Seventh-day Adventist® Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

USOMAJI BIBLIA

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 4:1-24 (15/05/2019)
Ndoa ya Samsoni

1 Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya Bwana. 2 Bwana akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake. 3 Wana wa Israeli wakamlilia Bwana; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini. 
4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. 5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue. 6 Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni? 7 Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako. 8 Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. 9 Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi. 10 Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye. 11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saanaimu, karibu na Kedeshi. 
12 Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori. 13 Sisera akayakusanya magari yake yote, naam, magari ya chuma mia kenda, na watu wote waliokuwa pamoja naye, toka Haroshethi wa Mataifa mpaka mto wa Kishoni. 14 Debora akamwambia Baraka, Haya! Inuka; maana siku hii ndiyo siku ambayo Bwana amemtia Sisera katika mkono wako. Je! Bwana hakutoka atangulie mbele yako? Basi Baraka akashuka katika mlima wa Tabori, na watu elfu kumi wakamfuata. 15 Bwana akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa makali ya upanga, mbele ya Baraka; basi Sisera akashuka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. 16 Lakini Baraka akayafuatia magari, na jeshi, hata Haroshethi wa Mataifa; na hilo jeshi lote la Sisera likaanguka kwa makali ya upanga; hakusalia hata mtu mmoja.
17 Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni.
18 Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti. 19 Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika. 20 Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana. 21 Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa. 22 Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake. 23 Basi hivyo Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani mbele ya wana wa Israeli siku hiyo. 24 Mkono wa wana wa Israeli ukazidi kupata nguvu juu ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hata walipokuwa wamemwangamiza Yabini, mfalme wa Kanaani.

MASWALI YA KUJADLI:
1. Unadhani Baraka alikuwa na sababu nzuri ya kusita kwenda kulikabili jeshi kubwa lenye zana nyingi na bora za kivita la Sisera hata kama ni Mungu amemwagiza kufanya hivyo?
2. Kwa nini kuwepo kwa Debora mwamuzi na nabii mke kulileta faraja kwa Baraka vitani? Upo wakati mwanamke anayetambulika kuwa mnyonge au dhaifu katika jamii nyingi anaweza kuwa msaada kwa wanaume kutimiza majukumu yao waliyopewa na Mungu?
3. Kwa nini katika kisa hiki Mungu alileta ushindi kwa msaada wa wanawake zaidi kuliko wanaume? Jambo hili lilitokea kwa bahati mbaya au kuna jambo Mungu anataka kutufundisha?
4. Kwa nini Sisera pamoja na kuwa na jeshi kubwa na zana bora za kivita alishindwa vitani? Hii inatufundisha nini juu ya umuhimu wa kumtegemea Mungu?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 5:1-31   (16/05/2019)
Wimbo wa Debora

1 Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema;
2 Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini Bwana.
3 Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia Bwana; Nitamhimidi Bwana, Mungu wa Israeli.
4 Bwana, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji.
5 Milima ikayeyuka mbele za uso wa Bwana, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa Bwana, Mungu wa Israeli.
6 Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nao wenye kusafiri walipita kwa njia za kando.
7 Maliwali walikoma katika Israeli, walikoma, Hata mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli.
8 Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arobaini wa Israeli?
9 Moyo wangu unawaelekea maliwali wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini Bwana.
10 Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu.
11 Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya Bwana; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa Bwana waliposhuka malangoni.
12 Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu.
13 Ndipo walitelemka mabaki ya waungwana na ya watu; Bwana alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa.
14 Kutoka Efraimu walitelemka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka maliwali, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi.
15 Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
16 Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
17 Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake.
18 Zabuloni ndio watu waliohatirisha roho zao hata kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni.
19 Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yo yote ya fedha.
20 Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera.
21 Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu.
22 Ndipo kwato za farasi zilikanyaga-kanyaga Kwa sababu ya kupara-para, Kupara-para kwao wenye nguvu.
23 Ulaanini Merozi, alisema malaika wa Bwana, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia Bwana, Kumsaidia Bwana juu ya hao wenye nguvu.
24 Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.
25 Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima.
26 Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.
27 Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.
28 Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia?
29 Mabibi yake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa nafsi yake jawabu.
30 Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbali mbali, Nyara za mavazi ya rangi mbali mbali ya darizi; Ya rangi mbali mbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka.
31 Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee Bwana.

MASWALI YA KUJADILI:
1. Kuimba nyimbo ni njia mojawapo ya kutambua na kushukuru jinsi Mungu alivyokutendea makuu siku zilizopita ulipokuwa ukikabiliwa na changamoto. Je unakuwa na mazoea ya kuimba nyimbo za sifa kwa furaha?
2. Debora na Baraka wanakiri kuwa ushindi wao umechangiwa kujitoa mhanga kwa hiari kwa viongozi wao. Je unatambua mchango wa viongozi wako katika kufikia mafanikio yako binafsi na mafanikio ya kundi lako la kiroho? Je kungekuwa na mabadiliko gani kama tungedumisha kawaida ya kutambua mchango wa wale waliochangia mafanikio yetu?
3. Kutia hamasa watu unaowaongoza katika kipindi cha kukata tamaa na woga kunasaidiaje kuamsha tumaini la ushindi? Kama kiongozi anaonesha woga kuna hatari gani kwa anaowaongoza?
4. Je wanawake wana mchango wowote katika vita ya kiroho na kiuchumi? Je wanafaa kuwa viongozi na kuleta mabadiliko yoyote ya maana?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 6:1-40    (17/05/2019)
Ukandamizaji wa Wamidiani

1 Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba 2 Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. 3 Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; 4 wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. 5 Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. 6 Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
 7 Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Midiani, 8 Bwana akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, Bwana, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; 9 nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao; 10 kisha niliwaambia, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu.

Gideoni aitwa na Mungu

11 Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. 12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? 15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. 16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. 17 Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. 18 Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi. 19 Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. 20 Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. 21 Ndipo malaika wa Bwana akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa Bwana akaondoka mbele ya macho yake.
 22 Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso. 23 Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. 24 Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.
 25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. 

Gideoni abomoa madhabahu ya Baali

27 Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. 29 Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. 30 Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. 31 Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake. 32 Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake. 33 Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. 34 Lakini roho ya Bwana ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata. 35 Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki.

Ishara ya ngozi ya kondoo

36 Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema, 37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema. 38 Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji. 39 Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote. 40 Mungu akafanya hivyo usiku ule; maana ile ngozi tu ilikuwa kavu, napo palikuwa na umande juu ya nchi yote.

MASWALI YA KUJADILI:

 1. Je mkakati wa kuidhoofisha Israeli kwa njaa ulifanikiwa? Kwa nini Israeli hawakujitetea wakati uvamizi huo ulipokuwa ukifanyika? Kwa nini Mungu hakuingilia kati kuwatetea Israeli wakati uonevu huu ulipokuwa unaendelea?
 2. Je Mungu anahitaji ushirika wa wanadamu ili kuleta ukombozi wa kifikra na kiroho? Kwa nini Gideon pekee ndiye aliyechukua muda kutafakari uonevu wanaotendewa? Je wengine walikuwa wameridhika? Kuna haja ya kujitoa mhanga kutetea jambo linalowahusu wengi wakati wahusika wenyewe hawaoneshi kukuunga mkono?
 3. Ilikuwa ni muhimu kwa Gidioni kutaka ishara kutoka kwa Mungu?
 4. Je kuharibu miungu ya kipagani kulikofanywa na Gidioni kulikuwa kwa halali na kwa muhimu? Je ilikuwa halali kwa watu kumtetea Baali aliyeshindwa kujitetea mwenyewe asibomolewe?
 5. Je panahitajika watu majasiri kama Gidioni leo hii?
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 7:1-25   (18/05/2019)
Gideoni awashinda Wamidiani

1 Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. 
2 Bwana akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. 3 Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. 
4 Bwana akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. 5 Basi akawaleta watu chini majini. Bwana akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. 6 Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. 7 Bwana akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. 8 Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.

9 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. 10 Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; 11 nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini. 12 Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. 13 Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. 14 Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. 15 Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu. 16 Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi. 17 Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika. 18 Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa Bwana, na kwa Gideoni.

19 Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. 20 Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa Bwana na wa Gideoni. 21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza. 22 Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye Bwana akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi. 23 Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani. 24 Kisha Gideoni akapeleka wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, telemkeni juu ya Midiani, na kuyashika hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. Basi watu waume wote wa Efraimu walikutana pamoja, wakayashika maji mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. 25 Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng'ambo ya pili ya Yordani.

MASWALI YA KUJADILI:

 1. Kumwacha Mungu kunakaribisha matatizo mengi maishani kama ilivyotokea kwa Israeli. Unadhani matatizo unayoyapitia yametokana na kumwacha Mungu.
 2. Ufumbuzi wa matatizo huja pale mtu anapotathmini maendeleo yake na kubaini mapungufu. Je unaridhika na maendeleo yako? Unadhani kuna ahadi unazoweza kuzidai kwa Mungu ili kuondokana na mkwamo huo?
 3. Sifa za mtu afaaye kutumika na Mungu kuongoza mapambano ya kujikomboa kwenye utumwa wa dhambi na utumwa mwingine wowote ni kujiona kutotosha kama Gideoni. Je, unadhani sifa hiyo bado inahitajika leo? Faida ya kuwa na sifa hiyo ni nini?
 4. Uhakika wa ushindi katika vita ya kiroho hautokani na uwingi wa wapiganaji au uwingi wa silaha na ubora wake. Ni nini kilichosababisha ushindi wa jeshi la Gideoni?
 5. Kwa nini Mungu anakubali kuwapigania watu waliokuwa wamechagua kumuasi? Mungu anapata faida gani kwa kufanya hivyo?
 6. Unadhani vijana wana nafasi ye yote katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jumuia za kidini na kwenye jamii zetu leo hii. Je wanaaminika?
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 8:1-35    (19/05/2019)
Gideoni ashinda na kulipiza kisasi

1 Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini wewe kututendea sisi kama haya? Hata usituite, hapo ulipokwenda kupigana na Midiani? Nao wakateta naye sana. 2 Lakini akawaambia, Je! Mimi nimefanya nini sasa kama mlivyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri? 3 Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo. 4 Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamepungukiwa na nguvu, lakini wawafuatia vivyo. 5 Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wanapungukiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani. 6 Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate? 7 Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo Bwana atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura nyama ya miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma. 8 Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu. 9 Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitauvunja mnara huu.

10 Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama kumi na tano elfu hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka watu mia na ishirini elfu waliokuwa wenye kutumia upanga. 11 Basi Gideoni alikwea kwa njia ya hao waliokuwa wenye kukaa hemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha, akalipiga hilo jeshi; kwa maana lile jeshi lilikuwa salama. 12 Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanya-tapanya hilo jeshi lote. 13 Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi. 14 Ndipo akamshika mtu mmoja hirimu katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba. 15 Kisha akawafikilia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate? 16 Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo. 17 Kisha akaupomosha mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo. 18 Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme. 19 Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye Bwana alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi. 20 Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu. 21 Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao.

Gideoni aabudu sanamu

22 Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani. 23 Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye Bwana atatawala juu yenu. 24 Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.) 25 Wakajibu, Tutakupa kwa mioyo. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu pete za masikio ya mateka yake. 26 Na uzani wa hizo pete za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia zao. 27 Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake. 28 Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni. 29 Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe. 30 Gideoni alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi. 31 Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki. 32 Basi Gideoni mwana wa Yoashi akafa mwenye umri wa uzee mwema, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake, katika Ofra ya Waabiezeri.

33 Kisha ikawa, mara alipokufa Gideoni, wana wa Israeli wakakengeuka tena, wakawaandama Mabaali kwa ukahaba, wakamfanya Baal-berithi kuwa ni mungu wao. 34 Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka Bwana, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote; 35 wala hawakuifanyia mema nyumba ya Yerubaali, yaani Gideoni, kwa kuyafuata hayo mema yote aliyowafanyia Israeli.

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 9:1-57     (20/05/2019) 
Abimeleki awania ufalme  

1 Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake, akanena nao, na wote waliokuwa wa nyumba ya baba ya mama yake, akasema, 2 Haya, neneni tafadhali masikioni mwa waume wote wa Shekemu, mkaulize, Je! Ni lipi lililo jema kwenu, kwamba hao wana wa Yerubaali wote, ambao ni watu sabini, watawale juu yenu, au kwamba mtu mmoja atawale juu yenu? Tena kumbukeni ya kwamba mimi ni mfupa na nyama yenu. 3 Hao ndugu za mama yake wakanena habari zake masikioni mwa hao watu wote wa Shekemu maneno hayo yote; na mioyo yao ikaelekea kumwandama Abimeleki; kwa kuwa walisema, Huyu ni ndugu yetu. 4 Wakampa vipande vya fedha sabini vilivyotoka katika nyumba ya Baal-berithi, na kwa fedha hizo Abimeleki akaajiri watu wapuuzi mabaradhuli, wafuatane naye. 5 Kisha akaenda nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini, akawaua juu ya jiwe moja; lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubaali, alisalia; kwa maana alijificha. 6 Kisha hao watu wote wa Shekemu wakakusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu.

Mithali ya miti
7 Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate kuwasikia ninyi. 8 Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. 9 Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? 10 Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. 11 Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? 12 Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. 13 Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? 14 Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu. 15 Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni. 16 Basi sasa ikiwa mmetenda kwa uaminifu na uelekevu, katika kumtawaza Abimeleki awe mfalme, na ikiwa mmemtendea mema Yerubaali na nyumba yake, na kumtendea kama ilivyostahili mikono yake; 17 (kwa maana baba yangu aliwatetea ninyi, na kuhatirisha uhai wake, na kuwaokoa na mikono ya Midiani; 18 nanyi mmeinuka juu ya nyumba ya baba yangu hivi leo nanyi mmewaua wanawe, watu sabini, juu ya jiwe moja, nanyi mmemtawaza Abimeleki, mwana wa kijakazi chake, awe mfalme juu ya watu wa Shekemu kwa sababu yeye ni ndugu yenu;) 19 basi ikiwa mmemtendea kwa uaminifu na uelekevu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi furahini ninyi katika huyo Abimeleki, yeye naye na afurahi kwenu ninyi; 20 lakini kwamba sivyo hivyo, basi, moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki. 21 Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye.

Kuanguka kwa Abimaleki
22 Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu. 23 Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu; 24 ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze. 25 Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang'anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa.
26 Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye. 27 Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki. 28 Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani? 29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje. 30 Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka. 31 Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako. 32 Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani; 33 kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi.
34 Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne. 35 Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia. 36 Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu. 37 Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu. 38 Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao. 39 Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki. 40 Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango. 41 Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu. 42 Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa. 43 Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga. 44 Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga. 45 Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi.
46 Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi. 47 Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja. 48 Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi. 49 Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake.
50 Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa. 51 Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji. 52 Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto. 53 Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. 54 Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. 55 Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. 56 Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini; 57 uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 10:1-18    (21/05/2019)
Tola na Yairi

1 Baada yake Abimeleki, akainuka Tola mwana wa Pua, mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, kuwaokoa Israeli; naye alikuwa akikaa Shamiri, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu. 2 Huyo akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na mitatu, akafa, akazikwa katika Shamiri.
3 Baada yake huyo akainuka Yairi, Mgileadi; naye akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na miwili. 4 Huyo alikuwa na wana thelathini waliokuwa wakipanda wana-punda thelathini, nao walikuwa na miji thelathini, ambayo inaitwa Hawoth-yairi hata hivi leo, nayo iko katika nchi ya Gileadi. 5 Yairi akafa, akazikwa huko Kamoni.

Waamoni wawadhulumu Waisraeli

6 Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha Bwana, wala hawakumtumikia yeye. 7 Hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni. 8 Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng'ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane. 9 Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana. 10 Ndipo wana wa Israeli wakamlilia Bwana, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali. 11 Naye Bwana akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti? 12 Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao. 13 Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena. 14 Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu. 15 Wana wa Israeli wakamwambia Bwana Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu. 16 Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia Bwana; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli.
17 Wakati huo wana wa Amoni walikutana pamoja, wakapanga marago huko Gileadi. Wana wa Israeli nao wakajikusanya wakapanga marago Mispa. 18 Na hao watu, wakuu wa Gileadi, wakaambiana wao kwa wao, Je! Ni mtu yupi atakayeanza kupigana na wana wa Amoni? Yeye atakuwa ni kichwa juu ya wenyeji wote wa Gileadi.

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 11:1-40     (22/05/2019)
Yeftha

1 Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. 2 Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. 3 Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye.
4 Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli. 5 Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; 6 wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. 7 Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu? 8 Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi. 9 Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu? 10 Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye Bwana atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako. 11 Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya Bwana huko Mispa. 
12 Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu? 13 Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata. 14 Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni; 15 akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni; 16 lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi; 17 ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi. 18 Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu. 19 Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu. 20 Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapanga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli. 21 Bwana, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, wenye kukaa nchi hiyo. 22 Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani. 23 Basi sasa yeye Bwana, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki? 24 Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika, awaye yote ambaye Bwana, Mungu wetu, amemfukuza atoke mbele yetu hao ndio tutakaowatamalaki. 25 Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lo lote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao? 26 Wakati Israeli waliokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona ninyi hamkuipata tena katika majira hayo? 27 Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye Bwana, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni. 28 Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea. 
Kiapo cha Yeftha
29 Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni. 30 Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, 31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. 32 Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake. 33 Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli. 

Binti wa Yeftha
34 Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye. 35 Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia Bwana kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma. 36 Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia Bwana kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye Bwana amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni. 37 Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu. 38 Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani. 39 Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume. Kisha ikawa desturi katika Israeli, 40 kwamba binti za Israeli waende mwaka baada ya mwaka ili kumkumbuka huyo mwana wa Yeftha, Mgileadi, siku nne katika mwaka.

MASWALI YA KUJADILI:
1. Moja ya matatizo yanayotokana na kuwa na ndoa za mitala ni magomvi ya waliozaliwa kwenye familia moja. Unadhani Yeftha alistahili kufukuzwa na ndugu zake na kunyimwa urithi?
2. Tabia mbaya za watoto wanaoitwa mitaani zinatokana na kukataliwa na familia zao au na tabia wanazojifunza mtaani? Nini kifanyike kupunguza wimbi la watoto wa mitaani?
3. Je ni busara kuwatumia au kuwathamini watu waliokataliwa na jamii zao pale vipawa vyao vinapohitajika kuokoa familia, kanisa, au jamii?
4. Je, inafaa kukubali kuwatumikia watu waliokukataa kwa dharau hapo mwanzo?
5. Utafanyaje mtu akikutaka urudishe mali yake ambayo Mungu alikuagiza uitwae? Utajisikia hatia na kumrudishia?
6. Ni muhimu kwa kiongozi wa kiroho kujua historia ya taasisi anayoiongoza na jinsi Mungu alivyoivusha katika nyakati ngumu huko nyuma. Unadhani Yeftha alipatia wapi uelewa huu? Hiyo inakuambia nini juu ya umuhimu wa viongozi leo kuijua historia ya kanisa na uwezo wa Mungu wanayemtumikia?
7. Yeftha alitoa ahadi yake kwa kukurupuka lakini akawa mwaminifu kuitimiza. Hii inatufundisha nini kuhusu kutoa ahadi au nadhiri?
8. Binti wa Yeftha alikuwa na tabia njema hata kuliko baba yake wakati alipokuwa mtoto ambaye aliungana na mabaradhuli. Hii inapingana na ukweli kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka? Tufanyeje ili watoto wetu wasirithi tabia zetu mbaya?
9. Ni muhimu kwa kiongozi wa kiroho kujua historia ya taasisi anayoiongoza na jinsi Mungu alivyoivusha katika nyakati ngumu huko nyuma. Unadhani Yeftha alipatia wapi uelewa huu? Hiyo inakuambia nini juu ya umuhimu wa viongozi leo kuijua historia ya kanisa na uwezo wa Mungu wanayemtumikia?
10. Yeftha alitoa ahadi yake kwa kukurupuka lakini akawa mwaminifu kuitimiza. Hii inatufundisha nini kuhusu kutoa ahadi au nadhiri?
11. Binti wa Yeftha alikuwa na tabia njema hata kuliko baba yake wakati alipokuwa mtoto ambaye aliungana na mabaradhuli. Hii inapingana na ukweli kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka? Tufanyeje ili watoto wetu wasirithi tabia zetu mbaya?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 12:1-15     (23/05/2019)
Makabila yazozana

1 Kisha watu wa Efraimu walikutana pamoja na kupita kwenda upande wa kaskazini; wakamwambia Yeftha, Kwa nini wewe kuvuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaipiga moto nyumba yako juu yako. 2 Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na matata makubwa na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao. 3 Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatirisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, Bwana naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami? 4 Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, mnaokaa kati ya Efraimu, na kati ya Manase. 5 Nao Wagileadi wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha ilikuwa, hapo watoro waliotoroka Efraimu mmojawapo aliposema Niache nivuke, hao watu wa Gileadi wakamwambia, Je! Wewe u Mwefraimu? Kwamba alisema, La; 6 ndipo wakamwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka wakati huo watu arobaini na mbili elfu wa Efraimu. 7 Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.
Ibzani, Eloni na Abdoni
8 Baada yake huyo, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli. 9 Alikuwa na wana thelathini; na binti thelathini akawapeleka waende mahali pengine, kisha akaleta wanawake thelathini kutoka mahali pengine kwa ajili ya hao wanawe. Akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka saba. 10 Huyo Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu. 11 Baada yake huyo, Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli akawaamua Israeli muda wa miaka kumi. 12 Huyo Eloni, Mzabuloni, akafa, akazikwa katika Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.
13 Baada yake huyo, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli. 14 Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini, waliokuwa wakipanda wana-punda sabini; akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka minane. 15 Huyo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, akazikwa huko Pirathoni katika nchi ya Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.

MASWALI YA KUJADILI:
1. Unawachukuliaje watu wanaopendelea kulalamika kutoshirikishwa waonapo mafanikio lakini ambao katika kipindi chote cha mapambano walikaa mbali bila kujihusisha?
2. Je mafanikio yaweza kuongeza idadi ya maadui maishani mwako? Ufanye nini ili hali hiyo isitokee?
3. Magomvi ya wanandugu hutokana na ubinafsi na kutafsiri vibaya mienendo ya wengine huku kukiwa na nia ovu ya kutaka kushika uongozi kinyume cha aliyepo madarakani kwa uhalali. Unadhani hali hiyo inajidhihirisha kwenye kisa hiki? Je, hali hiyo ipo kwenye familia au kanisani kwako?
4. Yapo mambo yanayowatofautisha hata ndugu wa jamaa moja na hivyo ni jambo lisilowezekana kufikiria kuwafanya watu wote wafanane maana ni Mungu aliyeruhusu tofauti hizo ziwepo kwa nia ya kuimarishana na kutoshelezana. Katika kisa hiki shetani alitumiaje tofauti za ndugu kwa faida yake?
5. Je tofauti zenu katika familia na katika kanisa zinawafanya mgombane na kuangamizana au zinawaleta pamoja?
6. Unajifunza nini kwa Tanzania yenye makabila mengi yasiyogombana wala kuchukiana ukilinganisha na majirani zetu? Kama hilo limewezekana katika nchi linashindikanaje kwenye familia yenu na kwenye jumuiya yako ya kidini?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 13:1-25    (24/05/2019)
Kuzaliwa kwa Samsoni

1 Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya Bwana, Bwana akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini.
2 Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. 3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. 4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; 5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. 6 Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake; 7 lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake. 8 Ndipo huyo Manoa akamwomba Bwana, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa. 9 Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye. 10 Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile. 11 Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi. 12 Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini? 13 Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari. 14 Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze. 15 Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako. 16 Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea Bwana. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa Bwana. 17 Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza? 18 Huyo malaika wa Bwana akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu? 19 Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea Bwana hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia. 20 Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa Bwana akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi. 21 Lakini malaika wa Bwana hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa Bwana. 22 Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu. 23 Lakini mkewe akamwambia, Kama Bwana angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu.
24 Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. 25 Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.

MASWALI YA KUJADILI:
1. Je, umekata tamaa na taarifa kuwa ugonjwa au hali mbaya uliyo nayo utadumu nayo siku zote? Habari njema ni kuwa Mungu aweza kubadilisha hali yako kama alivyobadilisha utasa wa mke wa Manoa. Je, unaamini hilo?
2. Malezi bora ya mtoto huanzia akiwa tumboni na hutokana pia na vyakula na vinywaji anavyotumia mama na mahusiano ya wazazi. Unadhani tabia mbaya za watoto tunazozishuhudia leo zinatokana na kukosa mambo hayo wakiwa hawajazaliwa?
3. Kwa nini katika kizazi cha leo inaonekana zuio la kunywa vileo na kula wanyama najisi ni kama halitokani na agizo la Mungu? Au ni kwa sababu ya kuelemewa na ulevi na ulafi kama Luka 21:34 isemavyo?
4. Mungu akitaka kuokoa familia au kikundi cha watu humuandaa mtu atakayewaongoza ambaye humwezesha kwa vipawa kadhaa na kumfanya kuwa tofauti na wengine. Unadhani umeandaliwa kuwa nani katika siku za usoni? Je unauthamini mpango huo wa Mungu?
5. Ujenzi wa tabia za watoto hukamilika katika miaka minane ya mwanzo na huendelezwa hata atakapokuwa mtu nzima. Kama mzazi au kiongozi wa kiroho unatumia muda gani kumuomba Mungu akuwezeshe kuwalea watoto wako? Je kwenye kanisa lako kuna utaratibu nzuri wa malezi ya watoto?
6. Unafahamu mwanao atakuwa nani katika siku za usoni? Umefanya sehemu gani kumwezesha kuwa vile anavyotaka au vile Mungu alivyompangia kuwa? Unazungumziaje wazazi wanaolazimisha watoto wao kuwa vile wanavyotaka wao?
7. Manoa na mkewe walikuwa watu wa kiroho kwa kuwa walikuwa wakitimiza taratibu za ibada za wakati huo na Mungu akaruhusu Samsoni - Mwamuzi mashuhuri wa Israeli kuzaliwa kwao. Hali ya ibada nyumbani kwako ikoje?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
Waamuzi 14:1-20    (25/05/2019)
Ndoa ya Samsoni

1 Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti. 2 Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe. 3 Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana. 4 Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la Bwana; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli. 5 Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. 6 Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya. 7 Basi akatelemka na kuzungumza na huyo mwanamke; naye akampendeza Samsoni sana. 8 Kisha baadaye akarudi ili kumtwaa, naye akageuka kando kuuangalia mzoga wa huyo simba; na tazama, nyuki wengi walikuwamo ndani ya mzoga wa simba, na asali. 9 Akatwaa asali mikononi mwake akaenda mbele, huku akila alipokuwa akienenda, akawafikilia babaye na mamaye, akawapa, nao wakala; lakini hakuwaambia ya kuwa ameitwaa hiyo asali katika mzoga wa simba. 10 Basi babaye akamtelemkia huyo mwanamke; Samsoni naye akafanya karamu huko; kwa kuwa vijana ndivyo walivyokuwa wakifanya. 11 Basi ikawa hapo walipomwona, wakamletea wenziwe thelathini, wawe pamoja naye. 12 Samsoni akawaambia, Mimi nitawategea ninyi kitendawili; kama mwaweza kunionyesha katika hizo siku saba za karamu, na kukitambua, ndipo hapo nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini; 13 lakini msipoweza kunionyesha ndipo hapo ninyi mtanipa mimi mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini. Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia. 14 Naye akawaambia, Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula, Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu. 15 Ikawa kwa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, Mbembeleze mumeo, ili atuonyeshe hicho kitendawili, tusije tukakuteketeza moto wewe na nyumba ya baba yako; je! Mmetuita ili mpate kuichukua mali yetu? Je! Sivyo? 16 Basi mkewe Samsoni akalia mbele yake, akasema, Wewe wanichukia tu, wala hunipendi; wewe umewategea kitendawili hao wana wa watu wangu, nawe hukuniambia mimi. Naye akamwambia, Angalia, sikumwambia baba yangu wala mama yangu, nami nikuambie wewe? 17 Naye akalia mbele yake hizo siku saba, wakati ulioendelea karamu yao; basi ikawa siku ya saba akamwambia, kwa sababu alikuwa akimsisitiza sana; naye akawaambia wale wana wa watu wake hicho kitendawili. 18 Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali? Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba? Naye akawaambia, kwamba hamkulima na mtamba wangu,Hamngekitambua kitendawili changu. 19 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake. 20 Lakini huyo mke wa Samsoni aliozwa mwenzake, ambaye alikuwa amemtendea kama rafikiye.

MASWALI YA KUJADILI:
1. Kuchagua mwenzi wa maisha kunahitaji umakini na muda wa kutosha wa kumchunguza. Unadhani uchaguzi wa Samsoni ulizingatia vigezo hivyo?
2. Katika nyakati hizo kulikuwa na faida gani ya kuoa mke kutoka katika jamaa ya karibu? Je sababu hizo zina mashiko kwa leo?
3. Wazazi wana nafasi gani katika kupendekeza mke au mume anayefaa kwa watoto wao katika siku tunazoishi? Ni kweli kuwa jambo hili halihitaji ushauri wa wazazi?
4. Unadhani Samsoni alipendezwa na nini kwa yule binti wa Wafilisti ambao ni maadui wa taifa lake? Je katika kuoa au kuolewa swala la kupendezwa au kuvutiwa na yule unayetaka kuoana naye ni la muhimu?
5. Je unadhani Samsoni alikuwa amefikia hatua ya kuoa au alikuwa bado ana mambo ya ujana yakimsumbua? Dalili ya kijana aliyefikia umri unaostahili kuoa au kuolewa ni zipi?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 15:1-20    (26/05/2019)
Samsoni awashinda Wafilisti

1 Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia. 2 Baba yake akasema, Hakika mimi nalidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nalimpa rafiki yako. Je! Ndugu yake mdogo mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake. 3 Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. 4 Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili. 5 Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni. 6 Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto. 7 Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika nitajilipiza kisasi juu yenu, na baadaye nitakoma. 8 Akawapiga upeo, mapigo makuu sana, kisha akatelemka akakaa katika ufa wa jabali la Etamu.
9 Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi. 10 Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. 11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao. 12 Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia. 13 Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini.
14 Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. 15 Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo;
16 Samsoni akasema, 
         Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, 
         Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.
17 Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi. 18 Kisha akaona kiu sana, akamwita Bwana akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa. 19 Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo. 20 Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.

MASWALI YA KUJADILI:

1. Je, ubabe usioandamana na uadilifu unafaa katika kuwakomboa watu na ukandamizaji wa maadui. Vitendo vya Samsoni vinaashiria kuwa ni mtu aliyetumwa na Mungu?
2. Katika kufanya kazi ya kuwatumikia watu kuna uwezekano wa kuingiza ubinafsi?
3. Je shida aliyoipata Samsoni kwa mkwewe ilitokana na kufungiwa nira na wasio na imani?
4. Uharibifu wa mazao ya Wafilisti uliofanywa na mbweha wa Samsoni ulikuwa wa lazima? Je, ulileta faida ye yote kwa Waisraeli?
5. Jitihada za Samsoni za kuwakomboa Waisraeli ziliwaletea usumbufu mkubwa kutoka kwa maadui zao kiasi cha kutamani Samsoni alegeze misimamo yake. Unadhani katika hatua hii ni nani alikuwa sahihi kati ya Samsoni na watu wake?
6. Mungu aweza kutumia chochote kilicho mkononi mwako kukuletea ushindi na mafanikio ikiwa utakitoa wakfu kwake. Unadhani iliwezekanaje taya la punda liue watu elfu tatu?
7. Unaridhika na namna Samsoni alivyoanza kuwaokoa Waisraeli?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 16:1-31    (27/05/2019)
Samsoni na Delila

1 Samsoni akaenda Gaza, akaona huko mwanamke kahaba, akaingia kwake. 2 Watu wa Gaza wakaambiwa, ya kwamba, huyo Samsoni amekuja huku. Wakamzingira, wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, Na tungoje mpaka mapambazuko, ndipo tutamwua. 3 Basi Samsoni akalala hata usiku wa manane, akaondoka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.
4 Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila. 5 Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. 6 Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe. 7 Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 8 Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo. 9 Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana. 10 Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani? 11 Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 12 Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi. 13 Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo. 14 Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung'oa ule msumari, na ule mtande.
15 Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. 16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. 17 Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 18 Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. 19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. 20 Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. 21 Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. 22 Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.
Kifo cha Samsoni
23 Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. 24 Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu. 25 Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili. 26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea. 27 Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza. 28 Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili. 29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto. 30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. 31 Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.

MASWALI YA KUJADILI:

1. Samsoni alikuwa na nguvu za kung'oa malango lakini hakuwa na nguvu za kushinda tamaa. Kipi kilikuwa muhimu kwake ili kufanikiwa kuwaokoa Waisraeli kikamilifu?
2. Je, kuna uwezekano wa kuutosheleza moyo ili usijisikie kutamani tena? Suleimani, Daudi, Samsoni, na hata Ibrahimu pamoja na matendo makuu waliyofanya walitamani. Nini kilimsaidia Yusufu asitamani mke wa Potifa? Unadhani inawezekana kuishinda dhambi hiyo leo?
3. Wakati Samsoni akitamani wanawake, Delila alitamani fedha alizoahidiwa ili kumsaliti mumewe. Ni nani kati ya hao anafanya dhambi zaidi? Je, ni halali kuwalaumu wanawake zaidi pale tabia za zinaa na uasherati zinaposhamiri?
4. Je, unadhani Samsoni alitambua makosa na udhaifu wake wakati anatoa siri ya nguvu zake? Je aliamini kwamba angeweza kukamatwa?
5. Kwa nini Wafilisti walimtumia mwanamke kumnasa Samsoni na si mwanaume Mfilisti mwenye nguvu kama Samsoni? Hii inakuambia nini juu ya uwezo wa wanawake kama ukitumiwa vizuri?
6. Kwa nini Wafilisti baada ya kumkamata Samsoni walihimidi miungu yao? Je hii ilikuwa ni vita ya kiroho baina ya Mungu wa mbinguni na Shetani chini ya kivuli cha miungu ya kipagani? Kwa hatua hii ni Mungu yupi alikuwa ameshinda?
7. Je, kuishiwa nguvu za kiroho ni dalili kuwa Mungu anakuacha au wewe unamwacha Mungu? Je, ukigundua nguvu zako zimepungua unaweza kumuomba Mungu akakurejeshea nguvu zako za awali?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 17:1-13    (28/05/2019)
Mika na Mlawi

1 Wakati huo alikuwako mtu mmoja wa nchi ya vilima ya Efraimu, ambaye jina lake alikuwa akiitwa Mika. 2 Naye akamwambia mama yake, Hizo fedha elfu na mia moja ulizonyang'anywa, ambazo uliweka kiapo kwa ajili yake na kusema masikioni mwangu, tazama, ninazo mimi hizo fedha; ni mimi niliyezitwaa. Mama yake akasema, mwanangu na abarikiwe na Bwana. 3 Basi akamrudishia mama yake hizo fedha elfu na mia moja. Mama yake akasema, Mimi naziweka fedha hizi kabisa ziwe wakfu kwa Bwana, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, ili kufanya sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu; basi kwa hiyo nakurudishia wewe. 4 Basi hapo alipomrudishia mama yake hizo fedha, mama yake akatwaa fedha mia mbili, akampa fundi mwenye kusubu fedha, naye akafanya sanamu ya kuchonga kwazo, na sanamu ya kusubu; ambazo zilikuwa ndani ya nyumba ya Mika. 5 Basi mtu huyo Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akafanya naivera, na kinyago, akamweka wakfu mmoja miongoni mwa wanawe, akawa kuhani wake. 6 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe.
7 Alikuwako mtu mmoja hirimu aliyetoka Bethlehemu-yuda, wa jamaa ya Yuda, aliyekuwa ni Mlawi, naye akakaa huko hali ya ugeni. 8 Mtu huyo akatoka katika huo mji, katika Bethlehemu-yuda, ili aende kukaa hali ya ugeni hapo atakapoona mahali; akafikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu katika safari yake, hata nyumba ya huyo Mika. 9 Mika akamwuliza, Watoka wapi wewe? Akamwambia, Mimi ni Mlawi wa Bethlehemu-yuda, nami naenda kukaa hali ya ugeni po pote nitakapoona mahali. 10 Mika akamwambia, kaa pamoja nami, uwe kwangu baba, tena kuhani, nami nitakupa fedha kumi mwaka kwa mwaka, na nguo ya kuvaa, na vyakula. Basi huyo Mlawi akaingia ndani. 11 Huyo Mlawi aliridhika kukaa na mtu huyo; kisha huyo hirimu akawa kwake kama wanawe mmojawapo. 12 Basi Mika akamweka wakfu huyo Mlawi, huyo hirimu, naye akawa kuhani wake, akakaa nyumbani mwa Mika. 13 Ndipo Mika akasema, Sasa najua ya kwamba Bwana atanitendea mema, kwa kuwa nina Mlawi kuwa kuhani wangu.

MASWALI YA KUJADILI:

1. Kuna hatari ya kung'ang'ania uelewa binafsi wa mambo ya kiroho na kupuuzia ule uelewa wa pamoja wa kundi la waumini katika siku tunazoishi. Unadhani hii inatokana na kila mmoja kujifanyia aonavyo kuwa ni mema machoni pao?
2. Mtu mwenye misimamo inayopingana na uelewa wa kundi la waumini afanyweje? Apuuzwe, asikilizwe, au aadhibiwe?
3. Kuna watu ambao hawaoni haja ya kuwa na viongozi wa kiroho waliopo unadhani wanafahamu madhara ya kutokuwa na viongozi? Unadhani lengo la msimamo wao huo ni kutaka wao ndiyo wawe viongozi?
4. Inawezekanaje mtu aliyewahi kumuamini Mungu wa kweli arudi nyuma hadi kuabudu vinyago? Hii inakuambia nini juu ya hatari ya kupoa kiroho? Kama unamnua mtu wa namna hiyo unapangaje kumsaidia?
5. Kuna watu wenye tamaa ya kutaka kuwamiliki na kuwatumia  viongozi wa kiroho kama mali yao na kuwashinikiza kufanya maamuzi wanayoyapenda kwa sababu ya jeuri ya pesa. Una maoni gani juu ya watu hao?
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 18:1-31   (29/05/2019)
Kuhama kwa Dani
1 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila ya Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hata siku hiyo urithi wao haujawaangukia kati ya kabila za Israeli. 2 Basi wana wa Dani wakatuma watu wa jamaa zao, watu watano katika hesabu yao yote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuiaua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hata nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko. 3 Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo hirimu, huyo Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Nawe wafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa? 4 Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake. 5 Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kwamba njia yetu tuiendeayo itafanikiwa. 6 Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea i mbele za Bwana.
7 Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote. 8 Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani? 9 Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Mwanyamaa tu? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo. 10 Hapo mtakapokwenda mtawafikilia watu wakaao salama salimini, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapana kupungukiwa na kitu cho chote kilicho duniani.
11 Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli. 12 Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu. 13 Nao wakapita huko hata hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikilia nyumba ya huyo Mika. 14 Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakajibu, na kuwaambia ndugu zao Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya. 15 Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafikilia nyumba ya huyo hirimu, Mlawi, hata hiyo nyumba ya Mika, nao wakamwuliza habari za hali yake. 16 Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango. 17 Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita. 18 Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi? 19 Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli? 20 Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu. 21 Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa mifugo, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao. 22 Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani. 23 Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii? 24 Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe?
 25 Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikiwe kati yetu, wasije walio na hasira wakakuangukia, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako. 26 Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa ni wenye nguvu kumshinda yeye, akageuka akarudi nyumbani kwake.
Wadani wafanya makao katika Laisha
27 Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, kwenye watu waliokuwa wenye starehe na hifadhi, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao. 28 Wala hakuwako mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa ni mbali sana na Sidoni, nao hawakuwa na shughuli na mtu awaye yote; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo. 29 Wakauita mji jina lake Dani, kwa kuliandama jina la baba yao Dani, aliyezaliwa kwake Israeli; lakini jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Laisha. 30 Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila ya Wadani hata siku ya kuchukuliwa mateka hiyo nchi. 31 Basi wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga aliyoifanya Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.
MASWALI YA KUJADILI:
1. Unadhani mpango wa kuuteka mji wa Laisha ulio katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu ulifanana na utekaji wa mji wa Yeriko? Je unadhani uliratibiwa na Mungu?
2. Kama haikuwa halali kwa kuhani kutumika kwa nyumba ya mtu mmoja ilikuwa halali kutumika kwa kabila moja la Wadani?
3. Huyu kuhani alikuwa na wito wa kufanya kazi yake alikuwa sawa hawa watumishi walioenea leo wanaopenda kufanyia kazi penye malisho mazuri na kutoa utabiri wa kufurahisha wateja wao?
4. Kwa nini hata leo sanamu za kuchonga zinatumika kwa makusudi ya ibada licha ya Mungu kupiga marufuku kwenye amri ya pili?
5. Watu wa Laisha hawakuwa na mwokozi huashiria kuwa hawakujishughulisha kutafuta usalama wao kutoka kwa Mungu ili alinde mafanikio yao. Ni nini uhakika wa usalama wa mwanadamu kando ya kumtegemea Mungu? Unachukua hatua gani kutorudia makosa ya watu wa Laisha?
6. Katika kisa hiki tunashuhudia maisha yaliyojaa ubabe na ukiukwaji wa haki za msingi kwa mujibu wa miongozo ambayo watu wamejiwekea na maagizo ya Neno la Mungu. Je unaishuhudia hali hiyo katika mahali unapoabudu? Unachukua hatua gani?
7. Wapo wanadamu wanaofanana na Wadani ambao hufanikisha mambo kwa utundu wao na kudai yametokana na Mungu ili kuyapa uhalali. Je hali hiyo Mungu anaikubali?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 19:1-30   (30/05/2019)
Suria wa Mlawi

1 Ikawa katika siku hizo, hapo kulipokuwa hapana mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa hali ya ugeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda. 2 Kisha huyo suria yake akaandama ukahaba kinyume chake, kumwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa kuko muda wa miezi minne. 3 Kisha mumewe akainuka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda wawili; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye. 4 Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, akamzuia; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala kuko. 5 Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu. 6 Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi. 7 Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi-sihi, naye akalala kuko tena. 8 Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili. 9 Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu. 10 Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye. 11 Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tugeuke kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu. 12 Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea. 13 Kisha akamwambia mtumishi wake, Haya, tuifikilie miji hii mmojawapo nasi tutalala katika Gibea au katika Rama. 14 Basi wakashika njia kwenda zao mbele; jua likawachwea walipokuwa karibu na Gibea, ambao ni mji wa Benyamini. 15 Wakageuka huko, wapate kuingia na kulala katika Gibea; akaingia ndani, akaketi katika njia kuu ya mji; kwa kuwa hapakuwa na mtu awaye yote aliyewakaribisha nyumbani kwake kulala.
16 Kisha, tazama, akatokea mtu mume mzee, atoka kazini kwake shambani, wakati wa jioni; mtu huyo alikuwa ni wa ile nchi ya vilima vilima ya Efraimu, naye alikuwa anakaa katika Gibea hali ya ugeni lakini wenyeji wa mahali hapo walikuwa Wabenyamini. 17 Naye alipovua macho yake, akamwona huyo mtu msafiri katika njia kuu ya mji; huyo mzee akamwuliza, Waenda wapi wewe? Nawe watoka wapi? 18 Akamwambia, Sisi twapita hapa kutoka Bethlehemu-yuda, twaenda huko upande wa mbali wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu; ndiko nilikotoka nami nilikwenda Bethlehemu-yuda; nami sasa naiendea nyumba ya Bwana wala hapana mtu anikaribishaye nyumbani mwake. 19 Walakini nyasi tunazo, na chakula cha hawa punda zetu; mkate pia tunao na divai kwa mimi na huyu kijakazi wako, na kwa huyu kijana aliye pamoja nasi watumishi wako; hapana uhitaji wa kitu cho chote. 20 Kisha huyo mzee alisema, Na iwe amani kwako; lakini na haya yaliyokupungukia na yawe juu yangu mimi lakini usilale njiani. 21 Basi akamtia ndani ya nyumba yake, akawapa punda chakula; nao wakaosha miguu, wakala na kunywa.
Hatia ya Gibea
22 Hapo walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, tazama, watu wa mji huo, watu mabaradhuli wakaizingira hiyo nyumba pande zote, wakagonga mlango; wakasema na huyo mwenye nyumba, huyo mzee, na kumwambia, Mlete nje mtu yule aliyefika nyumbani kwako, ili tupate kumjua. 23 Naye mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu. 24 Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii. 25 Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake. 26 Ndipo huyo mwanamke akaja alfajiri, akaanguka chini mlangoni pa nyumba ya mtu yule alimokuwamo bwana wake, hata kulipokucha. 27 Bwana wake akaondoka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aende zake, na tazama, huyo mwanamke suria yake alikuwa ameanguka pale mlangoni pa nyumba, na mikono yake ilikuwa i pale kizingitini. 28 Akamwambia, Haya ondoka, twende zetu; lakini hakuna aliyemjibu; ndipo akamwinua akamweka juu ya punda; mtu huyo akaondoka, akaenda mahali pake mwenyewe. 29 Naye alipokwisha kuingia nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika huyo suria yake, akampasua kiungo kwa kiungo, vipande kumi na viwili akampeleka katika mipaka yote ya Israeli. 30 Basi ikawa, wote walioliona jambo hilo wakasema, Jambo kama hili halijatendeka wala kuonekana tangu siku hiyo wana wa Israeli walipokwea kutoka katika nchi ya Misri hata leo; haya, lifikirini, fanyeni shauri, mkanene.

MASWALI YA KUJADILI:

1. Hali ya kukaa bila mfalme ni mfumo wa maisha usiozingatia sheria na maadili. Maelezo yanayopatikana katika sura hii yanafanana na maelezo yanayoripotiwa katika vyombo vya habari siku hizi. Hii inaashiria tumepuuzia sheria na maadili?
2. Kiongozi wa kiroho hakuwa makini katika kuchagua mwenzi wa maisha? Muda wa miezi 4 aliosubiri kabla ya kumfuata mkewe unadhihirisha uzembe au kukerwa na tabia ya ukahaba ya mkewe?
3. Kwa nini walio kwenye ndoa wamekosa uaminifu katika ndoa zao?
4. Mzazi wa mke wa kuhani alikuwa na lengo gani kuwachelewesha kuondoka wageni wake? Hakutaka waondoke au alitaka kuwafanyia ukarimu?
5. Tabia za watu Gibea zilifanana na watu wa Sodoma maana hawakuwapenda wageni na walikuwa hawana maadili. Unadhani ilikuwa busara kulala katika mji huo? Je chanzo cha tabia hii ni nini na nini kifanyike kuiondoa?
6. Kwa nini ili kujisalimisha walipendekeza wawatoe wanawake walionao ili wawatendee unyama? Je kama yule mwenyeji na Mlawi wangekuwa na upendo wa kweli wangependekeza nini badala yake?
7. Kitendo Mlawi alichomtendea mkewe kwa kumkatakata kwa mapanga kinadhihirisha alivyokuwa na roho mbaya au anavyochukia tabia ya ukahaba?
8. Kisa hiki kinatukumbusha jinsi baadhi ya ndoa zinavyopitia changamoto na manyanyaso wayapatayo wanawake? Je unadhani alichofanyiwa mwanamke kahaba alikistahili?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 20:1-48   (31/05/2019)
Kuvamiwa kwa Benjamini

1 Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hata Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkutanikia Bwana huko Mispa. 2 Hao wakuu wa watu, maana wakuu wa kabila zote za Israeli, wakajihudhurisha katika huo mkutano wa watu wa Mungu, watu waume mia nne elfu waendao kwa miguu, wenye kutumia upanga. 3 Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulikuwaje kutendeka? 4 Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale. 5 Nao watu waume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa. 6 Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli. 7 Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu. 8 Basi watu hao wote waliinuka kama mtu mmoja, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake. 9 Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kwa kura kwenda kuupiga; 10 nasi tutatwaa watu kumi katika mia katika kabila zote za Israeli, na watu mia katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili kwamba, hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli. 11 Basi waume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja.
12 Kisha kabila za Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu? 13 Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili kwamba tupate kuwaua, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli. 14 Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupiga vita juu ya wana wa Israeli. 15 Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba. 16 Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose.
17 Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni watu waume mia nne elfu, wenye kutumia upanga; hao wote walikuwa ni watu wa vita. 18 Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? Bwana akawaambia, Yuda atakwea kwanza. 19 Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao juu ya Gibea. 20 Watu wa Israeli walitoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea. 21 Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakaangamiza hata nchi watu ishirini na mbili elfu katika Israeli siku hiyo. 22 Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza. 23 Wana wa Israeli wakakwea juu na kulia mbele za Bwana hata jioni; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.
24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili. 25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga. 26 Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; nao wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. 27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo, 28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako. 29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.
30 Basi wana wa Israeli wakakwea kwenda kupigana na wana wa Benyamini siku ya tatu, wakajipanga ili kupigana na Gibea, kama walivyofanya nyakati nyingine. 31 Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kupiga na kuua katika hao watu, wapata kama watu thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika hizo njia kuu, ambazo njia mojawapo huendelea Betheli, na njia ya pili huendelea Gibea, katika shamba. 32 Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama kwanza. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu. 33 Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba. 34 Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakaja juu ya Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini hawakujua ya kuwa uovu ulikuwa karibu nao. 35 Bwana akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza watu waume ishirini na tano elfu na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga.
36 Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa; kwa kuwa watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea. 37 Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na hao wenye kuvizia wakaenda wakaupiga huo mji wote kwa makali ya upanga. 38 Basi hiyo ishara iliyoaganwa kati ya watu wa Israeli na hao wenye kuvizia ilikuwa ni hii, kwamba wafanye lipande wingu kubwa la moshi kutoka katika huo mji. 39 Nao watu wa Israeli walipogeuka katika vile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika vile vita vya kwanza. 40 Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, huo mji mzima ulikuwa wapaa juu katika moshi kwenda mbinguni. 41 Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walisitushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiliwa na uovu. 42 Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini vile vita vikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake. 43 Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyaga-kanyaga hapo walipopumzika, hata kufikilia Gibea upande wa maawio ya jua. 44 Wakaanguka watu wa Benyamini watu kumi na nane elfu, hao wote walikuwa ni watu waume mashujaa. 45 Kisha wakageuka na kukimbia upande wa nyika hata kulifikilia jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu watu waume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawapiga wengine wao watu elfu mbili. 46 Basi jumla ya watu wa Benyamini walioanguka siku ile walikuwa ni watu ishirini na tano elfu waliokuwa wanatumia upanga; wote hao walikuwa ni watu mashujaa. 47 Lakini watu waume mia sita wakageuka, wakakimbia upande wa nyikani mpaka jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne. 48 Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaitia moto.

MASWALI YA KUJADILI:

1.  Dhambi ya watu wachache isiposhughulikiwa ifaavyo na kwa wakati hugharimu maisha ya wengi au kundi zima. Unadhani kwa nini Benjamini walikataa kuwatoa mabaradhuli waliohusika na uovu uliotendeka? Je hiyo ingeepusha vita iliyotokea?2.  Je muda unaotumika kulumbana na kupigana vita katika familia na jumuia za kidini unapunguza muda wa kujiletea maendeleo na kumkabili adui yetu halisi?
3. Je kulipiza kisasi kama walikofanya Waisraeli kulikiwa kwa lazima?
4. Iliwezekanaje Waisraeli washindwe vitani hata baada ya kumuomba Mungu? Inawezekana kuna wakati tunamlazimisha Mungu  kufanya tunachotaka?
5. Katika kipindi kinachotajwa makabila yote ya Israeli hayakuwa katika mahusiano mazuri na Mungu. Je unayachukuliaje mazoea ya kumkimbilia Mungu wakati wa shida pekee?
6. Unadhani mataifa ya kipagani yaliyowazumguka Waisraeli walitamani kuwaona wakigombana au wakipatana?
7. Unadhani maovu yanakemewa kwa kiwango cha kuridhisha makanisani?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
WAAMUZI 21:1-25    (01/06/2019)
Kuokolewa kwa wabenjamini

1 Basi watu wa Israeli walikuwa wameapa huko katika Mispa, wakisema, Hapana mtu awaye yote kwetu sisi atakayemwoza binti yake kumpa Benyamini. 2 Basi hao watu wakafikilia Betheli, wakaketi kuko mbele ya Mungu hata jioni, nao wakainua sauti zao na kulia sana. 3 Wakasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, kwani jambo hili kuwa katika Israeli, ya kwamba hivi leo ni kabila moja limepunguka katika Israeli? 4 Kisha ikawa siku ya pili yake, hao watu wakaamka asubuhi na mapema, wakajenga madhabahu huko, wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. 5 Wana wa Israeli wakasema, Katika hizi kabila zote za Israeli ni ipi isiyofika katika mkutano kumkaribia Bwana? Kwa maana walikuwa wameweka kiapo kikuu katika habari za huyo asiyefika kumkaribia Bwana huko Mispa, huku wakisema, Hakika yake atauawa huyo. 6 Nao wana wa Israeli wakaghairi kwa ajili ya ndugu yao Benyamini, wakasema, Kabila moja imekatiliwa mbali na Israeli hivi leo. 7 Tufanyeje sisi ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa tumeapa kwa Bwana ya kwamba hatutawapa binti zetu ili wawaoe? 8 Basi wakasema, Ni ipi katika kabila za Israeli ambayo haikufika mbele ya Bwana huko Mispa? Na tazama, hakuja mmoja maragoni aliyetoka Yabeshi gileadi aufikilie huo mkutano. 9 Kwa maana hapo watu walipohesabiwa, hakuwapo hata mtu mmoja katika wenyeji wa Yabesh-gileadi. 10 Basi mkutano walipeleka huko watu kumi na mbili elfu wa hao waliokuwa mashujaa sana, kisha wakawaamuru, wakisema, Endeni mkawapige wenyeji wa Yabesh-gileadi kwa makali ya upanga, na hata wanawake na watoto wadogo. 11 Na jambo mtakalotenda ni hili; mtamwangamiza kila mume kabisa, na kila mwanamke ambaye amelala na mume. 12 Nao wakapata katika wenyeji wa Yabesh-gileadi wanawali mia nne, ambao hawajamjua mtu mume kwa kulala naye; basi wakawaleta maragoni huko Shilo, ulioko katika nchi ya Kanaani.
13 Basi mkutano ukatuma watu na kunena na wana wa Benyamini waliokuwako huko katika jabali la Rimoni, wakawatangazia amani 14 Basi Benyamini wakarudi wakati huo; nao wakawapa wale wanawake waliowaponya wali hai katika hao wanawake wa Yabesh-gileadi; lakini hawakuwatosha. 15 Nao watu wakaghairi kwa ajili ya Benyamini, kwa sababu Bwana alikuwa amefanya pengo katika hizo kabila za Israeli.
16 Ndipo hao wazee wa huo mkutano walisema, Je! Tufanyeje ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa wanawake wameangamizwa katika Benyamini? 17 Wakasema, Lazima kuwa urithi kwa hao wa Benyamini waliopona, isiwe kabila kufutika katika Israeli. 18 Lakini sisi hatuwezi kuwaoza binti zetu kwa maana wana wa Israeli walikuwa wameapa, wakisema, Na alaaniwe huyo atakayempa Benyamini mke. 19 Kisha wakasema, Angalieni, iko sikukuu ya Bwana mwaka baada ya mwaka katika Shilo, ulioko upande kaskazini wa Betheli, upande wa mashariki wa hiyo njia kuu iendeayo kutoka Betheli kwenda Shekemu, nao ni upande wa kusini wa Lebona. 20 Basi wakawaagiza hao wana wa Benyamini wakisema, Haya, endeni, mkaotee katika mashamba ya mizabibu, 21 mkaangalie, kisha tazameni, kwamba hao binti za Shilo watoka ili wacheze katika hiyo michezo, basi tokeni ninyi mizabibuni, nanyi kila mtu na amshike mkewe katika hao binti za Shilo, kisha rudini nchi ya Benyamini. 22 Kisha itakuwa, hapo baba zao au ndugu zao, watakapokuja kushitaki, sisi tutawaambia, Kwa ihisani yenu tupeni sisi; kwa kuwa hatukumtwalia kila mtu mkewe katika vita; wala ninyi hamkuwapa wao, au kama sivyo ninyi sasa mngekuwa na hatia. 23 Wana wa Benyamini wakafanya vivyo, wakajitwalia wake, sawasawa na hesabu yao, katika hao waliocheza, wakawachukua wakaenda nao; kisha wakaenda kuurudia urithi wao, na kuijenga miji na kuikaa. 24 Nao wana wa Israeli wakati huo wakaenda zao, kila mtu akaenda kwa kabila yake na kwa jamaa yake; nao wakatoka huko, waende kila mtu kuuendea urithi wake. 25 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.

MASWALI YA KUJADILI:

1. Waisraeli walijutia kuangamiza ndugu zao Wabenjamini kwa kuwa lengo lao lilikuwa kukomesha uovu usienee katika taifa zima. Je kuna umuhimu wa kupima adhabu tunazotoa kwa wakosaji ili zisivuke mipaka?
2. Viapo au nadhiri ni jambo linalopaswa kutolewa kwa uangalifu maana Yeftha katika Waamuzi 11:30 alitoa nadhiri iliyomgharimu. Unadhani kiapo walichotoa Waisraeli kutowapatia Benjamini wake wa kuoa kilikuwa cha lazima?
3. Waisraeli walilia sana walipogundua wamefanya kosa. Je toba ya kweli ni lazima wakati wote iandamane na kulia? Je kuna uwezekano wa mtu anayedai analia kwa sababu ya kujutia dhambi afanye hivyo kwa kuigiza?
3. Kwa nini ilikuwa lazima kabila moja ya Benjamini iliyopungua itafutiwe uwezekano wa kurejeshwa kwa namna ye yote ile?
4. Je njia iliyotumika kuwapatia wake wa kuoa ilikuwa sahihi?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
RUTHI 1:1-24    (02/06/2019)
Familia ya Elimeleki yaenda Moabu
1 Ikawa zamani za Waamuzi walipoamua, kulikuwa na njaa katika nchi. Akaondoka mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. 2 Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrathi wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko. 3 Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. 4 Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. 5 Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia.
Naomi na wakweze Wamoabi
 6 Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. 7 Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. 8 Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. 9 Bwana na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. 10 Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. 11 Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? 12 Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; 13 je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu. 14 Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. 15 Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. 16 Naye Ruthu akasema,
          Usinisihi nikuache,
             Nirejee nisifuatane nawe;
          Maana wewe uendako nitakwenda,
             Na wewe ukaapo nitakaa.
          Watu wako watakuwa watu wangu,
              Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
          17 Pale utakapokufa nitakufa nami,
              Na papo hapo nitazikwa;
         Bwana anitende vivyo na kuzidi,
              Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
 

 18 Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.
 19 Hivyo hao wakaendelea wote wawili hata walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote ulitaharuki kwa habari zao. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi? 20 Akawaambia, Msiniite Naomi niiteni Mara,kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana. 21 Mimi nalitoka hali nimejaa, naye Bwana amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa Bwana ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa? 22 Basi Naomi akarudi; pamoja na Ruthu Mmoabi, mkwewe; ambao walirudi kutoka nchi ya Moabu; nao wakafika Bethlehemu mwanzo wa mavuno ya shayiri.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Je lilikuwa wazo jema kwa Elimeleki na Naomi mkewe kwenda nchi ya wapagani ya Moabu kwenda kuhemea chakula? Unadhani wangebaki kwenye nchi yao Mungu asingewaponya kwa njaa?
2. Kulikuwa na jinamizi gani linawaandama hata mume na watoto wawili wakafariki na kubaki wajane 3 wasio na waume?
3. Dhana ya Naomi kuwa Mungu alikuwa amemkasirikia kutokana na vifo vilivyotokea (Ruthi 1:13,21) ina ukweli wowote au ni mawazo yatokanayo na uchungu wa kufiwa?
4. Ungekuwa unatakiwa kumfariji Naomi na wakweze ungewapa neno gani la faraja juu ya upendo wa Mungu?
5. Je lilikuwa wazo sahihi kwa Naomi na mumewe kuwaoza watoto wao kwa binti wa kipagani wa Moabu?
6. Kwa nini mabinti hawa wa kipagani (na hasa Ruthi) waling'ang'ania kuandamana na Naomi na kuwa sehemu ya jamii ya Israeli?
7.Wajane hawa watatu walifarijiana kulingana na machungu yanayofanana wanayoyapitia. Unadhani ipo haja ya wajane kujiundia umoja wa kufarijiana?
8. Unadhani familia na jumuiya za kidini zinafanya wajibu wao wa kutosha kusaidia wajane?
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
RUTHI 2:1-23    (03/09/2019)
1 Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. 2 Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. 3 Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. 4 Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, Bwana akae nanyi. Nao wakamwitikia, Bwana na akubariki. 5 Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? 6 Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; 7 naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. 8 Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. 9 Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. 10 Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? 11 Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. 12 Bwana akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. 13 Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. 14 Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. 15 Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. 16 Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. 17 Basi Ruthu akaokota masazo kondeni hata jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. 18 Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonyesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa. 19 Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi. 20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na Bwana, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwao waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa mbari yetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu. 21 Naye Ruthu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na vijana wangu, hata watakapomaliza mavuno yangu yote. 22 Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, wala watu wasikukute katika konde linginelo lote. 23 Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hata mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Ruthu alikuwa binti mwenye upendo wa kweli, mchapakazi, na mwaminifu asiye na majivuno. Mabinti wenye tabia za namna hii ni rahisi kupata ajira na wachumba. Ungekuwa mshauri wa vijana ungewashauri nini wasichana wanaotafuta kazi na wachumba?
2. Umuhimu wa Ruthu kuandamana na mkwewe unaonekana baada ya Ruth kuwa mtafuta riziki ya familia. Nini kinakosekana leo kwa wakwe kushindwa kuishi vizuri na wakwe zao?
3. Tatizo la ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha linazidishwa na tabia ya vijana wengi kuchagua kazi za kufanya. Unadhani Ruthu alikubali kufanya kazi ye yote kwa kuwa hakuwa mwenyeji wa nchi ile au kwa kuwa alikuwa na njozi ya maisha?
4. Boazi ni mfano bora wa matajiri wenye kuwafikiria wale waliokuwa nacho. Unadhani Mungu anawafikiria wanyonge wanaofanya kazi katika mazingira magumu ili kujikimu kimaisha? Je unatoa mchango gani kusaidia watu hao?
5. Mara nyingine tumeshuhudia ndugu wa karibu wakiwa wagumu kujihisisha na shida za ndugu zao kuliko watu baki. Unajifunza nini kutoka kwa Boazi kuhusiana na hali hii?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
RUTHU 3:1-18    (04/06/2019)
1 Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema? 2 Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani. 3 Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa. 4 Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya. 5 Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya. 6 Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza. 7 Ikawa huyo Boazi alipokwisha kula na kunywa, na moyo wake umekunjuka, alikwenda kulala penye mwisho wa chungu ya nafaka; na huyo mwanamke akaja taratibu, akaifunua miguu yake, akajilaza papo hapo. 8 Na ikawa usiku wa manane yule mtu akasituka, akajigeuza; na kumbe! Yupo mwanamke amelala miguuni pake. 9 Akasema, Ama! Ni nani wewe? Akamjibu, Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako; uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu. 10 Akamwambia, Mwanangu, ubarikiwe na Bwana; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo, kwa vile usivyowafuata vijana, kama ni maskini kama ni matajiri. 11 Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema. 12 Tena ndiyo kweli ya kuwa mimi ni wa jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi. 13 Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; Bwana aishivyo. Ulale wewe hata asubuhi. 14 Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga. 15 Tena alisema, Lete hapa shela yako uliyoivaa, uishike; naye akaishika; naye akampimia vipimo sita vya shayiri akamtwika; kisha huyo mwanamke akaenda zake mjini. 16 Basi alipofika kwa mkwewe, huyo akamwuliza, Je! Mwanangu, imekuwaje? Akamwambia yote yule mtu aliyomfanyia. 17 Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu. 18 Naye mkwewe akasema, Basi, mwanangu, tulia; hata utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili; kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Naomi alifanya sehemu yake kulipa ukarimu wa mkwewe kwa kuntengenezea mazingira ya kupata mchumba. Unadhani wazazi wana nafasi ye yote katika kuwatafutia vijana wao wachumba wanaofaa?
2. Unadhani mpango wa uchumba wa Ruthu na Boazi ulitoka kwa Mungu?
3. Je ikiwa binti anasukumwa kutoka kuolewa na mvulana aliyekidhi vigezo vyake atafanyaje kufikisha ujumbe huo kwa njia nzuri kwa yule mvulana?
4. Je tofauti ya umri ni sababu ya watu waliopendana kutooana? Tofauti kubwa ya umri kati ya wanaooana ina athari gani katika ndoa?
5. Je ni jambo linalokubalika kwa wachumba kutembeleana hali wakiwa wanaishi peke yao? Kuna faida na hasara gani ikiwa watafanya hivyo?
6. Ni sahihi kumpa mchumba zawadi? Je uchumba ukifa una haki ya kuidai zawadi hiyo?
7. Boazi alikuwa muungwana maana hakumwingilia kingono Ruthu walipokuwa peke yao usiku. Una maoni gani kwa vijana wanaofanya ngono wakati wa uchumba?
8. Kuomba ili Mungu akupe mchumba peke yake hakutoshi. Jitihada za kujiweka katika mazingira ya kuchumbiwa kama alivyofanya Ruthu ni za muhimu. Una jambo gani ulilojifunza kutoka kwa Ruthu linalofaa kuigwa na vijana wa leo?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
RUTHI 4:1-22    (05/06/2019)
1 Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi. 2 Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi. 3 Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki; 4 nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi. 5 Ndipo Boazi aliposema, Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu, ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake. 6 Basi yule jamaa aliyekuwa wa karibu akasema, Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafsi yangu, nisije nikauharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa. 7 Basi hii ilikuwa desturi zamani za kale katika Israeli, kwa habari ya kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israeli. 8 Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake. 9 Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi. 10 Tena, huyu Ruthu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi. 11 Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu. 12 Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa Bwana katika mwanamke huyu. 13 Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na Bwana akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume. 14 Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe Bwana, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli. 15 Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto saba, ndiye aliyemzaa. 16 Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake. 17 Nao wale wanawake waliokuwa jirani zake wakampa jina, wakisema, Naomi amezaliwa mwana; wakamwita jina lake Obedi; yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi. 18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi; Peresi alimzaa Hesroni; 19 na Hesroni akamzaa Ramu; na Ramu akamzaa Aminadabu; 20 na Aminadabu akamzaa Nashoni; na Nashoni akamzaa Salmoni; 21 na Salmoni akamzaa Boazi; na Boazi akamzaa Obedi; 22 na Obedi akamzaa Yese; na Yese akamzaa Daudi.
  
MASWALI YA KUJADILI:
1. Boazi alimpa mkubwa wake fursa ya kuamua juu ya urithi wa ndugu yao Elimeleki.n Unazungumziaje wale ambao kutoka na uwezo wa kiuchumi huwadharau wakubwa wao na kujitwalia madaraka ya kuongoza koo na familia zao isivyo halali?
2. Ndoa ni jambo nyeti linalostahili kuhusisha viongozi wa dini. Unatoa maoni gani juu ya ndoa Hza kimila na kuchukuana bila utaratibu zinazozidi kushamiri leo?
3. Ukoo wa Elimeleki walitambua za wajane Naomi na Ruthi na kupitia baraza la wazee wakaweka utaratibu wa kuwasadia. Kwa nini katika familia zingine wajane wananyanyaswa na kunyimwa haki zao? Je kanisa linaweza kufanya nini kuwasaidia wajane wasinyanyasike?
4. Ndoa zinazofungwa kanisani zina faida gani ukilinganisha na zile za kienyeji?
5. Unadhani ni furaha ya kiasi gani alikuwa nayo Ruthi - mwanamke mjane  na ambaye hakubahatika mtoto alipoolewa na kupata mtoto. Hii inatufundisha kutokata tamaa katika maisha?
6. Kuolewa kwa Ruthi na kuzaliwa kwa mtoto katika ukoo wa kifalme waYuda kulileta faraja gani kwa Naomi katika uzee wake? Unadhani alipata kitu cha kutuliza maumivu ya kufiwa?
7. Iliwezekanaje Ruthi Mmoabi awe katika ukoo wa Yesu? Unadhani Orpa (mjane mwenza wa Ruthi) kwa kurudi kwake Moabu kulimpotezea fursa ya kuwa miongoni mwa jamii ya Israeli?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 1:1-28    (06/06/2019)
1 Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu 2 naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. 3 Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. 4 Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; 5 lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 6 Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 7 Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. 8 Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? 9 Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana. 10 Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. 11 Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. 12 Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. 13 Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. 14 Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. 15 Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. 16 Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. 17 Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. 18 Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. 19 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. 20 Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana. 21 Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea Bwana dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake. 22 Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za Bwana, akae huko daima. 23 Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hata utakapomwachisha maziwa; Bwana na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hata akamwachisha maziwa. 24 Naye alipokuwa amekwisha kumwachisha maziwa, akamchukua pamoja naye, na ng'ombe watatu, na efa moja ya unga,na chupa ya divai,akamleta nyumbani kwa BWANA,huko Shilo ;na Yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. 25 Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli. 26 Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana. 27 Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; 28 kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Mtu anaweza kujiuliza Elkana aliwezaje kuwa na wake wawili? Je jambo hili lilikuwa halali machoni pa Mungu? Matatizo yaliyojitokeza kwenye familia yake yanathibitisha kuwa haukuwa mpango wa Mungu?
2. Tatizo la kukosa mtoto limeziumiza baadhi ya familia. Elikana alitumia njia gani unazozikubali katika kupunguza maumivu ya kukosa mtoto kwa mke wake?
3. Mara nyingi Mungu alipolifunga tumbo la mwanamke asizae alilifungua baadaye kwa kumpatia mtoto aliyekuwa muhimu kwa familia, jamii, na kwa ulimwengu kama ilivyotokea kwa Hana. Unapata ujumbe gani wa faraja kutokana na ukweli huo?
4. Unapokuwa na jambo nyeti unalotaka Mungu akutendee ni lazima uchukue hatua zisizo za kawaida. Hatua gani umevutiwa nazo ambazo Hana alizitumia kukabili changamoto yake ambazo ungependekeza kwa mtu anayepitia changamoto hizo?
5. Kuhukumu wengine kwa jambo tusilo na hakika nalo ni kosa linaloumiza wale wanaotuhumiwa. Umehusika kwa namna gani kutafsiri vibaya vitendo vya wengine? Je umeitikia tuhuma hizo kama alivyofanya Hana?
6. Hana alimtoa mwanawe kwa Mungu mara tu baada ya kuachishwa kunyonya. Umemtoa mwanao kwa Mungu mapema kiasi gani ili alelewe kiroho?
7. Unadhani Hana alijisikiaje siku aliyopata mtoto? Je 'wakati ulipowadia Hana akachukua mimba' unaeleza ukweli kuwa kila jambo lina wakati wake?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 2:1-36    (07/06/2019)
1 Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; 2 Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. 3 Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani. 4 Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. 5 Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. 6 Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. 7 Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. 8 Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. 9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; 10 Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake. 11 Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia Bwana mbele yake Eli, kuhani. 12 Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali Bwana, 13 wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu ye yote alipotoa dhabihu wakati wo wote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake; 14 naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko. 15 Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi. 16 Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu. 17 Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Bwana; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya Bwana. 18 Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za Bwana, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani. 19 Tena mamaye humfanyizia kanzu ndogo, na kumletea mwaka kwa mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka. 20 Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, Bwana na akupe uzao kwa mwanamke huyu, badala ya azimo aliloazimiwa Bwana. Kisha wakaenda nyumbani kwao. 21 Naye Bwana akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za Bwana. 22 Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. 23 Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. 24 Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa Bwana. 25 Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu Bwana amekusudia kuwaua. 26 Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa Bwana, na kwa watu pia. 27 Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, Bwana asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao? 28 Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa mbari ya baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto? 29 Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; ukawaheshimu wanao kuliko mimi, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema? 30 Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu. 31 Angalia, siku zinakuja, nitakapoukata mkono wako, na mkono wa mbari ya baba yako, hata nyumbani mwako hatakuwako mzee. 32 Nawe utalitazama teso la maskani yangu, katika utajiri wote watakaopewa Israeli; wala nyumbani mwako hatakuwako mzee milele. 33 Tena mtu wa kwako, ambaye sitamtenga na madhabahu yangu, atakuwa mtu wa kukupofusha macho, na kukuhuzunisha moyo; tena wazao wote wa nyumba yako watakufa wapatapo kuwa watu wazima. 34 Na hii ndiyo ishara itakayokuwa kwako, itakayowapata wana wako wawili, Hofni na Finehasi; watakufa wote wawili katika siku moja. 35 Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele. 36 Kisha itakuwa, ya kwamba kila mtu atakayesalia katika nyumba yako atakwenda kumsujudia, apate kipande kidogo cha fedha, na mkate mmoja; na kumwambia, Tafadhali unitie katika kazi mojawapo ya ukuhani, nipate kula kipande kidogo cha mkate.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Maombi ya kushukuru ya Hana yamejaa sifa kwa Mungu juu ya uwezo wake wa kuokoa. Kwa nini maombi yetu mengi yamejaa mahitaji badala ya sifa na kushukuru?
2. Kuna faida gani katika maombi ya sifa na shukrani?
2. Kwa kulinganisha na kisa cha wakoma 10, kwa nini idadi ya wanaorudi ili kumshukuru Mungu huwa ni chache? Kwa nini kuna shuhuda chache katika mikutano ya kiroho kwenye makanisa leo hii?
3. Wana wa Eli walifanya dhambi kwa kukiuka kanuni za utoaji sadaka kwa kujitwalia sadaka isivyostahili na kulala na wanawake. Dhambi hii ingalipo leo miongoni mwa watumishi wa Mungu?
4. Iliwezekanaje Samweli asiige tabia hii mbaya kutoka kwa wakuu wake wa kazi?
5. Hatua aliyochukua Eli baba yao na kiongozi wa kiroho dhidi ya tabia za watoto wao inaridhisha? Je ilikidhi matarajio ya waumini? Je ilikidhi matarajio ya Mungu?
6. Kwa nini wakati fulani viongozi na waumini hukosa ujasiri kuchukua hatua dhidi ya wale wanaomkosea Mungu kanisani? Je Mungu anaridhishwa na hali hiyo?
7. Je watumishi wa Mungu wanapofanya makosa katika utumishi wao ni halali kujitwalia nafasi ya Mungu na kuwahukumu kwa kutumia nguvu?
8. Je Mungu ana mpango wa kuwashughulikia watumishi wabovu wa kiroho wanaowapotosha watu? Kwa nini mara nyingi anaonekana kukawia kuchukua hatua hizo?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 3:1-21    (08/06/2019)
1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. 2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), 3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; 4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. 5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. 6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. 7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. 8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. 9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. 10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. 11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha. 12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho. 13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia. 14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele. 15 Naye Samweli akalala hata asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya Bwana. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo. 16 Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa. 17 Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lo lote katika hayo yote Bwana aliyosema nawe. 18 Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lo lote. Naye akasema, Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema. 19 Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini. 20 Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana. 21 Naye Bwana akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa Bwana akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la Bwana. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Iliwezekanaje Samweli kulala hekaluni tena karibu na sanduku (ndani ya vyumba vitakatifu) bila kuwa na hatia?
2. Kwa nini inasemwa nyakati za ukuhani wa Eli neno la Mungu lilikuwa adimu? Je yaweza kuwa watu walikuwa hawahubiriwi neno ila mapokea na siasa? Hali hiyo ipo kanisani kwenu?
3. Utatambuaje ikiwa mtu ameitwa na Mungu kwa kazi yake? Utawatambuaje wale wanaolazimisha wameitwa na Mungu kumfanyia kazi na kumbe wamejiingiza kwa nguvu kukidhi matakwa yao?
4. Unazungumziaje wale wanaokataa kufanya kazi ya Mungu hadi wabembelezwe au hadi watumiwe wajumbe maalumu? Je ni dalili ya unyenyekevu?
5. Mungu anamaanisha nini anaposema atatenda tendo katika siku za usoni ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha?
6. Je ni kweli kuwa Eli hakuzuia laana isiwakute watoto wake? Huruma kwa mwenye makosa inaweza kuwa njia ya kumtafutia laana mtu huyo?
7. Kwa nini uovu wa nyumba ya Eli ulikuwa hausafishiki kwa dhabihu wala kwa sadaka? Je kuna dhambi ambayo damu ya Yesu haiwezi kuitakasa?
8. Je kuna wakati kama mtumishi wa Mungu unaweza kuogopa kuwaeleza watu ukweli kwa kulinda maisha yako au maslahi fulani?
9. Waisraeli walitambua kuwa Samweli amewekwa na Bwana. Je leo kuna shida ya kutowatambua (kuwapa heshima wanayostahili) watumishi wa Bwana?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 4:1-22    (09/06/2019)
1 Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli, nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani;wakatua karibu na Ebenezeri ,nao Wafilisti wakatua huko Afeki. 2 Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne. 3 Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. 4 Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu. 5 Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. 6 Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la Bwana limefika kambini. 7 Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. 8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. 9 Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. 10 Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. 11 Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa. 12 Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake. 13 Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia. 14 Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli. 15 Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona. 16 Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu? 17 Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa. 18 Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini. 19 Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia. 20 Hata alipokuwa katika kufa, wale wanawake waliohudhuria karibu naye wakamwambia, Usiogope; kwa maana umezaa mtoto mwanamume. Walakini hakujibu, wala hakumtazama. 21 Akamwita mtoto, Ikabodi, akisema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; kwa sababu sanduku la Mungu lilikuwa limetwaliwa, na kwa sababu ya mkwewe na mumewe. 22 Naam, akasema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; maana sanduku la Mungu limetwaliwa.
 
 MASWALI YA KUJADILI:
1. Unadhani nini kilikuwa chanzo cha Waisraeli kuwa dhaifu na kupigwa na adui zao?
2. Uamuzi wa wazee kulileta Sanduku la Agano vitani lilikuwa sahihi na lilipata baraka za Mungu?
3. Unadhani nini kingekuwa sahihi kufanyika baada ya kipigo walichopata vitani?
4. Kosa la kubeba sanduku la agano kutoka chumba cha pili cha hekalu (ambako kuhani mkuu pekee alikuwa anaruhusiwa kuingia) kunatokana na dhambi walizotuhumiwa hapo awali ambazo hazikuwa zimeshughulikiwa?
5. Kwa nini sanduku lilishindwa kufanya miujiza kama lilivyofanya wakati wa kuvuka mto Yordani?
6. Kwa nini Mungu aliruhusu sanduku litwaliwe na Wafilisti na kuifanya miungu ya kipagani ionekane ina nguvu kuliko Mungu wa kweli wa Israeli?
7. Je kifo cha Hofni na Finehasi kinaashiria kuwa makuhani hao watukutu walikuwa wanapokea malipo ya uovu wao?
8. Je, Kuhani Mkuu Eli na mkwewe nao walikufa kwa sababu walikuwa wanawatetea makuhani hao waliojitwalia madaraka yasiyo wahusu   au kwa sababu ya kutambua kuwa Mungu ameliacha taifa la Israeli?
9. Unajifunza nini kuhusu kisa hiki unachopanga kurekebisha ili kuepuka hasira ya Mungu dhidi yako na dhidi ya kanisa lako?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 5:1-12    (10/06/2019)
1 Basi Wafilisti walikuwa wamelichukua sanduku la Mungu, wakaenda nalo kutoka Eben-ezeri hata Ashdodi. 2 Wafilisti wakalichukua sanduku la Mungu, wakalitia katika nyumba ya Dagoni, wakaliweka karibu na Dagoni. 3 Na watu wa Ashdodi, walipoamka alfajiri siku ya pili, kumbe! Dagoni imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana. Wakaitwaa Dagoni, wakaisimamisha mahali pake tena. 4 Hata walipoamka kesho yake asubuhi, kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu. 5 Kwa hiyo makuhani wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo. 6 Lakini mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaharibu, akawapiga kwa majipu, huko Ashdodi na mipakani mwake. 7 Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa, walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu. 8 Basi wakatuma watu waende kuwakusanya kwao mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Mungu wa Israeli? Nao wakajibu, Sanduku la Mungu wa Israeli na lihamishwe liende Gathi. Wakalihamisha sanduku la Mungu wa Israeli. 9 Ikawa, walipokwisha lihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa juu ya mji huo, kwa kuwafadhaisha sana; akawapiga watu wa mjini, wadogo kwa wakubwa, wakapatwa na majipu. 10 Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu mpaka Ekroni. Ikawa, sanduku la Mungu lilipofika Ekroni, watu wa Ekroni walifanya kelele, wakasema, Wamelileta hilo sanduku la Mungu wa Israeli kwetu, hata kutuua sisi na watu wetu. 11 Kwa hiyo wakatuma watu waende kuwakusanya mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Liondoeni hilo sanduku la Mungu wa Israeli, liende tena mahali pake, ili lisituue sisi, wala watu wetu; kwa sababu kulikuwa na fadhaa kubwa sana mjini mwote; mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko. 12 Na wale wasiokufa walipigwa kwa yale majipu; na kilio cha mji kikafika mbinguni.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Wafilisti waliamini miungu yao ndiyo iliyowawezesha kulitwaa sanduku la agano. Unadhani Mungu aliruhusu sanduku litwaliwe ili akadhihirishe ukuu wake dhidi ya miungu ya kipagani? Nini kilidhihirisha ukuu huo?
2. Je inawezekana mwanadamu kumtetea Mungu anapoona anadhalilishwa? Mungu anapotegemea utetezi wa wanadamu badala ya kujitetea mwenyewe anakuwa amepoteza sifa za kuwa Mungu?
3. Je kuwa na sanamu katika nyumba za ibada ni desturi ya dini za kipagani?
4. Je sanduku la agano lililotekwa lilikuwa mbaraka kwa Wafilisti? Kwa nini?
5. Wafilisti walikuwa na viongozi walioitwa mashehe. Je Wafilisti walikuwa Waislamu?
6. Kwa nini sanduku la agano halikuleta madhara makubwa kwa Wafilisti vitani kama lilivyoleta lilipofikishwa kwenye miji ya Wafilisti?
7. Mungu alitaka kuwafundisha nini Wafilisti na Waisraeli?
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 6:1-21     (11/02/2019)
1 Basi, hilo sanduku la Bwana lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba.2 Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Bwana? Tuonyesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake. 3 Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu. 4 Ndipo wakauliza, Na hayo matoleo ya kosa yatakuwa ya namna gani, hayo tutakayompelekea? Nao wakajibu, Na yawe majipu ya dhahabu matano, na panya wa dhahabu watano, sawasawa na idadi ya mashehe wa Wafilisti; kwa kuwa tauni moja ilikuwa juu yenu nyote, na juu ya mashehe wenu. 5 Kwa hiyo mtafanyiza sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu waiharibuo nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu. 6 Mbona, basi, mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya migumu mioyo yao? Hata na hao, hapo alipokwisha kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu, nao wakaenda zao? 7 Basi sasa jifanyizieni gari jipya, mtwae na ng'ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng'ombe garini, na kuwaondoa ndama zao na kuwatia zizini; 8 kisha, litwaeni hilo sanduku la Bwana, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda. 9 Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni ajali iliyotupata. 10 Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng'ombe wawili wakamwao, wakawafunga garini, na ndama zao wakawafunga zizini; 11 kisha wakaliweka sanduku la Bwana juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao. 12 Na hao ng'ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kuume wala wa kushoto; na mashehe wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi. 13 Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona. 14 Na lile gari likaingia katika konde la Yoshua wa Beth-shemeshi, na kusimama pale pale, palipokuwapo jiwe kubwa; basi wakaipasua miti ya lile gari, wakawatoa wale ng'ombe kuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. 15 Nao Walawi walilishusha sanduku la Bwana, na lile kasha lililokuwa pamoja nalo, lenye vile vitu vya dhahabu; wakaviweka juu ya lile jiwe kubwa; nao watu wa Beth-shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja dhabihu siku iyo hiyo kwa Bwana. 16 Na hao mashehe watano wa Wafilisti, hapo walipokwisha kuyaona hayo, walirejea Ekroni siku iyo hiyo. 17 Hii ndiyo hesabu ya yale majipu waliyoyapeleka wale Wafilisti, yawe matoleo ya kosa kwa Bwana; kwa Ashdodi moja, kwa Gaza moja, kwa Ashkeloni moja, kwa Gathi moja, na kwa Ekroni moja; 18 na panya wa dhahabu, kwa idadi ya miji yote ya Wafilisti, milki zao wale mashehe watano, miji yenye maboma na vijiji vya mashamba pia. Nalo lile jiwe kubwa, ambalo juu yake waliliweka sanduku la Bwana, liko hata hivi leo hapo kondeni pa Yoshua wa Beth-shemeshi. 19 Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa uuaji mkuu. 20 Nao watu wa Beth-shemeshi wakasema, Ni nani awezaye kusimama mbele za Bwana, huyu Mungu mtakatifu? Naye atapanda kwenda kwa nani kutoka kwetu? 21 Nao wakatuma wajumbe waende kwa wenyeji wa Kiriath-yearimu, kusema, Wafilisti wamelirudisha sanduku la Bwana; basi shukeni, mkalichukue kwenu.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Wafilisti hawakutaka kushindana na Mungu kama Farao na hivyo walikubali kuwa miungu yao imeshindwa na kuamua kulirudisha sanduku la agano. Kwa nini kwa miezi yote saba Waisraeli hawakufanya jitihada zozote za kulirejesha sanduku la agano?
2. Unadhani toba ya Wafilisti ilipokelewa na Mungu? Kwa hatua hii ya toba na mipango ya kurejesha sanduku Wafilisti wanaonekana kuwa wa kiroho kuliko Waisraeli?
3. Kama jibu ni ndiyo kwa nini na kama jibu ni hapana ni kwa nini?
4. Ng'ombe ambao hawajafungwa nira na gari jipya lililobeba sanduku viliongoza msafara bila kukosea. Nini kiliwaongoza ng'ombe hao wanyonyeshao wasiliache sanduku na kurudi nyumbani kwenda kuwahudumia ndama wao?
5. Kitendo cha kuwatoa kafara ng'ombe waliobeba sanduku kinadhihirisha ukatili kwa wanyama au kicho cha hali ya juu kwa Mungu wa mbinguni?
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 7:1-17    (11/06/2019)
1 Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la Bwana, wakalileta ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la Bwana. 2 Ikawa, tangu siku hiyo ambayo sanduku lilikaa Kiriath-yearimu wakati ulikuwa mwingi; kwa maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Israeli wakamwombolezea Bwana. 3 Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. 4 Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake. 5 Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana. 6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. 7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. 8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. 9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia. 10 Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini Bwana akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli. 11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari. 12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia. 13 Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli. 14 Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori. 15 Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake. 16 Naye huenda mwaka kwa mwaka kuzunguka mpaka Betheli, na Gilgali, na Mispa; akawaamua Israeli mahali hapo pote. 17 Na kurudi kwake kulikuwa mpaka Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Israeli; na huko akamjengea Bwana madhabahu.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Chini ya uongozi wa Samweli Israeli inashuhudia uamsho mkuu wa kiroho na matengenezo. Iliwezekanaje wakati huu waliwashinda maadui zao na kurejesha maeneo yaliyotekwa ingawa hawakuwa na sanduku la agano?
2. Unadhani ni uamsho na matengenezo gani yanahitajiwa leo kanisani kwako?
3. Kuna jambo gani maishani mwako linaloshuhudia kuwa hata sasa Bwana anakusaidia?
4. Kwa nini Wafilisti walioonekana kama wametubu na kumkiri Mungu wa Waisraeli waligeuka na kupanga kuwashambulia tena Waisraeli? Hii inaeleza nini kuhusu tabia ya mwanadamu?
5. Katika vita vya kiroho hatuhitaji kupigana kwa nguvu zetu maana Mungu ameahidi kutupigania. Unaamini kuwa kama ukiwa na imani Mungu aweza kuwasikilizisha sauti ya kishindo adui zako na kusababisha wakimbie?
6. Je, unachukua nafasi ya kuwalilia kwa maombi watu wa Mungu walio katika dhiki kuu? Ikiwa Mungu alisikiliza kilio cha Samweli hawezi kusikiliza cha kwako?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 8:1-22    (13/06/2019)
1 Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. 2 Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. 3 Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. 4 Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; 5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. 6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana. 7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. 8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe. 9 Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki. 10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana. 11 Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. 12 Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. 13 Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji. 14 Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. 15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake. 16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. 17 Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. 18 Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; Bwana asiwajibu siku ile. 19 Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; 20 ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu. 21 Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana. 22 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Kwa nini swala la Waisraeli kutaka kuongozwa na mfalme lilikuwa baya machoni pa Mungu. Kama viongozi hawafai ilitakiwa wachukue hatua gani muafaka?
2. Kwa nini matendo mabaya yanayotendwa kwa viongozi wa kiroho Mungu anayachukulia kama yametendwa kwake?
3. Kwa mujibu wa maelezo ya sura hii haifai kujichagulia kiongozi wa kukuongoza bila kumshirikisha Mungu. Unadhani ni njia gani sahihi ya kufanya ili usije ukachagua kiongozi atakayewaletea mateso badala ya baraka?
4. Tamaa ya kutaka kuendesha mifumo ya maisha yetu kama wafanyavyo wale wasio na hofu ya Mungu ipo hata leo hii.
5. Je kuna ubaya wa kuiga wafanyavyo maadui zetu?
6. Kwa nini Israeli walichoshwa kuongozwa na Mungu?
7. Kwa nini wakati fulani Mungu huruhusu kile tukiombacho hata kama kina madhara kwetu?

USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMWELI 9:1-27    (14/06/2019)
1 Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. 2 Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote. 3 Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. 4 Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. 5 Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi. 6 Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea. 7 Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi? 8 Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu. 9 (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) 10 Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu. 11 Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko? 12 Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu; 13 mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona. 14 Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu. 15 Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, 16 Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia. 17 Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. 18 Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? 19 Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. 20 Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako? 21 Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila ya Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo? 22 Naye Samweli akamtwaa Sauli na mtumishi wake, akawaleta ndani sebuleni, akawaketisha mahali pa heshima kati ya watu walioalikwa, nao jumla yao walikuwa kama watu thelathini. 23 Samweli akamwambia mpishi, Lete ile sehemu niliyokupa, hiyo niliyokuambia, Iweke akiba. 24 Basi mpishi akatwaa paja, na nyama iliyokuwa juu yake, akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, Iliyowekwa akiba ndiyo hiyo! Iweke mbele yako ule, kwa sababu umewekewa hiyo wewe hata wakati uliokusudiwa, maana nalisema, Nimewaalika watu. Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo. 25 Hata waliposhuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, akaongea na Sauli darini. 26 Nao wakaamka alfajiri; kisha ikawa, kulipopambazuka, Samweli akamwita Sauli darini, akisema, Inuka, nikupeleke kwenu. Basi Sauli akainuka, nao wakatoka wote wawili, yeye na Samweli. 27 Hata walipokuwa wakishuka mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, Mwambie mtumishi atangulie, (naye akatangulia), bali wewe simama hapa sasa, ili nikuambie neno la Mungu.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Kupotea kwa punda wa Kishi babaye Sauli kunahusianaje na mpango wa Mungu wa kuwapatia Israeli?
2. Je tunapokuwa tunahangaika kumpata kiongozi Mungu huwa ana mtu tayari aliyemuandaa?
3. Kulingana na yale Sauli aliyofanya baadaye na alivyokufa vitani baada ya kugeukia umizimu na nguvu za giza unadhani lilikuwa chaguo sahihi la Mungu?
4. Sauli kabla hajawa mfalme alikuwa mnyenyekevu pamoja na ukweli kuwa alikuwa nzuri kuliko watu wote. Kwa nini baada ya kuwa mfalme Sauli alipoteza hali hiyo?
5. Watu wanaotabiri yaliyotokea na yatakayotokea (Waonaji au Manabii) walikuwepo nyakati za Sauli na kupitia kwa Samweli Sauli alitambua kuwa punda wameonekana. Je watu hao ni muhimu na wanapatikana hata sasa?
5. Je dhana ya kuwalipa kwa huduma wanayoitoa kulingana na mawazo ya Sauli na rafiki yake ni sahihi kibiblia?
6. Unaizungumziaje huduma kama ya marehemu pastor Godson wa Hedaru? Kuna haja ya kuwepo mtu atakayechukua nafasi yake?
7. Kuna ukweli kuwa punda wale walipotea ili Sauli akutane na Samweli ili apewe ujumbe nzito kutoka kwa Mungu utakaobadilisha hatima ya maisha yake na maisha ya taifa la Israeli? Je kuna ukweli kuwa si kila baya linalotokea maishani mwako lina kusudi baya? Mwombe Mungu akusaidie kushukuru kwa kila jambo na kuacha kunung'unikia kila jambo maana lipo lililokusudiwa kukuletea mema.
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 Samueli 10:1-27    (15/06/2019)
1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta uwe mkuu juu ya urithi wake. 2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? 3 Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; 4 nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. 5 Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; 6 na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. 7 Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. 8 Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya. 9 Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. 10 Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao. 11 Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? 12 Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n'nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? 13 Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu. 14 Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli. 15 Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje? 16 Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo. 17 Basi Samweli akawakusanya watu mbele za Bwana huko Mispa 18 akawaambia wana wa Israeli, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea; 19 lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za Bwana, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu. 20 Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa.
 21 Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana. 22 Basi wakazidi kumwuliza Bwana, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye Bwana akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo. 23 Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu. 24 Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na Bwana, ya kuwa hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi! 25 Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za Bwana. Samweli akawaruhusu watu wote, waende kila mtu nyumbani kwake. 26 Sauli naye akaenda nyumbani kwake huko Gibea; na pamoja naye wakaenda kikosi cha watu, ambao Mungu alikuwa ameigusa mioyo yao. 27 Walakini wengine wasiofaa kitu wakasema, Huyu je! Atatuokoaje? Nao wakamdharau, wasimletee zawadi.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Huko zamani mtu mmoja tu alikuwa anatosha kumtangaza kiongozi aliyechaguliwa na Mungu kuongoza jumuiya ya kidini (kanisa) tofauti na sasa ambapo kazi hiyo inafanywa na kibaraza cha uchaguzi. Utaratibu huu wa zamani una faida na hasara zip? Je utaratibu huo inafaa kurejewa?
2. Je, kutiwa mafuta kulikofanywa kwa Sauli kunaweza kufananishwa na kuwekewa mikono kunakofanywa kwa wachungaji, wazee wa kanisa, na mashemasi leo hii? Kusudi la huduma hii ni nini?
3. Je, kuna uwezekano wa kutambua kitakachotokea katika ratiba yako ya siku husika hata kama wewe si nabii? Je Mungu yupo tayari kufanya hilo kwa kila mtu?
4. Ikiwa kila kinachotokea kilikuwa kimepangwa na Mungu nafasi ya mtu kufanya maamuzi yaliyo tofauti ipo wapi? Je mtu atawajibishwaje kwa kufanya yale yaliyopangwa na Mungu?
5. Sauli alipoanza kutabiri manabii walishikwa mshangao na kuanza kumkejeli. Tunawatia moyo kiasi gani wale wenye karama tulizonazo na wanaotamani kufikia viwango vya utendaji tulivyonavyo?
6. Sauli hakuwa na kiherehere cha kupenda uongozi au kujitangaza kama inavyotokea kwa baadhi yetu. Hata hivyo wapo wale ambao hawapokei kazi mpaka wabembelezwe. Unadhani Sauli alikuwa wa kundi gani? Unajifunza nini kutoka kwake?
7. Hotuba ya Samweli kwa Waisraeli ilionrsha Mungu ameafikiana na sherehe ya usimikwaji wa mfalme wa kwanza8 wa Israeli? Je Mungu alikuwa amezira? Matamko yale yalikuwa ya laana au baraka?
8. Kwa nini Sauli alipotambulishwa watu wote walipiga kelele za "mfalme aishi"? Waliridhika na nini kwa mtu huyu wa kabila ndogo ya Benjamini? Wale waliosema hawezi kutuokoa kwa nini wameitwa wasiofaa kitu? Ni kweli hawafai?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1SAMUELI 11:2-15    (16/06/2019)
1 Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni  ,akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi;na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi,na sisi tutakutumikia. 2 Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. 3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea. 4 Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. 5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi. 6 Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. 7 Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja. 8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu. 9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa. 10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema.
11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja. 12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue. 13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika Israeli. 14 Kisha Samweli akawaambia watu, Haya! Na twendeni mpaka Gilgali, ili tuuimarishe ufalme huko mara ya pili. 15 Nao watu wote wakaenda Gilgali; wakamtawaza Sauli mbele za Bwana huko Gilgali; wakachinja sadaka za amani mbele za Bwana; na huko Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Sifa ya kiongozi bora ni kuwa na uchungu na magumu yanayowakabili watu wako na kutafuta njia ya kuwatoa kwenye madhila hayo. Je hasira ni muhimu katika kufanikisha majukumu ya kiongozi?
2. Kwa nini wazee walitoa majibu kwa mfalme wa Amoni aliyetishia kuwang'oa jicho la kuume watu wote wa Israeli bila kumshirikisha mfalme wao Sauli? Je walikuwa hawana imani naye?
3. Waisraeli waliposikia taarifa za kung'olewa macho walilia sana. Je, kulia unapokuwa na matatizo kunatoa nafasi ya kupata ufumbuzi?
4. Ushindi wa kwanza wa Sauli kama mfalme wa Israeli uliimarisha kukubaliwa kwake. Je Sauli alijiinua kwa ushindi huu au alimtukuza Mungu?
5. Unapofanikiwa kama kiongozi sifa unazielekeza kwa nani? Je ushindi wako unathibitisha kuwa waliokuchagua hawakukosea au unathibitisha uwezo wa Mungu unaowainua wanyonge?
6. Je watu wanaobeza uwezo wako katika uongoze unawatendeaje wanapokwamisha juhudi zako au unapokuwa umepiga hatua ya mafanikio?
7. Unajifunza nini kuhusiana na namna Sauli alivyowatendea waliokuwa wanambeza?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 Samueli:12.1-25    (17/06/2019)
1 Kisha Samweli akawaambia Israeli wote, Angalieni, nimeisikiliza sauti yenu katika hayo yote mliyoniambia, nami nimemtawaza mfalme juu yenu. 2 Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo. 3 Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za Bwana, na mbele ya masihi wake,nalitwaa ng`ombe wa nani? au nalitwaa punda wa nani? au ni nani niliye mdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi. 4 Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote. 5 Akawaambia, Bwana ni shahidi juu yenu, na masihi 6 Samweli akawaambia watu, Ni yeye Bwana aliyewaweka Musa na Haruni, ndiye yeye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri. 7 Basi sasa simameni, ili niwahutubie mbele za Bwana, kwa kutaja matendo yote ya haki ya Bwana, aliyowatendea ninyi na baba zenu. 8 Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia Bwana, ndipo Bwana akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa. 9 Lakini wakamsahau Bwana, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao. 10 Nao wakamlilia Bwana, wakasema, Tumefanya dhambi, kwa kuwa tumemwacha Bwana, na kuwatumikia Mabaali na Maashtorethi; lakini sasa utuokoe na mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia wewe. 11 Bwana akawatuma Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama. 12 Hata mlipomwona Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, amekuja kupigana nanyi, mliniambia, Sivyo, lakini mfalme atatutawala; ingawa Bwana, Mungu wenu, ni mfalme wenu. 13 Basi sasa, mtazameni mfalme mliyemchagua na kumtaka; tazameni, Bwana ameweka mfalme juu yenu. 14 Kama mkimcha Bwana, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya Bwana, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata Bwana, Mungu wenu, vema! 15 Bali msipoisikia sauti ya Bwana, mkiiasi amri ya Bwana, ndipo mkono wa Bwana utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu. 16 Na sasa simameni, mkalione jambo hili kubwa, Bwana atakalolitenda mbele ya macho yenu. 17 Leo je! Si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana, kwamba apeleke ngurumo na mvua; nanyi mtajua na kuona ya kuwa uovu wenu ni mwingi sana, mlioufanya machoni pa Bwana, kwa kujitakia mfalme. 18 Basi Samweli akamwomba Bwana, naye Bwana akapeleka ngurumo na mvua siku ile; nao watu wote wakamwogopa Bwana sana, na Samweli pia. 19 Watu wote wakamwambia Samweli, Utuombee sisi watumwa wako kwa Bwana, Mungu wako, tusije tukafa; maana tumeongeza dhambi zetu zote kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme. 20 Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote. 21 Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili, 22 visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza Bwana kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe. 23 Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka 24 Mcheni Bwana tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu. 25 Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Kufanya tathmini ya uongozi wako kama Samweli (1 Sam. 12:3-4) na Yesu (Mathayo 16:15-16) ni jambo linalosaidia kutambua mapungufu yako kwa lengo la kuyaboresha au kupima mafanikio yako. Unadhani jambo hilo lina msaada katika wakati wetu?
2. Utaratibu wa kuachiana majukumu unataka kuwepo mwendelezo wa kazi bora zilizokuwa zinafanyika na kutengeneza mazingira bora ya kazi kwa anayeachiwa kijiti. Je katika mazingira unayoishi jambo hili linafanyika kwa ufanisi? Je kunakuwepo na makabidhiano yenye upendo na ari ya kumsaidia aliyepokea kijiti?
3. Kwa nini Samweli aliamua kuwakumbusha Israeli matendo yote ya Mungu katika nyakati zilizopita katika hotuba yake wakati anakaribia kufa?
4. Ahadi kwa Israeli kuwa "Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu" inasikikaje masikioni mwako wewe unayepitia sasa changamoto za maisha? Je waweza kuidai ahadi hiyo?
5. Kuacha kuwaombea watu wa Mungu kwa mujibu wa Samueli ni dhambi. Unachukua nafasi gani kuwaombea watu wa Mungu maishani mwako?
6. Wanadamu wa leo wamejiundia mifumo fulani ya kuliongoza kanisa la Mungu iliyojikita katika ukabila na ukanda ambapo hujenga misimamo ya kikanisa kutegemeana na tamaduni na mazoea ya makabila yao. Dhambi hii ni sawa na dhambi ya Israeli waliojichagulia mfalme na kumweka kando Mungu wa mbinguni? Jambo hili linahafifishaje kazi ya Mungu?
7. Neno la mwisho la Samweli kwa Israeli ni kuwa "mkiendelea kutenda mabaya mtaangamia". Umelipokeaje onyo hili ambalo linakuja kwako leo. Utakuwa tayari kushirikiana naye ili kukomesha matendo ya dhambi maishani mwako?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 Samueli 14:1-52    (19/06/2019)
1 Sauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha hapo alipoanza kutawala;naye akatawala miaka kadha wa kadha juu ya Israeli. 2 Naye Sauli alijichagulia watu elfu tatu wa Israeli; ambao katika hao, elfu mbili walikuwa pamoja na Sauli katika Mikmashi, na katika mlima wa Betheli na elfu moja pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini; nao wale watu waliosalia akawaruhusu waende kila mtu hemani kwake. 3 Yonathani akaipiga hiyo ngome ya Wafilisti, iliyokuwako huko Gibea, nao Wafilisti wakapata habari. Naye Sauli akapiga tarumbeta katika nchi yote, huku akisema, Na wasikie Waebrania. 4 Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali. 5 Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni. 6 Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wa katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika. 7 Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa akaliko huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka. 8 Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye. 9 Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. 10 Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. 11 Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi; 12 basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za Bwana; kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa. 13 Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. 14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye Bwana amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile Bwana alilokuamuru. 15 Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wapata kama mia sita. 16 Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi. 17 Nao watekaji wa nyara wakatoka katika marago ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali; 18 na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika. 19 Basi, hakuonekana mhunzi ye yote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajifanyizia panga au mikuki; 20 lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake; 21 ila walikuwa na tupa za kunolea sululu, na miundu, na mauma, na mashoka; na kwa kuinoa michokoo. 22 Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu ye yote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo. 23 Na jeshi la Wafilisti wakatoka hata mwanya wa Mikmashi.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Kitendo cha Yonathani kuwavukia maadui zao Wafilisti bila kumjulisha mfalme Sauli kilikuwa kitendo cha kishujaa chenye nia ya kusaidia ufalme wa baba yake au kilikuwa kitendo cha uasi?
2. Kitendo cha Sauli kutaka kumwangamiza Yonathani kilitokana na aibu ya kutoshirikishwa na maamuzi ya kushambulia Wafilisti na kutojibiwa kwa maombi yake au kulikuwa na nia ya kuzuia hasira ya Mungu isiwaangukie Israeli yote? Kwa nini Waisraeli walikataa mpango huo?
3. Kwa nini Yonathani alikuwa tayari kuuawa? Alihisi kuwa ana hatia?
4. Idadi ya watu haijalishi katika kuleta ushindi. Jeshi kubwa la Wafilisti lenye zana bora lilishindwaje na jeshi la watu wawili; Yonathani na mchukua silaha wake?
5. Je sheria ya kuzuia watu wasile siku ya ushindi wa vita ilikuwa ni ya lazima? Je inafaa kufunga siku ya Sabato?
6. Je ushindi dhidi ya Wafilisti waliowatia hofu Waisraeli ulitokana na Sauli, au Yonathani?
7. Je ni sahihi kumkatalia mtawala anapoonesha nia ya kuonea baadhi ya raia wake hata kama kwa kufanya hivyo utakuwa unahatarisha maisha yako?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 15:1-35     (20/06/2019)
1 Wakati huo Samweli akamwambia Sauli, Bwana alinipeleka nikutie mafuta, uwe mfalme wa watu wake Israeli; basi sasa, isikilize sauti na maneno ya Bwana. 2 Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri. 3 Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda. 4 Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu. 5 Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni. 6 Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki. 7 Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri. 8 Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga. 9 Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng'ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa. 10 Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema, 11 Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha. 12 Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali. 13 Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na Bwana, nimeitimiza amri ya Bwana. 14 Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng'ombe ninaousikia? 15 Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng'ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa. 16 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema. 17 Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. 18 Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia. 19 Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana? 20 Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. 21 Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali. 22 Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. 23 Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme. 24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao. 25 Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana. 26 Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli. 27 Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka. 28 Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe. 29 Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute. 30 Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu Bwana, Mungu wako. 31 Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu Bwana. 32 Ndipo Samweli akasema, Nileteeni hapa Agagi, mfalme wa Waamaleki. Basi Agagi akamwendea kwa utepetevu. Naye Agagi akasema, Bila shaka uchungu wa mauti umeondoka. 33 Lakini Samweli akamjibu, Kama upanga wako ulivyofanya wanawake kufiwa na watoto wao, vivyo hivyo mama yako atafiwa miongoni mwa wanawake. Basi Samweli akamkata Agagi vipande mbele za Bwana huko Gilgali. 34 Na baada ya hayo Samweli akaenda zake kule Rama; naye Sauli akakwea kwenda nyumbani kwake huko Gibea ya Sauli. 35 Wala Samweli hakuenda tena kuonana na Sauli hata siku ya kufa kwake; lakini Samweli alikuwa akimlilia Sauli; naye Bwana akaghairi ya kuwa amemtawaza Sauli awe mfalme juu ya Israeli.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Mungu anafahamu wakati ni njia bora ya kulipiza kisasi cha wale wanaotuonea. Kwa nini kwa kawaida mwanadamu huwa haruhusu Mungu alipize kisasi kwa niaba yake?
2. Kwa nini Sauli aliona vigumu kukiri kuwa hakuitii sauti ya Mungu? Je angekiri asingesamehewa? Kwa nini watu wengi wanapofanya makossa hupenda waonekane walikuwa na nia njema?
3. Kumleta Agagi mfalme akiwa hai Yerusalemu wakati aliagizwa amuangamize kulikuwa na faida kwa nani? Je tunapofanya kazi ya Mungu kuna uwezekano wa kutafuta sifa?
4. Je ile mifugo ambayo Mungu aliagiza iteketezwe isingefaa kwa kutolea kafara? Unadhani ilikuwa inakidhi vigezo vya kafara?
5. Je, kukataa neno la Mungu ni sawa na kumkataa Mungu?
6. Kama Mungu si mwanadamu hata ajute (1 Samwel 15:29), ilikuwaje katika (1 Samwel 15:11), anasema najuta kumtawaza Sauli kuwa mfalme?
7. Je kunahitajika ujasiri kuwakabili watu waliozoea kulitesa kanisa la Mungu? Je watu hao wanahitaji huruma yoyote?
8. Mungu aliagiza Waamaleki wauawe kutokana na ubaya waliowafanyia Waisraeli huko zamani. Je ujumbe huu una faraja ye yote kwako wewe unayeonewa sasa na Mungu kuonekana kana kwamba hachukui hatua ye yote?Kwa nini kuangamizwa kwa Waamaleki kuliandamana na kuharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo hata vile vyenye matumizi katika maisha? Huu si uharibifu wa mali?
9. Unadhani kwa nini Sauli alimwacha Agagi hai wakati alitakiwa amwangamize? Alimuonea huruma?
10. Kutofikia kwetu mafanikio ya juu katika nyanja mbalimbali kunaweza kuwa kunatokana na kutozingatia maagizo ya Mungu? Ni mazoea au mahusiano gani ya dhambi ambayo hujayaacha yanayohatarisha hali yako ya kiroho?
11. Kwa nini Sauli alisema 'nimeitimiza sauti ya Mungu' wakati akijua hajafanya hivyo? Kwa nini baadaye alikiri na kusema 'nimefanya dhambi kwa kuihalifu amri ya Bwana'?
12. Je ni vizuri kwa kiongozi kufanya maamuzi kwa lengo la kufurahisha watu? Ni nini hatari ya kufanya hivyo?
13. Kwa nini kuasi kunalinganishwa na dhambi ya uchawi na ukaidi unalinganishwa na  ukafiri? Je unaweza kufanya vitu vya maendeleo kwa taasisi unayoiongoza na bado ukaonekana hufai?
14. Je Sauli alikuwa na toba ya kweli? Kwa nini alichana vazi la kuhani? Ilitakiwa afanye nini kama kuhani alionesha kutaka kuondoka wakati yeye akiwa bado anahitaji msaada wake?
15. Ni mambo gani umepanga kuyaangamiza ambayo yamekuwa yakizuia ukuaji wako kiroho? Je unahitaji msaada wa Mungu kuyaangamiza?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 16:1-23    (21/06/2019)
1 Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. 2 Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. 3 Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako. 4 Samweli akafanya hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? 5 Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu. 6 Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. 7 Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. 8 Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu. 9 Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu. 10 Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. 11 Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. 12 Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. 13 Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. 14 Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua. 15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. 16 Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. 17 Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee. 18 Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye Bwana yu pamoja naye. 19 Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo. 20 Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. 21 Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake. 22 Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. 23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Ikiwa kiongozi ameonekana kutoyamudu majukumu yake inafaa kumuondoa kabla ya muhula wake? Je kufanya hivyo hakuwezi kuhatarisha maisha ya yule anayejaribu kumuondo?
2. Je ushauri kuwa mfalme Sauli anahitaji mtu wa kumpa tiba ya kiroho itakayomsaidia kumweka sawa kiafya ulikuwa sahihi? Je, Sauli alikuwa anasumbuliwa na kichaa, mapepo, au msongo wa mawazo?
3. Je hii kazi mpya ya Daudi iliyompeleka ikulu ilikuwa fursa ya kujifunza utawala na maisha kama maandalizi ya kazi yake katika siku za usoni?
4. Sauli aliendelea kufanya kazi ya Mungu huku amekataliwa na nafasi yake kupewa mtu mwingine? Kuna uwezekano wa leo kuwepo watu wanaodhani wanamfanyia Mungu kazi na kumbe walishakataliwa kitambo?
5. Kwa nini Daudi hakuingia ikulu mara tu baada ya kutawazwa?
6. Daudi alijisikiaje kufanya kazi ya kumtumbuiza mfalme wakati akijua yeye ndiye mfalme aliyetawazwa na anayekubalika na Mungu?
7. Daudi alipata kibali kwa Mungu na kwa mfalme Sauli bila jitihada za wazi za kujipendekeza au kutafuta fursa hizo kama inavyofanywa na watu wengine? Ni nini siri ya kukubalika kwake?
8. Viongozi wanahitaji washauri wema watakaowasaidia kuhimili mikiki mikiki ya uongozi inayoweza kuwapatia msongo watakaomshauri cha kufanya ili kulinda afya yake? Je huduma hiyo inafanyika kwa ufanisi katika taasisi za kidini na taasisi zinginezo? Je, machapleini wenye mafunzo ya huduma hii wanapewa kipaumbele?
9. Kwa nini uteuzi wa Daudi na kutiwa mafuta kwake kulifanywa kwa kificho na kwa kutunga sababu za uongo? Nini kingetokea kama ingefanyika kwa wazi?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 17:1-58    (22/06/2019)
1 Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. 2 Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. 3 Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. 4 Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. 5 Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. 6 Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. 7 Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. 8 Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. 9 Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. 10 Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. 11 Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana. 12 Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu. 13 Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake Abinadabu, na wa tatu Shama. 14 Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli. 15 Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu. 16 Naye yule Mfilisti hukaribia asubuhi na jioni, akajitokeza siku arobaini. 17 Ndipo Yese akamwambia Daudi mwanawe, Haya! Sasa uwachukulie ndugu zako efa ya bisi, na mikate hii kumi, ipeleke upesi kambini kwa ndugu zako; 18 ukampelekee akida wa elfu yao jibini hizi kumi, ukawaangalie, wa hali gani, kisha uniletee jawabu yao. 19 Basi Sauli, na watu wote wa Israeli, walikuwa katika bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti. 20 Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita. 21 Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili. 22 Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake. 23 Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia. 24 Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana. 25 Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli. 26 Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? 27 Nao watu wakamjibu vivyo hivyo, wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua. 28 Naye Eliabu, mkubwa wake, alisikia hapo alipoongea na watu; na hasira yake Eliabu ikawaka juu ya Daudi, akasema, Mbona wewe umeshuka hapa? Na kondoo wale wachache umemwachia nani kule nyikani? Mimi nakujua kiburi chako, na ubaya wa moyo wako; maana umeshuka ili upate kuvitazama vita. 29 Naye Daudi akamjibu, Je! Mimi nimekosa nini sasa? Je! Si neno kubwa hilo? 30 Naye akamgeukia ili kumwelekea mtu mwingine, akasema naye jinsi ile ile; na watu wakamjibu tena jinsi ile ile kama ya kwanza. 31 Na maneno hayo aliyosema Daudi yaliposikiwa, watu wakamweleza Sauli; naye akatuma mtu kwenda kumwita. 32 Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu. 33 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake. 34 Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, 35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. 36 Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai. 37 Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe. 38 Ndipo Sauli akamvika Daudi mavazi yake ya vita, akamtia chapeo cha shaba kichwani, akamvika dirii. 39 Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua. 40 Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti. 41 Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. 42 Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. 43 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. 44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. 45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. 46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. 48 Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. 49 Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. 50 Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. 51 Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia. 52 Nao watu wa Israeli na wa Yuda wakainuka, na kupiga kelele, nao wakawafuata Wafilisti mpaka ufikapo Gathi, na mpaka malango ya Ekroni. Nao majeruhi wa Wafilisti wakaanguka kando ya njia iendayo Shaarimu, mpaka Gathi, na mpaka Ekroni. 53 Kisha wana wa Israeli wakarudi kutoka katika kuwafukuza Wafilisti, wakateka nyara marago yao. 54 Naye Daudi akakitwaa kichwa chake yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu; lakini silaha zake akaziweka hemani mwake. 55 Basi Sauli, hapo alipomwona Daudi akitoka ili kumwendea yule Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, Je! Abneri, kijana huyu ni mwana wa nani? Abneri akamjibu, Ee mfalme, kama iishivyo roho yako, mimi siwezi kusema. 56 Basi mfalme akasema, Uliza wewe, kijana huyu ni mwana wa nani. 57 Hata na Daudi alipokuwa yuarudi kutoka katika kumwua yule Mfilisti, Abneri alimtwaa, akamleta mbele ya Sauli, naye anacho kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake. 58 Basi Sauli akamwuliza, Wewe, kijana, u mwana wa nani? Naye Daudi akamjibu, Mimi ni mwana wa mtumishi wako, Yese, mtu wa Bethlehemu.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Kwa nini maneno 'nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane isipokuwa kijana mdogo asiye na jukumu lolote katika jeshi. Je mfalme Sauli na Abneri mkuu wake wa majeshi walizipokeaje kejeli hizo?
2. Je ni wakati gani unatakiwa kumtetea Mungu na wakati gani anatakiwa ajitetee mwenyewe?
3. Kwa nini kaka zake Daudi walijaribu kumkatisha tamaa mdogo wao Daudi asifikirie kupambana na Goliath? Waliridhika na dharau wanayofanyiwa Israeli, walitaka kuokoa maisha ya mdogo wao, au walimwonea wivu?
4. Wajibu wa raia mwema kwa kiongozi aliyekata tamaa ni upi kukaa kimya, kumsema pembeni, au kumtia moyo?
5. Jina la Bwana laweza kuwa silaha vitani? Daudi alijuaje kuwa katika vita ile angeibuka mshindi?
6. Yule ambaye Mungu amemuandaa kuleta ushindi kwa familia, kanisa, na kwa taifa anaweza asishawishi watu kwa mwonekano. Mtu kama huyo anatakiwa afanye nini ili wenzake wajue yeye ndiye chaguo la Mungu?
7. Unadhani ushindi wa Daudi uliwafurahisha watu wote wa Israeli. Tahadhari gani unatakiwa kuchukua baada ya Mingu kuruhusu ushindi kupitia kwako?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 18:1-30    (23/06/2019)
1 Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. 2 Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. 3 Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. 4 Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. 5 Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia. 6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. 7 Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. 8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? 9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. 10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. 11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. 12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. 13 Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. 14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye. 15 Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. 16 Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao. 17 Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya Bwana. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake. 18 Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme? 19 Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi. 20 Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza. 21 Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu. 22 Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme. 23 Nao watumishi wa Sauli wakanena maneno hayo masikioni mwa Daudi. Daudi akasema, Je! Ninyi mwaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo? 24 Na hao watumishi wa Sauli wakampasha habari, wakisema, Ndivyo hivyo alivyosema Daudi. 25 Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yo yote, ila anataka govi mia za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti. 26 Na watumishi wake walipomwambia Daudi; maneno hayo, ilimpendeza Daudi sana kuwa mkwewe mfalme. Na siku zilikuwa hazijaisha bado; 27 basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake. 28 Sauli akaona na kutambua ya kwamba Bwana alikuwa pamoja na Daudi; na huyo Mikali, binti Sauli, akampenda. 29 Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; Sauli akawa adui yake Daudi sikuzote. 30 Wakati huo wakuu wa Wafilisti wakatoka; kisha ikawa, kila mara walipotoka, Daudi akatenda kwa busara zaidi ya watumishi wote wa Sauli hivyo jina lake likawa na sifa kuu.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Kwa nini Yonathani hakuona umaarufu wa Daudi kuwa tishio kwa nafasi yake ya mrithi wa kitu cha ufalme? Je aliridhika Daudi awe maarufu kuliko yeye?
2. Kwa nini Daudi anaonekana kufanikiwa kwenye kila eneo alilotumika? Hii ni kwa sababu Mungu alimpendelea au kwa kuwa alijituma na kutumia fursa vizuri?
3. Je wanawake walioimba walijua sifa wanazompa Daudi zinamchonganisha na mfalme Sauli? Je busara ilihitajika katika kumsifu Sauli? Unapokuwa na kiongozi anayependa yeye tu ndiye asifiwe mnafanyaje?
4. Je ilikuwa sahihi kwa Daudi aliye maskini na asiyekubalika kwa mfalme kumuoa binti wa mfalme? Ukipendwa na binti kutoka familia tajiri na wewe ni maskini utafanyaje? Je utaratibu wa kutoza mahari kwa namna ulivyofanywa na Sauli na namna unavyofanyika leo ni sahihi?
5. Kwa nini mfalme alimuogopa Daudi ambaye ni raia asiye na madaraka ye yote na kwa nini Daudi hakumuogopa Sauli?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUEL 18:1-30    (23/06/2019)
1 Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. 2 Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. 3 Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. 4 Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. 5 Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia. 6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. 7 Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. 8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? 9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. 10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. 11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. 12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu Bwana alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. 13 Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. 14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye Bwana alikuwa pamoja naye. 15 Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. 16 Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao. 17 Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya Bwana. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake. 18 Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme? 19 Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi. 20 Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza. 21 Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu. 22 Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme. 23 Nao watumishi wa Sauli wakanena maneno hayo masikioni mwa Daudi. Daudi akasema, Je! Ninyi mwaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo? 24 Na hao watumishi wa Sauli wakampasha habari, wakisema, Ndivyo hivyo alivyosema Daudi. 25 Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yo yote, ila anataka govi mia za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti. 26 Na watumishi wake walipomwambia Daudi; maneno hayo, ilimpendeza Daudi sana kuwa mkwewe mfalme. Na siku zilikuwa hazijaisha bado; 27 basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake. 28 Sauli akaona na kutambua ya kwamba Bwana alikuwa pamoja na Daudi; na huyo Mikali, binti Sauli, akampenda. 29 Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; Sauli akawa adui yake Daudi sikuzote. 30 Wakati huo wakuu wa Wafilisti wakatoka; kisha ikawa, kila mara walipotoka, Daudi akatenda kwa busara zaidi ya watumishi wote wa Sauli hivyo jina lake likawa na sifa kuu.
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 19:1-24   (24/06/2019)
1 Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. 2 Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; 3 na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lo lote nitakuambia. 4 Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. 5 Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure? 6 Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa. 7 Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza. 8 Baada ya hayo kulikuwa na vita tena; naye Daudi akatoka, naye akapigana na Wafilisti, naye akawaua kwa uuaji mkuu; nao wakakimbia mbele yake. 9 Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa Bwana ilimjilia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake. 10 Sauli akajaribu kumpiga Daudi hata ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule. 11 Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa. 12 Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka. 13 Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo. 14 Naye Sauli alipotuma wajumbe ili kumkamata Daudi, yeye alisema, Hawezi. 15 Basi Sauli akawatuma hao wajumbe ili wamtazame Daudi, akisema, Mleteni kwangu juu ya kitanda chake, nipate kumwua. 16 Nao wajumbe walipoingia, kumbe! Kuna kinyago kitandani, na mto wa singa za mbuzi kichwani pake! 17 Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue? 18 Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi. 19 Naye Sauli akaambiwa, kusema, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama. 20 Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, roho ya Mungu ikawajilia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri. 21 Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri. 22 Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kunako kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama. 23 Basi akaenda Nayothi huko Rama, na roho ya Mungu ikamjilia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama. 24 Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu husema, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Ungejihisi vipi kuwa na rafiki anayekusema vizuri kwa adui zako na aliye tayari kukujulisha njama zinazopangwa kinyume chako? Unafanyaje kuwa na marafiki wa jinsi hiyo?
2. Je kipi kinakupatia maadui zaidi kati ya kutenda mema na kutenda mabaya?
Kwa nini watu wengine wanapomchukia mtu kile wanachofikiria ni kumuua tu? Je kuua kunaweza kuwa ufumbuzi wa usumbufu wanaoupata kuhusu mtu huyo?
3. Kwa nini Mikali mkewe Daudi na binti wa Sauli alikubali kuhatarisha maisha yake kwa kumuokoa Daudi na kumdanganya baba yake. Je upendo wa mume na mke una nguvu kuliko upendo wa mtu na wazazi wake?
4. Kwa nini Samueli baada ya kushitakiwa na Daudi juu ya vitendo vya Sauli na nia yake ya kutaka kumuua hakwenda kwa Sauli kumuonya kama alivyokuwa akifanya huko nyuma?
5. Kwa nini kila jitihada za kumkamata Daudi zilipokuwa zinagonga ukuta hazikumshitua Sauli kuwa Daudi hakuwa na hatia na ya kwamba haukuwa mpango wa Mungu afe?
6. Kwa nini Sauli tofauti na wenzake wengine wote alitabiri akiwa amelala uchi mchana kutwa na usiku kucha? Unadhani ilikuwa sahihi kwa kiongozi kumuandama raia wake asiye na hatia bali anayeonekana kuwa tishio kwake?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 Samueli 20:1-42     (25/06/2019)
1 Kisha Daudi akatoka Nayothi huko Rama, akakimbia, akaenda kwa Yonathani, akasema mbele yake, Nimefanya nini? Uovu wangu ni nini? Dhambi yangu mbele ya baba yako ni nini, hata akaitaka roho yangu? 2 Naye akamwambia, Hasha! Hutakufa; angalia, baba yangu hatendi neno kubwa wala dogo bila kuifunulia mimi, na baba yangu ana sababu gani ya kunificha jambo hili? Sivyo usemavyo. 3 Daudi akaapa, akasema, Baba yako anajua sana ya kuwa nimeona kibali machoni pako, naye asema, Yonathani asilijue neno hili, asije akahuzunika; lakini ni kweli, aishivyo Bwana, na iishivyo roho yako, iko hatua moja tu kati ya mimi na mauti. 4 Ndipo Yonathani akamwambia Daudi, Kadiri roho yako itakavyo, nitakutendea. 5 Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni. 6 Baba yako akiona ya kuwa sipo basi sema, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa, aende upesi Bethlehemu, mji wake, kwa maana iko huko dhabihu ya mwaka kwa ajili ya jamaa yake yote. 7 Basi, akisema, Ni vema, mimi mtumishi wako nitakuwa na amani; bali akikasirika, ujue ya kuwa amekusudia kutenda jambo baya. 8 Basi, unitendee mema mimi mtumishi wako; kwa sababu umenitia mimi mtumishi wako katika agano la Bwana pamoja nawe, lakini ikiwa mna uovu moyoni mwangu, uniue wewe mwenyewe; kwa nini kunileta kwa baba yako? 9 Naye Yonathani akasema, Haya na yawe mbali nawe, kwa maana kama ningejua ya kuwa baba yangu amekusudia kukutenda neno baya, je! Singekuambia? 10 Basi Daudi akamwambia Yonathani, Ni nani atakayeniambia, ikiwa baba yako amekujibu maneno makali? 11 Yonathani akamwambia Daudi, Twende zetu nje mashambani. Wakatoka wote wawili, wakaenda mashambani. 12 Naye Yonathani akamwambia Daudi, Bwana, Mungu wa Israeli, na awe shahidi; nitakapokuwa nimekwisha kumwuliza baba yangu, kama wakati huu kesho, au siku ya tatu, angalia, kama liko neno jema la kumfaa Daudi, je! Nisikupelekee habari na kukufunulia neno hili? 13 Bwana anitende mimi, Yonathani, hivyo, na kuzidi, ikiwa yampendeza babangu kukutenda mabaya, nisipokufunulia haya, na kukupeleka uende zako kwa amani; na Bwana awe pamoja nawe, kama alivyokuwa pamoja na baba yangu. 14 Nawe utanionyesha fadhili za Bwana, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai; 15 lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule Bwana atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi. 16 Basi Yonathani akafanya agano na jamaa yake Daudi, akisema, Bwana naye atayataka mkononi mwa adui zake Daudi. 17 Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho yake mwenyewe. 18 Kisha Yonathani akamwambia, Kesho ni mwandamo wa mwezi, nawe utakosekana, kwa sababu kiti chako kitakuwa hakina mtu. 19 Nawe ukiisha kungoja siku tatu, shuka upesi ufike kuko huko ulikojificha, siku ya shughuli ile; nawe kaa karibu na kile kichuguu kule. 20 Nami nitapiga mishale mitatu kando-kando yake, kana kwamba ninapiga shabaha. 21 Kisha, angalia, nitamtuma mtoto na kumwambia, Nenda ukaitafute mishale. Hapo nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko upande wako huu, itwae; basi uje, maana iko amani kwako, wala hapana hatari, Bwana aishivyo. 22 Bali nikimwambia yule mtoto, Tazama, mishale iko huko mbele yako; basi enenda zako, kwa maana Bwana amekuamuru uende zako. 23 Na kwa habari ya neno lile tulilonena, wewe na mimi, angalia Bwana yu kati ya wewe na mimi milele. 24 Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula. 25 Mfalme aliketi kitini mwake kama sikuzote, katika kiti kilichokuwa karibu na ukuta; Yonathani alikuwa mbele yake; Abneri naye akaketi karibu na Sauli; lakini mahali pake Daudi palikuwa hapana mtu. 26 Lakini Sauli hakusema neno siku ile; maana alidhani ya kuwa, Amepatikana na neno, hakutakata; hakosi yeye hakutakata. 27 Hata siku ya pili baada ya mwandamo wa mwezi, mahali pake palikuwa hapana mtu; basi Sauli akamwambia Yonathani mwanawe, Mbona mwana wa Yese haji kula chakula, jana wala leo? 28 Naye Yonathani akamjibu Sauli, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu; 29 akasema, Tafadhali nipe ruhusa niende; kwa maana jamaa yetu wana dhabihu mjini mwetu; na ndugu yangu ameniamuru niende; basi sasa, kama nimeona kibali machoni pako, nakuomba, niondoke; nikawatazame ndugu zangu. Ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme. 30 Basi hasira yake Sauli ikawaka juu ya Yonathani, akamwambia, Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! Mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana wa Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako. 31 Maana wakati mwana wa Yese akiwa hai juu ya nchi, wewe hutafanikiwa, wala ufalme wako. Basi, sasa peleka, ukamlete kwangu, maana hakika yake atakufa huyu. 32 Yonathani akamjibu Sauli, baba yake, akamwambia, Auawe kwa sababu gani? Amefanya nini? 33 Sauli akamtupia mkuki wake ili kumpiga; basi Yonathani akajua ya kuwa baba yake ameazimu kumwua Daudi. 34 Basi Yonathani akaondoka pale mezani, mwenye hasira kali, wala hakula chakula siku ya pili ya mwezi, kwa sababu alimhuzunikia Daudi sana, na kwa sababu baba yake amemwaibisha. 35 Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye. 36 Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake. 37 Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako? 38 Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake. 39 Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe. 40 Naye Yonathani akampa mtoto silaha zake, akamwambia, Nenda, ukazichukue mjini. 41 Basi mara alipokuwa amekwisha ondoka yule mtoto, mara Daudi akatoka mahali pale karibu na kile kichuguu, akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi. 42 Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la Bwana ya kwamba, Bwana atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele. Daudi akaondoka, akaenda zake; Yonathani naye akaenda zake mjini.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Unazungumziaje urafiki wa Yonathani na Daudi? Unaye rafiki wa namna hiyo maishani?
2. Yesu aliyatoa maisha yake ili mimi na wewe tupone. Je una mpango wa kumfanya rafiki yako wa kudumu?
3. Utafanyaje ukigundua ndugu zako wanafanya njama za kumwangamiza rafiki yako ili kulinda nafasi yako ya ajira?
4. Utafanyaje utakapogundua watu fulani wanaojifanya wanakupenda sana kumbe wanapanga njama juu yako?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 21:1-15    (26/06/2019)
1 Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwani wewe kuwa peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe? 2 Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani. 3 Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au cho chote ulicho nacho hapa. 4 Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya sikuzote chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake. 5 Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi? 6 Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za Bwana, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa. 7 Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za Bwana jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli. 8 Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka. 9 Yule kuhani akasema, upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe. 10 Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. 11 Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake. 12 Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. 13 Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. 14 Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? 15 Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Unadhani Daudi alijihisi vipi kuona kuna kiongozi anayetambua umuhimu wake na mchango wake kwa taifa? Je kuna haja ya kumtambua na kujaribu kumhifadhi kiongozi asiyekubalika na kiongozi mkuu kwa chuki binafsi zisizo na maslahi kwa taasisi yenu?
2. Je Daudi na wenzake (ambao hawakuwa makuhani) walikuwa na sifa ya kuila ile mikate ya wonyesho? Pakiwa na mtu aliye katika hatari ya kufa kwa kukosa chakula naweza kumpa mikate iliyobaki kwenye Meza ya Bwana?
3. Kujitenga na wanawake (kutotenda ngono) ilikuwa sharti mojawapo la kushiriki ibada inayohusisha mikate ya wonyesho. Je hii ni kumaanisha wanawake ni najisi? Je sheria hii ipo leo au imekoma?
4. Upanga wa Goliati ulihifadhiwa kama kumbukumbu za kihistoria kwa ajili ya vizazi vijavyo. Unadhani tunafanya jitihada za kutosha kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria za kanisa letu? Nini kifanyike ili kumbukumbu hizo zisipotee?
5. Je katika kukabiliana na adui kuna wakati mbinu ya Daudi ya kujifanya kichaa huwa ni ya lazima? Yesu aliposema kuweni wapole kama huwa na werevu kama nyoka alimaanisha hiki alichokifanya Daudi.
7. Ukiwa vitani na ukajivika majani ili adui asikutambue utakuwa unafanya dhambi ya kudanganya?
 
USOMAJI BIBLIA KWA MPANGO:
1 SAMUELI 22:1-23     (27/06/2019)
1 Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. 2 Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne. 3 Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu. 4 Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni. 5 Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, Usikae hapa ngomeni; ondoka, ukaende mpaka nchi ya Yuda. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda zake, akakaa katika msitu wa Herethi. 6 Kisha Sauli akasikia ya kwamba Daudi ameonekana, na wale watu waliokuwa pamoja naye. Basi Sauli alikuwa akikaa Gibea, chini ya mkwaju katika mahali palipoinuka, naye alikuwa na mkuki wake mkononi, na watumishi wake wote wakimzunguka. 7 Naye Sauli akawaambia watumishi wake waliomzunguka, Sikieni sasa, enyi Wabenyamini; je! Huyu mwana wa Yese atawapa ninyi kila mmoja mashamba, na mashamba ya mizabibu, atawafanya kuwa maakida wa watu elfu, na maakida wa watu mia; 8 hata ninyi nyote mkafanya fitina juu yangu, wala hapana mtu anifunuliaye habari hii mwanangu afanyapo agano na mwana wa Yese, wala hapana mmoja wenu anayenisikitikia, wala kunifunulia ya kuwa mwanangu amemwondokesha mtumishi wangu juu yangu, anivizie kama hivi leo? 9 Ndipo akajibu Doegi, Mwedomi, aliyesimama karibu na watumishi wa Sauli, akasema, Mimi nalimwona mwana wa Yese akienda Nobu, kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu. 10 Naye akamwuliza Bwana kwa ajili yake, akampa vyakula, akampa na ule upanga wa Goliathi, Mfilisti. 11 Ndipo mfalme akatuma watu waende kumwita Ahimeleki, kuhani, mwana wa Ahitubu, na jamaa yote ya baba yake, hao makuhani, waliokuwako huko Nobu; nao wakaenda kwa mfalme wote pia. 12 Sauli akasema, Sikia sasa, Ewe mwana wa Ahitubu. Naye akaitika, Mimi hapa, bwana wangu. 13 Sauli akamwuliza, Mbona mmefanya fitina juu yangu, wewe na mwana wa Yese? Kwa maana umempa mikate, na upanga, nawe umemwuliza Mungu kwa ajili yake, ili aniondokee na kunivizia kama hivi leo? 14 Basi Ahimeleki akamjibu mfalme, akasema, Katika watumishi wako wote ni nani aliye mwaminifu kama Daudi, aliye mkwewe mfalme, tena msiri wako, mwenye heshima nyumbani mwako? 15 Je! Mimi nimeanza leo tu kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hasha! Mfalme asinidhanie mimi, mtumishi wake neno hili, Wala jamaa yote ya baba yangu, kwa maana mimi, mtumishi wako siyajui hayo yote, yaliyopungua au yaliyozidi. 16 Naye mfalme akasema, Kufa utakufa, Ahimeleki, wewe na jamaa yote ya baba yako. 17 Kisha mfalme akawaambia askari walinzi waliosimama karibu naye Geukeni, mkawaue hao makuhani wa Bwana, kwa sababu mkono wao u pamoja na Daudi, na kwa sababu walijua ya kuwa amekimbia, wasiniarifu. Lakini watumishi wa mfalme walikataa kunyosha mkono na kuwaangukia makuhani wa Bwana. 18 Basi mfalme akamwambia Doegi, Geuka wewe, ukawaangukia hao makuhani. Basi Doegi, Mwedomi, akageuka, akawaangukia makuhani, akaua siku ile watu themanini na watano wenye kuvaa naivera ya kitani. 19 Kisha akaupiga Nobu, mji wa makuhani, kwa makali ya upanga, wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, na ng'ombe, na punda, na kondoo. 20 Na katika wana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akaokoka mtu mmoja tu, aliyeitwa jina lake Abiathari, akamkimbilia Daudi. 21 Naye Abiathari akamweleza Daudi ya kwamba Sauli amewaua makuhani wa Bwana. 22 Daudi akamwambia Abiathari, Siku ile alipokuwako Doegi, Mwedomi, nalijua yakini ya kuwa atamwambia Sauli; mimi nimewapatia watu wote wa jamaa ya baba yako kifo. 23 Kaa wewe pamoja nami, usiogope; kwa maana yeye atafutaye roho yangu, ndiye atafutaye na roho yako; nawe utakaa kwangu salama.
 
MASWALI YA KUJADILI:
1. Daudi aliwakumbuka wazazi wake hata katika kipindi anachopitia machungu na magumu katika maisha kama Yesu alivyomkumbuka Mama yake pale msalabani. Umefanya nini kuwapatia wazazi unafuu wa maisha? Au unangoja siku mambo yako yatakapokaa vizuri?
2. Kwa nini Daudi alipata waungaji mkono wengi kiasi hicho? Je ni kwa kuwa alikuwa mtu wa watu au waliomuunga mkono walikuwa wanatofautiana na Sauli?
3. Kuwepo kwa Sauli madarakani kunawanufaishaje watu wa kabila lake la Benjamini? Hali hiyo ya viongozi kupendelea watu wa makabila yao bado ingalipo leo. Je inasaidia kuchochea maendeleo au kuyarudisha nyuma?
4. Je ilikuwa sahihi kwa Ahimeleki - kuhani mkuu kutoa upanga na chakula kwa Daudi na watu wake bila kumjulisha au kutaka ushauri wa mfalme Sauli? Je hukumu aliyopewa na mfalme ilikuwa ya haki na kwa maslahi ya nchi?
5. Ni nani kati ya Doegi aliyetii amri ya mfalme ya kuua makuhani na askari walinzi waliokataa kutii agizo la mfalme alikuwa ametenda jema machoni pa Mungu. Utatambuaje amri ya mkuu inayostahili kutiiwa na ile isiyostahili? Je Doegi atakuwa na hatia kwa kutekeleza agizo la mkuu?
6. Je Ahimeleki kuhani mkuu alikufa kifo cha kishujaa au cha kizembe na cha usaliti? Je uzembe wa Daudi umechangia kifo hicho?