Seventh-Day Adventist Church

PASTOR LETTA'S OFFICIAL WEBSITE

Menu

SIKU 10 ZA MAOMBI

Wahamasishe washiriki kuhudhuria vipindi kila siku, na kwa wakati ili wote wapate kushiriki mibaraka hii. Kadiri inavyowezekana, kanisa mahalia lipange muda muafaka utakaowawezesha washiriki wote kuhudhuria. Ikiwezekana kila Konferensi wabuni namna ya kufanya juma hili liwe ni la pekee na la kuvutia. Ili kufanya program hii iwe na mguso mkubwa wa kiroho, tunashauri zoezi hili lifanyike kwa kubadilishana wahudumu kanisa kwa kanisa au mtaa kwa mtaa. Ikiwa kuna visa vyovyote vya namna Mungu alivyodhihirisha uwezo wake kwenye jumuiya ya waumini (kanisa) au kwa mtu mmoja mmoja katika siku hizi kumi za maombi, basi visa hivyo vitumwe Union kupitia kwa Makatibu wa Chama cha Wachungaji wa Conference mahalia ili viunganishwe na visa vya sehemu zingine duniani. Bwana awabariki mnapopitia masomo haya na kuyaweka katika uzoefu. Taarifa hizi zitufikie ndani ya mwezi wa January 2019. Masomo haya yameandaliwa na Kitengo cha Uchungaji (Ministerial) – ‘Siku Kumi za Mombi’ cha Halmashauri Kuu ya kanisa la Waadventista wa Sabato (GC) na kuhaririwa na Makatibu wa Chama cha Wachungaji wa Union mbili za Tanzania ambao ni, Pastor Daniel Ndiegi wa NTUC na Pastor Hebert Nziku wa STUM. Yametafsiriwa na Moseti Chacha wa kanisa la Waadventista wa Sabato Lemara. 

Ni sisi Wajoli wenu

 

Mchungaji Daniel Ndiegi Mchungaji Hebert Nziku 
Simu: +255 767 543 904/784 543 904 Simu: +255 764 150 378/677 150 378
Baruapepe: dndiegi@yahoo.com Baruapepe: nzikulihove@gmail.com


UZOEFU WA KINA ZAIDI 
MWONGOZO WA KIONGOZI 
Karibu katika Siku Kumi za Maombi mwaka 2019! Mungu amefanya miujiza mingi kupitia programu hii ya Siku Kumi za Maombi tangu ilipoanza mwaka 2006 kama “Mvua za Utendaji Duniani.” Roho Mtakatifu amewezesha uamsho, mabadiliko, hisia za uinjilisti zilizojengwa upya, na mahusiano yaliyoponywa. Kwa kweli, katika maombi ndipo mahali uamsho unapozaliwa! Mwongozo huu umelenga kukusaidia wewe kama kiongozi. Sehemu ya kwanza ina mada zinazohusiana na “Siku Kumi za Maombi mwaka 2019” na sehemu ya pili inahusisha mambo yatakayokusaidia wewe na kikundi chako cha maombi. Kumbuka kwamba hizi ni rasilimali na mawazo tu. Unashauriwa kuwa huru kubadilisha baadhi ya mambo kadiri Roho Mtakatifu atakavyokuongoza. Katika kipindi hiki cha Siku hizi Kumi za Maombi, yaani Januari 9-19, 2019, kikundi chako kinapaswa kukutana kila siku ana kwa ana au kwa simu kwa muda wa saa moja ili kujumuika kwa maombi. Utagundua kwamba tarehe 19 ni siku ya 11. Hii si lazima, lakini tunapendekeza kwamba mtumie Sabato hii kusherehekea yale yote Mungu aliyofanya katika kujibu maombi ya pamoja. Tunatumaini kwamba mawazo na mapendekezo haya yatasaidia kufanya Siku hizi Kumi za Maombi mwaka 2019 ziwe ni uzoefu wenye nguvu kwa kikundi chako kidogo au familia ya kanisa kwa ujumla. 

Unapoanza safari hii, tumia muda kusoma baadhi ya shuhuda chache kutoka kwa wale walioshiriki Siku Kumi za Maombi mwaka 2018: 

TASHA, ST. KITTS NA NEVES


“Ilionekana kama kila kitu kilikuwa kikipewa kipaumbele isipokuwa kuwasiliana na Kristo, na maombi yaligeuka kuwa kawida za ibada tu. Siku hizi kumi zime nikumbusha jinsi ilivyo amani na furaha kuzungumza na Mwokozi wangu, na kuhisi uwepo wake.” 

YAN, INDONESIA

“Siku Kumi za Maombi kwangu zilikuwa ni uzoefu wa pekee sana! Kusanyiko letu lilikusanyika pamoja na kuomba kila siku. Tulitokwa machozi ya furaha katika kusanyiko hili takatifu, na kadiri tulivyoomba tuliuona upendo wa Mungu na majibu yake kwa maombi yetu.”

IMA, NIGERIA 

“Siku Kumi za Maombi zilikuwa na mguso wa peke na wa kutia moyo. Uzoefu wa kufurahisha zaidi ulikuwa wakati mchungaji mstaafu aliyekuwa wa kulala kitandani kwa sababu ya matatizo ya kisukari hata alikuwa hawezi kuongea, alipoanza kuwapigia watu simu, na sasa anaweza kukaa kwenye kiti cha magurudumu. Huu ni mwanzo tu wa taarifa yetu ya sifa!” 

SANDRA, MARYLAND, USA
 


“Somo la kila siku lilionekana kuandikwa likinilenga mimi. Daima imani yangu imekuwa imara na inazidi kuimarika. Maombi yanajibiwa kadiri ninavyoomba. Mengine hata kabla sijaomba. Wakati huohuo, nilikumbwa na mengine mengi ambayo sikuwa nimetarajia, majaribu yasiyotawalika, na kwa namna fulani Mungu amenisaidia kuyashinda. Ukuu wake ni wa ajabu!” 


RONALD, USA

“Siku hizi kumi za maombi zimebadilisha maisha yetu ya maombi.” 

JENNY, KOREA
 


“Ninahisi kama nimejazwa kwa nguvu na uwezo mpya. Nimebarikiwa sana kuwa sehemu ya kikundi cha watu wanaoomba. Mungu amejibu asilimia kubwa ya maombi yangu, na sasa ninayaacha maombi hayo katika hekima yake nikiwa bado ninahitaji majibu.” 


DORIS, VIRGINIA, USA 


“Mwaka huu ni wa nne wa kuunganika katika maombi. Tulifunga na kuomba kwa siku kumi. Tulimwona Mungu akitenda miujiza katika maisha yetu. Dada mmoja aliomba kwamba aweze kuwasiliana na ndugu zake katika nchi nyingine ambao hakuwa amewasiliana nao kwa miaka ishirini. Baada ya maombi ya dhati, Mungu aliwaunganisha tena! Tunaungana naye kumsifu Mungu.”

Mambo ya kawaida ya maombi katika siku kumi za maombi 

Kwa nini tuzungumzie Uzoefu wa Kina Zaidi? 

Ellen G. White anaandika kuwa, “Wale walioingia katika huduma kwa ajili ya Bwana wanahitaji uzoefu wa juu, wenye kina, na mpana zaidi, kuliko wengine ambao hawajafikiria kuingia katika hiyo huduma. Wengi ambao tayari ni washiriki wa familia kubwa ya Mungu wanafahamu kwa kiasi kidogo maana ya kuutazama utukufu wake, na kubadilishwa toka utukufu hata utukufu. Wengi wana mtazamo hafifu wa ukuu wa Kristo, na mioyo yao imejawa na furaha. Wanatamani mtazamo mkubwa na wenye kina zaidi wa upendo wa Mwokozi. Hebu hawa wakuze kila tamanio la nafsi walilo nalo la kumtafuta Mungu” (Gospel Workers, uk. 274). Tunataka kuchunguza wazo hili la kujenga uzoefu wa juu, wenye kina, na mpana zaidi pamoja na Yesu na kutazama namna uzoefu huu unavyowekwa katika uzoefu wa utendaji wa kila siku.

Kurasa za Wazo la Kila Siku 

Ukurasa wa wazo umeandaliwa kwa ajili ya kila siku husika ya hizi siku kumi za maombi. Ukurasa wa kwanza unanza na fungu la Biblia na sala fupi. Ukurasa wa pili unajumuisha mfumo unaopendekezwa wa muda wa maombi ukiwa ni pamoja na mawazo ya mambo ya kuombea, nyimbo zitakazoimbwa, na ahadi za kudai. Tunapendekeza kwamba unakili karatasi za wazo ili kwamba kila mshiriki aweze kuwa na wa kwake utakayomsaidia kufuatisha wakati wa maombi. Makanisa yote ulimwenguni yanaunganika katika maombi kuhusu wazo la kila siku. Ungana nao katika kuomba kupitia mafungu, nukuu, na maombi yaliyopo katika kila karatasi ya wazo. Hata hivyo, usijisikie kwamba unapaswa kuharakisha kukamilisha orodha yote ya mapendekezo ya maombi. Mnaweza kugawanyika katika vikundi vidogo vidogo na kuwa na maombi kadhaa kwa kila kikundi kutoka katika ile orodha ili kuyaombea. Baadhi ya maombi ni mahususi kabisa kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato Kiulimwengu. Ni muhimu kuomba pamoja kwa ajili ya familia yetu ya kanisa, lakini unaweza kutenga muda wako wa maombi na kutumia mawazo ya maombi ya jumla, hasa ikiwa kikundi chako kinao wageni kutoka katika jamii. Omba kuhusu namna bora zaidi utakayowakaribisha wageni na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya kundi lako. Muda unaopendekezwa kwa ajili ya kila Kipengele cha Maombi  Kiasi cha muda utakaotumika katika kila kipengele cha maombi kwa hakika kitatofautiana kidogo kila wakati mtakapoomba pamoja. 

Dakika zifuatazo ni mapendekezo ya muda unaofaa zaidi: 
1. Kukaribisha/Utangulizi – dakika 2 hadi 5
2. Kusoma mafungu na nukuu za maandiko ya EGW – dakika3 
3. Kipindi cha ibada ya kusifu katika maombi – dakika 10 
4. Kipindi cha toba na kuungama pamoja na kudai ushindi dhidi ya dhambi – dakika 3 hadi 5
5. Kipindi cha kujitoa na kuingilia kati kwa maombi – dakika 30 hadi 35
6. Kipindi cha shukrani katika maombi – dakika 10


 

Kumsihi Mungu na kuomba kwa jaili ya Watu Saba Uliowachagua 
Hamasisha kila mtu amwombe Mungu amwonyeshe watu saba atakaowaombea katika siku hizi kumi za maombi. Hawa wanaweza kuwa wanafamilia, marafiki, wafanyakazi, washiriki, n.k. Wahamasishe watu kumwomba Roho Mtakatifu awaongoze hawa saba anaowaombea wadumu katika Kristo. Wanakikundi pia wanapaswa kumwomba Mungu awaonyeshe namna wanavyoweza kuomba kwa ajili ya mahitaji mahususi na kuwafikia watu hao saba katika kipindi cha siku hizi kumi. Unaweza kutoa kadi au vikaratasi ambavyo watu watatumia kuandika majina saba watakayokuwa wakiombea. 

Huduma ya Sabato katika Kipindi cha Siku Kumi za Maombi mwaka 2019 
Maombi na yalenge katika kitu mahsusi mkishiriki shuhuda mbali mbali jinsi Mungu alivyojibu maombi katika kipindi kile cha huduma za ibada Sabato zote mbili. Kuwa mbunifu – kuna namna nyingi za kushiriki pamoja na familia ya kanisa mambo yanayotokea watu wanapokutana katika maombi kila siku. 

Sherehe za Sabato ya Kuhitimisha
 

Sabato ya mwisho, hasa, inapaswa kutayarishwa kama muda wa kufurahi sana kwa yale yote Mungu aliyotenda katika siku hizi kumi. Tenga muda wa kutosha kwa ajili ya shuhuda za maombi yaliyojibiwa, mafundisho, na mahubiri ya Biblia kuhusu maombi, na nyimbo. Ongoza kusanyiko katika muda wa maombi ili kwamba hata wale ambao hawakuhudhuria mikutano ya kila siku waweze kupata uzoefu wa furaha ya kuomba pamoja na wengine. Tafadhali tazama mwongozo wa Sherehe za Sabato kwa taarifa zaidi. 

Kufuatilia kipindi hiki cha maombi ya siku kumi mwaka 2019
 

Omba kuhusu namna Mungu anavyotaka kanisa au kikundi chako kuendeleza kile kilichoanza katika kipindi cha Siku Kumi za Maombi za mwaka huu. Pengine mtaendelea kukutana kila juma kwa ajili ya maombi. Au pengine Mungu anataka uanze huduma mpya ndani ya kanisa lako au ya kuifikia jamii. Kuwa muwazi na fuata kule Mungu anapoelekeza. Hakika utashangazwa kadiri unavyotembea pamoja naye. Tumejumuisha changamoto ya kuwafikia wengine walio nje, pamoja na mapendekezo mwishoni mwa Mwongozo huu wa Kiongozi. 

Ushuhuda 
Tafadhali shiriki visa vya namna Mungu alivyotenda kazi katika Siku Kumi za Maombi mwaka 2019! Visa vyako vitakuwa msaada kwa wengine wengi. Unaweza kutuma visa vya kwa stories@ministerialassociation.org au kutumwa mtandaoni kwenye www.tendaysofprayer.org. 
Vielekezi vya Maombi ya Pamoja 

Kubalianeni: 

Mtu anapoombea hitaji fulani kwa Mungu, hakikisha kuwa wengine pia wanaombea hitaji hilohilo na kukubaliana – kufanya hivi kuna nguvu! Usifikiri kwamba kwa sababu mtu mmoja ameomba kuhusu hitaji hilo, hakuna haja ya mwingine kuliombea. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 18:19). Inatia moyo kiasi gani kuinuliwa katika maombi! 

Kudai Ahadi za Mungu
 

Utakuta ahadi za Biblia zinazohusiana na mada husika zimejumuishwa katika kila kitini. Himiza kikundi kudai ahadi za Mungu kadiri wanavyoomba. Ni rahisi sana kujielekeza katika matatizo yetu. Lakini tunapodai ahadi za Mungu, tunaongeza imani yetu na kujikumbusha kwamba hakuna kinachoshindikana kwa Mungu. Ahadi hizo hutusaidia kuondoa macho yetu kwenye madhaifu na magumu tunayokabiliana nayo, na kuyaelekeza kwa Yesu. Tunaweza kupata ahadi za Biblia za kudai kwa kila udhaifu na kila pambano. Himiza watu kutafuta ahadi nyingi zaidi iwezekanavyo na kuziandika ili kwamba waweze kuzidai wakati ujao. 

Kufunga 

Alika wale wanaoungana nawe katika Siku Kumi za Maombi kufikiria aina ya kufunga watakayopendelea, kwa mfano kufunga kutazama televisheni, muziki wa kidunia, filamu, mtandao, vitu vitamu vitamu kama vile pipi, au aina nyingine ya vyakula ambavyo ni vigumu kumeng’enywa. Kutumia muda wa ziada kuomba na kujifunza Biblia, ukimuomba Mungu akusaidie wewe na kusanyiko lako kudumu zaidi katika Kristo. Kwa kuchagua mlo mwepesi, tunaruhusu akili zetu kuwa sikivu zaidi kwa sauti ya Roho Mtakatifu. 

Roho Mtakatifu 
Hakikisha unamwomba Roho Mtakatifu akuonyeshe jambo la kuombea katika maisha ya mtu au katika hali fulani. Bibia inatuambia kwamba hatufahamu tuombee nini, na kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayetuombea. 
“Hatupaswi kuomba tu kwa jina la Kristo, bali kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Hii huelezea maana halisi tunaposema kuwa Roho “hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” (Warumi 8:26). Mungu hufurahia kujibu ombi kama hilo. Tunapoomba kwa dhati na kwa nguvu tunaomba kwa jina la Kristo, katika nguvu hiyo kuna ahadi kutoka kwa Mungu kwamba anakaribia kujibu maombi yetu ‘zaidi ya tuyaombayo au tuyawazayo’ (Waefeso 3:20)” (Christ Object Lessons, uk. 147, msisitizo umeongezewa). 

Kuwa pamoja Kimwili
 

Unapokuwa unaanza kipindi cha maombi ya pamoja, ni vema kualika kila mmoja asogee karibu. Watu wanaposogeleana na kutengeneza duara, inasaidia kukuza roho ya umoja, ambayo ni muhimu sana kwa maombi ya pamoja. Ni ngumu kusikia maombi anayoomba mwingine ikiwa watu wametawanyika sana kwenye chumba. 

Kutunza Taarifa ya Maombi 

Kutunza daftari la kumbukumbu ya maombi kwenye kipindi chote cha Siku Kumi za Maombi kunaweza kuwa njia bora ya washiriki kuweka moyoni wazo kuu la maombi ya kila siku, kufanya maagano thabiti na Mungu, na kutambua mibaraka yake kwao. Kuandika maombi yetu na kutunza kumbukumbu ya majibu ya Mungu ni njia iliyothibitishwa ya kutia moyo. Ikiwa utapenda, utunzaji wa kumbukumbu unaweza kujumuishwa kwa namna mbalimbali katika Siku Kumi za Maombi. Unaweza kutenga muda wakati mnapokutanika kwa ajili ya maombi, ili watu wapate kuandika mwitikio wao kwa Mungu kwenye shajara zao binafsi za maombi. Au unaweza kutunza shajara ya kikundi ya maombi na majibu – inaweza kuwa ni daftari, au bango kubwa, au kutunzia mtandaoni. Njia rahisi ya kufanya hivi ni kuchora msitari katikati ya karatasi kubwa. Andika maombi kwenye upande wa kushoto na majibu upande wa kulia. Inafurahisha na pia inajenga imani unapotazama nyuma na kuona jinsi Mungu alivyojibu maombi! 


Kicho 

Himiza na kujenga mtazamo wa kicho na unyenyekevu. Tunakaribia chumba chenye kiti cha enzi cha Mfalme wa ulimwengu. Hebu tusitumie muda huu vibaya kwa mkao wetu na kwa mwenendo wetu na hata katika mazungumzo yetu. Hata hivyo, siyo lazima kila mmoja apige magoti muda wote. Unahitaji watu wawe huru kwa saa moja, hivyo wahamasishe watu kupiga magoti au kukaa au kusimama kadiri Mungu atakavyokuongoza na wanavyokuwa huru zaidi. 

Maombi kwa Sentensi 
Maombi na yawe mafupi, na yaelekezwe moja kwa moja kwenye hitaji. Kufanya hivi kutawapatia wengine pia fursa ya kuomba. Jaribu kufupisha ombi lako kwa sentenso chache, kila mmoja anaweza kuomba mara kadhaa. Maombi mafupi yatafanya kipindi cha maombi kuwa cha kufurahisha na sio cha kuchosha huku mkimruhusu Roho Mtakatifu kugusa vikundi na kuwaongoza akiwaonesha namna ya kuomba. Sio lazima kuanza na kumaliza kwa maneno “Mungu wetu mpendwa” na “Amina” kwa sababu ni maombi endelevu kwa mawasiliano na Mungu 

Ukimya 

Wewe kama kiongozi sio vema utawale kipindi cha maombi. Lengo kubwa ni kuwawezesha wengine kuomba. Kipindi cha ukimya kina thamani kubwa ajabu, kwani kinampa Mungu muda wa kuzungumza na mioyo yetu. Ruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi kwa kumpa kila mmoja muda wa kutosha wa kuomba. 

Kuimba 

Nyimbo za hapa na pale kutoka kwa vikundi zikichanganywa kwenye maombi, zinaongezea uzuri wa mkutano wa maombi. Nyimbo zinazofaa ziorodheshwe kabla ya kipindi, sio lazima ziimbwe zote ila kwa wakati muafaka kama itakavyohitajika. Kuimba pia ni njia nzuri ya kuhama kutoka kwenye kipindi kimoja kwenda kwenye kipindi kingine. 

Kukusanya Mahitaji ya Kuombea 
Usiulizie mahitaji ya kuombea kutoka kwenye kikundi. Badala yake, waambie watu wataje mahitaji yao katika maombi na kuwahimiza wengine kujiunga wakikubaliana nayo kwa kuungana katika maombi kimya kimya. Sababu kubwa ni kwamba, muda unaweza usitoshe kwa kuombea mahitaji ya mtu mmoja mmoja. Ukitaka kuzungumza kuhusu mahitaji ya kila mmoja unaweza kutumia muda wote wa maombi. Shetani anafurahi anapoona tunatumia muda wa maombi kuzungumza kuhusu matatizo yetu badala ya kuombea hayo matatizo. Wanakikundi wanaweza kuanza kushauriana na kupendekeza ufumbuzi. Uwezo unatoka kwa Mungu. Kadiri tunavyoongeza maombi ndivyo anavyoachia uwezo wake. 

Muda wako wa kila siku
 

Ni muhimu wewe kama kiongozi kuhakikisha unatumia muda wako mwingi katika miguu ya Yesu, ukizungumza naye na kusoma Neno lake. Ikiwa utafanya kumfahamu Mungu kuwa kipaumbele chako katika maisha, utafunguliwa uzoefu ulio mzuri wa ajabu. “Nguvu ya ajabu inayoweza kutingisha dunia hutoka katika sehemu yako ya siri ya maombi na kuleta matengenezo makuu. Pale mahali pa siri akiwa katika utulivu, mtumishi wa Bwana anaweka miguu yake katika mwamba wa ahadi za Mungu. (The Great Controversy, uk. 210) 


UTANGULIZI 
Karibu katika Siku Kumi za Maombi mwaka 2019! Tunashukuru sana kwamba tunaweza kuanza mwaka huu kwa maombi. Mungu amefanya miujiza mingi katika miaka iliyopita kadiri tulivyomtafuta kwa maombi na kufunga. Roho Mtakatifu amewezesha uamsho, mabadiliko, hisia za uinjilisti zilizojengwa upya, na mahusiano yaliyoponywa. Kwa kweli, kwenye maombi ndipo uamsho unapozaliwa! 
Tunaamini maisha yako na maisha ya wale unaowaombea yatabadilika kadiri unavyoungana na washiriki wenzako katika kuomba kwa ajili ya kumwagwa kwa Roho Mtakatifu, ambaye Baba ameahidi kuwapatia wale wamwombao. Hapa kuna matokeo matatu tu kutoka kwa wale walioshiriki katika Siku Kumi za Maombi za mwaka uliopita. 

HOWARD, ZIMBABWE 

“Nimebarikiwa sana kwa kipimo kilichofurika katika Siku Kumi hizi za Maombi. Katika kanisa letu huku Zimbabwe, Bwana amejibu maombi yetu na kuna umoja kanisani. Familia zimeunganika tena, na washiriki wapo tayari kumtumikia Bwana.” 

GLENNY, NEW YORK, USA 

“Kanisa limebarikiwa sana. Washiriki wengi wanauliza kama tunaweza kufanya tena. Kila mmoja anazungumza kuhusu kujisikia karibu na Mungu, na kuna hali kubwa ya umoja kati yetu.” 

DERECK, SOUTH AFRICA 

“Kupitia maombi wagonjwa waliponywa, wanafamilia waliofarakana waliungana tena, tumaini lilirejeshwa tena hata katika vifo vya wapendwa, na watu waliyatoa upya maisha yao kwa Mungu. Tunamtumikia Mungu aliye hai! Tunasubiri kwa hamu sana kuona kile Mungu alichotuandalia mwaka huu. Jina lake litukuzwe! 

Mada yetu ya Maombi: “Uzoefu wa Kina Zaidi” 

Katika Siku Kumi za Maombi mwaka 2019, tutaangalia namna ya kuwa na utajiri wa uzoefu wa Kikristo ulio wa kina zaidi. Washiriki wote, wawe ni waumini wapya au ni wa muda mrefu, tunahitaji kwa pamoja kukutana na Yesu kila siku na kwa upya. Mfululizo huu unahusisha mafundisho ya maisha halisi, ahadi za Biblia, na nukuu za kutia moyo kutoka kwenye Roho ya Unabii ili kuimarisha mahusiano yetu ya kila siku na Kristo. Tunasoma kuhusu waumini wa awali: “Waumini wa Korintho walihitaji uzoefu wa kina zaidi katika mambo ya Mungu. Hawakufahamu vema kuutazama utukufu wake kulimaanisha nini na kubadilishwa kutoka utukufu hata utukufu. Lakini waliona miale ya kwanza ya mapambazuko ya awali ya utukufu huo. Tamanio la Paulo kwao lilikuwa kwamba waweze kujazwa na ukamilifu waMungu, ikifuatiwa na kumfahamu “ (Acts of Apostles, aya 307, 308). Tunaomba kwamba hiki kitovu cha maombi kitusaidie kujenga uhusiano wa kina na wa kudumu pamoja na Yesu hadi tufikie “utimilifu wa adhuhuri ya Imani ya injili iliyo kamili” na kuakisi kwa ukamilifu tabia yake ya upendo. 

Mwongozo unaopendekezwa wakati wa maombi 
• Jitahidi kufanya maombi yawe mafupi – sentensi moja au mbili kuhusu mada moja. Kisha waachie wengine. Unaweza kuomba mara nyingi kadiri unavyojisikia, kwa namna ile ile unayozungumza na rafiki. 
• Msiogope kuwa kimya kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mnapata muda wa kumsikiliza Roho Mtakatifu. 
• Imbeni nyimbo pamoja kadiri Roho Mtakatifu atakavyowaongoza, huo pia ni mbaraka mkubwa. Wala hamhitaji kinanda ili kuwaongoza, imbeni tu bila kinanda, inapendeza 
• Badala ya kutumia muda mwingi mkijadili matatizo na mahitaji ya kila mmoja, ni vema kuyaomba tu. Wengine pia wanaweza kuomba na kutaja mahitaji yao katika maombi kila mmoja huku wakidai ahadi zinazoambatana na mahitaji hayo. 


Kudai Ahadi
 

Mungu ametupatia ahadi nyingi katika Neno lake. Ni faida kwetu kudai ahadi hizo katika maombi. Maagizo yote ya Mungu na mashauri yake pia ni ahadi, kwani hawezi kudai jambo fulani kutoka kwetu ambalo hatuwezi kufanya kwa uweza wake. Tunapoomba, ni rahisi kujielekeza katika mahitaji yetu, changamoto zetu au labda manung’uniko kuhusu hali fulani inayoweza kuwa imetokea. Hili silo kusudi la maombi, kusudi kubwa la maombi ni kuimarisha imani yetu. Ndiyo maana tunahimizwa kudai ahadi ambazo Mungu ametupatia katika maombi yetu. Ahadi zitakusaidia kuhamisha macho yako kutoka katika mahitaji yako na changamoto zako na kuyaelekeza kwa Yesu Kristo. Ni kwa kumwangalia yeye ndipo tunapobadilishwa na kuchukua sura yake. Kila ahadi katika Neno la Mungu ni kwa ajili yetu. Ni katika maombi pekee ndipo tunapoweza kuwasilisha haja zetu, kwa kuonesha kwenye Neno la Yehova, na kwa imani kudai hizo ahadi. Neno lake linatupatia uhakika kwamba ukiomba kwa imani, utapokea mibaraka yote ya kiroho. Endelea kuomba nawe utapata zaidi ya kile ulichoomba. (Heavenly Places, uk. 71).

Utadaije hizo ahadi za Mungu? Kwa mfano, unapoomba kwa ajili ya amani, unaweza kudai Yohana 14:27 na kusema, “Bwana umetuambia katika Maandiko yako kwamba ‘Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.’ Ninakuomba unipatie amani uliyoahidi kutuachia.” Kisha umshukuru Bwana kwamba atakupatia hiyo amani hata kama haujisikii kuwa na amani wakati huo. 

Ahadi zinazohusiana na mada zimejumuishwa katika kila somo. 

Kufunga 
Tunakuhamasisha kufanya Mfungo wa Danieli katika Siku hizi Kumi. Kuanza mwaka kwa maombi na kufunga ni njia bora ya kuweka wakfu maisha yetu kwa Mungu kwa mwaka unaoanza. Ellen White anatuambia, “Sasa na kuendelea hata mwisho wa wakati watu wa Mungu wanapaswa kuwa na bidii zaidi, kuwa macho zaidi, kutokuamini hekima yao wenyewe, lakini kuamini hekima ya kiongozi wao. Wanapaswa kutenga siku kwa ajili ya kufunga na kuomba. Kujitenga kabisa na chakula kunaweza kusihitajike, lakini wanapaswa kula vyakula rahisi zaidi” (Counsels on Diet and Foods, uk. 188, 189). Tunafahamu kuhusu Danieli, aliyekula matunda na mboga mboga kwa siku 10. Sisi pia tunakuhamasisha kuwa na mlo rahisi sana katika siku hizi kumi. Mlo rahisi unaoweka kando sukari, vyakula vilivyotengenezwa kiwandani, na soda huweza kutufaidisha kwa ngazi tofauti. Kwanza, kula chakula rahisi humaanisha muda mchache huhitajika kuandaa chakula na muda mwingi kutumika pamoja na Bwana. Pili, chakula chetu kinapokuwa rahisi zaidi, ndivyo inavyokuwa rahisi kwa tumbo kukimeng’enya, na akili zetu zitakua wazi zaidi. Sote tunafahamu kwamba sukari hufunika sehemu inayotawa kuwaza kwetu. Kama tunataka akili zilizo wazi zaidi ili kuisikia sauti ya Mungu, na kama tunataka kuwa karibu zaidi na Mungi, tunahitaji kuhakikisha kwamba chakula chetu hakiturudishi nyuma. 

Kufunga si kujitenga tu na chakula. Tunakuhamasisha pia kufunga kutazama televisheni, filamu, michezo ya kompyuta, na hata Facebook na YouTube. Wakati mwingine vitu visivyo vibaya, kama Facebook na YouTube, huweza kutuchukulia muda mwingi sana. Weka kando kila kinachowezekana ili uwe na muda mwingi wa kukaa na Bwana. Kufunga si njia ya haraka ya kupata mibaraka kutoka kwa Mungu. Kufunga ni kujinyenyekeza wenyewe ili kwamba Mungu aweze kufanya kazi ndani yetu na kupitia kwetu. “Kwa baadhi ya mambo kufunga na kuomba hushauriwa na hufaa. Mikononi mwa Mungu, mambo hayo ni njia ya kusafisha moyo na kujenga akili ya usikivu. Tunapata majibu kwa maombi yetu kwa sababu tunanyenyekeza nafsi zetu mbele za Mungu” (Medical Ministry, uk. 283). 


Roho Mtakatifu
 

Hakikisha unamuomba Roho Mtakatifu akuonyeshe unachopaswa kuombea katika maisha ya mtu au katika hali fulani. Biblia inatuambia kwamba hatufahamu namna ya kuomba na kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayetuombea. “Hatupaswi kuomba tu kwa jina la Kristo, lakini kwa msukumo wa Roho Mtakatifu. Hii huelezea kinachomaanishwa inaposemwa kwamba Roho “hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” (Warumi 8:26). Ombi kama hilo Mungu hufurahia kulijibu. Tunapoomba kwa dhati na kwa nguvu tunaomba kwa jina la Kristo, katika nguvu hiyo kuna ahadi kutoka kwa Mungu kwamba anakaribia kujibu maombi yetu ‘zaidi ya tuyaombayo au tuyawazayo’ (Waefeso 3:20” (Christ Object Lessons, uk. 147). 

Imani 
Tunasoma katika Roho ya Unabii kwamba “maombi na imani vitafanya kile ambacho hakuna nguvu duniani itaweza kufanya” (The Ministry of Healing, uk. 509). Tunahamasishwa pia kuomba na kuwa na imani kwamba Mungu amesikia na atajibu maombi yetu. “Kristo anasema, ‘Ombeni nanyi mtapewa.’ Katika maneno haya, Kristo anatupatia mwongozo wa namna tunavyopaswa kuomba. Tunapaswa kuja kwa Baba yetu wa mbinguni tukiwa kama watoto, tukimuomba zawadi ya Roho Mtakatifu. Yesu anasema tena, ‘Muombapo, aminini kwamba mmepokea myaombayo, nayo yatakuwa yenu.’ Unapaswa kuja kwa Baba ukitubu na kuungama dhambi zako, ukisafisha nafsi na kila dhambi na uchafu, na ni heshima kwako kuthibitisha ahadi za Bwana… Tunapaswa kuamini neno la Mungu, kwani kwa kujijenga juu ya imani ya kitakatifu zaidi tunapata jaribio la tabia. Mungu anathibitishwa kwako kupitia Neno lake. Haupaswi kusubiri kuwa na hisia nzuri za ajabu kabla ya kuamini kwamba Mungu amekusikia; hisia hazipaswi kuwa kigezo chako, kwani hisia hubadilika kama mawingu… Kadiri tunapokuwa duniani, tunaweza kupata nguvu kutoka mbinguni… kwani nimemjaribu Mungu mara elfu. Nitatembea kwa imani, sitaacha kumheshimu Mwokozi wangu kwa kukosa imani” (Review and Herald, Oct. 11, 1892, aya ya 1, 3, 6). Pia tunaambiwa kwamba “ahadi yo yote aliyoahidi, tunaweza kuiomba; kasha tunapaswa kuamini kwamba tumepokea, na kurudisha shukrani kwa Mungu kwamba tumepokea” (Education, uk. 258). Hivyo jenga tabia ya kumshukuru Mungu kabla kwa imani kwa kile atakachoenda kutenda na namna atakavyoenda kujibu maombi yako. 

 


Tunakuhamasisha kuombea kwa namna ya pekee watu saba katika siku hizi kumi ambao ungependa kuwaona wakipata “maisha yaliyojaa zaidi.” Wanaweza kuwa ndugu, marafiki, wafanyakazi wenzako, majirani, au hata watu unaowafahamu tu. Tenga muda na muulize Mungu angependa umuombee nani. Muombe pia akupatie mzigo halisi wa watu hawa. Andika majina yao kwenye karatasi na ulitunze sehemu, kama kwenye Biblia yako. Kuna jambo lenye nguvu katika kuyaandika majina hayo, na utashangazwa namna Mungu anavyofanya kazi katika kujibu maombi yako! 

Changamoto za Kuwafikia watu walio nje katika Siku Kumi za Maombi 
Kila mmoja anaweza kufanya kitu ili kuharakisha ujio wa Yesu kupitia Kuhusishwa kwa Washiriki Wote (TMI) “Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia” (Mathayo 25:35, 36). Katika kitabu cha Huduma ya Uponyaji (The Ministry of Healing) tunasoma kuwa, “Tunapaswa kuishi maisha yenye sura mbili – maisha ya mawazo na matendo, na maisha ya maombi ya kimya na kazi inayofanywa kwa juhudi” (uk. 512). Ni faida kwetu kuwaonyesha wengine upendo wa Yesu. Tumepokea vitu vingi sana kutoka kwa Mwokozi wetu; hebu tusivitunze kwa ajili yetu wenyewe. Hebu tuwashirikishe watu wengine upendo wake. 

Tunakuhimiza wewe na kanisa lako kumuuliza Mungu katika maombi namna unavyoweza kuwafikia wengine katika Siku hizi Kumi za Maombi. Chagua shughuli moja au shughuli kadhaa, na uchague siku, ili uwe mikono na miguu ya Yesu. Unapokuwa ukifanya kazi ya kupanga kila kitu, epuka kuruhusu shughuli hizi kukufanya ushindwe kuomba. “Unapoweka jitihada kwa ajili ya wengine, anza kwa maombi mengi ya siri; kwani ili kuelewa sayansi ya kuokoa roho unahitaji hekima kubwa. Kabla ya kuwasiliana na watu, wasiliana na Kristo. Pata maandalizi ya kuhudumia kwa watu kutoka katika kiti cha enzi cha neema ya kimbingu.” (Maombi, uk. 313). Tumeandaa orodha ya njia unazoweza kutumia kusaidia wengine. Chagua njia yo yote utakayoona inakidhi mahitaji ya wale unaokwenda kuwahudumia. Kuwa huru kufanya kitu ambacho hakijaorodheshwa ikiwa utaona kinafaa zaidi. 

1. Mpikie mgonjwa chakula.
2. Mkaribishe jirani/mfanyakazi mwenzako kwenye kusanyiko la kijamii. 
3. Mpatie chakula mtu asiye na makazi. 
4. Tafuta mzee mmoja. Mtembelee kila siku na umsaidie kazi, kununua mahitaji, kupika, au kazi za bustani. 
5. Oka mkate na ushiriki huo mkate na jirani. 
6. Saidia kwenye miradi katika maeneo yanayokuzunguka. 
7. Jitolee kukaa na mgonjwa au mtu asiyejiweza ili wale wanaomhudumia waweze kufanya shughuli zingine. 
8. Jitambulishe kwa jirani mpya aliyehamia maeneo yenu na kumpelekea chakula. Mfanye ajisikie kukaribishwa katika maeneo hayo. 
9. Nunua mahitaji ya jikoni na uyapeleke kwenye familia yenye uhitaji.
10. Toa msaada miwani yako ya zamani.
11. Jitolee kutoa masomo ya Biblia
12. Tembelea watu katika sehemu za kutunzia watu. 
13. Mpatie mwanafunzi fedha ya “chakula.”
14. Kusanya nguo kwa ajili ya wahitaji. Unaweza kuanzisha kabati la nguo kanisani kwako kwa ajili ya kushirki na wale walio na uhitaji. 
15. Toa msaada kompyuta yako au vifaa vingine vya kielektroniki. 
16. Toa msaada gari lako lililotumika.
17. Andaa “Tamasha la Kupima Afya.” 
18. Tuma kadi kwa mtu aliyefungiwa ndani. 
19. Andaa mfululizo wa mambo ya uinjilisti. 
20. Mpatie mtu kitabu unachodhani angekipenda.
21. Wapigie simu jirani zako na kuwajulia hali.
22. Gawa vijarida na vijuzuu kwa watu. Vinapatiakana: www.glowonline.org/glow
23. Mwalike mtu kumpokea Yesu.
24. Endesha darasa la mapishi.
25. Fanya “Mradi wa machapisho 28.” Katika Juma la kwanza, gawa kitabu kimoja. Juma la pili, gawa vitabu viwili. Juma la tatu, gawa vitabu vitatu. Endelea hadi utakapogawa vitabu vyote 28.
26. Mpelekee chakula mtu aliyepoteza (aliyefiwa na) mpendwa wake.
27. Mtembelee mtu hospitali ili kumtia moyo au kumsaidia kwa namna moja au nyingine.
28. Msomee mzee kitabu.
29. Tembelea makazi ya watoto na toa msaada kwa wafanyakazi wa hapo. 
30.  Anza kundi la kushona/kufuma ili kutengeneza nguo kwa ajili ya wahitaji.
31. Soma Biblia kwa sauti kwa ajili ya mtu asiyeona au asiyeweza kusoma. 
32. Endesha usiku wa vijana nyumbani kwako.
33. Toa makazi kwa watu walionyanyaswa.
34. Gawa baadhi ya vitabu kwenye makazi ya watoto.
36. Panga na kusimamia siku ya kufurahi kwa ajili ya watoto na wenye mahitaji maalumu pamoja na familia zao. 
37. Andaa siku ya kufanya usafi katika jamii.
38. Anzisha chama cha afya katika kanisa lako. Alika marafiki na majirani.
39. Muulize mtu kama angependa kuungana na wewe kutazama mkanda wenye ujumbe wa kiroho. Kadiri mnavyotazama pamoja, omba kwamba Roho Mtakatifu anene na moyo wa mtu huyo.
40. Buni mradi wako mwenyewe.

Kwa vitendea kazi zaidi juu ya ushuhudiaji, tembelea www.revivalandreformation.org/resources/witnessing.

USIKU WA MAOMBI 
Usiku wa Mkesha wa Hiari katika Siku 10 za Maombi

Kwa nini kuwa na Usiku wa Maombi? 
Hakuna chochote “kitakatifu” katika kukesha na kuomba usiku kucha au sehemu ya usiku. Hata hivyo, usiku unaweza kuwa wakati wa pekee ambao watu hawana mambo mengi au haraka. Tunaamini kwamba lengo lako halipaswi kuwa kukaa usiku kucha, bali ni kuomba sana kadiri inavyohitajika hadi utakapokuwa umeombea vitu vyote unavyohisi kwamba Mungu anataka uombee.Tunapendekeza kwamba baadhi ya watu waongoze usiku huo. Hakikisha kunakuwa na mapumziko. Kama kiongozi, unaweza kuona hali ilivyo na kufahamu wakati mapumziko yanapohitajika na wakati utakapoona unafaa kuhamia katika kipengele kinachofuata cha maombi. Tunapendekeza kwamba kuwe na mapumziko ya dk 10 angalau baada ya kila dakika 90. Unaweza pia kuingiza usomaji wa vifungu vya Biblia katika muda wako wa maombi. Unaweza kufanya mambo yote yaliyopendekezwa au baadhi yake, inategemea kile kilicho bora kwa kikundi chako. Kuwa huru kubadilisha mtiririko kadiri utakavyoona inafaa. 

Hapa kuna mfumo uliopendekezwa wa usiku huo wa maombi.

1. Anza na kipindi kwa sifa. Msifu Mungu katika maombi yenu na pia kupitia katika nyimbo. 
2. Tenga muda kwa ajili ya kuungama, ukihakikisha kwamba hakuna kitu kitakachomzuia Mungu kukusikia. Wapatie watu muda binafsi wa kuungama na pia muda wa kuungama pamoja. Hamasisha watu kuungama dhambi za siri kwa siri na kuungama zile dhambi za wazi hadharani. Katika Danieli 9:1-10 tunasoma kuhusu Danieli, aliyeomba na kuungama kwa wazi dhambi za watu wa Mungu. Hamasisha watu kuungama kwa wazi dhambi za kanisa. 
3. Ombea mahitaji ya watu waliohudhuria mikutano ya maombi. Watu wengi sana wanaumia au wanahitaji maombi au wanafahamu mtu mwingine mwenye hitaji kubwa la maombi. Tengeneza mduara, weka kiti katikati, na waalike wale wenye mahitaji ya pekee kuja mmoja mmoja na kushiriki mahitaji yao. Kasha kusanyikeni kumzunguka mtu huyo na uwaruhusu watu wawili au watatu kuombea hitaji mahususi la Mtu huyo na kudai ahadi za Mungu. Utashangazwa namna watu wengi wanavyoumia na kuhitaji maombi. 
4. Gawanya kikundi chako na kutengeneza viwili. Waelekeze wanakikundi wenye jinsia ya kike kwenye chumba kimoja na wale wa jinsia ya kiume katika chumba kingine. Chagua kiongozi katika kila chumba. Wakati mwingine kuna haja za faragha kwa jinsia maalum ambazo haziwezi kushirikishwa jinsia nyingine 
5. Baada ya kurudi pamoja, ombea orodha ya mahitaji inayopatikana hapa chini. Haya ni maombi yaliyopendekezwa kutoka katika kanisa la ulimwengu. Usijihisi kwamba unapaswa kuharakisha kumaliza orodha yote. Unaweza kugawa vikundi vidogo na kuwapatia kila kikundi sehemu ya orodha ili waiombee. 
6. Ombea watu saba uliokuwa umewaorodhesha ili kuwaombea katika siku hizi kumi. 
7. Chagau fungu la Biblia litakalotumika kuombea hitaji fulani. 
8. Hitimisha muda wa maombi kwa kipindi kingine cha kusifu na kushukuru.

Mahitaji ya Kuombea:

1. Tunakuomba ubariki mamia kwa maelfu ya shughuli za kuwafikia watu wa nje walioko ulimwenguni kwa mwaka 2019. Tunaomba hasa kwa mikutano ya injili inayohusisha kila mshiriki (TMI) nchini India, June 2019, na Papua New Guinea, May 2020. 
2. Tunaomba kwa ajili ya washiriki wa Kiadventista wanaopitia mateso na vifungo kwa sababu ya imani zao.
3. Tunaomba kwa ajili ya uamsho wa kiroho kati ya vijana Waadventista wa Sabato wanaohudhuria katika vyuo visivyo vya kanisa ulimwenguni. Hebu na wawe mabalozi wa Kristo.
4. Tunaomba kwa ajili ya asilimia 69 ya idadi ya watu duniani ambao hawajapokea bado utambulisho wa Yesu ulio halisi.
5. Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 62 katika nchi 28 ambazo hazijapata ujumbe wa Waadventista wa Sabato za Unioni iliyokuwa ya Urusi (Divisheni ya Ulaya ya Asia).
6. Tunaomba ili Mungu ainue wamisionari wenye busara walio tayari kufanya kazi katikati ya makundi 746 ya watu katika nchi 20 za Mashariki ya Kati.
7. Tunaomba kwa ajili ya Harakati 1,000 za Kimisionari katika Divisheni ya Kaskazini mwa Asia – Pasifiki na Divisheni ya Kusini mwa Asia – Pasifiki. Kadiri watu hawa wanavyotumika katika nchi kama Taiwan, China, Urusi, na Burma, wabatizwe kwa Roho Mtakatifu na kutiwa nguvu ya kufanya kazi ya Mungu. 
8. Tunaomba kwa ajili ya kundi kubwa la Waadventista wa Sabato walio tayari kumtumikia Mungu kwa kuwapenda wengine na kwa kushiriki pamoja na watu kutoka katika tamaduni na dini nyingine. 
9. Tafadhali inua wanafunzi Waaldensia wa siku za leo ambao watakuwa tayari kukutumikia katika sehemu ngumu.
10. Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 202 katika nchi 41 za Divisheni ya Kusini mwa Asia – Pasifiki ambazo hazijafikiwa sana ili waweze kumfahamu Yesu.
11. Tunaombea Idara ya Shule ya Sabato/Huduma Binafsi kwa kila kanisa mahalia kadiri wanavyotafuta mpango wa Mungu na kufikia jamii zao kwa huduma za upendo, kujifunza Biblia, na ushuhudiaji binafsi. 
12. Tunaomba kwa ajili ya Shirika la ADRA (Adventist Development and Relief Agency) kadiri wanavyofikia mahitaji ya watu ulimwenguni.
13. Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 16 katika miji 6 ya Divisheni ya Kusini mwa Pasifiki ambayo haijafikiwa sana. Tunaomba kwa ajili ya ubatizo unaofanyika kila siku wa Roho Mtakatifu kwa washiriki wanapowafikia wengine kwa upendo
14. Tunaomba kwamba Roho Mtakatifu atusaidie kufahamu namna ya kufikia watu milioni 406 katika miji 105 ya Divisheni ya Kaskazini mwa Asia – Pasifiki ambayo haijafikiwa sana.
15. Tafadhali bariki Idara ya Huduma za Kichaplensia ya kanisa la Waadventista wa Sabato kadiri inavyoratibu na kuwaongoza Wachaplensia na washiriki wanaopenda ili kuhudumia wale walio gerezani.
16. Bwana, tunawakumbuka waalimu wetu wa Shule ya Sabato. Tafadhali wajulishe namna kazi yao ilivyo muhimu kwa watoto wetu. 
17. Bwana, tunaomba ulinzi wako kwa ajili ya Vituo vingi vya Vivutio, programu za afya na familia, na vyama vya Watafuta Njia ulimwenguni.
18. Tunaomba kwamba vijana wengi zaidi waweze kuhusishwa katika Utume kwenye Miji Mikubwa.
19.

Tunaombwa kwamba utusaidie kuwapenda na kuwalea washiriki wapya.

20.

Bwana, tafadhali tuonyeshe namna ya kutuma machapisho yaliyojawa na ukweli zaidi (yaliyochapwa na ya kieletroniki) katika jamii zetu. Tunaomba kwamba watu wayasome na Roho Mtakatifu awasadikishe kuhusu ukweli wa Biblia uliomo katika machapisho hayo.

21.

Bwana, tunaomba ulinzi wako kwa wamisionari wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi. 

22.

Tafadhali inua wainjilisti wa vitabu, wanafunzi wanaojitolea, waandishi, wataalamu wa vyombo vya habari, na wafadhali wanaoweza kutoa fedha ili kueneza maneno ya tumaini na uzima.

23.

Tunaomba kwa ajili ya shule 8,208 za Kiadventista zenye wanafunzi karibia milioni 2. Hebu shule hizi zifundishe ukweli wa Biblia daima na kuwaongoza vijana katika utume na huduma.

24.

Bwana, tupatie hekima ya kufikia tamaduni zisizo na dini na ambazo hazina shauku katika mambo ya dini. Mruhusu Roho wako Mtakatifu avunje kuta zinazozunguka mioyo isiyo na dini.

25.

 Tunaomba kwa ajili ya watu ambao hawajafikiwa bado katika Asia, wakiwemo Waislamu, Wabudha, na Wahindu. Pengine hawajawahi kusikia jina la Yesu. Tupatie hekima ya pekee ya kufikia mahitaji yao. 

26.

Tubariki kadiri tunavyowafikia watu waliotekwa na ibada ya mizimu, ibada ya sanamu, na imani katika vitu vingine. Tusaidie kuelewa mtazamo wao na kuwatambulisha kwa Mwokozi binafsi

27.

Bwana, tafadhali hamasisha Waadventista wa Sabato ulimwenguni kuomba kwa namna ambayo hawajawahi kuomba. Hebu na tusihi pamoja kwa ajili ya mvua ya masika ya Roho Mtakatifu. Tunakuomba ukamilisho ulioahidiwa wa Yoeli 2, Hosea 6, na Matendo 2

28.

Tunaomba kwa ajili ya makundi 541 ya watu katika nchi 18 za Divisheni ya Kusini mwa Afrika – bahari ya Hindi. Tafadhali waelekeze katika ukweli wa Biblia. 

29.

Tuonyeshe namna ya kufikia mahitaji ya kimwili na ya kiroho ya wakimbizi. Hebu kanisa letu lifahamike kwa upendo wetu kwa watu wote, bila kujali ni watu wa aina gani, au wametoka wapi.

30.

Tunaomba kwa uaminifu na ukamilifu tutangaze ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14.  Hebu na tuwezeshe kukita mafundisho yetu yote katika upendo na haki ya Kristo.

31.

Tunakuomba uinue wamisionari wa mijini ili kuanzisha makanisa kwa makundi 806 ya watu katika nchi 20 za Divisheni ya Ulaya. 

32.

Tafadhali inua jeshi kubwa la watenda kazi ili kuanzisha makanisa kwa ajali ya makundi 948 ya watu katika nchi 38 za Divisheni ya Amerika.

33.

Tunakuomba utufundishe namna ya kutangaza Imani za misingi za kanisa letu kwa uwazi, ubunifu, na uhalisia wa Kiblibia. Upendo wa Yesu ukawe ndicho kiini cha kila tunachokiamini.

34.

Tunakuomba uwaandae vijana kuanzisha makanisa kwa ajili ya makundi 789 ya watu katika nchi 9 za Divisheni ya Kaskazini mwa Amerika.

35.

Tunakuomba uandae watu wa kujitolea ili kuhudumia makundi 70 ya watu katika Fildi ya Israeli.

36. Tunakuomba uweze kuinua wamisionari wa kitabibu ili kuanzisha makanisa kati ya makundi 830 ya watu kwenye nchi 11 za Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati.
37. Tunakuomba uinue askari wa maombi ili kuomba kwa ajili ya makundi 2,568 ya watu katika nchi 4 za Divisheni ya Kusini mwa Asia. Tunakumbuka hasa Televisheni ya Hope (Hope TV) India, na Shule ya Kisasa ya Vipofu.
38. Tunaomba kwa ajili ya wafanya kazi wa nyumba za uchapishaji katika Divisheni ya Kusini mwa Asia – Pasifiki.
39. Tunaomba kwamba utafanya kama ulivyahidi katika Zaburi 32:8, kwa kutuongoza na kutuelekeza kadiri tunavyofanya kwa ajili ya Changamoto za Kuwafikia Watu walioko nje Katika Siku Kumi hizi za Maombi. 
40.  Tafadhali ruhusu familia zetu zidhihirishe upendo wako katika nyumba na jamii zetu. Tunakuomba ulete uelewano katika nyumba zetu, uponye mahusiano yaliyovunjika, kulinda walio na hatari ya kunyanyaswa, na kudhihirisha nguvu zako za kutakasa katika hali inayoonekana kukosa matumaini
41. Tunaomba washiriki, wachungaji, na viongozi wetu ulimwenguni wajilishe neno la Mungu kila siku. Pia tukutafute kila siku katika maombi binafsi. Tukumbushe kwamba bila Wewe, hatuwezi kufanya lo lote.
42. Tunakuomba uinue wauguzi na madaktari ili kuanzisha makanisa katika makundi 1,978 ya watu kwenye nchi 22 za Divisheni ya Afrika Magharibi na Kati.
43. Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 49 katika miji 19 ya Divisheni ya Ulaya ambayo haijafikiwa sana.
44. Tunaomba kwa ajili ya watoto wetu. Tafadhali watie nguvu ya kusimama imara kwa ajili yako wanapokutana na vikwazo na misukumo. Wasaidie kufanya chaguzi sahihi na kusimamia ukweli (Isaya 44:3, 4).
45. Tufundishe kufuata mfano wa Kristo usio na ubinafsi wa kufikia mahitaji ya kila siku ya watu wanaotuzunguka. Tutengeneze tuweze kuhudumu kama wamisionari wa kitabibu, watu wanaojitoa kuhudumia jamii, na marafiki kwa wahitaji.
46. Bwana, tunaomba uamsho mkubwa wa Uungu wa asili upate kusafisha kanisa letu katika siku za mwisho. Tunaomba utuwezeshe kusimamia ukweli hata mbingu zikianguka. 
47.  Bwana, tuonyeshe namna ya kushiriki injili na makundi ya watu wenye Imani ya Kiislamu. Tunaomba kwamba waweze kusikia na kuitikia zawadi yako ya neema.
48. Tunaomba kwa ajili ya mbegu za ukweli zilizopandwa nchini Japani wakati wa mchakato wa mwaka jana wa kuwafikia watu unaohusisha washiriki (TMI outreach). Tafadhali tuma watenda kazi ili kufanya kazi na kuomba kwa ajili ya Japani. 

Ahadi za Kudai kwenye Maombi

Mungu ametupatia ahadi nyingi sana katika Neno lake. Ni faida kwetu kuzidai ahadi hizo katika maombi haya. Amri zake zote na mashauri ni ahadi. Kamwe hawezi kututaka tufanye kitu ambacho hatuwezi kufanya kwa nguvu zake. Ni rahisi sana kuweka umakini wetu katika mahitaji yetu, magumu yetu, changamoto zetu – na kuomboleza na kulalamika kuhusu hali zetu tunapoomba. Hili si lengo la maombi. Tunategemea kwamba maombi yataimarisha imani zetu. Ndiyo sababu tunakuhamasisha kudai ahadi za Mungu katika maombi yako. Acha kujitazama na kutazama madhaifu yako, bali mtazame Yesu. Kwa kumtazama, tunabadilishwa na kufanana nae. “Kila ahadi katika Neno la Mungu ni kwa ajili yetu. Katika maombi yako, wasilisha neno lililoahidiwa la Yehova na kwa imani udai ahadi zake. Neno lake linatuhakikishia kwamba ukiomba kwa imani, utapokea mibaraka ya kiroho. Endelea kuomba, na utapokea zaidi ya yale uyaombayo au hata uyawazayo” (In Heavenly Places, uk. 71). 

Unawezaje kudai ahadi zake? Kwa mfano, unapoombea amani, unaweza kudai Yohana 14:27 na kusema, “Bwana, umetuambia katika Neno lako kuwa, ‘Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.’ Nipatie amani uliyoahidi kutuachia.” Mshukuru Bwana kwamba anakupatia amani, hata kama hutahisi kuipata wakati huo huo. 
Ahadi za Roho Mtakatifu 

1. “Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.” Zakaria 10:1 
2. “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” Luka 11:13 
3. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia… Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.” Yohana 14:26; 16:8
4. “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yohana 14:12 – 14 
5. “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.” Zakaria 4:6

Ahadi kwamba Mungu Hujibu Maombi:

1. “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.” Yohana 15:7 
2. “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” Waebrania 4:16
3. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Marko 11:24 
4. “Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.” Zaburi 50:15 
5. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.” Mathayo 18:19 
6. “Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.” Mathayo 21:22
7. “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yohana 14:13, 14 
8. “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” Yohana 16:23, 24
9. “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” 1 Yohana 5:14, 15 

Ahadi kuhusu Nguvu ya Mungu:

1. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.” Mwanzo 18:14 
2. “Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.” Kutoka 14:14
3. “Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.” Marko 10:27 
“Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.” 1 Wathesalonike 5:24
4. “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.” Ayubu 42:2 
5. “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?” Warumi 8:31, 32 
6. “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” Hesabu 23:19
7. “Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.” Isaya 40:28 – 31

Ahadi za Ulinzi wa Mungu:

1. “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” Yoshua 1:9 
2. “Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” Mwanzo 28:15
3. “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.” Kutoka 23:20 
4. “Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.” Torati 4:29 
5. “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Yeremia 33:3 
6. “Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa; Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.” Isaya 40:4, 5 
7. “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.” Zaburi 32:8 
8. “Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” Torati 31:8 
“Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua.” Zaburi 25:12 
9. “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.” Mithali 3:5, 6 
10. “Na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.” Isaya 58:10, 11 
11. “Nao watatoka nje na kuitazama mizoga ya watu walioniasi; maana funza wao hatakufa, wala moto wao hautazimika nao watakuwa chukizo machoni pa wote wenye mwili.” Isaya 65:24 

Ahadi za Moyo Uliobadilishwa:

1. “Nami nitawapa moyo, wanijue ya kuwa mimi ni Bwana; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.” Yeremia 24:7 
2. “Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.” Torati 30:6 
3. “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.” Ezekieli 36:26 
4. “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;” Wafilipi 1:6 
5. “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” 1 Wakorintho 5:17
6. “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2:20
7. “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.” 1 Wathesalonike 5:23, 24 

Ahadi za Msamaha:

1. “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” 1 Nyakati 7:14 
2. “Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.” Zaburi 86:5 
3. “Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.” Marko 11:25
4. “Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” Waefeso 4:32
5. “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” 1 Yohana 1:9 
6. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Isaya 1:8 
7. “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.” Isaya 43:25
8. “Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.” Yeremia 31:34 
“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Waefeso 1:7  
Ahadi za Ushidi Dhidi ya Dhambi:
10. “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” 1 Yohana 5:4 
11. “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Warumi 8:37
12. “Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” 1 Wakorintho 15:57
13. “Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake.” Isaya 40:10 
14. “Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.” Waefeso 6:16 
15. “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2:20
16. “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Wafilipi 2:13 
17. “Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.” Wagalatia 5:16
18. “Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. Amina.” Warumi 16:20 
19. “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Warumi 12:2
20. “Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao.” Yohana 2:15 

Ahadi za Uponyaji:

1. “Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.” Kutoka 15:20
2. “Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako.” Torati 33:25 
3. “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai.” Zaburi 103:2 – 5 
4. "Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.” Mithali 3:7, 8 
5. “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Isaya 53:3-5 
6. “Uniponye, Ee Bwana, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.” Yeremia 17:14 
“Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.” Yeremia 30:17 
7. “Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.” Yeremia 33:6
8. “Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini.” Malaki 4:2
9. “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.” Yakobo 5:14, 15 

 Ahadi kwa ajili ya Nguvu za Kufanya Mapenzi ya Mungu:

1. “Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.” Zaburi 27:14 
2. “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.” 2 Wakorintho 4:16-18
3. “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.” Wagalatia 6:9
4. “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Wafilipi 4:13 
5. “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Wafilipi 2:13
6. “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.” 2 Wakorintho 12:9

Ahadi Kuhusu Kuwa Mashahidi wa Mungu:

1. “Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine.” Isaya 44:8
2. “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia.” Isaya 60:1 
3. “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho.” 2 Wakorintho 5:18 
4. “Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.” Yeremia 1:7
5. “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Matendo 1:8
6. “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.” 1 Petro 2:9
7. “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” 1 Petro 3:15

Siku ya kwanza 

Kufahamu na Kuamini
Fungu Elekezi: “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe” Isaya 49:15.

Je, mtoto anaweza kuelewa kwa ukamilifu upendo wa Mungu kama hajapata upendo wa baba yake wa hapa duniani? Kwa uzoefu wangu, ni vigumu sana. Nilijaliwa kuwa na wazazi wa kiume wanne. Baba aliyenizaa aliachana na mama yangu alipokuwa na ujauzito wangu. Hisia za kukataliwa zilikuwa nzito ndani yangu. Mume wa pili wa mama yangu alikuwa mlevi na mkorofi aliyejawa na lugha chafu – alijaribu hata kumuua mama yangu. Baba yangu wa kambo aliyefuata alikuwa mwema lakini mwenye tama sana. Yeye pamoja na marafiki zake wengine wawili, waliiba katika benki tatu. Aliishia jela, na wakapeana talaka na mama yangu. Miaka yangu ya utoto ilikuwa ya kawaida kwa nje, lakini haikuwa ya kuvutia. Sikuwa na usalama, nilikuwa sijiamini, na nilihisi kutokupendwa. Ilikuwa ni vigumu kwangu kuwa na marafiki shuleni. Kama kijana, nilitamani kukubalika kwa vijana wa rika langu, lakini hali yangu ya kutafuta upendo ilinifanya nizidi kuwa mpweke. Sikufahamu kwamba Baba yangu wa mbinguni alikuwa akifanya kazi nyuma ya pazia ili kujaza upweke huo. “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua… nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.” (Yeremia 1:5; Isaya 43:1). “Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike” 2 Wakorintho 6:18. “Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake” Zaburi 27:10. Nilipokuwa na umri wa miaka 19, rafiki mmoja alinikaribisha kuhudhuria tamasha la Kikristo katika kanisa lake. Mmoja wa viongozi wa kundi la muziki alitoa ukaribisho huu: “Kama maisha yako ni matupu na unajihisi mpweke, je, hutampatia Yesu nafasi?” maneno yake na muziki viligusa moyo wangu na niliitikia wito wa kusogea mbele na kumpokea Yesu.

Nilikuwa nikisoma Injili ya Yohana nilipokutana na fungu hili: “kwa maana Baba mwenyewe awapenda” (Yohana 16:27, sehemu ya kwanza). Lilinishitua! Nilisikia kwamba Yesu ananipenda, Je Baba? Ningeweza kweli kuamini hilo? Nilichokuwa ninafahamu kuhusu Mungu Baba ni kwamba alikuwa ni Baba aliyeonekana kuwa mbali na mimi – sehemu fulani mbinguni – na kwamba angeweza kuona chochote ninachokifanya. Nilikuwa namuogopa. Kadiri nilivyosoma Maandiko, nilizidi kumpenda Yesu. Hata hivyo, Yesu alikuja kuonyesha 
upendo wa Baba yake. Filipo aliposema, “Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba” Yohana 14:8, 9. Niliamua kukubali kwamba Mungu Baba alinipenda kweli kupitia kwa Mwana wake, Yesu Kristo. “Hatua ya kwanza ya kumkaribia Mungu ni kufahamu na kuamini upendo alionao kwetu; kwani tunavutwa kuja kwake kupitia kwa upendo wake” (Thoughts from the Mount of Blessings, aya ya 104, 105. “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao…” 2 Wakorintho 5:19. Baada ya kuelewa kwamba Mungu ananipenda bila kipimo, nilipata nguvu ya kuwasamehe baba zangu wa duniani kwa kunikataa. Mungu alinipatia neema ya kuendelea mbele. Nafahamu kuwa nina Baba wa mbinguni na kwamba mimi ni binti wa Mungu aliye Mkuu, na

Mfalme wa wafalme. Baba yetu wa mbinguni anaelewa hitaji la upendo na ile hali ya kutamani kukubalika iliyo kwa wanadamu. Hajanisahau mimi.
Sasa vipi kuhusu baba yangu wa nne? Nilikuwa na miaka 11 mama yangu alipoolewa tena. Kwa sababu wanaume wengine wote walituacha, nilikuwa najiuliza kama huyu naye atakaa. Kwa kweli huyu alikaa. Nilimchukulia kama baba yangu na kumpenda kama vile alikuwa baba yangu mzazi. Amenipatia ulinzi na upendo ambao baba anapaswa kuutoa. Mama yangu alishafariki, lakini baba yangu huyu anabaki kama sehemu muhimu ya maisha yangu. Baba ni zaidi ya damu. Vipi kuhusu wewe? Umetelekezwa na mzazi au mwanafamilia? Je, unatamani kukubaliwa na kulindwa? Je, unatamani kupendwa bila masharti? “Ishi ukiwa na mawasiliano na Kristo aliye hai, na atakushikilia kwa mkono ambao hautakuachia kamwe. Ufahamu na kuamini upendo Mungu alio nao kwetu, na utakuwa salama; upendo huo ni ngome inayozuia madanganyo na mashambulio ya Shetani” (Thoughts from the Mount of Blessing, uk. 119). “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama” Methali 18:10.

Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi


Sifa

1. Baba, tunakusifu kwa kutupenda kwanza. 
2. Tunakusifu kwamba unatuvuta kwa upendo wako (Yeremia 31:3). 
3. Tunakusifu kwa utunzaji wako usioshindwa. 
4. Bwana, tunakusifu kwa nguvu yako ya uponyaji. 

Kuungama:

1.  Bwana, tafadhali tusamehe dhambi zo zote zinazotuzuia kuwa na uzoefu wa kina zaidi na wewe. [Tumieni dakika chache katika maombi binafsi, ya kimya, mkimruhusu Roho Mtakatifu kutafuta ndani ya mioyo yenu na kuwaonyesha dhambi zo zote mnazohitaji kutubu kwa siri kwa Mungu, na si kwa wazi.] 

Kuomba na Kusihi

1. Bwana, tunaomba, kama alivyoomba Paulo katika Waefeso 3:17-19: o Kwamba upate makazi ya kudumu ndani ya mioyo yetu kadiri tunavyojifunza kukuamini. o Kwamba mizizi yetu izame ndani zaidi katika udongo wa upendo wako. o Kwamba tuelewe upanda, urefu na kina cha upendo wako. o Kwamba tujazwe na ukamilifu wa Mungu. 
2. Tunaomba kwamba utujaze upendo wako na kutufanya kuwa na shauku kuhusu kuwapenda wengine na kuwavuta kwa Yesu.
3. Tunaomba kwa ajili ya familia ambayo ulimwengu wake umejawa machafuko, huzuni, na kuchanganyikiwa. 
4. Tafadhali bariki mamia kwa maelfu ya shughuli za kuwafikia watu ulimwenguni kwa mwaka 2019. Tunaomba hasa kwa mikutano ya injili inayohusisha kila mshiriki (TMI) nchini India, June 2019, na Papua New Guinea, May 2020.
5. Tunaomba kwa ajili ya washiriki wa Kiadventista wanaopitia mateso na vifungo kwa sababu ya imani zao. 
6. Tunaomba kwa ajili ya uamsho wa kiroho kati ya vijana Waadventista wa Sabato wanaohudhuria katika vyuo visivyo vya kanisa ulimwenguni. Hebu na wawe mabalozi wa Kristo. 
7. Tunaomba kwa ajili ya asilimia 69 ya idadi ya watu duniani ambao hawajapokea bado utambulisho wa Yesu ulio halisi.  
8. Bwana, tunaomba kwa ajili ya watu saba (au zaidi) katika orodha ya maombi ya kila mmoja wetu. Tunaomba Roho Mtakatifu afanye kazi katika maisha yao. Pia tunaomba kwa ajili ya mahitaji binafsi ya watu waliokusanyika hapa na kwa ajili ya mahitaji mengine. 

Kushukuru:

1. Baba, tunakushukuru kwa ajili ya wale (taja majina) waliotupenda na kutulea. 
2. Tunashukuru kwamba ulituwekea mkono wako kabla hatujazaliwa (Zaburi 139:13).
3. Bwana, nakushukuru kwamba hata ningekuwa peke yangu, ungekufa kwa ajili yangu (Christ’s Object Lessons, uk. 187). 
4. Tunakushukuru kwa kujibu maombi yetu hata kabla hatujaomba. 

Nyimbo Zinazopendekezwa:

1. Niimbe Pendo Lake #31,
2. Uniangalie #125 

Ahadi za Kudai Kadiri unavyoomba: 
 “Kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba” Yohana 16:27. 
“Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu” Yeremia 31:3.
“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye” 1 Yohana 3:1. •  

• 

Siku ya Pili
Kutoka Ndani Kuelekea Nje

Fungu Elekezi: “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” Yohana 3:3.
Nilikuwa mtoto mzuri sana nilipokuwa ninakua. Sikuwa mgomvi kwa mama yangu; nilikuwa msikivu shuleni na mwenye heshima kwa walimu wangu. Sikushiriki katika sherehe mbaya, kunywa pombe, au kujaribisha madawa kama vijana wengine shuleni kwangu.
Baada ya kuwa Mkristo, nilijisifu kwamba nilikuwa mtu mwema. Nilikula vyakula sahihi, nilibadilisha muziki wangu wa dunia na kuwa wa Kikristo, nilivaa vizuri, nilifundisha lesoni ya Shule ya Sabato, nilipanga matukio ya kiinjilisti na kuwafikia watu, na hata kushiriki ushuhuda wangu binafsi. Nilimpatia Yesu moyo wangu, nikabatizwa, niliamini kwa ukweli Neno Lake, na kutazamia kuishi maisha ya milele katika ufalme wake. Ulimwengu wangu wote ulizunguka kanisa na shughuli zake huku nikitenda mambo mema. Kwa mwonekano wa nje, nilikuwa nikiishi maisha matakatifu. Hata hivyo, badae nilifahamu namna uzoefu wangu wa Ukristo ulivyokuwa mdogo – na namna nilivyomhitaji zaidi Yesu.
Jioni moja nilihudhuria semina katika kanisa langu juu ya maisha ya Kikristo. Mzungumzaji alisema mtu hawezi kuwa katika uhusiano na Kristo unaookoa, asipozaliwa upya. Alinukuu maneno haya kutoka kwa Ellen G. White: “Maisha ya Kikristo hayahusu kubadilisha au kustawisha hali ya zamani, lakini ni badiliko la asili ya mtu. Ni kifo cha ile hali ya ubinafsi, na dhambi, kasha kuwa na maisha mapya kabisa.” (The Desire of Ages, uk. 172). Uhalisi ulinigusa: kuna zaidi katika maisha ya Kikristo kuliko nilivyofikiria! Ilikuwa kweli, maisha yangu yalikuwa tofauti kabla sijampokea Kristo, lakini baada ya kumpokea, yalistawishwa na kubadilishwa. Nilikuwa Mkristo, lakini asili yangu bado ilikuwepo. Bado nilikuwa na hasira na niliudhiwa kwa urahisi. Nilikuwa najivunia na nilitaka mambo kufanywa ninavyotaka. Nilikuwa sijajitoa kwa Kristo. Nilifikiri wokovu wangu ulikuwa salama kupitia mambo yote niliyokuwa nafanya, lakini nilikuwa nikikosa furaha ya wokovu wangu! Nilifanya Kristo akawa ni taaluma yangu, lakini sikuwa na upendo wa Kristo; sikuwa nimejisalimisha kwake. Nilimhitaji Yesu ajengeke ndani yangu.
Ni kwa namna gani mtu anajisalimisha kwa Kristo? Kwanza, ni muhimu kutambua hitaji la Mwokozi – kumchagua.
“Elimu, ustaarabu, kujitawala nia, kujibidisha, hivi vyote vina mahali pake katika maendeleo ya watu, lakini katika hali hii ya uovu havifai kabisa. Pengne vyaweza kumfanya mtu awe na mwenendo mzuri mbele ya watu; lakini haviwezi kuugeuza moyo wake, haviwezi kuitakaa chemchemi ya maisha yake. Ni lazima uwepo uwezo ufanyao kazi kutoka ndani, maisha mapya kutoka juu, kabla wanadamu hawajabadilishwa kutoka dhambini na kuingia katika utakatifu. Uwezo huu utokao juu, ni Yesu Kristo. Neema yake tu ndiyo iwezayo kupuliza uhai ndani ya mtu ambaye ni mfu dhambini, na kumfanya afurahie mambo ya Mungu ya utakatifu.” (Steps to Christ, uk. 18). Sikuweza kubadilisha moyo wangu, lakini niliweza kuchagua kumpatia dhamira yangu. Niliitikia zawadi ya toba na kuungama dhambi yangu ya kujihesabia haki, kujiona wa muhimu, kujipendeza, kujihurumia, na kisha nikaweka nia yangu upande wa Kristo, ili aweze kuiongoza.
Jambo la pili, tumia muda wa kutosha kumfahamu yeye aliye Maisha ya Milele. “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yohana 17:3). Kadiri nilivyotumia muda katika Maandiko na maombi, nikiungana na Mwokozi wangu kwa ukaribu, maisha yangu yalianza kuwa na maana mpya. Yesu alianza mchakato wa kutengeneza kitu kipya ndani ya maisha yangu. Akili yangu ilifanywa upya – mitazamo mipya na hisia mpya zilitengenezwa. Tamanio langu la kumtumikia Mungu liliongezeka.
Unaweza kusema, “Nilizaliwa ndani ya kanisa hili. Nimekuwa Mkristo maisha yangu yote!” “Sijawahi kuwa huko ulimwenguni!” “Nimemtumikia Bwana wangu kwa muda wote ninaokumbuka.” Mambo haya yanaweza kuwa ya kweli, na Mungu atukuzwe kwa hayo! Hata hivyo, unaweza kuwa na yote haya na bado usiwe na Mwana.
Pengine wewe, pia, umeguswa na Roho Mtakatifu kwamba uzoefu wako wa Ukristo ni mdogo sana. Unaweza kufanya nini? Unaweza kuomba ombi hili” “Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele” (Zaburi 139:23, 24). Salimisha moyo na maisha yako kwake na, atadhihirisha maeneo ya maisha yako yanayohitaji kubadilishwa, moja baada ya jingine. Kadiri unavyoshirikiana naye, kamwe maisha yako hayatabakia jinsi yalivyokuwa!

Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Baba, tunakusifu kwa kuwa umetusafisha kutoka katika dhambi na udhalimu wote.
• Bwana, tunakusifu kwa kuwa unaweza kutuepusha kuanguka na kwamba unatutambulisha kwa Baba kwa furaha kubwa (Yuda 24).
• Tunakusifu kwa kuthibitisha dhambi ndani yetu na kuongeza neema.

Kuungama
• Bwana, tunakuomba utuoneshe maeneo katika maisha yetu ambapo bado ubinafsi u hai
• Tunakuomba utusamehe pale ambapo tumejihesabia haki, tukijiona bora na kudhani kwa tu wanyenyekevu kuliko wengine.
• Tunakuomba udhihirishe maeneo ya maisha yetu ambayo yanahitaji kuadilika (unaweza kuchukua muda kidogo kutafakari)

Maombi ya Kunyenyekea na Kusihi
• Bwana, tafadhali tujaze ufahamu wa nia yako, na tunaomba tutembee tukiwa tumestahili kuwa nawe.
• Tunaomba kwa ajili ya walio katika magereza za kiroho na kiakili ili waweze kufunguliwa kutoka katika hatia zao.
• Tunakuomba utujaze kwa tunda la uadilifu.
• Bwana, tunaomba kwa ajili ya hali ya ongezeko la Waadventista ambao watamtumikia Mungu kwa kuwapenda wengine na kushiriki pamoja na watu kutoka katika dini na tamaduni nyingine.
• Tafadhali inua wanafunzi Waaldensia wa siku za leo ambao watakuwa tayari kukutumikia katika sehemu ngumu. 49. Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 62 katika nchi 28 ambazo hazijapata ujumbe wa Waadventista wa Sabato za Unioni iliyokuwa ya Urusi (Divisheni ya Ulaya ya Asia).
• Tunaomba ili Mungu ainue wamisionari wenye busara walio tayari kufanya kazi katikati ya makundi 746 ya watu katika nchi 20 za Mashariki ya Kati.
• Tunaomba kwa ajili ya Harakati 1,000 za Kimisionari katika Divisheni ya Kaskazini mwa Asia – Pasifiki na Divisheni ya Kusini mwa Asia – Pasifiki. Kadiri watu hawa wanavyotumika katika nchi kama Taiwan, China, Urusi, na Burma, wabatizwe kwa Roho Mtakatifu na kutiwa nguvu ya kufanya kazi ya Mungu.
• Tunaomba pia kwa ajili ya orodha yetu ya watu saba au zaidi [taja majina halisi].

Kushukuru
• Bwana, tunakushuru kwa watu waliotuongoza kufanya maamuzi kwa ajili yako.
• Tunakushukuru kwa kutokututelekeza kwa makosa na madhaifu yetu ya zamani.
• Tunakushukuru kwa zawadi ya ungamo na kwa kudhihirisha umuhimu wako kwetu.
• Tunakushukuru kwa kufahamu mwisho tangu mwanzo na kwa kujibu maombi yetu kwa muda na namna upendayo mwenyewe.

Nyimbo Zinazopendekezwa
• Nataka Nimjue Yesu – No. 54

• Hadithia Kisa cha Yesu – No. 34
• Niwe Kama Yesu – No. 136

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” 2 Wakorintho 5:17
• “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu” Maombolezo 3:22, 23.
• “Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu” Tito 3:4-6.
• “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama” Ezekieli 36:26.
• “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu” Wagalatia 2:20.


Siku ya Tatu

Pambano Kubwa Zaidi
Fungu Elekezi: “Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote” Yeremia 29:13.
“Moyo wote unapaswa kukabidhiwa kwa Mungu, bila hivyo badiliko linaloweza kuturejesha katika kufanana naye haliwezi kufanyika kamwe ndani yetu… vita dhidi ya nafsi ni pambano kubwa zaidi ambalo limewahi kutokea. Kujitoa, kusalimisha yote kikamilifu katika nia ya Mungu, kunahitaji kupambana; lakini nafsi inapaswa kusalimishwa kwa Mungu ili ipate kutengenezwa upya katika utakatifu” (Steps to Christ, uk. 43). Tamaa yangu kubwa tangu utotoni, ilikuwa ni kuwa kama Yesu. Kadiri nilivyoweka wakfu maisha yangu kwake kila siku, niliomba aweze kunibadilisha. Alijibu ombi langu kwa namna ya kuvutia zaidi.
Baba mkwe wangu, George, alihamia kwetu baada ya mke wake kufariki kwa Kansa. Tulikuwa na furaha kuwa karibu nae na tulitaka awe sehemu ya maisha ya binti yetu mdogo. Tulitumaini kwamba kuishi nyumbani kwetu na kushiriki katika ibada ya famila kungekuwa na mvuto chanya wa kiroho kwake.
Tuliishi katika shamba lenye ghala ya nafaka, ziwa, malisho, na misitu iliyozunguka eneo hilo. George alikuwa mwanaume makini, aliyependa kujishughulisha, hivyo sehemu hii ilikuwa nzuri zaidi kwa maisha yake ya kustaafu. Kila asubuhi alitembea kuelekea ziwani. Siku moja alipochelewa kurudi kutoka katika matembezi yake, mume wangu alikwenda kumtafuta. Alikuwa amekunguwaa katika kichaka cha matunda madogo na kuanguka. Katika wiki chache zilizofuata, George alilalamika kwamba miguu yake ilikuwa na maumivu, na alipata shida kutembea. Uchunguzi ulionyesha uvimbe ambao ulijiunda ndani ya uti wake wa mgongo. Daktari wake aliandaa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo, ambao hatimaye ulisababisha kupooza kwa kudumu kutoka kiunoni kwenda chini.
Badala ya kumpeleka katika kituo cha kulea, tuliamua kwamba nimhudumie nyumbani. Sikuwa na mafunzo yo yote ya uuguzi, ila kozi ndogo tu niliyopewa na muuguzi aliyeturuhusu tulipoondoka hospitali. Siku yangu ilijumuisha kumuogesha George, kuhudumia vidonda vyake, kusimamia dawa zake, na kumhamisha kutoka kitandani kwenda kwenye kiti, na kumrudisha kitandani tena. Lilikuwa jambo la kudhalilisha sana kwake kwamba hakuweza kujihudumia tena, na nilikuwa na mzigo mkubwa wa hali yake ya kukata tamaa.
Mimi na mume wangu tulipanga kutoka siku za mwisho wa wiki na tulipanga kijana mdogo kumhudumia George kwa muda tulioondoka. Usiku kabla hatujaondoka, nilimuweka George kitandani, nikambusu katika paji lake la uso, na kumkumbusha kwamba tungeondoka asubuhi iliyofuata kwa siku zote za mwisho wa wiki. Kwa hasira aliropoka, “Mimi ni wajibu wako! Huna haki ya kuniacha na mtu mwingine!” nilimjibu. “Wewe ni mzee mbinafsi na usiyefikiri!”
Wakati huo huo, nilishawishika kwamba matendo yangu hayakuwa sahihi na si kama ya Kristo kabisa. Huku nikilia, nilikimbia chumbani kwangu na kujilaza kitandani. “Bwana, nina shida gani? Kwa nini siwezi kutawala hasira yangu? Je, unafanya kazi kweli katika maisha yangu?” Jibu lilikuja kwa upole sana, “Ninafanya kazi katika maisha yako. Ninajibu ombi lako la kuwa zaidi kama Mimi. George anakuudhi. Anatumia muda wako mwingi, akikufanya ujihisi kugharikishwa na kukosa njia ya kutokea. Kuudhika ni dhambi, na kama ukinipatia dhambi hiyo, nitakupatia neema ya kuendelea kumhudumia George.”
“Wengi wanaoweka wakfu maisha yao kwa dhati katika huduma ya Mungu wanashangazwa na kukatishwa tamaa wanapojikuta wakikumbwa na vikwazo na kusongwa na majaribu ya kuchanganya kwa namna ambayo haijawahi kutokea. Wengi hao huwa wanaomba kwa ajili tabia inayofanana na ya Kristo, kwa ajili ya kufaa kwa kazi ya Bwana, na wanawekwa katika hali ambazo huonekana kuondoa uovu wao wote wa asili … [Kisha] Anawapatia fursa ya kurekebisha makosa hayo na kujiweka tayari kwa ajili ya huduma Yake” (The Ministry of Healing, uk. 470, 471). “Kuungama ni pamoja na kuhuzunika kwa ajili ya dhambi na kuiacha dhambi hiyo kabisa. Hatutaikataa dhambi mpaka hapo tutakapoona ubaya wake ulivyo hasa” (Steps to Christ, uk. 23).
Niliona maudhi yalivyo, na sikutaka yawe ndani ya moyo wangu. Niliungama dhambi yangu na kuamua kuishi kwa ajili ya Mungu. Nilimuomba anioshe na kunipatia moyo mpya. Niliamka kutoka kitandani, nikafuta macho yangu, na nikamuomba George msamaha. Amani iliujaza moyo wangu, na kushidwa kwangu kuligeuka kuwa ushindi. Kadiri hali yake ilivyozidi kuwa ngumu kwangu kuhudumia, ilitubidi kumpeleke George katika kituo cha kuhudumia. Jioni moja tulipokea simu iliyotutaka kwenda, kwani George alipata ugonjwa wa kupooza.
Mume wangu alikaa kando yake na kunong’oneza katika sikio lake, “Baba, unafahamu Yesu anakupenda? Ukiomba moyoni mwako, atakuokoa.” Alama pekee inayoonekana kudhihirisha kwamba George aliielewa ilikuwa chozi lililodondoka katika shavu lake. Katika nyakati zake za mwisho, naamini kwamba alimpokea Yesu kama Mwokozi wake.
Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwamba unatupatia nguvu na kuwa unatushikilia tunapokuwa dhaifu.
• Tunakusifu kwamba tunapoanguka, hautuachi.
• Tunakusifu, Bwana, kwamba unatupa dhambi zetu katika kina cha bahari na kuzisahau kabisa.

Kuungama
• Bwana, tusamehe pale tuliporuhusu ubinafsi kutawala.
• Tafadhali tusamehe tunapokutambulisha vibaya kwa wengine.
• Tusamehe kwa sababu ya nyakati tulizong’ang’ania dhambi badala ya kukuruhusu kuiondoa katika maisha yetu.
• Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele (Zaburi 139:23, 24). [Tumia dakika chache kwa maombi binafsi ya kimya, mkimruhusu Roho Mtakatifu kuchunguza mioyo yenu.]

Kuomba na Kusihi
• Bwana, tusaidie kuwa wavumilivu na wema, tukionyesha upendo na huruma yako kwa wale wanaotukasirisha na kutunenea vibaya.
• Tafadhali tusaidie kustahimili katika magumu, hasa upendo unapoonekana kutofaa.
• Tunaomba kwa ajili ya wale wanaohudumia wazee na/au wanafamilia wagonjwa. Wapatie uvumilivu, uwezo, na upendo.
• Bwana, tafadhali punguza hofu ya wale wanaopitia magonjwa yasiyotibika. Wapatie ujasiri na amani ya Yesu.
• Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 202 katika nchi 41 za Divisheni ya Kusini mwa Asia – Pasifiki ambazo hazijafikiwa sana ili waweze kumfahamu Yesu.
• Tunaombea Idara ya Shule ya Sabato/Huduma Binafsi kwa kila kanisa mahalia kadiri wanavyotafuta mpango wa Mungu na kufikia jamii zao kwa huduma za upendo, kujifunza Biblia, na ushuhudiaji binafsi.
• Tunaomba kwa ajili ya Shirika la ADRA (Adventist Development and Relief Agency) kadiri wanavyofikia mahitaji ya watu ulimwenguni.
• Tunaomba pia kwa ajili ya orodha yetu ya watu saba au zaidi [taja majina halisi].

Kushukuru
• Tunakushukuru kwamba utachunga midomo yetu na kutunza milango ya ndimi zetu.
• Tunakushukuru kwa upendo kama wa Kristo unaotupatia kwa ajili ya wale walio wagumu kupenda.
• Tunakushukuru kwamba kadiri tabia yako inavyofanyika katika maisha yetu, wengine watavutwa kwako.
• Bwana, tunakushukuru kwa kutusikia, kwa kujibu maombi yetu, na kwa kufanya kazi nyuma ya pazia ili kukamilisha nia yako.

Nyimbo Zinazopendekezwa
• Nitembee Nawe Mungu #14
• Umetuahidi #13 • Usinipite Mwokozi #22

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana, Naye aipenda njia yake. Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza” (Zaburi 37:23, 24).
• “Bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia” (Isaya 40:31).
• “Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru” (Zaburi 28:7).


Siku ya Nne
Thamani ya Kujisalimisha

Fungu Elekezi “Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu” Luka 15:7.
Huyu alikuwa ni mdogo kati ya watoto wane, na alikulia katika nyumba ya wagomvi. Ndugu zake walikuwa wakubwa zaidi na walikuwa na maisha yao; baba na mama yake walikuwa wametingwa katika kusimamia kilabu cha pombe katika mji mdogo walipokuwa wakiishi. Mara nyingi Eddie aliachwa ajihudumie mwenyewe. Ukumbi wa kuoneshea filamu uligeuka mahali pa kumlea hasa siku za mwisho wa wiki, na mara nyingi alirudi nyumbani kukuta nyumba tupu. Mara nyingine alikaa katika gari ya familia baada ya watoto wengine wa miaka saba kulala vitandani mwao na kulia kwamba mama yake atoke katika kilabu cha pombe na kumpeleka nyumbani.
Eddie alipokuwa na miaka 14, mama yake aliongoka na kuwa Mkristo wa kanisa la Waadventista wa Sabato aliyezaliwa mara ya pili, na ghafla mambo yalibadilika. Badala ya kusimamia kilabu ya pombe, mama yake alianza kuhudhuria mikutano ya maombi na ibada za kanisani. Eddie aliungana na mama yake kujiunga na Kanisa la Waadventista wa Sabato na akajiandikisha katika shule ya kanisa. Hata hivyo, alipokuwa na miaka 17, alipoteza shauku kanisani. Miaka miwili baadaye, aliandikishwa katika huduma za jeshi. Mchungaji wake alimhamasisha kubatizwa tena kabla ya kukabiliana na hatari za vita. Jambo hili lilionekana kama mpango mzuri, na Eddie alikubali kufanya hivyo alipokuja nyumbani wakati wa likizo. Alisoma misingi ya imani ya Kanisa la Waadventista kwa mara ya pili. Kitendo hiki kilimpatia uelewa wa hiyo misingi, lakini bado hakuwa anamfahamu Yesu.
Eddie aliona kwamba kujaribu kuishi kwa viwango vya kanisa kwa jitihada zake mwenyewe ilikuwa changamoto. Alichoka kujaribu kuwa Mkristo, akiigiza kuja kanisani, akijaribu kutii. Hakuwa na nguvu katika kudumisha maisha ya Kikristo na alianguka katika mienendo yake ya zamani. Tatizo lilikuwa ni nini? “Kuna wale wanaodai kumtumikia Mungu, wakati wanategemea jitihada zao wenyewe kutii sheria yake, kutengeneza tabia sahihi, na kuulinda wokovu. Mioyo yao haiguswi kwa hisia yo yote ya upendo wa Kristo, lakini wanatafuta kufanya majukumu ya maisha ya Kikristo kama ambayo Mungu anataka wafanye ili kuingia mbinguni. Dini ya aina hii haina thamani yo yote… kuwa Mkristo bila upendo wake [Kristo] wa kina, ni maneno matupu yasiyokuwa na maana, na kazi bure” (Steps to Christ, uk. 44).
Mama na dada yake Eddie walihudhuria mkesha wa maombi kanisani usiku wa mwaka mpya. Walimuombea Eddie. Waliona jibu kwa maombi yao katika wiki chache zilizofuata mambo yalipoanza kumuendea vibaya. Alipoteza mchumba wake, akapotea kazi yake, na gari lake. Kwa nini ulimwengu wangu unaporomoka? Alijiuliza. Baada ya kunywa pombe usiku pamoja na marafiki zake, Eddie alirudi nyumbani katika hali ya kulewa. Alilia, “Mungu, kama wewe ni halisi, ninakuhitaji! Ninafahamu mambo mengi kuhusu wewe, lakini sasa ninataka kukufahamu!” sauti ndogo, tamu, iliyotulia ilipenya katika akili yake: “Mimi ni halisi, na ninakupenda.” Jambo hili lilipondaponda moyo wake. “Unawezaje kunipenda jinsi ninavyoishi?” aliuliza. “Nimechoka maisha yangu jinsi yalivyo. Tafadhali nifanye kuwa Mkristo wa kweli. Ninataka kukutumikia maisha yangu yote, lakini siwezi kufanya hivyo peke yangu.”
Usiku ule, Eddie alisalimisha maisha yake kwa Yesu na akamkubali kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Aliamini kwa imani kwamba dhambi zake zilisamehewa na kwamba alikuwa kiumbe kipya katika Kristo Yesu; mambo ya kale yalikuwa yamepita. Kupitia kitendo hiki rahisi cha kuamini ahadi ya Mungu, Roho Mtakatifu alianza kufanya kazi ndani ya moyo wake. Maisha mapya yalianza, na Eddie hakurudi nyuma.
“Sasa ukiwa umejitoa kwa Yesu, usirudi nyuma, usijiondoe kutoka kwake, lakini siku kwa siku sema, ‘Mimi ni wa Kristo; nimejitoa kwake;’ na mwombe akupatie Roho wake na akutunze kwa rehema zake. Kwani ni kwa kujitoa kikamilifu kwa Mungu, na kumwamini ndipo unapokuwa mwana wake, hivyo unapaswa kuishi ndani yake. Mtume anasema, ‘Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye.’ Wakolosai 2:6 (Steps to Christ, uk. 52).
Eddie alianza kusoma Biblia na alijifunza kuomba. Kadiri alivyosoma Maandiko na kujifunza zaidi kuhusu upendo wa Mungu kupitia maisha ya Yesu, maisha yake yalibadilishwa. Ulevi, uvutaji wa sigara, na chaguzi zingine za mtindo wa maisha ambazo hapo kwanza zilimfurahisha hazikuwa sehemu ya maisha yake tena.
Mama yake Eddie alipendekeza asome kitabu kidogo cha Jipatie Amani Moyoni (Steps to Christ) ili kimsaidie katika safari yake mpya. Mwanzo alipata shida kusoma – nyakati fulani akili yake ilihama – lakini kadiri alivyostahimili, akisoma ukurasa mmoja baada ya mwingine, kitabu hiki kilikuwa cha thamani kwake. Alipata upendo wa Kristo katika kurasa zake, na kwa imani alikubali kwamba ahadi za Mungu zilikuwa kwa ajili yake. Hatimaye alipata amani.

Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwa kuwa haujawahi kukata tamaa juu yetu.
• Tunakusifu kwa kazi zako za ajabu kwa ajili ya watoto wa wanadamu.
• Bwana, tunakusifu kwa furaha tunayoipata katika uwepo wako na kwa kutupatia tumaini na mategemeo ya baadaye.

Kuungama
• Tafadhali, Bwana, utusamehe kwa kushikilia mambo ambayo yanatutenga nawe.
• Tusamehe kwa nyakati tulizojaribu kuishi maisha ya Kikristo kwa uwezo wetu wenyewe.
• Tunakiri kwamba tunahitaji uzoefu wa binafsi na wewe, wala siyo ufahamu wa kichwani tu.

Maombi ya Kunyenyekea na Kusihi
• Bwana, tunakuomba utupatie mioyo iliyojisalimisha kikamilifu kuishi katika utii wa neno lako.
• Tafadhali tubatize kila siku kwa Roho Mtakatifu na tufanye tuwe na bidii zaidi katika jitihada zetu za kuvuta watu.
• Tunaomba kwamba wapendwa wetu walioiacha imani wakumbuke ilivyokuwa walipokuwa katika ushirika na Wewe na watamani kuunganika tena na Wewe. Wasaidie kuhisi na kukubali upendo na msamaha wako.
• Tafadhali timiza ahadi yako katika Yoeli 2:25: rudisha katika hali yake miaka ambayo nzige [dhambi] walikula katika maisha yetu na katika maisha ya wapendwa wetu. Tupatie imani ya kuamini kwamba utatimiza ahadi yako.
• Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 16 katika miji 6 ya Divisheni ya Kusini mwa Pasifiki ambazo hazijafikiwa sana. Tunaomba kwa ajili ya ubatizo unaofanyika kila siku wa Roho Mtakatifu kwa washiriki wanapowafikia wengine kwa upendo.
• Tunaomba kwamba Roho Mtakatifu atusaidie kufahamu namna ya kufikia watu milioni 406 katika miji 105 ya Divisheni ya Kaskazini mwa Asia – Pasifiki ambyo haijafikiwa sana.
• Tafadhali bariki Idara ya Huduma za Kichaplensia ya kanisa la Waadventista wa Sabato kadiri inavyoratibu na kuwaongoza Wachaplensia na washiriki wanaopenda ili kuhudumia wale walio gerezani..
• Tunaomba pia kwa ajili ya orodha yetu ya watu saba au zaidi [taja majina halisi].

Kushukuru
• Tunakushukuru, Bwana, kwa kuwa ulitupatia Roho Mtakatifu kutuongoza daima katika kweli yote.
• Tunakushukuru kwa kushughulika na kujibu maombi yetu kwa njia tusizoweza kuona.
• Bwana, tunakushukuru kwa kutujibu maombi yetu kabla hatujapokea majibu, si kwa sababu tunastahili, bali kwa sababu Yesu anastahili.

Nyimbo Zinazopendekezwa
• Kristo Wa Neema Yote #10
• Njiani Huniongoza #155
• Mlango Wazi #110

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba” (1 Yohana 5:14, 15).
• “Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha” (Hosea 14:4).
• “Yuko mwingine anayenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli” (Luka 5:32).
• “Rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya” (Yoeli 2:13).Siku ya Tano

Fursa ya Ubia

Fungu Elekezi “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” 2 Wakorintho 5:17.
Nilipokuwa na umri wa miaka 19, nilimpatia Yesu moyo wangu na maisha yangu yote yakabadilika. Kujifunza Biblia na maombi vikawa marafiki zangu wa kila siku. Niliamua kuhudhuria mikutano ya maombi, makundi ya kujifunza Biblia, Shule ya Sabato, na kanisani – kila mahali Neno la Mungu lilipotolewa na shuhuda zilipotolewa. Nilikuwa na njaa ya Yesu zaidi na zaidi. Kadiri Kristo alivyojaza maisha yangu, ndivyo ladha yangu katika muziki, maburudisho, nguo, kila kitu, vilivyobadilika! Mwalimu wangu wa Shule ya Sabato, aliyekuwa mwema sana kwangu, alipenda kusema kwamba tunapojitoa kikamilifu kwa Kristo, tukiweka wakfu maisha yetu katika huduma yake, “hatuishi tena kulingana na tama zilizopita, lakini kwa imani ya Mwana wa Mungu tuafuata hatua zake, tunaakisi tabia yake… vitu tulivyovichukia hapo awali sasa tunavipenda, na vitu tulivyovipenda hapo awali sasa tunavichukia” (Steps to Christ, uk. 58 msisitizo umeongezwa).
Niligundua jambo hili ni kweli. Nilihisi tamanio moyoni mwangu kumwambia kila mmoja niliyeweza kwamba Kristo alinipenda na alisamehe dhambi zangu zote, kwamba nilikuwa safi na wa thamani kwake. “Mtu anapokuja kwa Kristo ndipo ndani ya moyo wake panapozaliwa tamanio la kutangaza kuwa rafiki aliyempata ndani ya Yesu ni wa thamani kiasi gani; ukweli unaookoa na kutakasa hauwezi kufungwa ndani ya moyo wake. Kama tumevikwa haki ya Kristo, na tumejazwa furaha ya Roho wake anayekaa mioyoni mwetu, hatupaswi kuzuia amani yetu. Kama tumeonja na kuona kwamba Bwana ni mwema tutakuwa na kitu cha kuwaambia wengine” (Steps to Christo, uk. 78).
Ningeanzia wapi? Sikuwa na dokezo lo lote la namna ya kushiriki na wengine, hivyo niliomba na kumuuliza Mungu nilichopaswa kufanya. Nilivutiwa na maneno, “mmepata bure, toeni bure” (Mathayo 10:8). Haya maneno yalikuwa rahisi kusemwa kuliko kutendwa. Ninawaambia nini? Niliwaza. Wakati wa maombi yangu, nilipata nukuu hii: “Mashetani walikuwa na ushuhuda kwamba Yesu alikuwa Masihi. Wangeweza kusema walichokifahamu; walichokiona wenyewe, kukisikia, na kuhisi kuhusu nguvu ya Kristo. Hili ndilo jambo ambalo kila mmoja ambaye moyo wake umeguswa na neema ya Mungu anaweza kufanya… tunaweza kusema namna tulivyoonja ahadi yake, na kugundua ahadi hiyo ni ya kweli. Tunaweza kushuhudia kile tulichofahamu kuhusu rehema za Kristo, huu ni ushuhuda kwamba Bwana wetu anaita, na kwamba ulimwengu unaangamia” (The Desire of Ages, uk. 340). Nilisubiri Bwana anipatie fursa ya kumshuhudia.
Nilikuwa nikifanya kazi sehemu ya mapokezi katika ofisi wakati taarifa za ghafla zilipopita katika runinga, zikitutadharisha kwamba kimbunga kilikuwa kimelikumba jimbo la Florida na kilikuwa kikisogea kuelekea kaskazini ukanda wa pwani ya Atlantiki kuelekea Carolinas. Kadiri tulivyokuwa tukitazama taarifa hiyo, mmoja wa wafanyakazi wenzangu aliyeitwa Ginger aliuliza, “Ni nini kinachotokea? Mambo yanachanganya tu!” niliropoka kuwa, “Yesu anakuja!” sikuwa nimefanya kazi pale kwa muda mrefu na nilishangaa kwamba nilijibu ukweli! Niliharakisha kurudi katika meza yangu. Baada ya muda mfupi, Ginger alikuja mbele ya meza yangu na kuketi kwenye kiti. Alisema, “Kwahiyo, niambie kuhusu habari hizi ya kuja kwa Yesu. Ningependa kufahamu!” Nilimpatia somo fupi la Biblia juu ya dalili za kuja kwa Yesu mara ya pili huku nikiomba kimoyomoyo, na nikashiriki namna nilivyoandaa moyo wangu kumfahamu huyo Yesu kama Rafiki na kuwa tayari kuonana naye. Kisha niliongeza nikimkaribisha kuwa yeye pia afanye vivyo hivyo. Bwana alifungua mlango, na nilichagua kuingia kupitia katika huo mlango. 

Mungu amenipatia fursa ya kufanya kazi pamoja naye kwa takribani miaka 40 sasa. Nimekuwa mfanyakazi wa Biblia; nilifundisha Biblia katika shule ya bweni ya Kiadventista kwa miaka sita; nimehubiri mbele ya maelfu ya watu nchini Ufilipino; nimeshiriki ushuhuda wangu mbele ya mamia ya wanafunzi wa sekondari wakati wa majuma ya maombi; na nimeendesha semina kwa ajili ya mikutano ya wanawake ya urejeshaji; makambi; na makanisa. Zote hizo zimekuwa fursa nzuri za kushiriki kile Mungu alichofanya, lakini namna nzuri zaidi ya kuvuta roho kwa Bwana ni kwa kuwakaribia watu kupitia mguso wa upole, kwa kufikia mahitaji yao na kuteka usikivu wao. Kisha unaweza kuwaalika kumfuata Yesu.
“Wale wanaosubiri ujio wa Bwana Harusi wanapaswa kuwaambia watu, ‘Mtazame Mungu wako!’ miale ya mwisho ya mwanga wa neema, ujumbe wa mwisho wa neema unaotolewa kwa dunia, ni ufunuo wa tabia yake ya upendo. Watoto wa Mungu wanapaswa kudhihirisha utukufu wake. Katika maisha na tabia yao wenyewe wanapaswa kudhihirisha kile neema ya Mungu ilichofanya kwa ajili yao” (Christ Object Lessons, uk. 415)

Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakushukuru kwa kuwa umetubadilisha. Tumekuwa viumbe vipya!
• Tunakusifu kwa ulinzi tunaoupata ndani yako (Isaya 49:16).
• Tunakusifu kwa rehema za kila siku unazotuonyesha.

Kuungama
• Bwana, tusamehe hasa katika nyakati ambazo hatukushiriki imani zetu kwa sababu ya hofu.
• Tunakiri kwamba tunahitaji nguvu zako ili kushuhudia kwa ufanisi.
• Bwana, tafadhali tuonyeshe maeneo katika maisha yetu ambayo hutufanya tusiwe na ushuhuda chanya kwa ajili yako.

• Tusamehe, Bwana, kwa kutokudhihirisha tabia yako ya upendo kwa wengine.
Kuomba na Kusihi
• Bwana, tafadhali fanya upya mioyo ya wale wote katika huduma walio na wasiwasi. Wakumbushe kwamba wanafanya mapenzi yako. Tafadhali turuhusu tuone matunda ya kazi yao, hata kama ni roho moja tu.
• Bwana, tunawakumbuka waalimu wetu wa Shule ya Sabato. Tafadhali wajulishe namna kazi yao ilivyo muhimu kwa watoto wetu.
• Bwana, tunaomba uongozi wako kwa ajili ya Vituo vingi vya Vivutio, programu za afya na familia, na vyama vya Watafuta Njia ulimwenguni.
• Tunaomba kwamba vijana wengi zaidi waweze kuhusishwa katika Utume kwenye Miji Mikubwa.
• Tunaomba utusaidie kuwapenda na kuwalea washiriki wapya.
• Bwana, tafadhali tuonyeshe namna ya kutuma machapisho yaliyojawa ukweli zaidi (yaliyochapwa na ya kieletroniki) katika jamii zetu. Tunaomba kwamba watu wayasome na Roho Mtakatifu awasadikishe kuhusu ukweli wa Biblia.
• Bwana, tunaomba ulinzi wako kwa wamisionari wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi.
• Tafadhali inua wainjilisti wa vitabu, wanafunzi wanaojitolea, waandishi, wataalamu wa vyombo vya habari, na wafadhili wa kifedha ili kueneza neno lako la tumaini na uzima.
• Tunaomba pia kwa ajili ya orodha yetu ya watu saba au zaidi. Tafadhali fanya kazi kwa nguvu katika maisha ya watu hawa. Tunadai andiko la 1 Yohana 5:16.

Kushukuru
• Tunakushukuru kwamba unajibu maombi yetu sawasawa na mapenzi yako.
• Tunakushukuru kwa kututumia kushiriki na wengine!
• Tunakushukuru Bwana, kwa kuwa ahadi zako ni za kweli na za kuaminika.

Nyimbo Zinazopendekezwa
• Namwandama Bwana #128
• Nina Haja Nawe#126
• Kuwa na Yesu #51

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema” (Luka 12:12). • “Ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma” (Isaya 55:11). • “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu” (1 Petro 3:15).


Siku ya Sita
Karama ya Toba

Fungu Elekezi “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake” 1 Petro 5:6.
Mr. G alikuwa mwalimu aliyeheshimika katika shule ndogo ya bweni katika milima ya Mashariki mwa Washington nchini Marekani. Shule hii haikufundisha tu kanuni za usomaji, uandikaji, hesabu, na sanaa lakini pia ilifundisha kanuni za msingi za maisha ya Kikristo. Wanafunzi walijifunza kutoa masomo ya Biblia, kufundisha katika mikutano ya injili, na kuongoza majumbani kwao kwa kufundisha lesoni ya Shule ya Sabato, kuhubiri, na kufanya shughuli za kuifikia jamii. Mr. G alikuwa sehemu ya muhimu ya elimu hiyo.
Katika darasa la kumi na moja, Mr G alifundisha akitumia kitabu cha “Jipatie Amani Moyoni.” Alitumia mbinu za vitendo kufikisha ujumbe wa urahisi wa Injili katika fikra za wanafunzi wake, na mzigo wake mkubwa ulikuwa kwamba wapokee kanuni za jinsi ya kutembea na kudumu ndani ya Kristo kila siku. Maisha yake yalikuwa ni ushuhuda wa uweza wa Mungu, na hivyo alisisitiza katika fikra za wanafunzi wake umuhimu wa kuanza siku na Kristo. “Jikabidhi kwa Mungu asubuhi, na ufanye hii kuwa ni kazi ya kwanza kila siku. Hebu maombi yako na yawe: “Nichukue ee Bwana jinsi nilivyo, niwe wako kabisa. Ninaweka mipango yangu yote miguuni pamo. Nitumie leo katika huduma yako. Udumu ndani yangu na kazi zangu na zipambike ndani yako. (Steps to Christ, uk. 70)
Mr. G alifundisha darasa la Biblia kwa wanafunzi wa madarasa ya juu na useremala kwa wavulana wa darasa la tisa. Darasa liligawanywa katika sehemu mbili. Kwanza, walijifunza nadharia kutoka kweny kitabu; kisha, waliweka katika vitendo kile walichojifunza. Siku moja wakiwa darasani, Mr. G alikuwa akisaidia wavulana watatu kujenga ukuta wa kutegemeza, wakati huo, wengine watau walikuwa wakicheza kwenye rundo la mbao. Mr. G aliwaomba wavulana wale kutoka kwenye mbao zile kwani zingeweza kuanguka na kuumiza mtu. Wavulana wale waliendelea kucheza kwenye mbao, na alipokwenda kuzungumza nao, ubao mkubwa ulimwangukia mguuni. Alizunguka kwa maumivu, huku akishikilia mguu wake. Wavulana wale, waliliona kama jambo la kufurahisha, walicheka na kumnyooshea vidole. Ghafla, Mr. G alikasirika. Maneno makali yalitoka kinywani mwake. Kama Musa, aliyeshindwa kuzuia hasira yake kwa watoto wa Israeli, alishindwa kuzuia hasira yake mbele ya wanafunzi wake.
Mr. G alimlilia Mungu, huku akikimbilia katika ofisi iliyokuwa karibu, “Nimepitiwa, Bwana! Siwezi kufundisha tena!” Kwa ukimya, neema ya upole na huruma ya Yesu ilifariji moyo wake, ikileta toba. “Wengi walio makini sana, na wanaotamani kuishi kwa ajili ya Bwana, mara nyingi [Shetani] huwaongoza kudumu katika matatizo na madhaifu yao wenyewe, na hivyo kwa kuwatenga kutoka kwa Kristo anategemea kupata ushindi… Pumzika kwa Mungu. Ana uwezo wa kuweka kwake yale uliyotenda. Ukijiachia katika mikono yake, atakuvusha ukiwa zaidi ya mshindi katika yeye aliyekupenda” (Steps to Christ, uk. 71, 72).
Alipokuwa akiomba, wazo lilimjia, “Huwezi kukaa katika ofisi hii kwa siku nzima; unapaswa kwenda na kuwaambia vijana wale kwamba uliniwakilisha vibaya kwa matendo yako.” Kwa unyenyekevu, alirudi kwa wavulana wale, waliokuwa wamesimama nje na kujilaumu kwa hasira zake. “Sikumuwakilisha Yesu leo, na ninaomba mnisamehe,” aliwaomba msamaha. Wavulana walijaribu kumfariji wakisema, “Ni sawa! Kila mmoja hufanya hivyo. Ni kawaida!”
Kipindi cha Mr. G kilichofuata siku hiyo kilikuwa cha Biblia. Aliwapatia wanafunzi wake kazi ya kusoma sura ya tano ya kitabu cha Jipatie Amani Moyoni. “Kujitoa kwa Mungu,” na kuandika wazo lililomvutia. Alipoingia darasani, hakujisikia tayari kihisia kuweza kufundisha. Wanafunzi waliingia na kuketi, na mmoja kati ya wasichana aliweka kazi yake mezani. Mr. G. aliangalia chini, na macho yake yalitua katika sentensi moja: “Tumaini lako halipo ndani yako; lipo ndani ya Kristo” (Steps in Christ, uk. 70). Sentensi hiyo moja ndiyo kitu pekee alichohitaji.
Miaka iliyofuata baadaye, alipokea barua kutoka kwa mmoja wa wavulana wale. “Ninafahamu kwamba hukufurahishwa na matendo yako siku ile katika darasa la useremala,” barua ilisomeka. “Lakini ninataka ufahamu kwamba mfano wako wa kujinyenyekeza na kurekebisha mambo, kutuomba msamaha, ulinena mengi ndani ya moyo wangu. Sasa nikiwa baba, mara nyingi nimekuwa nikiwaomba watoto wangu msahama ninapokosea, na kwa sababu ya mfano wako, umenisaidia kuwa baba bora.”
“Tunapaswa mara nyingi kuinama na kulia katika miguu ya Yesu kwa sababu ya madhaifu na makosa yetu, lakini hatupaswi kuvunjwa moyo. Tunaposhindwa na adui, hatujatupwa, hatujaachwa na kukataliwa na Mungu. La hasha; Kristo yupo mkono wa kume wa Mungu, akituombea” (Steps to Christ, uk. 64).

Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwa sababu ya Wakili wetu, Yesu Kristo, anayeomba kwa niaba yetu.
• Tunakusifu kwa sababu unaweza kugeuza kushindwa kwetu kuwa ushindi.
• Tunakusifu, Bwana, kwa kuwa hata tukianguka, hatutashindwa kuinuka, wala hatutasononeka na kutelekezwa.

Kuomba na Kusihi

Bwana, tunakuomba utupatie Roho yako ya amani tunapokabiliwa na masumbufu.
Tunaombea shule 8,208 za Kiadventista zenye wanafunzi karibia milioni 2. Hebu shule hizi zifundishe ukweli wa Biblia daima na kuwaongoza vijana katika utume na huduma.
Bwana, tupatie hekima ya kufikia tamaduni zisizo na dini na ambazo hazina shauku katika mambo ya dini. Mruhusu Roho wako Mtakatifu avunje kuta zinazozunguka mioyo isiyo na dini. 
Tunaomba kwa ajili ya watu ambao hawajafikiwa bado katika Asia, wakiwemo Waislamu, Wabudha, na Wahindu. Pengine hawajawahi kusikia jina la Yesu. Tupatie hekima ya pekee ya kufikia mahitaji yao. 
Tubariki kadiri tunavyowafikia watu waliotekwa na ibada ya mizimu, ibada ya sanamu, na imani kwa vitu vingine. Tusaidie kuelewa mtazamo wao na kuwatambulisha kwa Mwokozi binafsi. 
Bwana, tafadhali hamasisha Waadventista wa Sabato ulimwenguni kuomba ambavyo hawajawahi kuomba. Hebu na tusihi pamoja kwa ajili ya mvua ya masika ya Roho Mtakatifu. Tunakuomba utimilifu ulioahidiwa wa Yoeli 2, Hosea 6, na Matendo 2.
Tunaomba kwa ajili ya makundi 541 ya watu katika nchi 18 za Divisheni ya Kusini mwa Afrika – bahari ya Hindi. Tafadhali waelekeze katika ukweli wa Biblia. 
Tuonyeshe namna ya kuwatimizia wakimbizi mahitaji ya kimwili na ya kiroho. Hebu kanisa letu lifahamike kwa upendo wetu kwa watu wote, bila kujali ni watu wa aina gani, au wametoka wapi. 
Tunaomba kwa uaminifu na ukamilifu tutangaze ujumbe wa malaika watatu wa Ufunuo 14. Hebu na tuweze kuyakita mafundisho yetu yote katika upendo na haki ya Kristo. 
Tunaomba pia kwa ajili ya orodha yetu ya watu saba au zaidi [taja majina halisi].

Kushukuru

Asante, Bwana, kwa kuwa unaweza kutuepusha na kuanguka (Yuda 24). 
Asante kwa toba, msamaha, na upatanisho.
Tunakushukuru kwa mfano wa huduma ambayo Kristo alituachia. Tafadhali tupatie nguvu ya kufuata mfano wake.

Mapendekezo ya Nyimbo za Kuimba

Namtaka Bwana Yesu #145
Ni Wako Bwana #144
Nitwae Hivi Nilivyo #140

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yohana 1:9). • “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki” (1 Yohan 2:1).


Siku ya Saba
Utukufu wa Kusudi

Fungu Elekezi “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” Mathayo 25:40.
“Kazi ile inayoweza kuonekana kwa mioyo yenye ubinafsi kama ni huduma inayodhalilisha, kuwahudumia wale walio wanyonge na kwa kila namna wakionekana kuwa duni katika tabia na nafasi katika jamii, ndiyo kazi wanayofanya malaika wasio na dhambi. Roho ya upendo wa Kristo wenye kujitoa ni roho iliyoenea mbinguni na ni kitovu cha furaha yake. Hii ni roho ambayo wafuasi wa Kristo watakuwa nayo, katika kufanya kazi” (Steps to Christ, uk. 77).
“Bwana, sidhani kama naweza kufanya kazi hii! Umefaya kosa kubwa sana safari hii! Ninataka kukufanyia kazi, lakini siyo hapa!” hiki ndicho kilikuwa kilio changu kwa Bwana baada ya kuniweka katika shule mbadala ya vijana waliohtaji kukamilisha elimu yao na kujiandaa kwa ajili ya kazi ulimwenguni. Wengi wa watoto hawa walikuwa ni wale wasio na makazi, wahanga wa unyanyasaji, au waliohusishwa katika makundi mabaya, madawa ya kulevya, na hata ukahaba. Nilitumia miaka zaidi ya 20 kufundisha katika maeneo ya shule ya Kikristo, na kazi hii mpya ilionekana kuwa zaidi ya kile nilichoweza kuhimili.
Siku ya kwanza wanafunzi waliingia darasani wakiwa wameshikilia nguo zao na wakiwa wamevaa skafu zilizofunika nyuso zao. Matatizo yalitokea katika saa ya kwanza kijana mmoja alipoanza kupiga kelele akitishia vijana wengine wawili kwa maneno machafu. Naam, nilitekewa nikiwa nje kabisa ya hali yangu ya amani, huku ugomvi ukikaribia kuanza. Niliogopa. Lugha ya ukatili, muziki, na picha zilizoonekana katika kompyuta zao zilinifanya nitamani mazingira yangu yenye usalama. Sikustahili kuwa hapa. Nilijihisi kama mwanakondoo kati ya mbwa mwitu; kama wanafunzi kwenye bahari iliyochafuka, nililia, “Bwana, niokoe!”
Nilikuwa nimesoma Yeremia katika ibada yangu, na Bwana akaniletea akilini maneno haya: “’Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana… Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe,’ asema Bwana, ‘ili nikuokoe’” (Yeremia 1:8, 19).
Nilipokuwa nikiomba kwa ajili ya msaada, nikimsihi Bwana atimize neno lake alilompatia Yeremia na kuleta amani ndani ya darasa lile. Kisha, kwa ujasiri usio wa kawaida, niliwaambia wanafunzi, “Sitaruhusu tabia ya aina hii katika darasa hili. Kila mmoja wenu anapaswa kuketi na kwa ukimya aanze kufanya kazi zake.” Fikiria mshangao wangu walipoitikia kwa ukimya! Nilimtukuza Mungu moyoni mwangu, nikimsifu kwa wema na rehema zake. Katika majuma machache yaliyofuata, niliendelea kumsihi Bwna kunitoa katika maeneo haua ya kazi. Niliamini sikuwa mmoja wa pale. Alijibu maombi yangu kwa namna isiyo ya kawaida – kwa kunionyesha hali ya moyo wangu mwenyewe.
Nilikuwa nikifanya kazi na mwanafunzi mmoja wa kiume katika kompyuta aliponiuliza swali la ajabu, “Jodi, ulitokea kwenye shue ya Kikristo, ni kweli? Nilipojibu, “Ndio,” alisema, “Sasa ni kwa nini upo hapa nasi?” Swali lake lilichoma moyo wangu. Bwana alinishawishi, “Haupo tayari kuhudumia ulimwengu. Hadi utakaposonga zaidi ya chuki na huzuni zilizojengeka ndani yako ndipo utakapoweza kudhihirisha upendo wangu kwa watoto hawa. Upo hapa kufanya tofauti katika maisha yao, kudhihirisha tabia yangu kwao.” Mungu alikuwa sahihi! Sikuwa tayari kuhudumu kwa sababu sikuwa na upendo. Basi nilimjibu kuwa, “Nahisi ninahitaji tu kuleta tofauti katika maisha yako.” Baadaye mchana, tukio kama hilo lilitokea, wakati huu akiwa binti mdogo.
Ni tofauti gani ninayoweza kuleta? Nilianza na mambo madogo, kama kutoa chakula cha asubuhi cha afya ili waweze kuanza siku kwa chakula kizuri. Nilivuta ujasiri wao kwa kusikiliza hadithi zao na kuingia katika mateso yao na kuwa rafiki na mshauri.
Sunami ilipoikumba Asia, wanafunzi walitaka kugundua kile nilichofikiria kuhusu janga hilo. Niliwaambia kwamba sunami ilikuwa ni dalili ya ujio wa Yesu unaokaribia. Mmoja wa wanafunzi wangu, aliyedai kwamba alikulia kanisani, alisema, “Jambo hilo halizungumziwi katika Ufunuo?” Nilimualika kusoma kifungu. Wanafunzi walikuwa watulivu sana nilipoelezea kwamba Yesu alikuwa akitoa angalizo kwa ulimwengu kujiweka tayari. Niliongeza kwamba kama mtu ye yote angetaka kufahamu namna ya kujiandaa na ujio wa Yesu, ningefurahi kumuelezea. Baadaye siku hiyo, msichana mmoja alikuja ofisini kwangu na kusema, “Tafadhali, ninahitaji kufahamu.” Nilimwambia kuhusu upendo wa Yesu kwake na kwa kijana wake na nilimuongoza kumpokea Kristo kama Mwokozi wao. Kwa mwaka mzima, nilikuwa na fursa kadhaa za kumtambulisha Yesu kwa “watoto wangu” na kuwaongoza kumkubali.
“Kamwe Mungu hawaongozi watoto wake tofauti na vile ambavyo wangechagua kuongozwa, kama wangeweza kuona mwisho toka mwanzo, na kutambua utukufu wa kusudi wanalolitimiza kama wafanyakazi pamoja Naye” (Conflict and Courage, uk. 278).
Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwa jinsi unavyokuwa mwepesi kuhisi mateso yetu.
• Tunakusifu kwa wale waliotulea katika imani, wakituongoza katika uhusiano wa karibu na Yesu.

Kuugama na Kudai Ushindi Dhidi ya Dhambi
• Baba, tafadhali tuonyeshe dhambi tunazopaswa kuungama kwa wazi na zile tunazopaswa kuungama kwa siri. Tunadai ushindi wako dhidi ya dhambi hizo.
• Baba, tusamehe kwa sababu ya kuwa na mashaka kwa uongozi wako. Tuusamehe kwa kujaribu kutafuta namna yetu wenyewe ya kujitoa katika hali zinazotupatia changamoto, wakati wewe ulituweka hapo kwa sababu maalum.
• Tusamehe nyakati tuliporuhusu hofu au chuki kutuzuia kushiriki upendo wako na wengine.

Kuomba na Kusihi
• Bwana, tunaomba kwa ajili ya ulinzi wako kwa watoto na vijana wadogo wenye hatari ya kuumizwa. Tunaomba kwamba uwalinde kutoka kwa wale wanaojaribu kuwaharibu.
• Bwana, tunawaombea wale wanaotunza watoto wasio na makazi wawezeshe kuwa na mioyo ya uhuruma, mikono ya upole, na maneno ya ukarimu.
• Tunaomba kwa ajili ya wanafamilia wa watoto walio katika uasi dhidi ya utawala. Tafadhali wapatie neema ya kushughulika na hali hiyo kwa upole.
• Tunakuomba uweze kuinua wamisionari wa mijini ili kuanzisha makanisa kwa makundi 806 ya watu katika nchi 20 za Divisheni ya Ulaya.
• Tafadhali inua jeshi kubwa la watenda kazi ili kuanzisha makanisa kwa ajali ya makundi 948 ya watu katika nchi 38 za Divisheni ya Amerika.
• Tunaomba kwa ajili ya mizigo ya moyo ya washiriki wa kanisa letu na kila mmoja aliyepo katika muda huu wa maombi.
• Tunainua majina saba tuliyoandika katika karatasi zetu. Baba, wewe pekee ndiye ujuaye hali za marafiki zetu, familia, na wanafanyakazi wanaokutana nao. Waongoze katika njia yako na wavute karibu nawe.

Kushukuru
• Asante kwa upendo wako usioshindwa na huruma yako kwetu. • Baba, asante kwa kututazama kwa upendo. • Asante kwa kutuelewa na kutuhurumia katika madhaifu yetu.

Nyimbo Zinazopendekezwa:

Waponyeni Wafu #56 
Kuwatafuta #100
Fanyeni Kazi Zenu 59
Popote Mashamba Yajaa #94

Ahadi za Kudai Unapoomba

“Mfanyieni hukumu maskini na yatima; Mtendeeni haki aliyeonewa na fukara; Mwokoeni maskini na mhitaji; Mwopoeni mikononi mwa wadhalimu” (Zaburi 82:3, 4). 
“Naam, Bwana asema hivi, Hata jeshi la wafungwa wake aliye hodari watapokonywa mikononi mwake, na mateka yake aliye jabari wataokoka; kwa maana nitateta na yeye atetaye nawe, nami nitawaletea wana wako wokovu” (Isaya 49:25). 
“Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa” (Yakobo 1:27). 

Siku ya Nane
Katika Bonde

Fungu Elekezi: “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa” Zaburi 34:18.
Tulikuwa katika safari ya wiki mbili kwenye mji wa Iloilo, Ufilipino, nilipoitwa kwenye ofisi ya kanisa ya masuala ya biashara. “Dada, una simu kutoka Marekani – njoo haraka!” Moyo wangu ulidunda kadiri nilivyokimbia kuelekea ofisini kupokea simu ile. Nikiwa ninahema, nilisema, “Halo?” Upande wa pili ilisikika sauti yenye woga ikisema, “Jodi, Danny amefariki!” niligusa kifua change nikiwa siamini. “Imekuwaje? Ni nini kimetokea?” niliuliza.
Kaka yangu mdogo kabisa, Frank, alinipatia taarifa kwamba kaka yetu mkubwa, Danny, aliyekuwa mlevi na mtumia madawa, alipatikana akiwa na sindano kwenye mkono wake ndani ya chumba cha hoteli. Alizidisha madawa ya heroini yaliyochanganywa na pombe. Kwa mshtuko, nilikata simu na kuanguka nikilia mikononi mwa mume wangu. Nilikuwa mbali sana na nyumbani, sikuweza kukimbilia upande wa familia yangu, hivyo ilinibidi kusubiri wiki nyingine hadi safari yetu ilipoisha.
Katika safari ndefu ya ndege kuelekea nyumbani, kumbukumbu za utoto wangu zilitawala akili yangu. Nilikumbuka nyakati za pekee nikicheza na kaka yangu. Nilikumbuka namna alivyokuwa akinilinda. Niliwaza kuhusu maisha ya Danny, juu ya chaguzi alizokuwa amefanya. Moyo wangu ulitamani awe na maisha bora zaidi, maisha ya kumfahamu Mungu na kupata amani na kuridhika.
Danny hakupata shida kufanya marafiki. Alionekana kuwa “maarufu.” Lakini alipoingia sekondri, marafiki zake walikuwa wale waliopenda sherehe, kunywa pombe, na kujaribisha madawa ya kulevya. Haikuchukua muda mrefu kwa Danny kuwa mlevi na teja wa madawa, jambo ambalo lilimfanya kuwa mgeni wa mara kwa mara katika jela la mkoa na vituo vya kimahakama vya kutibu waraibu. Mwishowe, mwanasheria aliyeteuliwa na mahakama alimwonya Danny kwamba kama asingeondoka mjini na kwenda mbali na marafiki zake, kwa hakika angeishia gerezani. Hivyo dani alikuja kuishi pamoja na mimi na mume wangu kwa muda.
Alipokuwa nyumbani kwetu, Danny alionyesha shauku katika mambo ya kiroho. Alishiriki katika ibada zetu za familia na hata kujiunga na kozi ya kujifunza Biblia. Alifahamu majibu yote sahihi na alimaliza masomo yake kwa muda sahihi. Maisha yake yalianza kubadilika na, akijiamini kuwa sawa, alirudi nyumbani. Muda mchache, alirudi kwa marafiki zake wa zamani na kwenye madawa – muda huu kwa nguvu zaidi, akitumia madawa yenye nguvu zaidi, ambayo hatimaye yalichukua maisha yake. Ni kwa namna gani jambo hili liliuvunja moyo wa Mungu kumuona yule aliyemlipia thamani kubwa ya wokovu katika hali hiyo, kushushwa kwenye utumwa wa mazoea. “Upendo wa kimbingu hutoa machozi ya uchunguzi kwa wanaume walioumbwa kwa mfano wa Muumbaji ambao hawatakubali upendo wake” (The Spirit of Prophecy, Vol. 3, uk. 13).
Niliumia sana kwa ajili ya Danny. Tulipokuwa tukiona jinsi alivyopambana dhidi ya uraibu, ilikuwa ikiumiza sana familia yetu. Mara nyingi aliwaonea wazazi wetu, akiwaibia ili aweze kukidhi mahitaji ya uraibu wake na mara nyingi kusema uongo ili kuficha vitendo hivyo. Hawakuweza kumruhusu kuendelea kuishi nyumbani kwao, hivyo akawa mtu asiye na makazi. Hali hiyo iliuvunja moyo wa mama yangu akimfikiria kijana wake anavyolala mitaani wakati wa baridi, akila katika makazi ya watu, kama aliweza kula, huku akizunguka mitaani akitafuta madawa zaidi. Mara nyingi mama alimpatia “nafasi ya pili” lakini kamwe hakubadilika. Alikufa akiwa peke yake. Ninaogopa sana ulimwengu huu na uongo wa Shetani kwa walio dhaifu na wasio na Kristo. Kamwe haukuwa mpango wa Mungu kwamba wanadamu waishi wakipata maumivu na upweke, wakiwa wamefungwa na Shetani.
Mara nyingi huwa najiuliza ikiwa kweli Danny aliamini kwamba Mungu alimpenda. Ninajiuliza kilichokuwa kikizunguka akilini mwake katika nyakati zile za mwisho za maisha yake. Je, alimuita Mungu? Je, ataokolewa? Kamwe sitafahamu jibu katika maisha haya, lakini nina uhakika kwamba Baba yetu wa Mbinguni aliweka mkono wake kwa Danny tangu wakati alipozaliwa. Ninafahamu kwamba upendo wa Mungu ulikuwa rafiki wake wa kudumu, daima akimvuta kwa upendo na kumpatia wokovu.
Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwa ajili ya zawadi ya Yesu, aliyekufa ili kutuokoa sisi na wapendwa wetu.
• Bwana, tunakusifu kwa kuwa unatsikia tunapozungumza nawe na kwamba unatujibu kulingana na mapenzi yako.
• Tunakusifu kwa nguvu yako ibadilishayo maisha.


Kuungama na Kudai Ushindi Dhidi ya Dhambi
• Baba, tafadhali tuonyeshe ni dhambi zipi tuziungame kwa siri. Tunadai ushindi dhidi ya dhambi hizo. • Tusamehe kwa nyakati ambazo hatukuwa tayari kufuata mapenzi yako yaliyoandikwa katika Neno Lako.
• Tunakushukuru kwamba unatusamehe kulingana na andiko la 1 Yohana 1:9.

Kuomba na Kusihi
• Baba, tunasihi kwa ajili ya wale ambao wanaweza kuwa wahanga wa mazingira au wanaoongozwa na uraibu. Tafadhali vunja vifungo vinavyowafunga! Tunaomba tuweze kuwarudisha kwako kupitia katika upendo na kujali kwetu.
• Bwana, tafadhali tupatie mioyo yenye uelewa na huruma kwa ajili ya wanafamilia ambao wametutumia vibaya. Wasaidie waweze kuona upendo wako kupitia matendo yetu.
• Tafadhali tufundishe namna ya kutangaza misingi ya kanisa letu kwa uwazi, ubunifu, na uhalisia wa Kiblibia. Upendo wa Yesu n kawe kiini cha kila tunachokiamini. • Tunakuomba uwaandae vijana kuanzisha makanisa kwa ajili ya makundi 789 ya watu katika nchi 9 za Divisheni ya Kaskazini mwa Amerika.
• Tunakuomba uandae watu wa kujitolea ili kuhudumia makundi 70 ya watu katika Fildi ya Israeli.
• Tunakuomba uinue wamisionari wa kitabibu ili kuanzisha makanisa kati ya makundi 830 ya watu kwenye nchi 11 za Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati.
• Tunakuomba uinue askari wa maombi ili kuomba kwa ajili ya makundi 2,568 ya watu katika nchi 4 za Divisheni ya Kusini mwa Asia. Tunakumbuka hasa Televisheni ya Hope (Hope TV) India na Shule ya Kisasa ya Vipofu.
• Tunaomba kwa ajili ya wafanya kazi wa nyumba za uchapishaji katika Divisheni ya Kusini mwa Asia – Pasifiki.
• Tunaomba kwamba utafanya kama ulivyahidi katika Zaburi 32:8, kwa kutuongoza na kutuelekeza kadiri tunavyofanya Changamoto ya Kuwafikia Watu Katika Siku Kumi za Maombi.
• Tunakushukuru, Baba, kwa kumtuma Roho wako Mtakatifu kuwabadilisha wale watu saba katika orodha yetu ya maombi.

Kushukuru
• Bwana, tunakushukuru kwamba Shetani hana nguvu tena dhidi yetu.
• Tunakushukuru kwamba unaweza kutoa mlango wa kutokea ili kwamba jaribu lisitutawale (1 Wakorintho 10:13).
• Tunakushukuru kwamba unapotuweka huru, tunakuwa huru kweli kweli! (Yohana 8:36).
• Tunakushukuru, kwa kujibu maombi yetu, kabla hatujapokea majibu.Nyimbo Zinazopendekezwa
• Hivi Nilivyo Unitwae #140
• Moyo Safi #116
• Naendea Msalaba #115

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu” (Wafilipi 4:19).
• “Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao” (Zaburi 147:3).
• “Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo” (Zaburi 91:2, 3).
• “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17).


Siku ya Tisa
Nguvu Kubwa Kuliko Mashaka

Fungu Elekezi: “Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile” (2 Timotheo 1:12).
“Vipimo vinaonesha majibu ni chanya, una ujauzito! Sikuweza kusubiri kushiriki habari hizi njema pamoja na mume wangu. Binti yetu alikuwa anakaribia miaka miwili, na ujauzito huu ungewaachanisha watoto vizuri. Furaha yetu iligeuka huzuni, hata hivyo, si mara moja, bali mara mbili. Baadaye siku hiyo hiyo nilipata maumivu katika tumbo langu la chini na kuishia hospitali. Vipimo vilithibitisha wasiwasi wa daktari – mimba iliyokuwa imetungwa nje ya kizazi. Mmoja katika mirija yangu ya falopia ulikuwa umepasuka, na kusababisha kuvuja kwa damu ndani ya mwili kulikohatarisha maisha. Upasuaji ulitibu madhara ya kimwili, lakini si moyo wangu ulioumia.
Baada ya miaka mingi ya kushindwa kupata ujauzito, daktari wangu aliniambia kwamba haikuwezekana kwa sababu ya mkusanyiko wa seli za mwili zilizoharibiwa kutokana na utoaji mwingi wa damu. Nilikusudia kumdhihirishia kwamba amekosea! Moyoni mwangu nilisema, “Ninamtumikia na kumtumaini Mungu mkuu; Alifanya muujiza kwa Sara, akimruhusu kupata ujauzito kinyume na asili yote, na ana uwezo wa kufanya muujiza kwangu pia.” Niliweka imani yangu yote mikononi mwa Mungu, na haikuchukua muda mrefu kabla ya kujikuta ni mjamzito tena. Mungu alijibu ombi langu! Tulijawa na furaha sana. Imani yetu katika ahadi za Mungu na upendo wetu kwake uliongezeka.
Mimi na mume wangu tulikuwa tukitembea kando ya mto mtulivu siku ya Sabato mchana nilipohisi maumivu niliyowahi kusikia ndani yangu. Nilishahisi hivi hapo kabla, lakini niliyatuliza haraka. Baadaye jioni ile, maumivu yalizidi, na tena, niliishia hospitali. Vipimo vilithibitisha hofu yangu – ilikuwa mimba ya pili iliyotungwa nje ya kizazi, na nilihitaji upasuaji wa haraka.
Ni nini kinachotokea pale Mkristo anapoweka imani yake yote katika ahadi za Mungu, na hatimaye kukatishwa tu tamaa? Yako wapi mema yaliyonenwa katika Warumi 8:28? Mawingu ya mashaka yalinifunika. Nikajiuliza kuwa, Kwa nini, Mungu? Sielewi! Kwa nini ulijibu ombi langu, kisha kuondoa tena majibu? Kwa nini umeniangusha?
Nililala katika kitanda changu hospitalini nikijihisi kuvunjika moyo sana. Kimwili nilikuwa na maumivu na nilikaushwa kihisia. Sikutaka kumuona ye yote! Nesi wangu alinihakikishia kwamba maji ya moto yangenisaidia kujisikia vizuri zaidi na alinisaidia kuingia bafuni. Machozi yalidondoka usoni kwangu. Wazo la kuomba lilinijia, lakini sikuweza. Nilihisi kama vile Mungu amenitelekeza. Mvuke kutoka kwenye bomba la maji ulikuwa kama mawingu meusi ya dhoruba. Ibilisi hakuchelewa kujitokeza, akipendekeza kuwa: “Je, hivi ndivyo Mungu anavyowalipa wale wanaoweka imani yao kwake? Je, hivi ndivyo anavyoonesha upendo wake?”
Lakini Mungu hakuwa ameniacha. Nilishawishika kurudia maneno yafuatayo kwa sauti: “Mungu ananipenda.” Sikuwa na uhakika kama ningeweza – au hata nilitaka kusema hivyo. Lakini nilishawishika mara ya pili kwa uzito mkubwa, hivyo nikasema, “Mungu ananipenda.” Nilirudia maneno hayo hayo mara tatu, kila saa nikisisitiza neno tofauti. “MUNGU ananipenda.” “Mungu ananiPENDA.” “Mungu ANANIpenda!” Nilipotamka mara ya tatu, giza lote lilinitoka! Nilirudi katika kitanda changu nikiwa nimechoka sana na nilitaka kuwa mwenyewe.
Kasisi wa hospitali hiyo alipoingia katika chumba changu, aliangalia katika chati yangu na kuuliza, “Mrs. Genson?” Nilipoitika, alikuja upande wangu na kunishika mkono, akisema, “Ni vigumu sana kupoteza mtoto, sivyo? Mawingu yalirudi! Nikiwa sitaki kulia mbele yake, nilifunika kichwa changu kwa blanketi na kusema kwa sauti, “Mungu ananipenda! Ninamfahamu niliyemwamini! Nimempatia Kristo maisha yangu, na kile anachoamua kufanya kwangu ni SAWA, kwa sababu maisha yangu yamefichwa ndani ya Kristo.” Kwa maneno haya, mawingu yaliniacha tena.
Maneno ambayo Yesu alimwambia Petro baadaye yalileta faraja katika moyo wangu: “Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye” (Yohana 13:7). Niligombana na Mungu kuhusu kukosa kwangu. Sikuweza kuelewa kwa nini jambo hilo lilitokea, hasa nilipokuwa nikifanyia kazi imani yangu. Ingechukua miaka kumi kabla sijaelewa kwamba Mungu alitaka nipitie imani ambayo inapaswa kuvuka mawingu hadi kwa visivyoonekama, kwamba neema yake hufanywa kamilifu katika madhaifu yetu. Niliomba muujiza, na Mungu alinipatia. Nilijifunza kwamba muujiza wa kweli ni kwamba nguvu za Mungu zilikuwa zaidi ya mashaka yangu na kwamba angeweza kunishikilia katika magumu yo yote. Kama Ayubu, ninaweza kusema, “Tazama, ataniua; sina tumaini; ila hata hivyo nitaithibitisha njia yangu mbele yake.” “Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu” (Ayubu 13:15; 23:10).
“Mungu anatupatia masomo ya imani. Anaweza kutufundisha tunapopaswa kutafuta msaada na nguvu nyakati za shida. Hivyo tunapata ufahamu halisi wa nia yake ya kimbingu, ambao tunahitaji sana katika maisha yetu. Imani huwa imara katika mapambano dhidi ya mashaka na hofu” (Testimonies, vol. 4, uk. 116, 117). “Katika maisha yajayo mafumbo yaliyotukasirisha na kutuvunja moyo yatawekwa wazi. Tutaona kwamba maombi yetu yanayoonekana kutokujibiwa na matumaini yaliyovunjika yamekuwa kati ya mibaraka yetu mikubwa” (The Ministry of Healing, uk. 474).
Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwamba wewe ni Baba wa huruma, na Mungu wa faraja (2 Wakorintho 1:3-7).
• Tunakusifu kwa kuponya mioyo yetu iliyovunjika na kutufunga majeraha.
• Tunakusifu kwa kuturuhusu kuweka mizigo yetu kwako. Utatutegemeza katika nyakati zetu za huzuni, kwani umepitia katika huzuni.

Kuungama na Kudai Ushindi Dhidi ya Dhambi
• Tunaomba Roho Wako Mtakatifu atuonyeshe dhambi zinazotutenga na wewe.
• Tusamehe, Baba, mashaka yetu yanapofunika uwezo wetu wa kukuamini.
• Tunakushukuru kwa msamaha unaoutoa kwetu.

Kuomba na Kusihi
• Bwana, tunaomba hekima na neema ya kukubali mambo yanayotukatisha tama, tukifahamu kwamba unatupenda na utatutendea mema, ingawa hatuwezi kuelewa sasa. • Tunaomba kwamba imani yetu iimarishwe kadiri tunavyokabili mashaka na hofu.
• Tafadhali ruhusu familia zetu kudhihirisha upendo wako katika nyumba na jamii zetu. Tunakuomba ulete uelewano katika nyumba zetu, uponye mahusiano yaliyovunjika, ukilinda walio katika hatari ya kunyanyaswa, na udhihirishe nguvu yako ya kutakasa katika hali zinazoonekana kukosa tumaini.
• Tunaombea washiriki, wachungaji, na viongozi wetu ulimwenguni wajilishe neno la Mungu kila siku. Pia tukutafutea kila siku katika maombi binafsi. Tukumbushe kwamba bila Wewe, hatuwezi kufanya lo lote.
• Tunakuomba uinue wauguzi na madaktari ili kuanzisha makanisa katika makundi 1,978 ya watu kwenye nchi 22 za Divisheni ya Afrika Magharibi na Kati. • Tunaomba kwa ajili ya watu milioni 49 katika miji 19 ya Divisheni ya Ulaya ambao haijafikiwa sana.
• Tunaomba kwa ajili ya watu saba katika orodha zetu za maombi. Wapatie mioyo ya kukufahamu kama Neno Lako linavyosema katika Yeremia 24:7.

Kushukuru
• Baba, tunakushukuru kwamba kwa sababu Kristo anatuombea, tuna tumaini na matazamio ya mbeleni.
• Tunakushukuru kwa kutufariji katika matatizo yetu yote, ili tuweze kuwafariji wengine.
• Tunakushukuru, Mungu, kwamba nguvu yako hukamilishwa katika madhaifu yetu.

Nyimbo Zinazopendekezwa
• Yesu Kwa Imani #123
• Ni Salama Rohoni Mwangu #127
• Cha Kutumaini Sina #69

Ahadi za Kudai Unapoomba
• “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28).
• “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu” (Isaya 41:10).
• “Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele” (Zaburi 55:22).


Siku ya Kumi
Achia Masumbufu
Fungu Elekezi: “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu” Wafilipi 3:13, 14. Baba yetu aliyetuzaa alitutelekeza mimi na kaka yangu mkubwa. Kwa sababu alimwacha mama yetu tulipokuwa wadogo sana, hatujawahi kukutana nae. Kitu pekee tulichofahamu kumhusu ni kwamba alikuwa nahodha, mrefu na mzuri, mwenye nywele nyekundu na madoa kwenye ngozi, na alizungumza kwa lafudhi ya kusini. Harakati zote za kumtafuta hazikufanikiwa, hivyo tulikata tamaa. Nilikuwa nikijiuliza kuwa ni kwa nini hakututaka, jambo ambalo liliacha kovu katika moyo wangu mdogo. Nilikuwa mzito, mara nyingi nikianguka bila “sababu” uwanjani. Nilichekwa shuleni. Nywele zangu zilikuwa fupi na zilinyolewa muundo wa boksi kuzunguka uso wangu dhaifu. Macho yangu yalikosa mng’ao wa furaha ambao unapaswa kumtambulisha mtoto wa miaka minane. Mara nyingi nilikuwa sehemu kubwa ya kuelekeza utani.
Kwa sababu mara nyingi nilikuwa nikicheza peke yangu, kipindi cha mapumziko ndio muda wa siku ambao sikuupenda, lakini muda wa darasa la mazoezi ulikuwa mbaya zaidi. Tulicheza mpira wa besiboli, ambao niliuchukia. Mchezo huo ulihusisha kupiga teke mpira na kukimbia kuzunguka katika vituo vya mchezo huo. Kadiri watoto walivyopanga mstari, manahodha walichagua timu zao. Kila mara nilikuwa nikichaguliwa wa mwisho. Timu zilisimama katika nafasi zake, na nilikuwa nikipelekwa sehemu ya mbali ya uwanja kwa sababu sikuwa mzuri sana katika mchezo huo. Timu yangu ilipoanza kupiga kelele, “Rudi nyuma! Timmy anakuja!” kila mara Timmy alikuwa akipiga mpira kwa nguvu sana. Nilikuwa nikisimama nikiwa nimekunja mikono yangu. Ghafla, nilisikia kelele, “Ewe DeWeese mjinga! Mpira unakuja kwako! Udake!” Huku nikitazama juu, niliona mpita ukija moja kwa moja kwangu. Nilikunjua mikono yangu na kuudaka! Watoto walipiga kelele za shangwe wakiwa hawaamini, “Oooh, DeWeese mjinga amedaka mpira!” kwa muda mchache, nilikuwa shujaa, niliyesifiwa na wanadarasa wenzangu, lakini sifa zilidumu kwa muda mchache sana. Mambo yalirudi katika hali ya kawaida ilipokuwa zamu yangu kupiga teke mpira na kuanguka, nikiisababishia timu yangu kushindwa mchezo.
Hali ya kukosa usalama na kutojiamini iliambatana nami katika ujana wangu na utu uzima. Matukio katika miaka ya awali ya utoto huweza kuathiri tutakavyokuja kuwa hapo baadae, lakini hatupaswi kuishi hivyo. Nilikuwa na haki zote za kuwa na hasira; kwani, nilikataliwa na baba yangu, sikuwa na marafiki, na ilikuwa rahisi kwa watu kunionea kwa sababu nilitamani kukubaliwa. Kadiri nilivyozidi kufikiri juu ya hayo, ndivyo yalivyozidi kuwa uhalisia. Nilikusanya rundo la miiba. Lakini kushikilia uzoefu wa nyuma, kwa namna ya uchungu ule ule uliokuwa hapo awali, huwa mzito zaidi na hatimaye huweza kuathiri afya zetu. Tunakuwa watumwa wa hisia zetu. Hivi karibuni nilisoma nukuuu hii ya Ellen White: “Wengi, wanaotembea katika safari ya maisha, hufikiri sana makosa na mambo waliyoshindwa na masikitiko, na mioyo yao hujazwa na huzuni na kukata tamaa.
Nilipokuwa Ulaya, dada aliyekuwa akipitia hali hii, na aliyekuwa katika msongo mzito, aliniandikia, akiniomba baadhi ya maneno ya kutia moyo. Usiku uliofuata baada ya kusoma barua yake niliota kwamba nipo katika bustani, na aliyeonekana kuwa mmiliki wa bustani hiyo alikuwa akinitembeza kwenye njia zake. Nilikuwa nikikusanya maua na kufurahia harufu yake, wakati dada aliyekuwa akitembea kando yangu, alielekeza umakini wangu kwenye baadhi ya maua ya waridi mwitu ambayo yalikuwa yakizuia njia yake. Alikuwa akiomboleza na kuhuzunika. Hakuwa akitembea katika njia, akimfuata kiongozi, lakini alikuwa akitembea kati ya maua ya waridi mwitu na miba. ‘Oh,’ alilia, ‘Je, si huzuni kwamba bustani nzuri sana hii imeharibiwa na miba?” Kisha kiongozi alisema, ‘Iache miba, kwani itakuumiza tu. Kusanya maua ya waridi, na maua mengine mazuri.’ Je, hakukuwahi kuwa na madoa yang’aayo katika uzoefu wa maisha yako? … Unapotazama nyuma kwenye sura za uzoefu wa maisha yako, Je, hupati baadhi ya sura zinazofurahisha? Je, ahadi za Mungu si kama maua yenye harufu nzuri, yakikua kando ya njia yako pande zote? Je, hautaruhusu uzuri wake uujaze moyo wako kwa furaha? … Si jambo la busara kukusanya vitu vyote vilivyopita visivyofurahisha – udhalimu na masikitiko yake, - kuvizungumzia na kuviombolezea hadi tunapojazwa na kukata tama. Roho iliyokata tama imejawa na giza, ikifungia nje mwanga wa Mungu kutoka kwenye nafsi yake na kujaza kivuli kwenye njia za wengine” (Steps to Christ, uk. 116, 117).
Nilichagua kuachia miba yangu na kukusnya maua ya waridi. Kristo alipokuja katika maisha yangu, nilitambua mtu niliyekuwa ndani yake! Hapo kabla nilikuwa msichana mdogo mwembamba ambaye alifikiri hawezi kufanya jambo lolote kwa usahihi – lakini nikawa mtoto wa Mungu, binti wa kifalme wa Mfalme wa wafalme (1 Petro 2:9). Sio tena mtoto asiye na baba, kwani Mungu alikuwa Baba yangu (Zaburi 27:10; Yohana 16:27). Sio mtu wa kukataliwa tena na kutokuwa na marafiki, kwani Baba yangu wa mbinguni huniita rafiki yake (Yohana 15:15). Ninafahamu kwamba nina thamani kubwa, kwani alitoa maisha yake kwa ajili yangu (Yohana 3:16). Ni sababu kubwa ya kufurahia!
Mapendekezo ya Mfumo wa Muda wa Maombi
Sifa
• Bwana, tunakusifu kwa ajili ya nguvu yako ya kubadilisha!
• Tunakusifu kwamba umetuita sisi ni marafiki zako (Yohana 15:15).
• Tunakusifu kwa kutuchagua kuwa watoto wako.

Kuungama na Kudai Ushindi Dhidi ya Dhambi
• Bwana, tunadai ushindi wako dhidi ya dhambi katika maisha yetu.
• Tusamehe kwa kuchagua kufikiria “miba” ya wakati uliopita na kuruhusu uzoefu huo kutukatisha tamaa. Tunakushukuru kwamba tukiungama dhambi zetu, wewe ni mwaminifu na wa haki hata utusamehe dhambi zetu na kutusafisha (1 Yohana 1:9).

Kuomba na Kusihi
• Bwana, tunawainua viongozi wetu wa kanisa ulimwenguni kote. Tafadhali wapatie hekima kadiri wanavyokuwa wakifanya maamuzi ya muhimu na kuwaongoza watu wako.
• Tunaomba neema yako ili tuwasamehe wale waliotukosea. Bwana, tafadhali leta uponyaji na urejeshwaji katika familia zetu.
• Bwana, tunaomba kila mmoja wetu awe rafiki wa wasio na marafiki, tukidhihirisha upendo wa Mungu kwa wale wenye uhitaji wa upendo.
• Tunaomba kwa ajili ya watoto wetu. Tafadhali watie nguvu ya kusimama imara kwa ajili yako wanapokutana na vikwazo na misukumo. Wasaidie kufanya chaguzi sahihi na kusimamia ukweli (Isaya 44:3, 4).
• Tufundishe kufuata mfano wa Kristo usio na ubinafsi kwa kufikia mahitaji ya kila siku ya watu wanaotuzunguka. Tutayarishe kuwa wahudumu kama wamisionari wa kitabibu, watu wanaojitoa kuhudumia jamii, na marafiki kwa wahitaji.
• Bwana, tunaomba uamsho mkubwa wa uungu wa asili usafishe kanisa letu katika siku za mwisho. Tunaomba tuweze kusimamia ukweli hata mbingu zikianguka.
• Bwana, tuonyeshe namna ya kushiriki injili na makundi ya watu Waislamu. Tunaomba kwamba waweze kusikia na kuitikia zawadi yako ya neema.
• Tunaomba kwa ajili ya mbegu za ukweli zilizopandwa nchini Japani wakati wa mchakato wa mwaka jana wa kuwahusisha Washiriki wote (TMI Outreach) kuwafikia watu. Tafadhali tuma watenda kazi ili kufanya kazi na kuomba kwa ajili ya Japani.
• Tunaomba kwa ajili ya majina saba katika orodha zetu. Tafadhali tuonyeshe ni kwa kiasi gani Yesu anampenda kila mmoja wao.

Kushukuru
• Bwana, tunakushukuru kwa ahadi yako: “…Yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.” (Wafilipi 1:6)
• Tunakushukuru, Bwana, kwamba unaweza kutujaza furaha na amani.
• Tunakushukuru kwamba tayari unafanya kazi katika mioyo ya watu tunaowaombea.

Nyimbo Zinazopendekekezwa
• Kuwa na Yesu #51
• Mwanga Umo Moyoni #45
• Yesu Unipendaye #30

Ahadi za Kudai Unapoomba

“Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake” (Zaburi 27:10).
“Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” (Warumi 8:31). 
“Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe” (Isaya 49:15). 


Sherehe ya Siku ya Sabato ya Mwisho
Uzoefu wa Kina Zaidi

Mfumo Uliopendekezwa kwa ajili ya Sabato ya Mwisho
Sabato hii ya mwisho inapaswa kuwa muda mzuri wa kufurahia katika yale yote Mungu aliyoyafanya kwa ajili yako na kanisa lako kwa kipindi hiki cha Siku Kumi za Maombi. Tayarisha siku yako kwa namna ya kusherehekea wema wa Mungu na nguvu yake ya ajabu. Fikiria uzoefu wa kumwagwa kwa Roho Mtakatifu uliopitia katika kipindi chote cha siku kumi. Sabato hii ni fursa ya kufurahia kile alichokifanya, anachokifanya, na atakachokifanya.
Hitaji la kila kusanyiko ni tofauti, hivyo tafadhali fanya kazi pamoja na viongozi wa kanisa lako kutengeneza mpango mahususi kwa ajili ya kanisa lako. Hapa kuna baadhi ya mapendekezo ya kujumuisha katika ibada ya Sabato ya mwisho katika kanisa lako.
FUNGU KUU
“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” (Yohana 17:3)
Shuhuda:
Tenga muda wa kutosha kwa ajili ya shuhuda kwa maombi yaliyojibiwa. Wale walioshiriki katika Siku Kumi za Maombi wanapaswa kuwa na visa vingi wanavyoweza kushiriki na mkutano, lakini wahimize kuzungumza kwa ufupi ili kila mmoja apate kushiriki. Wengine pia wanaweza kuwa na visa. Inaweza kuwa vema kuwa na baadhi ya shuhuda zilizoandaliwa kabla, lakini pia unaweza kuwa na muda wa kushiriki kwa uwazi.

Muda wa Maombi: Alika mkutano wote kujumuika katika muda wa maombi ya pamoja. Unaweza kuongoza mkutano katika maombi ya pamoja kama ulivyokuwa ukifanya katika siku zote kumi. Unaweza kuombea kifungu mahususi pamoja. Shughuli hii inaweza kufanyika na watu wakiwa katika makundi madogo au kila mmoja kwa pamoja. Namna nyingine inaweza kuwa na aina tofauti kadhaa za maombi katika muda wote wa ibada – kuomba Mafungu, makundi madogo, watu binafsi, kwa pamoja, kimya kimya, na kadhalika. 
Kuimba: Siku hii ni ya kufurahi kwa yale yote aliyoyafanya Mungu, na muziki ni njia nzuri ya kusherehekea. Kama kuna wimbo umekuwa wimbo mkuu kwa kundi lako, hakikisha unaimbwa na mkutano wote.
Mipango ya mbele: Kama Mungu amekuongoza katika kuwafikia watu kwa namna ya pekee au huduma katika Siku hizi Kumi za Maombi, fahamisha familia yako ya kanisa kuhusu mipango yako na waalike waweze kuungana nawe. (Baadhi ya mapendekezo yamehusishwa katika Mwongozo wa Kiongozi wa Siku Kumi za Maombi.) 
Watoto/Vijana: Hadithi ya watoto kuhusu maombi itakuwa inafaa zaidi. Pia, kama ulikuwa na watoto au vijana waliohusika katika mikutano ya maombi, waruhusu waweze kushiriki shuhuda zao na waongoze katika muda wa maombi.

Uwezo wa Kubadilika: Hakikisha unaweza kubadilika katika mipango yako ili uweze kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu katika muda wote wa ibada.