuwa tayari kuishi nao katika mazingira hayo. Mapungufu hayo ni kama kutokuwa na nguvu za kiume, kukosa viungo vya uzazi nk. “Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” (Mathayo 19:10-12)

Biblia inafafanua kuwa haki mojawapo ya msingi ya wanandoa ni tendo la ndoa. “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.” (1 Wakorintho 7:3). Tendo la ndoa lina uhali likitendwa kwenye ndoa na watu wanaotambulika kisheria kuwa ni wanandoa. Nje ya hapo tendo hilo ni kosa na dhambi ya uzinzi na uasherati. “Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.” (Kutoka 20:17). Tendo hilo linapotendwa nje ya ndoa huweza kuleta madhara makubwa kwa wahusika na kwa jamii kwa ujumla. “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika.” (Mithali 6:32-33). Ili kuepuka kuWaingiao kwenye ndoa inawapasa kufikia umri ambao via vya uzazi vimekomaa na vimekamilika kuweza kuhimili majukumu ya uzazi na kutoshelezana.

Kwa nini vijana wanachelewa kuoa?

Swala la kuoa na kuolewa kwa mujibu wa tamaduni nyingi huamuliwa na wanaume zaidi kuliko wanawake. Mwanamke hata kama atampenda mvulana ni nadra kwake kumtamkia. Anachoweza kufanya msichana aliyempenda mvulana   (kama amezidiwa sana) ni kumwonesha kwa matendo ya huruma na adabu kuwa anampenda. “Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu.” Mwanzo 24:19, 20, 22

Wale wavulana waliofikia umri wa kuoa wanashauriwa wasiendelee kukaa peke yao bali waoe. Wasiahirishe kuoa au kuolewa eti kwa madai kuwa hawajajipanga. Kuingia kwenye maisha ya ndoa hakuhitaji uwe umejikamilisha katika kila jambo isipokuwa yale ya mambo nyeti ya kujitegemea kwa chakula, malazi, na mavazi tu. Jambo muhimu zaidi ni kumchagua mwenzi wa maisha atakayeishiriki ndoto yako ya maisha na atakayekuwa msaada katika kuifikia. Kama una shughuli inayokuingizia maisha na mipango mizuri ya maendeleo ya siku zako za usoni, hivyo ni vigezo tosha kuwa na mwenzi wa maisha. Mipango mingine itakamilika mkiwa pamoja.   

Kuchelewa kuoa na kuolewa kwa baadhi ya wavulana na wasichana kumethibitika kuwa kumewafanya baadhi yao kujitafutia njia mbadala za kutimiza tamaa zao za kimwili. Wengine hujianzishia mazoea mabaya ya kujichua viungo vyao vya uzazi na wengine huingiliana wanaume kwa wanaume na wanawake, hali wengine hujianzishia mazoea ya kusagana. Njia hizi zote si salama kiafya na zinaumiza dhamira zao kila zinapofanyika jambo linalowafanya wenye mazoea hayo kupoteza uwezo wa kujiamini. Wengine wanatuhumiwa kufanya ngono katika kipindi wanachodai kujipanga au kutafuta wachumba jambo linalowafanya wasione haja ya kufanya haraka ya kuoa au kuolewa kwa kuwa wamekuwa wakioana kila siku. 

Kijana zikimbie tamaa za ujanani. “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.” 2 Timotheo 2:22. Ukawe shujaa kama Yusufu aliyeshinda tamaa za ujanani pale alipotaka kubakwa na mke wa bosi wake. “Huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje.” (Mwanzo 39:12). Yesu anawategemea vijana maana wao wakiamua huweza kufanya yale yasiyowezwa na wengine. “. . . Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu. . . (1 Yohana 2:13) “. . . Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.” 1 Yohana 2:14

Madhara ya kuanza ngono mapema

Biblia inatahadharisha vijana kutoyaanza mapenzi mapema na kukifananisha kitendo hicho na kuyachochea mapenzi. “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.” (Wimbo Ulio Bora 2:7). Moja ya matatizo ya kuanza ngono mapema ni magonjwa ya zinaa kama kaswende, na magonjwa yasiyo na tiba kama UKIMWI. Kwa wasichana madhara ya kuanza ngono mapema ni mogonjwa ya kansa ya kizazi na mimba zisizotarajiwa. Licha ya matatizo hayo, imethibitika pia kuwa wote waanzao mazoea ya ngono nje ya ndoa huendelea na tabia hiyo hata baada ya kupata wenzi wa maisha.

Matatizo mengi yanayosumbua ndoa leo yanatokana na mazoea ya kukosa uaminifu katika kipindi cha uchumba ama mapema kabla ya uchumba. Kijana ni vizuri kuzingatia ushauri wa Mungu, ule wa wazazi, na ule wa kanisa lako. Fedheha utakayoipata kwa kukosa uaminifu yaweza kukugharimu maisha yako yote.  “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” (1 Wakorintho 6:18) Wengine huingia katika mazoea haya mabaya kwa kushawishiwa na wenzao. Maandiko yanasema “Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.” (Mithali 1:10) Yesu anawapenda vijana na anawahakikishia kuwa atawapigania ikiwa watahitaji msaada wake.  

Epuka makundi yenye mazoea mabaya

Mbinu nyingine ya kujizuia na majaribu ni kuachana na makundi mabaya. “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika.” (Marko 9:43) Mkono unaoelekezwa kukatwa hapa ni hayo makundi maovu.  Wakati mwingine mambo yanayoweza kukushawishi kuingia kwenye mazoea ya ngono za ujanani ni mazungumzo mabaya au picha mbaya za uchi. “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.” (1 Wakorintho 15:33). Unapoona mazungumzo mabaya yameanza wewe ondoka mahali hapo au wakanye kutoendelea na mazungumzo hayo. Usikae barazani pa wenye mizaha. Zaburi 1:1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

 Akili huathiriwa na yale ambayo macho huona. Usijiruhusu kuangalia mambo yatakayoiathiri akili yako itamani kufanya ngono. Chukua msimamo wa mwandishi wa kitabu cha ayubu. “Nilifanya agano na macho yangu; Basi nawezaje kumwangalia msichana” (Ayubu 31:1). Msichana anayetajwa hapa (ambaye haifai wavulana kumwangalia) ni yule aliye kwenye mazingira ya kumtamanisha mtu kingono. Awe ni yule apitaye barabarani, aliye kwenye picha za mnato au aliye kwenye video, weka agano la kutowaangalia wanawake hao. Kumbuka kuwa tendo la ngono daima huanzia kwenye mawazo. Mara nyingi ni wanaume wanaoshawishika kingono kwa kuangalia. Wanawake huweza kushawishika kirahisi kingono kwa kuguswa kuliko kuangalia.  “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.” 1 Wakorintho 7:1. Wengine walitumbikia kwenye mtego wa ngono kwa kuruhusu kuguswa na hiyo ikawapotezea uwezo wa kulishinda jaribu. Usijaribu.

 1. 1.     Nini kifanyike kuepuka mimba zisizotarajiwa na ngono za utotoni?


JUMANNE

Sababu za kuchelewa kuchumbiwa

Zipo sababu nyingi zinazofanya wasichana wachelewe kuchumbiwa. Hapa nitazungumzia baadhi ya sababu za kujitakia zilizopelekea baadhi ya wasichana kujikuta wakichelewa kuchumbiwa.

 • Wasichana wengine kwa kujichukulia kuwa wao ni wazuri sana na wana soko, wamekuwa wakiwakataa wavulana wanaowaulizia uchumba hata pale wanapokuwa wamekidhi vigezo kwa mataraji ya kumpata mwenye vigezo vya juu kuliko wengine wote.
 • Wengine huwakataa wachumba kutokana na shinikizo la wazazi wenye kutaka mvulana mwenye uwezo wa kiuchumi au wa kabila lao. Wakiwa na matarajio kuwa wachumba wataendelea kuja ghafla hushangaa kuona idadi ya wachumba ikipungua na kugundua kuwa soko lao limeshuka jambo linalowaweka kwenye wasiwasi wa kukosa wachumba wa kuwaoa.   
 • Wengine hukutwa na janga la kutochumbiwa kutokana na kutumia kejeli na lugha za kashfa katika kuwakataa wachumba wanaowajia na hivyo kuchukuliwa kuwa ni msichana mwenye dharau jambo ambalo karibu wavulana wote hukerwa nalo.
 • Wengine huchelewa kupata mchumaba kutokana na kujiweka katika mazingira ya soko la nje zaidi kuliko soko la ndani. Maana yangu hapa ni kuwa msichana anayejiremba na kuvalia kama watu wa duniani hawezi kutarajia kupata wavulana wa kanisani wamuulizie uchumba.
 • Wengine huchelewa kupata wachumba kutokana na kutojiweka wazi kuwa wanahitaji mchumba na kutokuwa karibu na yule wanayevutwa naye kuwa mchumba wao.
 • Sababu nyingine ya kuchelewa kuchumbiwa ni tuhuma zilizozagaa zingine zikiwa za kweli na zingine zisizothibitishwa kwamba binti au mvulana fulani ana tabia mbaya. Mabinti wengine wamezushiwa kuwa ni malaya eti tu kwa sababu ana mazoea na wavulana bila kujua kuwa wapo wasichana wanaofanya hivyo si kwa sababu ya umalaya. Wapo waliotuhumiwa kuwa ni walevi, wezi, wavutaji kwa sababu tu ya makundi wanayoshirikiana nayo. Kama watu wamekutuhumu kwa lolote baya na unajua hiyo itakuharibia sifa yako jitulize. Kama tabia hiyo unayo tubu na kwa msaada wa Mungu iache tabia hiyo. Na kama ni kwa sababu ulizalia nyumbani endelea kumlilia Mungu wako ili wanaokulaumu watambue ulifanya kwa ujinga na ya kuwa unajutia kitendo hicho na kwamba Mungu amekusamehe. Usigombane na watu. Wewe endelea kumtumaini Mungu naye atakupa haja za moyo wako.

Uchumba uliokidhi vigezo

Kuoa au kuolewa ni jambo nyeti sana linalohitaji umakini kulipangilia. Ukihisi umefikia wakati unaohitaji kupata mchumba utakayefunga naye ndoa, chukua tahadhari kubwa. “Uangalifu mkubwa ni lazima ufanyike na vijana wa Kikristo katika kuunda urafiki na katika kuchagua mwenzi wa maisha. Uwe macho, isije ikawa kile ukidhaniacho kuwa ni dhahabu kikageuka kuwa chuma cha kawaida.” (Adventist Home uk. 45)

Hakikisha umemshirikisha Mungu kwa kila hatua ya uchumba.   Usikurupuke ukamvamia asiye wako. Mungu wako anakujali na amekuandalia mtu mtakayechukuliana naye. Unachotakiwa ni kumwomba kwa dhati akuoneshe mwenzi aliyekuchagulia. Kumbuka mke mwema mtu hupewa na Bwana. Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.” (Mithali 31:10) “Katika hali ya kawaida ni jambo gumu kumpata mume au mke mwema. Wengine hujikuta wakiambulia waume na wake ambao hawakuwatarajia maishani. Kwa nini? Hawakumwalika Mungu. Mungu anakuomba umshirikishe ili akusaidie kupata mwenzi mwema.

Angalia ahadi za Mungu kwa wanaomtumainia. “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.” (Mithali 19:14). “Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.” (Zaburi 84:11). “Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.” (Zaburi 37:4).  

Kigezo cha mchumba afaaye:

 1. 1.     Chagua Anayempenda Mungu:

Kigezo nambari moja cha mchumba anayefaa ni yule anayemheshimu Mungu. Yule asiyemheshimu Mungu atakuwa kikwazo katika ndoa na matarajio yako.  Ndoa huundwa na watatu. Ninyi wawili kwa upande mmoja na Mungu kwa upande mwingine. “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure.” (Zaburi 127:1). Ikiwa mmoja wenu hana mahusiano na Mungu ni dhahiri safari yenu ya ndoa mtakuwa mmeianza vibaya. Ni lazima kuanza na Mungu katika hatua ya uchumba na kuendelea na Mungu katika kipindi chote cha ndoa vinginevyo muunganiko huo badala ya kuwa mbaraka utakuwa laana. Ikumbukwe ndoa si kitu cha majaribio kwamba baada ya kugundua uliyefunga naye ndoa hafai unaweza kuvunja na kuanza upya. “. . . Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” Mathayo 19:6.

Ni lazima unayeunganishwa naye kwenye ndoa awe unayefanana naye, hasa katika maswala yanayohusu imani. Mungu aliye mwasisi wa ndoa, alipomtafutia Adamu mchumba alimtafutia anayefanana naye. “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” (Mwanzo 2:18). Ni wazi kuwa wasiofanana hawawezi kutembea pamoja. “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?” (Amosi 3:3). Hali kadhalika mpagani hawezi kwenda njia moja na Mkristo. Mungu anawaagiza vijana na watu wazima kutooana na wasio wa imani moja nao. “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza.” (2 Wakorintho 6:14).

Walio kwenye imani moja husaidiana kiroho walio imani tofauti hupingana. “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua!” (Mhubiri 4:9-10). Aliyeoana na asiye wa imani moja naye ni kama aliye peke yake. Atakuwa na wakati mgumu kuilinda imani yake. Vijana wa Kiadventista mnahimizwa kuoa na kuolewa na wenzenu waliopo kanisani. Msijaribiwe kuoa huko nje, waliojaribu kufanya hivyo wamefikwa na matatizo mazito ya kuhuzunisha na sasa wanajutia maamuzi waliyoyafanya ujanani.

 

 1. 2.     Chagua unayempenda

Kigezo cha pili muhimu cha mchumba anayefaa ni yule unayempenda. Kupenda kunakokusudiwa hapa si misisimko au mihemko inayosukumwa na tamaa za mwili bali ni upendo halisi utokao moyoni unaomkubali mtu jinsi alivyo. Yule ambaye Mungu amekuchagulia utamtambua kwa kuona upendo ndani yake; upendo unaokuelekea wewe ukiwa na makusudi ya dhati, ya kudumu, na yasiyofichika. Upendo huo siyo mpofu usioruhusu akili kuchambua na kujiridhisha. Ni upendo usio na haraka, usiolazimisha na usiotafuta faida zake wenyewe. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.” (1 Wakorintho 13:4-7.

Usijilazimishe kuoana na usiyempenda ama kwa sababu ya kumhurumia, kwa sababu ya kuwaridhisha watu fulani au kwa sababu ya kutafuta faida fulani tu. Viapo vya siku ya ndoa vimewekwa ili kuthibitisha kama mnaoana kwa hiari mkisukumwa na upendo peke yake. Zimekuwepo siku hizi ndoa zinazodumu kwa muda mfupi kama hiyo moja niliyowahi kufunga iliyodumu kwa chini ya mwezi mmoja. Inakuwa kama watu wanafanya mzaha na ndoa. Vijana acheni kutafuta sifa ya kuwa mmefunga ndoa na kumbe mna mpango wa kuachana baada ya muda mfupi. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” (Waebrania 13:4).

 

 1. 3.     Vigezo vingine muhimu vya mchumba afaaye:

Mchumba akiwa anampenda Mungu na wewe mwenyewe uwe pia unampenda huyo mchumba hiyo inatosha kukuhakikishia kuwa yeye ni mchumba mwema mradi Mungu awe amekuonesha kuwa huyo ni wako. Kutegemea ndoto au ishara katika kumtambua mchumba ambaye Mungu amekuchagulia si salama katika kizazi hiki cha udanganyifu. Mahusiano yako ya karibu na Mungu, yanatosha kukufanya umfahamu yule aliye wako hasa. Vigezo vingine vya kimo, kabila, utaifa, rangi, elimu, umri, hali ya kiuchumi na kadhalika si muhimu sana katika kuamua mchumba afaaye ingawaje wakati fulani huweza kusaidia. Hata hivyo inashauriwa tofauti ya mambo hayo isiwe kubwa kiasi cha kuathiri maelewano na ukaribu katika ndoa.

Washirikishe watu makini wenye kukutakia mema

Swala zito kama uchumba linahitaji kushirikisha watu makini wenye kukutakia mema. Wajulishe wazazi na kuwauliza ushauri wao. pima ushauri wao na kama unalingana na mashauri ya Mungu uuchukue. Viongozi wa kanisa, marafiki na jamaa wengine utakaowahusisha hakikisha wana sifa ya kuwa watu makini wenye kukutakia mema na wamchao Mungu. Itakapotokea ushauri wa watu hao unapingana na maagizo ya Mungu chukua tahadhari. Mshirikishe zaidi Mungu kwa kuwa na maombi ya dhati ya mara kwa mara huku ukichukua hatua ya kufunga katika siku kadhaa. Mungu atakuelekeza cha kufanya katika kila hatua hata kama kuna magumu yanaweza kujitokeza.

 1. 1.     Nini kifanyike ili kuepuka makosa ya kuchagua mchumba asiyefaa?
 2. 2.     Nini kifanyike kupunguza wimbi la vijana wetu kuoana na wasio wa imanni moja nao?
 3. 3.     Ni muda upi ufaao kuanza kutafuta mchumba?
 4. 4.     Kipindi cha uchumba kinatakiwa kisizidi na kisipungue muda gani? 
 5. 5.     Je ni muhimu kupima afya na mchumba wako ili kujua kama ameathirika?
 6. 6.     Je ni vizuri kumwacha mchumba baada ya kuthibitika ameathirika?

 

JUMATANO

Chukua tahadhari

Usisite kuvunja uchumba, utakapogundua kuwa kuna jambo litakalowaletea shida huko mbeleni kwa kuendelea na uchumba. Mambo hayo yaweza kuwa kukosa uaminifu, udanganyifu, maradhi ya kuambukiza na yasiyotibika nk. Ili kuepuka hatua hii ya kuvunja uchumba ambayo huleta maumivu kwa wahusika, kanisa limeweka utaratibu wa kwenda kupima afya kabla ya kuendelea na uchumba ili ikiwa mmoja wa wachumba ameathirika uchumba uweze kuvunjwa.

Hatua hii ni vema ichukuliwe mapema kabla ya kuwaona wazazi, ili kuepuka usumbufu wa kurudisha mahari na mambo mengine kama hayo. Usijilazimishe kuendelea na uchumba kwa kuwa ulipewa zawadi ambazo sasa zinakulazimu kukubali kuchumbiwa na usiyempenda tena. Ni afadhali kutafuta uwezekano wa kurudisha zawadi hizo (ikiwa mwenye kuzitoa amesisitiza zirudishwe) kuliko kujilazimisha kuolewa naye. Ili kutojiweka kwenye mtego wasichana na wavulana kujiepusha na zawadi. “Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.” (Mithali 15:27)

Epuka ndoa za gharama kubwa

Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwazuia vijana wengi kuoa mapema ni gharama kubwa inayoandamana na mchakato wa kuoa. Gharama hiyo inasemekana huanzia kwenye mahari kubwa wanayotozwa wavulana na wazazi wa binti, ghrama zinazoandamana na tukio la kufunga ndoa, na gharama za sherehe yenyewe ya ndoa. Malalamiko haya kwa sehemu yana ukweli. Kanisa limeendelea kuelimisha wazazi wa mabinti kutotoza mahari kubwa asiyoimudu mvulana anayechumbia. Pale inapowezekana mahari isingetozwa kabisa kwani ni kawaida ya kipagani. Viongozi wa makanisa mahalia wana wajibu wa kuingilia kati pale mchumba anapolalamikia mahari kubwa aliyotozwa ili isiwe kigezo cha wawili hao kushindwa kuoana.

Ndoa ili itambulike ni halali na yenye baraka zote za Mungu, za kanisa, na za wazazi haihitaji mambo mengi kama inavyofanywa leo. Inahitaji wawili wanaooana na wasimamizi wao, wakiwa katika mavazi yoyote ya heshima waliyoyachagua. Kuvaa shela ama suti si sharti la ndoa; ni mapendekezo ya wanandoa wenywe. Kuvaa shela au kutovaa, kuvalishana pete ama kutovalishana, kuwa na wasindikizaji (si wasimamizi) au kutokuwa nao havileti tofauti yoyote kwenye ndoa. Adamu na Eva hawakuwa na vitu hivyo na bado ndoa yao ilikuwa halali na ilidumu kwa muda mrefu kuliko nyingi zinazofungwa kwa mbwembwe leo hii.

Tunawahimiza vijana kufunga ndoa rahisi isiyo na gharama na isiyo na sherehe za anasa. Ndoa yaweza kufungwa siku ya Sabato baada au kabla ya ibada na wanandoa wakarudi nyumbani baada ya ibada wakiwa wamehalalishwa kuwa ni mume na mke. Pale inapokuwa ni lazima kuweka sherehe, viongozi wa makanisa mahalia wahakikishe sherehe zinaisha mapema na zinafanyika kwenye maeneo yanayoleta utukufu kwa Mungu.

Maeneo ya kanisani yakiwekewa mandhari nzuri yanaweza kufaa kwa sherehe hizo kuliko kufanyia ukumbini ambako mara nyingi ni aghali na ambako mazingira yake yanakimbiza uwepo wa Mungu. Kamati za harusi zisiachiwe kuendesha sherehe za vijana wetu kwa kukiuka maadili ya kanisa na kwa kuweka bajeti kubwa isiyo ya lazima inayowafanya vijana wasio na uwezo kuhofia kufunga ndoa zao mapema au kuogopa kufungia kanisani. Wengine kwa kuogopa hali hiyo wameenda kufungia ndoa zao serikalini na hata wengine wamediriki kuchukuana bila ndoa. Matokeo yake idadi ya ndoa za kubariki kwenye makanisa yetu mengine imezidi ile ya wanaofunga ndoa mpya. Tutafika wapi na hali hii?

Tusiige wamataifa waendeshavyo michakato ya ndoa.

Ni kweli kuwa kanisa siyo kisiwa na kwa hiyo haliwezi kujitenga kabisa na yote yatokeayo katika jamii. Hata hivyo tahadhari imetolewa kujiepusha na mitindo inayoibuka isiyo na mwonekano wa kiristo au unaokubalika katika jamii. Swala la ndoa namna inavyofanywa leo ina kila dalili kuwa imeingiliwa. Hatukuwa na Send off, na kitchen party pale zamani lakini sasa vimeshamiri. Hatukuwa na watoto watanguliao mbele ya msafara kama mfano wa maharusi lakini leo wapo. Hatukuwa shampaign kwenye sherehe za harusi lakini leo zipo. Kwa ujumla hatukuwa na mambo mengi ambayo leo hii yamo hasa katika ndoa zinazofungwa mjini.

Ushauri hapa ni kuwa ikiwa ni lazima kumwaga binti yako basi iwe sherehe ya kawaida isiyo na gharama kubwa ikiwahusisha ndugu wachache wa karibu na ikiwezekana ifanyikie nyumbani. Lengo hapa liwe kumpatia binti wosia ambao pengine usingefaa kutolewa siku ya harusi kutokana na ufinyu wa nafasi siku hiyo au unyeti wa mashauri yenyewe. Wosia uhusu pamoja na mambo mengine namna ya kudumisha maadili mema aliyojifunza hapo nyumbani, na jinsi ya kuhusiana na mume mtarajiwa, ndugu, na watu watakaowatembelea au watakaokuja kuishi hapo nyumbani kwao.  Jambo hilo likifanyika kiroho si tu kwamba litawaongoa waliohudhuria bali litawafanya kutamani kuiga na hivyo kuwa jambo lenye mbaraka kwa wengine. Hata hivyo mara nyingi imeonekana sherehe hii ya kumwaga binti ingefaa ifanyike mara baada ya kufunga ndoa na si kabla. Makanisa yaendelee kulitolea elimu jambo hili.

Shughuli za Ibada ya ndoa na sherehe za harusi vithibitiwe na makanisa mahalia yakishirikiana na wazazi wa maharusi ili kuzuia kuwepo kwa mambo yatakayoondoa utukufu wa Mungu.  Mavazi ya maharusi na wasindikizaji wao, ni lazima yawe ya adabu na yanayosetiri mwili. “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani.” (1 Timotheo 2:9). Mazoea ya kuwaweka watoto kama mfano wa maharusi zinashusha utukufu wa tendo lenyewe. Ifahamike ile inayofanyika pale kanisani ni ibada kamili ya ndoa yenye kicho kama ibada zingine zote. Hapatakiwi vigelegele, wala mbwembwe na matangazo ya mshereheshaji (MC) na mambo mengine kama hayo yanayofukuza uwepo wa Mungu.

Maisha baada ya ndoa

Mungu alianzisha ndoa ili watu wakae pamoja kwa umoja na kujifunza kupendana. Zaburi 133:1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kweli kuwa kupendana ni jambo gumu kwetu wanadamu hasa pale kila mmoja wetu anapoifikiria nafsi yake tu. Mungu alitufundisha kupendana pale alipotupenda kuliko nafsi yake. Wafilipi 2:6-8 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Yesu aliteswa na kudhihakiwa kwa ajili yetu.

Kwa kuianzisha ndoa, Mungu alitaka tuendeleze upendo huo baina yetu wenyewe kwa wenyewe. Viumbe karibu wote wanajaribu kufanya hivyo. Sijawahi kuona kwa mfano ugomvi wa kuku wa jinsia mbili tofauti. Ukiwaona watakuwa ni watoto wasiojua kupenda, ila wale wakubwa huwa hawapigani. Jogoo akitaka kupigana humtafuta jogoo mwenzake. Ugomvi baina ya mwanaume na mwanamke au mume na mke huonekana mara nyingi kwa wanadamu pekee. Je, hii ni kudhihirisha kuwa sisi tumeathirika zaidi na dhambi?

Jogoo huonesha heshima kubwa kwa kuku jike kiasi cha kuchukua muda wake kumtafutia chakula na kufanya ishara ya kumwalika kwenye chakula hicho. Na haya huyafanya kumhakikishia kuwa yeye akiwa karibu atambue yupo ndani ya mikono salama. Kwa nini hali hiyo wakati fulani inaadimika kwa wanadamu hadi wengine kufikia hatua ya kuona ni afadhali kuishi peke yake kuliko kuishi na mwanamke?

Anza na Bwana

Kipi ni sahihi zaidi, kukaa peke yako au kukaa na mwenzi wa maisha? Inadhaniwa kuwa Mwandishi wa Mhubiri na wa Mithali ni yule yule mfalme Suleimani. Katika Mhubiri 4:9 anasema, “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao,” Lakini tena katika Mithali 21:9 anasema, “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.” Haya mafungu mawili yanaonekana kupingana huku moja likishauri ni heri kukaa wawili na jingine likishauri ni heri kukaa peke yako. Lipi ni wazo sahihi kati ya haya mawili?

Ni kweli kuwa huyo wa pili unayekaa naye akiwa mgomvi ni heri kukaa peke yako. Ndoa na familia nyingi zinaathiriwa na magomvi ya mra kwa mara. Magomvi mengi yatokeayo nyumbani ni sababu ya kumfungia nje yeye aliye mwanzilishi wa ndoa. “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” (Yohana 15:5) Wengine wamejikuta katika matatizo ya unyumba sit u kwa sababu walimwacha Mungu hapo njiani bali hata hawakuanza naye.  Unapoanza na Mungu kwenye maisha ya ndoa mibaraka yake huwa tele nyumbani. Wale ambao mlitoroshana na mnaendelea kuishi bila ndoa nawashauri mkabariki ndoa zenu au kama vipi mkafungie serikalini ili zitambuliwe kisheria.

Wengine mnaishi bila ndoa na bila ridhaa ya wazazi. Hiyo ni mbaya zaidi. Unatarajiaje kunyookewa na maisha wakati mnaishi kwa kificho kiasi hicho? Wale mnaoishi bila kujitambulisha kwa wazazi (ridhaa) nawashauri hebu nendeni mkawaone wazazi mpate baraka zao. Kuishi kama watu mnaofanya majaribio kwenye ndoa ni jambo lisilofaa kabisa. Moja ya matatizo ya kisheria utakayoyapata (hasa wewe mwanamke) siku mumeo atakapofariki utakuwa na wakati mgumu kuwashawishi ndugu wa marehemu kuwa wewe ni mjane na mrithi halali wa mali na watoto.

Hata wale waliofunga ndoa zao serikalini, kanisa linawapa fursa ya kuja kuzibariki ndoa hizo kanisani. Na kwa wale walioanza kuishi pamoja bila cheti cha ndoa nao wanaalikwa kuja kubariki ndoa zao na kuzirasimisha kwa kuwapatia cheti cha ndoa kinachotambulika kisheria. Ili Mungu aendelee kukaa na wewe uliye kwenye ndoa, ni lazima umtengenezee mazingira ya kumwalika. Someni Neno lake pamoja. Ombeni mnapoamka na mnapoenda kulala na wakati wa chakula. Tengeni muda wa kufanya kazi ya Mungu kwa kutembelea majirani zenu na kujifunza nao kile ukijuacho kuhusu Mungu. Kwa njia hiyo mtakuwa unaupalilia upendo wenu na Mungu atawafundisha kupendana. “Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.” (1 Wathesalonike 4:9)

 1. 1.     Je, kubariki ndoa ni jambo linalolingana na mapenzi ya Mungu?
 2. 2.     Je, sherehe gani ni za muhimu kabla ya kufunga ndoa na kwa nini?
 3. 3.     Je kuna mambo yanayohitaji mabadiliko katika namna tunavyofunga ndoa zetu leo? Yataje.
 4. 4.     Je, kanisa lako linaweza kufanya nini kusaidia vijana kubeba gharama za ndoa na sherehe za harusi?

 

ALHAMISI

Kuupalilia upendo.

Ukimpenda mtu utafikiria kumtendea mema tu. “Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.” (Mithali 31:10-12). Matatizo mengi ndani ya nyumba huja pale mnapotafutana mabaya. “Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.” (Mithali 17:13). Usitafute mabaya ya mwenzako kwa nia ya kumuumbua, kumkejeli au kumkosesha amani. Usitafute kujua kama nyuki wanauma kwa kuwarushia mawe kwenye mzinga. Kupenda kunahitaji nidhamu. Kupendana kunaendana na kustahiana. “Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.” (Waefeso 5:33).

Upendo hauji wenyewe bila kupaliliwa. Njia mojawapo ya kupalilia upendo ni kutaja waziwazi bila kificho mazuri ya mwenzako. Tafuta mema yake na kuyataja mbele yake. Mithali 31:29 Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote. Mwambie akisikia kwamba unampenda. Mtu anayejua kwamba anapendwa huongeza juhudi ya kufanya vyema zaidi. Msifu pia anapofanya jambo jema. Isaya 41:7 Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. Kuishi kwa upendo ni jambo la kuchagua. Maneno mengine yanayoimarisha mahusiano kwenye ndoa ni maneno kama, samahani, pole, asante, naomba, na nakupenda nk.

Maneno yenye neema

“Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” (Wakolosai 4:6). Sote tunajua chakula kisicho na chumvi kisivyo na ladha. Ndivyo yalivyo maneno yaliyojaa ukali na kukatishana tamaa. Yanaharibu anayeyatoa na anayeyasikia pia. Yanaharibu hali ya hewa na yanafukuza uwepo wa Mungu.  Majibu ya hasira ni mabaya yanachoea hasira hivyo yaepukeni kwenye nyumba yenu. “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.” (Mithali 15:1).

Kila mmoja awe na hekima ya kujua mazungumzo yanayoendelea kama yanaweza kuzaa  amani ama yatazua vita. Na ukishagundua yatazaa vita iepushe vita isitokee. Maneno yaumizayo siku zote huzaa magomvi. Ni sawa na kupiga ngumi pua unategemea nini kitatokea? Ni damu itatokea. “Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.” (Mithali 30:33)

Usitafute pua ya kupiga ili mwenzako atoke damu. Jizuie na kukubali uonekane mjinga kwa kuepusha magomvi. Mungu humchukulia yule anayeepusha magomvi kama mwenye busara na anayechochea ugomvi kama mjinga.  “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.” (Mithali 22:3). Wengi wanaopata majeraha na vilema vya kudumu kutokana na magomvi ya kwenye ndoa waliyapata kutokana na kuwa wabishi wasiokubali ushauri huu wa Mungu wa kunyenyekea na kujibu kwa hekima.

Kaeni kwa amani na watu wote

Amani ni hitaji la kwanza kwa kila jamii. Amani ni hitaji muhimu kwa kila familia. Kwa nini familia na jamii nyingi hazina amani? Nini kifanyike ili kurejesha amani iliyotoweka? Hili ndilo somo letu la leo. Ni kweli kuwa mawasiliano na mahusiano mabaya yamechangia kuondoa amani nyumbani. Lakini sababu ya msingi ya kukosekana kwa mahusiano na mawasiliano mazuri nyumbani ni kukosekana kwa roho ya msamaha. Yesu anapendekeza kwetu. “Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.” (Luka 17:3-4) Amani ya kweli haiwezi kuwepo mioyoni mwa watu wasiosamehe.

Msamaha ni kwa faida ya nani?

Kusamehe kwa sehemu kubwa kunaleta nafuu na msaada kwa yule anayesamehe kabla hakujaleta nafuu kwa anayesamehewa. Kusamehe kunadhihirisha kuwa mtu ana moyo mkuu unaoweza kutawala hisia. Wengine kwa kukosa kusamehe wamejikuta wakitenda makosa ya jinai ya kuua, kupiga, kutukana na hata kupeana talaka. Talaka haitatui tatizo bali inalikuza na kuwaingiza kwenye mgogoro wasiohusika na ugomvi huo yaani watoto.

Moja ya vitu vilivyozoeleka sana leo kwa wanadamu na ambacho Mungu anakichukia sana ni talaka. “Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.” (Malaki 2:16). Kuachana ni jambo lenye maumivu makali kwa sababu waliooana walipoambatana walishikamana kama karatasi mbili zinazounganishwa kwa gundi zinavyokuwa vigumu kuziachanisha. Lazima upande mmoja wa karatasi utaenda upande mwingine. Hivyo ndivyo walivyoachana wanavyopitia maumivu.

Badala ya kugombana ama kuachana watu wanatakiwa kuondoa tofauti zao kwa mazungumzo wakiweka mbele nia ya kusamehe. Kusamehe kwa kweli hakuhamasishwi na namna upande wa pili unavyolipokea kosa. Kusamehe kunatangulia hata kabla upande wa pili haujakiri kosa. Yesu alipowasamehe waliokuwa wakimsulubisha hakufanya hivyo kwa sababu walionyesha toba kwa makosa yao. Yesu aliwasamehe kwa sababu aliona wanahitaji msamaha ili uwasaidie kurudi katika fahamu zao na watambue ubaya wa kile wanachofanya. “Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.” (Luka 23:34)

Njia moja ya kupata ujasiri wa kusamehe watu ni kuwachukulia kama ambao hawajui watendalo. Sote tunatambua kuwa ni rahisi kusamehe kosa linapotendwa na mtoto mdogo ama kichaa wakati ni vigumu kusamehe kosa lile lile linapokuwa limetendwa na mtu mzima. Kwa nini? Kiwango cha maumivu huongezeka unapotambua kuwa aliyekutendea alifanya kwa makusudi. Wafanyao makosa kwa wenzao mara nyingi wanakuwa wameghafilika, ama kwa sababu ya hasira ama tafsiri potofu, ama kuchoka, ama kuumwa, ama msongo wa mawazo nk. Unapokosewa jitahidi kuangalia upande wa pili wa yule aliyekukosea na utafute namna ya kumrejesha. “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.” (Wagalatia 6:1)

Hakuna aliye Mwema

Namna nyingine ya kujihakikishia unakuwa na amani moyoni ni kutojidhania kuwa umekuwa mkamilifu. Biblia inatuthibitishia kuwa hakuna aliye mkamilifu katika wanadamu ila Yesu tu. “Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.” (Mhubiri 7:20) Watu wengine wameingia kwenye migogoro na wenzao kwenye ndoa kutokana na kukataa kukiri makosa. Watu wanaopenda kulumbana ili waonekane hawana makosa watakuwa na kibarua kigumu kuzifanya nyumba zao kuwa na amani ya kweli.

Nataka nikuambie hata kama utakuwa bingwa wa kusukumia wengine makosa yako hiyo haitakuletea amani ya kweli. Utakanusha, kwa viapo na ushahidi bandia na kufanikiwa kushawishi watu lakini amani ya moyoni itakosekana. Na kukosekana huko kwa amani kutakufanya ufanye makosa mengi zaidi na kukosana na watu wengi zaidi. Njia sahihi ni kutafuta amani ya moyoni kwa njia ya toba ya kweli. “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.” (Zaburi 32:1-2) Mungu anatutaka tuwe na amani na watu wote. Huwezi kuwa na amani moyoni kama huna amani na wenzako.  “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.” Warumi 12:18

Chukulianeni mizigo

Mojawapo ya jukumu la muhimu la wanandoa wanaoishi pamoja ni kufahamiana tabia. Mtu yeyote unapomfahamu tabia huwa ni rahisi kuishi naye. Kwa kawaida tabia zimegawanyika. Zipo zile zinazoweza kurekebishika kirahisi na zile ambazo kurekebishika kwake huchukua muda mrefu. Mfano, tabia ya kucheka kwa sauti kubwa au kupiga miayo kila wakati, tabia ya kutafuna chakula kwa kutoa sauti na bila kufumba mdomo, tabia ya kupandisha makamasi, tabia ya kuweka vidole puani, tabia ya kuweka mikono nyuma au mifukoni unapoongea, tabia ya kukoroma unapolala, tabia ya kufikicha masikio kwa vidole na tabia nyingi nyingine kama hizo mtu huzaliwa nazo na hubadilika kwa shida sana.

Tabia nyingine ya kupenda kutawala na kuwatumia wengine, au tabia ya kuongea sana hata kukosa usiri, au tabia ya kuwa na misimamo isiyotaka kubadilika, au tabia ya unyamazifu uliovuka mipaka ni tabia pia zilizo ngumu kubadilika na ambazo kwa namna fulani watu wamezaliwa nazo. Ikiwa wanaoishi pamoja wana tabia hizo zilizotajwa na zinazokinzana kuna uwezekano wa migongano kutokea. Njia ya kuepuka hiyo migongano ni kuchukuliana. “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.” (Wagalatia 6:2)

Yesu alituchukulia mizigo pale alipokubali kufanya urafiki na sisi wakati akijua tu watukutu. Urafiki wake na sisi haukuwa wa kulazimishwa bali wa hiari, kama ambavyo urafiki wako na huyo mwenzi wako wa maisha ulivyo wa hiari.  Kama Kristo aliweza kuchukuliana nasi kwa nini sisi tushindwe kuchukuliana? 3:13 “Mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” (Wakolosai). Katika hali ya kawaida huwa rahisi kwetu sisi wanadamu wenye dhambi kuchukuliana kuliko Mungu asiye na dhambi kutuchukulia sisi wenye dhambi. Lakini uzoefu unaonesha kuwa mambo ni kinyume kwa kuwa Mungu anatuchukulia sisi kirahisi kuliko sisi wenyewe wadhambi tunavyochukuliana.

Wakati mwingine mambo yanayoweza kuleta ugomvi na mke kushindwa kupika vizuri au kushindwa kuwa msafi. Mambo haya uliyajua wakati unamuoa kwa nini leo unayanung’unikia hata kwa watu walio nje? Mambo haya si uliyajua kabla hujamuoa? Unachotakiwa ni kumsaidia kubadilika kwa upendo si kwa kumdhalilisha na kumuumbua mbele za watu. Watu wanaoelekezwa kwa upendo hubadilika.

Maandiko yanakataza wanaume kuwa na uchungu na wake zao. Wakolosai 3:19 Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Usiwe na donge limekukaa tangu asubuhi hadi jioni kwa ajili ya mwenzi wako wa maisha. Tabia ya kununiana na kutosemeshana kati ya wanandoa haifai hata kidogo. Licha ya kuharibu mahusiano yenu inaharibu afya ya mwili pia. Ni sawa na mtu anayejilundikia sumu mwilini. Matokeo yake ni vidonda vya tumbo, mashinikizo ya damu na kupungua kwa kinga mwilini. Mnapofanya hivyo pia mnamkaribisha shetani katikati yenu. Biblia imeagiza kutoelewana kukitokea kusiruhusiwe kudumu zaidi ya masaa ishiri na manne. “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;wala msimpe Ibilisi nafasi.”  (Waefeso 4:26-27).

Mambo yasuluhishwe mapema iwezekanavyo. Msiache kiporo cha magomvi ya miaka mitatu minne kabla hayajasuluhishwa. Na mambo hayo yakisha suluhishwa yasibaki katika kumbukumbu zenu. Tufanye kama Mungu afanyavyo anapotusamehe. Mungu anapotusamehe anazifuta dhambi zetu na kuzisahau. “Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena.” (Waebrania 8:12)

 1. 1.     Kwa nini ni muhimu kuchukuliana mizigo katika mahusiano ya ndoa?


IJUMAA

Chunga mdomo wako

Ili kusameheane kuwe rahisi msitamkiane maneno magumu yasiyoweza kufutika kirahisi. Jizuie kumtukania mwenzi wako mama yake au baba yake au kusema ulemavu au udhaifu ulio nyumbani kwao. Hata kama mmetofautiana kiasi gani jizueni kutukanana. Tabia ya kutukanana imepitwa na wakati. Watu wastaarabu huwa hawatukanani. “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya.” (Waefeso 4:29, 31).

Tena kama ninyi ni watumishi wa Mungu au mnaomwamini Mungu haifai kabisa kugombana kwa kupigana ama kuumbuana kwa matusi ya hadharani au faraghani.  “Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.” (2 Timotheo 2:24-26)

Ibrahimu hakuitwa bure baba wa imani, maana yeye hakuwa mgomvi. Alijua kuepuka magomvi wakati mwingine kwa kukubali kuingia hasara. “Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi.Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu.”  (Mwanzo 13:7-8) usiwe na mazoea ya kupeleka kwa mjumbe au kiongozi wa dini, kila aina ya ugomvi unaotokea. Jaribuni kuyasuluhisha mambo hayo ninyi wenyewe mkitegemea hekima ya Mungu naye atawasaidia.

Malezi ya watoto

Watoto ni sehemu ya ndoa na familia na ni jambo la mbaraka kuwa nao. Kusudi mojawapo la Mungu la kuanzisha ndoa ni kuunda taasisi ambayo ingehakikisha wanadamu wanaongezeka kwa njia ya mwanamke kushika ujauzito na kuzaa watoto. Mpango huo haujabadilika. Kwa bahati mbaya kutokana na dhambi, ndoa zingine zimekosa kupata watoto ama kutokana na mke kushindwa kushika ujauzito ama kutokana na mimba kuharibika au watoto kufariki wakiwa wachanga. Matatizo ya mke kutoshika mimba au kuchelewa kushika mimba, hutokana na sababu nyingi zingine zikiwahusu wanandoa wenyewe, mazingira, na zingine zikiwa hazijulikani sababu zake kwa usahihi.

Tunawahimiza wanandoa wenye kupitia hali hiyo ya kukosa uzazi, kuwaona wataalamu wa afya ambao wamekuwa wakitoa ushauri mbalimbali ambao umewasaidia wengine kupata watoto. Matatizo yanayosababisha kutoshika ujauzito si lazima yatokane na mwanamke. Wakati mwingi matatizo hayo yameonekana kusababishwa na mume kutoa mbegu zilizo hafifu zisizoweza kushika mimba. Tatizo hilo linaweza kurekebishwa kirahisi kwa kubadili mtindo wa maisha kwa kadri utakavyoelekezwa na wataalamu. Hata hivyo ifahamike kuwa watoto hawahalalishi kuwepo kwa ndoa. Ndoa isiyo na watoto ni ndoa halali kabisa kama ile yenye watoto. Mtu asijaribiwe kumwacha mkewe au kuongeza mke wa pili kwa kuwa tu mke aliyenaye hajampatia mtoto.

Kuzaa kwa mpango

Pamoja na kuwa watoto ni mbaraka, lakini watoto hao wakija bila mpango maalumu hugeuka kuwa laana na familia hiyo huingia lawamani. Watoto wana mahitaji yao ya msingi ambayo hawapaswi kunyimwa. Watoto wanahitaji chakula, mavazi, malazi, matibabu, elimu nk. Watoto ili wayapate mahitaji hayo kwa uwiano unaofaa ni lazima wapangiliwe waje lini, wapishane umri kwa umbali gani, na waje idadi gani. Mungu aliposema “mkaijaze nchi” hakusema hilo kwa familia moja tu. Hivyo usijidanganye kuwa wewe peke yako utaijaza nchi kwa kuleta watoto wengi duniani.

Ikiwa uwezo wako wa kuwatunza watoto unaishia watoto watatu basi ishia hao hao watatu. Lakini kama uwezo unakuruhusu kuongeza basi pia waweza ongeza. Kanuni ya msingi ni kuhakikisha hushindwi kuwatunza watoto wako. “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” (1 Timotheo 5:8). Njia utakayotumia kuhakikisha unakuwa na idadi ya watoto uliyoichagua utapanga wewe na mwenzako. Kwa bahati mbaya njia nyingi za kitaalamu na za kienyeji zinazotumika kupanga uzazi si za kuaminika na zina madhara kiafya. Jambo la muhimu ni kupata ushauri wa wataalamu na wenye uzoefu ili kujua ni njia gani bora utatumia kupanga uzazi.

Inashauriwa kuwa wanandoa wapya wasikimbilie kupata mtoto hadi watakapoishi kwa muda wa kutosha wakizoeana na kufurahia maisha mapya ya ndoa. Kwa kawaida watoto wana kawaida ya kunyang’anya upendo wa mama (ule aliokuwa anautoa kwa mume) jambo linaloweza kukaribisha migogoro isiyo ya lazima mapema. Hata hivyo wengine huona ni vyema kupata idadi ya watoto wanaowahitaji mapema ili wawe na muda wa kuwalea na kufurahia ndoa yao. Ili kuwasaidia kumudu majukumu ya malezi na kumsaidia mama kurudisha afya yake inashauriwa watoto wapishane umri wa kuanzia miaka mitatu.

Wengine wametatizika kwenye ndoa zao sababu ya kukosa watoto wa kike au wa kiume. Hiyo imewafanya baadhi kujikuta wakizaa watoto wengi ambao hawakuwahitaji kwa matarajio ya kumpata mtoto wa jinsia nyingine iliyekosekana. Mtoto ni mtoto tu haijalishi ni mwanaume ama ni mwanamke. Wapo waliotunzwa vizuri na watoto wao wa kike kuliko wa kiume na wapo waliotunzwa vizuri na watoto wao wa kiume kuliko wa kike. Kinachohitajika ni kuwapatia mahitaji yao na kuwarithisha maadili mema. Hata hivyo leo wataalamu wanajua namna ya kuwawezesha wanandoa kupata mtoto wa jinsia wanayoitaka, waoneni wataalamu hao wawasaidie.  

Njia nyingine ya kukabili tatizo la kutopata mtoto kwenye ndoa ni kuchukua watoto wasio na wazazi kutoka kwa mamlaka husika na kuwarithi kama wanao. Hiyo ingekuwa njia bora zaidi ya kupunguza watoto wasio na walezi duniani. Ni nani ajuaye kama Mungu hakuruhusu usipate mtoto wako mwenyewe ili umlee huyu mtoto wa mwenzako ambaye hayupo duniani? Wengine wamepata Baraka kubwa kwa kulea watoto wa namna hiyo. Ikiwa hilo litakuwa gumu basi amueni kukaa na watoto wa ndugu zenu walio katika mazingira magumu, mkiwasomesha na kuwasaidia kuwa raia wema wa hapa duniani na ufalme ule ujao. “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.” (Mwanzo 12:5)

Njia nyingine ya kukabili tatizo la kukosa au kuchelewa kupata mtoto ni kuwa na maombi. Hana alikuwa na tatizo hilo na Sara mkewe Ibrahimu naye alikuwa na tatizo hilo hilo. Hawa na wengineo wengi waliotajwa kwenye Biblia walilikabili tatizo hilo kwa kutumia maombi. “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.” (1 Samwel 1:10-11, 20). Maombi ni sayansi ya ajabu inayofungua yaliyoshindikana na wanadamu. Usikate tamaa upesi hebu ijaribu njia hii maana kupitia njia hii wengi wameweza kupata watoto.

 1. 1.     Kwa nini kulea ni kugumu kuliko kuzaa?
 2. 2.     Tutumie njia gani kuhakikisha tuna idadi ya watoto tunaowamudu kuwahudumia?
 3. 3.     Kwa nini watoto wa mitaani wamekuwa wakiongezeka?
 4. 4.     Kanisa lako linawasaidiaje wajane katika kutunza watoto wao?

 

JUMAMOSI

Malenzi yanaanza lini?

Malezi ya watoto huanza wakati mtoto akiwa bado tumboni. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mtoto hujifunza mwenyewe anapofikisha miezi kadhaa kabla ya kuzaliwa. Upo wakati mtoto aliye tumboni husikia kinachoendelea nje ya tumbo na hupokea mawasiliano kupitia mazungumzo, nyimbo, maombi nk.  “Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.” (Luka 1:44). Huu ni udhihirisho wa kutosha kuwa kitoto   kichanga kina uwezo wa kufanya mawasiliano na walio nje wakati kikiwa tumboni mwa mamaye. Mtoto aliye tumboni anahitaji kuzungukwa na mandhari yenye amani, tulivu, ikiwa na mazungumzo yenye amani, nyimbo za kiroho na maombi mengi. Ikiwa patakuwa na patashika ya magomvi wakati wa ujauzito kuna uwezekano wa magomvi hayo kumwathiri mtoto.

Kitu kingine ambacho ni muhimu kwa makuzi ya mtoto akiwa tumboni ni chakula na vinywaji anavyotumia mama mjamzito. Watoto wanaozaliwa wakiwa na majukumu muhimu ya kubeba katika jamii lazima wakuzwe katika mazingira ya kuwaepusha na mazoea ya kula na kunywa vinayopingana na kanuni za afya. “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi.” (Waamuzi 13:2-4). Pombe, uvutaji sigara, na ulaji wa wanyama najisi unaofanywa na mama mjamzito, hudhuru afya ya mtoto tangu akiwa tumboni.

Mkinge mwanao

Kanisa linawahimiza wakina mama wajawazito na wenye vitoto vichanga kujiunga na madarasa ya watoto wakati wa vipindi vya shule ya Sabato ili kuwasaidia watoto wao waliojifungua na walio matumboni kupata mafunzo yao yanayowastahili. Mtoto azoezwe kuomba kabla ya kunyonya na kabla ya kulala hata wakati akiwa mchanga kabisa. Mtoto aendelee kuimbiwa nyimbo za kiroho na kumweka mbali na miziki yenye midundo mizito ya kidunia. Mama aliyejifungua asikawie bila sababu kumleta mtoto kanisani ili apate mafunzo yanayomhusu.

Kuwekewa mikono watoto

Kila inapowezekana mtoto afanyiwe huduma ya kuwekewa mikono mapema sana bila kusubiri hadi amekuwa mkubwa wa kutembea mwenyewe. Huduma ya kuwekewa mikono inafanywa kwa watoto wachanga ili kuwaimarishia ulinzi wao wa kiroho na kimwili. Siku ya kuwekewa mikono mtoto aandaliwe sadaka ya shukurani, picha za ukumbusho, na sherehe fupi. Picha za matukio mbalimbali ya mtoto katika hatua za ukuaji wake zihifadhiwe vizuri kwa ajili ya kumbukumbu yake atakapokuwa mtu mzima. Sambamba na kuwa na cheti cha ubarikio (kuwekewa mikono) ifanyike jitihada ya kuhakikisha mtoto anapata cheti chake cha kuzaliwa mapema. Wazazi wanapaswa kuzingatia maagizo wanayopewa wakati wa kuwekewa mikono watoto. Watoto wapewe kipaumbele katika kuwapatia lesson zao kila robo na wazoezwe pia kuendesha mijadala ya lesson nyumbani.

Watoto watahadharishwe kuwa makini na watu wanaowabembeleza kwa zawadi na kuwashika shika kwenye sehemu za miili yao. Usiwaruhusu watoto kulala kitanda kimoja na wageni wanaotembelea hapo nyumbani kwako hata kama ni ndugu wa karibu, maana wengine kwa kufanya hivyo walisababisha watoto wao kulawitiwa. Watoto wasipewe uhuru unaovuka mipaka. Wapangiwe ratiba ya mambo ya kufanya hata wanapokuwa likizo. Mama asifanye kazi zote za nyumbani bila kuwashirikisha watoto. Hata kama kuna msichana wa kazi asiwe wa kufanya kazi zote na watoto wakiwa hawajui hata kutandika vitanda vyao wenyewe.

Watoto wanahitaji kucheza michezo yao ya kitoto. Usiwazuie. Wakina baba wengi huwa si wavumilivu kwa michezo ya watoto ambayo huandamana na kuwepo kwa zana nyingi za mifano ya magari, wanasesere, kuchorachora ardhini na hata kwenye samani, kuchimba chimba vishimo na kadhalika, ambavyo kwa kiasi fulani huharibu mazingira. “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.” (Waefeso 6:4) “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” (Wakolosai 3:21). Ukali wa wazazi kama hao ndiyo uliowakimbiza baadhi ya watoto na sasa wapo mitaani wakiitwa watoto wa mitaani. Watoto wanahitaji kuoneshwa upendo.

Pale inapokuwa lazima ni muhimu watoto waadhibiwe. Kumwadhibu mtoto kuna lengo la kumrekebisha tabia na si kumharibu. Adhabu ilingane na uzito wa kosa na uwezo wa mtoto kuistahimili. Usimhurumie sana mtoto kiasi cha kumwacha afanye apendacho. “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.” (Mithali 23:13). Kuiga utamaduni wa kimagharibi unaozuia kuadhibu watoto kunapingana na mashauri ya Mungu. Watoto wasioadhibiwa huwa wajinga. “Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.” (Mithali 22:15).

Unapomwadhibu mtoto jitahidi kumjulisha sababu ya kumwadhibu na uhakikishe ameridhika na sababu hiyo vinginevyo utamtengenezea usugu na roho ya chuki. Adhabu inapotolewa iafikiwe na wazazi wote wawili na kusiwepo na kusalitiana. Wakina mama wamelaumiwa sana kwa kuacha adhabu zote zitolewe na baba. Hata kosa lililotendwa baba akiwa safarini husubiri baba arudi ili alitolee adhabu. Watoto wanakuwa wakimuona baba kuwa katili kuliko mama na mtoto huyu akiwa mtu mzima ana uwezekano wa kumhudumia vizuri zaidi mama kuliko baba. Wakina mama msitafute kuonekana wazuri kwa watoto wenu kwa kuwapendelea wasiadhibiwe.

Mambo mengine ya kubagua watoto yanatokana na watoto wa kambo. Kawaida ni kuwa ukimpenda mtu mpende na watoto wake. Hakuna sababu ya kuwabagua watoto wa mumeo au mkeo eti kwa kuwa hukuwazaa. Mradi mmekubaliana kuishi pamoja wafanyeni watoto wenu kujisikia wamoja. Kubaguana kunaweza kuzua vita mbaya nyumbani kwako. Kubaguana kwingine kunatokana ama mtoto fulani amefanana na baba au mama na ama anaitwa kwa jina la baba yako au mama yako. Tujifunze kutoka kwa Yakobo alivyompendelea Yusufu. Ndugu zake walimchukia hadi wakamuuza utumwani. “Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.” (Mwanzo 37:3-4). Kupendelea watoto hakufai kabisa.

Wokovu wa watoto kwa sehemu kubwa unategemea wazazi wao. Halikadhalika kuangamia kwa watoto kunategemea misimamo ya wazazi. Watoto hujifunza kwa kuangalia na kwa kusikia yale yatokayo kwa wazazi wao. Wataalamu wanatuambia watoto hujifunza mengi yanayojenga tabia zao za ukubwani wakiwa watoto.  Hujifunza kwa uzuri zaidi kwa njia ya kuona kuliko kusikia ama kwa njia ya kusikia kunakoandamana na kuona. Ndiyo maana waswahili wakasema samaki mkunje angali mbichi maana akikauka atavunjika. Mazoea yaliyojengeka utotoni ni vigumu kuyageuza ukubwani. “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.” (Mithali 22:6).

Ikiwa mzazi atakuwa mwaminifu kwa Mungu na kuwarithisha wanawe mambo yale ajifunzayo kwa Mungu kwa bidii, watoto hao hata kama hapo katikati wataiacha imani, wakifikia utu uzima kuna uwezekano wa kuirejea imani yao ya zamani.  Hakuna urithi wa maana anaowekeza mzazi kwa watoto kama elimu ya kumjua Mungu. Mzazi usikubali mwanao asome shule inayomnyima mwanao fursa ya kutunza Sabato kama ilivyoagizwa na Maandiko Matakatifu. Mtoto huyu hata kama atafaulu vizuri masomo yake, atakuwa amepungukiwa uadilifu. Wazazi wenye kuwathamini watoto wao watajitahidi kuwasisitiza kumheshimu Mungu. 

Kanisa la Waadventista wa Sabato, limeweka utaratibu nzuri unaowahusu watoto. Idara ya shule ya Sabato ya Watoto, Idara ya Watoto, vyama vya Wavumbuzi na Watafutanjia ni vyote hivyo ni vitengo ndani ya kanisa vinavumuandaa vyema mtoto. Usiache kumhimiza mwanao kushiriki katika vitengo hivyo na kujitahidi kumtimizia mahitaji yake kama yanavyolekezwa na vitengo hivyo. Watoto wanaokosa miongozo, makadi na sare za vyama vyao huumia na kukatishwa tamaa. Usiache mwanao aonekane kituko katikati ya wenzake.

Wajane, walioachika na waishio peke yao

Wajane, walioachika na waishio peke yao ni makundi mengine yanayojisikia kutengwa na jamii na ambayo kanisa ni lazima ifanye jitihada ya kuyafikia na kuyahudumia. Wajane ni wanawake waliofiwa na waume zao wakati wagane ni wanaume waliofiwa na wake zao. “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.” (Matendo 6:1). Kilio cha wajane kusahauliwa hata leo kipo. Wanasahauliwa kutembelewa; wanasahauliwa hata kuandaliwa masomo yao makanisani na kwenye makambi. Makanisa yaanishe wajane ilionayo wakiwapanga wale wenye uwezekano wa kuolewa tena na wale ambao umri umepita. Wale wafaao kuoa na kuolewa wahimizwe kuwa na wachumba.

Biblia inawataja wajane kama walioonesha kiwango cha juu cha imani na waliowategemeza watumishi wa Mungu. “Wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.” (Luka 4:26). Hii inatupa picha kuwa licha ya kuondokewa na wenzi wao, wajane na wagane wanayo kazi ambayo Mungu angetaka waifanye. Wanatakiwa kujikita katika kufanya kazi zao za mikono kwa umakini na juhudi nyingi. Wengine katika kundi hili ni walioachika. Makanisa yenye uwezo yawatafute washauri nasaha watakaosaidiana na wakuu wa huduma za familia katika kuwashauri walioachika maana mara nyingi huwa katika hali ya msongo. Wasiposaidiwa vya kutosha hawa hufikia mahali hawataki tena kuoa wala kuolewa. Watoto wanaolelewa na wazazi wa aina hii wanakosa huduma muhimu ya baba. Hivyo walioachika wenye uwezo wa kuolewa wasikate tamaa wanaweza kuolewa tena.

Kanisa mahalia liwe na siku ya familia ambapo chakula kitaandaliwa kwa wote na zawadi kutolewa kwa makundi hayo maalumu na makundi mengine kanisani.  Kanisa litambue familia zinazofanya vizuri kwa uinjilisti, na zifanye kila liwezekanalo kuwashirikisha katika huduma za kanisani kama kuongoza shule ya sabato na kadhalika. Kila familia iwekewe malengo ya kuongoa na utaratibu wa kutoa taarifa ya uinjilisti nyumbani. Familia zipange ziara za kutembelea maeneo mbalimbali yenye mandhari nzuri ili kubarizi na kujiburudisha. Kila mgeni aliye kwenye familia za Kiadventista afanyiwe kazi na kualikwa kanisani mara kwa mara. Hivyo ndivyo familia za kikristo zitakuwa vituo vya wokovu, mbingu ndogo, na kiwanda cha kutengenezea jamii iliyo bora.

 1. 1.     Kanisa lako (kupitia huduma za familia) lina utaratibu gani wa kuyatambua makundi mbalimbali katika familia na kuyafanyia sherehe?
 2. 2.     Kanisa lako lina utaratibu gani wa kupunguza shida ziwapatazo watoto walio kwenye jamii yenu kwa kuanzisha vituo vya kulelea yatima, albino, na makundi mengine yenye mahitaji maalumu?
 3. 3.     Kanisa lako linawatumia nani kutoa ushauri nasaha kwa familia zenye magomvi? Je, kuna haja ya kutafuta mtaalamu wa kutoa ushauri kwa hatua mliyofikia?