Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

FUNDISHO LA WOKOVU

FUNDISHO LA WOKOVU
Wokovu ni mada kuu inayojadiliwa kwa kirefu katika Maandiko Matakatifu, hasa katika Agano Jipya. Mwandishi mashuhuri kwa mada hii ni mtume Paulo. Hata hivyo mada hii ipo katika kila kitabu cha Biblia kati ya vitabu vyake 66 vinavyotambulika rasmi. Wokovu ni nomino inayotokana na kitenzi cha okoa. Kuokoa ni kuondosha kwenye hatari. Au kuweka kwenye mazingira yasiyotishiwa na hatari iliyokuwepo.

Wokovu ni hatua ya Mungu katika kukabili dhambi na matokeo yake. Dhambi ilipoingia ilimwingiza mwanadamu katika matatizo makubwa. Alitengwa na Mungu na akawa mtumwa wa dhambi. Tena alikabiliwa na adhabu ya kifo na kupoteza urithi na hadhi aliyokuwa nayo. Tangu wakati huo Mungu ameendelea kumtafuta mwanadamu kwa lengo la kumrudisha kwenye hali yake ya mwanzo.

Mungu alitambua hali ya kuasi ya mwanadamu kabla haijatokea. Akaweka mpango unaojulikana kama mpango wa wokovu. Mpango huu uliwekwa kabla ya ulimwengu kuweko. (Uf. 13:8) mpango huu ulifafanua namna Mungu atakavyoshughulikia matatizo yaliyoletwa na dhambi na hatimaye kumrejeshea mwanadamu hali yake ya mwanzo kabla ya dhambi. Kusudi la kitabu hiki ni kufafanua mpango huu kwa kina.

Fundisho la wokovu limekawia kupata nafasi inayolistahili katika kanisa la Mungu hadi hivi karibuni. Mwaka 1888 wainjilisti wawili maarufu A. T. Jones na E. J. Wagonner waliwasilisha fundisho hili na kusababisha taharuki kubwa. Fundisho hilo waliloliita kuhesabiwa haki kwa imani lilionekana kama linalolenga kudhoofisha dhana ya umuhimu wa sheria katika mango wa wokovu. Fundisho hilo halikupokelewa hadi baadaye sana. Sasa hivi fundisho la wokovu – linalofafanua jinsi tunavyohesabiwa haki, lipo katika misingi ya imani ya kanisa la Waadventista wa Sabato.

Fundisho la wokovu, moja ya mafundisho sita makuu ya Waadventista wa Sabato, linabeba msingi wa nane unahusu pambano kuu, msingi wa tisa unaohusu maisha, mauti, na ufufuo wa Kristo, msingi wa kumi unaohusu uzoefu wa wokovu, na msingi wa kumi na moja unaohusu kukua katika Kristo. Tutaifafanua kwa kina, misingi hiyo inayojadili fundisho la wokovu katika makala haya.
Utambuzi huu wa fundisho la wokovu kwa kanisa, unatokana na maagizo na matamko mbalimbali ya Biblia na vitabu vya Roho ya Unabii vinavyoonesha umuhimu wa fundisho hili kufundishwa na kueleweka katika wakati huu. Kanisa limeitwa kupeleka ujumbe huu kwa uliwengu katika wakati huu kama tusomavyo katika ujumbe wa malaika yule wa kwanza. “Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji”. (Ufunuo 14:6)

Injili ya milele ni sehemu ya yale yanayopatikana katika fundisho la wokovu. Injili inafungamanishwa kabisa na utangazaji wa ujumbe wa onyo kwa wanadamu waliovunja sheria za Mungu. Injili hutangaza habari njema kuwa Mungu ametafuta suluhisho la dhambi na kwa hiyo mwanadamu hana sababu ya kuifanyia ukarabati sheria ya Mungu ambayo kazi yake kuu ni kutambulisha dhambi. Injili hutangaza kuwa mwanadamu hana sababu ya kuendelea kumwogopa Mungu maana uadui uliokuwepo Yesu ameuondoa kwa kifo chake pale msalabani.

Neno kuu katika fundisho la wokovu ni Yesu. Yesu anakuwa kiini cha fundisho kwa sababu yeye ndiye anayetegua kitendawili cha dhambi kilichokuwa kikiwakabili wanadamu. Habari hii njema ilianza kusherehekewa mapema sana wakati taarifa zilipoenea kwamba amezaliwa. “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote;  maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” (Luka 2:10)

Huyu ndiye aliyeahidiwa kwamba angekuja kuweka uadui baina yetu na shetani na kumuondolea shetani mamlaka juu yetu. “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (Mwanzo 3:15). Nabii Isaya alitabiri kuja kwake akimuweka katika sura ya kubeba uwezo mwingi wa kila namna. “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” (Isaya 9:6)

Yesu ndiye kamanda wa wokovu maana hata jina lake linahusiana na wokovu. “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” (Mathayo 1:21). Akitangaza sera zake na kazi iliyomleta hapa duniani, mwinjilisti Luka anasema. “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.” (Luka 19:10). Yeye mwenyewe alipokuwa akianza huduma yake alitangaza lengo la kuja kwake. “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” (Luka 4:18-19).

Fundisho la wokovu linapofafanua namna tunavyohesabiwa haki huzua simtofahamu ambayo haikupaswa kuwako. Wengine katika kufundisha dhana hii wameenda mbali na kufanya idhaniwe kuwa kuhesabiwa haki kwa imani kunahafifisha sheria ya Mungu na kunaalika watu waendelee kuishi kwenye dhambi. Paulo Mtume anakanusha dhana hiyo. “Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.” (Warumi 3:31) Kiukweli fundisho la kuhesabiwa haki kwa imani linaimarisha umuhimu wa sheria na nafasi yake katika wokovu. Paulo anainawirisha hoja hiyo kwa kutetea kuwa lengo la fundisho la wokovu ni watu wakome kutenda dhambi. “Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (Warumi 6:2)

Sheria ya Mungu ina nafasi gani katika mpango wa wokovu? Kama sote tujuavyo sheria huwekwa ili kuratibu mambo. Na hii ni kwa sababu bila sheria watu huweza kujifanyia watakavyo jambo linaloweza kuingilia uhuru wa wengine na kusababisha machafuko. Mungu aliweka sheria ili kuratibu shughuli za wanadamu, malaika, na viumbe wengine aliowaumba. Mungu mwenyewe hutawaliwa na sheria pia. “Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.” (1 Wakorintho 14:33) Mwanadamu aliyeishi kabla ya dhambi aliweza kuishi katika utii mkamilifu wa sheria. Baada ya anguko la dhambi mwanadamu alipoteza uwezo huo. Alianza kuziasi sheria na hivyo akaitwa mdhambi. “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.” (1 Yohana 3:4)

Sheria ya Mungu inawakilisha tabia yake. Tabia yake ya utakatifu na tabia yake ya upendo. Hata hivyo tabia inayochomoza zaidi kupitia sheria yake ni ile ya upendo. “Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.” (Warumi 13:10).

Mwanadamu aliyeanguka dhambini hakuweza kustahimili kuiangalia sheria hiyo ya upendo kwa sababu inakinzana na tabia yake ya choyo na ubinafsi. Ile sheria ambayo kwa asili ni njema kwake ilionekana ni mbaya. “Lakini twajua ya kuwa sheria ni njema, kama mtu akiitumia kwa njia iliyo halali.” (1 Timotheo 1:8). “Lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.” (Warumi 7:23).

Mtume Paulo anachosema hapa ni kuwa dhambi ilipandikiza sheria nyingine akilini anayoiita ya dhambi, ambayo kwa kawaida haipatani na sheria ya Mungu. Paulo anahitimisha kwa kutoa sababu kwa nini mwanadamu mwenye dhambi hawezi kutii sheria. “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.” (Warumi 8:7) 
Kutokana na ukweli huo, sheria iliyokuwa iwe kielelezo cha tabia ya Mungu na mwongozo katika jitihada za kurekebisha tabia ikaongezewa jukumu jingine la kuwa chombo muhimu cha kutambulisha kuwepo kwa dhaambi. “Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” (Warumi 3:20)

Mwanadamu mwenye asili ya dhambi ana kawaida ya kukana makosa. Anakana makosa kwanza kwa sababu hajui kama amekosea. Dhambi inakuwa imempotezea uwezo wa kupambanua baya na jema. Anakuwa kipofu wa kiroho. Anaizoea dhambi kiasi cha kutoona ubaya wake. Lakini sababu ya pili ya kukana makosa ni hofu ya adhabu. Kukubali kuwa amekosea kunaonekana kwake kama kitendo cha kujifanyia ukatili kwa kuwa kukiri huko kunaweza kutumika kama ushahidi wa kuhalalisha adhabu yake. Kwa kuwa ni muhimu mwanadamu atambue kuwa amekosa ili arekebishwe na kupewa tiba, Mungu ameweka kitu cha kumsaidia kujitambua kuwa mkosaji na kitu hicho ni sheria yake. Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani”. (Warumi 7:7).

Nafasi ya sheria katika mpango wa wokovu ni kutambulisha dhambi ili mkosaji aone haja ya kumwendea Kristo. “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.” (Wagalatia 3:24). Sheria inachukua jukumu hili kwa kuwa haijapewa uwezo wa kuokoa. Uwezo wake unaishia katika kutambulisha dhambi basi. Jambo hilo la kutambulisha dhambi linafanyika ndani ya dhamiri yake hata kama huyo mtu alikuwa hajakutana na andiko la sheria ya Mungu. “Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea.” (Warumi 2:14)

Sheria isingekuwepo kazi ya Kristo ya kuwakomboa wadhambi isingefanikiwa. Hakuna ambaye angekubali kuwa ni mdhambi maana pasingekuwepo na kipimo cha kumtambulisha mwenye dhambi. Lakini kwa kuwepo sheria ya Mungu utata huo umetoweka. Sasa wanadamu wote wanatambulika kuwa ni wadhambi maana sheria imewahukumu. “Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” (Warumi 3:23). Utukufu huo uliopungua ni ile tabia ya Mungu ya Haki na Upendo vinavyowakilishwa katika sheria yake.

Kwa kawaida sheria haina mahusiano mema na mdhambi. Mahusiano yao ni kama ya daktari anayetoa majibu ya vipimo vya UKIMWI na mwathirika. Au ya dereva mwenye makosa na askari wa barabarani. Ili kujipunguzia udhia unaotokana na sheria mwanadamu hujaribu kupindisha sheria ili isifanye kazi yake iliyokusudiwa. Hili ndilo Pambano Kuu lililoanza kule mbinguni na amablo linaendelea hapa duniani. Mwasisi wa pambano hilo ni malaika aliyeitwa Lusifa. Jina hilo alipewa likimaanisha nuru ya asubuhi kutokana na majaliwa mengi aliyokirimiwa na Mungu. Malaika huyu hakuridhika kutawaliwa na sheria ya Mungu. Hivyo kwa kuwa alikuwa kiongozi wa malaika, akawagomesha malaika wenzake waiasi sheria ya Mungu. Alidhamiria kuupindua utawala wote wa Mungu. “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake.” (Ufunuo 12:7)

Njama za kuipindua serikali ya Mungu ziliposhindwa, malaika huyo ambaye sasa jina lake lilibadilishwa na kuitwa shetani alishuka duniani na kuwadanganya wazazi wetu wamwasi Mungu. “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” (Ufunuo 12:9). Mungu alifanya jitihada za kutosha kuwaaminisha wanadamu wale kuwa sheria zake ni njema na wanapaswa kuzitii kwa hiari maana zipo kwa faida yao, lakini hiyo haikusaidia. Waliziasi wakafukuzwa kutoka bustani nzuri ya Edeni walikokuwa wakiishi. Mtume Paulo amerudia kauli hiyo ya Mungu alipozitetea kuwa ni njema. “Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema.” (Warumi 7:12).

Sheria za Mungu zinafafanua namna ya kuhusiana na binadamu wenzetu na namna ya kuhusiana na Mungu wetu. Ni sheria za mahusiano. Mungu wetu anapendezwa na mahusiano. “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” (Zaburi 133:1). Mungu na sisi ni ndugu. Tuliumbwa kwa mfano wake. “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu. . .” Mwanzo 1:26. Baada ya kuiumba dunia kwa siku sita, siku ya saba Mungu aliitenga kuwa siku ya kuimarisha mahusiano kati yake na wanadamu. “Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.” (Mwanzo 2:2-3)

Baadaye Mungu akauweka utratibu huu katika muundo wa agizo na kuwa mojawapo ya Amri zake Kumi zinazowahusu wanadamu wa vizazi vyote. “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:8-11)

Kama wanadamu wangetii angalau agizo hili na kudumisha mahusiano maalumu ambayo alipanga yafanyike kila inapofika siku ya saba ya juma wanadamu wangekuwa wamepata pumziko muhimu la kiroho ambalo lingewasogeza karibu zaidi kwa Kristo. Uadui wao juu ya sheria za Mungu ungethibitiwa na utunzaji wa sheria ungeonekana kitu chepesi. Siku hii ya Sabato Yesu huitumia kuwapa watu pumziko kama lile walipatalo wanapokwenda kwake kwa msamaha wa dhambi. “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.”   (Ezekieli 20:12).

Lakini kutokana na sheria kuonekana kuwazuia watu kufanya wapendavyo na kutokana na wanadamu kutaka kujihesabia haki wenyewe, sheria za Mungu zimepigwa vita, zimevunjwa, zimenyofolewa na kubadilishwa. Hali hii ilitabiriwa tangu zamani sana. “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” (Danieli 7:25).

Sheria iliyobadilishwa ni ya nne inayohusu siku ya kuabudu naye   aliyeibadilisha ametajwa tena na mtume Paulo. “Yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” (2 Wathesalonike 2:4). Sheria hiyo ilibadilishwa na wanadamu bila kibali cha Mungu.
Ibada iliyokuwa ifanyike siku ya saba yaani Jumamosi ikahamishiwa siku ya kwanza ya juma yaani Jumapili siku ambayo Mungu hakuagiza. Badiliko hili lilifuatiwa na jaribio linguine lililofanikiwa la kuiondosha kabisa amri ya pili inayozuia kuabudu sanamu. Kuondolewa kwa amri hiyo kulipunguza idadi ya amri kutoka kumi hadi tisa jambo lililolazimu kuigawa amri ya kumi vipande viwili ili kutimiza idadi ya amri kumi. Badiliko hili pia lilifanywa na wanadamu bila kibali cha Mungu. Zile amri za Mungu zilizotolewa mlima Sinai bado zingali vilevile na ukitaka kujiridhisha angalia Kutoka 20:1-17.

Wanadamu waliofanya hivyo ama waliongozwa na hofu ya adhabu hivyo wakapunguza idadi ya amri ama walisukumwa na kiu ya kutaka kumsahihisha Mungu na kuupindua utawala wake kama shetani alivyojaribu kufanya kule mbinguni. Jitihada hizo zote zilikuwa zinadhaminiwa na Shetani mwenyewe ambaye katika zama za giza 538 BK hadi 1798 BK alisimamia uteswaji wa watetezi wa Neno la Mungu wakipinga mabadiliko yaliyokuwa yanaingizwa kanisani kinyume na Maandiko Matakatifu. “Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili. Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni.Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.” (Ufunuo 13:4-7)

Leo hii, kawaida ya kufanya ibada siku ya kwanza ya juma, iliyoanzishwa na mwanadamu kwa usimamizi wa shetani, imepokelewa na kuheshimiwa na kila kabila na jamaa na lugha na taifa, kama fungu lisemavyo hapo juu. Shetani anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa duniani akishindana na Mungu. Pamoja na ukweli kuwa sheria haiokoi bado ina nafasi yake muhimu katika wokovu wa mwanadamu. Ni muhimu wanadamu wote wapewe fursa ya kujua kile Mungu alichowaandikia katika sheria ya mwanzo iliyotoka mikononi mwake. Sheria ya awali haina mabadiliko hayo yaliyofanywa na wanadamu. Wakati huu Mungu anawaita watu wa kila kabila na jamaa na lugha na taifa, kumrudia yeye aliyeziumba mbingu na nchi kwa sababu kutii sheria zilizowekwa na wanadamu ni kuwafanya walioziweka kuwa Miungu. “Akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.” (Ufunuo 14:7)

Wale wote wanaompenda Mungu hawatajaribu kufuata au kufundisha sheria zilizopotoshwa na wanadamu. Yesu anawaonya akisema; “Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” (Mathayo 5:19). Juu ya wale wanaozitunza na kuzifundisha sheria zile za awali zilizotolewa mlima Sinai, Yesu anawaita rafiki zake; “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.” (Yohana 15:14). Unaalikwa kuwa rafiki wa Yesu. Unaalikwa kuwa mtu mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Je, utakuwa tayari kupokea mwaliko huu. Mungu akubariki unapojikabidhi kwake.

Mungu anatambua changamoto ya dhambi na ameweka sheria na Neno lake viwe nyenzo za kumsogeza mwanadamu kwa Kristo. Sheria inatuongoza kwa Kristo pale inapotutia hatiani. Hali ya kuwa hatiani humfanya mtu kukosa amani. Amani ikikosekana mtu hutafuta namna ya kujinasua. Shetani huleta ushauri wa kukanusha ile hatia jambo ambalo mara nyingi halileti matokeo yaliyotarajiwa. Kukanusha kunaposhindikana mwenye hatia husukumia kosa kwa wengine au husingizia mazingira ya tukio. Hali hii ya kutapatapa huishia katika hali isiyo na mafanikio yoyote. “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” (Mithali 28:13).

Mungu ameweka hali ile ya kujisikia hatia ili kumhimiza mdhambi atubu. Hali hiyo inakuwepo pia mjumbe wa Mungu anapotoa maonyo juu ya dhambi za wasikilizaji wake. Mtume Petro katika hotuba yake ya siku ya Pentekoste alitoa ujumbe nzito uliwatia hatiani wasikilizaji wake pale alipowathibitishia kuwa walihusika na kifo cha Yesu. Katika hali ya kuhangaika kutokana na hatia wakataka kujua wachukue hatua gani. “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu (Matendo 2:37-38)

Ujumbe mkali unatolewa pale mwanadamu anapokuwa na ukiziwi wa kiroho. Mtu anapojifariji katika dhambi na kukataa kusikia maonyo, Mungu hutuma mjumbe mkali kwake. “Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.” (Mithali 17:11). Ndiyo maana katika ujumbe wa malaika yule wa tatu wa kitabu cha Ufunuo kwa watu wote, Mungu anatoa maonyo makali sana kwa watakaodharau ujumbe wa malaika wa kwanza na wa pili. “Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.” (Ufunuo 14:9-10)

Tusijijengee utamaduni wa kuchukia wahubiri, au Neno la Mungu au Sheria yake. Hivyo havina madhara kwa anayeishi kulingana navyo. Ikiwa umetofautiana navyo dawa si kupambana na kushupaza shingo, dawa ni kunyenyekea. “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.” (Mithali 29:1) Njia salama ya kujiepusha na hatia moyoni ni kufanya vile Mungu alivyoagiza bila kupunguza wala kuongeza na kuungama mara moja unapotenda dhambi. “Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.” (Mithali 30:6). “Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.” (Warumi 4:7-8)